Simulizi : Miss Tanzania
Sehemu Ya Tano (5)
Kule ndani ya uwanja wa ndege, Ngamao alitoa radio maalum ya kipolisi na kubonyeza kitufe kwenye kifaa kile huku akikipeleka mdomoni kwake.
“Gari liko tayari? Tuko eneo la makutano tukiwa na mtuhumiwa!” Aliongea kwenye kile kifaa.
“Ndio!” Jibu fupi tu lilisikika kwa sauti ya mkoromo kutokea kwenye kile kifaa kilichokuwa mkononi mwake.
Hilo lilimtosha.
Aliirudisha ile redio yake mfukoni, akatoa bastola na kuiweka tayari kwa mkono wake mmoja huku kwa mkono mwingine akiwa amemkamata Candy kiwikoni.
“Kuna haja ya kutoa bastola kweli afande?” Abiyah Byabato alimuuliza.
“Shut-up suti nyeusi! Niko kwenye fani yangu hapa! Wewe subiri mahakani huko!” Ngamao alimkemea na kumuongoza Candy kuelekea kule nje ya korido ambako ndege kadhaa zilikuwa zimeegeshwa, akifuatiwa na wale askari wenzake pamoja na wale mawakili wawili wa kike.
Walitokeza nje na moja kwa moja Ngamao akawaongoza ubavuni mwa jengo lile. Hatua kama kumi tu kutoka kwenye mlango wa lile jengo korido kulikuwa kuna magari mawili meusi aina ya Landrover Discovery yaliyokuwa yameegeshwa moja mbele ya jingine.
“Tunaenda kwenye yale magari pale!” Ngamao aliwaanmbia huku akimkokota Candy kwa mwendo wa haraka kuyaelekea yale magari. Wale askari wawili aliofika nao pale uwanjani usiku ule wakiwa kila upande wake, nao wakiwa wametoa bastola zao, wale mawakili wawili wakiwafuata nyuma yao, na mwisho kabisa akiwa yule askari waliyemkuta akiwasubiri kwenye ile lifti.
Moja kwa moja Ngamao alifungua mlango wa nyuma wa ile Discovery ya nyuma na kumsukumia Candy ndani yake, naye akafuata nyuma yake kule nyuma.
“Wewe WP pita huku nyuma pamoja nasi! Nyie wengine muingie kwenye lile gari la mbele!” Ngamao alitoa maelekezo.
“No way! Mimi na mteja wangu! Mwanzo mwisho!” Abiyah Byabato alidakia huku akiingia yeye kule nyuma pamoja na Candy.
Ngamao akatoa sauti ya kukereka.
“Lazima kuwe na askari wa kike pamoja na mtuhumiwa humu garini!” Ngamao akapinga.
“Na mimi pia lazima niwe pamoja na mteja wetu!” Yule msaidizi wa wakili Abiyah naye akadakia.
“Msitake kunichanganya nyiwe wanawake! Hii ni kazi ya kipolisi na mimi ndiye ninayeiongoza kwa hiyo…”
“Kwa hiyo we’ kaa siti ya mbele, tuache wanawake tukae nyuma!” Abiyah Byabato alimkatisha.
Ngamao akasonya.
“Huyo kijakazi wako aruke nyuma huko! Mi’ nakaa na mtuhumiwa wangu huku huku!” Alimkoromea.
Yule dereva aliyekuwa kwenye mavazi ya kiaskari kule mbele alikuwa ametulia kimya tu muda wote huo.
Candy akawekwa katikati ya Ngamao na yule askari wa kike kule nyuma, Abiyah akiwa amejibanza kule kule nyuma kando ya yule askari wa kike. Yule dada msaidizi wa wakili Abiyah akakaa kwenye moja ya viti vidogo vilivyokuwa sehemu ya nyuma kabisa ndani ya lile gari.
Ngamao akawageukia wale askari wawili wakiume waliobaki nje ya lile gari..
“Okay…nyie mtakuwa kwenye gari la mbele pale, lakini mtasubiri siye tuondoke nanyi mtatufuata nyuma, right?” Aliwaambia.
“Ndio afande!” Yule aliyefika pamoja naye pale uwanjani aliafiki.
“Mimi kazi yangu inaishia hapa afande!” Yule mwingine waliyemkuta akiwasubiri kwenye lifti alisema.
“Okay, sawa. We’ tulikukuta hapa hapa…kazi nzuri askari!” Ngamao akamwambia, akamwamuru dereva wake waanze safari.
Msafara ukaanza.
Huku nyuma yule askari wa kiume aliyeongozana na Ngamao pale uwanjani usiku ule aliingia kando ya dereva wa lile gari jingine nao wakaanza safari kulifuata lile la kwanza.
Yule askari mwingine aliyekutwa kwenye lifti na akina Ngamao alitembea haraka kurudi kule kwenye jengo la uwanja wa ndege, na kupitiliza moja kwa moja ubavuni mwa jengo lile hadi kwenye pikipiki kubwa iliyokuwa imeegeshwa pale kando ya lile jengo. Aliikwea na kuindoa kwa kasi ya wastani kuyafuata yale magari…
***
Simu ya Wakili Abiyah Byabato iliita.
“Vipi wewe? Uko wapi? Candy amechukuliwa na maaskari na kupelekwa sijui wapi tu huko! We’ umechukua mpunga halafu huonekani eneo la tukio hadi mteja wako anachuku…” Kokos alimpayukia baada ya kuipokea simu ile.
“Tulia Kokos! Niko na Candy hapa…vipi wewe?” Abiyah alimkatisha kwa kukereka.
“Uko naye?” Kokos alisaili kwa kutoamini.
“Yap! Tuko kwenye gari la polisi hapa tunapelekwa…” Abiyah alimjibu na hapo akamgeukia Ngamao, “Hivi unatupeleka wapi Inspekta?”
“Central Polisi, wapi kwingine?” Ngamao alimkoromea kwa nongwa.
“There you got it…tunapelekwa polisi central…” Abiyah akamjuza Kokos simuni.
“Basi na siye tunakuja huko huko!” Kokos alimwambia.
“Okay…” Abiyah aliafiki na kukata simu.
Kupitia kioo cha pembeni cha kuonea nyuma yule askari aliyekuwa akiendesha lile gari alimuona muendesha boda boda akichomoka kwa kasi sana kutokea nyuma ya lile gari la wenzao waliokuwa wakiwafuata nyuma, na hata pale alipokuwa akimakinika na yule mwendesha pikipiki, aliiona ile bodaboda ikilichomekea lile gari la wenzao ghafla sana, naye akatabasamu na kuongeza kasi ya gari lake…
***
Dereva wa ile Discovery iliyokuwa nyuma ya ile waliyokuwamo akina Ngamao alishtukia mwendesha bodaboda akikatisha ghafla mbele yake kutokea nyuma na huku tusi kubwa likimtoka akakanyaga breki. Mwendesha bodaboda aliserereka vibaya hatua kadhaa mbele yake na hapo hapo kishindo kikubwa kikasikika wakati gari lililokuwa nyuma ya ile Discovery ya polisi lilipojigonga vibaya nyuma ya ile Discovery.
Wale askari wawili waliachia sauti za hamaniko mle garini na kugeuka nyuma kilipotokea kishindo, tayari mayowe ya wapita njia wachache usiku ule yakisikika kutokea huku na huko, na hapo hapo honi zilianza kurindima kila upande. Kule mbele yule dereva wa bodaboda alijirusha chini kutoka kwenye pikipiki yake na kulikimbilia lile gari huku akitupa mikono hewani kwa ghadhabu, akijitia kulalamika kwa kukoswa-koswa kugongwa, na alipolifikia lile gari alipigiza kiganja cha mkono wake kwa nguvu juu ya boneti wakati hapo hapo kwa mkono wake mwingine akizamisha kwa nguvu kisu kikali kwenye tairi la mbele la lile gari. Yule askari aliyekuwa kando ya dereva wa ile Discovery alifungua mlango na kuruka nje kwa hasira, na yule mwendesha bodaboda aliyekuwa akifuata maelekezo maaluma aliyokiwshapewa awali, alikichomoa kisu chake kutoka kwenye tairi na kutimua mbio kurudi kwenye pikipiki yake.
Msongamano ukaibuka eneo lile wakati yule mwendesha boda boda alipoiinua pikipiki yake na kutimka kwa kasi kutoka eneo lile.
Kazi aliyolipwa kuifanya alikuwa ameitimiza.
Muda huo yule askari mwingine aliyekuwa akiyafuata yale magari kwa pikipiki alipita kwa kasi eneo lile, akifuata ule ulekeo wa lile gari la akina Ngamao bila hata ya kuwatazama wale wenzake waliokuwa kwenye matatizo.
Mmoja wa wale askari alianza kuwasambaza raia kutoka eneo la tukio na hapo askari wa usalama barabarani akafika kuchukua nafasi yake.
“Afande sisi yatupasa twende! Yule bodaboda mshenzi kakimbia…huyu aliyetugonga kwa nyuma atamalizana na askari wa barabarani…tuwawahi wenzetu!” Dereva alimwambia mwenzake, lakini kuingia kwenye gari safari haikuwezekana.
Tairi lao la mbele lilikuwa limepata pancha!
Limepataje pancha…hawakuwa na namna ya kuelewa kwa haraka wakati ule.
Jamaa walichanganyikiwa.
Mmoja wao akatoa simu na kumpigia Ngamao…
***
Simu ya Ngamao iliita garini, na kama aliyekuwa akisubiri ile simu iite, yule dereva kule mbele akiwa amehakikisha kuwa amepandisha vioo vyote vya lile gari na kuviloki pamoja na milango yenyewe, alichomoa kichupa kidogo kutoka kwenye mfuko wa shati lake na kufyatua kizibo maalum kwenye kichupa kile na moshi mwepesi ukafumuka kutoka kwenye kile kichupa na kuenea haraka sana ndani ya lile gari, naye akabana pumzi kwa muda huku akipeleka mkono wake mmoja chini ya kiti cha gari lile.
“Tumepata ajali…!” Sauti ya mmoja wa wale askari waliokuwa kwenye lile gari la nyuma yao ilimfikia Ngamao kupitia kwenye simu yake.
“Mme…wapi? Kivipi?” Ngamao alimaka simuni.
“Hah! Hiyo harufu…ni nini?” Abiyah naye alimaka ghafla alipofikwa na harufu ya ule moshi mwepesi.
“Ahh, huu moshi…unat…toka wapi?” Candy naye alimaka na yule askari wa kike naye akapayuka maneno kama hayohayo.
Ngamao alichanganyikiwa garini.
Huku anasemeshwa kwenye simu kuwa wenzao wamepatwa ajali, huku anaona moshi ukieenea garini na wasafiri wenzake wakilalama.
“Simamisha gari wewe!” Alifoka huku akikata ile simu.
“Aaahh! Kloro…klorofoooom!” Yule msaidizi wa wakili Abiyah alibwata kwa hamaniko kutokea kule nyuma kabisa ya lile gari.
Dereva aliliegesha gari kando ya barabara na kujiinamia huku akivutia usoni kwake kile kitu alichokichomoa kutoka chini ya kiti chake.
Kule nyuma Ngamao alianza kuhisi pumzi zikimuwia nzito, wale wenzake garini nao wakaanza kutapatapata kusaka hewa. Ngamao alipeleka mkono kujaribu kufunga mlango lakini ukawa umekomewa kutokea kule mbele, akajaribu kubonyeza kishushio cha kioo lakini nacho kilikuwa kimekomewa kutokea kule mbele.
“What the…??”
Kando yake, Candy na wakili wake wakalaliana shaghala baghala, kama mateja yaliyokolewa na usingizi mzito wa madawa.
“Nin…ni pah…pale…?” Aliuliza kwa taabu huku naye akihisi usingizi mzito ukimuelemea.
Alimgeukia yule askari mwenzake wa kike, na kuona alikuwa amejiegemeza kwenye kioo cha dirisha la mlango wa upande wake, kinywa kikiwa wazi na mchirizi mzito wa udenda ukiwa unatambaa pale mlangoni kutokea kinywani mwake, amelevywa na usingizi.
“Oooh…!” Alibwabwaja huku akijilazimisha kupeleka mkono wake kiunoni kutoa bastola lakini hapo alimuona yule dereva akimgeukia kutoka kule mbele, sasa akiwa amejiziba uso na kiziba pua na mdomo maalum, yaani “gas mask”, kilichomkimnga kutokana na athari za ule moshi mbaya wa gesi aina ya Chloroform, usoni akiwa amevaa miwani myeusi iliyoficha macho yake, kofia yake ya kiaskari akiwa ameishusha chini kabisa usoni kwake.
Na mkononi alikuwa amemuelekezea bastola.
“Tulia hvyo hivyo Inspekta! Acha bastola hiyo!” Jamaa alimkoromea, sauti yake ikisikika kama isikikavyo ya mtu anayeongea huku akiwa amebana pua, bila shaka kutokana na kile kiziba pua na mdomo alichojivika kutoka chini ya kiti cha gari lile.
Ah! Ni yule jamaa wa hotelini kwa Candy huku (akamtukania mama yake). Jamaa limenizidi kete kwa mara nyingine, pumbavu zangu!
Ndilo wazo la mwisho kumpitia kichwani mwake, kabla naye hajatekwa na usingizi mzito uliotokana na ile gesi kali ya usingizi.
Nyuma ya kile kiziba pua na mdomo alichovaa, yule dereva alitabasamu na kuugeukia usukani wa gari lile.
Alilirejesha gari barabarani na kuendelea na safari kwa mwendo wa kasi, sasa akibadili uelekeo na kufuata njia ya Vingunguti jijini Dar…
Kule uwanja wa ndege mmoja wa wafagiaji wa pale uwanjani aliyemaliza zamu yake usiku ule alishtushwa na sauti ya kugongwa-gongwa kitu kama chuma hivi kutokea nyuma ya mlango wa kichumba kidogo cha kuhifadhia mifagio na zana mbalimbali za usafi, alipokuwa anapita kuelekea kwenye mlango wa kutokea nje ya jengo lile la uwanja wa ndege.
Akiwa amejawa udadisi, akaufungua ule mlango. Hapo udadisi wake ukabadilika na kuwa mshangao pale alipomkuta mtu asiyemfahamu akiwa amefungwa kamba miguu ilhali mikono yake ikiwaimefungwa kwa mgongoni na mdomoni akiwa amebandikwa plasta kubwa iliyomfanya ashindwe kuongea au kupiga kelele.
Jamaa alikuwa amevaa chupi na fulana mchinjo tu, miguuni alikuwa amevaa soksi huku viatu aina ya buti vikiwa pembeni yake.
“Aka! We’ umekuwaje tena?” Mfagiaji aliuliza kibwege, na yule jamaa alimtolea sauti za miguno huku akiwa amemtumbulia macho kwa hasira, na kwa miguu yake iliyofungwa pamoja akilipiga tenakwa nguvu pipa kubwa lililokuwa jirani yake mle ndani.
Mfagiaji akatoka mbio nje ya chumba kile na kwenda kuwaita wana usalama.
Ni baada ya kufunguliwa na wanausalama wa pale uwanjani, ndipo yule jamaa alipojitambulisha kuwa yeye niaskari wa jeshi la polisi.
Jamaa walizidi kumshangaa.
Akawatoa mshangao kwa kuwaambia kuwa alikuwa amekuja na wenzake kumkamata mhalifu aliyekuwa anashuka na ndege ya usiku ule, yeye akiwa ni dereva wa moja kati ya magari mawili yaliyokuwa yakisubiri wenzao pale uwanjani. Akiwa anasubiri ndani ya gari lake, alifikiwa na mmoja wa wafanyakazi wa pale uwanjani aliyemjuza kuwa alikuwa anahitajika na mkuu wao wa msafara, na akamtaja kwa jina kabisa huyo mkuu wao wa msafara…Inspekta Kijambia. Basi yeye akakomea gari na kumfuata yule mfanyakazi. Walipofika kwenye ile korido pweke jamaa alimzubaisha kidogo kisha akampiga na kitu kizito kosogoni.
Alipozinduka ndio akajikuta akiwa amefungiwa kwenye kile chumba kama alivyokutwa na yule mfagiaji. Akiwa amevuliwa nguo zake za kiaskari na ufunguo wake wa gari ukiwa umetoweka pamoja na nguo zake zile.
Lah!
Badala ya kuondokewa na mshangao jamaa walizidi kubaki vinywa wazi. Hapo hapo ilipigwa simu polisi kituo cha kati na wakaomba kuongea na Inspekta Kijambia. Huko nako wakaambiwa kuwa Inspekta Kijambia hajafika na hajulikani alipo, ilhali wale wenzake waliokuwa kwenye lile gari jingine, walikuwa wameshafika pale kituoni baada ya kulazimika kubadilisha tairi lililohujumiwa na mtu aliyejifanya kuwa ni mwendesha bodaboda mwenye hasira.
Inspekta Kijambia na mtuhumiwa wake pamoja na askari mwingine wa kike aliyekuwa naye kwenye gari ambalo yeye ndilo alitakiwa awe analiendesha, hakuwa akijulikana alipo. Simu yake na ya yule askari wa kike aliyekuwa naye zote zilikuwa hazipatikani.
Tafrani!
Jamaa aliazimwa nguo na askari wenzake wa usalama wa pale uwanja wa ndege na kupatiwa usafiri wa kupelekwa kituoni kwake akiwa amechanganyikiwa vibaya sana.
Inspekta Kijambia na mtuhumiwa wake Candy Gamasala, walikuwa wametekwa.
***
Wakati haya yote yanatokea, kule maeneo ya Vingunguti gari alilokuwa amepanda Inspekta Kijambia na mtuhumiwa wake pamoja na wale wenzao waliolevywa kwa ile gesi usingizi lilifunga breki kwa mikiki mbele ya geti la jengo moja kubwa lililojengwa kama bohari na haraka mtu aliyekuwa amekaa nje ya geti lile kama mlinzi, ambaye kwa hakika alikuwa ndio yule mwendesha bodaboda aliyezusha kizaazaa kule barabarani, alilifungua lile geti haraka na ile Discovery ikaingia ndani naye akalifunga ile geti na kubaki pale nje.
Ndani ya lile jengo ile Discovery ilisimama katikati ya eneo pana la karakana ya kutengenezea zana za aluminiam, ambayo kwa usiku ule ilikuwa pweke, taa kali za mianzi zikimulika eneo lile.
Mlango wa ile Discovery ulifunguliwa na Greg Pasha akateremka haraka, akiwa ameshavua kile kiziba pua na mdomo alichokuwa amevaa garini kujikunga na ile gesi ya usingizi aliyowapulizia akina Ngamao.
Alienda kuufungua mlango wa nyuma wa ile discovery na kumvuta Candy kwa nguvu nje ya lile gari, bila kujali jinsi alivyokuwa akiwasukasuka akina Abiyah waliokuwa wamezimika kwa usingizi mzito kama Candy mwenyewe.
Muda huo jamaa mwingine alitokea kutoka kwenye kona moja ya karakana ile na kumsogelea Greg pale alipokuwa.
“Funga kamba wote hao humo garini…wakiamka wasiweze kutusumbua!” Greg alimwambia, na kuendelea, “…kisha futa alama zote za vidole kwenye hili gari na uondoke nalo haraka kutoka eneo hili, ukalitelekeze maporini huko pamoja na hao abiria wake humo ndani…na baada ya hapo ufute alama zote za vidole vyako kwenye hilo gari na utoweke. Sawa? Mi’ naambaa na huyu mrembo hapa!” Alimalizia kumwambia yule kibaraka wake huku akimbeba Candy begani na kuelekea naye kwenye kona nyingine ya karakana ile ambako gari lake ghali aina ya Porsche lilikuwa limeegeshwa.
Yule kibaraka alirudi mbio kule alipotokea kwa lengo la kwenda kuchukua kamba ili kutekeleza kile alichoagizwa na Greg aliyekuwa kwenye mavazi ya ki-askari.
“Wote tulieni hivyo hivyo, pumbavu!” Sauti kali iliwakemea kutokea nyuma ya ile Discovery aliyofika nayo Greg mle ndani muda mfupi tu uliopita, na Greg na kibaraka wake wakashtuka,kila mmojaakigeukia kule sauti ile ilipotokea kutokea alipokuwa.
“Wewe?” Greg alimaka huku bado akiwa amembeba Candy begani, akimtumbuliamacho yule mwanadada msaidizi wa wakili Abiyah Byabato, sasa akiwa amesimama huku amewanyooshea bastola kubwa na ndefu, urefu wa ile bastola ukiwa umetokana na kufungwa kiwambo cha kuzuia sauti, yaani “perforated cylinder”.
“Ni mimi yule baniani wangu. Mweke chini huyo mrembo kwa upole zaidi…” Nuru alimjibu Greg huku akiwa amemtulizia macho ya ghadhabu, na kuendelea, “…na mwambie huyu kibaraka wako aje alale chini hapo mbele yako…HARAKA!”
Greg alibaki akiwa amepigwa na butwa, vitu viwili vikijidhihirisha akilini mwake.
Kwanza alimkumbuka yule mwanadada kuwa ndiye yule yule aliyekutana naye kule kwenye ile gereji ya Mushi maeneo ya gerezani alipoenda kuchukua zile sare za bandia za polisi, na pili alishangaa inakuwaje yeye hakuleweshwa na ile gesi ya usingizi aliyoieneza mle garini, ambayo ilikuwa imewalevya wenzake wote.
Nuru aliona jinsi alivyochanganyikiwa.
“Naona umenikumbuka gabachori feki…si ulijitia kuniita malaya mimi kule gerezani wewe? Ulijiona mjanja wakati ule, lakini muda wote ni mimi ndiye niliyekuwa mjanja zaidi yako fala wewe!Mweke chini huyo mrembo na uje ulale chini na wenzako hapa, alla!” Nuru alimkoromea, na Greg akazidi kuchanganyikiwa.
“Nimewapulizia gesi nyote nyie…sasa how…?”
“Uliwapata wale wasioijua harufu ya Klorofom fala wewe…mimi naijua na mara moja nikawahi kujiziba pua kwa kitambaa na kulala kifudifudi kule nyuma.” Nuru alizidi kumshangaza Greg, na hapo hapo Greg akamshusha Candy kwa kitendo cha haraka kutoka begani na kumweka mbele yake kama ngao.
“Tupa chini bastola hiyo Malaya! Vinginevyo umpige risasi huyu kinyago hapa!” Greg alikoroma huku akiwa amemuweka Candy kifuani kama kinga dhidi ya risasi kutoka kwa Nuru, na hapo hapo Nuru akafyatua risasi na Greg akashitukia maumivu makali sana sikioni wakati risasi ya Nuru ilipompunyua sikio.
“Yalaa!!”Greg alimaka huku bila kupenda akimuachia Candy na akijishika sikio, Candy akisambaratika chini kama gunia. Greg alitazama kiganja chake kilichotapakaa danmu na kumgeukia Nuru kwa mshangao huku uso ameukunja kwa kutoamini.
“Sijakukosa kwa bahati mbaya pale gabachori…nilidhamiria kukupunyua sikio, na sasa uko wazi mbele yangu. Kaa chini upe..” Nuru alikuwa anasema, lakini hapo aliona mtikisiko kutokea kule alipokuwa yule kibaraka wa Greg, na akawahi kujigeuza haraka.
Na hapo Greg Pasha akazinduka.
Spana kubwa iliyotupwa na yule kibaraka ikamkosa Nuru na kwenda kuangukia sakafuni hatua kadhaa kutoka pale alipokuwa.
Aliachia ukulele wa ghadhabu na kumgeuka haraka Greg, na kukumbana na teke kali la mkono, bastola ikamtoka. Hapo hapo yule kibaraka wa Greg naye akamrukia kwa ngwara kali. Nuru aliruka juu kuikwepa ile ngwara, lakini hapo hapo Greg akampiga kwa nguvu kifuani kwa kitako cha kiganja chake, na Nuru akatupwa nyuma mzima mzima na kusambaratika vibaya sakafuni.
“Funga kamba wale wote kwenye gari humo na uondoe hili gari mahala hapa upesi wewe! Huyu malaya niachie mimi sasa!” Greg Pasha aliunguruma kwa hasira kumwambia kibaraka wake huku akimrukia Nuru pale chini.
Nuru alijizungusha haraka pale chini na Greg Pasha akaiparamia sakafukwa kishindo huku muungurumo wa ghadhabu ukimtoka. Nuru alijitupa wima huku sauti ya kujikakamua ikimtoka, na kwa pembe ya jicho lake akamuona yule kibaraka wa Greg akiwa ameingiza sehemu ya juu ya kiwiliwili chake sehemu ya nyuma ya ile Discovery ambako akina Ngamao walikuwa wamelaliana.
Muda huo na yule kibaraka naye akausikia ule muungurumo wa ghadhabu kutoka kwa Greg hivyoakaanza kugeuka ili kuona kulikoni.
Nuru aliruka na kuubamiza kwa unyayo wa kiatu chake ule mlango na kumbabatiza kichwa yule jamaa pale mlangoni.
Jamaa aliachia yowe la maumivu huku akienda chini. Nuru akaachana naye na kuruka pembeni huku akigeukia tena kule kwa Greg Pasha, ambako Pasha ndio alikuwa anajisukuma kutoka pale chini kwa mikono yake yote miwili huku amepiga magoti. Nuru alijisereresha sakafuni na kumfyeka ile mikono ngwara kali, na kwa mara nyingine Greg Pasha akapigiza uso sakafuni kwa kishindo, yowe jingine la maumivu likimtoka.
Nuru akajibiringisha pale sakafuni nakujitupa wima, kisha hapo hapo akamtandika teke zito la mbavu. Pasha akatupwa pembeni kwa pigo lile huku akigumia.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kule kwenye gari Nuru alimuona yule kibaraka wa Greg akijiinua kwa taabu kutoka ubavuni mwa ile Discovery alipoangukia baada ya kubabatizwa na mlango wa lile gari.
Aliruka kwa hatua moja kubwa, akamkanyaga mgongoni Greg aliyekuwa akijiinua kwa haraka kutoka pale chini, akaenda tena hewani na kumshidilia teke la mgongo yule kibaraka aliyekuwa anainuka kutoka pale chini, akimwacha Greg Pasha akisambaratika tena sakafuni huku nyuma.
Kibaraka aliachia yowe la mshituko na kujibamiza uso wake kwenye ukingo wa paa la lile gari, paji lake la uso likichanika na damu ikamtapakaa. Nuru alimshukia na kumkamata ukosi wa shati lake kwa nyuma na kumbamiza tena uso wake kwa nguvu kwenye ukingo wa lile gari, na jamaa akaachia kilio cha uchungu, na Nuru akambamiza tena kwa nguvu zaidi, na jamaa akawa mlenda mikononi mwake.
Akamwacha akianguka chini kibwege naye akageukia kule alipokuwa Greg Pasha, na hapo alimuona yule jamaa akimrukia kwa teke lililokuwa linaelekea kumkita kifuani, naye akajitupa chini haraka.
Lile teke likamkosa, na Greg Pasha akapitiliza kama ng’ombe aliyepotezwa maboya na mchagishaji kwenye mchezo wa ng’ombe uchezwao sana kule kisiwani pemba na kwenda kuliparamia lile gari kwa kishindo. Greg aliunguruma kwa ghadhabu na hapo hapo akijigeuza kumfuata Nuru pale alipo.
Nuru alijigaragaza pale chini na kutafuna namna ya kujiinua lakini Greg alikuwa amemfikia na kumshushia mguu wake wa nguvu ili amkandamize pale chini. Nuru alijirusha pembeni na kijigaragaza zaidi, na Greg akatimba sakafu huku mguno wa hasira ukimtoka. Akamrukia tena pale alipojirushia na kutupia teke jingine kali. Nuru alijitahidi kujirusha tena mbali naye huku akitafuna namna ya kujiinua kutoka pale chini, lakini teke la Greg likampata vilivyo ubavuni.Yowe la uchungu likamtoka huku akitupwapembeni. Greg alimuwahi tena na kumtandika teke jingine la shingo na Nuru akahisi kiza kikimtanda usoni.
Huku akimtukania mama yake, Greg Pasha alimkwida ukosi wa koti lake la suti na kumwinua kimabavu kutoka pale chini, kishaakamshidilia bichwa la uso, lakini Nuru aliwahi kuinamisha uso wake.Wakaishia kugongana mapaji ya uso, na wote wakaanchia milio ya maumivu.
Nuru alimsukumia goti lake kwa nguvu kwenye eneo la uume wake, lakini Greg alijirusha nyuma huku akimsukumia kwa nguvu kwenye ubavu wa lile gari.Nuru alijibamiza vibaya kwenye lile garinayowe la uchungu likimtoka. Greg alimfuata kasi na kumshindilia makonde manne mazito sana ya haraka haraka kutokea nyuma yake, mawili kila ubavu, na bila kupenda Nuru akakaa chini, akitweta.
Greg alimlenga teke kali la kisogoni, lakini kabla hajamfyatulia teke lile aligutushwa na kishindo kikubwa kutokea kule kwenye lile lango la kuigilia mle ndani ya ile karakana, naye aligeuka kwa wahka.
Kutokea kule langoni alimwona yule kibaraka wake mwingine aliyekuwa ameweka ulinzi nje ya lile geti la kuingilia pale walipokuwa akibururwa mle ndani na askari wa jeshi polisi huku akiwa amewekewa bastola shingoni.
“Kaa chini mmanga koko!Uko chini ya himaya yangu sasa!”Morandi Gwaza ndani ya mavazi ya kiaskari aliunguruma huku akizidi kumsogelea Greg, akiwa amemkwida yule kibaraka aliyemkuta pale nje ya lile geti.
“Huyo ni mhindi koko wewe…sio mmanga koko! Mara ngapi nikwambie jambo hilo na wewe?” Nuru alimkoromea Morandi kwa taabu huku akigeuka na kubaki akiwa amejiegemeza kwenye tairi la lile gari la akina Ngamao, hoi bin taabani.
Morandi alitabasamu kwa kali ile huku akitembeza macho haraka mle ndani, na kuona athari za tafrani alilotembeza Nuru mle ndani.
“Mnh! Kazi nzuri sana kisura…!” Alisema hatimaye, na kutokea alipokuwa Nuru aliguna tu.
“What…??” Greg Pasha alibutwaika, akitembeza uso wake kutoka kwa Morandi, kwenda kwa Nuru pale chini, na kuugeuzia tena kwa Morandi. Na hata pale alipokuwa akimgeukia tena Morandi Gwaza, alimshuhudia yule mtu mrefu mweusi aliyejivika sare za kiaskari akimpiga kwa nguvu kisogoni yule kibaraka wake kwa kitako cha ile bastola yake, na yule kibaraka akaachia mguno hafifu na mfupi huku akienda chini.
Sasa ile bastola iliyokuwa shingoni kwa yule kibaraka wake aliyepoteza fahamu pale sakafuni ilikuwa imemuelekea yeye.
“Hah! Wewe nani…?” Greg aliuliza huku akili ikimzunguka.
“Uko okay kisura?” Badala ya kumjibu, Morandi alimuuliza Nuru ilhali bado akiwa amemuelekezea ile bastola Greg Pasha na amemkazia macho yenye umakini wa hali ya juu.
“Yeah…siko vibaya sana!” Nuru alimjibu kutokea pale alipokuwa, akianza kuinuka.
“Good.Kwa hiyo kila kitu kitaendelea vile vile kama tulivyopanga?” Morandi aliendelea kuongea naNuru huku bado akiwa amemuelekezea Greg bastola, na macho yake bado yakiwa kwa Greg.
“Nyie vipi? Ni nani nyie…?” Greg alizidi kumaka.
“Yeah…kila kitu kinaendelea vilevile!”Nuru alijibu huku akitweta.
“Mbona siwaelewi nyie lakini?”Greg naye aliendelea kubwata.
“Lala chini hapo gabachori koko …upesi tena!”Morandi alimkoromea huku akimtazama kwa macho yaliyojaa vitisho. Greg alizungusha jicho kuitazama bastola ya Nuru iliyokuwa hatua chache kutoka pale aliposimama.
“Usijaribu kabisa hilo, kemcho!” Kama aliyesoma mawazo yake Morandi alimkemea huku bado akiwa amemnyooshea bastola na akimtazama kwa makini.
Greg Pasha aliifikiria bastola yake aliyokuwa ameichomeka kiunoni kwake kwa nyuma. Alianza kurudisha nyuma mkono wake taratibu huku akimtazama yule jamaa ambaye alijua kuwa kama yeye, naye hakuwa askari wa kweli.
“Tunaweza kuongea kirafiki tu na kufikia makubaliano kaka…kwani tatizo ni nini?” Alijitia kumzubaisha huku akizidi kupeleka mkono wake mgongoni kwake.
“Gabachori n’takuchabanga risasi ujue!Tupa mikono mawinguni hiyo!” Morandi alimkoromea kwa hasira, na hapo hapo Greg alishitukia akipigwa teke kwa nguvu nyuma ya goti lake na bila kupenda akaenda chini akipiga goti moja pale sakafuni huku akigumia kwa hamaniko. Hapo hapo Nuru akamuwekea soli ya kiatu chake mgongoni baina ya mabega yake na kumsukuma mbele kwa nguvu. Greg akatoa mguno wa mwingine huku akiangukia uso pale chini na Nuru akamwekea goti katikati ya uti wa mgongo pale sakafuni.
“Heeeey! What the….?” Greg alimaka.
“Shut up!” Nuru alimkoromea huku akimkamata mkono wake na kuuvutia mgongoni kwake. Greg alijikurupusha na Morandi akaikoki bastola yake.
“Tulia hivyo hivyo wewe!”Alimkoromea.
Nuru akamfunga pingu mikono yake yote miwili kwa nyuma, na bila kuamini Greg alibaki akiwa amelala pale chini huku akimkodolea macho yule mwanadada kwa hamaniko.
“Hebu nifungueni nyinyi!Mnafanyamnachokifanya lakini nyinyi?”Greg alimaka na kuuliza kwa hasira.
“Ulikuwa unatarajia nini kuteka gari la polisi namna ile, wewe, eeenh?Sasa wangelikuta humu ndani unadhani wangeshindwa kukufuatilia kupitia kwa mmiliki wa eneo hili?”Badala ya kumjibu Nuru alimuuliza.
“Nani aliyewaambia kuwa nilikuwa nampango wa kuliacha hili gari humu nyinyi? Mna makubaliano gani na Candy mpaka mnamlinda namna hii, eenh?” Greg Pasha aliwajibu na kuwatupia swali.
“Unaoneje ukianza wewe kwa kutueleza ukitakacho kwa Candy…wewe pamoja na wenzako akina GTZ na Ngamao?” Morandi alimuuliza, na hili lilionekana kumshtua sana Greg.
“GTZ na Ngamao…?” Aliuliza kibwege.
“Tunajua vingi kuhusu wewe na hao wenzako gabachori, hivyo usitake kujitia unashangaa hapa.Mnamtakia nini Candy ninyi?”Morandi alimuuliza.
“Sina muda wa kujibu maswali yenu mimi hapa! Ila kama mnataka tunaweza kuelewana tu. Nifungueni hizi pingu halafu tuongee…” Greg alimjibu.
Morandi alimtazama kwa muda,kisha akamsogelea pale alipolala akiwa amefungwa mikono kwa nyuma.
“Ningependa sana nikuweke kiti moto na nikupe kifinyo cha haja mpaka useme yote wewe…” Alimwambia kwa ghadhabu.
“Kama jinsi ulivyomfanya GTZ?Si unifungue basi halafu ujaribu?” Greg alijikuta akiropoka kwa hasira, ilimfunukia kuwa hakika huyu ndiye mtu aliyemkongoroa goti mdogo wake.
“Tena zaidi ya nilivyomfanya GTZ fala wewe. Ila bahati mbaya tu hatuna muda wa kupoteza nawe hapa…kwani hatutaki maaskari waje watukute pamoja nawe hapa gabachori…” Morandi alimwambia kwa hasira na hapo hapo, kabla Greg hajajibu kitu, akamtandika teke zito sana la upande wa kichwa, juu kidogo ya sikio.
Grega Pasha aliachia kilio hafifu huku akiona kiza kikikolea mbele ya uso wake, na fahamu zikamhama.
“Okay, twende kazi!” Morandi alimgeukia Nuru huku akiiweka bastola yake mfukoni, naakitoa glovu ambazo alizivaa mikononi mwake. Nuru naye alitoa glovu kutoka kwenye mfuko wa suruali yake ya suti ya kiwakili na kuzivaa. Kwa dakika kumi zilizofuata wawili wale walifanya kazi haraka haraka, bila maongezi yoyote.
Waliwafunga kamba pamoja Greg Pasha na wale vibaraka wake wawili kwenye moja ya nguzo za ile karakana. Morandi alichukua simu ya Ngamao ambayo kama alivyotarajia aliikuta ikiwa imezimwa na akaiwasha, akijua kuwa ni yule jamaa aliyewateka ndiye atakuwa ameizima ili wenzake wakimtafuta wasimpate.
Na hata pale alipomaliza kuiwasha tu ile simu ikaanza kuita.
Muda huo Nuru alikuwa akimkokotea Candy kule kwenye lile gari la Greg. Morandi aliiacha simu ya Ngamao ikiita mapajani mwa yule askari aliyezimika mle garini, na kwenda kumsaidia Nuru kumuingiza Candy ndani ya lile gari. Kisha Nuru alichukua ufunguo wa lile gari kutoka mfukoni kwa Greg aliyepoteza fahamu.
“Niko tayari miye!” Alimwambia Morandi huku akiishindilia mfukoni ile bastola yake ambayo awali ilianguka pale sakafuni wakati akipambana na Greg Pasha.
“Okay kisura. Unajua mahala gari letu lilipo. Nenda na hili gari hadi kwenye gari letu, mhamie kwenye gari letu na hili uliache hapo…mi’na we’ tutakutana mafichoni. Na huko majibu ya maswali yetu yote kuhusu miss Tanzania wetu hapa yatapatikana, bloody hell!” Morandi alisema.
Bila kusema neno Nuru aliliondoa lile gari kutoka mle ndani, Candy akiwa amelala bila fahamu kwenye kiti cha nyuma cha gari lile.
Morandi alitoka nje ya ile karakana nakulifunga lile geti kwa nje, akijua kuwa muda watakapoamka, akina Ngamao watawapigia simu polisi na eneo lile litazagaa maaskari wa kutosha.
Aliiparamia ile pikipiki yake kubwa aliyokuwa ameiegesha nje ya karakana ile, na kuondoka kwa kasi eneo lile.
***
Hali kituo cha polisi cha kati jijini Dar ilikuwa zaidi ya tete usiku ule.Taarifa za kutoweka kwa Ngamao Kijambia akiwa na mtuhumiwa Candy Gamasala pamoja na mawakili wake wawili zilikuwa zimeenea jengo zima la kituo kile cha polisi, na uwepo wa jopo la wanakamati ya Miss Tanzania pale kituoni usiku ule wakihitaji maelezo ya mahala alipopelekwa mrembo wao haukusaidia kabisa katika kupunguza utete wa hali ile, na badala yake uliizidisha.
Ulikuwa ni mtafaruku mkubwa.
Hakeem Labemba alikuwa anamtaka mkuu wa kituo awakutanishe na mrembo wao ambao yeye alikuwa anaamini kuwa amefichwa na wanausalama kutokana na tuhuma alizotuhumiwa kwazo. Mkuu wakituo alikuwa anajitahidi kumelewesha hali iliyotokea lakini ni wazi Hakjeem hakuwa akimuelewa.
Askari atatowekaje na mtuhumiwa hivi hivi tu?
Bishkuku naye alikuwa akiwajia juu maaskari pale kituoni akiwa bega kwa begana Hakeem, wakati Kokos Wandiba naye akiwa anagombana na simu kwenye gari lao lililokuwa limeegeshwa nje ya kile kituo cha polisi.
Kutokana na historia ya uhasama baina yake na jeshi la polisi, Kokos hakutaka kabisa kuingia pale kituoni. Aliamua kuwasubiri wenzake ndani ya gari huku akijaribu bila mafanikio kumpigia simu wakili Abiyah.
Simu ya Abiyah ilikuwa imezimwa.
Alijaribu kwa mara nyingine tena kumpigia Morandi Gwaza ili ajue kilichokuwa kikiendelea, na kwa mkanganyiko mkubwa akajikuta akipokea ujumbe kuwa mtumia ji wa simu anayoipigia, yaani Morandi, alikuwa hapatikani.
Lah!
Akamjaribu Nuru, naye hali ikawa nihivyo hivyo.
Kokos Wandiba, kama ilivyokuwa kwa wenzake waliokuwandani ya kituo cha polisi cha kati usiku ule, alichanganyikiwa vibaya sana.
Ni nini kilikuwa kinatokea tena?
Ni kilikuwa kinatokea?
Kokos Wandiba hakuwa na jibu, lakini kule ndani ya jengo la makao makuu ya polisi dalili za jibu zilionekana pale simu ya Inspekta Ngamao ilipoanza kuita, baada ya kuwa haipatikani kwa muda mrefu tangu kutoweka kwake kwa namna ya kutatanisha .
“Afande!Afande…simu inaita!” Askari wa kike aliyepewa jukumu la kuendelea kumpigia simu Ngamao mpaka apatikane usiku ule alivamia kwa pupa ofisini kwa mkuu wa kituo, ambaye alikuwa anaendelea kuwekwa kwenye wakati mgumu na Hakeem Labemba na Bishkuku.
Labemba, Bishkuku na Mkuu wa kituo walitazamana, kisha mkuu wa kituo na Labemba waliropoka kwa pamoja kila mmoja akisema lake.
“Amepokea?Lete hapa hiyo simu!” Mkuu wa kituo.
“Ina maana huyo polisi alikuwa ametekwa kweli?”Labemba.
“Hapokei…inaita tu!” Konstebo Happiness, ambaye ndiye aliyehakikisha kuwa Ngamao anajiwasilisha kwa wakuu wake wa kazi pale makao makuu baada ya kukutwa akiwa hana fahamu kule hospitali ya Aga Khan alimjibu mkuu wake wa kazi huku akimkabidhi ile simu.
“Akh!Sasa unanipa ya nini wakati hapokei?” Mkuu wa kituo alisema huku bila kujijua akiipeleka sikioni ile simu, na hata pale alipokuwa akisema maneno yale, sauti ya kike ilimsemesha kutoka kwenye ile simu.
Akamakinika ghafla huku macho yakimtoka na akajiweka vizuri kitini.
“Ama!Nani wewe?” Alihoji kwa ukali, na mbele yake wale waliokuwa pamoja naye mle ofisini wakamkodolea macho ya kuuliza, kisha wakatazamana…
***
Wakili Abiyah Byabato alirudi kwenye fahamu zake kwa taabu huku akikerwa na sauti isiyokoma ya wimbo wa taarabu, naye alikuwa antaka sana kuendelea kuuchapa usingizi mtamu kuliko alivyowahi kulala maishani mwake hapo kabla, lakini ile taarabu ilizidi kumkera masikioni.
Alijisukuma na kupeleka mkono wake hadi pale sauti ya ile taarabu ilipokuwa ikitokea, na kugundua kuwa ilikuwa ni simu iliyowekwa muito wa wimbo wa taarabu. Huku akisonya aliipeleka sikioni ile simu, akili ikiwa inamzunguka asijue ilikuwaje hata akalala usingizi mzito namna ile.
“Yaa…Hallooo…?” Aliongea kivivu kwenye ile simu huku akiangaza macho mle garini na kustaajabu kuona jinsi walivyokuwa wamelaliana na yule askari mwingi wa kisirani na yule askari mwingine wa kike.
Sauti kali ikamsemesha kutokea upande wa pili wa ile simu, na hapo akawa makini zaidi.
“What do you mean mimi nani…wewe si ndo uliyepiga?” Alimkemea muongeaji wa upande wa pili.
“Nasema hivi, hapa unaongea na mkuu wa kituo cha polisi cha kati, nahitaji kuongea na mmiliki wa hiyo simu, sasa wewe ni nani na yu-wapi mwenye hiyo simu, na wewe uko wapi hapo ulipo, na kama uko naye mpe simu niongee naye mara mo…” Mkuu wa kituo alimvurumishia ma-amri bila kituo.
“Oh hebu ngoja kwanza…ngoja kwanza…maana mi sielewi lolote hapa, sijui imekuwaje…nahisi tulipuliziwa dawa ya usingi…” Abiyah alianza kujibu na hapo ikamfunukia kuwa Candy hakuwa pamoja nao mle garini.
“HAH! Candy! Where is… oh my God, Candy katoweka jamani!” Alimaka kwa hamaniko, akiacha kuendelea kutoa maelezo kwa mkuu wa kituo.
Mkuu wa kituo akamjia juu kutoka kule alipokuwa.
“Hey, hebu tulia hapo anti, na utoe maelezo ya kueleweka…Candy katoweka? Na Ngamao je…?” Mkuu wa kituo alimaka, na mbele yake Bishkuku aliishiwa nguvu, hukun Labemba akizidi kutumbua macho. Abiyah aliiacha ile simu na kuanza kuwaamsha akina Ngamao kwa pupa. Alichungulia kule nyuma ambako yule askari wa kike aliyeambiwa na Morandi Gwaza aongozane naye kwa kujifanya kuwa ni msaidizi wake alikuwa amekaa, na kukuta patupu.
Akili ikatulia zaidi.
Alielewa sasa kuwa ni ile ilikuwa ni moja ya mbinu za Morandi kutaka kumnusuru Candy dhidi ya hatari aliyokuwa akiihofia.
Simu ya Ngamao ikaanza kuita tena. Kando yake Ngamao alianza kujitikisa kwa taabu, na yule askari mwenzake wa kike naye akatoa mguno wa mkoromo.
Akaipokea ile simu ya Ngamao na kuteremka nje ya gari lile. Alijikuta akikodolewa macho na wale jamaa watatu waliofungwa kamba pamoja kwenye nguzo ya lile jengo walilokuwamo, ilhali midomo yao ikiwa imezibwa kwa plasta pana, na woga ukampanda.
Hata pale alipokuwa akiwakodolea macho wale jamaa, mmoja wao aliyekuwa kwenye mavazi ya kiaskari alianza kumtolea sauti za miguno huku akimtubulia macho na akimuashiria kwa kichwa chake kuwa amsogelee.
Kwa woga mkubwa akamweleza yule mkuu wa kituo cha polisi kati juu ya hali halisi aliyokuwa nayo pale huku akiwakodolea macho ya woga wale jamaa waliofungwa pale kwenye nguzo.
“Kwa hiyo Ngamao uko naye hapo?” Mkuu wa kituo alihoji.
“Jamaa yuko katopewa usingizi garini humo! Ni miye tu ndo niliyeamka mpaka sasa…” Abiyah alimjibu na mkuu wa kituo akatoa sauti ya kulaani hali ile.
“Sasa hapo mko mahala gani…?” Mkuu aliuliza, na kabla hajajibu Abiyah alisikia kishindo kutokea kule kwenye gari.
Inspekta Ngamao Kijambia alitoka nje ya lile gari akiwa ametumbua macho kwa hamaniko.
“Askari wako ameamka…huyu hapa!” Abiyah aliongea kwenye simu, na kumkabidhi Ngamao ile simu. Jamaa aliipokea ile simu huku akiwa amepigwa butwaa.
“Bosi wako huyo…!” Abiyah alimwambia huku akili ikimzunguka.
***
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Uunhh!Wah…wapi…Nn…Niko wapi hapa?” Candy aliuliza kwa taabu huku akijiinua kutoka kwenye kiti cha nyuma ndani ya gari aina ya Suzuki Escudo mali ya Kokos Wandiba, iliyokuwa ikienda kwa kasi.
“Oh, sleeping beauty umeaka hatimaye?” Nuru aliuliza huku akizidi kuendesha gari kwa kasi kutokea kwenye kiti cha dereva, na akimchungulia abiria wake kutokea kwenye kioo cha kutazamia nyuma kilichokuwa ndani ya lile gari.
“Oh, who…yaani...wewe ni nani? Wako wapi wenzangu?” Candy aliuliza kwa hamaniko zaidi sasa, akijiinua zaidi na kujisogeza karibu na kile kiti cha dereva kutokea kule nyuma.
“Umenisahau Candy?” Nuru alimuuliza huku akiendelea kuendesha kwa kasi.
Candy alichanganyikiwa.
“Unanijua? Mi’ nilikuwa chini ya ulinzi…sasa mbona niko humu, na wewe sikukumbuki kabisa mimi!” Alimaka.
“So unataka nikurudishe huko chini ya ulinzi?Au kule kwa jamaa yako aliyekuibukia kule mikumi siku ile?” Nuru alimuuliza na hapo Candy akaelewa,
“AH! Ni wewe! Mbona uko hapa? Yaani…na mbona ulikuja kuniokoa siku ile kule mikumi…? Ni nani wewe?”
“Hilo na mengine mengi tutayaongea tukifika huko twendako mrembo wetu…by the way, hongera sana kwa kutwaa ushindi wa pili huko Miss world, Candy.” Nuru alimjibu na Candy akazidi kuchanganykiwa.
Alikuwa na maswali makubwa kabisa kuhusu namna mambo yaliyokuwa yanaendelea kumtokea, na huyu dada badala ya kumjibu, eti anaanza kumpongeza kuhusu ushindi wa miss world kama kwamba hajui juu ya tuhuma nzito zinazomkabili.
“Inabidi uniambie tunaenda wapi sasa!” Alimwambia kwa msisitizo.
Nuru akapiga kimya kwa muda.
“Nataka uelewe kuwa mimi sio adui kwako, Candy. Na kwamba ninakokupeleka ndio mahala pekee pa salama kwako kwa sasa. So just sit back mrembo, and enjoy the ride!”
Baada ya hapo Nuru hakumjibu lolote katika maswali aliyokuwa akimvurumishia.
Mrembo Candy Gamasala alibaki kuwa abiria mwenye viulizo vingi sana ndani ya lile gari.
Safari yao iliendelea kimya.
***
“Niambie kilichotokea Ngamao!” Mkuu wa kituo alimsemesha Ngamao simuni, na Ngamao aliyekuwa akizidi kuamka kadiri sekunde zilivyokuwa zikisonga alijikuta akimeza mate kwa hamaniko pale wazo la kile kilichomtokea lilipojidhihirisha akili mwake.
“Na…nadhani tulileweshwa kwa madawa afande…” Alijibu huku akiangaza huku na huko, na akirudi tena kule kwenye gari.
Akimtafuta Candy.
“Tena? Yaani umeleweshwa tena Ngamao? What’s the matter with you?” Mkuu alifoka, na Konstebo Happiness akadakia.
“Muulize yuko wapi afande tumfuatilie!”
“No! No…Candy katoweka!” Ngamao alibwabwaja simuni huku akizidi kuangaza garini na maeneo ya jirani na pale.
“Katowekaje Ngamao? Kwani hapo ni wapi? Sema upesi tutume usaidizi sasa hivi!” Mkuu wa kituo alifoka na Ngamao akahisi miguu ikimuisha nguvu.
“Alikuwa ni askari mwenzetu…tulijua ni mwenzetu…akatupulizia gesi ya usingizi…nd’o kwanza tunazinduka afande! Dereva…”
“Dereva wako tuko naye hapa. Huyo uliyeondoka naye wewe alikuwa wa bandia! Sema ulipo Inspekta!” Mkuu alimkemea na wakati huo huo Ngamao akawaona wale jamaa waliofungwa pale kwenye nguzo.
“Ah! Mbona yule askari aliyetuteka kama yuko hapa…?” Ngamao alisema kwa mashaka huku akiwaendea wale jamaa.
“What?? Hebu sema ulipo Inspekta…”
“Vinguguti! Yuko vingunguti afande! Tumefuatilia eneo simu yake inapotumia mawasiliano…yuko eneo la vingunguti!” Askari mwingine aliingia mle ndani na kufahamisha kwa kiherehere.
“Lets Go!” Mkuu alisema huku akiinuka kutoka kitini kwake.
“Bado sijajua tulipo afande ila…” Kutokea upande wa pili Ngamao alimjibu huku akiwaangalia wale jamaa kwa makini, moyo ukiongeza mapigo.
“Tumeshajua mlipo. Usikate simu ili tuweze kukufikia hapo…mko vingunguti!” Mkuu wa kituo alimwambia, kisha akawageukia akina Bishkuku.
“Ninyi nendeni nyumbani sasa! Tunafuatilia swala hili na tutawajulisha kila kitakachojiri!” Alisema huku akitoka nje.
“No! Na sie tunakuja….!” Bishkuku alimaka, lakini Hakeem Labemba alimkamata mkono na kumzuia.
“Waache polisi wafanye kazi yao Bishkuku…hapa kuna mambo mazito kuliko tunavyoweza kufikiri aisee…”
Kule vingunguti Ngamao aliiweka ile simu juu ya boneti la ile gari huku ikiwa bado iko hewani, kisha akaenda kusimama mbele ya Greg Pasha aliyeinamisha uso wake. Alimtazama kwa muda kisha akapiga goti na kumshika kidevu, akamuinua uso wake.
Hamadi!
“Greg? Ni wewe?” Alimaka kwa sauti huku akiwa amemtumbulia macho yule mtoto wa aliyekuwa mpenzi wake, kwa kutoamini.
Greg alibaki akimkodolea macho ya ghadhabu.
“Yaani mnajuana?” Wakili Abiyah aliuliza kwa kutoamini. Greg akatoa sauti za miguno kumshinikiza Ngamao ambandue ile plasta aliyobandikwa kinywani. Ngamao akambandua kwa hasira.
“Umefanya nini sasa wewe?” Alimuuliza kwa mshangao mkubwa.
“Sikia Ngamao. Tumpoteze huyu malaya, nifungue, mi’ nipotee…ama si hivyo n’taishia jela…na mimi jela sirudi tena aisee!” Greg alimwambia kwa msisitizo.
“Kwa nini ulifanya hivi lakini Greg?” Ngamao alimuuliza kwa uchungu.
“Kwa sababu Candy anastahili kufa kama alivyomuua mama yetu, sio kufungwa maisha kama wewe ulivyokuwa unataka kufanya, bloody fool! Hilo ndilo GTZ analolitaka na ndilo mimi ninalolitaka pia. Na sisi ndio wenye uchungu zaidi na Bi. Shakira, mama yetu, kuliko wewe! Sasa nifungue haraka tumpoteze huyu mwanamke mi nitoweke!”
Ngamao alimshangaa.
“Do it now, Ngamao! Nifungue hapa! Wenzako watafika muda wowote sasa…” Greg alimshinikiza.
Ngamao alimtazama yule jamaa kwa kutoamini.
“Yaani ndio mefikia hatua ya kupanga mkakati kama huu na GTZ? Wakati mi’ niliwaambia kuwa nitahakikisha kuwa sheria inachukua mkondo wake dhidi ya Candy, Greg?”
“Tumpoteze huyu malaya now, Ngamao. Ni mtu pekee anayejua kuwa mimi na wewe tunajuana…mi’ n’tatoweka na we’ utaendelea na kazi zako za kipolisi!”
“Excuse me? Mnataka kufanyaje?” Wakilli Abiyah aliuliza kwa mashaka.
Ngamao na Greg walitazamana.
***
na.
***
Nuru aliegesha gari kwenye eneo la kuegeshea magari la jengo la Millenium Tower, Kijitonyama jijini Dar.
“Hapa ni wapi?” Candy alimuuliza kwa mashaka.
“Tulia miss Ti-Zedi!” Nuru alimwambia, na Candy akatulia.
Muda huo Morandi alijitokeza kutoka nyuma ya moja ya nguzo zilizotapakaa eneo lile na kuiendea ile Escudo. Alikuwa ameshavua zile nguo za kiaskari, na sasa alikuwa amevaa nguo aina ya jinzi, zote zikiwa nyeusi.
“All okay?” Aliuliza kupitia kwenye dirisha la Nuru, na Candy akatoa sauti ya mshituko.
“Yah…mpaka hapo mambo yote safi.” Nuru alimjibu.
“Okay, basi tusipoteze muda hapa.” Morandi alimwambia. Nuru akamgeukia Candy.
“Okay Candy. Mimi naishia hapa. Kutokea hapa utaondoka na huyu mwenzangu hadi sehemu salama…huko kila kitu kitawekwa wazi kwako.”
“Na wewe utatuweka sisi wazi vile vile!” Morandi alidakia.
“Mn! Huyu ni nani…na kwa nini inabidi iwe hivi?” Candy alihoji.
“Bibie…kuna jamaa wanaotaka kukuua huko mitaani, na pia kuna askari wanaotaka kukuweka chini ya ulinzi wakiamini kuwa uliua mtu. Sisi tunakuweka mbali na wote hao kwa sasa mpaka hapo itakapokuwa salama kwako kujitokeza mbele ya jamii. Shuka kwenye gari njoo twende…muda hamna tena hapa!” Morandi alimkoromea kwa msisitizo.
Candy alisita.
“Fanya asemavyo anti…sisi tumetumwa na Kokos!” Nuru alimwambia, na Candy akatekeleza haraka.
Morandi akamvisha kofia ya kuendeshea pikipiki, naye akavaa ya kwake, kisha akampandisha yule mrembo kwenye pikipiki lake kubwa na kuondoka naye kwa kasi kutoka eneo lile. Nuru aliondoka na gari la Kokos na kuchukua uelekeo wa Mbezi beach, nyumbani kwa Kokos Wandiba.
***
Simu ya Kokos iliita. Namba ilikuwa ngeni kwake. Akapokea.
“Nuru hapa. Utanikuta nyumbani kwako.” Nuru alimwambia, na kabla Kokos hajasema neon zaidi, akakata simu.
Kokos akalaani.
Akaipiga tena ile namba. Akapata ujumbe kuwa namba haipatikani. Akajaribu tena na tena, jibu likawa lile lile.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Shit!
Hapo Labemba na Bishkuku wakafika kwenye gari alilokuwamo wakitokea ndani ya kituo cha polisi. Alipoelezwa kilichojiri huko ndani, akaachia mguno na kubaki akitikisa kichwa kwa masikitiko.
“Okay, nadhani yatupasa kwenda nyumbani tu kwa sasa!” Alisema hatimaye, na dakika kumi baadaye, yeye na Bishkuku walikuwa njiani kuelekea nyumbani kwake Mbezi Beach, wakiwa wameachana na Hakeem Labemba na wale watendaji wenzake wa kamati ya Miss Tanzania.
***
Kwa pamoja Ngamao na Greg walimgeukia Abiyah na kumtazama kwa macho ambayo mtazamwaji hakuyaelewa. Alijikuta akirudi nyuma hatua moja.
“Mnataka kufanya nini? Wewe ni afisa wa polisi, na hao watu ni wahalifu…nakutarajia utimize wajibu wako kwa misingi ya sheri…” Abiyah alianza kujihami huku akirudi nyuma.
“Kimya mwanamke! Ngamao nifungue upesi!” Greg alimkemea Abiyah na kumgeukia tena Ngamao.
Inspekta Kijambia aliinuka na kumgeukia Abiyah.
Akasimama kwa butwaa, macho yake akiwa ameyaelekeza kule kwenye gari.
Yule askari wa kike aliyekuwa naye garini naye alikuwa amezinduka na sasa alikuwa amesimama nje ya lile gari huku akiwa amejishikilia kwenye mlango wa lile gari, akitumbulia macho kile kilichokuwa kinatokea pale.
Abiyah alimgeukia yule askari wa kike na akajisogeza pembeni zaidi.
“Ngamao ukifuata ushauri wa huyo jamaa yako, basi itakubidi utuangamize sisi sote hapa, pamoja na hao vibaraka wengine aliofungwa nao hapo…” Alimwambia.
“Ah…atuangamize…? Kiv…kivipi?” Yule askari wa kike alidakia huku akijikongoja kuelekea pale alipokuwa Ngamao.
Macho yalimtembea Ngamao.
“Muulize mwenzio …anashauriana nini na huyo jamaa hapo?” Abiyah alimjibu kichochezi.
“Hebu kelele wewe! Nani ameongelea juu ya kuangamiza mtu hapa?” Ngamao alikuja juu.
“Si huyo jamaa yako hapo chini amekushauri sasa hivi, au hukusikia?” Abiyah anaye akamjia juu.
“Jamaa yako huyu afande?” Yule askari wa kike naye akamtupia swali Ngamao kwa kutoamini.
Ngamao akachanganyikiwa, na wakili Abiyah akashusha pumzi za ahueni, kwani aliona kuwa tayari ameshamuwekea ugumu Ngamao kufanya lolote lisilo ndilo.
“Hajui analoongea huyu mama!” Ngamao alimjibu mwenzake huku akionekana kuwa kwenye mtanziko mkubwa.
“Na hawa ni nani sasa?” Yule askari wa kike alizidi kusaili huku akiwatazama akina Greg, lakini kabla hajajibiwa vishindo vikasikika kutokea nje ya geti la ile karakana waliyokuwamo.
“POLISI! Fungua!” Sauti kali ilisikika kutokea kule nje, na wote mle ndani wakatazamana.
Kilichofuatia ni kizaazaa.
Lile eneo la vingunguti usiku ule likabadilika na kuwa mchana. Magari ya polisi yalikuwa yamezagaa huko nje, taa zikiangaza eneo lote lile.
Ngamao Kijambia alijikuta kwenye wakati mgumu sana kuelezea hali iliyokutwa pale.
Alibaki akitazama bila msaada wakati akina Greg Pasha wakitiwa nguvuni na kupelekwa kwenye gari la polis huko nje. Greg alijikukurusha kwa nguvu lakini alidhibitiwa itakiwavyo, hakuwa na namna. Kilio cha uchungu na kushindwa kikamtoka.
Ni katika hekaheka ile, ndipo wakili Abiyah alipoikumbuka simu yake, na kugundua kuwa ilikuwa imezima au imezimwa, ingawa yeye mwenye aliiacha ikiwa wazi kabla ya kukutwa na ule uvamizi wa usingizi wa kulazimishwa.
Aliiwasha na kumpigia Kokos.
***
Eneo jingine la jiji Candy alikuwa akimtazama yule jamaa mrefu mweusi aliyevaa nguo nyeusi tupu kwa woga mkubwa. Walikuwa ndani ya nyumba moja pweke sana maeneo ya makongo jijini Dar. Morandi alikuwa amemuelekeza aketi kwenye moja ya makochi ya mle ndani naye akaketi.
Kisha jamaa likamletea gilasi ya maziwa ya baridi kutoka kwenye jokofu.
“Kunywa haya…sijui ulipuliziwa dawa gani ya kulevya ila nahisi ni klorofom. Maziwa yatasaidia kuondoa sumu yoyote mwilini mwako!” Alimwambia, na Candy akapokea maziwa yaLe na kuanza kunywa taratibu.
Morandi akaketi kwenye kochi lililokuwa mbele yake na kukunja nne huku likimtazama kwa utulivu wakati akinywa yale maziwa.
Na Candy naye akawa anamtazama kwa woga.
“Aam…Kokos yuko wapi? Na…ulisema kuna watu wanataka kuniua…ni akina nani hao?” Hatimaye Candy alimuuliza kwa woga, na yule jamaa akamshangaza kwa kuangua kicheko cha kivivu.
“Candy, Candy, Candy…yaani we’ hujui uliwakorofisha akina nani huko utokako hata wanataka kukuua?” Alimuuliza, na Candy akazidi kuchanganyikiwa.
“Mimi? Ni nani wa kutaka kunuia mimi jamani? Hivi unajua kuwa nimesingiziwa kesi ya mauaji mimi? Halafu we’ umeenda kunitorosha nikiwa chini ya ulinzi…si utazidi kuniletea matatizo zaidi?” Candy aliuliza.
“Okay ni kweli, lakini si miye niliyekutorosha mikononi kwa askari…mimi nimekuchukua ukiwa huna fahamu kutoka mikononi mwa huyo aliyekutorosha kutoka mikononi mwa polisi…sasa huyo ndiye atakayeangukiwa na hilo jumba bovu, si miye. Mimi nimetumwa kuhakikisha kuwa hudhuriki tu. Kama ungeendelea kuwa mikononi mwa polisi hadi mwisho leo hii wala nisingeingilia kati…” Morandi alimjibu kwa kirefu.
Candy alizidi kutoelewa.
“Sasa ni nani huyio aliyenitorosha kutoka mikononi mwa askari…na kwa nini anataka kuniua?” Aliuliza.
Morandi alimtazama kwa muda, na katika muda ule aliona jinsi kutoelewa kwa yule binti kusivyokuwa kwa bandia.
Ina maana ni kweli huyu binti haelewi kinachomtokea?
“Okay. Huu sio wakati wake mrembo wa Kokos Muda ukifika, utatueleza sote kisa chako cha kweli, sio kile cha kisanii ulichowaeleza akina Kokos…” Morandi alimjibu huku akimtazama kwa makini, na akaona yule binti akitembeza macho baada ya kusikia kauli yake ile.
Kweli mtoto aliwadanganya akina Kokos huyu!
Morandi aliwaza baada ya kuona namna Candy alivyotembeza macho kwa kuambiwa kuwa aliwadanganya akina Kokos.
“Nitawaeleza nyote? Nyote na nani?” Candy alihoji.
“Pumzika kwanza mrembo. Umechoka sana wewe.Hapa utakuwa salama kwa muda…ingawa hutakiwi kuwepo hapa kwa muda mrefu sana.” Morandi alimjibu na kutoka pale sebuleni. Alijishugulisha kukomea milango yote ya nyumba ile, kisha akaingia kwenye chumba kingine mle ndani na kumpigia simu Nuru.
“Tumefika eneo la tukio salama bila tukio…vipi wewe?” Alimuuliza.
“Okay good, Mimi niko na Kokos na Bishkuku hapa…nao wameingia hapa kwake muda si mrefu uliopita.” Nuru alimjibu.
“Good. Basi msiuweke hapo…!” Morandi alimwambia na kukata simu.
***
Nyumbani kwa Kokos Nuru aliwatazama Kokos na Bishkuku.
“Okay, Candy yuko salama na Morandi sasa…” Aliwaambia, na Bishkuku akashusha pumzi za ahueni, wakati Kokos akiachia tabasamu la ushindi.
“Good. Mlitupa wakati mgumu kiasi…ingawa nilikuwa najua kuwa mtakuwa mko kwenye usukani wa swala zima hili. Kwa hiyo nini kinafuata?”
Kabla hajajibu simu ya Kokos ikaita. Alikuwa wakili Abiyah.
“Ah! Abiyah! Pole sana kwa misukosuko…uko salama wewe? Uko wapi sasa?” Alimuuliza.
“Hili la kutekwa na kupuliziwa nusu-kaputi sikulisaini kabisa kwenye mkataba wangu na wewe Kokos, so jiandae kuongeza malipo!” Abiyah alimnong’oneza kwa hasira, kisha hapo hapo akaendelea, “Okay, tulitekwa na kupulizia dawa ya usingizi. Sina hakika na Candy, lakini nadhani jamaa zetu wanaye…”
“Yes, Morandi yuko naye…”
“Okay good. Sasa hapa nasubiri kutoa maelezo yangu kwa maaskari halafu bila shaka nitaachiwa. Nini kifuate baada ya hapo?” Abiyah alieleza na kuhoji.
“Nipe niongee naye!” Nuru alidakia, na Kokos akampa simu.
“Okay mkuu wangu wa kazi….hapo nadhani utaulizwa maswali na utatakiwa utoe maelezo kisha watakuachia tu...”
“Ndio hivyo…” Abiyah alimwmbia.
“Basi ukiachwa tu nitakuhitaji pale mlimani city usiku huu huu…utampigia simu Kokos halafu ataniambia. I hope hawatakukawiza sana hapo!” Nuru alimwambia.
“No problem.” Abiyah alimjibu na kukata simu wakati akimuona mmoja wa wale askari walioingia na kuvamia eneo lile akimsogelea.
***
ri walioingia na kuvamia eneo lile akimsogelea.
***
Yule mkuu wa kituo cha polisi cha kati alimtazama wakili Abiyah kwa muda.
“Ulikuwa unaongea na nini hapo?” Alimuuliza.
“Mpenzi wangu.”
Jamaa akamtazama kwa muda zaidi, akataka kuendelea kumsaili kuhusu huyo aliyekuwa akiongea naye kisha akaghairi.
“Ngamao katuambia wewe ni wakili wa mrembo Candy aliyetoweka katika mazingira tata…”
“Ndiyo. Mrembo ambaye ametoweka akiwa mikononi mwa huyo huyo inspekta Ngamao. Nami nataka kujua inakuwaje mteja wangu anatoweshwa kinamna za kisanii namna hii akiwa mikononi mwa polisi!” Abiyah alimjia juu.
Askari mwingine alijiunga na yule Mkuu wa kituo.
“Tutathitaji maelezo ya kina kutoka kwako. Tunataka kujua ni wpai mlikuwa mmepanga kwenda na Candy baada ya kutoka naye pale uwanja wa ndege, na pia tunataka kujua ni wapi Candy anaishi ili tujaribu kwenda kumtafuta huko kwake, na pia tunahitaji kujua ni vipi Candy aliweza kukuajiri kuwa wakili wake akiwa huko Venezuela…”
“Na mimi nimekuwa mtuhumiwa sasa?”
“Kwa mazingira yalivyo na namna Candy alivyotoweka, kila mtu ni mtuhumiwa hapa, jibu maswali wakili!”
“Okay. Tulipotoka uwanja wa ndege Ngamao alikuwa anatupeleka kituo cha polisi, njiani tukapuliziwa gesi ya usingizi na huyo aliyekuwa dereva wetu, ambaye ndio yule mliyemkuta amefungwa nguzoni hapa akiwa ndani ya mavazi ya kiaskari…”
“Hilo haliingii akilini, kama ni yeye ndiye aliyewateka, mbona tumemkuta naye kafungwa…na Candy hayupo, ni nani aliyemfanya hayo?”
“Unaniuliza mimi afande?”
“Wewe ndiye uliyekuwa wa kwanza kuamka hapa, na ndiye uliyepokea simu ya Ngamao tulipokuwa tukimpigia…tuna kila sababu za kukushuku wewe kuhusika na tukio zima hili!”
Abiyah alikunja uso kwa ghadhabu.
“Mnataka kunigeuzia mimi kibao? Itabidi mfanye kazi zaidi ya hiyo…”
“Sio nia yetu, ila ni kazi yetu kuuliza maswali kama hayo mwanadada. Jibu swali!”
“Basi kuhusu hilo inabidi mumuulize huyo Ngamao, maana ye’ ndo anayejuana na yule mtekaji wetu. Nina hakika Ngamao anahusika na tukio hili!”
“Ngamao anajuana na nani…huyu jamaa aliyewateka?” Mkuu wa kituo akamakinika.
“Hujaambiwa? Muulize yule askari wa kike tuliyelazwa naye usingizi humo garini…”
“Naye anajua?” Mkuu wa kituo akazidi kuwa makini.
“Alisikia kila kitu! Ngamao na yule ponjoro koko aliyetuteka lao moja! Na nitamshauri mteja wangu pindi atakapopatikana akiwa hai, tumfungulie mashitaka ya kutumia nafasi yake katika jeshi la polisi kutaka kumdhuru mteja wangu akishirikiana na huyo ponjoro wake!” Abiyah alikuja juu.
Mkuu wa kituo na yule askari mwingine wakatazamana.
“Na kama mteja wangu akipatikana akiwa hana uhai basi mimi mwenyewe nitalifungulia kesi jeshi la polisi kwa kifo chake, maana mmefanya tamasha la kumtia pingu mbele ya kila mwananchi pale uwanja wa ndege, sasa tena atoweke halafu akutwe amekufa…mbona mtatueleza!” Abiyah alizidi kuwatia tumbo joto.
Mkuu wa kituo alimeza funda la mate.
“Una hakika na haya uyasemayo kuhusu Ngamao?” Hatimaye alimuuliza.
“Afande,ongea na Ngamao na huyo askari wa kike. Mtafute mmiliki wa hili eneo naye umsaili..inakuwaje gari la polisi litekwe halafu lije kukutwa kwenye karakana yake. Mimi ni wakili na ninajua wajibu wangu kwenye mazingira kama haya. Sasa niambie…niko chini ya ulinzi au vinginevyo? Ni usiku sana huu na yaliyonikuta mpaka hapa ni mazito. Nahitaji kwenda kumpumzika huku nikiamini kuwa jeshi la poisi litashughulikia upatikanaji wa mteja wangu!” Abiyah alikata mzizi wa fitna kirefu.
Mkuu wa kituo na askari wake walitazamana kwa mara nyingine. Wakamuuliza tena kama anajua anapoishi Candy, akasema hajui. Ilikuwaje Candy alimuajiri yeye kumtetea akiwa kule Venezuela, akawajibu kuwa si Candy aliyewasiliana naye bali ni mfadhili wake, Kokos Wandiba aliyekuwa huko huko Venezuela wakati Candy anakamatwa.
Ukimya ukachukua nafasi kwa muda.
“Okay, uko huru kwenda wakili, ila kesho saa nne asubuhi tutakuhitaji kituoni kwa ajili ya maelezo zaidi au maelekezo zaidi. Tuko pamoja?” Aliambiwa.
“Umeeleweka. Sasa nahitaji kufikishwa barabarani ili nikamate usafiri…au mtanipekea nyumbani kabisa?” Abiyah alisema na kuuliza.
“Hatuna muda huo.” Mkuu wa kituo alimjibu, kisha akatoa amri askari mmoja amfikishe barabarani na ahakikishe amepata usafiri.
Dakika kumi baadaye askari alimuona Abiyah akipanda teksi na akamsikia akimpa dereva maelekezo kuwa ampeleke Kinondoni Block 41. Wakati ile teksi inaondoka, askari alinakili namba za gari lile kama alivyoelekezwa na mkuu wa kituo.
Ambalo hakulijua ni kwamba walipofika Buguruni Abiyah aliteremka na kumlipa yule dereva wa teksi, kisha akapanda bodaboda ambayo aliiamuru impeleke kwenye baa moja maarufu iliyokuwa maeneo ya ubungo external. Aliingia kwenye ile baa na kumaucha mwendesha bodaboda akiondoka zake. Alipoteza dakika kama kumi na tano pale baa, kisha akatoka na kukamata teksi, ambayo aliiamuru impeleke Mlimani City. Akiwa ndani ya ile teksi alimpiga simu Kokos kama alivyokubaliana na Nuru…
***
Nusu saa baadaye, Abiyah alikuwa ameketi ndani ya sebule ya Morandi kule Makongo. Pamoja naye walikuwepo wadau wote wa kadhia ya Candy, yaani Bishkuku, Kokos, Nuru na Morandi mwenyewe. Wote hawa walikuwa wameelekeza macho yao kwa muhusika mkuu wa kadhia ile, mrembo Candy Gamasala, ambaye alikuwa ameketi kwenye sofa la mtu mmoja lililokuwa mbele ya makochi waliyokalia wao.
“Okay jamani, nimeona tukutane wote hapa ili kupata hali halisi ya kadhia hii ya aina yake…” Morandi aliongea.
“Kwa hali ilivyo tuna masaa machache sana ya kulifanya lililo mbele yetu, kwani habari za kutoweka kwa mrembo wa taifa Candy zikizagaa tu mitaani kesho asubuhi, hatutakuwa na uhuru tena wa kufanya mambo yetu. Candy yuko kwenye supu ya moto sana na anaendelea kuchemka kwenye supu hiyo. Amekuwa kwenye matatizo muda mrefu huku akijitahidi kuficha ukweli wa matatizo yake. Mimi na Nuru, kama tulivyoagizwa na bwana mkubwa Kokos the madly in love Wandiba…” Morandi aliendelea, na wote mle ndani waliguna kwa lile jina alilomchomekea Kokos, Candy akimakinika zaidi na neno lile huku akimtupia jicho Kokos.
Morandi akaendelea, “…tumekuwa tukimlinda asikutwe na madhara kutoka kwa watu waliokuwa wanataka kumuangushia, wakiongozwa na jamaa aendaye kwa jina la GTZ…”
“GTZ?” Candy alipayuka ghafla, na wote mle ndani wakamakinika naye, na yeye akaendelea kumuuliza Morandi, “Ndiye huyo ambaye ulisema kuwa anataka kuniua?”
Wote walitazamana mle ndani, na Morandi akamgeukia Candy kwa utulivu.
“Ndiyo Candy, ni GTZ akishirikiana na mwenzake mwenye asili ya kihindi hivi…”
“Oh My God…Greg!” Candy alipayuka tena huku akijishika paji la uso, na kwa mara nyingine wote mle ndani wakatazamana.
“Na huyo pia unamfahamu?” Kokos aliuliza kwa wahka, macho yake yakirukia kwa Morandi na kuyarudisha tena kwa Candy, ambaye alikuwa akiafiki kwa kichwa kuwa hakika alikuwa anawafahamu GTZ na huyo mwenzake huku akiwa ameinamisha uso.
“Ni akina nani hao?” Bishkuku alidakia.
Muda wote wakili Abiyah alikuwa akifuatilia yale maongezi kwa makini, na sasa alidakia.
“Eh, jamani ngojeni kwanza…ngojeni. Ieleweke kuwa Candy anatuhumiwa kwa mauaji na kuwa mimi niliyeteuliwa kuwa wakili wake ndiye ninayetakiwa nimhoji kuhusu haya mambo. Anaweza kuwa na habari za kujitia hatiani huyu, na sitaki ziwe wazi kwa kila mtu hapa kwa ajili ya kunisaidia katika utetezi wangu kwake…”
“Sasa undhani sisi tutaenda kusemea au vipi?” Bishkuku aliuliza kwa ukali.
“Sio hivyo. Kama ana taarifa za kujitia hatiani kuhusuana na tuhuma zinazomkabili, na ninyi mkazijua…basi mtawajibika kisheria kwenda kuziripoti polisi, ama si hivyo nanyi nyote mnakuwa washiriki katika jinai inayomhusu…mnaweza kushurutishwa na mahakama kwenda kutoa ushahidi mahakamani dhidi yake na hamtakuwa na namna…”
“Hilo halipo. Sisi hatuwezi kuwa upande wa mahakama dhidi yake hata iweje! Ni lazima tujue ukweli kuhusu yeye…na Candy lazima awe muwazi kwetu maana tumekuwa pamoja naye tangu huko nyuma tulipojua kuwa kuna mambo anaficha!” Morandi alikuja juu.
“Sasa hiyo ilikuwa kabla hajatuhumiwa mauji Morandi! Hali hii ni tofauti sasa! Ni mtuhumiwa huyu!” Abiyah alibisha, na Candy akadakia.
“Nitaongea kila kitu hapa hapa!”
Kimya kilitanda mle ndani.
“Una hakika Candy?” Abiyah aliuliza, na Candy akamtazama na kuafiki kwa kichwa.
“Okay, twende kazi mrembo. Tupe ukweli sasa!” Morandi alihitimisha huku akimtazama yule mrembo aliyezungukwa na utata mzito.
Na hapo Candy akashusha pumzi ndefu, kisha akaanza kuongea.
***
“Kwanza naomba niwatake radhi sana wafadhili wangu Kokos na Bishkuku…ukweli ni kwamba sikuwa muwazi sana kwenu tangu mwanzo, na kwa hili sitaacha kujilaumu maisha yangu yote yaliyobakia. Kwa namna mlivyonipokea na kunithamini, nilipaswa niwe muwazi zaidi kwenu…lakini nilikuwa nimekumbwa na woga mkubwa wa kutokataka maisha yangu ya huko nyuma yajulikane.” Candy alianza na Bishkuku na Kokos walitazamana.
“Ni kweli kwamba nilikuja hapa mjini nikitokea Magu, lakini si kweli kuwa huko ndiko maisha yangu yalipokuwa siku zote, na si kweli kuwa nilikuwa nikilelewa na walezi ambao walipofariki dunia na jamaa zao walipoanza kugombea mali ndio nikaamua kutorokea huku mjini…
“Ukweli ni kwamba nilikwenda kuishi Magu nikitokea Tarime kwenye nyumba ya watoto yatima, na kule Magu niliishi kwenye jumba la mjane tajiri aliyeitwa Bi. Shakira Swadafu.”
Hapa kila mmoja mle ndani akawa makini.
“Ndiye huyo unayetuhumiwa kumuua?” Abiyah alihoji.
“Sijamuua jamani…hilo ni uzushi mtupu, lakini ndiye huyo. Nadhani mkikisikiliza kisa changu mtajua kuwa sikumuua. Ila sijui kama mikono ya sheria nayo itaniamini juu ya hili!” Candy alimjibu.
Na hapo aliwaelezea kisa chote kilichomtokea tangu kule tarime hadi kule Magu na maisha ya pale kwa Bi. Swadafu.
Alipofikia sehemu alipokuatana na John Koccho kwa mara ya kwanza kule Magu, Nuru alidakia.
“Na huyo ndiye yule jamaa aliyekukurupusha kule Mikumi?”
“Ndiye yeye haswa. Na mpaka sasa sielewi ni kwa nini amekuwa vile, maana yeye ndiye alikuwa mkombozi wangu kule Magu!” Candy alimjibu.
“Ama? Yule jamaa ndiye alikuwa mkombozi wako?” Morandi alihoji.
“Kabisa kaka! Hata sielewi…”
“Endelea…” Morandi alimwambia, na alipofikia siku ile anabakwa na GTZ, Candy hakuweza kuendelea, kilio kikubwa kilimbana.
Abiyah na Bishkuku hawakuweza kuyadhibiti machozi.
Kokos alihisi donge kubwa likimkaa kooni. Akili ilimzunguka na akakumbuka siku ile alipokutana kwa mara ya kwanza na yule binti. Siku alipomuopoa kama changudoa na binti akalia sana kuhofia kufanya naye ngono. Sasa alielewa ni kwa nini alikuwa vile na roho ilimuuma sana. Candy alikuwa ameathirika kisaikolojia kutokana na kubakwa, na kwa vyovyote vile hangeweza kushiriki naye tendo lile katika mazingira yale. Na hapa ilimthibitikia wazi kuwa Candy hakuwa akisema uongo pale aliposema kuwa ile ilikuwa ni mara yake ya kwanza kujiingiza kwenye ukahaba na kwamba hakuwa amewahi kufanya jambo lile hata siku moja. Na yeye alihisi machozi yakimchonyota.
“Unasema kuwa Ngamao naye alijua juu ya kubakwa kwako usiku ule, na bado hakuchukua hatua yoyote?” Morandi alimuuliza kwa hamaniko.
Candy alitikisa kichwa kumaanisha kuwa Ngamao hakuchukua hatua yoyote, huku akiendelea kulia.
Muda ulipita wakati akina Bishkuku wakimbembeleza yule binti. Na baada ya hapo akaendelea kutoa sehemu ya mwisho ya kisa kilichomkuta Magu, na wakati anasimulia, Candy alijisahau kabisa kuwa alikuwa jijini Dar es Salaam mbele ya watu wachache waliokuwa upande wake katika kisa kile cha maisha yake. Akili yake ikamridisha kule Magu,miaka miwili nyuma, na kwenye matukio yaliyofuatia ule usiku mbaya kabisa maishani mwake, matukio yaliyofuatia ule usiku ambao GTZ alimbaka…
Kumbukumbu ya majibizano ya mwisho kati yake na Bi. Swadafu na wanawe ikamrudia kama kwamba ndio ilikuwa imetokea jana yake tu.
Kama ningekuwa wewe ningekuwa makini sana na huyu mtoto…anaonekana ni hatari sana…kigoda kingetawanyikia kisogoni kwako hicho kama sikuwahi kumzuia…!
Greg Pasha huyo.
Ulitaka kuniua mimi wewe?
GTZ huyo, huku akimtazama kwa hasira.
Sasa na we’ uliyonifanyia ni mazuri? Nataka nikuue wewe na mama yako, wanyama wakubwa nyie!
Naye akafoka.
Ah! Anasemaje kisonoko huyu…?
Bi. Swadafu mwenyewe huyo.
Ngamao akaingilia kati naye akaenda kujifungia chumbani kwake huku akilia kwa uchungu…
***
Alilia usiku kucha. Asubuhi ya siku iliyofuata hakuweza kufanya lolote. Akili yake ikiwa imezongwa na mawazo na moyo wake ukiwa umegubikwa na uchungu usiosemeka, alibaki akiwa amejifungia chumbani kwake mchana kutwa,hadi alipokwenda kutolewa kimabavu na Bi. Swadafu, akilazimishwa kwenda kuosha vyombo.
Roho ilimuuma.
“Hivi kweli mama mimi nafanyiwa kitendo kama hiki nyumbani kwako na wewe unaunga mkono tu?” Alimuuliza huku akibubujikwa machozi.
“Usinichulie mimi saa hizi. Osha vyombo huko! We ulitarajia nini kujipitisha-pitisha mbele ya mtoto wa kiume namna ile?” Bi. Swadafu alimjibu kwa fidhuli.
Jibu lile lilimchoma moyo vibaya sana, na kwa mara nyingine alitamani yule mama aanguke chini na kufa pale pale.
“Ah! Kama mimi nilijipitisha hivyo usemavyo mbele ya mwanao basi Mungu atanijibia…lakini si kweli usemayo. Mwanao amenidhulumu haki yangu kwa tamaa zake za kihayawani tu! Sasa kama ameniambukiza ukimwi mimi nitakuwa mgeni wa nani tena duniani hapa?”
“Hiyo hainihusu. Mtajijua nyie wenyewe na balaa lenu!” Bi.Swadafu alizidi kuwa kiburi.
“ Ah! Sawa. Kwa kuwa mi’ mnyonge na sina wazazi wa kunitetea. Basi angalau nirudishe uliponitoa we’ mama…mimi sitaki tena kukaa hapa!” Candy alimlilia kwa kuomboleza.
Jibu la bi mkubwa yule lilikuwa ni msonyo mkali sana, kisha akaingia ndani na kumwacha pale pale uwani akilia pekeyake.
Candy alijikunyata chini ya mti huku akilia. Alijiona kuwa amedhalilishwa kwa kiasi kisichosemekana. Hakuwa na nguvu ya kuosha vyombo wala kufanya lolote zaidi ya kulia.
Kulia kulikuwa ni kama liwazo fulani kwake sasa.
“Heeeyy, mtoto shoo…ni nini kilichokukuta tena jamani? Mbona unalia peke yako huku uwani?” Sauti ya mnong’ono ya John Koccho ilimfikia, naye akakurupuka huku akijifuta machozi, akimtazama kwa woga mkubwa yule mchunga ng’ombe wa Bi. Swadafu.
Kwa namna Fulani kiumbe chochote chenye jinsia ya kiume kiliondokea kuwatishio kubwa sana kwake.
“Ham…hamna kitu kaka John….niache tu!”
“Ahh! Nikuache vipi Candy katika hali kama hii mtoto shoo? Niambie ni nini kimekusibu…naweza kuwa na msaada…”
Candy akapata matumaini kidogo.
“Kweli kaka John? Unaweza kunisaidia?”
“Of course! Mimi na wewe sote ni watafutaji tu hapa mtoto shoo, kwa nini tusisaidiane?”
“Basi mi’ nataka kuondoka hapa kaka John…kwa gharama yoyote ile mi’ nataka kuondoka kwenye hili jumba la madhalimu wenye roho mbaya na wabakaji waliobobea…!” Candy alisema kwa hasira, na Koccho akamakinika.
“Wabakaji?”
Candy akalia upya.
“Umebakwa humu ndani?” Koccho akamuuliza tena na safari hii Candy akaafiki kwa kichwa, huku akizidi kulia.
“Oh, Mungu wangu…GTZ huyo…atakuwa ni yeye tu mkware mkubwa!” Koccho alisema kwa hisia.
“Ndiye kaka John, ndiye! Naomba unisaidie niondoke kwenye jumba hili tafadhali. Wamenizuia kuondoka na siwezi kwenda polisi kwa kuwa huko nitakutana na Ngamao tu, ambaye yuko upande wao…”
Kimya kilitanda kwa muda. Koccho akaangalia huku na huko kuhakikisha kuwa hakukuwa na mtu anayewaona au anayewasikiliza.
“Usijali mtoto shoo. Hukutakiwa kufanyiwa hivyo kabisa…na hawa watu huwezi kushindana nao kwa kweli. Wameshika kila nyanja muhimu hapa mjini, kuanzia hao maaskari hadi huko kwenye mahospitali na serikali za mitaa. Niulize mimi. Usidhani mi napenda kuendelea kuwa nachunga ng’ombe tu hapa mpaka leo…sina hamu jinsi walivyonifanya hawa watu!”
Candy akawa makini.
“Na wewe wamekuzuia kuondoka hapa? Na umekubali?” Aliuliza kwa mshangao. Koccho aliguna na kutikisa kichwa kwa masikitiko.
“Sijalipwa mshahara mwezi wa sita huu sasa. Nilipokwenda serikali ya mtaa kulalamika ndio nikaona nguvu ya hawa jamaa. Siku za nyuma nilipata ajali ya kushambuliwa na mmoja wa ng’ombe zao wakati nawaongoza kwenda malishoni. Nikalazwa hospitali wiki mbili. Jamaa wakadai eti gharama za matibabu waliyonitibia ni zaidi ya mshahara wangu wa mwaka mmoja, hivyo niendelee kufanya kazi tu hapa bila malipo yoyote hadi hizo gharama zao zifidiwe. Msaada wao kwangu ni kuwa niwe nakula bure na kulala bure tu hapa kwao. Ulishawahi kusikia uonevu kama huo motto shoo?” Koccho aliongea kwa uchungu. Candy alichoka.
“Hah! Hivi hawa ni watu wa aina gani lakini kaka John, eenh?”
“Hao ndio matajiri mdogo wangu…miungu wa duniani hao!”
“Heh, ama kweli duniani kuna mambo. Mi’ nataka kuondoka haraka sana humu ndani kaka John…” Candy alisema.
“Basi mi’ n’takusaidia, Candy!” Koccho alisema kwa kujiamini.
“Kweli kaka John…?”
“Of course mtoto shoo…”
“Oh, n’tashukuru sana yaani…”
“…lakini na wewe itabidi unisaidie vile vile!” Koccho alinong’oneza huku akimtazama kwa makini, na Candy akahamanika.
“Nikus…na wewe pia?” Aliuliza huku akimtazama yule jamaa kwa kutoamini.
John Koccho alimtazama kwa sekunde kadhaa bila ya kumjibu, na ndani ya sekunde zile mawazo kadhaa, yote mabaya, yalipita kichwani kwa Candy.
“Sikiliza mtoto shoo…unataka msaada wangu nami nataka wako. Unajua mahala funguo za nyumba zinapokaa?”
Candy hakuelewa.
“Unataka nikutajie hilo ndio uwe msaada wangu kwako?”
“Unapoteza muda…tukikutwa hapa itakuwa balaa. Unajua zinapokaa?”
“Ndio…Bi. Swadafu huwa analala nazo chumbani kwake, za akiba huwa anakuwa nazo GTZ…”
“Okay…na Bi. Swadafu akiingia chumbani kwake huwa anajikomea kwa ndani?”
“Mnh! Hapana…maana siku nyingine huwa ananiita akiwa ameshaingia humo chumbani na kutaka aidha nimpelekee maji au hata mipombe yake, mwenyewe akiwa amejilaza kitandani…huwa naukuta mlango wazi…”
“Good. Sasa siku atakayokuwa amelewa vilivyo na akiwa peke yake, nataka uingie uchukue ule ufunguo na ufungue huu mlango wa mbele, kisha uje kule bandani kwangu, usiku huo huo unishtue. Ukinisaidia hilo, nami nitakutorosha humu ndani usiku huo huo. Kazi kwako!” Koccho alimjibu kisha bila kusubiri kauli au maswali zaidi kutoka wa Candy aliondoka haraka eneo lile huku akipiga mbinja.
Candy alishusha pumzi za ahueni.
Kumbe msaada wenyewe ni huo tu!
Hakika alidhani Koccho naye anataka alipwe ngono ili amsaidie.
Lilikuwa ni sharti gumu, lakini kwa jinsi alivyotaka kuondoka kwenye jumba lile la maadui, wala hakujufikiria zaidi swala lile.
Alikuwa makini kuisubiri hiyo siku ya siku, akiugulia machungu yake moyoni huku akiendelea kutumikishwa kama punda pale kwa Bi. Swadafu.
***
Siku tatu baada ya tukio la kubakwa kwake, Greg Pasha alimuaga mama yake na kwenda jijini Dar kuendesha maisha yake huko. Ni siku ambayo alimwona Bi. Swadafu akiwa na simanzi sana. Siku mbili baadaye Bi. Swadafu alirudi nyumbani kutoka kwenye sherehe akiwa amelewa chakari, na Candy akajua kuwa ile siku aliyokuwa akiisubiri ilikuwa imewadia.
Alipoenda kuosha vyombo vya chakula cha usiku ule, alipitiliza hadi kwenye banda ambalo Koccho huwa anaishi, mbali kidogo na lile jumba kuu.
“Leo amelewa…tufanye kile kitu?” Alimuuliza kwa mashaka.
Koccho alionekana kumakinika na ile taarifa.
“Yes. Nafasi haziji mara mbili mbili mrembo…mpe muda alale, kisha fanya vilivyo ndivyo!” Koccho alimjibu.
Saa sita usiku Candy alinyata hadi chumbani kwa Bi. Swadafu na kufanya alivyoagizwa, kisha akanyata kule nje na kumshitua Koccho.
“Tayari! Twende!” Alimwambia, huku akiwa ameshabeba begi lake. Koccho alifanya mambo haraka haraka. Alimuongoza hadi kwenye kona ya wigo wa jumba lile na kumwambia amsubiri pale, kisha akageuka na kuanza kuelekea kule kwenye jumba la Bi. Swadafu.
“Unaenda huko tena? Tunachelewa!” Candy alimnong’oneza kwa ukali.
“Nisubiri!” Koccho alimnong’oneza kisha akatoka mbio za kunyata kuelekea kule kwenye jumba la Bi. Swadafu.
Candy alijikunyata pale kwenye kona ya wigo wa jumba lile akiwa na wasi wasi mkubwa.
Dakika zilipita. Kumi, kumi na tano…na Candy akazadiwa na wahka.
Ghafla akasikia kama ukelele kutokea kule kwenye jumba, na hapo hapo mbwa wa nyumba ya jirani akaanza kubweka.
Oh, My God, huyu John vipi tena…?
Mara alisikia kishindo nyuma yake na akaruka huku kiyowe kidogo kikimtoka.
“Twen’zetu mtoto shoo…!” Koccho alimnong’oneza. Wala hakumuona alipotokea.
“Ulikuwa wapi? Mbona uko hivyo?”
Koccho alionekana mwenye wahka mkubwa, mkononi alikuwa ameshika kifurushi kidogo. Badala ya kumjibu, alimuongoza kwenye kichaka kilichokuwa kwenye ile kona ya ule wigo ambako kulikuwa kuna tobo la kuweza kupenya na kutokea nje ya wigo ule wa ukuta mkubwa wa jumba la Bi. Swadafu.
“Ng’ombe wangu siku nyingine huwa wanapenya hapa…na hakuna ajuaye. Twende sasa mrembo!” Koccho alimwambia.
Na usiku ule John Koccho alifanikiwa kumtorosha kwa Bi. Swadafu. Walitembea kwenye njia za pembezoni hadi kwenye sehemu ambako kulikuwa kuna mnada wa n’gombve na mbapo pia ng’ombe huwa wanasafirishwa.
Alimpandisha lori la mmoja wa marafiki zake waliokuwa wakifanya biashara za kusafirisha ng’ombe kwenda maeneo mbali mbali nchini, kutokea pale Magu. Pamoja naye kwenye lile lori,walikuweko akina mama wengine wawili pamoja na mtoto mmoja. Candy alijiona salama kiasi.
“Okay, Mtoto shoo. Umenisadia, nimekusaidia. Huyu jamaa ni mtu safi. Anaelekea Mwanza mjini. Ukifika huko ni juu yako…tutaonana mungu akipenda!” Koccho alimwambia.
“Ah, ahsante sana. Sasa…wewe je?” Candy alihoji.
Koccho akamsukumia noti ya shilingi elfu kumi mkononi.
“Kamata hii hela mtoto shoo…. Mimi sirudi tena kule. Nimekuwa nikifanyishwa kazi na kurushwa mshahara kwa miezi sita sasa. Sio siri, mi’ nimemuibia yule mshenzi na sirudi tena huko!” Koccho alimwambia kwa hasira.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Candy alibaki akimshangaa huku akiwa ameishikilia ile elfu kumi mkononi.
Lori lilianza safari, naye akabaki akimtazama Koccho akiwa amesimama na kifurushi chake mkononi mpaka alipopotea kabisa kwenye upeo wa macho yake…
***
“Na hiyo ndiyo ilikuwa mara yangu ya mwisho kumuona John Koccho kule Magu miaka miwili nyuma ndugu zangu…kabla hajaniibukia kivingine kabisa kule mikumi wiki chache zilizopita.” Candy alimalizia kisa chake, na wote mle ndani walibaki kimya kwa muda.
“Ile elfu kumi ndio iliyonisaidia hadi nikafika hapa Dar. Niliomba msaada kwenye basi la Mwanza - Dar, nikijua kuwa ile hela haikutosha kwa nauli. Kondakta aliichukua yote ile hela. Nilikuwa na kama elfu mbili na mia tano nilizotoka nazo kule kwenye nyumba ya watoto yatima…siku zote ilikuwa kwenye begi langu. Ile ndiyo iliyonifikisha Manzese…kwa rafiki yangu Jackie ambaye tulikuwa naye wote kule kwenye nyumba ya watoto yatima, na ambaye kisa chake nimeshawaelezea. Lakini pamoja na hayo yote niliyowaeleza ambayo ni kweli tupu, mimi sikumuua Bi. Swadafu jamani!” Aliongezea.
“John Koccho ndio muuaji. Hilo liko wazi kabisa!” Morandi Gwaza alihitimisha, na kila mtu mle ndani alitikisa kichwa kuafikiana naye.
“Sasa kwa nini alimuua? Mi’ sikujua kabisa kama alikuwa na nia hiyo!” Candy alimaka.
“Hilo si kazi yetu. Kazi yetu ni kukuvua wewe kwenye hili balaa lililokuangukia!” Wakili Abiyah Byabato alimjibu huku akinekana kuwa na mawazo mazito kichwani mwake. “Kivipi sasa? Tunamvuaje Candy kwenye tuhuma hizi baada ya kusikia kisa chote hiki?” Kokos aliuliza kwa mashaka makubwa.
“Nadhani hapa ndio mahala ambapo umahiri wa Abiyah unapohitajika! Sisi…mi’ na Mo tumeshafanya yote yaliyokuwa ndani ya uwezo wetu mpaka kufikia hapa.” Nuru alidakia.
“True!” Kokos na Morandi waliafikiana naye kwa pamoja, kisha macho ya wote mle ndani yakamgeukia wakili Abiyah Byabato, ambaye bila kusita akachukua nafasi yake.
“Yah, hii ni kesi ngumu kama haiko kwenye mikono makini, lakini pia ni nyepesi sana kwa mtu makini…” Abiyah alianza, na Kokos akadakia.
“Na ndo maana nikasisitiza upewe wewe hii kesi Abiyah…”
Abiyah alimkata jicho lakini hakumjibu, akamgeukia Morandi Gwaza.
“Nakubaliana na wewe Mo, kuwa hatuna muda mrefu sana wa kuendelea kuwa na Candy humu ndani. Baada ya kusikia kisa chake, tayari nimepata namna kadhaa za kuishughulikia hii kesi, ila ningependa kujua wewe na Nuru mmegungudua nini zaidi kuhusu huyu Koccho na hawa akina GTZ ambao sasa naelewa kuwa mlikuwa mkiwafuatilia muda wote huu wakati Candy anashiriki mashindano ya urembo hapa nchini na kule Venezuela…”
Morandi na Nuru walitazamana, kisha Morandi akaeleza kwa kifupi juu yale aliyoyabaini kutoka kwa GTZ siku ile alipommong’onyoa kokwa la goti kule Mabwepande, kisha akaongelea juu ya mikabala yao miwili na John Koccho, na akamalizia na habari juu ya ule ugunduzi wake wa alama za vidole za yule mtu alizozipata kutoka shavuni kwa Nuru alipozabwa kofi na Koccho kule Mlimani City usiku Candy alipotawazwa urembo wa taifa.
“Hmnn, inazidi kuwa tamu hii. Kwa hiyo tunachohitaji sasa ni kuoanisha alama za vidole za John Koccho na za muuaji wa Bi. Swadafu, kama zipo…” Abiyah alisema.
“Haswa! Tatizo taarifa tulizonazo ni kwamba polisi wana alama za vidole za muuaji wa Bi. Swadafu, lakini hawamjui mwenye alama za vidole vile ni nani! Ni sisi hapa sasa hivi ndio tunaojua kuwa alama walizonazo ni za Koccho…” Morandi alisema.
“Mnh! Mo…kumbuka kuwa tuligundua kuwa rekodi za alama za vidole za John Koccho zipo polisi, ila utambulisho wa muhusika wa zile alama za vidole umefichwa, na hautatolewa mpaka liingizwe neno maalum la siri, yaani “password” kwenye mtandao wa rekodi za kipolisi ndio utambulisho upatikane. Huoni kuwa huyu askari mwenye password ya kuzibainisha taarifa hizi lazima atakuwa anajua kuwa muhusika ni Koccho?” Nuru alidakia.
“Kama ingekuwa hivyo unadhani Ngamao angekuwa anahangaika na Candy mpaka leo kisura wangu? No. Nimepata muda wa kulitafakari kwa kina hili swala, maana ndilo lililokuwa likinipa taabu sana kulielewa. Hawa hawamjui muuaji, ndo maana Ngamao kang’ang’ana na Candy tu, akiamini kuwa ndiye muuaji kutoka na mazingira ya kutoweka kwake pale nyumbani kwa Bi. Swadafu usiku ule ule ambao yule mama aliuawa…” Morandi alimjibu.
“Hiyo kitaalamu tunaita “circumstantial evidence”…” Abiyah alidakia.
“Yaani ushahidi wa kimazingira tu, ambao huwa hauna nguvu pindi ukipatikana ushahidi halisi!” Kokos alidakia kwa jazba.
“Sasa huo ushahidi halisi ndio upi?” Candy alihoji.
“Ushahidi kama huo kuwa alama za vidole vya muuaji wa Bi. Swadafu kwa hakika ni alama za vidole vya John Koccho!” Abiyah alifafanua.
“Heh ama hakika huu ni msongamano wa mambo! Yaani kumbe huyu khanithi Kijambia ametunyima urembo wa dunia kwa ushahidi wa kufikirika tu(akamtukania mama yake)?” Bishkuku alisema kwa hasira ya kukata tamaa.
Wote mle ndani walitikisa vichwa kwa masikitiko.
“Okay Abiyah, tunafanyaje sasa?” Kokos aliuliza hatimaye.
Kwa dakika zipatazo ishirini baadaye wakili Abiyah Byabato akatoa maelekezo fasaha juu ya nini kifanyike. Kwisha kufanya wote wakatawanyika kutoka kwenye nyumba ile, Morandi akiwa wa mwisho kuondoka akibaki kufunga milango ya nyumba yake.
***
Muda wote wakati Candy akitoa maelezo ya kisa chake mbele ya “jopo” la akina Morandi, na kabla wakili Abiyah hajavunja mjumuiko wa jopo lile usiku ule kwa kutoa maelekezo fasaha kwa kila mmoja wa mjumuiko akiwemo Candy mwenyewe, kule kituo cha polisi cha kati mambo yalikuwa ni magumu sana kwa Inspekta Ngamao Kijambia.
“Unaniambia kuwa huyu jamaa aliyeteka gari la polisi na wewe ukiwemo unamfahamu Ngamao?” Mkuu wa kituo alimuuliza tena ili kujihakikishia kile ambacho alishakisikia awali kutoka kwa Abiyah na pia kutoka kwa yule askari wa kike aliyeandamana na Ngamao kule uwanja wa ndege.
“Ndiyo afande…sikutegemea kabisa kama angefikia hatua ya kufanya hivi, lakini…”
“Fafanua Inspekta! Ni vipi unajuana naye?”
“Ni mtoto wa marehemu Shakira Swadafu, mtu ambaye aliuawa na Candy Gamasala afande!” Akiwa hana namna, Ngamao alijibu kwa kukata tamaa kukubwa kabisa. Hakuweza kabisa kumvua Greg kwenye kadhia ile iliyokuwa inaelekea kumharibia mafao yake ya uzeeni katika jeshi la polisi. Mkuu wa kituo alitupa mikono hewani kwa kuhamanika.
“Sasa unajua yule wakili ana mpango gani na jeshi la polisi? Kutushitaki kwa uzembe…na kukushitaki wewe binafsi kwa kuhusika na kutoroshwa kwa mteja wake Ngamao...una nini la kutuambia juu ya hilo?”
Ngamao akameza mate.
“Afande…Candy ni muuaji, hilo halina mjadala…na ndio maana ametoroka!”
“Ametoroka ametoroshwa? Tena akiwa mikononi mwako. Swala hapa ni yuko wapoonekana ni msala mkubwa sana kwa jeshi la polisi, na mimi sibebi msalaba huo!”
“Sijui afande! Lakini nina hakika ni yule yule jamaa aliyenizuia nisimuweke chini ya ulinzi kule hotelini ule usiku Candy alipoondoka nchini kwenda Venezuela atakuwa anhusika“
”Mtu ambaye hana sura! Ngamao uko kwenye matatizo, tena matatizo makubwa. Una ushahidi wowote kuwa ni Candy ndiye…”
“Afande kuna alama ya wazi ya vidole vya muuaji wa Shakira…Bi. Swadafu! Ninachohitaji ni kumpata Candy na kumchukua alama za vidole vyake tu!”
“Jambo ambalo limeonekana kuwa gumu sana kwako mpaka sasa!”
Ngamao akauma midomo na kukunja uso.
“Afande kuna alama ya wazi ya vidole vya muuaji wa Shakira…Bi. Swadafu! Ninachohitaji ni kumpata Candy na kumchukua alama za vidole vyake tu!”
“Jambo ambalo limeonekana kuwa gumu sana kwako mpaka sasa!”
“Nahitaji nafasi nyingine ya kuweka wazi ushahidi kuwa ni yeye ndiye muuaji Kamishna…”
“Nafasi ngapi tena upewe Ngamao? Mtu mpaka tumefikia hatua ya kumtia yule binti chini ya ulinzi ughaibuni huko! Na habari zinasemekana kuwa alikuwa anelekea kuleta taji nchini yule mtoto for crying out loud, Ngamao…una hakika na hizo shutuma zako kweli wewe? Maana hii ni skendo kubwa sana inanukia…utatakiwa ukajieleze kwa wakubwa huko. Mimi kazi yangu ni kumtafuta Candy na kumweka tena chini ya ulinzi akiwa salama tu sasa!” Mkuu wa kituo alikuwa anafoka, na hapo askari wa kike, Konstebo Happiness, aliiingia mle ofisini.
“Samahani afande…tumeshamtambua mmiliki wa ile karakana ambamo akina Inspekta hapa walikuwa wamepelekwa baada ya kutekwa…” Yule askari alisema huku akimtupia Ngamao jicho la pembeni.
Ngamao na Mkuu wa kituo wakawa makini.
“Okay, ni nani huyo, na kwa nini mpaka sasa hajafikishwa hapa kituoni?” Mkuu wa kituo aliuliza kwa kisirani kikubwa.
“Er, ndio kwanza tumeligundua hilo afande…Tuliona tukufahamishe kabla hatujachukua hatua…”
“Hatua ziko wazi Kontebo! Huyo ni wa kutiwa ndani moja kwa moja. Lazima atakuwa anahusika tu!” Mkuu wa kituo alifoka.
“Ni nani huyo…?” Ngamao naye aliuliza.
“Anajulikana kwa jina la Gino Tzaspaparos afande, na…” Konstebo Happiness alijibu na Ngamao akaachia mguno wa fadhaa.
Mkuu wa kituo akamgeukia.
“Vipi Inspekta? Usiniambie kuwa na huyo pia unamfahamu!”
“Oh, my God! Hawa watoto wamekuwaje lakini jamani?” Ngamao alijisema kwa fadhaa kubwa.
“Unaongea vitu gani wewe lakini?” Mkuu wa kituo alisaili kwa kukereka.
“Huyo ni mtoto mwingine wa marehemu…”
“Oh, Shiit!” Mkuu wa kituo alilaani na kutazama pembeni.
Kimya kilichukua nafasi mle ndani kwa muda, kisha mkuu wa kituo akafoka huku akiibamiza meza yake kwa kiganja cha mkono wake.
“Kamaata huyo naye na weka ndani, bloody fool!”
Konstebo Happiness alitoka mbio nje ya ofisi ile.
Mkuu wa kituo akamtupia Ngamao jicho kali.
“Kama hukuwa umekuja kwangu kwa maelekezo kutoka ngazi za juu haki ya mungu mimi mwenyewe ningekuweka ndani sasa hivi Ngamao!” Alimwambia kwa hasira. Ngamao alibaki akimtazama kwa kukata tamaa tu.
“Toka mbele ya uso wangu Inspekta. Nampigia simu mkuu kumpa habari zako bloody bwege wewe…”
“Naomba tuheshimiane afande!” Ngamao alimjia juu mkubwa wake.
“Uheshimike kwa kipi wewe? Nakurudisha kwa mkuu aliyekupa mamlaka ya kumkamata Miss Tanzania…yeye ndio atajua akuchulie hatia gani baada ya kusikia madudu yako na hao watoto wa huyo marehemu!”
Ngamao akapandwa hasira, lakini hakuwa na nguvu ya kujibu mapigo tena, GTZ na Greg walikuwa wamemtumbukiza kwenye dimbwi zito la kashfa isiyofutika. Aliinuka na kuanza kutoka nje ya ofisi ile, akiwa mtu aliyeshindwa. Muda huo simu ya mkuu wa kituo ikaita. Mkuu yule aliipokea wakati Ngamao akiendelea kutoka nje ya ile ofisi yake.
“WHAAAAT?” Ngamao alimsikia mkuu wa kituo akimaka kwa kutoamini nyua yake, na akageuka kumtazama.
“Una hakika?” Mkuu wa kituo aliuliza tena kwenye simu, macho yakiwa yamemtoka pima. Ngamao akawa makini zaidi, moyo ukimuingia woga mkubwa.
“Okay. Ashikiliwe hapo hapo Inspekta…natuma vijana sasa hivi!” Mkuu wa kituo alitoa amri simuni na kukata maongezi na yule mtu aliyepiga ile simu.
Akamgeukia Ngamao aliyekuwa amesimama mlangoni akimtazama.
“Huyo alikuwa afisa wa zamu wa kituo cha polisi msimbazi. Candy Gamasala amejiwasilisha mwenyewe pale kituoni!” Mkuu wa kituo alimwambia Ngamao huku akiwa amejawa na mshangao usoni.
“Niachie nikamkamate afande!” Ngamo alisema kwa pupa.
“No way! Kaa mbali na Candy kwa sasa wewe! Umeshaambiwa mtu kajisalimisha mwenyewe kituoni, sasa ukamkamate wapi!” Mkuu alimjibu bila haya, na hapo hapo akatuma askari watatu, akiwemo Konstebo Happpiness, kwenda kituo kidogo cha polisi mabatini maeneo ya sinza kumchukua miss Tanzania Candy Gamasala na kumfikisha pale kituo cha polisi cha kati.
Ilikuwa ni saa nne tangu Candy ashuke nchini kutoka Venezuela…
***
“Hebu rudia tena maelezo yako bibiye, maana naona kama unatuchanganya tu hapa!” Mkuu wa kituo alikuwa akimuuliza Candy kiasi cha saa moja baadaye. Usiku ulikuwa umesogea na sasa ulikuwa unataka kuupisha wakati wa asubuhi ili uchukue nafasi. Baadhi ya majogoo yenye viherehere yalikuwa yameshaanza kuwika ingawa asubuhi yenyewe ilikuwa haijashamiri ipaswavyo.
Candy alionekana kuchoka sana, na aliachia mwayo mrefu kabla ya kujibu.
“Samahani afande…ni sehemu gani ya maelezo yangu ambayo hukuielewa? Ningeomba niitiwe wakili wangu tafadhali!” Candy alimjibu, na yule mkuu wa kituo pamoja na askari wake wawili walitazamana.
Inspekta Kijambia alikuwa ameketi kwenye kona mle mle ofisini lakini hakuruhisiwa kabisa kutia neno na yule mkuu wa kituo ambaye alikuwa amemzidi cheo na mamlaka pia.
“Anza upya! Na hii habari ya kung’ang’ania wakili wako awepo inakusidiwa kututishia au kitu gani?” Mkuu wa kituo alihoji.
“No…mi nakumbuka niliposhuka pale uwanja wa ndege wakili wangu aliniambia kuwa nisijibu maswali yoyote bila ya yeye kuwepo…sasa mbona nyie mnanishinikiza kwa maswali?”
“Huelewi. Ssis hakuhoji kuhusu tuhuma za mauaji zilizopo dhidi yako…tunakuhoji kuhusu tukio zima la kutoweka kwako kimaajabu na kujirudisha kwako mwenyewe mikononi kwa sheria kimaajabu pia…sasa hilo nalo mpaka uitiwe wakili? Rudia maelezo!” Mkuu alimkoromea.
Candy akashusha pumzi ndefu na kujiinamia. Akilini alikumbuka maelekezo fasaha ya wakili wake Abiyah.
Umeshaonesha kuwa una uwezo mkubwa wa kudanganya Candy. Sasa kama uliweza kuwadanganya akina Kokos na Bushkuku ambao ni wafadhili wako sidhani kama itakuwa taabu kwako kusema uongo kwa wale maaskari utakapokwenda kujisalimisha. Yaani kunusurika kwako na kesi hii kunategemea sana umahiri wa kusema uongo katika hili…sikwambii kuwa uongo ni mzuri Candy, lakini huu wa sasa ni uongo wa kunusuru nafsi yako Candy, kwa hiyo danganya kwa nguvu zote. Ukitetereka tu nitakuwa na kazi ngumu sana ya kukuvua shutuma za kushiriki njama za kutoroka na pia itakuwa vigumu kwa akina Morandi kuficha uhusika wao kwenye kisanga chote hiki!
Aliinua uso wake na kumtazama moja kwa moja machoni yule askari, na kurudia maelezo yake. Alirudia kuwaambia wale askari kuwa yeye ndiye alikuwa wa kwanza kuzinduka kutoka kwenye ule usingizi wa madawa, na alishangaa sana kujikuta akiwa amelaliana na Inspekta Kijambia mle garini. Wazo lake la kwanza ni kuwa wenzake wote walikuwa wmaekufa na hakujua ilikuwaje hata wakafa namna ile. Na wakati anapitiwa na mwazo hayo akasikia vishindo huko nje ya gari. Ndipo alipoona watu wawili wakipigana vikali sana, na wengine wakiwa wamelala chini…hakujua kama walikuwa wamekufa au wazima.
“Sasa nd’o nakuuliza tena, hao watu waliokuwa wakipigana ni akina nani?” Mkuu alimkatisha.
“Afande, kama nilivyokwambia, mmoja wao nilimtambua kabisa kuwa alikuwa Greg Pasha ambaye nilimjua kutokea kule Magu nilipokuwa naishi zamani, ila yule mwingine alikuwa amejiziba sura kwa soksi hivi…sikuweza kumtambua!” Aliongopa motto wa kike.
“Ah, come on! Una hakika wewe?” Mkuu alimjia juu na kule alipokuwa Ngamao, ambaye aliomba abaki kusikiliza tu mahijiano yale, alidakia,
“Muongo huyo!”
Hakuna aliyemtilia maanani.
“Nina hakika kuwa yule mtu alikuwa amejiziba sura. Mi’ nikakimbia nje ya jengo lile bila kujielewa. Hakika niliogopa sana na nilikuwa naamini kabisa kuwa Greg ndio alikuwa amewaua wale watu na kuwa angekumuua na yile mtu aliyekuwa akipigana naye, kisha angekuja kunuia na mimi…nikakimbia!”
“Kutoka Vingunguti mpaka Msimbazi?” Mmoja wa wale askari waliokuwa na mkuu wa kituo alihoji.
“Hapana jamani. Nilikimbia hadi barabarani. Huko nikadandia pikipiki hadi kariakoo mtaa wa Aggrey nilipokuwa naishi na Bishkuku. Pale nikakuta nyumba imefungwa nikashindwa kuingia ndani. Hela ya kumlipa dereva wa bodaboda sikuwa nayo…ndio nikaona niende polisi msimbazi! Pale nikamuomba yule askari anilipie nauli kwa dereva wa boda boda…nikamwambia kuwa nitamlipa wakili wangu akija. Nikamwambia mimi ni Miss Tanzania. Ndio yeye akapiga simu huku kwako. Huo ndio ukweli jamani. Sasa naomba niitiwe wakili wangu please! N’na usingizi na nimetishika na nimechoka sana!”
Candy alihitimisha.
Mkuu wa kituo alimtazama kwa muda mrefu.
“Utadanganya hapa lakini ujue mahakamani kila kitu kitajulikana…hebu mpigieni simu yule wakili wake huyu!” Mkuu alishurutisha.
“Hapana, nadhani tungemchukua alama zake za vidole kwanza afande!” Ngamao alidakia. Mkuu wa kituo alimkata jicho kali sana, lakini hakumjibu.
“Peleka mahabusu huyu mpaka wakili wake afike hapa!” Mkuu wa kituo alimwamuru Konstebo Happiness.
Huku akimtupia Ngamao jicho la pembeni, Candy alipelekwa mahabusu.
Huko nje, jogoo alisikika akiwika.
***
Abiyah aliingia kituo cha polisi akiwa ndani ya pajama, uso ukiwa umemhamanika vilivyo.
“Yu-wapi mteja wangu afande, na…is she okay?” Alisaili bila salamu alipoingia pale kituo cha polisi cha kati jijini, mishale ya saa tisa na nusu za usiku. Alionekana wazi kuwa alikuwa ametoka kulala, ingawa lililokuwa moyoni mwake lilibaki kwake mwenyewe.
Mkuu wa kituo alionekana kuwa amechoka sana. Alishusha pumzi ndefu na kujiegemeza vizuri kitini kwake
“Mteja wako, ambaye pia ni mtuhumiwa wetu, yuko salama.”
“Nahitaji kuonana naye…”
“Si ndio maana tumekuita?” Jamaa lilimjibu huku likimtazama kwa makini. Kwenye kona ya ofisi ile Ngamao Kijambia bado alikuwa amejibanza kitini akiwa amekunja nne. Abiyah Byabato alijitahidi sana kutomtazama yule jamaa, kwani kwa taarifa alizozipata kutoka kwa Candy kuhusiana naye, hakujiamni kabisa kumtazama bila kumuonesha kuwa kuna mambo anayoyajua kuhusu yeye.
Alikutanishwa na Candy. Sekunde moja kabla hajakumbatiana na mrembo yule, alimkazia jicho la kuuliza iwapo alifanikiwa kuucheza mchezo kama ambavyo alimuagiza, na kutoka kwenye uso wa mrembo yule mwenye madhila, akaona kuwa mambo yalikuwa yameenda sawa.
“Oh Candy!” Alisema wakati akimkumbatia, kisha akamketisha chini na kujitia kumuuliza.
“Umekutwa na nini? Ulikuwa wapi wewe? Uko salama lakini? Umeulizwa lolote kuhusu tuhuma zako na hawa askari?” Alimvurumishia maswali mfululizo chini ya uangalizi mkali wa askari mwingine wa kike.
“Ah, wakili! Ni hadithi mbaya sana…niliogopa. Ila niko sawa…na...sikuulizwa maswali kuhusiana na kesi. Polisi tu walitaka kujua nilipokuwa kabla ya kufika hapa!” Candy alimjibu.
“Dah, pole sana. Mimi wameniambia kuwa ulijisalimisha mwenyewe polisi msimbazi…”
“Yah, ndivyo hivyo…” Candy alimjibu na kuendelea kumpa habari za namna ilivyokuwa hata akafika pale kituo cha kati, kama jinsi alivyoelekezwa kufanya na Abiyah kule nyumbani kwa Morandi Gwaza masaa kadhaa yaliyopita usiku ule ule.
Abiyah alipiga kimya baada ya Candy kumaliza maelezo yake. Akamgeukia yule askari wa kike.
“Nahitaji kuonana na mkuu wa kituo tafadhali…” Alimwambia.
Akapelekwa kwa mkuu wa kituo, Candy akabaki kule mahabusu.
“Nahitaji kumtoa mteja wangu kwa dhamana…”
“Hii ni kesi ya mauaji wakili…hujui hilo? Hawezi kutoka, japo kwa usalama wa maisha yake tu.” Mkuu alimjibu. Ngamao hakuweza kuvumilia, akaingilia kati.
“Huyu ana kesi ya kujibu. Tutahitaji kuchukua alama za vidole vyake tuzithibitishe na ushahidi usiopingika unaoonesha kuhusika kwake na mauji ya Bi. Swadafu! Sasa kwa kuwa wakili wake umeshafika, tungependa kufanya hivyo mara moja!”
Mkuu wa kituo alimkata jicho kali, wakati Abiyah alimtulizia macho ya kuuliza.
“Kumbe mna ushahidi wa alama za vidole?”
“Of course, na mahakamani kila kitu kitawekwa wazi…”
Abiyah akatikisa kichwa.
“Kwanza nitahitaji maelezo ya kitendo cha mteja wangu kutekwa. Ameniambia kuwa katika watu aliowaona wakipigana kwenye eneo la utekwaji, alimtambua mmoja wao, ambaye anahusina na wewe Ngamao…na pia mimi mwenyewe kwa masikio yangu nimekusikia ukiongea na mtu huyo huyo, maongezi yenu yakinithibitishia kuwa mnajuana vizuri tu. Sasa una lipi la kusema juu ya hayo? Utakuwa tayari kusimama mahakamani na kujibu swali hilo na mengine mengi kama hayo wakati wa kesi ya Candy?” Akamtupia maswali.
Ngamao akameza mate.
“Huna jibu afande? Basi naomaba ulitafakari upya swala la kumfikisha mahakani mteja wangu na huo ushahidi wako wa kimazingira na bila shaka wa kupikwa. Ninapata picha na ninaamini kuwa nina uwezo mkubwa wa kuthibitisha kuwa kumuandama kwenu Candy kunatokana na chuki zako binafsi wewe Ngamao, na umelitumia jeshi la polisi kama kono la shetani tu la kukusogezea makaa ya moto pembeni ili umpate Candy kutimiza hizo chuki zako! Una lipi la kusema juu ya hilo? Utakuwa tayari kujibu hilo na mengine mengi zaidi ya hayo mahakamani?” Abiyah alizidi kumsaili Ngamao kwa vitisho.
Ngamao akakunja uso na kufunua kinywa, lakini mkuu wa kituo akaingilia kati.
“Inspekta Kijambia hahusiki tena na hii kesi kutokea hapa wakili! Kama una maswali utayafikisha mahala husika. Na hilo litafanyiwa utaratibu…”
“Good point! Basi mwambie Ngamao akae kimya afande!” Abiyah alisema, na Ngamao akatoka nje kwa hasira.
Abiyah na mkuu wa kituo wakatazamana.
“Okay, naomba mumfungulie mashtaka mteja wangu haraka sana, maana nataka nikabiliane nanyi mahakamani na niwasambaratishe haraka iwezekanavyo…niwaumbue kuliko mlivyowahi kuota kwenye ndoto zenu mbaya kabisa hapo kabla. Lini linafanyika hili?” Alimkoromea mkuu wa kituo.
Mkuu wa kituo aliguna.
“Usidhani utanitisha mimi kama unavyomtetesha Ngamao wewe umesikia? Mimi kazi yangu kutia nguvuni watuhumiwa na kuwakabidhi kwa waendesha mashitaka. Hao ndio utakaopambana nao huko mahakamani. Tayari taratibu zimeshaanza kufanywa na wanasheria wetu na waendesha mashtaka. Zikikamilika basi mashtaka yatafunguliwa…”
“Kwa hiyo kwa muda huo mteja wangu anaendelea kusota mahabusu tu humu? Miss Tanzania huyu mjue!” Abiyah alimaka.
“Hata angekuwa miss jua na mwezi!” Mkuu wa kituo alimaka pia.
“Okay. Hamna taabu!” Abiyah alisema na kutoa simu yake. Akampigia simu mwendesha mashtaka mkuu wa serikali.
“Mheshimiwa Ntobi habari za asubuhi na samahani kwa kukupigia usiku namna hii, nina tatizo!” Aliongea na yule mwendesha mashtaka mkuu wa serikali, na hapo hapo akaona Mkuu wa kituo akimtumbulia macho kwa kutoamini.
Abiyah akakunja nne kitini.
“Najua kuwa ni karibia saa kumi alfajiri saa hizi mheshimiwa, lakini haki ya mtanzania iko hatiani mikononi mwa polisi hapa, nami nataka kuhakikisha kuwa hilo haliendelei kutokea kwa muda mrefu kuliko itakiwavyo…” Abiyah aliongea zaidi kwenye simu, na kusikikiliza kwa muda, kisha akaendelea.
“Okay, ni kuhusu miss Tanzania…Candy Gamasala…yuko hapa kituo cha polisi cha kati. Yaah, ni mteja wangu huyu na ninaona mazingira ya kukamatwa kwake yamejaa utata. Ninachoomba ni mashtaka yafunguliwe upesi na kesi ifikishwe mahakamani haraka iwezekanavyo…iwapo bado utakuwa na hamu ya kuifikisha mahakamani baada ya kusikia upande wangu wa kisa hiki!” Abiyah aliongea na kusikiliza.
“Najua mheshimiwa kuwa uchunguzi lazima ukamilike kwanza, lakini afande mmoja hapa Ngamao Kijambia anasema wana ushahii usiopingika wa alama za vidole vya mteja wangu kutoka wkeney eneo la tukio, sasa hapi kuna uchunguzi gani tena zaidi?” Abiyah alizidi kujibizana na mwendesha mashtaka.
“Anaitwa Inspekta Ngamao Kijambia naambiwa…!” Alizidi kumjibu yule mwendesha mashtaka,
“Saa nne kamili ofisini kwako? Hamna taabu mheshimiwa, ahsante sana na salamu kwa wifi hapo. Nitakie radhi kwa kukukurupusha kutoka ubavuni kwake mida kama hii. See you later mheshimiwa, na ahsante sana.” Akakata simu, akamgeukia mkuu wa kituo na kumchanulia tabasamu pana.
“Sasa ndio umempigia mwendesha mashtaka wa serikali kuonesha nini?” Mkuu wa kituo alimjia juu.
“Yeye ndiye ambaye naweza kuongea naye lugha moja, tukaelewana. Ninachotaka ni kwamba hii kesi iendeshwe haraka iwezekanavyo.” Abiyah alimjibu.
“Kwa sababu mteja wako ni Miss Tanzania?”
“Kwa sababu miss Tanzania amebahatika kunipata mimi kuwa wakili wake, that’s all!” Abiyah alimjibu bila kuonesha kujali, na kuomba kuonana tena na Candy.
“Okay, mrembo, Tuko vizuri so far…itabidi uendelee kubaki hapa kwa muda, na kama mambo yataenda kama ninavyoyasuka, basi hutakaa sana humu ndani…” Alimwambia.
“Ah, Anti Abiyah…ina maana itanibidi nikasimame kizimbani kweli? Idhilali gani hii lakini inaniandama Candy miye!” Candy aliuliza na kulalama.
Abiyah akatabasamu.
“Niamini mimi mrembo…kesi haifikia mahakamani hii. Na kama ikifika basi ni kwa wewe kwenda kutoa ushahidi tu dhidi ya akina Ngamao!” Alimjibu na kumkonyeza.
Akaondoka, akimwacha Candy akiwa ametumbua macho kwa kutoamini.
***
Saa mbili kamili asubuhi Inspekta Ngamao Kijambia aliingia kwenye jingo lililokuwa na ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa serikali. Mkobani kwake kulikuwa kuna faili lake muhimu sana kuhusiana na kesi ya mauaji ya Shakira binti Swadafu.
Mpenzi na muhibu wake aliyeuawa kikatili sana, naye siku zote alikuwa ameazimia kulipiza kifo chake kwa kumtia mbaroni na kumfikisha kwenye mikono ya sheria muuaji wake, Candy Gamasala.
Kwa gharama yoyote ile!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Muda mfupi baada ya kutoka pale ofisini kwa mkuu wa kituo cha polisi cha kati alipokea simu kutoka kwa mkuu wake wa kazi wa muda hapa jijini, ambayo ilimtaka awasilishe ushahidi wote aliokuwa nao kwa mwendesha mashtaka wa serikali ili aanze kupanga kesi yake dhidi ya Candy, na Ngamao alikuwa akijiamini asilimia mia moja kuwa hilo ndilo alilokuwa akilitaka.
Ushahidi aliokuwa nao haukuwa na mjadala.
Tatizo kubwa ni kuhusiana na namna akina Greg walivyoharibu mipango yake ya kumtia kitanzini Candy pumbavu zao, lakini yeye alishaamua la kufanya. Hatojaribu kuwatetea hata kidogo. Ataafiki kujuana nao na kuwa nao pamoja katika msiba wa mama yao na mambo kama hayo, lakini katu hatokubali kuwa alijua kuwa walikuwa na mpango wa kumuua Candy. Watakaloamua wakuu waamue tu, ila yeye na akina GTZ tena uhusiano ndo umeshakatika tena.
Aliingia ofisini kwa mwendesha mashtaka mkuu, na katibu muhtasi wa yule mwanasheria akamwelekeza apite moja kwa moja hadi ndani. Alibisha hodi kwenye mlango alioelekezwa na kuusukuma mlango ule.
Ndani aliwakuta mkuu wake wa kazi wa muda hapa jijini, mkuu wa utawala katika jeshi la polisi, akiwa pamoja na mwendesha mashtaka mkuu mwenywewe, bwana Nikas Ntobi, pamoja na mwanadada ambaye hakumfahamu mara moja, wakiwa wameketi kwenye makochi mle ndani wakimsubiri.
Baada ya salamu za lazima jamaa akaketi kwenye kiti alichoelekezwa na hapo akatambulishwa kuwa yule mwanadada aliyemkuta mle ndani kuwa ni msimamizi wa mashitaka ya jinai katika ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu.
“Karibu Ngamao…” Mkuu wake wa kazi alimwambia baada ya utambulisho, na kuendelea moja kwa moja kwenye swala lililowakutanisha, “Kutokana na hii kesi iliyo mbele yetu...kuna maendeleo mengine yamejitokeza tangu mtuhumiwa husika arejee hapa nchini. Sasa waziri wa utamaduni vijana na michezo tayari ametaka maelezo juu ya hili la mrembo wetu wa taifa kukamatwa na kupigwa pingu hadharani kama ilivyotokea usiku wa jana…tunadhani naye ameshaulizwa juu ya hilo na ofisi kubwa juu ya swala hili. Huyu mtoto alienda kuliwakilisha taifa kule, na amekamatwa kwa namna ambayo kwa uchache sana inatufanya sote tuonekane mabwege…kupeleka mtu hadi huko kabla hajachunguzwa iwapo ana rekodi ya jinai…”
“Er, lilikuwa ni jambo la ghafla sana mkuu, na…tulikubaliana kwa pamoja kuwa kwa wakati ule ilibidi akamatwe huko huko kama ilivyotokea….” Ngamao alidakia.
“Ni kutokana na ushawishi na ushahidi uliokuwa nao ambao mimi ulinionesha…sasa nataka uuwasilishe kwa mwendesha mashtaka hapa na mtaalamu wake waone uzito wa jambo hili!” Mkuu wake alimjibu.
“Yaani hapa kinachohitajika ni kuthibitisha kuwa ni kweli huyu Candy ndiye muhusika wa mauaji anayotuhumiwa kwayo. Nimesikia kuwa una ushahidi usiopingika juu ya hilo…” Mwendesha mashtaka mkuu alidakia.
“Ndio! Ninao kabisa!” Ngamao alijibu.
“Na ulimwambia hivyo wakili wa mtuhumiwa…Abiyah Byabato?” Mwendesha mashtaka alizidi kusaili.
“Yah, nilimwambia. Hiyo ndiyo hali halisi bwana. Ushahidi huu haupingiki!”Ngamao alijigamba, na mwendesha mashtaka akatikisa kichwa kwa masikitiko.
“Basi huna ushahidi wewe!”Alimwambia, na Ngamao akakodoa.
“What do you mean sina ushahidi wakati nakwambia ushahidi ninao hapa?” Alimuuliza huku akiupiga ule mkoba wake kwa kiganja cha mkono wake.
“Humjui Abiyah wewe. Kama umemwambia jambo kama hilo, naye akaamini kuwa ushahidi wako ungeweza kumuangamiza mteja wake, asingenipigia simu kuniambia hayo uliyomwambia!” Mwendesha mashtaka alimwambia.
“Sikuelewi kabisa ujue!” Ngamao alimtolea macho.
Mwendesha mashtaka akaguna.
“Kwamba Abiyah amenipigia simu mimi moja kwa moja na kuniambia kuwa eti polisi ina ushahidi wa kumtia hatiani mteja wake inamaanisha kuwa tayari yeye ana taarifa anazozijua ambazo zitamvua mteja wake kutoka kwenye kesi hii, na ndio maana ametaka ifike kwangu haraka ili atupige mweleka mahakamani…kama tutafikia hatua hiyo!” Mwendesha mashtaka aliele za kwa kirefu.
Bado Ngamao alionekana kutoelewa. Akamgeukia mkuu wake wa kazi.
“Wamesoma darasa moja hao, na wanajuana uwezo waliokuwa nao, hivyo natumai ushahidi huo utakubalika na mwendesha mashtaka hapa!”Mkuu wake alimwambia.
“Wamesoma darasa moja? Kina nani?” Ngamao aliuliza.
“Abiyah na mwendesha mashtaka hapa…wamesoma darasa moja…na wote walikuwa wakali darasani…” Yule dada aliongea kwa mara ya kwanza, kisha akaendelea, “hebu tupe huo ushahidi ulio nao ili tuone tunakabiliana vipi na Abiyah tafadhali.”
Ngamao alibaki akiwa kimya kwa muda akiitafakari taarifa ile, kisha bila kusema neno akafungua mkoba wake na kutoa picha moja kubwa ya rangi na kuiweka mezani ambapo kila mmoja aliyekuwamo mle ndani aliweza kuiona bila taabu.
“Hivyo ndivyo Bi. Shakira Swadafu alivyouawa kikatili miaka miwili iliyopita kule Magu. Nina ushahidi wa kutosha kabisa kuonesha kuwa ni Candy ndiye aliyemuua!” Alisema baada ya kuiweka ile picha pale mezani.
Kwa muda hakuna aliyeongea wala aliyeichukua ile picha kutoka pale mezani, bali wote walibaki wakiikodolea macho tu.
Ilimuonesha mwanamke mtu mzima, mnene akiwa amelala chali kitandani huku amevaa gauni laini ya kulalia. Uso wake ulikuwa umekunjamana kwa uchungu uliochanganyika na woga, hali macho yake yakiwa yametumbuka katika mshangao wa kudumu. Kifuani kwake alikuwa ametapakaa damu, mpini, au kiufasaha zaidi, vishikio vya mkasi mkubwa vilionekana wazi wazi vikiwa vimechomoza kutoka kifuani kwake, makali ya mkasi ule yakiwa yamezama mwilini mwa mama yule na kuuondoa uhai wake. Mkono wake wa kushoto ulionekana ukiwa unaelea sentimeta kadhaa juu ya vishikio vya mkasi ule ilhali vidole vya mkono ule vikiwa vimejikunja kwa nguvu kama kwamba alikuwa akijaribu kuidaka roho yake ilipokuwa inautoka mwili wake, na mshangao ule wa mwisho ulioganda pale usoni kwake ukiwa ni matokeo ya kutoamini kuwa ameshindwa kuidaka roho yake isimtoke na hivyo kumuacha bila uhai.
Ilikuwa ni picha ya kuogopesha haswa.
“Huyo mtu ameuawa kinyama sana wandugu. Muuaji alimshindilia huo mkasi mkubwa kwanza katikati ya kifua, halafu akaushindilia tena pembeni kidogo ya kifua, juu kidogo ya ziwa lake la kushoto. Na katika kufanya hivyo mikono yake yenye damu ikaacha alama za vidole kwenye mpini wa mkasi huo na pia usoni kwa marehemu. Ninaamini alama za vidole vile ni za Candy Gamasala!” Ngamao aliongezea maelezo.
Mwendesha mashtaka alishusha pumzi ndefu kisha akaichukua ile picha na kuitazama kwa karibu zaidi, kisha akairudisha tena mezani.
“Unadhani huyo Candy, hiyo miaka miwili iliyopita, alikuwa ana nguvu za kuweza kuzamisha mkasi kifuani kwa huyo marehemu kiasi hicho?” Alimuuliza Ngamao huku akimtazama moja kwa moja usoni.
“Nililitafakari hilo pia, na bado ninaamini kuwa angeweza kuuzamisha huo mkasi mwilini kwa marehemu…” Ngamao alijibu, na yule mwanadada aliguna.
“Fafanua…” Mwendesha mashtaka alimwambia.
“Tazama jinsi huo mkasi ulivyozama hadi kwenye mpini hapo…unadhani ni nini kinaweza kuuzamisha mkasi kiasi hicho mwilini kwa mwanadanmu kama huyo?” Badala ya kufafanua kama alivyotakiwa, Ngamao alisaili.
“Ni nguvu ya hali ya juu ndio inayoweza kuuzamisha huo mkasi namna hiyo Inspekta, na mimi inaniwia vigumu kuamini kuwa Candy, tena miaka miwili nyuma, angeweza kuwa na nguvu ya kiasi hicho…” Mwanadada alimjibu.
Ngamao akaguna.
“Ni kweli…lakini ni kwa kuwa kwanza humjui Candy kama nimjuavyo miye, halafu pili, si nguvu peke yake inayoweza kusababisha hilo. Kuna kitu kingine ambacho kinaweza kufanya hivyo hata kama mtendaji hana nguvu!” Ngamao alimjibu.
“Okay, wewe Candy unamjua vipi? Na ni kitu gani hicho?” Mwendesha mashtaka akauliza.
“Hasira, ghadhabu…chuki. Hivyo vitu vikiwepo wakati wa kufanya kitendo hicho, bado hata kama mtendaji hana nguvu, matokeo yake yatakuwa ni kama hayo unayoyaona hapo kifuani kwa marehemu. Huyo ni Candy tu!”
Jamaa walimtazama.
“Kwa hiyo unataka kutuambia kuwa Candy alikuwa na hasira, ghadhabu na chuki kubwa dhidi ya marehemu ndio maana akamuua?”
“Kabisa!”
“Na una ushahidi wa kuthibitisha hilo?”
“Kwa masikio yangu nilimsikia akitamka kuwa anamchukia marehemu na mwanaye, na kwamba anataka kuwaua wote…” Ngamao akabainisha.
Watu wakatazamana mle ndani.
“Mnh! Hebu tueleze kila unalolijua kuhusu huyu Candy na huyo Bi. Swadafu kwanza, halafu ndio tutazame hivyo vithibitisho vingine…” Mwendesha mashtaka alimwambia.
Ngamao akajiweka sawa kitini, na uso ukambadilika wakati akikumbuka yale matukio ya siku ya maafa kule Magu. Kama ilivyokuwa kwa Candy saa kadhaa zilizopita, naye akaanza kueleza matukio yaliyoishia kwenye kifo cha Bi. Swadafu. Na wakati akiwaeleza wale watu mle ndani, akili yake ikamrejesha kule Magu miaka miwili nyuma…
Ilikuwa ni siku ya ijumaa, na Ngamao na mpenziwe Shakira walikuwa wameenda kutazama na kuburudika na taarabu usiku ule kwani kundi maarufu la muziki huo kutoka jijini Dar lilikuwa limefanya ziara kule Magu, nao kwa kuwa ni wanazi wa muziki wa aina ile hawakutaka kukosa.
Muziki uliendelea hadi saa sita usiku lakini ilipofika saa tano tayari Shakira alikuwa ameshalewa.
“Okay waubani…twen’zeu home sasa. Naona umeshachoka wewe, na mimi kesho nina safari ya asubuhi sana kwenda Mwanza mjini kikazi, nisingependa kuchelewa.” Ngamao alimwambia.
Kama kawaida, Shakira alibishabisha lakini hatimaye walikubaliana na wakaondoka. Kutokana na kuwa alikuwa na safari ya kikazi asubuhi iliyofuata, hakutaka kulala nyumbani kwa Shakira usiku ule hivyo alimrudisha nyumbani mpenziwe kisha yeye akageuza gari lake na kurudi nyumbani kwake.
Huku nyuma Shakira akauwa.
Na kwa hilo Ngamao hakujisamehe hata siku moja. Aliamini kuwa kama asingeondoka na kurudi nyumbani kwake usiku ule, Shakira Swadafu asingeuawa.
Saa kumi na mbili asubuhi alipigiwa simu na GTZ huku akilia.
“Mama kauawa Ngamao! Mama hayuko tena duniani…ooh mama yangu jamani, Ngamao ulikuwa wapi wewe mama anauawa namna hii?” GTZ alilia kama mtoto, na Ngamao akahisi ubaridi ukimtambaa mwilini na akili ikimtetema.
“Kauawa? Na nani? I mean…lini?”
GTZ alizidi kulia tu huku akibwabwaja maneno yasiyo na msaada wowote.
“Tulia GTZ! Uko wapi hapo sasa?”
“Chumbani kwake….mama kachomwa mkasi kifuani…”
“Usiguse chochote. Asiondoke mtu yoyote humo ndani …nakuja!” Ngamao aliamuru, na dakika kumi na tano baadaye alifunga breki kwa makeke nje ya jumba la Bi. Swadafu, ambapo tayari watu walikuwa wameshajirundika pale nje, naye akapitiliza moja kwa moja hadi ndani, akiwa amevaa suruali yake ya michezo tu na fulana nyepesi.
Alimkuta GTZ akiwa amejibweteka nje ya mlango wa chumba cha bi. Swadafu, chupa ya pombe kali ikiwa mkononi, machozi yakimbubujika kama bomba.
Ngamao aliingia chumbani kwa Bi. Swadafu, na kumkuta mpenziwe akiwa katika ule mshangao wa mwisho hapa duniani.
Mguno wa fadhaa ulimtoka na pamoja na uzoefu wake wa kipelelezi, alijishtukia akiyumba na kuangukia kwenye kochi lililokuwa karibu na kile kitanda.
“Haya ni mauaji haya! Tena ya kinyama!” Alijisemea mwenyewe kama anayejifundisha jambo jipya kabisa maishani mwake.
Dakika tano baadaye askari wenzake walifika pale kwani alishawapigia simu na kuwataka wakutane pale nyumbani kwa Bi. Swadafu. Harakati na kulichunguza eneo la mauaji zikaendelea pamoja na kutafuta alama za vidole mle ndani. Ikagundulika kuwa vito vyote vya thamani vya Bi. Swadafu, pamoja na pesa taslimu ambazo huwa hazikosekani mle chumbani kwake, vilikuwa vimetoweka pia.
Sio tu kumetokea mauaji, bali na wizi pia.
Ngamao akatoka nje na kuwaita wafanyakazi wote wa mle ndani kwa ajili ya kuwahoji.
Ndipo ilipobainika kuwa Candy hakuwemo mle ndani.
Mara moja akili yake ikamrudisha kwenye lile tukio la kubakwa yule binti mle ndani siku chache nyuma, na yale matukio yaliyofuatia tukio lile.
Alikumbuka jinsi Candy alivyotaka kumbamiza GTZ na kigoda kisogoni, na Greg akawahi kumzuia. Akakumbuka kauli ya Candy kuwa alitaka kumuua Bi. Swadafu na mwanaye GTZ.
“Nipeleke chumbani kwake huyu binti!” Alimuamuru mmoja wa wale wafanyakazi mle ndani, na alipofika huko, na kukuta kuwa begi lake la nguo halipo, jibu liijipigia mstari kichwani kwake.
Akawakusanya wafanyakazi wote mle ndani na kuwahoji mmoja baada ya mwingine, akitaka kujua iwapo Candy alionesha dalili yoyote ya kupanga mikakati ya kutoroka au kuonesha nia ya kufanya jinai ile.
Wa mwisho kuhojiwa alikuwa ni mchunga ng’ombe wa Bi. Swadafu, John Koccho.
Wote hawakuwa na taarifa zozote za kumsaidia katika kubaini iwapo Candy alionesha dalili zozote za kufanya jinai ile, wala kujua ni wapi atakuwa ameelekea baada ya kutoweka katika mazingira yale.
“Mtoto kaua bloody bitch, atafutwe haraka sana!” Alifoka huku akitoka na kurudi sebuleni.
Na ni hapo ndipo msako mkali sana dhidi ya Candy ulipoanza. GTZ alitangaza dau la milioni tano kwa yeyote atakayetoa taarifa za kukamatwa Candy Gamasala. Habari zilienezwa magazetini na kwenye vyombo vya habari. Ngamao alitoa vipande vya magazeti kutoka kwenye mkoba wake na kuwakabidhi wale watu aliokuwa akiwasimulia kisa kile mle ndani. Dau lilitangazwa gazetini lakini matangazo yote hayakuambatana na picha ya mtuhumiwa, jambo ambalo lilifanya kupatikana kwake kuwe kugumu sana. Uchunguzi wa chumba cha mauaji yalipotikea, uliibuka na alama za wazi za vidole vya muuaji.
Ngamao akaichukua ile kesi mwenyewe na kuendelea na upelelezi wa kumtafuta Candy huku akipeana habari na watoto wa marehemu, Greg Pasha na GTZ.
“Na haikuwa mpaka wiki kadhaa nyuma wakati alipotangazwa kuwa Candy ndiye Miss Tanzania, ndipo nilipoweza kumtambua. Nikaja Dar kumtia nguvuni. Lakini kuna matukio mazito niliyokutana nayo hapa ambayo yalinifanya nisiweze kumkamata hadi siku aliporudishwa hapa nchini kutoka Venezuela.” Ngamao alimalizia, na wote mle ndani wakapiga kimya kwa muda.
“Umetueleza kisa cha matukio yaliyoishia kwenye mauaji ya Bi. Swadafu, lakini bado hatujasikia tukio lolote ambalo lingesababisha huyu Candy awe na chuki na Bi. Swadafu kiasi cha kumuua…hatuoni “motive” hapo mpaka sasa. Vipi hapo?” Mwendesha mashitaka alihoji hatimaye.
Ngamao alijiramba midomo. Aliacha makusudi kuelezea tukio la kubakwa kwa Candy, na alijiandaa kwa swali kama lile.
“Ni kweli. Candy alijiona kuwa amesalitika maana Bi. Swadafu alimuahidi kumsomesha pindi akifika pale nyumbani kwake, lakini hakufanya hivyo. Na siku waliyokuwa wakizozana, Candy akitaka arudishwe kwao kwa kuwa hakupelekwa shule, na Bi. Swadafu naye akigomba kuwa hamrudishi, mtoto akatamka maneno hayo!” Ngamao akaongopa waziwazi.
“Sasa unadhani hilo ndio linaweza kusababisha Candy achukue hatua ya kumuua na kumuibia yule mama?” Mwanadada aliuliza.
Ngamao akabetua mabega.
“Si mauaji yameshatokea hayo? Na ushahidi wa alama za vidole upo, na dhima au “motive” ya kufanya mauaji hayo inajionesha wazi hapo?”
Mwendesha mashtaka na mtendaji wake walitazamana.
“Na unasema wakati wanazozana na Candy akasema hayo maneno...wewe ulikuwepo. Ilikuwaje hata ukawepo…ulikuwa jamaa wa karibu na familia?” Hatimaye mwendesha mashtaka akauliza lililokuwa lilimbughudhi kichwani mwake tangu Ngamao aseme kuwa alisimsikia Candy akitangaza nia ya kumuua Bi. Swadafu na mwanaye.
Ngamao aliinama kidogo.
“Yah, nilikuwa karibu sana familia ile…” Alijibu kwa upole.
“Kivipi?” Mwanadada aliuliza.
Ngamao akatulia tu.
“Yaani ulikuwa mjomba, jirani au shemeji?” Mwanadada akakazia swali.
Ngamao alimtazama moja kwa moja machoni.
“Bi. Swadafu alikuwa mpenzi wangu!”
“Oh, come on, Ngamao! Sasa ungewezaje kuendesha upelelezi wa kifo cha mpenzi wako na wewe?” Mkuu wake wa kazi alimhoji, wazi kuwa hili ndio analijua muda ule. Mwendesha mashtaka na mtendaji wake wakatazamana.
“Nimekuwa makini sana kutenganisha hisia binafsi na kazi katika hili wazee!” Ngamao alijitetea.
Mwendesha mashtaka akaguna.
“Mweleze hilo Abiyah mahakanai uone atakavyokunyabua! Hilo ni kosa kubwa sana Inspekta, nawe walijua hilo. Au mkiwa huko mikoani ndo mnajifanyia tu vitu kama mtakavyo?” Alimkemea. Ngamao akavimbisha midomo tu.
“Hebu tuoneshe hizo alama za vidole zilizokutwa eneo la tukio!” Mwendesha mashtaka akaamuru.
Ngamao akatekeleza.
Walizitazama zile alama za vidole zikiwa kwenye jalada maalum, na kwa muda wale waendesha mashtaka wakamakinika.
“Inaonekana ni vidole vidogo kiasi hivi!” Yule dada alisema, na Ngamao akaachia tabasamu la ushindi.
“See? Kama si Candy basi ni nani huyo?” Aliuliza.
Kimya kikatanda.
“Okay. Tutakutana na wakili wa Candy baadaye leo hii. Tutahitaji huu ushahidi wakati tukikutana naye.” Hatimaye mwendesha mashtaka alisema, uso wake ukionesha mashaka fulani.
“Be my guest!” Ngamao alisema kwa kujiamini, akimaanisha kuwa awe huru tu kufanya vile atakavyo.
Saa nne kamili asubuhi Abiyah Byabato aliingia ofisini kwa mwendesha mashtaka kama walivyokubaliana, na kumkuta akiwa na mtendaji wake. Walisalimiana kistaarabu, kisha wakaketi kwenye chumba maalum cha mikutano .
“Okay Abiyah, masikio yetu yako wazi. Umekuja na hoja gani?” Mwendesha mashtaka alimwambia, na Abiyah akatabasamu.
“Nadhani mpaka sasa umeshafanya homework yako kuhusu kesi ambayo polisi wanayo dhidi ya mteja wangu Candy. Sitaki kupoteza muda. Nadhani serikali haina kesi hapa, ni bora muahirishe kufungua mashtaka yoyote mnayotaka kuyafungua dhidi yake kwani hayatakuwa na mashiko mahakamani. Mtapoteza muda bure na wakati huo huo kumpa nafasi muuaji halisi azidi kupotea.” Abiyah aliwaambia.
Jamaa wakamtazama.
“Kuna ushahidi wa alama za vidole Abiyah, kama ulivyoambiwa na askari…unasema nini juu ya hilo?”
“Nitathibitisha kuwa hizo alama sio za mteja wangu. Na nikithibitisha hilo mahakamani ujue hutakuwa na kesi tena na itakuwa ni aibu kubwa kwa upande wa serikali, hasa ukizingatia kuwa mmeshajianika wazi mbele ya wananchi kwa kumkamata miss Tanzania na kueleza wazi kuwa anakabiliwa na kesi ya mauaji.”
Abiyah alijibu na kubaki akiwatazama wale waendesha mashtaka.
“Kwa hiyo unataka tufute nia ya kumshitaki mteja wako halafu tumshitaki nani?” Mwanadada alimuuliza. Abiyah alimtazama yule mwenzake, kisha akamgeukia bwana Ntobi.
“Siyo kazi yangu hiyo. Ni kazi yenu kutafuta muaji halali. Langu miye ni kumvua mteja wangu hizi tuhuma za kubambikiwa zilizosukumwa na visasi potofu na binafsi!”
Wakatazamana.
“Visasi binafsi?” Ntobi aliuliza.
Abiyah akacheka kidogo.
“Ntobi unajua mimi huwa siingi kwenye kesi kichwa kichwa. Nina taarifa za kutosha kuonesha kuwa Ngamao alikuwa na kisa binafsi na Candy na hivyo maamuzi yake katika kumfungulia tuhuma hizi yalikuwa na msukumo binafsi zaidi kuliko vinginevyo…pia nmajua kuwa alikuwa na uhusuano na marehemu. Nitalibebea bango swala hilo mahakamani mpaka kieleweke. Nikishamtoa thamani namna hiyo mbele ya mahakama hakuna ushahidi wake wowote utakaotiliwa maanani. Unalijua hilo, so usipoteze muda bure. Una ushahidi gani wewe wa kumtia Candy hatiani?” Abiyah alimwambia na kumuacha na swali.
Ntobi akamtupia jicho kali, lakini hakujibu.
“Come on Ntobi! Nashauri tuangalie ushahidi wa kila mmoja wetu hapa hapa ili tuone kama tuna silaha za kutosha kuingia vitani mahakamani…kama hatuna tuachane na hili swala!” Abiyah alimwambia.
“Lete kwanza taarifa ulizo nazo ili tuone kama zina uzito wowote wa kutushinda mahakamani!”
“Hatwendi hivyo Ntobi na wewe wajua. Ninyi ndio mnaofungua kesi, na mimi ndio nina nafasi kubwa ya kuwaaibisha mahakami. Kuweni wawazi hapa ili kuepusha aibu ya kubwagwa mahakamani!
Ntobi akaachia tabasamu.
“Mbishi sana Abiyah wewe…kwa nini usihamie serikalini lakini wewe?” Ntobi akamwambia.
Abiyah akaguna.
“Halafu nije kufanya kazi chini yako? Unajua mimi na wewe hatuwezi kufanya kazi vizuri tukiwa upande mmoja. Inabidi mmoja wetu awe upande mwingine. Sasa inakuwaje?” Abiyah alimjibu.
Ntobi akamwambia yule mtendaji wake amueleze juu ya ushahidi waliokuwa nao dhidi ya Candy, kama walivyoupata kutoka kwa Ngamao.
Abiyah aliusikiliza kwa makini na akazitazama zile picha za mauaji ya Bi. Swadafu na zile alama za vidole.
Alipiga kimya kwa muda.
“Hapa kuna kitu hakipo sawa…unasema kuwa katika watu waliohojiwa baada ya Candy kutoroka alikuwako mchunga ng’ombe wa bi. Swadafu?” Aliuliza hatimaye.
“Ndivyo ilivyo. Kama tulivyoelezwa na Ngamao…” Mwendesha mashtaka alimjibu.
Abiyah akaguna.
“Okay. Kwa hiyo Ngamao ndio shahidi wenu mkuu sio?” Alihoji. Akaona kutokana na macho yao kuwa hiyo ndivyo ilivyo.
“Basi kwanza eleweni kuwa nitamvunjavunja mahakami Ngamao ili asiwe shahidi. Baada ya hapo hamtakuwa na shahidi mwingine zaidi ya watoto wa marehemu, ambao hivi niongeavyo wako chini ya ulinzi kwa utekaji…”
“Unataka kusemaje sasa Abiyah…?” Ntobi aliuliza.
Abiyah alitoa simu yake ya kisasa na kuibofya kwa muda.
“Nataka msikilize maelezo ya mteja wangu kuhusiana na hilo tukio la Magu miaka miwili nyuma. Ila naomba muelewe kuwa wakati anaongea mambo haya hakuwa na habari kabisa kuwa mimi nilikuwa namrekodi kwa simu hii. Hivyo mtaona kuwa si mtu anayeongea huku akijua kuwa anarekodiwa. Sikilizeni kwanza halafu tuongee kuhusu muuaji wa Bi. Swadafu!” Aliwaambia, kisha akabofya sehemu kwenye simu yake, na muda huo sauti ya Candy Gamasala ikasikika mle ndani.
Abiyah alijiegemeza kochini na kuwatazama wale watu wakisikiliza maelezo ambayo Candy aliyatoa kule nyumbani kwa Morandi, Makongo.
***
“Kwa hiyo unataka kusema huyu mchunga ng’ombe ndio muuaji?” Mwendesha mashtaka alisema baada ya kumaliza kusikiliza maelezo ya Candy.
“Yap! Kila kitu kiko wazi hapo…” Abiyah alimjibu.
“Si kweli. Huyo Mchunga ng’ombe alikuwepo nyumbani kwa marehemu siku ile Candy alipotoweka!” Mwanadada alisema.
“Anaitwa John Koccho huyo jamaa…” Abiyah alisema.
Jamaa wakamtazama kwa mshangao.
“Unajua hadi jina lake?”
“Hiyo ni kuwaonesha kuwa ninajua mambo mengi kuliko nyie kwenye kesi hii. John Koccho ni mtu mbaya na mjanja sana. Alimuua Shakira na akataka amlengeshe Candy kwenye mauaji yale. Alimwambia Candy kuwa yeye harudi kule, kisha akarudi na kujitia alikuwa pale pale muda wote. Namna ile alifanikiwa kuhamisha tuhuma kutoka kwake kabisa na kuzipeleka moja kwa moja kwa Candy. Na rafiki yenu Ngamao kama bwege akaingia kichwa kichwa!” Abiyah aliwaambia.
Kimya kikatanda.
Abiyah akaendelea kuwaeleza jinsi Koccho alivyomuibukia Candy kule mikumi na kutaka kuanza kumdfai mryungula ili asitaje mahala alipo.
“Seriously?” Mwendesha mashtaka aliuliza.
“Kabisa! Na kama mking’ang’ania kufika mahakamani, haya yote yatawekwa wazi na mteja wangu!” Abiyah alijibu.
Kimya kikachukua nafasi tena wakati wale waendesha mashtaka wakitafakari hali ile.
“Sasa kuna hizi alama za vidole Abiyah. Na ukweli zinaonesha kabisa kuwa muuaji alikuwa na mikono midogo…vidole ni vidogo hivi!” Mwendesha mashataka alitia hoja.
“Nakubali. Kuna wanaume wenye mikono midogo mithili ya kike, napia kuna wanawake wenye mikono mikubwa. Ni maumbile tu. Hizo alama sio za mteja wangu!” Abiyah alitia hoja.
“Basi na tuiache mahakama iamue juu ya hilo, eenh?” Ntobi alimwambia kibishi.
Abiyah alitikisa kichwa.
“Okay. Kama hizo ni alama zake, basi naamini huo ndio unaweza kuwa ushahidi pekee wa nguvu mtakao kuwa nao dhidi ya Candy...zaidi ya hapo hamna kesi. Sawa?”
Jamaa walitazamana. Kisha Mwendesha mashtaka akaafiki kwa kichwa.
Abiyah akatabasamu.
Alishawafikisha wale jamaa mahala alipokuwa anapataka.
Na sasa akatupa karata yake ya mwisho.
“Nikiruhusu mteja wangu achukuliwe alama zake za vidole sasa hivi na zikalinganishwa na hizo mlizo nazo, na ikaonekana kuwa alama za muuaji kwa hakika sio za kwake…mtafuta mashataka dhidi yake?”
“Utafanya hivyo kweli au unatuuliza tu?” Mwendesha mashtaka alimuuliza.
“Nataka nifaye hivyo!”
“Una hakika? Kwa sababu kama ni mteja wako ndio mwenye hizo alama za vidole utakuwa umemuangamiza kabla hata hajafika mahakamani!” Mwendesha mashtaka alisema akiwa makini sana.
“Nitafanya hivyo kama nanyi mtakuwa tayari kuachana na tuhuma zenu dhidi ya mteja wangu na kumtafuta John Koccho, iwapo hizo alama za vidole hazitaona.” Abiyah naye alijibu kwa kujiamini.
“Deal! Kama hazioani, Candy anavuliwa tuhuma hizi!” Mwendesha mashtaka alisema.
“Good!” Candy alisema huku akitoa mkataba amabao alikuwa ameshauandaa mapema tu asubuhi ile baada ya kutoka kule kwa mkuu wa kituo cha polisi cha kati.
“Naomba saini kwenye makubaliano haya….kabla sijaruhusu mteja wangu kuchukuliwa alama zake za vidole.” Alisema huku akimkabidhi mwendesha mashtaka karatasi ile.
Ntobi alimtumbulia macho.
“Yaani we ulikuwa umejiandaa kabisa kwa hili, eeenh?”
“One step ahead Ntobi, one step ahead…unakumbuka mwalimu wetu alikuwa anatusisitizia hilo kila siku darasani?” Abiyah alimjibu huku akitabasamu.
Nikas Ntobi alibaki akitikisa kichwa tu kwa mastaajabu, huku akiusoma ule mkataba.
***
Saa moja na nusu baadaye vipimo vilionesha kuwa alama za vidole vya Candy ni tofauti kabisa na zile zilizokutwa kwenye eneo la mauaji ya Bi. Shakira Swadafu, na nusu saa baadaye, Candy alitoka nje ya kile kituo cha polisi akiwa mtu huru.
Ilikuwa ni furaha iliyoambatana na vilio wakati alipokutanishwa tena na akina Bishkuku. Siku ile ile msemaji wa jeshi la polisi alilazimika kutoa maelezo kwa umma kuwa shutuma zilizotolewa dhidi ya mrembo Candy zilikuwa na makosa, na kwambna uhakika ni kwamba Candy alikuwa anatakiwa kama shahidi muhimu katika kesi ya mauaji yaliyotokea miaka miwili nyuma huko nyuma.
Msemaji alichukua fursa ile kumuomba radhi Candy hadharani kwa usumbufu aliokutana nao.
Maandamano na kelele nyingi zilifuatia taarifa hii, kutoka kwa watanzania, wakilaani kunyimwa nafasi ya kushangilia ushindi mzuri ulioletwa nchini na Candy
***
Wiki moja baadaye ujumbe wa Miss world ulishuka Tanzania na kumkabidhi rasmi Candy zawadi zake zote ambazo zilizuiwa kule Venezuela.
Ilikuwa ni sherehe kuvwa sana.
***
Ngamao Kijambia alistaafishwa kazi kwa manufaa ya umma, na alitakiwa awe shahidi katika kesi iliyokuwa ikiwakabili GTZ na nduguye Greg Pasha. Jamaa walipatikana na hatia ya hujuma za kuteka gari la polisi na kula njama za kutaka kuua. Greg alifungwa miaka saba jela, na GTZ akapewa miaka mitana kwa kosa la kushiriki kwenye njama zile.
***
Msako wa John Koccho uliendela kwa muda mrefu, na hatimaye alikamtwa miezi mitatu baadaye akijaribu kuvuka mpaka wa Tanzania kuingia Msumbiji. Alihukumiwa kifungo cha maisha kwa kosa la kumuua Bi. Shakira Sawadafu.
***
Kokos Wandiba alifanikiwa kutangaza nia ya kutaka kuwa karibu zaidi na Candy.
“Inabidi uanze upya Kokos…safari hii uanze vizuri na kwa nidhamu zote…labda naweza kukufikiria!” Candy alimibu huku akicheka, na baada ya kuzubaa kwa muda, Kokos naye akacheka sana na wakakumbatina kwa furaha.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
***
Morandi Gwaza alifungua kampuni rasmi ya upelelezi binafsi, akishirikiana na mpenziwe Nuru. Kwa pamoja wawili hawa walikabiliana na harakati nyingi za kipelelezi katika kuendesha kampuni yao hiyo.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment