Search This Blog

Tuesday, 1 November 2022

SUPRISE - 1

 






 IMEANDIKWA NA : RAMAAH MZAHAM



*********************************************************************************



Simulizi : Suprise

Sehemu Ya Kwanza (1)



Msichana mrembo kwelikweli, mwenye rangi halisi yenye mvuto wa kipekee, nywele zake nyeusi tii japo si ndefu lakini zilipendeza zilivyosukwa. Alivaa miwani ya jua na kuipandisha kichwani, ni mrefu mwenye umbo linaloendana na mwili wake.

Kifupi alikamilika kila idara, hivyo ninaposema ni mrembo, basi jua nina maanisha kile ninachokisema. Yaani ni mrembo wa haja kweli, ukizingatia na nguo alizovaa, ndio utata kabisa, msichana huyo alikuwa amevaa pedo ya rangi ya bluu na kiblauzi cheupe.

kilichoshonwa na kuacha sehemu ya mbavu ikiwa wazi, chini alivaa viatu kama vya Yesu, yaani vile vya kufunga kamba hadi karibu na magoti, kifupi alipendeza mno na katu asingetokea mtu yeyote wa kulikanusha hilo.

Alikuwa akishuka ngazi taratibu kwa maringo kama Twiga jike mwenye mimba huku akiongea na simu, Victor alicho kifanya ni kumpisha apite na kuanza kumtazama kwa nyuma hadi alipopotea machoni mwake, ndio alipo kumbuka kuwa anatakiwa kumfuata Lidya.

Akaongeza kasi kuelekea kwa Lidya. Bila hata ya kugonga mlango wa ofisi ya Lidya, akaingia na kusimama huku akitweta na kusema

“Hivi Shem, maajabu ya Dunia yapo mangapi?”

“Yapo 7, kwani vipi Shemu wangu?” aliuliza Lidya akiwa na shauku ya kutaka kujua ni nini

“Ni hatari lakini salama ila amani hakuna…” Victor alisema huku akikaa mezani badala ya kukaa kwenye kiti, halikumshangaza Lidya hilo, aliisha mzowea shemeji yake

“Hata sikuelewi Victor, hebu nieleze kuna nini?”

“Usikonde Shem, tutaongea zaidi nje,lakini kuanzia leo nitakuwa sikosi ofisini kwako, kwanza mambo vipi?” yaani baada ya maongezi yote yale, ndio Victor anakumbuka kuwa hata hajasalimia

“Mh! Poa…” kabla hajamaliza, simu ya Lidya akaiangalia na kumuuliza Victor

“Ommy upo nae?” huku akipokea simu

“Ndio, mwambie ndio tunashuka!” Lidya akatikisa kichwa kukubali na kuanza kuongea

“Hellow my love, mambo? Tunakuja sasa hivi, hapa nafunga ofisi” haraka haraka Victor akamsika mkono Lidya na kuanza kutoka nae, kichwani mwake alikuwa haamini kama Yule aliemuona ni jinni ama Malaika.

Kwa sauti ambayo yeye aliamini ni ya moyoni kumbe ni ya mdomoni akajikuta katamka ‘Pengine ni jini’ Lidya akasikia na kumuuliza Vctor anasemaje? Huku akishangaa na kuona aibu, akajibu kuwa wataongea zaidi hotelini.

Tayari walikuwa wameisha ifikia gari ya Ommy, walimkuta yeye akiwa amesimama pembeni ya gari akiongea na simu kwa bashasha, Victor alifika na kumfungulia Lidya mlango wa mbele upande wa pili wa dereva nae akangia nyuma, Ommy akaja na kuingia, wakatokomea mbele.

* * * * *

Baada ya kila mtu kuagiza chakula, Ommy alimtazama Lidya na kumuuliza ni kwanini walichelewa sana kule ndani, Victor ndio akaliwahi swali kwa kutoa jibu kwa njia ya swali

“Ommy ndugu yangu, hivi haiwezekani kuongeza maajabu ya dunia kutoka 7 hadi kufikia 8?”

“Ah bwana mie sikuelewi, eti Lidya vipi?” Ommy alimuuliza Lidya huku akimtazama nae akatikisa mabega kuonyesha hajui lolote, sasa wote wawili wakawa wakimtazama Victor alie onekana kama vile yupo mbali sana kimawazo hadi Lidya alipo mshtua kwa kumuita Shem kama mara tatu hivi ndio akashtuka

“Ah! Jamani nisameheni bure, ujue leo nimekutana na mtu mmoja naweza kusema ni wa ajabu mno” hapo sasa Victor akawapa habari kamili bila kuacha chochote. Aliponyamaza, Lidya akamuuliza alivyovaa, Victor akamuelekeza, lakini Lidya alishindwa kumtambua, akaishia tu kuuliza tena wamekutana ghorofa ya ngapi.

“Ni ile ile ya pili wakati mimi nikipanda, yeye alikuwa akishuka” akiwa hajiamini, Victor alisema na kumpa wakati mgumu zaidi Lidya, akaanza kuvuta taswira lakini akachemsha huku akimuangalia Ommy aliekuwa akila taratibu.

“Pale kuna wasichana wa5 na wanawake wa3 sijui ni nani kati yao? Lakini usikonde Shem kama ni mfanyakazi wa Classic leo hii hii nitamjua huyo alie ushika moyo wako kiasi hicho” alipomaliza kuongea Lidya hayo yake, Ommy nae akaongeza

“Sasa mkubwa unaweza kuendelea kula, tayari umehakikishiwa usalama au vipi?”

“Poa na tule kwa furaha ya huyo mrembo tusie mjua” wakacheka wote kwa sauti ya juu na kuendelea kula hadi walipomaliza wakaondoka.

Safari yao ilianzia ofisini kwa Lidya, wakamuacha kisha nao wakanyoosha jadi Victoria nyumbani kwa wazazi wa Victor, walikaa huko hadi saa kumi jioni ndio wakarudi nyumbani kwa Ommy na kutizama TV hadi Lidya aliporudi, alipoingia ndani na kuwasalimia hakutoka tena hadi Victor alipo muita.

Lidya alimuomba amvutie subira kidogo kwani kuna kazi ndogo anaimalizia, muda si muda Lidya akajitokeza na kwenda kukaa na mpenzi wake Ommy, na alipokaa tu wakatazamana nae akawa ni mtu wa kwanza kumuuliza habari za huko, Lidya alitabasamu na kumwambia Ommy aache upambe huku akimziba mdomo kwa kidole

“Haya bwana acha mie ninyamaze, Victor uliza mwenyewe, labda anafikiri mie ninataka kufanya mapinduzi,” Ommy aliongea kimzaha na wote wakacheka na kisha Lidya akaendelea

“Hakuna mtu wa aina ile pale ofini kwetu, nimeulizia kila idara, hakuna mtu alie vaa kama vile kwa leo, labda awe ni ngeni Fulani, nimeonana na Maryam, Flavy, Ire nikaingiane, nikaenda kwa Doreen bado sijamuona, nikaingia ofisini kwa Nusura pia kwa Grace, nikamalizia kwa Aisha kote nimemkosa, sijui nikusaidiaje shem wangu?”

“Duh kazi ipo, hata sijui tufanyeje?” alisema huku akijiweka vema pale chini, Ommy alifikiri kqwa sekunde kadhaa na kusema

“Mpenzi wangu pale awali ulituambia ofisini kwenu kuna mabinti wa5, lakini wewe umetutajia majina manne tu, huoni kuwa kuna jina moja hujatutajia?”

“Labda inawezekana akawa ni Evelyn, lakini yeye hajaja kazini leo” alimalizia hivyo Lidya huku akimtazama mumewe

Victor akanyoosha mkono kama vile anaomba nafasi ya kuongea kwa mwalimu, kisha walipo muangalia akasema kumwambia Lidya

“Shem unaonaje kama kesho pia mie nije ofisini kwako?”

“Unasemaje Victor? Yaani namaanisha uende ukafanye nini huko?” Aliuliza Ommy kwa mshangao akiwa hata hajaelewa ni nini Victor amelenga

“Nitakwenda ili kumsaidia Lidya kumtafuta huyo binti ninae mtafuta au sio Shem wangu?”

“Sawa tu, we njoo tena kwenye breakfast itakuwa ni juu yangu, usiache” Alisisitiza Lidya

“Ahsante sana Shem, nashukuru na sasa nakwenda” Victor aliaga na kuondoka, Ommy hakumshindikiza, ila alimvuta mkono Lidya na kumwambia

“Ni muda mrefu sana tangu nimjue Victor lakini sijawahi kumuona hata siku moja katika hali kama hii tangu alipokuwa na Rose hadi alipo olewa, Msaidie rafiki yangu, sawa mpenzi wangu?”

Lidya akaitika kukubali na kumbusu mdomoni mumewe kisha akamwambia anaenda kuandaa chakula cha usiku na kumuogesha mtoto wao aitwae Jamila ili wawe huru na kukaa kwa amani.

Kama walivyokuwa wamekubaliana siku iliyopita saa nne asubuhi walikutana kwenye mgahawa mmoja uliokuwa jirani na Classic house na kupata kifungua kinywa kwa gharama za Lidya. Walionekana kuwa ni wenye furaha kwa kuwa pamoja muda ule, Victor alikuwa akimueleza Lidya ni jinsi gani usiku uliopita ulivyokuwa ni mrefu kwake

Alimwambia kuwa ule usiku mmoja alikuwa akiuona kama ni nyusiku kumi, Lidya alicheka na kumtoa hofu kuwa asikonde, leo wafanyakazi wenzake wapo wote hivyo watakwenda wote hadi ofisini na kumtambulisha kama mgeni wake anae hitaji kuanzisha bendi, hivyo anataka kujua jinsi ya kuendesha bendi hiyo.

Victor alifurahi kwa wazo hilo la Lidya, wakanyanyuka na kuanza safari ya kuelekea ofisini kwa Lidya. Saa 5 juu ya alama Lidya aliingia ndani ya ofisi yake akiwa ameongozana na Victor na kumtaka akae kwenye sofa iliyokuwepo mle ndani ofisini kisha akapiga simu sehemu mbili tofauti.

Sehemu ya kwanza ilikuwa ni kwa Maryam na sehemu nyingine aliongea na Irene, wote aliwaita ofisini kwake. Muda si mrefu sana akaanza kuingia Irene na kuwasalimia, walipoitika salamu yake Lidya akamuamuru akae kwenye kiti jirani na alipo keti mgeni wake bila kuwafahamisha. Akaendelea na shughuli zake hadi mlango wake ulipogomgwa tena.

Aliruhusiwa kuingia, alipoufungua, hakuwa mwingine bali ni Maryam akiwa ameitika wito, nae akaoneshwa sehemu ya kukaa baada ya salamu, kisha Lidya akaanza kuongea

“Ngoja niwatambulishe kwanza.” Huku akimuangalia Maryam akasema

“Mary, huyu ni Victor…” kisha akamuangalia Irene na kurudia maneno yaleyale ila ni jina tu alilibadili, kisha akaendelea kusema huku akiwa ameshika kalamu mkononi anachezea





“Huyu ni Victor, ndio rafiki mkubwa wa Ommy, ndio kwanza amerudi, hakuwepo nchini kwa muda mrefu, ndio tunatarajia atakuwa mmiliki waClassic Band muda si mrefu. Nadhani wote mnajua kuwa mara baada ya sisi kufunga ndoa tutahama hapa Tanzania?” wakaitikia wote kwa kutikisa vichwa vyao, kisha Lidya akaendelea

“Sasa muda wowote atakao kuja akiwa na shida, ninaomba asikilizwe, maana hajui lolote kuhusiana na mambo ya Bendi, hivyo asaidiwe bila masharti yoyote, sawa?”

“Sawa dada Lee, tumekuelewa” walijibu kwa pamoja na kunyanyuka kwenda kumsalimia kwa kumpa mkono Victor na kumwambia

“Tunashukuru kukufahamu Victor” alisema Irene, wakati huo Maryam alikuwa akiongea na Lidya huku wakicheka pasina kusikika ni kipi wanacho kiongea. Victor akamjibu Irene

“Nami nafurahi kukutambua Irene” kisha Maryam nae akageuka na kumpa mkono Victor huku akisema kwamba anakaribishwa muda wowote.





Mara baada ya kauli ile ya Maryam, Lidya alicheka sana na kumfanya Victor atabasamu

“Nashukuru sana na nina amini nitapata ushirikiano wa kutosha.” Jibu hilo pia likawafanya wacheke kabisa huku Irene naMaryam wakitoka na kusababisha Victor arudi kuketi kwenye sofa kama awali, na kumpa nafasi Lidya ya kumuuliza kama kuti ya wale pale wawili kuna mmoja wao?

"Hapana hapo hayupo ila anataka kufanana na Maryam kwa kila kitu, sijui ni mapacha?" Victor alimuueleza huku akimtazama kwa umakini Lidya. Lidya akatikisa kichwa na kusema

"Aaanh! Kumbe wewe umemuona Everlyne, ni ndugu yake Maryam, ni mtoto wa mkubwa na mdogo, ngoja nimuite umuone, yeye yupo kwenye jengo letu pacha, ni mtangazaji wa Radio"

"Radio gani Lidya?" aliuliza kwa shauku

"Classic FM inamilikiwa na RM Classic group, nafikiri umewahi kumsikia akijiita E Lyn?" aliuliza Lidya huku akinyanyua simu ya mezani na kupiga. wakati huo Victor alionyesha dalili ya kukataa kumjua wala kumsikia E Lyn radioni.

Simu ilipokuwa ikiita upande wa pili, Lidya akasema kumwambia Victor

"Maryam anauliza wakati utakapo kuja kutaka msaada, wakupe aina yoyote ya msaada ama baadhi?" Hapo ndio sasa Victor akajua ni kwanini walicheka, akatikisa kichwa akiwa na tabasamu huku akisikiliza maongezi ya simu kwa umakini kati ya Lidya na upande wa pili.

Lidya alimsalimia mtu wa upande wa pili na kumuuliza kama anaweza kuongea na Evelyn? akajibiwa kuwa muda ule Evelyn yupo kwenye maandalizi maana muda si mrefu anaingia kwenye kipindi chake cha Lunch time, hivyo hawezi kuongea nae kwa sasa na kama ni muhimu aache maagizo.

Alichoweza kukisema Lidya kuwa si muhimu sana kwa muda ule bali atamtafuta baadae akitoka studio. akakata simu na kumtazama Victor aliekuwa akisikiliza yote aliyokuwa akiongea Lidya na majibu aliyopewa pia aliyasikia.

Victor hakuridhishwa kabisa na kauli aliyoitoa Lidya ya kumtafuta baada ya kipindi chake kuisha ndio kilimtoa mchezoni na kumfanya awe mnyonge. Lidya akalielewa hilo na kumuahidi siku ileile kabla haijaisha yeye atakuwa ameongea nae, Victor akamsisitizia ajitahidi.

hawakukaa tena pamoja kwa muda mrefu, Victor akaaga na kurejea kwake akiwa na furaha, akiamini tayari ameanza mwanzo mpya ambao ulionyesha dalili njema japo hakuwa na uhakika kama mtu amtakae ndio huyu mtangazaji wanae mhangaikia ma lah

Lakini alijipa moyo kuwa Lidya atakuwa amemfahamu ni nani, baada ya kumuelekeza kupitia Maryam. Alikiendea kitanda na kukilalia huku akiwaza haya na yale hadi usingizi ilipompitia ikiwa ni kama saa 8 na nusu.

Saa kumi na nusu jioni kwa mbali Victor alisikia mwito wa simu yake ikiita, kiuvivu akainyanyua na kuiangalia huku akijiuliza ni nani alie muamsha kwenye usingizi wake mtamu wa jioni, alipoiangalia namba ilikuwa ni ngeni, hakuweza kuitambua, hata hivyo alipokea na kuijibu

"Hellow"

"Lidya hapa, vipi wewe? inaonekana ulikuwa umelala, unaumwa ama ndio mapozi?"

"Hapana Shem, mawazo mengi kichwani, hapa Evelyn kule majibu ya Interview, si unajua kuwa majibu ni kesho"

"Pole sana Shem, majibu nayo yanatishia amani nini?" akatoa kicheko cha kirafiki Lidya

"Ajira Shem wangu, ok kwanza hebu tuongelee mengine, niambie..."

"Oooh, nipo na Evelyn hapa, na ndio mwenye simu hii niliotumia kukupigia, je tunaweza kupata kampani yako jioni hii...?" hata kabla hajamaliza Lidya, Victor akamkatisha kwa pupa

"Hilo sio swali Lidya, suala ni kuniambia ni wapi mlipo" akawa akiongea huku akinyanyuka kitandani

"Eeenh Victor, taratibu basi, sisi tupo huku Coco beach, utakuja?"

"Naomba dakika 45 tu zinanitosha kuwa hapo mlipo" Victor akaingia maliwatoni, baada ya kama robo saa alikuwa nje akifunga mlango wake na kuenda mbele kidogo akakutana na boda boda akaisimamisha na kupanda akimtaka dereva ampeleke maeneo ya jirani na Coco Beach.

Alipokaribia Coco maeneo ya Ubalozi waVatican, akampigia simu Lidya kumuuliza ni wapi walipo, Lidya akamwambia kuwa wao wapo mbele ya hotel wamekaa kwenye gari yake, hakuchukua muda akawa amewaona, alimlipa dereva wa bodaboda na kushuka.

Taratibu alianza kuelekea kule walipo Lidya na Evelyn na Evelyn alikuwa ni mtu wa kwanza kumuona Victor na hakujua kama huyo ndie mtu wanaemsubiri pale, bali akaongea

"Mvulana huyu anaekuja amependeza sana, mie hupenda sana kutoka na mtu anaejua kuvaa, angalia ile jeans aliyovaa na zile Rubber na tazama ile T shirt yake ya mikono mirefu zilivyo mtoa" Lidya muda huo alikuwa akimtazama Evelyn aliekuwa akiongea.

Alipogeuka na kumtazama anaesemwa, akatabasamu na kuweka chini juisi aliyokuwa nayo mkononi, kisha akaanza kukimbia akiwa ametanua mikono kama ishara ya kumpokea Victor

"Karibu Mr." alisema Lidya huku akimkumbati Victor, nae akajibu huku akimkumbatia

"Nimeisha fika Mrs. Ommy mtarajiwa" wakacheka wakiwa wamemsogelea kabisa Evelyn ambae alikuwa akiwatazama kwa tabasamu lakini akionekana kuwa na aibu usoni.

Mkono wa kulia wa Lidya, ukiwa umemshika Victor begani na mkono wa kulia wa Victor ulikuwa umeushika mkono wa kushoto wa Lidya, hapo sasa wakiwa wanatembea kuelekea alipo Evelyn, ndio wakaanza kusalimiana wakiwa na tabasamu tele usoni.

Walipomfikia Evelyn ndio Lidya akamtazama usoni na kusema

"Evelyn, kutana na Victor, ni shemeji yangu na ndio rafiki mkubwa sana waOmmy" kisha bila kupumzika akamgeukia Victor na kumwambia

"Hellow Victor, huyu ndie Evelyn, mtu alietusumbua kwa siku mbili mfululizo" Wakacheka wote

"Dada Lee acha mambo yako..." alikuwa amemnyooshea kidole Lidya kisha akamgeukia Victor

"Victor mambo?"

"Shwari Everlyn, nimefurahi kukuona na kutambulishwa kwako" akampelekea mkono

"Nami pia nimefurahi kukutambua" nae akaupokea mkono wa Victor kwa sekunde kadhaa na kuuachia.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Walifurahi na kuongea hadi jua jekundu nalo lilipopotea wao walikuwa bado wanapata vinywaji. Usiku ulipobisha hodi, ndio kwa shingo upande wakaamua kuondoka, lakini hawakuwa radhi kabisa kuachana muda ule. Victor hakuonyesha dalili yoyote ya kimapenzi kwa Evelyn.

Waliingia garini, Victor akashika usukani na pembeni yake akaingia Lidya, Evelyn akaingia kwenye siti za nyuma, safari ikaanza kwa kumrudisha Evelyn kwao maeneo ya Mwananyamala kwa Mama Zacharia wakaagana na kisha wao nao wakaelekea makwao, ambapo Victor alibaki kwake Ilala, kisha Lidya akaondoka na gari lake kuelekea nyumbani kwake.

Lakini kabla ya kushuka Victor, wakiwa wamebaki wao pekee wawili garini, Victor alitaka kujua ni vipi aliweza kutoka na Eve hadi kule beach. Lidya alicheka kwa sauti kubwa na kumwambia hayo ni mambo ya kike ndio yaliyotumika cha msingi ni yeye tu sasa kumaliza kazi ambayo Lidya kaisha ianzisha.

"Mwali tayari kaisha kolea mwenyewe na viwalo vyako, unajua wakati unatokeza mbele yetu kule beach hata kabla hajakujua, alisifu sana mavazi yako."

"Acha utani Shem, unasema kweli?" Aliuliza Victor huku akimtazama Lidya.

"Ohoo! Shauri yako, chelewa chelewa, mimi kazi yangu imeisha"

"Kweli Shem, subiri matokeo na zawadi bomba toka kwangu"

"Zawadi si muhimu, nitafurahi matokeo yakiwa bomba, hiyo ni zawadi kubwa kwangu na yatosha" wakatabasamu na kwa kuwa tayari walikuwa wamefika nyumbani kwa Victor, Lidya akahamia upande wa dereva na kumuacha Victor akiingia kwake nae akaelekea nyumbali kwake.

* * * * *



Ni usiku tulivu, mida ya saa nne hivi, Victor ndio kwanza amezima TV na kuamua kuingia chumbani kwake ili akalale. Akaona ni vema muda ule kabla hajalala, ampigie simu Evelyn na kujitambulisha rasmi. moja kwa moja akachukua simu yake na kujitupia kitandani. Akaitafuta namba ya simu ya Evelyn na kuipiga.

JIbu lilimvunja moyo lilikuwa likisema "Namba unayopiga..." akaikata hata kabla haijamaliza kutoa maelezo, na baada ya dakika kama 5 hivi akajaribu tena, jibu likawa ni lile lile, alihisi kukata tamaa.

akatulia na kufikiri ni nini cha kufanya, subira ilimfikisha kwenye wazo zuri, wazo la kutuma sms kwenye namba ya Evelyn ikimtaka mara tu Eve atakapowasha simu ambeep ili yeye ampigie. baada ya hapo akili yake ikamuagiza tafute sehemu yenye muziki laini utakao msaidia kumliwaza ili kupata usingizi kwa haraka.

Akanyanyuka na kuchukua Remote ya Sub woofer na kuanza kutafuta Radio station yenye muziki wa taratibu. akakumbuka ni vema muda huu asikilize Classic FM, kuna kipindi cha Romantic Love, akaamini pale atapata muziki mtamu.

Hakuwa amekosea, alipoipata tu, akakutana na wimbo mmoja mzuri sana wa kizungu wa mkongwa Lionel Richie uitwao 'I call it love' kisha akakutana nakitu kingine cha kizungu kiitwacho 'Good girl' kutoka kwa Joe Thomus.

Akawa akiufuatisha wimbo ule kwa taratibu akijenga taswira kuwa wimbo ule ni kama ulitungwa kwa ajili yake, hasa pale alipofikia kwenye maneno 'I gotta believe there's only 4 me, somewhere in this world, I will never gonna stop, search till I trap, till Im find that girl



Joe Thomus alikuwa akimaanisha anaamini kuwa kuna sehemu katika hii Dunia kuna mtu ambae moyo wake umemdondokea, hivyo hatolala wala hatoacha kumtafuta, hadi amtied mkononi mrembo huyo. kitu ambacho hata Victor aliamini hapaswi kumuacha Eve achukuliwe na mtu mwingine.

Ghafla akiwa ndani ya lindi la mawazo, akasikia sauti tamu ya kike ikiongea baada ya kuukatisha wimbo uliokuwa ukisikika, sauti ile haikuwa ni ngeni, aliizowea kuisikia kila mara na kuichukulia ya kawaida tu, lakini siku ile aliichukulia tofauti kabisa, alihisi imezidi uzuri.

Sauti ile ilisema hivi sasa ni saa 5 kamili usiku, moja kwa moja Victor akajua ni kwanini Eve hapatikani hewani, kumbe yupo Studio, kwenye kipindi ambacho kinatarajiwa kuisha saa 7 usiku, akatabasamu kwa kujua hilo, akatafuta Remote na kuongeza sauti.

Chochote kinachofanywa na mtu umpendae hata kama hakina maslahi basi kitakufurahisha, ndio hata Victor aliamini hivyo, kwamba chochote ambacho atakisikia kutoka kwa Eve tangu muda ule, kitamfurahisha na kumfanya azidi kuwa karibu nae kwa sababu kimefanywa na ampendae.

Bado kichwa chake kilikuwa kimetawaliwa na mawazo kadhaa, kwanza alifikiria ni jinsi gani alivyotokea kumpenda Eve kwa kumuona mara moja tu pia alikuwa akiwaza matokeo ya Interview aliyo fanya siku iliyopita na kisha matokeo yake yanatarajiwa kuwa hadharani siku ifuatayo, alipokuwa akifikiri hilo, alikuwa anapungua mwenyewe na kuwa mdogo.

Mawazo yalipomzidi, akaamua kumpigia simu mama yake na kumwambia kuwa ana wasiwasi na ule usaili alioufanya siku iliyopita, mama yake akampa moyo kuwa asihofu na wala asikate tamaa, kwani lolote linaweza kutokea, anapaswa kuwa tayari lakini sio kuogopa.

"Unatakiwa kuwa tayari na matokeo ya aina yoyote, ila amini kuwa utashinda na kuipata kazi ileile uliyoiomba" baada ya kauli ile iliyompa nguvu kiasi akamshukuru mama yake na kumtaka radhi kwa kumsumbua usiku ule, mama akamtoa shaka kuwa ni wajibu wake kumwambia tatizo lolote linalomsumbua, hivyo asihofu, kisha Victor akakata simu.

Faraja iliingia moyoni na kumshukuru Mungu kwa kumpa wazazi wenye hekima, akawa amemaliza moja kati ya masuala mawili yenye kumuumiza kichwa. Kwa kuwa alikuwa ameisha lipatia ufumbuzi lile moja basi akaamini halitamsumbua tena kwa usiku ule hadi siku ifuatayo muda wa alasiri ambao waliambiwa watapata matokeo ya usaili wao.

Likabaki suala moja tu kichwani... Evelyn! je usiku huu itakuwaje? atalala kweli? Hayo ni baadhi tu ya maswali machache kati ya mengi aliyo kuwa akijiuliza kichwani mwake pasina kupata majibu.

Saa saba kamili usiku, ikiwa ni siku nyingine hiyo tayari, Eve akaaga na kutoka Studio wakati huo Victor hata dalili ya usingizi yeye hana, kuna kipindi ulitaka kumchukua, lakini akahisi Eve anaweza kumpigia simu na ikaita hadi kukatika bila yeye kuisikia, hivyo isipokelewe na wakati huohuo ni yeye ndio alietaka kupigiwa. Ndio sababu akaamua asilale tu asubiri.

Kimya kikaendelea hadi saa 7 na robo hata simu ikawa haijapigwa kwake wala SMS ikawa haijapokelewa, nae kichwani usingizi umeruka kabisa, kawa hana hata lepe la usingizi, akaona sasa leo, kazi ipo, hadi akajiuliza kama pale ataulizwa achague kimoja kati ya kazi ama Eve, basi aliona kabisa kuwa hakuwa na chaguzi, vyote alivitaka sana.

Uamuzi wa mwisho aliouchukua ni kuomba ushauri kwa jamaa yake na ndugu yake wa karibu ambae ni Ommy, alihisi akiendelea kuwa kimya kwa suala lile ataumia. akanyanyua simu na kuanza kumtafuta Ommy, simu iliita kwa muda lakin hatimae ikapokelewa kivivu na Ommy

"Hey vipi Mzee? hujalala hadi muda huu? kuna tatizo gani?"

"Ommy ndugu yangu nisaidie, Evelyn amekimbiza usingizi wangu"

"Imekuwaje tena? Si Lidya ameniambia tayari amekukutanisha nae? Tatizo nini tena?"

"Ni kweli lakini sijaongea nae, nilipanga kufanya hivyo usiku huu, ila sasa simu yake haipatikani na kipindi kilichokuwa kikiendeshwa nae sasa kina zaidi ya nusu saa tangu kiishe, lakini bado hajawasha simu, sijui ni kwanini?" Ommy japo alikuwa na usingizi mwingi, lakini alitabasamu kwa swali la Victor, maana hata wangefanyeje wasingeweza kujua ni kwanini Eve hajawasha simu.

"Unasikia Victor, Jitahidi usiku huu umuache tu kama alivyo ila kesho asubuhi ndio umpigie, kwani muda huu huwezi kujua, labda amechoka na hataki usumbufu ndio maana hajawasha simu. Victor, kama mawasiliano ya awali yamekamilika, hofu ya nini jamaa yangu? Lidya yupo, ninakuhakikishia ushindi kwa asilimia 100, sawa mdogo wangu?"

"Poa mtu wangu, nashukuru sana kwa msaada wako lakini pole kwa usumbufu wangu"

"Hakuna neno Swahiba, Usiku mwema!" Aliaga Ommy na Victor akaitika na kukata simu.

Ndio sasa akavuta shuka ili kuutafuta usingizi akiwa na ushauri mpya kutoka kwa Ommy. Kweli hakuchukua muda mrefu akapata usingizi, na kulala kama pono. Simu ndio iliyomshitua asubuhi ya siku iliyofuata.

* * * * *



'Im waiting 4so long, 4 a miracle to come, but my heart told me to be strong...'

Hiyo ni sehemu ya wimbo wa mwanadada mwenye asili ya Canada anaeishi Marekani, aitwae Celine Dion, uitwao 'A new day has come' ambao ni sauti ya muito wa simu (Ringtone) ya Victor inapoita.

Leo muda huu inaita ni saa 3 asubuhi ndio iliyo muamsha na kumfanya akurupuke kitandani, akaangalia namba inayopiga na kukuta ni namba mpya kabisa kwenye simu yake na tena ni namba ya simu ya mezani, akapokea na kusalimia

"Hellow Victor!" Ilijibu sauti nzito ya kiume upande wa pili.

"Nani mwenzangu na una shida gani?" Aliuliza Victor kwa sauti ya usingizi

"Hapa ni Temeke Veterinary na unaongea na afisa utumishi, Mr. Katembo"

"Ooh! Sawasawa, habari ya kazi Mr. Katembo?" aliuliza Victor akiwa na wasiwasi huku akinyanyuka kutoka kitandani na kwenda kusimama jirani ya dirisha.

"Habari ni nzuri, lakini upande wako inaonekana ni nzuri zaidi, maana unalala hadi saa 3 mheshimiwa" Alitania Mr. Katembo.

"Hapana bwana mkubwa, ni vile tu jana nilichelewa sana kupata usingizi kwa kufikiria matokeo yetu ambayo yanatarajiwa kutoka jioni ya leo"

"Ooh! Pole sana kijana wangu, matokeo tayari yameisha toka, lakini kabla sijakupa matokeo rasmi, utapokeaje jibu lako?"

"Mr. Katembo..." Aliita Victor na Mr. Katembo akaitika, kisha Victor akaendelea

"Usiku uliopita nilikuwa na wasiwasi sana, ikanilazimu hadi kupiga simu kwa wazazi kuwaambia, walinipa moyo na kuniambia napaswa kuwa tayari kwa lolote, aidha kukosa ama kupata, lakini nijipe moyo kuwa nitaipata kazi na ikitokea nikaikosa, basi nisife moyo, kwani kuikosa mtu kazi uliyoiomba, haimaanishi umekosa maisha"

"Ok! Kijana unamaanisha upo tayari kwa lolote?"http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

"Haswaa Mkuu!" Alijibu Victor akijionyesha anajiamini na hali hakuwa akijiamini hata kidogo

"Sawa ninaweza kukupa hongera..."

"Ya nini bwana Katembo?" aliuliza Victor

"Kati ya watu 25 waliofanya Interview, ni watu wawili tu mliofanikiwa kuchaguliwa na kupata ajira, wewe na mwenzako ambae nae tayari nimeisha mjulisha, hivyo mnatakiwa leo hiihii kuripoti hapa ili kuja kuchukua maelekezo na mikataba, kwani mnatakiwa kuanza kazi wiki ijayo, mahali mtakapo pangiwa, sawa kijana?"

"Ndio mkuu nimekuelewa"

"Tafadhali fika kabla ya wakati wa chakula cha mchana, sawa?"

"Sawa nitafika kabla ya muda huo"

"Ok! Siku njema kijana" hivyo ndivyo alivyoaga Bwana Katembo

"Nawe pia" alijibu Victor huku akifurahi kwa kuruka ruka , akapiga magoti na kupiga ngumi tupu hewani, kama ishara ya kufurahi, si siri alifurahi sana.

Kabla ya kufanya uamuzi wowote, alikumbuka kwenye simu yake kuna ujumbe mfupi wa maneno, akaifungua sms ile na kukuta imetumwa saa 9 usiku akiwa amelala na ndio maana hakuiona, akaanza kuisoma na kuiona ilikuwa imeandikwa hivi;

"Samahani Victor wakati unasoma Sms nilikuwa Studio nikiwa nimezima simu, ndio nimewasha muda huu na ninajua kuwa utakuwa umelala, Im sorry siwezi kukupigia muda huu, nami nitazima simu tangu sasa hadi saa 4 asubuhi, tutawasiliana'



Victor akajisemea moyoni kuwa ni heri tu angepiga Eve, aliamini angesikia.

Hapo hapo nafsi yake ikapingana na akili yake, maana mbona ile sauti ya Sms haikuisikia? nafsi yake ikamwambia ni heri tu vile hajapiga. akachukua taulo lake na kuelekea zake bafuni kuoga.

Alipotoka kuoga alimkuta Ommy amekaa kwenye Sofa akiwa na Remote mkononi kabla hata ya salamu, Victor akasema;

"Ah! Mkurugenzi umekuja wakati muafaka sana, maana leo nimeamka na zali, kwanza umekuja na gari gani?"

"Escudo! lilikuwa jibu fupi tu la Ommy huku akibonyeza remote kubadili channel

"Ok! ngoja nijipambe tutoke!" Victor akaelekea chumbani kwake.

* * * * *



Baada ya dakika kadhaa Victor alitoka ndani akiwa amevaa suruali ya kitambaa cha rangi ya kijani na juu alivaa shati la rangi ya bluu ya bahari na chini alivaa viatu vyeusi vya ngozi.

"Heshima Mzee, umependeza mbaya, ama kuna mikataba unakwenda kusaini?"

"E bwana eeeh umejuaje? Twende zetu TMK Veterinary, mambo kule ni safi" Victor alilijibu swali la Ommy huku akifunga mlango wa chumba chake na kutoka kuingia garini.

Wakiwa ndani ya gari Victor akamueleza kila kitu Ommy kuhusu maongezi yake na Mr. Katembo, Victor alipomaliza kuongea, Ommy akamwambia

"Goli la kwanza hilo limetinga wavuni, tuombe Mungu ujihakuikishie ushindi kwa goli la pili, ama sio mjomba?" Swali la Ommy Victor hakuwa amelielewa, kifupi lugha ilimchanganya.

"Hapo kaka sijakusoma kabisa, sie wengine wakuja hapa mjini, lugha zenu utata" Wakacheka

"Namaanisha na kwa Evelyn napo nafasi ijae, mambo yaende vema kama TMK"

"Ndio hata nami nimekuwa nikiomba hivyo tangu asu..." Hata kabla hajamaliza kauli aliyotaka kuiongea, simu yake ikaita, akaichomoa mfukoni na kuangalia, akasema kwa furaha

"...kaka ndio yeye huyu..." alisema huku akipeleka simu sikioni na kusalimiana nae na kisha wakaulizana walipo. Victor ndio alianza kumjibu Evelyn

"Mie nipo maeneo ya Buguruni naelekea pande za Temeke, je wewe upo wapi muda huu?"

"Mie nipo nyumbani najiandaa, maana nina kipindi leo mchana"

"Ahaa! Sawa sasa mie nitakupitia hapo kazini kwako saa kwa ajili ya chakula cha mchana, Eve"

"Mh! Hapana.. mie ninamaliza kipindi saa 9 kamili, hivyo wewe njoo saa 10 jioni"

"Ok haina shida, nitakufuata muda huo, kwaheri kwa sasa"

"Ahsante, baadae" wakamaliza maongezi yao na kukata simu. Victor akamgeukia Ommy na kumwambia

"Kaka nilitaka goli hata la offside, sasa nimepata Penalty, sifanyi kosa"

"Kosa lolote dogo litakugharimu furaha yako, kazi kwako mdogo wangu"

"Huyo wa kukosea yupo wapi? Niamini mdogo wako" Victor alisema akijipiga piga kifuani kwa kujiamini sana hadi Ommy akatabasamu na kumchomekea neno

"Ufanye kweli labda utaacha kutusumbua watu usiku wa manane" Victor akacheka kwa sauti ya juu huku akirudisha simu mfukoni.

Tayari walikuwa wamefika maeneo ya Veterinary ambapo ndio safari yao ilikuwa inaishia pale, Ommy akamwambia Victor aingie ofisini kwake akamalizane nao, atakapo maliza ampigie simu ili amfuate

"Tayari umeanza mambo yako" Victor akamsemesha huku akifungua mlango wa gari.

"Halafu unajua nini Boss? Mie naona kuanzia leo tukitoka hapa, uanze kutumia ile Mark X maana nionavyo muda sio mrefu, mambo yako yatakuwa kama bahari, utakuwa na mambo mengi, sasa utanisumbua"

"Unataka kuniua sasa wewe" alitania Victor

"Ni bora ujiendeshe mwenyewe, wewe kama kufa ni bora ufe kwa hiari yako"

"Sawa Mkurugenzi, si unataka niuze sura sio? Mbona utanipenda? Baadae basi" Sasa ndio akashuka ndani ya gari na kufunga mlango kisha akaelekea ndani ya jengo, akimuacha Ommy akitabasamu na kutikisa kichwa.

Ndani ya ofisi Victor alipokelewa na Katibu Muhtasi, alimsalimia na kumuuliza ilipo ofisi ya Mr. Katembo. Bahati nzuri tayari palikuwa na maagizo

"Nafikiri wewe ndio Victor?"

"Yeah! Ndio mimi" alijibu Victor huku akiweka bahasha yake mezani.

"Sawa unasubiriwa ndani, mwenzio yeye tayari ameisha wasili kitambo, hivyo unasubiriwa wewe tu, ingia mlango huu..." akamuonyesha mlamgo kwa kutumia kidole, haukua mbali nao

"Nashukuru mrembo"

Akaingia ndani na kukuta watu wawili ambao aliwatambua bila hata ya kutambulishwa, mmoja alikuwa amekaa kwenye kiti kilichokuwa nyuma ya meza ya pale ofisini, huyu alimtambua kuwa ni Mr. Katembo, maana tayari alikuwa amemuona na kujitambulisha tangu siku ya usaili.

Na yule mwingine aliekuwa ameketi sofani, akahisi huyu ndio atakuwa ni Mr. Yakub Iddy, alikaribishwa na Katembo na kuketi sofani akiwa mkabala na Mr. Katembo na jirani ya Mr. Yakub , kisha Katembo akanza kuongea...

"Nafikiri si vibaya tukafahamiana, mimi ninaitwa Emmanuel Daniel Katembo, ni afisa utumishi katika ofisi hii" akawageukia Victor na Yakub kwa zamu, kisha akaendelea

"Naomba nikutambulishe Victor kwa Yakub, ninyi wote ni waajiriwa wapya katika ofisi yetu hii, muda mchache uliopita nilikuwa nikipongea nanyi kwa simu na sasa tunaongea ana kwa ana, karibuni sana vijana wangu" Alipomaliza kuongea vile, Victor na Yakub wakashukuru kwa pamoja, kisha Katembo akaendelea

"Nikianza na wewe bwana Yakubu, naweza kusema hongera kwani umepangiwa Ilala kwenye kituo chetu cha Amana hospitali, pale ndio utatakiwa kuripoti siku ya Jumatatu saa 2 asubuhi bila kukosa wala kuchelewa, kila kitu kuhusu mikataba yako utakikuta kwenye bahasha nitakayo kupa, sawa bwana Yakubu?"

"Nashukuru bwana mkubwa" aliitika kwa unyenyekevu na kunyanyuka kwenda kupokea bahasha kubwa ya kaki ambayo Bwana Katembo alikuwa ameinyanyua pale alipo kuwa amekaa. aliipokea kwa mikono miwili na kuiweka pembeni kidogo ya sofa alilokuwa amekaa.

Bwana Katembo sasa akamgeukia Victor na kumwambia

"Nikija upande wako bwana Victor, naweza kusema kuwa japo uliomba sehemu tofauti, lakini kutokana na vyeti vyako ulivyo wasilisha na matokeo ya usaili tulio ufanya juzi, tumeamua tukupe nafasi ambayo hujaiomba, hivyo kama nilivyo mwambia mwenzio, nawe pia jumatatu asubuhi unatakiwa kuwa hapa" Alisema huku akimtazama Victor aliekuwa akitikisa kichwa kukubali, kisha akaendelea

"Wewe utatakiwa kuripoti hahapa na utanikuta mie hapa ambapo niytakukabidhi ofisi hii tuliyopo nami nitarudi kwenye ofisi yangu, maelezo zaidi yanapatikana ndani ya bahasha hii" Katembo aliongea huku akimkabidhi bahasha ile Victor, nae alinyanyuka kwa nidhamu na kwenda kuipokea na baada ya kuichukua, nae akashukuru na kuketi tena.

Hawakukaa sana bali wakaaga na kutoka wakionekana ni wenye furaha sana, maana walisahau hata kumuaga Katibu Muhtasi alie wapokea pale, lakini walipo kumbuka, wakakuta yeye akiwa anawatazama kwa tabasamu na kuwaaga, wakatoka kuendelea na majukumu mengine.

Jioni ya siku hiyo ya Jumatano kulikuwa na kijimvua cha rasharasha, Victor akiwa ndani ya gari aina ya Toyota Mark X aliyopewa kutumia kwa muda na Ommy, alimfuata Evelyn ofisini kwake na kumchukua kumpeleka Namanga Best bite ili kuwa na wasaa mzuri wa kubadilishana mawazo.

Waliagiza vinywaji baridi na vitafunwa laini wakiwa wanabadilishana mawazo kama watu wenye miaka kadhaa tangu walipojuana, mwenendo ulikuwa ni wa kuimaliza siku yao vizuri sana, walifurahi sana. Dakika kadhaa mbele ukimya ukatawala, Victor akauvunja ule ukimya

"Evelyn..." Aliita Victor kwa sauti ya chini na ya taratibu lakini yenye msimamo iliyo mshitua Eve

"Yeah Victor" Eve aliitika akiwa anakoroga ndani ya glasi yake kwa kutumia mrija wake

"Naomba usikivu wako" hapa alikuwa akimtazama usoni

"Sawa nakusikiliza Victor"

"Evelyn sababu ya kuomba kuja nawe sehemu yenye utulivu kama hii ni kutaka kukufikishia kile kilichopo ndani ya moyo wangu" Victor sasa ndio akamwambia ni jinsi ganianavyo mpenda tangu alipo muona kwa siku ya kwanza, hakuacha kitu, alimueleza kila kitu alichopanga na kumalizia kwa kumwambia

"Naomba uwe mwandani wangu, nahitaji Eve uwe mpenzi wangu!"





"Mmh Victor, kumuona mtu mara moja tu ukampenda na kumpenda hapohapo?" aliuliza Eve

"Ndio Evelyn, kuna watu wanapendana hata kabla hawajaonana, unashangaa hii?"

"Sawa hali hiyo hutokea, mtu anaweza kumpenda mtu kwa kumsikia sauti yake tu" aliunga mkono kauli ya Victor na kumpa nguvu zaidi Victor ya kuendelea kufunguka

"Umeona eeh? na wakati mwingine hata kwa kusikia habari zake bila hata ya kumfahamu"

"Usemayo ni kweli, lakini ulipaswa kunichunguza kwanza ili nami nipate muda huo pia na kama tunakuwa wapenzi basi ni wale wamaojuana vema"

"Ni kweli Eve, lakini mie nipo tayari kukuchunguza wewe ukiwa nami, kwani hapo ndio nitaijua vizuri zaidi tabia yako, maana nitakuwa nawe muda mrefu"

"We huo ni upande wako, upande wangu je?"

"Hata nawe nakuomba unichunguze ukiwa nami pamoja, hapo hakuna kudanganyana, maana kila kitu unakuwa unakiona kiuhalisia, au vipi mrembo?" Alikuwa akichombeza kweli kweli Victor

"Hapana ni mapema mno kukubaliana na hayo uyasemayo Victor" Alijibu Eve huku akinyanyua mrija wake na kuuweka usawa na mdomo kisha akanyonya kidogo juisi yake ya Passion aliokuwa akinywa na kuendelea huku Victor akiwa anamtazama

"Unajua Victor, haina haja ya kukupa moyo wala kukudanganya, tambua kila kitu kinakwenda kwa wakati, mie niliapa kutokuwa na mpenzi kwa miaka miwili na sasa ndio kwanza nina miezi 9 tangu niweke ahadi hiyo, na siku zote nimekuwa nikikataa miito yote ninayopewa na mwanaume, hata hii yako pia, amini bila Lidya nisingekuwa hapa"

"Oh! Eve... acha kusema maneno makali hivyo mithili ya wembe mpyausemayo yanachana kati moyo wangu na kuniachia maumivu makali mno, tafadhali Evelyn..."

"Unajua Victor, nisizunguke sana, kifupi ni hivi, mimi kwa sasa sijaamua kuwa na mpenzi, hivyo nakushauri ni bora utafute mpenzi anaekufaa, sipendi kuumizwa, hivyo nami sipendi kumuumiza mtu, kiasi nilicho umizwa kimetosha na sasa sitaki tena..." Eve akabadilika ghafla sauti na sura

"Naomba sasa hivi unirudishe nyumbani, umenikumbusha machungu yaliyoanza kunitoka" huku akilia, alinyanyuka na kuelekea garini akimuacha Victor hata hajielewi, amepigwa na butwaa.

Wakati Victor anakurupuka na kukumbuka kumuita, Eve wala hakusimama wala kugeuka ikamlazimu amkimbilie na kumwambia

"Shika funguo hizi ukanisubiri garini nakuja, narudi kulipia" Eve bila hata ya kujibu akapokea funguo na kuelekea garini, Victor nae akarejea hotelini na kulipia walivyotumia kisha akaenda garini kuungana na Evelyn aliemkuta akiendelea kulia huku akiwa amejikunyata.

Akafungua mlango wa gari upande wadereva kwa nia ya kuingia ndani, lakini kabla hajaingia, akaufunga na kusimama nje akaegemea gari na mikono ikiwa juu kwenye roof, akionekana kuwa na mawazo mengi sana hadi aliposhtushwa na sauti ya Eve

"Victor nipeleke nyumbani nikabadili nguo, ninatakiwa kurejea kazini kwani nina kipindi cha usiku leo" Victor hakujibu chochote, aliingia garini na kuchukua funguo katika mikono laini ya Eve na kuwasha gari.

Lakini kabla hajaondoka akamgeukia Eve na kumtazama kisha akamwambia kwa sauti ya taratibu

"Samahani Eve, sikuwa na nia ya kukuumiza wala kukukumbusha maumivu yaliyopita, lakini nia yangu ni hiyo tu niliyo kueleza ya kuwa wapenzi mie nawe kwa sasa ili baadae tuwe wachumba na mwisho tufunge ndoa, samahani sana kwa kukukwaza Eve"

"Nimekuelewa Victor..." kabla hajaendelea zaidi, dirisha la upande waEve liligongwa na Muhudumu na alipofungua muhudumu akamwambia

"Samahani dada, ulisahau hii pochi pale ulipokuwa umekaa, ninaamini ni yako maana nilikuona wakati ukiingia hapa ulikuwa nayo, ama nimekosea?" huku akiipokea pochi ile, Eve akajibu kiupole

"Oh! Ahsante sana Anti, ni yangu hii pochi, nashukuru sana, subiri nikupe hata hela ya soda"

"Hapana anti, wewe ni mteja wetu, karibu tena siku nyingine" Mhudumu alimjibu Evelyn huku akiondoka kwa mwendo wa haraka na kuwaacha wakiwa hawana cha kufanya.

Victor akapandisha vioo vya gari na kurudi nyuma kidogo, akageuza na kuondoka kimya kimya bila kuongea chochote hadi wanafika kwa kina Eve, wote walionekana kuwa na mawazo tele vichwani mwao, akamuacha pale kwa Mama Zacharia kituoni, kisha nae akaelekea Victoria Kijitonyama kwa wazazi wake.



"Mama, baba yupo wapi?" Ni swali la kwanza Victor alimuuliza mama yake baada ya salamu, "Bado hajarudi, kwani vipi... mbona una furaha kiasi hicho?"

"Mama nimeipata ile kazi nilio iomba, tena palepale makao makuu ya ofisi, mikataba ndio hii, nitaijaza leo usiku nikiwa nimetulia nyumbani"

"Hongera sana mwanangu, sasa ninaamini utaanza kufaidi matunda ya jasho lako ulilo lihangaikia" Mama Victor alipo maliza kuongea vile, wakasikia sauti ya Mzee Johnson Maganga, baba yake Victor akija huku anaongea na simu akicheka.

Victor akaenda kujificha, Mzee Johnson alipofika alipo mkewe, bila hata ya salamu akamuulizia ni wapi alipo mwanae wa pekee, Mama Victor akajibu kuwa bado hajafika

"Aaah mke wangu, Ommy hawezi kuwa hapa halafu mie nisijue, maana ni lazima ningemkuta hapa ulipo wewe"

"Sasa nani kasema Ommy yupo hapa?"

"Je hiyo gari imekuja yenyewe hapo nje?" Huku akiendelea kumtafuta mwanae, akasema

"Leo nina habari nzuri sana kwake yeye..." Kabla hajamaliza, Victor akadakia

"Zipi hizo baba?" akajitokeza na kusalimiana na mzazi wake huku akitabasamu

"Anhaa kumbe upo mwanangu?" wakasalimiana kisha Mzee Johnson akaendelea

"Hongera sana mwanangu, nimepigiwa simu na jamaa yangummoja hivi anasema ameliona jina lako Temeke Veterinary, ukiwa umechaguliwa kuwa ni Afisa utumishi, je ni kweli?"

"Ndio baba ni kweli!" Mzee wake akampa hongera nyingi sana nae akautumia muda ule kuwaeleza ni vipi amechaguliwa.

Alikaa na wazazi wake hadi alipokula chakula cha usiku n abaadae akaaga na kuondoka pale Victoria kwa wazazi wake awapendao sana ikiwa ni saa mbili na dakika 45 usiku.

* * * * *



"Mambo vipi?" Ilikuwa ni sauti ya Victor ikimsalimia Evelyn

"Poa tu Victor, nakula saa hizi, karibu tule"

"Ahsante sana, mimi tayari nimekula, je nikuijie saa ngapi kukupeleka kazini?"

"Hapa nikimaliza tu kula napaswa kuondoka kwani nimechelewa sana, lakini usihofu, nitakwenda hadi pale kituoni uliponishusha na kuchukua Bajaj, wala usisumbuke Victor"

"Hapana Eve, napenda kufanya hivyo kwa leo" akaamua kumtania kidogo Eve ili kumchangamsha na kutaka kujua yupo katika hali gani tangu walivyo achana jioni hadi muda ule

"Nilisahau kukwambia kuwa ninamiliki Helicopter" Evelyn akacheka sana, na hicho ndio kitu ambacho Victor alikuwa akikihitaji kupita kiasi., akaendelea

"Muda huu tunaongea mie nawe, nipo hapa nje ninakusubiri"

"Victor ujue huu sio wakati wa utani, unaweza kusababisha nichelewe kazini bure"

"Oh, haya tu kama huamini, toka nje hata mara moja utaniona ninakusubiri"

"Ok! Tutaona kama ni kweli, namalizia kula nakuja" Evelyn akakata simu na kuendelea kula kwa haraka haraka, kwani iilikuwa kila kitu tayari kaisha fanya, yaani tayari hata mavazi alikuwa kaisha vaa, viatu pia vilikuwa miguuni, akatoka nje.

Hakuamini Evelyn pale alipo mkuta Victor nje ya nyumba yao akiwa ameka juu ya boneti ya gari akichezea simu yake. akamsogelea na kumuuliza amefika pale saa ngapi? Victor akamjibu kuwa tangu alivyomleta muda ule wala hajaondoka tena

"Eh muongo wewe mtu, sijapata kuona" aliongea Eve huku Victor akishuka kwenye boneti

"Mi ninakwambia kweli Eve, ningekuwachaje katika hali ile?" Alijitetea huku akimfungulia mlango na kumuonesha ishara kuwa aingie.

Muonekano na upokeaji wa tukio lile ilionyesha kuwa ni kama vile Evelyn hajawahi kufanyiwa kitendo kile na mpenzi wake, akashukuru na kuingia, Victor akafunga mlango ule nae akazunguka na kuingia upande wake na kisha akawasha gari na kuondoka kuelekea kwenye ofisi za Classic FM maeneo ya katikati ya Jiji.

Njiani walizungumza mambo mengi sana ya kimaisha bila kugusia kabisa suala la mapenzi. Saa 3 na dakika 45 usiku wakawa tayari wamewasili Classic FM na Victor akaisimamisha gari usawa wa jengo la Classic House. Hakugeuka upande wowote, bali alikuwa akitazama mbele huku mikono yake yote miwili kaiweka juu ya sterling.

Eve ndio alikuwa mtu wa kwanza kumuangalia Victor kwa jicho la utata kidogo na kumuuliza kwa sauti ya taratibu yenye mapenzi mazito





"Sasa?" Victor akamgeukia kumtazama na kutabasamu huku akitikisa mabega na kubenjua midomo kuonyesha dalili ya kusema sijui wewe, Eve akaendelea

"Nitakuppigia simu nikiwa ndani ya kipindi, ama kuna tatizo kwa simu za usiku?"

"Kwangu mimi sina tataizo lolotae na simu za muda wowote, na ujue ninapenda tuongee muda wote wa usiku hadi kunakucha kama itawezekana" Aliomba Victor

"Duh! mwenzio ninakuwa kazini na kesho tena asubuhi ninaingia kazini" Alijitetea Eve

"Hakuna shaka ninajitolea kama nilivyokueleza pale awali kuwa nitakufuata nyumbani kwenu na kukurejesha kila siku usiku kutoka kazini" Aliongea Victor huku akimtazama usoni.

"Hapana Victor, mbona ni mapema mno? Vuta subira, kwanza hebu nenda, ninaweza kuchelewa wakati tayari nimewahi" Evelyn akafungua mlango na kushusha mguu mmoja nje na mwingine ukiwa ndani akaendekea kusema

"Usiku wa leo nitakuwa Studio peke yangu, hivyo nitakupigia simu wakati kipindi kinaendelea, ninaamini tuataongea zaidi na utanifariji kutokana na upweke wa studio, ama sio Victor?"

"Wala usihofu juu ya hilo" Alijibu Victor kiufupi tu huku akimuaga na kuondoka.

* * * * *



"Victor kuna kitu ndani ya moyo wangu sijui kwanini sikukwambia palepale hotelini au wakati ule tukiwa ndani ya gari? ilikuwa ni sehemu muafaka wa kukwambia kile kilichopo moyoni mwangu! Sio siri umefanikiwa kuuteka moyo wangu kwa kiasi kikubwa, kifupi umeuteka moyo wangu mzimamzima, tena bila kipingamizi, hongera kwa hilo, lakini ninaomba uniahidi kitu kimoja tu, upo tayari?"

Ni swali lililomzindua Victor toka kwenye usingizi wa mang'amung'amu uliompitia akiwa anasikiliza Classic FM kwenye kipindi cha Romantic kilichokuwa kikiongozwa na Evelyn na wakati huo alikuwa akipitia baadhi ya vipengele vya mkataba wa kazi anayo tarajia kuianza wiki ijayo.

Alitazama saa yake ya ukutani na kuona ni saa 5 na nusu, akagundua kuwa tayari alikuwa amelala kwa zaidi ya nusu saa. Akanyanyuka kwa nia ya kwenda kufunga mlango awe tayari tayari kulala, simu yake ikaita, moja kwa moja kutokana na kuwa na usingizi, hakutaka hata kuiangalia, akaipokea.

Aliamini kwa asilimia mia moja atakuwa ni Eve, akapokea kwa shauku, kumbe hakuwa amepatia, aliepiga simu ile hakuwa Eve

"Kamanda vipi?" Ilisikika sauti ya kilevi ya Ommy, lakini hata kabla hajajibu

"Upo wapi saa hizi?" Aliuliza tena Ommy na ndio Victor akamjibu

"Nipo nyumbani nimelala"

"Kwanini ulale muda huu bila kunipa habari za Evelyn?"

"Usihofu, kesho asubuhi nitakuja kwako na kukueleza kila kitu na hatua niliyofikia"

"Poa bwana mdogo, mie nitakuwepo, je kuna tatizo lingine lolote?"

Maongezi yalipokuwa yanakuwa marefu, yalimkera Victor na sasa akaamua kuwa anajibu kifupi tu, akamjibu Ommy kuwa hakuna tatizo lolote, alimjibu vile ili tu Ommy akate simu mapema nae aendelee kuisubiri simu ya Eve ambayo alimuahidi kumpigia usiku ule.

Si muda mrefu baadae tangu amalize kuongea na Ommy, Eve akampigia simu nakuongea nae baada ya salamu na kumuuliza kama hajalala hadi muda ule

"Nilale wakati nina ahadi ya kuongea na mrembo"

"Mrembo yupi huyo anaekuweka macho muda wote huu?" Moyo wa Victor ukapiga mshindo, akajiuliza kwenye akili yake ina maana tayari amesahau kama tulipanga kuongea nae usiku huu?

"Aah! Eve, si nilikuwa na ahadi ya kuongea nawe usiku huu, ina maana umesahau?"

"Sasa Victor mie ndio mrembo? Ina maana hujaona warembo wewe? Eti mrembo.. mie ningekuwa mrembo katu nisingeumizwa..." kabla hata hajamaliza, Victor akahisi kuna tatizo akamuwahi kumkata kauli yake na kumwambia

"Aaah Eve achana na wasio jua thamani ya upendo, ndio maana mie nimejitokeza kwako, nimekuja kukuonyesha kuwa wapo watu wengi hawayajui mapenzi, ninaomba unipe nafasi ya kuwa wa ubavuni kwako, katu hutajuta wala kujilaumu, Eve tambua sijawahi kupenda kiumbe mwenzangu yoyote kwa kiasi kikubwa hivi nilivyo kupenda wewe"

"Victor ungeweza kunidanganya zamani na sio sasa, ni nani asie wajua nyie wanaume? hiyo ndio kawaida yenu. Ooh mie sijawahi kupenda hivi wakati huohuo kuna mwanamke mwingine pia unamwambia maneno hayohayo"

"Si mimi wa kufanya hivyo Eve, hao ni matapeli wa mapenzi" Alijitetea Victor bila kujua kuwa anazidi kuliweka pabaya zaidi

"Ahaa! Sasa unafikiri mie nitajuaje kuwa huyu ni tapeli wa mapenzi?" Aliuliza Eve na kumpa wakati mgumu mno Victor na kuwaza kichwani mwake 'Leo kazi ninayo' kisha akajibu

"Eve unatambua fika kuwa mapenzi hayana shule, hivyo ni akili yako wewe mwenyewe tu ndio inayo kuongoza, kama unampenda mtu ni juu yako kumchunguza hasa mnapokuwa tayari ndani ya mapenzi na sio kubweteka tu ama unajiachia kwa sababu eti umempenda, utaumia kila siku" maneno yale yalikuwa ni maneno kuntu kwa Eve ambae akanyanyua mdomo na kusema

"Hee wewe Victor ni laghai sana, una maneno matamu sana, sasa ngoja nikuulize swali moja lakini linaweza kuzaa swali lingine kutokana na jibu lako, sawa?" Alihoji Evelyn na kabla hajajibu, ikafanya Victor akumbuke ndoto yake alioiota muda mchache uliopita '...uniahidi kitu kimoja tu, je upo tayari?' akili ikarejea kwa Eve na kumruhusu amuulize swali lolote.

"Je unanipenda kwa dhati?"

"Ndi Evelyn, nakupenda kutoka moyoni kabisa."

"Nitaamini vipi hilo ulisemalo?" aliuliza Eve, swali hilo halikuwa gumu kwa Victor.

"Eve nipe nafasi ndio utaamini kile ninenacho"

"Ikitokea nimekupa nafasi hiyo, hutaniumiza kama mpumbavu niliekuwa nae kabla yako?"

"Hiyo ndio ahadi yangu ya kwanza kwako Eve."

"Je una malengo gani nami hapo baadae?" Victor alishusha pumzi na kujisemea tena moyoni

"Leo... Mwandishi wa habari ni mwandishi tu, maswali hayaishi!" akatengeneza sauti kidogo

"Kwa sasa awali ninahitaji uwe mpenzi wangu, kisha baada ya muda fulani ninataka tuwe ni wachumba na baadae tufunge ndoa ili tujenge familia bora" hilo ndio lilikuwa ni jibu la Victor.

Baada ya jibu hilo, ukimya ukatawala kidogo, yawezekana kila mmoja alikuwa kaitafakari ni kipi kifuatacho baada ya mazungumzo yao yale ya awali. lakini kadri ukimya ulivyozidi kutawala, ukamtisha Victor na kuhisi huenda Eve hajaridhishwa na majibu yake hivyo kakata simu.

Akamsemesha kwa kumuita jina na Eve akaitika na kumwambia yupo hewani anamsikiliza

"Victor sijui ni kwanini nimetokea kukuamini, haya bwana, mie nimekubali kukupa nafasi ndani ya moyo wangu, lakini una bahati moja mbaya..." lakini kabla hajamaliza kauli yake ile akamwambia

"Samahani Victor, nisubiri hivyo hivyo kwenye Line, usitoke hewani" Kichwa cha Victor kikaanza kuuma hasa pale alipokuwa akijiuliza ni bahati mbaya gani aliyonayo? Ama labda hawezi kuwa mpenzi wake? Lakini mbona tayari amekiri na kumpa nafasi moyoni?

Akiwa bado yupo kwenye lindi la mawazo, Evelyn akamsemesha

"Nakusikia vizuri Eve, unaweza kuendelea tu bila shida." Alijibu kwa sauti lakini akiwa hajiamini

"Bahati yenyewe mbaya ni kuwa, ukijaribu kunisaliti basi jua sifi peke yangu, nakufa nawe. Sitakubali usaliti wa aina yoyote wala aina yoyote ya maumivu, kifupi sitaki kuumizwa tena, umenielewa vizuri?" Victor akashusha pumzi za matumaini na kusema

"Kutoka kwangu Eve usitegemee aina yoyote ya usaliti na ninaapa sitakuja kukuumiza"

"Sasa ikitokea je?" Eve alizidi kumbana Victor

"Kamwe usitegemee kitu hicho Eve, mimi ninakupenda zaidi ya neno lenyewe linalowakilisha mapenzi." alimtepetesha Eve kwa maneno yake laini, Eve akalegea na kukubali

"Haya bwana, wewe lala acha mie niendelee kuchapa kazi" Alimaliza maongezi yao Eve kwa kuridhika na majibu aliyokutana nayo kwa Victor, nae akatoa shukran zake kwa Eve na kusema

Poa Eve, nashukuru sana kwa kupokea pendo lango, mimi napenda kukuhakikishia furaha tangu muda huu na hadi milele daima"

"Nitashukuru kama itakuwa ni kweli Victor, nami ninakuahidi furaha kila siku ya maisha yako"

"Naiwe hivyo!" aliongezea Victor na kumfanya Eve acheke na kuaga

"Usiku mwema Victor."

"Ok! I love U Evelyn."http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

"Me too! Nakupenda sana Victor" Wakaagana tena na lakini hakukuwa na mtu aliekuwa tayari kukata simu, kila mmoja alikuwa na hamu ya kuendelea kuongea na mwenzie, hadi Eve alipomwambia Victor kuwa akate simu ila wawasiliane asubuhi ifuatayo.

Victor akakubali na kabla ya kukata simu akamwambia atampigia asubuhi kabla hajatoka kwenda kazini. Maongezi yakaanza upya kwa kuulizana Eve anaingia kazini saa ngapi, nae akajibu kazini anaingia saa 2 na kutoka saa 4 asubuhi ileile. Walikubaliana Victor asipige tena simu, bali amfuate baada ya kipindi.





Sasa ndio wakaagana rasmi na Victor ndio aliekata simu, kwani alikuwa na hamu ya kushangilia ushindi, aliitupia simu kitandani na kurukaruka juu kwa furaha. Alifurahi kuliko siku zote katika maisha yake, sasa aliamini ndio ameyaanza rasmi maisha, kwani anaamini hakuna kazi kama kutafuta kazi, ambayo tayari anayo na ameipata bila usumbufu.

Kingine alichokuwa akiamini ni kigumu ilikuwa ni kumpata mpenzi, ambae nae ndio huyo tayari kaisha mpata tena ni yuleyule aliempenda mwenyewe toka moyoni mwake, gari ya kutembelea anayo japo si yake lakini yeye ndio mmiliki kwa kipindi kile.

Nyumba ndio hiyo anaishi peke yake, alihisi furaha ya ajabu mno, akaanza sasa kutamani asubuhi ifike haraka ili aweze kumfuata Eve, akajilazimisha kupanda kitandani na kuanza kuutafuta usingizi, hivi unafikiri hata alichelewa kuupata? baada ya kuzima taa, dakika 5 zilikuwa ni nyingi sana..

*******



Asubuhi ya siku ya Alkhamisi, Victor aliamka na kwenda kujiandalia kifungua kinywa, akakumbuka kuwa aliahidi kumpigia simu Evelyn, akarudi chumbani na kuchukua simu yake lakini kabla hajapiga akakumbuka kuwa ahadi ni saa 4 ndio ampigie baada ya kumaliza kipindi ili amfuate.

Simu akaitupia kwenye sofa na kuelekea bafuni kuoga. alipomaliza kujiswafi na kujipamba, akafungua kinywa kwa haraka na kutoka kuelekea kwa Ommy kama alivyo muahidi hapo ikiwa ni saa 2 na nusu asubuhi

Nyumbani kwa Ommy alimkuta akiwa na wageni watatu, wawili wakiwa ni wanawake na mmoja ni mwanaume, aliwasalimia na kuketi kwenye ile sofa aliyokuwa ameketi Ommy na kuchukua moja ya magazeti aliyokuwa ameyakuta pale mezani.

Alivutiwa na gazeti moja la kiingereza liitwalo Classic News lililokuwa na habari za usajili wa ligi mbalimbali za Ulaya na Dunia nzima kiujumla. Akalinyanyua gazeti lile na kutoka nalo nje, akaanza kupitia habari zile ambazo zilikuwa ni mpya kwake, alipomaliza akaliweka chini na kutoa simu yake mfukoni.

Akangalia muda na kuona ni wakati muafaka kwake sasa kuweza kuongea na mpenzi wake, akaenda hewani jibu sasa... 'The number Your Calling...' Ha! Alishangaa Victor, akahisi huenda labda amekosea namba, akarudia kwa namba zilizo hifadhiwa kwenye simu yake badala ya kuzitoa kichwani kama awali.

Jibu lilirudi kuwa ni lile lile lakini tofauti ikaja kwenye lugha tu, kwani sasa hivi alipata jibu kwa lugha ya kiswahili, akaikata hata kabla haijamaliza na kushusha pumzi kwa nguvu. Akasimama mikono akiwa kaiweka kiunoni na kuanza kufikiri huenda Eve ana tatizo maana si kawaida kuzima simu muda ule.

Lakini moyoni akajisemea huenda amejisahau tu kuzima simu, akaangalia tena simu yake na kurudi tena barazani alipoketi Ommy na wageni wake.

Nae akaungana nao japo alikuwa kimya akitafakari kuhusu kutokupatikana kwa Evelyn mpenzi wake muda ambao walielewana atakuwa hewani.

Wazo likamuijia ni vema amtumie sms ili akiwasha simu ajue kuwa alitafutwa na mpenzi wake. Akaandika hivi.. 'Mpenzi Eve, mambo vipi? Nilipenda kujua hali yako lakini sikufanikiwa kukupata hewani, je hujambo? Na vipi mbona umezima simu? Siwezi kufurahi hadi nisikie sauti yako, ukiwasha tu, nijulishe. Nakupenda Eve..’ akaituma kwa Eve na kubaki akisubiria majibu.

Sasa akapata nafasi ya kuongea na Ommy na kumpa michongo kamili juu ya Eve, Ommy alimpa moyo sana kwa hatua ile aliyofikia na kwa kuwa walikaa kwa muda mrefu, alimuhadithia kila kitu alichoongea nae na hadi ile ahadi ya kwenda kumchukua asubuhi ile na kuteseka kwake kwa kutokupatikana hewani kwa Eve.

Ommy alimtahadharisha kuwa asiwe na papara sana kwani hatua aliyofikia si ndogo, saa 6 mchana Victor aliondoka na kurejea kwake. Akiwa njiani kila mara alikuwa akiitazama simu yake ili kujua kama Eve amepokea sms yake, alitamani sana kuongea nae.

Aliingia ndani na kuchukua makaratasi yake ya mikataba na kumalizia sehemu ambazo alikuwa hajazimalizia kujaza kisha akazirejesha ndani ya bahasha yake ya khaki, kitendo cha kutupia tu bahasha kitandani, simu yake nayo ikaita.

Akaipokea na kumsikiliza yule aliepiga simu ile ambaealianza kwa kujitetea

“Victor Mpenzi wangu nilikuwa mkutanoni hapahapa ofisini tangu saa nne asubuhi nilipotoka kwenye kipindi na sasa ndio tumemaliza, mambo vipi lakini hubby?” alianza hivyo Evelyn.

“Ah mambo mabaya, wewe unafikiri mimi nimewaza nini? Kwa sababu mimi nilikujulisha tangu awali kuwa nitakupigia simu, mbona wewe hukunijulisha kama hautakuwa hewani?”

“Mmmh Victor, ina maana ndio umekasirika?” Aliuliza Eve kwa sauti ya mahaba

“Ndio, tena nina hasira...” Akatania Victor na Eve akaelewa, akacheka na kusema

“Pole mchumba wangu na leo ninaomba usitoke kwenda popote mpenzi wangu kwani nipo na Lidya hapa na baadae tutaelekea kwake, hivyo wewe jitayarishe, nataka uvae Jeanz ya blue na T shirt ya rangi yoyote na buti ya ngozi, hivyo vyote vipo?” Alihoji Eve

“Yeah! Vyote vipo na hata kama vingekuwa havipo, ningevitafuta tu, wewe tena umesema...”

“Ok! Ukae kwako ukiwa tayari tayari, nikifika kwa Lidya wakati wowote ninakupigia tuonane pale, sitaki wewe ufike kabla yangu, ila kwa sasa nami ninaenda nyumbani kwanza, sawa wangu?” Eve alimtikisa mkwara Victor

“Mapenzi yako yatimizwe” alijibu Victo kifupi, kauli iliyomchekesha Eve na kushukuru

Wakaagana kwa muda na kukata simu.

Simu ilipokatika tu, Victor akaelekea ilipo kabati yake ya nguo na kutoa aina zile za nguo alizo ambiwa na mpenzi wake, akazitupia kitandani. Alitoa jeanz ya blue ya kuiva sanaaina ya Xtra Brain na T Shirt nyeupe iliyo andikwa ‘Ramson Wear 80’ sehemu za kifuani ikiwa ni ya mikono mifupi.

Sehemu ya chini ya kabati alifungua na kutoa kiatu kimoja kikali sana aina ya ‘CAT’ aliyoinunua Uingereza wakati alipokwenda Field alipokuwa akisoma India. Alipotazama nguo zile akagundua kuwa bado hazijatimia.

Akatoa sox za rangi ya kijani mpauko zilizoandikwa ‘Sixers’ ambazo alipewa zawadi japo zilikuwa ni za mtumba, lakini zilikuwa sio za taratibu. Akazibusu na kuzitupia kitandani. Bado lakini hakuwa ameridhika na vile viwalo, akapeleka mkono wake juu ya kabati na kuvuta kofia.

Ilikuwa ni kofia aina ya Kapelo iliyo kuwa na chata kama ile iliyokuwa imewekwa kwenye Tshirt yake, yaani ‘Ramson Wear 80’ hapo sasa akaridhia na kuviweka tayari tayari ili muda wowote akisikia simu ajipambe na kwenda kuitikia wito.

Kwa kuwa alikuwa anaona muda unaruhusu wa yeye kufanya mambo yake na hakuwa na cha kufanya, alikuwa amevaa Pocket ya kijani na singland nyeupe akaenda na kufungua friji na kutoa kiboksi cha maziwa fresh na kutoka nje ya nyumba akakaa na kupoteza muda.





Alikaa kwa dakika kadhaa hadi ilipotimu saa 10 alasiri akaona ni heri aende kutayarisha chai ya jioni. Akatenga maji kwenye jiko lake la gesi na kurudi kuketi kwenye sofa. Kila alichofanya aliona hakifai, akawa anaona kama chumba hakijakaa sawa, aliona hapako kwenye kiwango.

Polepole bila haraka akaanza kupafanyia usafi huku akipanga hiki na kile japo hapakuwa pachafu ila baada ya marekebisho yale machache, paling’aa zaidi nae akaridhika na kuelekea jikoni, akaipua maji moto na kuyamimina kwenye chupa ya chai na kuiweka inapotakiwa.

* * *



Kahawa yenye maziwa na sukari ikiwa ndani ya kikombe cha chai, alimimina maji ya moto kwenye kwenye kikombe hicho na kukoroga, kisha akatoka pale jikoni na kuelekea Sitting Room akawasha TV na kuanza kuangalia, hakuridhishwa na vipindi vilivyokuwa vikiendelea muda ule.

Alizima TV na kuangalia saa, akaona ni saa 11 na robo jioni, akaona sasa ni wakati muafaka wa kumpigia simu Eve ili amuulize ni vipi mbona kimya? Maana yeye tayari alikuwa ameisha choka kukaa peke yake, na kama bado sana basi ni heri amjulishe ili nae atoke aende kwa jamaa wa jirani akapige story au aende akacheze Pool.

Hata kabla hajatimiza azma yake akasikia wimbo mmoja wa zamani sana, ni zile nyimbo maarufu kama zilipendwa, ilikuwa ni wimbo wa Marehemu Kabasele ya M’panya maarufu kama Pepe Kalle wimbo uitwao Hidaya. Sio siri ilimkumbusha mbali sana, enzi zile za kutoa show kwenye harusi.

Basi akanyanyuka na kuelekea chumbani sehemu alipohifadhi CD zake. Hakuchukua muda mrefu kukiona kile alichokuwa akikitafuta na kurejea Sitting room hadi kwenye muziki wake mkubwa. Akaidumbukiza ile CD aliyotoka nayo chumbani na kwa sauti ya kawaida kabisa ulisikika mziki wa zamani kidogo.

Unaweza kuhisi ni muziki gani uliosikika? Baadhi ya maneno yaliyo sikika ni haya

‘Evelyn Evelyn (Evelyn) Evelyn mtoto wa Burkina Faso. Oooh, Eeeh, Evee...’ akafurahi mwenyewe na kumpigia simu Eve kujua ni wapi alipo na kama vipi Victor amfuate hukohuko.

“Sehemu nilipo si mbali sana na hapo kwako, fanya hivi, hebu toka nje utaniona”

“Eve elewa mi sitaki usumbufu” huku akitoka nje, hakuamini kabisa macho yake baada ya kuiona Escudo ya Ommy ikiwa na watu watatu ndani na imepaki nje ya nyumba yake.

Akatikisa kichwa na kukata simu kisha akawakaribisha ndani huku akisema anawashukuru sana ama siku ile wamemuweza sana. Ommy akacheka na kukataa kuwa hawaingii ndani

“We vipi? Kumbe hata kujiandaa hujajiandaa bado?” Ommy aliuliza

“Ndio maana nataka muingie ndani, Lidya hebu mshawishi Ommy akubaliane nami...” huku akimgeukia Eve akaendelea kusema

“Eve mpenzi wangu, karibu kwangu, karibu ndani” wote wakamuangalia Eve kama vile yeye ndio mwamuzi wa mwisho, akavunja ukimya kwa kuuliza;

“Dada Lee, tunaingia ama hatuingii? Eti shem Ommy?” Ommy akatoa jibu huku akifungua mlango wa gari na kushuka

“Ok! Tuingieni lakini tusikae sana, si mnakumbuka nimewaambia kuwa kuna sehemu tumealikwa?” swali la Ommy lilijibiwa na Victor akiwa ni mwenye furaha tele

“Ninawaahidi hatutakaa sana humo ndani, karibuni sana” wakashuka wote garini na kuelekea mlangoni, Victor akiwa mbele na kufuatiwa na Ommy, Eve na Lidya walifuatia nyuma kabisa wakiwa wameshikana mikono.

‘Ooh, eeh Evee...’ ndio neno la kwanza walilolisikia mara tu mlango ulipofunguliwa na Victor na kuwakaribisha ndani. Lidya na Ommy walimtazama Evelyn na kucheka, Eve akabaki ametabasamu bila kujua ni kipi kinacho wachekesha wale wapendanao wawili.

Victor nae hakujua ni kipi kilicho wafurahisha, akamuuliza Eve kina Ommy wanacheka nini? Eve nae akajibu kuwa hajui, ndio Ommy akajibu huku anatabasamu

“Dah mzee nimeaminia, inaonekana wimbo huu kwa sasa unapata taabu sana” kwa jibu hilo ndio Victor na Eve wakaelewa ni nini kilicho kuwa kikiwachekesha, nao wakacheka kisha Victor

“Hujatulia wewe, karibuni ndani” baada ya kuwakaribisha yeye akapotelea chumbani kwake. Baada ya kama robo saa hivi, Victor alirudi Sitting room, akiwa amebadilika kabisa, alikuwa amevaa vilevile alivyotaka Eve, akakurupuka Lidya kumfuata Victor huku akisema

“Ooow umependeza kweli handsome” Akamkumbatia huku Ommy akitabasamu

“Oh ahsante sana, nami sasa nipo tayarivipi hapo Ommy? Nafikiri nami sasa naweza kuongozana nanyi” aliuliza Victor huku akijigeuza huku na kule

“Yeah! Sasa una haki zote” Ommy alijibu huku akinyanyuka kwenye kiti alichokuwa ameketi

“Mrembo vipi? Naweza kutembea nawe sasa hata barabarani?” victor aliuliza kiuzushi akiwa mbele ya Eve huku akijigeuzaa geuza. Kabla Eve hajajibu, Lidya akawahi kusema

“Sipati picha sijui itakuwaje? Eti Eve...” Eve hakusema maneno mengi bali alicho kisema ni

“Victor umependeza sana” wote walikuwa wameisha simama kasoro Eve tu, Victor akamnyanyua na kumkumbatia akimnong’oneza

“Ahsante mpenzi wangu kwa kunichagulia nguo nzuri za kuvaa, naona sasa tunaweza kuondoka”

Kisha akamgeukia Ommy na kumuuliza ni wapi wanapoelekea jioni ile? Ommy akajibu

“Unasikia Victor, wewe ndio upo nyuma ya wakati, kifupi ni hivi kuna sherehe tumealikwa na jamaa zangu huko maeneo ya Afri Center, inategemea kuanza saa moja usiku na hapa ninaona kama kuna nusu saa tu hapa imesalia, hivyo ninaona ni vema tungeanza safari, kadi yenu nitawapa tukifika ukumbini, sawa rafiki?” ommy alimshika kiuno Lidya na kuanza kutoka

“Ah mie sina wasiwasi nawe” nao walitoka nje na kuelekea ilipo Escudo, lakini Eve aliekuwa kimyaa muda mrefu akasema

“Shem unajua jinsi tulivyovaa sisi haipendezi kushuka kwenye gari moja nanyi, mimi nashauri ni vema ninyi mkatuachia gari yenu kisha mkatumia baloon kwani mavazi yenu yanaonekana ni ya kiheshima zaidi, ama waonaje Shem?” Aliuliza Eve huku akimtazama Ommy.

“Ayaa! Ayaa... Lidya muda si mrefu Victor atatuachia vumbi tu, nawea kusema kama atamtumia vizuri huyu Eve, atafika mbali sana kwa muda mfupi, anafikiria mbali mno kwa haraka sana, kifupi Evelyn hata nami nakubaliana nawe”

Jibu la Ommy liliendana na kitendo cha Ommy kuingiza mkono mfukoni na kutoa funguo ya Escudo na kumpa Victor ambae aliupokea ufunguo ule na kumshika mkono Evelyn kisha wakaelekea ndani kufuata funguo ya Baloon.

“Mpenzi hiki ndio chumba ninacholala, ninaamini mara nyingine utakapokuja, utakifahamu zaidi”

“Usihofu mpenzi wangu, twende zetu nje wanatusubiri” Victor akachukua funguo za gari juu Dressing table na kugeuka, walipoanza tu kutoka, Victor akahisi kama kuna mvuto fulani hivi umetokea. Akageuka na kumtazama Eve na kukuta hata nae anamuamgalia kwa umakini.

Baada ya Eve kutambua kuwa anaangaliwa, akasema kwa aibu huku akiangalia chini

“Victor umependeza” Victor hakijibu, bali alimsogelea na kumvuta kisha akamkumbatia, akaanza kumchezea mwilini.

Ghafla kama mtu aliekumbuka kitu fulani, Eve akakurupuka na kumsukuma kule Victor

“Hebu niache, ujue tunasubiriwa huko nje” Victor akamuachia na kushusha pumzi kwa nguvu, akambusu na kisha wakatoka nje Eve akiwa mbele na kumkuta Ommy ameegemea Baloon huku Lidya akiwa anamchezea tai yake na amemuegamia.

Victor akafunga milango yoteya nyumba na kumrushia funguo ya Baloon Ommy nao wakaingia ndani ya Escudo, safari kuelekea Afri Center ikaanza, Baloon ikiwa mbele, ndani walikuiwepo Ommy na mpenziwe Lidya na nyuma kwa karibu ilifuatia Escudo iliyokuwa imewabeba wapenzi wawili ambao walionekana wao ni wenye furaha zaidi.



http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

*******

Ommy hakuwapa kadi kama alivyokuwa amewaahidi pale awali kuwa atawapa kadi wakifika ukumbini, bali alipofika pale alishuka na kuongea na watu fulani waliokuwa getini walionekana kama ni watu wanao husika na sherehe ile walio alikwa kina Ommy. Walikubaliana jambo fulani na kisha Ommy akaondoka kuelekea ilipo Escudo.

Alipofika kwa Victor alimwambia kuwa kuna sehemu imeandaliwa maalum kwa ajili yao, akamtaka apaki gari sehemu atakayo onyeshwa kisha aende getini na ataonyeshwa ni wapi sehemu ya wao kukaa. Mwisho akamwambia maswali yote ayahifadhi, atauliza wakati wa kurejea nyumbani.

Ommy alijua kabisa kuwa ni lazima Victor anataka kuhoji ndio maana akamuwahi, hakumpa nafasi hata kidogo ya kuuliza swali, yeye akapotelea ndani, Victor akatabasamu na kusema

“Dah! Kaniotea huyu, kashtuka kama nilitaka kumuuliza, ah lakini hamna tabu” Victor alimtazama Eve aliekuwa ametabasamu na kuongeza

“Ukiona hivyo ujue kuna kitu, labda muhusika wa sherehe hii ni mtu wa karibu yako, hivyo wanataka kukufanyia Suprise kama nilivyokufanyia mimi leo, vipi ile, umeipenda?” Eve alicheka wakati Victor akijidai kanuna, kisha akasema

“Ulifikiri utanikuta na mtu ndani eti? Wewe subiri Suprise nitakayo kufanyia mimi, hutasahau hadi unakufa” huku akitafuta sehemu nzuri ya kupaki gari, Eve akamjibu kwa kubeza

“Thubutuu, huwezi kuizidi hii yangu” Victor akakubali kushindwa na mpenzi wake

“Poa tu Eve, si tupo wote pamoja? Wewe mwenyewe utanikubali.” Wakatoka na kufunga milango ya gari lao.

Baada tu ya kupaki gari lao, mlinzi mmoja alievaa sare maalum aliwafuata na kuwauliza kama wao ndio Mr. & Mrs. Victor Maganga? Wakatazamana na kuitika ndio kwa pamoja, jamaa akawakaribisha ndani. Walimfuata hadi ndani ya ukumbi na kuwatambulisha kwa mlinzi aliekuwa pale mlangoni kisha yeye akarudi zake getini.

Waliruhusiwa kuingia ndani ya ukumbi na kukutana na ajabu nyingine, ndani ya ukumbi walikuta watu kadhaa, ila viti vilikuwa ni vinne tu na viwili kati ya vile viti vinne tayari vilikuwa vimekaliwa na watu walio onekana kama ni wapenzi.

Muziki laini ulikuwa ukitumbuiza kwa mbali na mlinzi akawaambia wao wanatakiwa kuketi kwenye zile siti mbili zilizosalia, wakasogea na kuwasalimia wale walio wakuta pale.

Lakini ilionekana Eve alikuwa akimjua vema yule jamaa aliekuwa ameketi akiwa na mwanamke na mtu huyo huyo pia alionekana akimfananishaVictor kama ni mtu aliewahi kumuona sehemu fulani.

Msichana aliekuwa na yule jamaa, Victor wala hakupata taabu kumfahamu maana alikuwa ni Secretary kwenye ile ofisi ambayo anatarajiwa kukabidhiwa wiki ijayo pindi atakapoanza kazi.

Alimsalimia kwa bashasha na kisha kuagiza kinywaji chake akipendacho na kukibugia taratibu akimtazama mpenziwe aliekuwa akitazama waalkwa wenzie waliosimama.

Muziki wa taratibu ulikuwa ukisikika kwa mbali ulidumu kwa muda mchache tu kisha MC akaingia na kusimama. Baada ya salamu akafungua rasmi sherehe ile japo hata nae hakujua ni shughuli ile ni ya nani lakini alijitetea kuwa ratiba ipo na ndio itamuongoza.

Kwa kuanza tu akawaamuru kutambuana wenyewe kwa wenyewe,watu walio karibu karibu waanze kutambuana wenyewe. Akasema kuwa anatambua fika kuwa hakuna aliekuja peke yake mle ukumbini, hivyo akawaomba wanapojitambulisha wajitambulishe wote ili wakati wakuondoka mle ndani isije kutokea ugomvi.

Mwisho kabisa kasema kuna pairs mbili ni muhimu na hizo atazitambulisha mwenyewe mbele ya hadhara ile na kisha akatoa nafasi kwa waungwana wale kutambulishana.

Victor alikuwa ni mtu wa kwanza kunyanyuka na kumnyanyua pia mpenzi wake ambae alionekana ni mnyionge kidogo. Yule jamaa aliekuwa ameketi nao pale nae akasimama na kumnyanyua mwenzi wake alieonekana kuwa na furaha.

Wanaume ndio walianza kupeana mikono, Victor ndio alikuwa mtu wa kwanza kuanza kuongea

“Mimi ninaitwa...” Hata kabla hajaanza kujitambulisha yeye, Eve alimkatisha kauli na kusema

“Ladies first” kisha akaendelea “Naitwa Evelyn Dotto, sihitaji kujitambulisha zaidi, kwa faida ya Aunt hapo, mimi ninafanya kazi Classic FM ni mtangazaji pale na hasa vipindi vya taratibu. Huyu kulia kwangu ni Victor J. Maganga, ni Afisa uhusiano mtarajiwa waa TMK Veterinary na ndie mchumba wangu” Hivyo ndivyo alivyo maliza utambulisho Eve.

“Nimefurahi kukufahamu Mr. Victor, mimi ninaitwa Ondiek Maneno,ni meneja wa Classic FM na ndio maana bi Evelyn alisema ninamtambua vema, ni kweli maana nimefanya nae kazi kwa muda mrefu sana. Victor alitikisa kichwa kuonyesha ishara ya kukubaliana na maneno ya Ondiek

Kisha Ondiek akaendelea

“Huyu pembeni yangu ni Bi Yasmeen Mussa, nae ninafikiri muda si mrefu Mr. Victor utakuwa nae pale TMK Veterinary maana yeye anafanya kazi kule kwa sasa ni mchumba wangu na ninategemea kufunga ndoa nae mwakani” Nae alimaliza kutambulisha upande wao na wote wakashikana mikono.

Waligonga glasi zao na kunywa vinywaji vyao kisha wakaketi. Tukio kama hilo lilitokea karibu kila sehemu palipokuwa na watu zaidi ya wawili. Sherehje iliendelea kama kawaida, kila mara Victor alikuwa akimtafuta Ommy pale ukumbini hamuoni, akaamua kumpigia simu, wakati mwingine akawahapatikani.

Hata alipopatikana alisema anawasubiri wahusika na ndio atakao ingia nao pale ukumbini hivyo akawataka wasiwe na wasiwasi, kweli roho zao zikatulia, MC akapanda tena jukwaani na kusema

“naona muda muafaka wa kujua sherehe yetu ni ya nini, sasa umewadia... niseme ama niache?” aliuliza kwa mbwembwe MC akiwa na lengo la kuwachangamsha waalikwa nao wakajibu kwa pamoja “Semaa” akageuka huku na huku kisha akaendelea

“Tumekusanyika wote hapa kuja kufurahi katika sherehe hii ambayo imetayarishwa kwenu na Ramson Entertainment ikiwa ni kwa ajili ya Ommar Bazzo na Bi Lidya Camara, nao ninaomba waingie ndani... makofi kwao tafadhali” akanyamaza na kuwaongoza wageni waalikwa kupiga makofi kisha akaendelea

“Sherehe hii ni maalum kwa ajili ya kuvishana pete ya uchumba katika usiku huu tulivu,”

Sio tu Victor na Eve walioshangaa, bali kila mtu alibaki ameduwaa na kushikwa na butwaa, hakuna hata mmoja alieweza kudhani kama inaweza kuwa ni hivyo. Wote kwa pamoja wakapiga makofi.

Mc akaendelea na ratiba kama ilivyokuwa inaonyesha hadi wakavishana pete, ukafika wakati wa chakula na vinywaji, kampuni ya SSB ndio iliyohusika na kuandaa na kugawa chakula hicho. Walipokuwa wakiendelea kula, Ondiek alimuuliza Victor

“Samahani bwana Victor, huenda nimekufananisha, je wewe ndio Victor Johnson?” Victor alishtuka na kukubali kisha akamuuliza yeye nae ni nani

“Oh Mr. Ni muda mrefu sana hatujaonana mie nawe, tulisoma pamoja shule ya msingi Victory, unamkumbuka Uday Maneno?”

“Ha siamini” Wote wakamyanyuka bila kuambiana na kuanza kucheza muziki wa zamani kidogo wa Twist kutoka Kenya huku wakiimba

‘Watu wa Nairobi wanapenda sana kuimba imba na kucheza Twist...’ Sio siri walionekana kufurahi sana na kukumbuka mbali mno. Zaidi ya yote wale waliokuwa nao meza moja walifurahi kwa kuwa walikuwa wakijuani nini kinaendelea.





Wale waliokuwa mbali walionekana kushangaa tu, Victor na Ondiek wakakumbatiana na kisha wakarudi kuketi na kuendelea kula kama awali ila sasa ikiwa furaha imetawala zaidi ya ile ya awali.ukawadia wakati wa muziki, MC akasimama na kusema

“Kama bado yale maji ya dhahabu hayajaingia barabara ndani ya ubongo, naqfikiri mtakumbuka niliwaahidi kuwa kuna double na tena ni pair mbili, ambazo nitazitambulisha kwenu, mnakumbuka?” wote ukumbini wakapiga mbinja na kuitika ndio kukubali.

Kisha MC akaanza kuwapa maelezo ya pair zile mbili kuwa ni za kuwakilisha familia mbili zabwana na bibi Ommy ambazo hazikufanikiwa kufika kwenye sherehe hizi kwa sababu zilizo nje ya uwezo wa wahusika na uharaka wa sherehe yenyewe.

Hakuna alieweza kuhisi kuwa meza hii iliyokuwa hapa mbele ndio walengwa wa MC.

Mc akaendelea kwa kuomba kwanza autambulishe upande wa Mr. Ommy, na kuwaambia wale atakao wataja pale anaomba wasimame na kuwasalimia wageni waalikwa na kisha atawapa zawadi maalum kwa ajili yao. Akameza mate kidogo kisha akaendelea

“Mr Victor J. Maganga simama pamoja na Miss Evelyn Dotto” pasina kujiamini wakasimama na kupunga mikono hewani. Wakiwa bado wanashangaa kwa tukio lile, watu wote akiwepo Ondiek ambae hakujua kuwa muda wote amekaa na wawakilishi wa wazazi wa Ommy bilahata kutambua.

Mc alikuwa mtundu sana, bila hata ya kuwasiliana na Victor na Eve, akasema kwamba zawadi walio ichagua wawakilishi wa wazazi wa Ommy ni kufungua muziki, hivyo akamuamuru DJ aende akawasiliane nao ili ajue ni aina gani ya muziki waitakayo wakati wao wa kufungua muziki utakapofika.

MC alizima mic yake na taratibu muziki wa vyombo vitupu ukawa ukisikika kwa mbaali, DJ kasogea pale mezani na kusikiliza wimbo am,bao Victor na Eve watauomba. Walitazamana na kutabasamu mara DJ alipofika kisha Eve akataja wimbo na DJ akatikisa kichwa kukubali.

‘Ur not alone, I’ll be with U, don go away, Ur always in my heart, Ur not alone...’ Ni wimbo wa Marehemu msanii nguli wa muziki wa Pop, Michael Jackson uitwao ‘Not alone’ ndio wimbo ambao Eve aliouomba ili kufungulia musiki, wao tayari walikuwa mbele wakifungua muziki.

Lakini hata kabla wimbo haujafika hata kwenye Chorus, sakafu yote Ya ukumbi ilishajaa wapenzi kadhaa waliovamia na kuwaunga mkono Victor na Evelyn ambao walicheza vizuri sehemu za wimbo ule ambao kwao ilikuwa ni Suprise lakini wakaitendea haki.

Wimbo ulikwisha na ukafika wakati wa kutoa zawadi, kwa kuwa hakuna aliekuwa amejiandaa kwa hilo, hivyo watu wote walinyanyuka nakwenda kuwapa mikono ya hongera, meza kuu waliyokuwa wamekaaVictor na wenzie ndio ilikuwa ni meza ya kwanza kwenda kuwapa hongera.

Kama kawaida, Victor huwa hakosi la kusema hasa anapokuwa na Ommy, akamwambia kuwa hata kama ni Suprise, ile yake ilipita kiwango, akamwambia hadi muda ule kwa siku ile moja tu, tayari amesha kutana nazo 3, Ommy alicheka na kusema imebaki moja ya mwisho.

Victor nae akacheka na kurejea sehemu yake na kuketi, taratibu zote zilifuatwa kama ratiba ilivyo onyesha, ukawadia wakati wa kufunga muziki, kila mmoja akawa anataka kujua ni nani atakae wakilisha upande wa Lidya? Yasmin akamuuliza Evelyn mbona hawakuwaambia kama wao ni wawakilishi wa wazazi wa Ommy?

Eve akatabasamu na kumwambia kuwa hata wao hawakujua kama wapo pale kwa ajili hiyo,kauli hiyo ikamshangaza Yasmin na kujikuta akimwambia Eve kuwa muziki walio uomba ni mzuri na pia hata kuucheza, waliucheza vema, ajabu tu kuwa hawakujiandaa.

Eve akasisitiza kuwa walishitukizwa tu na wala hawakuomba kufungua muziki. Yasmin alitikisa kichwa kushangaa. Sauti ya MC ikasikika ikiwataja majina ya wawakilishi wa wazazi na familia ya Lidya kuwa ni

“Naanza na bi Yasmin Mussa tafadhali simama na bwana Ondiek Maneno, salimieni ndugu na jamaa zetu,” Japokuwa Victor na Eve walikuwa hawajajiandaa, lakini Ondiek na Yasmin wao ndio walionekana hawakujiandaa kabisa

Baada ya kupunga mikono hewani kuwasalimia wageni waalikwa, DJ alisogea ili kuwasikiliza ombi lao, Yasmin akamtupia mpira Ondiek ataje wimbo, Ondiek akachagua wimbo wa Bob Rudala uitwao ‘Nimekuchagua wewe’ ndio uliofunga sherehe hizo na kila mtu akaondoka kurejea kwake

Wakiwa njiani kurejea kwao, Victor alimuomba Eve walale pamoja usiku ule, Eve aligoma kabisa, basi Victor akaona si vema kumlazimisha kitu ambacho muda wake bado, maana aliamini ule usemi usemao ‘U cant make ana Omlette without breakinig an Egg’ yaani huwezi kukaanga yai bila kulivunja. Alikuwa akimaanisha kila kitu kina hatua.

Hatua ya kwanza ya Victor ilikuwa ni kumtia mikononi Eve, hivyo hapaswi kulazimisha kurukia hatua ya 3 kabla ya kuvuka hatua ya pili ambayo ni kujitambulisha nyumbani kwa wazazi wa Eve, mawazo yalikuwa yakimpitia kichwani mwake yeye mwenyewe.

Walifika nyumbani kwa kina Eve ikiwa ni saa 7 usiku, wakaagana kwa mabusu motomoto na kubadilishana ndimi zao kama wafanyavyo njiwa wanapowalisha makinda yao, walipoachiana, walitoka nje ya gari na kusimama wakiwa wamekumbatiana Eve akasema kumwambia Victor

“Nakupenda sana”

“Hata nami nakupenda pia” Eve akamuaga Victor aliekuwa ameegamia gari, Eve akaanza kuondoka, Victor akawa akimtazama kwa nyuma hukua kimuhesabia hatua anazopiga Eve..

“1, 2, 3, 4, 5...” alipofika hapo, Eve akageuka na kubusu mkono wake wa kulia kisha akamtupia Victor ambae alitabasamu na kumpungia mkono kisha akaingia garinina kuondoka kuelekea nyumbani kwake kupumzika akiwa anazitafakari Suprise 3 alizokutana nazo siku ile.

*******



Ni mwezi mmoja sasa umepita tangu Vict aajiriwe na kuanza kazi, hali yake kimaisha imeanza kuwa nzuri japo si sana ila pia si sawa na kipindi cha nyuma ambacho hakuwa nakazi kabisa. Sasa aliweza kufahamiana na watu wengi na aliisha kwenda kwao na Eve kujitambulisha ambao nao walimkubali bila masharti yoyote.





Alikuwa karibu sana na Ondiek, ambae alimshauri kuwa kama atakuwa na muda wa ziada, ni heri aende akatimize ndoto yake aliyokuwa akiiota wakati yupo shule ya msingi, wakati wakisoma, Victor alikuwa akitamani sana kuwa mtangazaji wa Radio. Hivyo Ondiek alimpanafasi ya kutangaza katika Radio yao ya Classic FM.

Hakukubali wala kukataa, bali aliomba muda zaidi wa kujifikiria, alipoonana na mpenziwe Eve alimueleza jambo hilo na kumshangaza Eve ambae wala hakujua kama Victor alikuwa na ndoto ya kuwa mtangaaji, lakini mwisho wa siku alimwambia hata nae atafurahi kama watafanya kazi pamoja kwani kuwa na kazi nyingine tofauti na uliyonayo, inakuwa ni sababu ya kuongezeka kwa kipato cha muhusika.

Eve akamshauri Victor akubali Ofa ile aliyopewa na Ondiek hasa kutangaa kwene kipindi kilekile cha Romantic breath Ambacho kinaendeshwa na Eve, na baada ya majadiliano ya muda mchache, walifikia muafaka kuwa Victor afanye kazi kwenye kipindi kilekile cha Eve na si kipindi kingine chochote.

Wakafunga mjadala kwa Victor kumpigia simu Ondiek na kumwambia amekubali ofa yake na tangu muda ule yupo tayari kufanya nao kazi. Ondiek alifurahi na kumuuliza kama kuna kipindi chochote anapenda kuanzisha, Victor akameambia kwa sasa ataanza na kipindi cha Romantic.

Ondiek alikubaliana nae na kumwambia muda wowote atakapokuwa tayari afike Studio ili kumaliza mambo mengine ya kimaslahi na kimikataba, walimalia maongezi yao huku Eve akiwasikiliza kwa umakini.

**********



Saa kumi za jioni ndio kwanza Victor anatoka kazini, akapita kwsa Ommy na kukuta kuna kikao cha dharula kinachohusu ndoa baina ya wapendanao wale wawwili, yaani Ommy na Lidya, Ommy alipomuona tu Victor akasema ni vema amekuja jamaa yake.

Akamueleza mzozo uliopo kuwa wanataka kufunga ndoa ila kama wajuavyo wotekuwa Ommy ni Muislamu na Lidya ni mkristo, sasa hakuna alie tayari kufuata dini ya mwenzie na ndio sababu ya kikao kile cha faragha, akamuuliza yeye anaonaje?

Hilo ndio lilikuwa ni swali la Ommy kwa Victor, kabla Victor hajalijibu akaenda kwenye friji na kuchukua soda baridi, akafungua na kunywa kama funda mbili hivi, Lidya na Ommy wakimuangalia kwa umakini, walitegemea kabisa atatatua tatizo lao, walimuamini sana.

Ni kweli walikuwa sahihi kumuamini, aliwatazama kwa zamu na kutabasamu kisha akaegamia kwenye ile sofa aliyokaa na kuwaambia kuwa jambo lile ni dogo sana, wala lisiwaumize vichwa, akawashauri waende kwa Mkuu wa wilaya na kufunga ndoa ya kiserikali ambazo hufungwa siku za Jumamosi, kisha mambo mengine yatafuatia baadae.

Huku akishika chupa yake ya soda ili apige funda, nae sasa akawauliza nao wanalionaje hilo? Wote wakaonyesha kukubaliana kabisa na wazo lake ambalo wao hawakuweza kuliwaza hata kidogo japo ndio ukweli wenyewe. Walimpongeza na kuahidi kufanya hivyo.

Hakukaa sana akondoka na kurejea kwake kujiandaa kwani siku ile alipanga kwenda kuingia Studio kwa mara ya kwanza, hivyo alimuahidi Eve atawahi kumpitia kwao ili waandae mada ya siku ile mapema, hivyo saa 1 usiku, Victor tayari alikuwa jirani na kwa kina Eve na kumuita.

Ilichukua wastani wa dakika kama kumi Evelyn akatoka akiwa yupo tayari na kuingia garini, wakiwa garini ndio walipanga mada ya siku ile, kila mmoja akichukua jukumu fulani, huyu akipanga muziki gani upigwe muda gani, huyu nae atazungumzia kitu gani muda gani.

Waliwasili studio na Victor akaanza kazi pale Classic FM, usiku wa ile siku ya kwanza ya Victor kuanza kazi alitambulishwa na Eve kama Partner wa kipindi chake, hivyo akawaomba mashabiki wake tangu siku ile na kila siu ya kipindi chake watakuwa pamoja, hivyo wawaunge mkono.

Sio siri kipindi kile cha kwanza kwa Victor siku ile kilipendeza sana na kuanza kuchukua umaarufu kwa kasi ya ajabu hadi kutishia vipindi vikongwe vya taratibu vya radio nyingine jijini Dar na nchi nzima kiujumla, mashabiki nao hawakuwaangusha, walikuwa nao bega kwa bega.

Eve mwenyewe hakuamini kama Victor ana kipaji kikubwa vile cha utangazaji, alikuwa akimshangaa tu jinsi alivyokuwa akiongea kama kwamba ni mzoefu na mambo ya utangazaji. Victor nae alijiona kama kachelewa sana, alitokea kuipenda tu sana kazi ile hasa baada ya wafanyakazi wenzie wa Classic FM kumkubali pia kukubalika na wasikilizaji wa kipindi cha Romantic breath, ilimfurahusha na kujituma zaidi.

Kawaida ikawa wakitoka studio nao wanapanda gari yao hadi nyumbani kwa Victor, siku zote Victor ndio aliekuwa akiwahi kuamka na kuandaa staftahi kisha humuamsha Evelyn na kwenda kuoga. Watokapo maliwatoni hufungua kinywa na kila mmoja kwenda kazini kwake, wakati Victor hutoka na gari yao, Eve huijiwa nagari ya kazini.

Polepole Eve akaanza kuzoea mazingira yale, akawa zile siku ambazo hana vipindi asubuhi, anapoamka hufanya yale yote ambayo hufanywa na mwanamke anayopaswa kufanya nyumbani kwake kila asubuhi na wakati mwingine hutumia hata gari ya kazini ili kufanya mahemezi yanayo hitajika nyumbani kwa Victor. Ndio mazoea aliyo jijengea...

********



Ndoa ya Ommy na Lidya ikafungwa kama ilivyopangwa na baada ya kutangazwa kwenye ofisi ya Mkuu wa wilaya ikifuatiwa na sherehe ndogo waliyoifanyia nyumbani kwao, japo ilikuwa ni ya watu wachache, lakini ilifana sana.

Kabla sherehe haijaisha MC akasimama na kusema kwamba anatoa nafasi kwa wanandoa kutoa zawadi kwa wapendwa waalikwa. Hiki hakikuwa ni kitu cha kawaida, hivyo MC akasema;

“Hii ni Suprise nyingine tena, huu ni uamuzi uliofikiwa hapa hapa ukumbini wakati sherehe ikiendelea” Aliongea MC aitwae Kitenge mwenye makeke mengi, huku akijigeuza kwa madaha

“Ni wakati muafaka kwao sasa kutupatia zawadi yetu, namuomba bwana harusi asogee, nafasi ni yake...” alisimama Ommy huku akipigiwa makofi na watu karibu wote waliokuwepo ukumbini.





MC Kitenge akamsogelea na kumpa mic, kisha Ommy akaanza kuzungumza kwanza

“Ndugu zangu mabibi na mabwana kwa furaha kubwa mno ninapenda kuwakaribisha kwenye hii sherehe yetu hii ndogo ya harusi yetu tuliyofunga asubuhi ya siku ya leo...” Ommy hakuwa msemaji sana anapokuwa hajapiga vyombo, akameza mate na kuelekea kwenye mada nyeti

“Zawadi ninayoitoa kwenu ni tofauti kidogo na zawadi zile tulizozizoea sote, kwani tumezoea zawadi zetu huwa ni za furaha...” Kauli ile ikawafanya watu wazidi kuwa makini kumsikiliza Ommy, Eve akamtaama kama vile anamuuliza Victor kuna nini? Kumbe hata Victor nae hakujua chochote masikini wa Mungu. Ommy akaendelea

“Zawadi ninayoitoa leo ni si zawadi ya furaha, bali ni zawadi ya majonzi.” Waungwana walishituka na kuweka vinywaji vyaao mezani ili kuipa akili umakini zaidi, Ommy akaendelea

“Kupitia sherehe hii na nafasi hii adhwiim, ninapenda kuwaaga rasmi, kwani jumatatu jioni, mimi na familia yangu tunataraji kuondoka hapa nchini na kwenda kuanza maisha mapya hapo nchi jirani ya Kenya. Hivyo ndugu zangu, kwa huzuni na majonzi tele, naweza kusema kuwa hii ndio zawadi yangu kwenu, ambayo ni zawadi ya masikitiko kwenu na kwangu pia, ila ninawaahidi nitakuwa pamoja nanyi siku zote, ahsanteni sana.”

Alimaliza kutoa zawadi yake na kuinama kidogo kisha akamkabidhi mic MC Kitenge. Alipo ipokea tu ile mic akawahi kuongea

“Usijali kaka Ommy, tunaamini tutakuwa pamoja kama usemavyo”

Shughuli zikaendelea kama zilivyopangwa lakini kidogo furaha kwa baadhi ya watu ilipungua mara tu baada ya kujua kuwa Ommy anaondoka muda si mrefu ujao akiwepo Victor. Kama kawaida, popote alipo Victor, isipokuwa kazini TMK veterinary, basi Evelyn alikuwepo kushoto

Muda wa zawadi ulipowadia watu wakaenda kutoa zawadi zao mbalimbali kama walivyo ziandaa. Yasmin na mpenzi wake Ondiek walitoa zawadi ya chakula cha usiku kwa maharusi kwa siku ifuatayo, zawadi ambayo Ommy na mkewe Lidya wakaipokea kwa mikono miwili.

Eve nae alitaka kupeleka zawadi waliokuja nayo, lakini Victor alimshika mkono na kumnong’oneza maneno fulani, Eve akaelewa na kurudi kuketi, shughuli ilipokwisha watu wote walisambaa kurudi makwao na kuwaacha Lidya na Ommy wakianza maisha ya ndoa halali.

********

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Siku ya Jumapili asubuhi, ndio kwanza wameamka wakiwa bado wapo kitandni, Victor na Evelyn walifanya tathmini ya maisha yao kwani sasa ilikuwa ni miezi mitatu tangu wawe wapenzi. Ndani ya kipindi hicho kifupi waliweza kufanya mambo mengi mno kwa faida ya maisha yao ya baadae.

Walitembelea sehemu mbalimbali kama Morogoro kwenye maporomoko ya maji kwenye safu za milima ya Uluguru, walikwenda kutembelea mbuga ya wanyama ya Ngorongoro huko Arusha na walifika hadi Zanzibar kwenye majengo ya Makumbusho.

Katika upande waajira nako hawakubaki nyuma, waliweza kuboresha kipindi chao na kuweza kuliteka kabisa soko la vipindi vya taratibu hapa nchini. Kila wakati Romantic Love ilipokuwa hewani watu walikuwa wakikumbushana.

“0yaa! Weka Classic FM, muda ndio huu. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kila siku wakati muda wa kipindi hicho ulipokuwa umewadia.

Kule TMK Veterinary napo karibu wafanyakazi wote walifurahi kufanya kazi na Victor, kwani aliwa furahisha na kuwaburudisha, zaidi ya yote aliwajali na kuwathamini kama vile ni sehemu ya familia yake, kifupi alihubiri amani na upendo baina yao.

Kila mara alikuwa akiwaambia kwamba laiti Dunia ingeongozwa na upendo, pangelikuwa hakuna vita, ila kwa kuwa Dunia inaongozwa na pesa, basi tujitahidi tu kupendana japo ni vigumu kwa asie na pesa kupendwa. Hivyo wengi walipenda kukaa nae ili kuvuna maneno yake ya busara na hekima tele.

*******



Siku hiyo ya Jumapili ambayo walikuwa wameiandaa kwa ajili ya kutathmini maisha yao ya kila siku na kupanga kutokutoka kabisa siku ile hadi jioni walipotoka kwenda maeneo ya jirani na pale kwao na kununua Pop cone kisha wakarudi na kuendelea na majukumu waliojipangia.

Usiku wa siku ile, familia nzima ya Ommy Bazzo ilielekea nyumbani kwa Ondiek na kujumuika na familia ile iliyo waalika kwa chakula cha usiku wakiwa ni wenye furaha tele pia wakitumia muda huohuo kwa kuagana, baada ya kumaliza kula chakula kile kilicho andaliwa kwa ajili yao, walishukuru na kuaga kisha wakaelekea nyumbani kwa Victor.

Waliwakuta Victor na Evelyn wakicheza cheza na kukimbizana hapa na pale ndani ya nyumba yao sehemu za uwani. Ilikuwa ni usiku unaokaribia saa nne na nusu, lakini kwa wapendanao wale waliona ni kama saa kumi za jioni.

Victor alikuwa ndiomtu wa kwanza kuwaona Ommy na Lidya wakati wakiingia, akawakarimu

“Ohoo karibuni wapendwa! Wale ambao ni mabingwa wa Suprise, Ommy jamaa yangu ni heri uende, kwani nimechoka kabisa na Suprise zako, dah! Hata mimi wa kunifanyia hivyo wewe?” wakati Victor akisema hayo kumwambia Ommy, Eve alikuwa akimkaribia Lidya aliekuwa amembeba mtoto wake aitwae Jamillah.

Alipomfikia alimsalimia na kumkumbatia, kisha akampokea mtoto aliekuwa amelala

“Poleni sana mdogo wangu tumewaharibia pozi lenu, maana wenyewe mlikuwa mmejiachia kama mchana vile” Aliongea Lidya huku akimpa mtoto Eve, nae akamjibu

“Hapana dada muda wenyewe ulikuwa ni wa mazoezi na sasa ulikuwa umekwisha hata hivyo”

Wakati huo Victor na Ommy walikuwa wameketi kwenye majani yale yale waliyokuwa wameketi Eve na Victor awali walipokuwa wakipumzika mara baada ya kuchoka kukimbizana, walikuwa wakiongea. Lidya na Eve nao wakaenda kuungana nao pale chini walipoketi.

Kama kawaida popote alipo Victor ni lazima ajulikane kama yupo, hivyo akawa yeye ndio mtu wa kwanza kuongea huku akimtazama Lidya.

“Shem afadhali mmekuja, sisi tumepanga kuwakaribisha kesho kwa ajili ya chakula cha mchana, ina maana mnapaswa kuja hapa na mizigo yenu yote mnayotaka kuondoka nayo ili muondokee hapahapa muda utakapofika, ama mnaonaje?” aliwahoji huku akiwaangalia kwa zamu.

Evelyn alikuwa amezama mchezoni na Jamillah ambae sasa alikuwa ameamka, wala hakushughulika kabisa na wazazi, bali yeye alikuwa na Jam basi. Swali la Victor lilikuwa gumu kwa Ommy na Lidya, wakatazamana na kutegea kila mtu aone mwenzie atatoa jibu gani, Ommy akakata mzizi wa fitna kwa kusema

“Wewe tena umesema mkuu, nani wa kupinga?” waliongea sana huku Victor na Eve wakipokezana kucheza na Jam hadi saa 7 kasoro usiku, ndio Ommy na familia yake wakashtuka na ndio wakaaga na kuondoka kurejea kwao





Siku iliyofuata ilikuwa ni suku ya jumatatu ambayo ilkuwa ni siku ambayo Ommy na familia yake walikuwa wakiondoka nchini kuelekea Kenya, si Victor wala Eve aliekwenda kazini siku ile tena walijidamka mapema kuliko kawaida na kuanza kujiandaa kwa maandalizi ya chakula cha mchana, ambacho kilikuwa ni chakula cha kuagana.

Wakiwa begabega, waligawana majukumu, Victor akiwa anakata nyanya na kuzisaga, Eve nae alikuwa busy na kuosha mchele, ilimradi huyu akiwa kashika hiki, mwingine kashika kile, hivyo ndivyo ambavyo walifanya kazi zao.

Pamoja na kuwa na kazi nyingi, hawakuacha kutaniana na kupoteza muda wao kwa kucheza michezo ya kimapenzi. Kuna muda Victor alikwenda kuweka muziki wa taratibu na kumlazimisha Eve aache kupika na kuanza kucheza nae pamoja. \

Na hata kuna wakati mwingine Eve nae alipomuona Victor ametulia na kufanya kazi fulani, alienda na kumvuruga.

Kuna muda alikwenda na kumdandia mgongoni, wakati mwingine alisogea na kumbusu, ilimradi tu utulivu ukawa haupo. Pamoja na hayo yote waliweza kumaliza mapishi yao mapema kabla ya saa 7 za mchana. Wakatayarisha kila kitu mezani na kuingia bafuni kuoga.

Walimaliza na kuanza kujipodoa, pia napo wakamaliza bila Ommy na mkewe kufika wakakaa nje ya nyumba yao na kuwasubiri wageni wao ambao waliwasili saa nane mchana. Waliingia na kuonekana kama ni watu wenye wasiwasi sana, Ommy hata kabla ya kusalimia akasema

“Shemeji tafadhali tuandalie kabisa chakula, maana muda hauruhusu kukaa hata nusu saa”

“Kwani Shem mlikuwa wapi?” aliuliza Eve na kujibiwa na Lidya

“Si unajua kuwa kuna jamaa wanao kuja kuaga? Kuna wengine hawajui kuwa muda hauruhusu, ukimwambia mtu una haraka anaona kama vile unaringa”

Haraka haraka wakakaa mezani na kuanza kula chakula kilicho andaliwa, wakiwa wanaendelea kula Ommy akaanza kuongea na Victor

“Victor mdogo wangu sisi ndio hivyo tunaondoka, tuna mali zetu nyingi sana hapa na pia hapa ndio nyumbani hatuwezi kusema kuwa tutauza mali zetu zote, hivyo ni lazima baadhi zibaki” aliongea Ommy akimtazama Victor, kisha akaendelea

“Japo mimi sina ndugu yoyote hapa karibu, ninajivunia uwepo wako kwani wewe ni zaidi ya ndugu yangu, ndio maana hata hiyo Balloon nimependa wewe uichukue na kunilipa polepole na utaendelea kunilipa polepole hivyohivyo kwa kuniwekea kwenye akaunti yangu hadi utakapo limaliza deni lako, sawa Victor?” Victor alitikisa kichwa kukubaliana na kile akisemacho Ommy

Ommy leo yeye ndio alikuwa ndie msemaji mkuu tofauti na siku zingine ambazo Victor huongoza jahazi, leo hali ilikuwa ni tofauti, alikuwa ni mpole sana

“Jana usiku nukiwa na mke wangu Lidya, baada ya kutoka hapa tulifurahi sana jinsi tulivyo wakuta na mpenzi wako Eve, tukajadiliana na kuamua kuwa hii gari ya Lidya yaani Escudo, nayo pia tuiache hapa kwako na itakuwa ni njema zaidi kama shemeji yangu Eve akalinunua kama atalipenda na iwapo atakuwa tayari kwa jambo hilo kwa kumlipa mwenzie taratibu, au mnasemaje?”

Hakuna alieshangaa kama Eve, hakuwa na ndoto kabisa ya kumiliki gari kwa sasa, leo inaletwa gari ya kulipa kwa mafungu, waliatazamana Victor na Eve bila kujua kama nao wanatazamwa na Ommy na Lidya, Victor akajibu kuwa wamekubali na wanashukuru sana.

Lidya aliekuwa kimya muda mrefu sasa muda wake wa kuongea nae ulifika, akasema

“Wapendwa ndugu zangu, hilo la magari limekwisha, hebu tuje kwenye suala la nyumba sasa, kwa kuwa hapa mpo kwenye nyumba ya kupanga, mnaonaje kama nyumba hii mtairudisha kwa mwenyewe na kisha nyie mkaenda kukaa pale kwenye ile nyumba yetu... ama pale hamjapapenda?”

Kauli ya Lidya ilijibiwa haraka sana na Victor,

“Shem, mema mliotutendea kwa kweli yametosha, hiyo nyumba acha tu mikononi mwetu sisi tutaipangisha, nasi tutaendelea kukaa hapahapa, vitu vyenu vyote nitavichukua na kuviweka hapa, imetosha sana kwa hayo mliotufanyia, hadi sasa sioni cha kuwalipa, mkizidi hapo sasa..,

Mkizidi hapo sasa, tutakuwa wanyonge na mwishowe maisha yetu yataharibika kabisa” aliongea Victor kwa kujiamini na Eve akaongeza

“Kweli Shem, suala la nyumba tuachieni tu, tutaipangisha na kuweka fedha ya pango kwenye akaunti yako”

“Ok basi msijali, naona sasa ni wakati wetu muafaka wa kuondoka, kwani Ondiek tutakutana nae Airport, ataleta makabrasha yote ya Classic band ambayo tangu sasa itakuwa chini yako Mr, najua ni majukumu mengi nakuachia bwana mdogo, lakini hayo ndio mafanikio ya kuwa na akili na hasa unapokuwa na ‘President’ kama mimi.” Alitania Ommy na kunyanyuka kwenda kunawa kwenye bomba palepale Dining room.

Walitoka nje na kuongozana kuelekea JK International Airport, Victor alishika sukani ya Escudo na siti ya pembeni yake aliketi Eve aliekuwa kambeba Jamillah. Mdogo mdogo safari ya kuelekea uwanja wa ndege ikaanza. Wakiwa garini, Eve alitoa zawadi na kumkabidhi Ommy huku akisema

“Shem Ommy pamoja na dada Lee, zawadi tuliyo waandalia ni ndogo sana lakini tunaomba muipokee, zawadi nyingine kubwa zaidi tutawatumia mara mkifika Kenya na kutujulisha anwani yenu.” Akawakabidhi kibox chenye ukubwa wa wastani kilichokuwa na rangi nyeusi na manyoya madogomadogo, sio siri kilivutia sana.

Ommy hakukifungua japo ndie aliekipokea, akampa Lidya. Lidya alitabasamu na kusema kiutani kumwambia Ommy kuwa anafikiri Eve ni mfuasi wa Al Shabab? Eve hawezi kuweka bomu kisha akatupa sisi nae akiwa garini humuhumu, wakacheka wote garini kwa sauti.

Lidya akakifungua, ajabu hata Victor hakujua kina nini ndani, si Lidya alie kifungua Ommy wala Victor alie amini kwa walichokiona ndani ya kiboksi kile, ndani kulikuwa na sa 3 aina ya Rolex moja ikiwa ni ya kiume na nyingine ni ya kike wakati ile ya mwisho ilikuwa ni ya mtoto.

Zote 3 zilikuwa ni zaaina ileile moja ya Rolex zilizokuwa na vitufe na mishale ya almasi, kifupi zilikuwa ni nzuri sana, Victor kama kawaida yake, akachomeka neno huku akiendesha gari, akasema Suprise zinaendelea. Kwa niaba ya familia yake Ommy akawashukuru Victor na Eve kwa zawadi ile waliyowapa.





Aliwambia haamini kama nae leo na familia yake wanavaa Rolex akawashukuru tena huku akivaa saa ile na kumwambia Lidya amvalishe Jamillah saa yake, kama yeye hataki kuvaa atajijua mwenyewe, wakatabasamu. Ilikuwa ni siku nzuri sana, lakini ndio ilikuwa inakwenda kumalizikia.

Walifika Airport na kuonana na Ondiek ambae tayari alikuwa amefika pale akiwa na bahasha kubwa ya kaki, wakasalimiana na kisha akampatia Ommy ile bahasha, nae baada tu ya kuipokea, akamkabidhi Victor na kumwambia maelekezo yote yapo ndani ya bahasha ile.

Akamwambia ikitokea kutokuelewa chochote wala asisite kuwasiliana na Ondiek, atamsaidia, na kama kuna zaidi ya hapo basi awasiliane nao wao moja kwa moja, akawaombea maisha mema na kuwataka wabaki salama.

Kwa masikitiko makubwa wakaagana, hawakushindwa kuonyesha mapenzi yao makubwa hadharani pale machozi yalipo watoka baada ya kukumbatiana wale wanaume wawili na wapenzi wao.

“Safari njema dada Lee, mtujulishe mkifika Salama, Nakupenda sana dada Lidya” hiyo ndio ilikuwa kauli ya mwisho ya Eve kwa Lidya ambae alijibu kwa chozi lililo dondokea shavuni, wakaachana na kuingia ndani kwenye ukaguzi wa tiketi.

Walikaa hadi ndege ilipo tangazwa kuondoka ndio nao wakaanza safari kurejea nyumbani. Safari hii Eve ndio alikuwa amekaa upande wa kulia na Victor alikuwa ameketi kwenye siti iliopo upande wa kushoto.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Njiani ndio Victor akamuuliza Eve kwanini aliamua kununua saa kama zawadi? Eve akamjibu kuwa siku za nyuma yeye alikuwa na saa kama ile, Lidya alikuwa akiipenda sana, lakini hakuwa mtu wake sana kama sasa hivyo hata hakujali.

Hivyo ilivyotokea fursa ile ya kurejesha zawadi, akaona zawadi muafaka ni ile ambayo mtu anaihitaji kuliko kumpa aliyonayo.

Victor akajibu asemacho ni kweli, lakini mbona hata yeye hakumwambia? Eve akacheka na kusema ule ni mwendelezo wa Suprise, Victor akatabasamu na kusema Suprise zikizidi huwa ni mbaya. Wakafika nyumbani na kuanza kutayarisha mada ya siku ile kwenye kipindi chao cha mahaba cha Romantic love.

*******







ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog