Search This Blog

Tuesday, 1 November 2022

SUPRISE - 2

 








Simulizi : Suprise

Sehemu Ya Pili (2)





Kurudi kwa kasi, maendeleo mazuri na kupendeza kwa Evelyn kulimfanya Ondiek amtamani tena na wakati huohuo Ondiek ndie mtu alie muumiza Evelyn, kwani alimuacha kwa kashfa nyingi na matusi bwerere hadi ikafikia Eve kuapa kuwa hatopenda tena.

Lidya ndio akaingilia kati juu ya suala hilo kwa kuwa karibu nae huku akimtoa Out na kumpa ushauri mara kwa mara akimliwaza kwa maneno na hadithi mbalimbali na zaidi ya wiki mzima alikaa nae kwake wakati Ommy akiwa kasafiri kuelekea Congo kwenye biashara zake.

Ikafikia hatua Eve akaona Lidya si rafiki tena bali ni kama ndugu wa kuzaliwa nae tumbo moja, ndio maana ilipofika suala la Victor kumtokea Eve kupitia Lidya wala haikumsumbua, kwani Lidya ndio mtu wa karibu na Eve kuliko mtu yeyote

Sasa Ondiek alianzisha mashambulizi upya kwa Evelyn kimyakimya, haikuwa ni kazi rahisi lakini bahati nzuri hata yeye mwenyewe Ondiek alilijua hilo ila haikumfanya akate tamaa wala kuvunjika moyo.

Siku moja Ondiek alisikika akimwambia Eve kwamba yale yaliyopita ilikuwa ni ushawishi tu toka kwa watu wasio wapenda, na hii yote ilitokea baada ya Lidya kuondoka nchini, maana Lidya alipokuwepo Ondiek hakuweza kumsogelea Eve hata hatua moja kutokana na maneno makali ya Lidya aliokuwa akimropokea.

Ndio maana hata Ondiek alipopata nafasi ya kuongea na Ommy na kumuomba ushauri wa kwenda kuishi nje ya nchi hii ili kupata changamoto mpya na kufungua miradi mipya, ndio akatumia nafasi ile kwa kumshawishi aende nchini Kenya ambako ni kwao yeye Ondiek.

Alimuahidi kumsaidia baadhi ya mambo yaliyo ndani ya uwezo wake kwa sababu kule ni kwao na anafahamiana na watu wengi ambao akiongea nao watakuwa nae bega bega pindi akifika kule lakini lengo likiwa ni kumsogeza mbali Lidya.

Ommy akiwa bado yupo Tanzania hajaondoka, tayari Ondiek aliweza kumpatia nyumba nzuri jijini Nairobi na kumuwekea sawa kila kitu alicho kihitaji pasina wao kuelewa lengo lililo kichwani mwa Ondiek, bali wao walimshukuru kwa dhati wakiamini ni rafiki wa kweli.

Alificha makucha yake kwa kufanikisha masuala yao yote waliyo taka pia alipotezamuda wake mwingi, hakika angetokea mtu akawaambia ni kwanini Ondiek anafanya vile, yeye ndio angeonekana ana matatizo.

*******



Ni miezi takriban 10 tangu Victor na Eve wawe pamoja na kwenye kipindi hiki ndio mimba yenye miezi mitatu ya Eve ikanza kuonekana kwa mbali kutokana na umbo lake. Wapendanao wle walikuwa wamekaa kitandani wakipanga ni nini wakifanye ili kuboresha zaidi maisha yao ambayo kwa sasa ni mazuri kwa kiasi fulani.

Kitu kimoja walicho kiongelea ni kununua shamba huko maeneo ya Lwangai, nje ya Jiji la Dar Es Salaam na kuamua jambo hilo walifanye siku ifuatayo ambayo itakuwa ni siku ya Jumamosi ndio waitumie kuelekea huko Lwangai.

Walijidamka mapema sana na kuwasha Escudo yao kuelekea huko. Walifika mapema na kuanza kumtafuta mwenyeji wao ambae ni mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji alieitwa Haji Kibwe. Walimpata na kumueleza kile kilichowapeleka pale. Bahati ilikuwa upande wao, Mwenyekiti aliwauzia shamba yeye mwenyewe na kurejea nyumbani wakiwa ni wenye furaha tele.

Baada ya kurudi nyumbani na kufanya shughuli za pale walitoka usiku na kukaa bustanini. Kama kawa Victor hakai kimya, akamwambia Eve kuwa siku ile ya leo anaonekana kama ana furaha sana, akamuuliza ni kwanini? Eve akishangaa tu na kumwambia hata yeye anamuona kam Victor amefurahi sana kuliko yeye, nae akataka kujua.

“Ah we niambie tu, mie ndio nilikuwa wa kwanza kukuuliza swali hilo, pia inasemwa Ladiest First, niambie Mpenzi,” Alibembeleza ili tu aweze kuwa ni sehemu ya furaha ya mpenzi wake

“Nikikwambia je nawe utaniambia kwa nini una furaha?” aliuliza Eve na hali anajua kabisa kuwa kile anachohoji jibu lake lazima litakuwa ni ndio

“Lazima nikwambie Eve, sasa nisipokuambia wewe nitamwambia nani?”

“Muone kwanza na maneno yake ya kilaghai, unakubali kiurahisi, tukimaliza hapa utasema usingizi unataka kulala.” Alisema Eve kwa sauti ya maringo na kudeka

“Baby mi leo silali hadi nikuhadithie, niambie basi my love” akambusu shingoni.

“Ok! Mi leo nimeikumbuka sana siku ile uliyo nivisha pete ya uchumba...” Victor akadakia

“Aah siku ilee! Duh ni kama miezi 6 iliyopita.” Wote wakaanza kuikumbuka siku ile.

*******



Ilikuwa ni siku ya Jumamosi asubuhi nyumbani kwa Victor aliemuomba mpenzi wake Eve ajitayarishe na watoke asubuhi ile. Walikwenda hadi katikati ya Jiji na kusimama mbele ya duka moja la nguo liitwalo Rahma Boutique ambalo nalo lipo chini ya Classic Group.





Duka hili lilikuwa ni maalum kwa ajili ya wafanyakazi wa makampuni ya Classic na wadau wote wa makampuni hayo. Walichagua nguo mbalimbali zile zilizo wavutia, Victor alichukua suti moja kali ya rangi ya Bluu ambayo kwaa wakati huu ilikuwa ndio ipo kwenye chati ya juu na kweli ilikuwa imesimama sana.

Nae Eve akachukua gauni moja zuri sana na nguo zingine kadhaa akazinunua. Ila kuna gauni moja jeupe Eve alilipenda sana, lakin Victor akamshauri waliache asilichukue, kwa shingo upnde Eve akakubali, Victor akalipia zile nguo na kuondoka.

Kumbe hata Victor alilipenda lile gauni ila tu hakupenda kulinunua akiwa na Eve, akapanga kumzunguka. Walipita sehemu mbalimbali nawalipofika nyumbani, Victor alikuwa akiongea na mar kwa mara, kisha akamwambia Eve kwamba yeye anatoka mara moja na hatochelewa kurudi, anakwenda kule alipokuwa akiishi Ommy, Eve akamsisitiza asichelewe tu kurudi.

Akatoka na kuingia garini kisha akaelekea Rahma Boutique, akalinunua lile gazeti alilomzuia Eve kulinunua, kisha akaingia sehemu wanapouza mapambo ya mwili, akanunua pete moja nzuri mno ya dhahabu, inayo ashiria uchumba, akatoka dukani na kuingia garini, akavihifadhi vizuri mlemle garini kisha akaondoka.

Safari yake baada ya hapo haikuelekea nyumbani kwake, bali aliekea nyumbani kwao maeneo ya Victoria, aliwasili na kuwasalimia kama kawaida ya mtoto kwa wazazi kisha akawaalika kwenye sherehe ya rafiki yake kipenzi, akawaambia kuhusu suala la usafiri, wala wasihangaike, kwani watafuatwa saa moja jioni palepale nyumbani.

Wakamuelewa mtoto wao nae akaaga na kuondoka. Baada ya kutoka pale akaendelea na safari ya kuelekea kwa wazazi wa Eve maeneo ya Mwananyamala kwa mama Zacharia. Aligonga hodi na kukaribishwa ndani na Mzee Dotto aliekuwa amekaa Sitting room.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Karibu mwanangu Victor” alijisikia faraja sana kukubalika nyumbani kwa wakwe zake, akaketi na kusalimiana na mkwewe. Punde tu kidogo mama yake Eve nae akasogea na kuungana nao baada ya kuisikia sauti ya Victor, akawaeleza kilichompeleka pale na pia akawataka radhi kwa kuchelewa kuleta taarifa ile.

“Japo ni haraka wazazi wangu, naomba mkubali mwaliko wetu leo kuna sehemu tunapenda kuwakaribisha kwa chakula cha usiku, hivyo wazee wangu, naomba mjitayarishe na itakapofika saa 12 jioni, gari itawafuata, samahani sana wazazi wangu” aliongea kwa dhati kabisa.

“Ooh hapana baba wala usihofu, tutajumuika nanyi, vipi tufanye mazoezi?” Alitania mama Eve na Victor alimuelewa anamaanisha nini, alicheka na kujibu huku akisimama.

“Mama hilo sio swali la kuuliza, jiandaeni vizuri” Wakataniana kidogo na wazee wale kisha akaaga na kuondoka. Njiani alipokuwa akirudi, simu yake ikaita, kwa sauti ya muziki iliyosikika, alijua dhahiri huyo alikuwa ni Eve.

Akapokea na kumwambia ndio yupo njiani anarejea kwani aliamua kwenda hadi mjini kuchukua chakula cha mchana. Eve akamuelewa na kumsisitiza asichelewe zaidi, kwani hajisikii vizuri. Muda wote huo Victor bado alikuwa akiendelea kuwasiliana na watu wake kadhaa kupitia simu yake ya mkononi.

Alipokuwa akirudi alipita kwenye baadhi ya nyumba za majirani zake na kuongea nao mambo ambayo hakuna aliejua ni nini kinazungumzwa, aliejua anacho waambia ni Victor mwenyewe. Kufikia saa 7 na nusu adhuhuri, alirejea nyumbani kwake akiwa na chakula mkononi.

*******



“Eve... Eve mpenzi wangu,” Sauti ya Victor haikujibiwa, alimtafuta kila sehemu lakini alimkosa, akajiongeza kuwa ni bora apige simu, jibu alilolipata lilimvunja moyo kabisa, akatamani hata kulia, maana namba ilikuwa haipatikani, hakutaka hata ile sauti ifike mwisho.

Palepale alipokuwa amesimama akakaa akiwa na mawazo kedekede, akijiuliza ni wapi alipokwenda msichana wake na kwa nini hakumuaga na azime simu? Ghafla akasikia sauti ya Eve ikimzomea na kumcheka kwa kushindwa kumpata.

Victor akashusha pumzi kwa nguvu na mapigo ya moyo yakarejea katika hali yake ya kawaida na kumwambia Eve kwamba anaweza kumuua kwa presha, Eve akamsogelea na kusema

“Pole mpenzi wangu, mbona uliniacha mpweke wewe ukaenda zako huko peke yako na kuchelewa kurudi?” aliuliza kwa sauti ya deko huku nae akikaa chini pale alipokaa Victor na kumuegamia begani

“Poa mpenzi wangu, wakati nipo nawe hapa si unakumbuka kuwa uliona simu yangu ilikuwa busy sana?” akaitikia Eve kwa kutikisa kichwa tu huku akichezea shati la Victor

“Kuna jamaa yangu ametualika chakula cha usiku leo hii, nimemuambia tutakwenda,

“Pia ameomba atumie gari lako usiku wa leo, nikamkubalia mpenzi wangu, ama nimekosea baby?”

“Ndio umekosea, kwanini utoe gari yangu bila idhini yangu tena bila kuniambia mwenyewe?” japo alikuwa akitania, lakini alijidai amekasirika kabisa huku akigeuka upande.

“Ooh mpenzi, subiri nimjulishe kuwa asije tena kuchukua gari la...” Victor akapiga namba fulani wakati huo Eve alikuwa akimuangalia kwa jicho pembe.

Victor alipo nyanyua tu ile simu yake na kuiweka sikioni, Eve akampokonya na kuikata na kusema huku akiiweka simu ile chini

“Ah mpenzi wangu hutaniwi? Mimi nilikuwa ninakutania tu”

“Dah! Eve, sio siri niliogopa sana maana ni kweli nilifanya makosa, ndio maana nilitaka nirekebishe makosa muda huuhuu, ahsante sana mpenzi” akamaliza Victor kuelezea.

Akamkumbatia na kumbusu Eve, wakaanza kushikana miili yao, kilichofuatia mimi sikukiona, maana niliondoka eneo la tukio, sikupenda kabisa kuwa ni shuhuda.

*******



Saa 11 jioni, simu ya Victor ikaita na kumuamsha kutoka kwenye usingizi wa mchana, akatoka nje na kumuacha Eve akiwa amelala na kuongea na aliempigia simu, alikuwa ni dereva wa TMK Veterinary ambae Victor alikuwa amemuomba amsaidie, sasa hakuwa na ratiba, hivyo alipiga ili kujua ratiba kamili

Victor akamwambia muda wowote kuanzia pale wanapoongea, anaweza tu kuijia gari ili ikifika saa 12 na nusu jioni akawachukue wazazi wake Victor na kuwapeleka jengo la Millenium Tower lililopo Kijitonyama, awaonyeshe kwenye ukumbi uitwao Twiga Grill, wakutane pale.

Kisha alipomaliza kumpa maelekezo dereva wao, akampigia dereva wa Classic FM na kumpa maelekezo kama hayo ila huyu sasa akamtaka akawachukue wazazi wa Eve, baada ya hapo akarejea ndani na kumuamsha Eve ili waende kuoga na kujitayarisha kwa ajili ya kutoka. Wakaigia bafuni...

Iliwachukua kama dakika 45 wote wakiwa wapo tayari na walipendeza sana, Eve alivaa pedo ya bluu na kiblauzi cheupe kizuri sana. Victor nae alivaa Pensi ya Pocket rangi ya Cadet na tisheti nyeusi ya mikono mifupi, hakika walipendeza sana hadi wenyewe walishangaana.

Victor ndio alianza uchokozi

“Kumbe naishi na Malaika humu ndani halafu sijui?” alishangaa Victor na Eve akajibu mapigo

“Ah ah ah we handsome, muda wote huwa wapi wewe?” huku akimsogelea na kumgeuza geuza.

Wakacheka kwa furaha na kutoka nje, hawakuikuta Escudo, hivyo wakatua tayari imeondoka nao wakaingia garini, kabla hawajaondoka, Victor akasema

“Oh mpenzi samahani ngoja nichukuenguo baadhi, tumpitishie dobi anyooshe, si unajua kesho kutwa ni siku ya kazi? Nami sitaki kesho usumbuke dear wangu, dakika 3 tu zinatosha kuchukua hizo nguo ndani” akashuka haraka haraka hata kabla Eve hajajibu kitu.

Akaingia ndani na kuchukua suti yake ile mpya waliyonunua na kuchukua pia viatu muafaka mabvyo aliona vinaendana na suti ile, kisha akaangalia viatu vya Eve ambavyo vinaendana na lile gauni alilolinunua kwa ajili ya Eve na kuweka vyote kwenye begi, akatoka na kuweka begi kwenye buti ya gari ambapo kulikuwa na mizigo mingine ambayo alikuwa amenunua.

Akaenda upande wa pili wa gari alipokuwa amekaa Eve na kumgongea dirishani, Eve alikuwa busy akichat na Lidya kupitia Whatsapp, akateremsha kioo, Victor akatoa Lock na kufungua mlango kisha akamwambia ateremke.

Kwa shingo upande Eve akateremka na kusimama akimtazama, Victor akaingia yeye kwenye ile siti na kumwambia Eve akaendeshe gari.

Eve alitabasamu na kuguna, kisha akatikisa kichwa na kumpa simu yake Victor aendelee kuchat na Lidya wakati yeye akiendesha gari kuelekea Millenium Tower.

Walifika Millenium Tower na kuungana na wageni wengine walio wakuta pale, hapakuwa na viti zaidi ya viti viwili tu vilivyokuwa mbele kabisa ya ukumbi uliokuwa umepambwa vizuri, muda wote waalikwa walikuwa wanaruhusiwa kujihudumia vinywaji kwani meza za vinywaji vilikuwa vimezunguka ukumbi mzima.

Katikati ya ukumbi palikuwa pana meza ndefu sana zilizokuwa zimepambwa na mapambo ya kila aina zikiwa zimefunikwa na vitambaa vilivyo andaliwa vizuri kwa ajili ya shughuli kama hii na zaidi ya yote maua halisi mabichi. Kifupi ukumbi ulipendeza sana





Watu wote pale ukumbini walikuwa wamesimama na glasi zao mikononi. Pamoja na kuwa meza za vinywaji ziliruhusu mtu kujihudumia, lakini pia walikuwa wakipita wahudumu waliokuwa na sahani zilizokuwa na vinywaji na pia mlangoni walisimama warembo wawili nao wakiwa na sahani zilizo kuwa na glasi za vinywaji.

Victor alipitia moja na Eve nae akapitia yake na wote wakaungana na watu waliokuwa mle ndani, walipita huku ma kule kuwasalimia ndugu, jamaa na marafiki, kisha wakaenda kuwasalimia wazazi wao ambao tayari walikua wameisha wasili.

Muda wote huo muziki wa taratibu ulikuwa ukiendelea taratibu, ghafla MC ambae ni yuleyule aliekuwa akiongoza sherehe za Ommy, aitwae Kitenge, akaanza manjonjo yake;

“Habari za usiku mabibi na mabwana?” naona sasa ni wakati muafaka kwetu kuanza shughuli yetu japo wahusika sijawaona, naomba tuwasubiri kwa kuendelea kupata vinywaji, ahsanteni kwa kuitikia wito, na kwa niaba ya wahusika wa shughuli yetu hii, ninapenda sana kuwakaribisha, karibuni sana ndugu waalikwa!” akazima Mic na muziki ukaendelea.

MC akaanza kuzunguka ukumbini akiongea na wageni waalikwa na akiwakaribisha lakini lengo lake alilijua mwenyewe, kwa hiyo huku kote alikuwa akijizungusha tu hadi alipofika kwa Victor na kumnong’oneza jambo fulani, Victor akatikisa kichwa kukubali na kuanza kujisachi mfukoni.

Baada ya muda mchache wa kujisachi mfukoni akakumbuka na kumuomba Eve ampe funguo ya gari, Eve akampa funguo ile Victor ambae nae akamkabidhi MC kitenge. MC nae baada tu ya kuichukua toka kwa Victor, akamuita mhudumu mmoja wa kiume aliekuwepo pale na kumnong’oneza jambo fulani, akakubali na kumpa funguo ile.

Mc akaendelea na safri yake ya kusalimia wageni na baada tu ya dakika kadhaa muhudumu yule alirudisha ile funguo na kusema tayari. Victor alipokea funguo za gari yake na kuziweka mfukoni mwake.

MC aliona kitendo cha funguo kurejeshwa kwa Victor, akaondoka kule alipokuwepo na kuelekea kwa DJ na kuongea nae kwa sekunde chache kisha akasema kuwaambia waalikwa kwamba wanaomba samahani sana wahusika wa shughuli ile kwani wamechelewa kwa dakika 3 kutokana na ratiba yao, lakini hata hivyo kwa muda ule tayari wamefika.

Watu walipiga makofi bila hata ya kuwaona wahusika, MC akaendelea kuwaambia kwamba kuna upungufu mmoja umejitokeza, kwani mpambe wa bibi harusi aliepaswa kukalia moja ya viti vile pale mbele hajatokea na hawana taarifa yoyote.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Akasema kuwa nao pale ukumbini ili shughuli yao isiharibike wakaona wanapaswa kutafuta mtu wa kuziba pengo lile kwa haraka, na hivyo wamejaribu kutafuta mtu wa kuziba pengo lile kwa kweli hawajamuona zaidi msichana mwingine tofauti na binti mmoja humu ukumbini akiwa amekuja ameongozana na Victor J. Maganga.

Hapo akamuomba Victor kama yupo tayari wanamuomba amuongoze binti aliekuja nae hadi chumba namba 408 ghorofa ya pili ili aweze kuokoa jahazi hili lisizame, akasisitiza kwa maombi laini ya kumshawishi akubali.

Kwa msisitizo alioutoa MC hata kama ungekuwa ni wewe basi ni lazima tu ungekubali kumtoa mpenzi wako kwa kuhofia kuzamisha jahazi ambalo na wakwe zako piawazazi wako wapo, tena wamefika kwa mwaliko wako wewe.

Kifupi watu wote ukumbini walishtuka, ila mshituko alioupata Eve, ulikuwa ni mkubwa zaidi, walikuwa mbalimbali kidogo na Victor, Eve akawa anamtazama Victor alie onekana akimfuata taratibu kule aliko. Alipomfikia akamkumbatia na watu wote wakishuhudia kitendo kile.

Alimuachia na kumshika mkono akimuongoza kuelekea kule alipo elekezwa, watu wote walipiga makofi na hata kuufunika muziki uliokuwa ukisikika pale ukumbini. Kule chumbani walipoelekea Eve akishangaa tena, kukuta gauni kama lile alipendalo na viatu ambavyo alikuwa na uhakika kuwa ni vyake.

Alihoji Eve lakini Victor alimrusha tu na kumwambia wataongea zaidi nyumbani ila kwa sasa wafanye kile kinachopaswa kufanywa, akamuomba autumie muda ule mchache kwa kuijitayarisha, kweli ndani ya nusu saa tu Eve hakuwa yule aliekuja kavaa kipedo na blauzi.

Kwa msaada wa wataalamu wa mapambo toka Rahma Salon & Hair Care alibadilika na kuwa kama Malikia wa nchi fulani, alipendeza kweli kweli. Waliendelea kumuongezea mapambo wataalamu wale na kuanza wao kwanza kupiga nae picha za Selfie na kuzitupia mtandaoni.

Hapo sasa hata Victor nae alikuwa hajamuona maana nae alikuwa chumba kingine akiwa na kundi la wataalamu wa3 nae wakimuandaa. Hivyo wale wataaalamu waliokuwa wakimuandaa Eve walipomaliza wakawasiliana na MC nae akawataarifu wageni waalikwa kuwa mpambe ataingia punde, hivyo akaomba taa zote zizimwe na watu wote wanyamaze na kutazama mbele.

Dakika ileile zikazimwa taa zote ukumbini na palepale akaanza kuonekana binti aliependeza sawasawa akiingia akiwa amebeba mshumaa unaowaka kwenye kisahani mikononi mwake na MC akawaa kimuongoza sehemu ya kukaa. Alipoketi tu taa nazo zikawashwa kwa sekunde kadhaa, maana watu wote walikuwa wametoa macho wakimtazama yule alie ingia ni nani.

Huwezi kuamini, watu wote walipigwa na butwaa na kushindwa kuamini kama kweli aliekaa mbele yao ni Eve, alipendeza kwelikweli, kipindi hichohicho Eve akawa akitembeza macho yake kwa aibu kumtafuta mpenzi wake Victor ambae alikuwa hamuoni.

Kabla hata hajapata nafasi ya kujihoji vizuri mwenyewe ni wapi alipo Victor, MC akavunja ukimya kwa kusema

“Jamani sasa ninaomba nimkaribishe mtu mwingine muhimu kwenye sherehe yetu hii... karibu mheshimiwa unakaribishwa ndani.” Taa zenye mwanga mkali zikazimwa na kubaki taa moja yenye mwanga wa mbali, yaani mwanga hafifu, tena ukiwa ni wa rangi. MC akamuomba Eve asimame mara tu muziki utakapoanza kusikika.

Sauti ndogo ilisikika toka kwenye spika kubwa zilizopo mle ndani ya ukumbi, ulikuwa ni wimbo wa mwanadada Shania Twain uitwao ‘From this moment’ ulimnyanyua kitini Eva na kumruhusu mtu muhimu kwenye sherehe ile kuingia ndani ya ukumbi akiwa amebeba furushi la maua halisi mabichi saizi ya kati (Rose Bouquet)

Watu wote walimuona mwanaume lakini hawakuweza kumtambua ni nani hadi pale taa zilipowashwa na Ndio hapo walipoweza kumuona Victor akiwa amesimama mbele ya Eve, kutokana na wao wenyewe kujishangaa kutokana na walivyopendeza, Victor akasahau kutenda kile alicopaswa kukifanya pindi akiwa na Eve kama alivyokuwa amepanga.

Ukumbi mzima ulishangilia kwa mshangao, hakuna alie amini tukio lile, na zile kelele za mshangao ndio zilimfanya Victor akumbuke kile alichotakiwa kukifanya. Akamshika bega Eve na kumwambia apige magoti, kisha akampa lile furushi la maua, wanaume waliokuwepo mle wakapiga makofi na kinamama wakapiga vigelegele kwa nguvu sana.

MC akasema kuwaambia wageni waalikwa kuwa ukisikia Suprise ndio hii, kisha akaendelea

“Wageni waalikwa kabla wenyeji wetu hawajakaa, ninaomba Eve asimame na kuliweka hilo ua lake kwenye kiti chake kisha nae asimame mbele ya hichokiti” kwani hadi muda ule MC anaongea maneno hayo, Eve alikuwa amepiga Magoti na maua yake mkononi.

Kati ya watu waliokuwepo mle ukumbini, pia alikuwepo Ondiek na mpenziwe Yasmin. Hapo sasa ndio Ondiek alishindwa kuamini kama Eve ni mzuri kiasi kile, hakuwahi hata kuota kama Eve anaweza kuwa mzuri zaidi ya vile anavyo onekana, akajiapiza kuwa, ni lazima ampate.





Victor na Evelyn walikuwa ni kama watoto muda ule wakihitaji kuelekezwa kila kitu. MC akawaambia wageukiane na kutazamana kisha Victor apige goti moja la kushoto na atoe pete na kumvisha Evelyn. Huku akilia Eve akanyoosha mkono na Victor akakishika kidole cha pete na kumvalisha, akaibusu pete ile na kunyanyuka.

Aliponyanyuka akamkumbatia na kumbusu kwa mara nyingine na kumketisha kwenye kiti chake, watu walipiga makofi ikiwa ni mwendelezo wa furaha yao iliyo anza tangu walipoingia mle ndani, ile waliiweka vichwani mwao kuwa ni sherehe ya kukumbukwa hata kabla haijaisha.

Mambo mengi yaliyofanyika pale yalikuwa ni mambo mapya kwa watu wengi na yalionekana kabisa ni kama yalipangwa kwa siku nyingi sana na wakati ile ni Suprise. Shughuli ziliendelea kama zilivyopangwa, ila Eve alilalama sana kwa sababu Victor alimtenga, yaani hakumshirikisha.

Victor akamwambia kuwa anapaswa ajue kuwa ile ilikuwa ni Surprise, hakuna Surprise ya kumshirikisha yule unaemfanyia, Eve akaelewa na kukubali matokeo. Watu walikula chakula kizuri na kingi kilichoandaliwa vema na wataalamu wa mapishi toka Classic Decorating & Catering.

Muda wa zawadi ulipowadia, kwa sababu ya kutokuwepo zawadi, ikaaamuliwa wapenzi wale wawili ndio watoke pale meza kuu na waende kutoa mikono kwa wageni waalikwa na kila mmoja aanzie upande wake, Victor alianzia upande wa kulia kwenda kushoto na Evelyn akaanzia kushoto kwenda kulia.

Wageni wao waalikwa waliwapa hongera nyingi sana kwa jinsi sherehe yao ile walivyo iandaa. Victor alipofika kwa Ondiek, akamkumbatia jamaa yake na Ondiek akamwambia kwa bashasha

“Victor surprise yako imefunika hata ile ya Ommy na Lidya, hongera sana” alitabasamu zaidi Victor na kuendelea kusalimiana na wageni wengine. Eve na Victor walipokutana wakisalimia wageni wao ukumbini, walitazamana na kucheka, maana muda wote sura zao zilikuwa na tabasamu.

Eve alipomfikia Ondiek, akataka kumkumbatia, akakataa kiaina ila akampa tu mkono na hata hivyo Ondiek alimwambia kwa kumnong’oneza sikioni kwamba amependeza sana mpenzi wake wa zamani. Kauli ile haikumfurahisha kabisa Eve na kuendelea kusalimia wageni wengine.

Mbele yake alikuwepo Yasmin, Eve alimkumbatia na kupokea hongera zake za dhati. Walipomaliza kusalimia wageni wao, hawakurudi tena kukaa kwenye viti vyao bali walijichanganya na waalikwa na kuanza kubadilishana nao mawazo hadi MC alipowaita kule mbele na kuwaomba waketi vitini kwao ili ratiba iendelee.

Kilichofuata kwa mujibu wa ratiba aliyokuwa nayo MC ilionyesha kuwa ilikuwa ni wakati wa nasaha za wazazi. Kwa kuanzia tu MC alitoa nafasi kwa wazazi wa Eve kuongea kwanza kwa wao ndio waliozaa mke mwema. Alisimama Mzee Dotto na kutabasamu, alikosa na kuongea.

Baada ya dakika za ukimya uliosababishwa na kutokujiandaa, lakini alichoweza kukisema ni kwamba, tangu amekuwa na akili timamu, yaani tangu akiwa mvulana hadi sasa ni mzee, hajawahi kukutana na Surprise kama hii akaendelea kuongea kuwa kuanzia sasa wanatakiwa waanze maandalizi ya Harusi yao.

Akapenda kuwakumbusha kutojiweka mbali na ibada na mwisho akawaambia wao kama wazazi wa Eve wapo pamoja nao kwa kila hali, kisha akashukuru na kumrudishia kipaza sauti MC Kitenge, ambae kwanza alicheka na kusema kuwa kuongea napo ni fani kisha akampongeza mzazi yule wa Eve.

Ikafuatia zamu ya upande wa kina Victor, upande huo ukamteua baba mzazi wa Victor ndio aongee kwa niaba ya familia yake. Akasimama Mzee Johnson Maganga, nae hakuongea sana ila aalionyesha mshangao wake kwa tukio lile lilivyo andaliwa na kuwataka wasivuke miezi mitatu wawe tayari wamefunga ndoa.

Akaahidi kuwa popote watakapokwama katika kipindi chote cha maandalizi ya harusi, wasisite kuwaona kama wazazi wao na watakuwa nao bega kwa bega kama alivyosema msemaji alietangulia ambae ni baba Eve. Baada ya kumaliza maneno yale machache akamkabidhi Mic MC nae akawachekesha kidogo watu pale ukumbini.

Mwishoni mwa ratiba ile ilionyesha wazi kabisa kuwa wazazi wa kike, yaani mama yake Eve na mama yake Victor ndio watakao fungua muziki. Mwanzo kila mmoja alikataa, lakini MC akawanyanyua Victor na Eve wawaombe kwa njia yoyote wanayoweza ilimradi wafanikiwe kuwanyanyua wazazi wao na waombe wimbo.

Evelyn ndio alikuwa wa kwanza kupewa mic amnyanyue mama Victor, huku akiona aibu, Eve akashika mic na kumtazama Victor, mpenzi wake nae akamtazama na kumpa ishara ya endelea. Eve akaanza kwa kumuita mama huku akienda kule alipo alipomkaribia kwenye meza aliyokaa, akainama na kupiga magoti, kisha akasema;

Najua ni jinsi gani unanipenda mwanao, na hupendi kuona nikihangaika huku na kule ili kutafuta furaha ambayo kwako inapatikana bila gharama, si ndio mama yangu?” hata mama Victor alijibu basi? Alinyanyuka na kwenda kumnyanyua mkwewe pale chini na kumkumbatia na kusema kuwa yeye tayari amekubali.

Waalikwa walipiga makofi na Eve akarejesha mic kwa MC ambayo nae akaipeleka moja kwa moja kwa Victor ambae alikuwa muda huo amemkumbatia mpenzi wake Eve akimpongeza kwa maneno mazuri aliyoyasema japo hakuwa amejiandaa.

Mc ndio alikuja kuwatenganisha kwa kumpa mic Victoria na kumwambia afanye awezalo kumnyanyua mkwewe. Victor akipokea mic na kukohoa kidogo ili kuweka sauti sawa, hali iliyowafanya waalikwa karibu wote wacheke.akapiga hatua kuelekea kule alipo mama Eve bila kumtazama wala kumsemesha yeye.

Alipokaribia meza ya wakwe zake, akamuita baba Eve na kumwambia ahsante sana mzee wangu kwa kunisaidia kuliweka jambo hili mapema kabla halijatokea, akasema ama kweli utu uzima dawa. Kisha akamuuliza mkwewe alijuaje kama akikwama kwa jambo lolote arudi kwao? Sasa Mzee mie ninarudi kwako kabla sijaenda kwa mama moja kwa moja.





Ukumbi mzima ukishangilia na hadi mama Eve akacheka kweli kweli na kumsogelea mkwewe na kumpa mkono hata kabla mzee Dotto hajaongea lolote, Victor nae akambusu mkwewe kwenye mkono, watu wakishangilia kisha akamshika mkono na kumpeleka mbele kule alipo mama yake.

Mc akawaomba watu wapige makofi, kisha nae akawachukua kina mama wale hadi kwa DJ na kuwaacha huko kisha akaruhusu muziki uendelee wakati wao wakichagua muziki kule na DJ. Victor na mpenziwe walikuwa wakiongea wakiwa wamekaa mbele pamoja na Yasmin ambae alionekana amefurahi sana kwa kitendo kile.

Dakika kadhaa mbele kinamama wale wawili walifungua muziki kwa wimbo wa Nyota Wazir na kundi la Njenje kisha watu wote wakaungana nao pale mbele kulisakata Rhumba hadi wakati wakufunga muziki ulipowadia.

Kila mtu aliweza kutabiri ni kina nani watafunga muziki ule baada ya kinamama kufungua, kila mmoja alijua sasa itakuwa ni kina baba kufunga muziki, hata wao tayari walijipanga na kuamua kuchagua wimbo maalum ambao walichagua kuwa watafungia muziki, lakini hali ikawani tofauti kabisa na walivyo tegemea.

Aliwaomba MC watu wote waiache stage wazi ili awatangaze watakaofunga muziki, kisha akawaita Ondiek na Yasmeen na kuwataka wachague muziki wa taratibu mmoja kwa ajili ya kufungia muziki, kila mmoja akaambiwa achague aupendao na isifanane.

Walitazamana na kisha Ondiek akaanza kuongea kwa sauti akiomba wimbo wa Especially 4U wa Killie Minoque na kupigiwa makofi, akafuatia Yasmin na kutaka kuchezewa wimbo wa As long as U love me wa Backstreet Boyz, wimbo huu ulipigiwa makofi zaidi.

Eve alimuita Yasmin na kumpongeza kwa kuchagua wimbo mzuri kwa kumkumbatia na kumbusu kwenye paji la uso kisha muziki ukaendelea nao wakiwa wameruhusiwa kujiachia. Ajabu miziki walioiomba ikachezwa na watu wakaruhusiwa kucheza bila kizuizi.

Ghafla tu MC akakatiza muziki na kuwaita Eve na Victor na kuwaambia kuna Suprise ya mwisho, akawaambia yeye binafsi amewachagulia wimbo wa Shania Twain uitwao Still the One ndio watakao fungia muziki siku ile na pia utakao watoa mle ndani na kuwapeleka kwenye gari kwa ajili ya safari ya kuelekea nyumbani kwao.

Walifungua muziki, watu walipoingia kuungana nao, wakawaaga na kuanza wao kutoka wakifuatiwa na waalikwa nao wakatoka na kurejea makwao wakiwa na furaha tele iliyo na mshangao juu ya sherehe hiyo ya uchumba wa Suprise.

Bado wameketi palepale bustanini, Eve anamuuliza Victor kama bado analikumbuka tukio lile.

“Yah! Sana tu, we unasemaje ile? Si unaona kwamba ilifunika zenu zote zilizopita?” aliuliza Victor huku akimuweka vizuri miguu na kuweka kichwa chake mapajani kwa mpenzi wake ambae alilijibu swali lile kwa kuuliza

“We ulifikiri siku ile ulinifurahisha sana eti? Hujui tu, uliniudhi sana wewe” Eve alisema huku akim minya kwenye paji la uso kwa kidole cha shahada, Victor akamwambia yale yaliisha

Eve akamwambia sasa nae amueleze ni siku gani anayoikumbuka. Akasema anaijua nae akarudisha swali kwa Eve kama anataka amwambie, jibu likawa ndio kama tu anaijua siku yenyewe. Victor akanyanyuka huku akimuangalia Eve, Eve nae akamzingua

“Hiloo! Niambie kama waijua.. we unafikiri mie nitaijuaje siku uliyofurahi iowapo wewe mwenyewe hutaniambia?” akamwambia huku akimbinya pua mpenzi wake.

“Tatizo wewe mtoto unajidai nunajua sasa na hali hujui lolote, haya ngoja nikwambie...”

Victor akameza mate na kuanza kumwambia siku ambayo hatoisahau na aliyoipenda sana ni ile siku ya kwanza kumuona alipokuwa akishuka ngazi huku akiongea na simu, akamuomba simu ili amuonyeshe alivyokuwa akiuongea. Eve akatoa simu na kumpa Victor huku akitabasamu.

Akaichukua na kuishika kwa mapozi, akaanza kutembea kama anashuka ngazi huku akiongea kwa kuigiza

“Yeah! Mmh... Poa, jioni basi” uzalendo ukamshinda Eve akaangua kicheko kikubwa, akasimama na kuanza kumkimbiza Victor, walikimbizana kwa takriban dakika mbili tatu, wakaingia ndani.

*******



Juhudi za Ondiek kumrudisha Eve mikononi mwake hazikuishia njiani. Siku moja Victor alipokuwa akitoka kazini, katika pitapita yake mitaani akaiona Escudo ya Eve ikiwa imepaki sehemu Fulani, akatoa simu yake na kumpigia kumuuliza sehemu alipo, bahati mzuri Eve alitaja sehemu ileile ilipoonekana gari lake.

Eve nae akahoji ni wapi alipo Victor nae akamwambia ukweli. Eve akatumia nafasi ile kumuomba Victor aje aungane nae pale mezani. Victor hakubisha bali akaenda na kuungana nae, alishangaa kumkuta na Ondiek pale lakini hakujali, kwani alimtambua kama mfanyakazi mwenzao na tena ni bosi wao.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Alijiunga kwenye furaha na kadri muda unavyo kwenda ndio nao aliona kama unapotea bure. Puinde kidogo simu ya Ondiek iliita na akaomba kwenda fargha kuongea na simu ile. Walimruhusu ila wakabaki wao wawili tu, hapo sasa ndio Victor akapata nafasi ya kuhoji

“Ehe, Eve, imekuwaje saa hizi unakuwa upo sehemu kama hizi tena na mtu huyu ambae ni mume wa mtu ama kigezo ni kufanya nae kazi” Victor alikuwa na wivu sana na hakutamani kurudi nyumbani na kumkosa Eve

“Hapana Victor, mbona hichi ni kitu cha kawaida tu jamani?”

“Kawaida tu eti kwa mke wa mtu kukaa na mtu wa mtu baa si ndio?”

“Sio hivyo! Mimi nilipotoka kazini tu nikapita hapa ili nipate kinywaji, nimekaa muda mrefu peke yangu hadi alipotokea huyu na kujiunga name, sasa mazungumzo ndio yamefanya tuchukue muda wote huu mpenzi wangu” Kauli za Eve hazikumridhisha Victor ambae sasa alionekana kukasirika dhahiri japo alikuwa akijificha ficha, lakini ghafla akajikuta akiropoka kwa jazba

“Ni mazungumzo gani hayo yasiyokwisha kila siku? Kwanza mi…” kabla hajamaliza kauli yake Ondiek alitokea na kuwataka radhi kwa kuchelewa kisha akakaa. Victor akarudi katika hali yake ya kawaida na hakuonyesha dalili yoyote ya kukasirika, ila kile kitendo tu cha Ondiek kukaa, Victor akaaga na kuondoka.





Waliosalia pale wakabaki na mshangao, Ondiek akahoji ni vipi? Eve akajibu kuwaVictor hajafurahi kumkuta pale, nae akaaga na hata kabla Ondiek hajajibu, tayari Eve alikuwa ameisha nyanyua mkoba wake na muda huo akiwa amesimama kuelekea kwenye gari yake.

Victor alipofika nyumbani akaingia ndani na kuelekea moja kwa moja kwenye friji na kuchukua vinywaji kisha kuelekea nje kwenye kibaraza na kuketi juu ya kile kibaraza ambacho kimetumika kama fence fupi. Dakika chache baadae Eve nae akafika na kupaki gari kisha akashuka na kuelekea kule alipo mpenzi wake.

Alifika na kumsalimia Victor mpenzi wake, lakini hakuitikia kwa bashashsa kama ambavyo Eve amezoea kuitikiwa salmu yake na Victor, ikabidi amuulize tena

“Hivi Victor bado unayo tu yale ya huko mjinin? Hayajaisha tu”

“Hivi Eve unafikiri nini juu ya kitu hicho? Najua unahisi sijui chochote kilichopo kati yenu, lakini tambua nimeisomea Psychology (Saikolojia) hivyo kwa kumtatazama mtu ninaweza kujua kuwa Fulani ana tatizo ama ana kitu kinamtatiza pasina yeye mwenyewe kuniambia, sasa nawe twende ndani ukaniambie ni nini kipo kati yenu” Victor aliteremka pale juu alipokuwa amekaa.

Alimshika mkono Eve na kuanza kumburuza kuelekea ndani, huku akisikitika na kusisitiza kuwa hakuna kitu chochote kati yao zaidi ya mahusiano ya kikazi. Victor alimtazama Eve usoni na kumwacha pale Sitting room kisha yeye akaingia chumbani na kwenda kulala ikiwa ni saa 1 usiku.

Eve akabaki na mawazo kibao akijiuliza imekuwaje, baada ya nusu saa hivi alielekea chumbani kwake na kumkuta tayari Victor amelala muda mrefu uliopita. Siku hiyo hakutaka hata kwenda hata Studio, bali Eve alipoingia na kumuamsha, akamwambia yeye aende tu peke yake.

Nae akagoma kwenda peke yake, Victor akageuka upande wa pili na kuendelea kuchapa usingizi, hapo ndio Eve akajua kuwa leo amelikoroga barabara, ikambidi Eve ampigie simu DJ wa kuipindi chao na kumwambia acheze tu muziki muda wote wa kipindi chao, kwani wao hawatafika kwani wana matatizo.

Alikubali na kuwapa pole na kuahidi kutekeleza alilomwambia na kisha Eve nae akapanda kitandani kulala ikawa ni moja kati ya siku walizowahi kulala kuliko zote tangu waanze kuishi pamoja. Hivyo ndivyo siku zao za furaha katika maisha ya Victor na Eve zilivyoanza kuhesabika

*******

Siku moja katikati ya wiki Victor aliingia kazini na kumkosa Yasmin, ni kawaida kumkuta kwa kuwa yeye huwahi kufika kila siku, kwa zile siku ambazo haji kazini ama hujua kuwa atachelewa, basi hutoa taarifa mapema.

Tofauti na siku hiyo,Victor hakuwa na taarifa yoyote hadi muda ule juu ya kuchelewa ama kutokufika kwa Yasmin. Aliona ofisi ile bila Yasmin ni kama vile imekuwa kubwa kuliko na hadi inatia uvivu yaani anashindwa pa kuanzia, anakuwa hajui ni wapi aanzie.

Victor alihisi labda Yasmin ni mgonjwa, akavuta simu ya ofisini na kumpigia, jibu likawa hapatikani, akaacha na kuamua atampigia tena baadae kama alivyoshauriwa na kampuni husika ya simu, akahisi hana cha kufanya akaona ni heri ampigie simu Eve, waliongea na kufurahi.

Eve alikuwa ndani ya gari lake akielekea kazini, kwani siku ile alikuwa na kipindi cha mchana, walimaliza maongezi yao kwa kutakiana kazi njema. Baada ya maongezi yao, kwa mara nyingine Victor akakosa cha kufanya, akawa akifunua funua makaratasi mezani kwake.

Wazo lililofuata kichwani mwake ni kutoka ofisinin kwake na kueleka ofisini kwa Mzee Katembo kwenda kumsalimia. Alipofungua tu mlango wake na kufika kwenye ofisi ya Katibu Muhtasi wake, alimuona Yasmin amekaa kwenye kiti chake, akiwasha simu yake, macho yakiwa mekundu sana huku yakitoa machozi.

Ilionyesha kabisa hakuwa ameanzakulia muda ule, bali ni muda mrefu uliopita, akamsogelea

“Yasmin, vipi mama? Una tatizo gani?”

“Aah Boss, mie sina tatizo, ila samahani kwa kuchelewa kufika kazini” alijibu Yasmin huku akisimama na kujifuta machozi kwa kitambaa chake cha mkononi.

Victor nae hakujali ile samahani aliyo ombwa ila kilichomshangaza ni kumuona Yasmin akilia, alimwambia asijali lakini akaomba tena amwambie kama ana tatizo linalo msumbua. Victor alizidi kumsogelea.

Yasmin akamtazama na kumwambia ni kweli ana tatizo lakini ni la kifamilia tu ambalo hapaswi kumshirikisha mtu wan je ya familia yake.

Hapo ndio Victor alikuwa akipataka, akamuuliza tena kama anaweza kumsaidia. Yasmin akamjibu kwamba asingependa kuona mtu yeyote akipata usumbufu kwa ajili yake, sasa Victor akazunguka kabisa na kuingia ndani alipo Yasmin na kumshika bega huku akimwambia

“Oh Yasmin, kumbuka hata name nipo nawe hapa kama sehemu yako, maana tupo pamoja mien awe kwa muda mrefu kuliko hata familia yako, usijali nakuahidi kukusaidia, niamini”

Alijitahidi kutumia kila aina ya maneno ya kushawishi hadi ikafikia hatua akatepeta na kukubali kumwambia tatizo lake. Alimweleza tatizo lenyewe ni kwamba mumewe, ina maana Ondiek kwa sasa amebadilika tabia, kwani hamjali tena kama mkewe.

Kibaya zaidi amekuwa akimwambia moja kwa moja kuwa anataka kurudiana na mpenzi wake wa zamani ambae walitengana na sasa dalili zinaonyesha kuwa bado wanapendana, muda wowote tangu sasa wanaweza kurudiana.

Yasmin alimweleza mambo mengi sana ambayo anafanyiwa na Ondiek, mazuri machache yalikuwepo ila mabaya yalikuwa ni mengi zaidi lakini alivumilia, ila alisikitika zaidi kwa huyo mwanamke kuingilia kati penzi lao na hali nae ni mke wa mtu.

Victor alishangaa na kumuuliza swali moja tu, je anamjua? Yasmin akaruka kimanga na kujitetea kuwa anamsikia tu Ondiek akisema hivyo. Kifupi japo Yasmin alikana, lakini alikuwa akimjua mwanamke mwenyewe anamtetemesha kwenye ndoa yake.

Maswali yakaendelea kutoka kwa Victor kuelekea kwa Yasmin, kama kuna mwanamke yoyote anaemuhisi. Akakataa tena na kusema hana lolote ajualo na hapaswi kuongozwa na hisia ndio maana anaona amalize machungu yake kwa kulia kuliko kupata aibu ya kumvamia mtu na bahati mbaya akawa si yeye, hivyo bado anafanya uchunguzi.





Elimu ya saikolojia alioisoma Victor hapa sasa ikafanya kazi yake, akaanza kuongea nae juu ya maisha na kumshauri juu ya mapenzi. Walizungumzia kuhusu furaha na matatizo akimwambia hivyo ni vitu ambavyo ni lazima mtu upambane navyo katika maisha yako.

Baada ya muda mchache tu, Yasmin akajisikia vizuri tu na kuanza kufanya kazi zake kana kwamba hakuna lililotokea, tabasamu lilrejea usoni kwake na hadi akatoa ofa kwa bosi wake kwenda kunywa chai, Victor akacheka na kumwambia aagize chai wanywe palepale ofisini, Yasmin akanyanyuka kwa furaha na kutoka nje, Victor akatabasamu na kurejea ofisini kwake.

*******



Siku zilikwenda mbio, miezi ikakatika, mida ya Evelyn kujifungua ikakaribia, akachukua likizo na kwenda kwao Mwanyamala kwa Mama Zacharia ambapo ni nyumbani kwa wazazi wake.

Siku moja usiku Lidya alimpigia simu Victor na kuongea nae kwa muda mchache tu, kumwambia anataka kuongea na Eve ambae kwenye simu yake hampati, shida yake kuu ni kumsalimia. Victor akamweleza kuwa ameenda kwao kujifungua kwani hadi sasa zimesalia siku kati ya 9 ama 10 tu ambazo walikadiriwa hospitali.

Lidya akalaumu sana kwa kuwasumbua wazazi wa Eve na hali umri wao umewatupa mkono, kuna baadhi ya mambo wanapaswa kupumzishwa, likiwepo hilo la kusimamia mzazi, mwisho Victor akamuuliza yeye ana maoni gani.

Hapo ndio akamwambia anataka yeye aende kujifungulia Jijini Nairobi nyumbani kwake. Victor hakukubali wala kukataa, isipokuwa alimwambia Lidya, aongee na Eve mwenyewe na ndio atatoa maamuzi ya mwisho, walikubaliana hivyo na kisha akamtumia namba ya mama Eve.

Baada ya maongezi yao kwisha kati ya Lidya na Victor, Lidya akapiga simu kwa mama Eve na kumsalimia, kisha akaanza kuongea na Eve na kumshawishi, Eve nae pia hakupinga bali tu akaomba muda hadi asubuhi wa kujadiliana na wazazi wake hivyo wakaahidiana kuwasiliana mapema tu siku ifuatayo.

Siku ya pili asubuhi, Victor alipoamka tu, kama kawaida yake mtu wa kwanza kuwasiliana nae alikuwa ni Eve, baada tu ya salamu ya asubuhi akamuuliza kama ameongea na Lidya, akakubali na kumueleza maongezi yao yalivyokuwa.

Victor bado hakumwambia msimamo wake bali akamwambia akimaliza maongezi na wazazi wake, amjulishe nae maafikiano watakayo fikia.

Wazazi wa Eve hawakuwa na kipingamizi, muda uleule Eve akamjulisha Victor juu ya kukubali wazee wake kwenda kujifungulia huko Kenya, kisha akamuuliza yeye Victor anasemaje? Nae akajibu hana tatizo na akamuahidi akitoka kazini atakwenda huko Mwananyamala kumuona.

Mwisho akamuuliza kama ameisha wasiliana na Lidya. Eve akamwambia hawezi kuwasiliana na Lidya na kumueleza yote bila ridhaa yake mume. Victor akafurahi kusikia vile na kumwambia wawasiliane tu na amwambie jinsi makubaliano yao yalivyo. Eve akamwambia wakimaliza tu kuongea, atampigia na kumwambia.

Swali la mwisho lilikuwa ni lini Eve atapenda kuondoka hapa nchini? Akajibu hata kesho yey yupo tayari kuondoka, Victora akamwambia basi leoleo atakwenda kumfanyia mpango wa tiketi ili siku ifuatayo aondoke iwapo atapata tiketi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Kama alivyoahidi, jioni alipita Classic Agencies nmbao walikuwa ni mawakala wa shirika la ndege la Fast jet akachukua tiketi moja ya siku ifuatayo na kuanza safri kuelekea Mwananyamala kwa kina Eve. Alikaa kule hadi usiku ndio akarejea nyumbani na kuahidi kesho atamfuata.

“Nitakufuata kesho ili kukupeleka Airport, kama tiketi inavyosema, muda wa kuwasili uwanjani ni mchana, hivyo maandalizi yako fanya asubuhi, sitaki kucheleweshana mie”

“Sawa mume, wewe si unanjua mkeo jembe?” alitania Eve na kumfanya Victor acheke, kisha akanyanyuka na kuaga na akarejea kwake kulala.

Asubuhi victor aliripoti kazini kwake na kufikia saa 5 akaondoka kuelekea Mwananyamala kwa wakwe zake. Walikaa na kula kabisa chakula cha mchana kisha wakaondoka familia nzima kuelekea Airport kumshindikiza Eve. Njiani Victor alimwambia Eve kuwa wataendelea tu kuwasiliana kila mara hadi siku atakayojifungua.

Wakakubaliana mara baada ya yeye kujifungua ndio Victor nae atapanda ndege kumfuata ili warejee wote nyumbani.

Kwa muda waliowasili Airport, hawakukaa muda mrefu sana ndege ya Fast Jet ikatangazwa na kuondoka. Walikaa hadi walipoona imeruka angani ndio nao wakaondoka kurejea nyumbani. Victor aliwarejesha kwanza wakwe zake kwao Mwananyamala kisha ndio nae akarejea nyumbani kwake.

Alipofika hakukaa muda mrefu akaanza maandalizi ya kipindi chao na mpenzi wake cha Romantic kwa kuandaa mada moto na kuanza kuwasiliana na meneja wa Classic Band kujua maendeleo, maana alikuiwa na muda mrefu hawajawasiliana, alipohakikishiwa mambo ni mazuri, akatoka na kufunga mlango wake kisha akaenda Studio akiwa ni mpweke.

* * * *



Siku ya jumapili usiku, Victor aliingia Studio akiwa peke yake, maana tangu Eve aanze likizo ya uzazi, karibu kila siku alikuwa akiingia peke yake, lakini mara nyingi alikuwa akipata mtu wa kuwa nae Studio kumpa kampani.

Watu kama Ondiek na wengineo wakiwemo hata mabinti wa pale Classic FM walikuwa kila mara wakiomba wajumuike nae kwenye kipindi chake.

Daima hakuwakatalia, bali alikubaliana nao na kuwashirikisha hadi kwenye kuandaa mada ya siku wenyewe.

Na katika kukiboresha zaidi kipindi chao, kuna baadhi ya siku alikuwa akiwaalika wageni tofauti, wakiwepo wadau wake wakubwa wa kipindi chake na wataalamu mbalimbali wa mada alizokuwa ameziandaa kwa siku husika, hivyo kila siku kipindi chake kilikuwa kinaleta ladha tofauti kabisa, kilikuwa hakiishi hamu.

Saa 3 kamili usiku siku hiyo ya jumapili kipindi cha Romantic Love huanza muda huo, kikiwa ni kipindi kipya kabisa na ni tofauti na kile cha siku za kazi ambacho huanza saa 4 na robo usiku. Muda huo umeongezwa kutokana na maombi ya wananchi wanaopenda vipindi hivi.

Mada ya siku ile ilikuwa ni ‘Usaliti mapenzini, nani alaumiwe’ akiwa bado anachombeza chombeza kwa maneno na muziki laini, mada hajaiweka mezani bado, alikuwa akitayarisha nukta zake muhimu, simu yake ya mkononi ikaita.

Ilikuwa ni namba ya nje ya nchi lakini hakuijua ni ya nani, lakini alipoiangalia akagundua ni code ya Kenya, akajua kabisa ni jamaa zake hao japo hakujua ni mkewe Eve, jamaa yake Ommy ama shemejie yake Lidya.

Alipopokea simu ile akakutana na lawama kutoka kwa Ommy alie kuwa akimlaumu kwamba pamoja na mkewe kuwa kule, lakini bado alikuwa hataki hata kupiga simu. Victor alicheka na kisha akamjibu kwamba sio kama anavyofikiria yeye bali muda unakuwa haumtoshi kabisa, maana hadi muda ule bado alikuwa yupo kazini tena peke yake.





Alijitetea sana kwa kumweleza kuwa akitoka kazini kwake anajikuta anatakiwa ajiandae tena kwa ajili ya kwenda Studio kwa kuandaa mada ambayo kila mtu ataipenda, hali hiyo humfanya awe na kazi nyingi na kujipa ahadi ya kuwasiliana nao jioni, lakini hatimae siku inaisha.

Ommy alimuelewa na kumpa pole kisha akamwambia Eve anataka kuongea nae, Victor akamwambia Ommy amwambie atampigia usiku akitoka kazini, maana muda wa kuweka mada mezani umefika na anajua akianza kuongea na Eve, muda ataupoteza sana.

Cheko ya Ommy ikamfanya Victor ashangae, Ommy akamwambia amsalimie tu dakika moja kisha atakata simu, hata kabla Victor hajajibu, Ommy akawa tayari amempa simu Eve, Eve akamsalimia mpenzi wake akiwa anaonekana ni mwenye furaha tele kutokana na sauti yake.

“Mpenzi wangu leo nina habari kubwa na nzuri sana kwako, unaweza kuibashiri wewe mwenyewe?” Eve alisema kwa madaha, Victor akacheka na kumjibu

“Ah! Nimeisha jua, ni lazima utakuwa umejifungua kipenzi change, uongo ama kweli?” aliuliza huku mapigo yake ya moyo yakienda kasi na kama angeulizwa ni kwa nini kwa yakini kabisa angejibu kuwa kwa asilimia 100 hajui ni kwa nini na kwa ukweli huo ndio ulikuwa ukweli wenyewe, hakujua sababu.

“Haya umepatia, swali lingine nimejifungua mtoto gani?” Aliuliza Eve huku Victor akiwa na furaha ya ajabu, kama vile haamini amini vile, akajibu kimasihara, kasahau tena kama alikuwana haraka ya kuanza kuweka mada mezani, akamwambia mkewe

“Mtoto wangu aliezaliwa leo, kama sio wa kike, basi lazima atakuwa ni wa kike, nimepatia ama nimekosea?” Eve akacheka sana na kumwambia achague jinsia moja anayohisi ndio ya mtoto wake, hakufanya hivyo, bali wakaanza utani karibu dakika 5 nzima. Mwisho Eve akamuuliza swali ambalo alimwambia litakuwa ni la mwisho.

Swali lilikuwa ni jina la mtoto, alitaka kujua yeye kama baba wa mtoto, je kama mtoto ni wa kike aitwe nani na kama ni wa kiume apewe jina gani? Victor akasema kama ni wa kiume aitwe Bill na kama ni wa kike, basi anamuachia nafasi yeye mwenyewe achague jina zuri atakalolipenda.

“Kama angekuwa ni wa kike angeitwa Rachel, lakini jina ulilolitaja ina maana linapita bila kupingwa, kwa hiyo kuanzia sasa, wewe ni Baba Bill, name ni…” kabla hata Eve hajamaliza, Victor akadakia

“…Mama Bill…” kisha akapiga kelele za kushangilia hadi Eve akasikia na kushangaa. Akajua ni kiasi gani mumewe amefurahi, kwa taarifa ile. Alitegemea kuwa atafurahi, lakini si katika kiwango kile alichiokisikia.

Sasa wale waliokuwa Studio nao wakishangaa mbona kelele zinatokea ndani na hali si kawaida kuwa vile? Wakasogea mbiombio kujua kuna nini kinaendelea. Victor sasa ndio akashtuka kuwa yupo Studio na muda huu anaongea na simu badala ya kuweka mada mezani.

Akatazama saa na kugundua tayari dakika zisizopungua 20 zilikuwa zimeisha potea tangu alipoingia kwenye kipindi na huwa sio kawaida ya kipindi chao. Akamwambia mkewe

"Haa Mama Bill, ujue nipo Studio na nimechelewa kuanza kipindi kwa dakika zaidi ya 20, sasa niache kwanza, nitakupigia baadae, I love U sana mama Bill." Upande wa pili Eve alishindwa kujibu lolote bali alitabasamu tu kutokana na kupagawa vilivyo kwa Victor, isipokuwa alimwambia tu

"Kazi njema mpenzi, usisahau kunipigia baadae, nimekukumbuka sana Baba Bill." Simu ikakatwa na mawazo yake sasa akayarudisha Studio ambapo muziki wa taratibu ulikuwa ukiendelea. Aliuacha ukaendelea hadi muda aliopanga ulipotimu kisha akasema

"Unaendelea kusikiliza Romantic Love kutoka Classic FM ikikutangazia kutoka katikati ya Jiji la Dar Es Salaam, imetimia saa nne na nusu usiku" akavuta pumzi na kuendelea

"Umefika muda muafaka wa kuiweka hewani mada yetu ya leo, mada yenyewe ya leo inasema;

Utapokeaje ujumbe toka kwa mpenzio ama mkeo anaekujulisha kuwa amejifungua mtoto wenu ambae anakuwa ndio wa kwanza?" akairudia tena na kisha akasema

"Haya wapenzi wasikilizaji wetu, nasubiri majibu yenu hapo itakapotimia saa tano kamili usiku huu kupitia namba zetu zile zile za kila siku kwa mwenye kutaka kwenda hewani moja kwa moja , basi apige simu kwenye namba yetu ya mezani, na kwa wale wanaotaka kutuma sms, watumie namba zetu zile zile za mkononi" akanywa maji kidogo ili kupoza kiu na kupata nafasi ya kupumzisha koo kisha akaendelea

"Wakati tukiwa tunasubiri muda huo kufika, tupate burudani mfululizo, na kwa kuanzia tu tutaanza na mze mzima Michael Bolton katika kibao chake maarufu kiitwacho 'Said I loved U but I lied' ambacho kitafuatiwa na Tamia Davis akisema 'Im so into U' mpendwa msikilizaji, tuonane hapo baadae itakapotimu saa tano kamili."

Kawaida hata usiku uwe ni mrefu vipi, lazima asubuhi itafika tu, ndivyo ilivyokuwa, muda hata kabla haujatimu, tayari kulikuwa na ujumbe kadhaa zimeingia kwenye simu ya Victor pale studio. Muda ulipotimu, simu nazo zikaanza kumiminika, karibu watu wote walikuwa wakisema itakuwa ni furaha tupu itakayotawala siku hiyo.

Wapo baadhi walijitokeza na kudai kuna suala la woga huwa nalo lipo, walisema wahusika baadhi hupata woga kwa kujua kuwa familia imeongezeka, wazo ambalo lilipingwa vibaya sana na wachangiaji wengine kwa kusema

"Kama hujajiandaa mapema ulitaka mtoto wa nini?" Bwana mmoja ambae ni msikilizaji mkubwa na mpenzi wa kipindi hicho aliejitambulisha kwa jina la Lingu aliuliza hivyo na kisha akaendelea

"Ile miezi 9 ya mtoto tumboni inatosha kabisa kwa mzazi kujiandaa, sasa wewe unataka ujiandae kivipi? kujiandaa zaidi ya miezi 9? hapana bwana..."

Kwa kweli mada ilikuwa ni nzuri na ilipendwa sana na wachangiaji wengi walijitokeza, hadi saa 7 usiku, muda ambao ni wa kufunga mjadala bado watu walikuwa na shauku ya kuchangia mada ile. wakajitokeza watu wawili wakiomba mada ile irejewe tena siku ya pili.

Victor akawaambia kuwa hilo sasa ni suala jingine. maana mada huwa ni siku ya jumapili, hivyo haitawezekana kuweka mada siku ya Jumatatu kwani hiyo siku ni ya kitu kingine. Watu wengi wakawa wameridhika na jibu lile japo wasioridhika walikuwa wapo, lakini wengi wape.





mada ikafungwa rasmi na Victor akatoka ofisini ili kurejea nyumbani akiwa na furaha tele moyoni, kwanza kwa kufanikiwa kupata mtoto, pili mkewe kujifungua salama na mwisho alifurahi kwa kuweka mada ambayo aliweka ghafla lakini ikakubalika mbele ya wasikilizaji.

Alifika nyumbani kwake saa 8 na kuingia ndani. Badala ya kulala, akaanza kuutumia muda ule kuwapigia wazazi wa pande zote mbili, pia ndugu na jamaa zake wa karibu kuwajulisha juu ya mkewe kujifungua salama na kupata mtoto wa kiume. wengi walifurahi na kumpongeza, zaidi wakamtakia maisha mema na familia yake.

Sasa ndio akampigia simu Eve mkewe kama alivyo muahidi na kuongea nae kwa takribani nusu saa nzima wakiwa ni wenye furaha kedekede kwa kupata mtoto wao wa kwanza. Waliongea kama vile ule ni mchana wa jua kali, kumbe ulikuwa ni usiku mnene, walijisahau kabisa.

Victor akamuaga Eve kwa ahadi kuwa ndani ya siku mbili za mbele nae atakuwa ndani ya Jiji la Nairobi na kukata simu. Victor alijiona yeye ni mshindi kupita kiasi. Akapiga ngumi hewani ishara ya ushindi huku akijisemea moyoni

"Ukipanda mbegu, unapaswa kuona mmea na baadae uvune, Ahsante Mungu kwa kuniwezesha kupata shamba na kupanda mbegu na kuona mmea bora na sasa nimevuna" Akamshukuru tena Mola na kuvuta shuka kulala, ikiwa ni alfajiri kabisa.

Siku iliyofuata kama kawaida, asubuhi Victor aliamka na kwenda zake kazini akiwa ni mwenye furaha tele kwani hadi muda ule tayari alikuwa ameongea na mama Bill zaidi ya mara mbili kwa asubuhi ile tu na akiwa amepokea simu za pongezi kibao toka kwa marafiki.

Alishangaa kuona hata wale ambao alikuwa hajawapa taarifa, nao walimpigia na kumpa pongezi. Alipokea simu nyingi mno, hadi akaona raha ya kuwa ni Super star. Baadhi ya watu walijitambulisha kama wasikilizaji wazuri wa kipindi chao.

Kifupi Victor alipokea pongezi zote kwa dhati. Baada ya muda mchache aliwasili ndani ya ofisi yake akiwa amechelewa kidogo kutokana na kusimama mara kwa mara pindi alipokuwa akisimamishwa na wadau wa kipindi chake pia watu kadhaa anaowajua na asio watambua.

Wote hao hawakuwa na jipya zaidi ya kumpa hongera ya kupata mtoto wake wa kwanza na wapo waliomsimamisha ili tu kujua jinsia yake na jina lake, hakuwaficha, akiwa na tabasamu kubwa usoni, aliwaambia kuwa ni mtoto wa kiume na jina lake ni Bill.

Aliingia moja kwa moja hadi kwenye ofisi yake na kumkuta Yasmin tayari ameketi kwenye kiti chake. Victor kwa jinsi alivyoamka siku ile, alishindwa kuizuia furaha yake. Hata Yasmin alipomuona tu akajua kuwa leo bosi wake ana furaha kubwa mno.

Salamu ilipokwisha tu, kabla hawajaongea mengi, Yasmin akampa pongezi kwa mkewe kujifungua mtoto wa kiume. Victor akishangaa na kumuuliza kajuaje kama Eve kajifungua? Nae akamwambia kuwa taarifa zile amepewa na Ondiek tangu jana usiku, kwani nae yupo huko.

Victor hakujali kwani alijua Ondiek kule Nairobi ni kwao na pia si mbaya kwa mtu kwenda kuwatembelea watu aliokuwa akiishi nao kwa amani tena akifanya nao kazi bega kwa bega, hakuwa na mawao yoyote chanya juu ya kauli ya Yasmin.

Kumbe lengo la Yasmin ilikuwa ni kutaka kujua Victor atalipokeaje hilo suala baada ya kumwambia. Kwa kuwa Victor hakushtuka, Yasmin akajua kuwa Victor hajui lolote linaloendelea kati ya Eve na Ondiek.

Akamtazama kwa huzuni wakati Victor akiongea na simu akiwa kashika kitasa cha mlango wa ofisi yake. Alipomaliza kuongea na simu akarudi tena kwa Yasmin na kumuomba watumie muda wao wa chakula cha mchana kwa ajili ya kwenda madukani kumnunulia nguo na mapambo mtoto wake, pia zawadi chache kwa ajili ya mkewe.

Victor alimchagua Yasmin kwa kuwa Yasmin tayari ni mzoefu, maana yeye tayari ana mtoto mmoja wa kike aitwae Ummy, hivyo aliamini atakuwa anaweza kuchagua kilicho bora kwa ajili ya mtoto. Bahati mzuri hakukataa, kwa yakini kabisa akakubali kwenda nae.

Muda uliwadia nao wakajimwaga madukani na kununua kila walichokiona kinafaa kwa ajili ya mtoto wake kisha wakanunua zawadi kwa ajili ya Mama Bill. Wakatoka na kuingia hotelini kwa ajili ya chakula cha mchana, kisha Victor akamrejesha Yasmin ofisini nae akaenda nyumbani.

Nyumbani alipofika tu, kitu cha kwanza alielekea kwenye kabati yake ya nguo na kufungua sehemu ya kati ya kabati lao la milango mitatu ambapo palikuwa na vitu vidogo vidogo, akapanga nguo mpya kabisa alizomnunulia mkewe kama zawadi.

Akaenda na kufungua chumba kimoja kilichokuwa kitupu na kukisafisha, hakikuwa kichafu sana, bali ilikuwa ni kama kufuta futa vumbi, akaanza napo kupanga vitu vya mtoto alivyonunua, kama vile kitanda, midoli na vyote alivyonunua ambavyo alihisi vinafaa kukaa pale chumbani.

Napo alipomaliza na kujiridhisha kuwa pamekuwa vile atakavyo, alitazama saa yake na kuelekea chumbani mwake. Akachukua simu na kumpigia Eve. Upande wa pili Eve alikuwa akimbembeleza mwanae aliekuwa akilia, hivyo alipopokea simu tu akaiweka karibu na Bill.

Sauti ya kilio cha Bill ilimfikia Victor moja kwa moja ambae alifurahi sana kuisikia sauti ya mwanae wa kwanza, kwa mara ya kwanza

“Umesikia sauti ya Bill?” aliuliza Eve wakati Victor akiwa bado yupo makini akimsikiliza Bill.

“Ndio, kwanini analia kiasi hicho?” aliuliza Victor akishangaa.

“Mwanao njaa inamsumbua, ananyonya kama leo kaambiwa anaacha ziwa.”

“Ha ha haaa! Mwambie kuna magereza.” Wakaanza kutaniana, mwisho Eve akamuuliza Victor

“Unajua Bill kafanana na nani?”

“Najua vizuri sana kuwa kafanana na Mzee John na nina hakika na hilo.” Jibu hilo lilimfanya Eve agune na kusema;

“Nilijua tu, lazima Ommy atakwambia…” kumbe wala Victor alikuwa hajui lolote, akauliza

“Vipi kwani baby nimepatia?”

“Usijidai kuuliza kiumbea, mie najua utakua tayari umeambiwa na shem.”

Waliongea kwa muda mchache tu kisha Victor akamwambia ameruhusiwa kuondoka Jumatano ila Jumatatu ijayo anapaswa kuwa kazini. Akamueleza kuwa anatarajia kuondoka siku hiyo na basi la Classic na watarudi pamoja siku ya Jumamosi kwa ndege, wakaagana.





Japo Nairobi ndio kwao na Ondiek, alikwenda kule kificho tena kwa kutoroka, hakumuaga yoyote. Ndio maana hata Victor hakujua hadi pale alipomsikia Yasmin akizungumzia uwepo wa Ondiek kule. Sababu iliyompeleka kule, haikuwa nyingine, bali aliamini anaweza kuongea na Eve kwa kirefu na kwa nafasi, maana kule Nairobi, mtu wanaemuhofia, hatokuwepo.

Mtu waliekuwa wakimuhofia huku Dar alikuwa ni Victor. Kwa kuwa kule Nairobi alikuwa hayupo, Victor alijua akimuomba Ommy na mkewe nafasi ya kumtembeza Eve, hawatamkatalia, watamruhusu kwa kuamini yeye ni mwenyeji kuliko wao.

Lakini kumbe alikuwa akijidanganya, maana Lidya alishtuka, walimpa nafasi ya kutoka na na Eve, lakini kila walipotoka Eve na Ondiek, Lidya alikuwa pembeni yao. Hadi siku za Ondiek kukaa kule zikamuishia pasina kupata nafasi nzuri ya kuongea na Eve, ikamlazimu siku iliyofuata mara baada ya Eve kujifungua, yeye ageuze kurudi Bongo.

Usiku wa siku ile ya kujifungua Eve, Ondiek alimpigia simu na kumwambia dhumuni hasa la yeye kuwepo pale. Akaomba samahani nyingi na kuahidi hatomuumiza tena iwapo atampa nafasi nyingine ya pili. Mwanzo Eve akawa akimsikiliza tu Ondiek akitamba kuhusu mtoto.

“Na kuhusu suala la mtoto, niachie mimi, tena wala usiwe na shaka juu ya hilo kwani nitamtunza kama ninavyomtunza mwanangu wa kumzaa mwenyewe Ummy” akameza mate na kuendelea

“Kwa kukuonesha kuwa ninajali, nimejitolea kuja mapema zaidi hata kabla baba halisi wa mtoto hajafika hapa Nairobi.” Ondiek aliendelea kutoa ahadi kemkem kwa Eve na mwanae mchanga, akamuahidi yupo tayari kumfungulia Bill akaunti ya watoto kama atakubali kurudiana nae.

Eve alilipinga hilo kwa nguvu zake zote na kumtaka Ondiek aache mara moja kumsumbua, na akamuasa kama ataendelea kumsumbua, basi atamjulisha Victor mara moja kuhusu usumbufu wake, kisha akakata simu.

Kipindi Eve alipokuwa akiongea na Ondiek, Lidya hakuwa mbali na aliweza kusikia kila kitu kilichokuwa kikizungumzwa na akatumia nafasi ile kumshauri Eve asije kujidanganya na kurudiana na Ondiek. Akamwambia kama kuna siku akisikia juu ya wao kurudiana, hana adhabu ya kumpa zaidi ya hiihttp://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Unasikia Eve, siku nikisikia kabisa kuwa umerudiana na Ondiek, tambua dhahiri kuwa tangu siku hiyo usinisemeshe tena.” Lidya hakuwa akitania, bali alikuwa yupo serious kwelikweli. Japo wanasema kauli imetoka mdomoni, ile ilikuwa ni lazima ipite mdomoni, lakini ilitoka ndani kabisa kwenye uvungu wa moyo.

Kama angeweza kumuonyesha kwa kitendo ni jinsi gani hataki hata ukaribu na Ondiek, basi angemfungulia moyo akaona kwamba kile anacho kisema ndio anacho kimaanisha na hata hatanii. Eve akamuahidi hawezi kufanya hivyo hata kwa bahati mbaya wala kwa mtutu wa bunduki, maana hata nae anamchukia sana Ondiek.

Lidya akamchukua mtoto na kuanza kucheza nae kwa kumrusha rusha juu na kumdaka huku akimuimbia nyimbo mbalimbali, wakati huo Eve alikuwa mbali kimawazo. Japo alionekana mkimya kama vile anamtazama mwanae anaerushwa rushwa juu na Lidya, lakini mawazo yake hayakuwepo pale kabisa.

Moyo wake ulikuwa ukiongea peke yake, ulikuwa ukijiuliza

“Hivi kwa Victor nakosa nini? Mbona kila kitu nakipata? Mahitaji yote muhimu nayapata, penzi la kweli na heshima, vyote navipata, sasa ni nini cha kunifanya nihadaike na Ondiek? Siwezi kurudiana nae hata kwa nini! Kama kazi ninayo, gari ipo, nyumba na hata shamba hivyo vyote vipo, tatizo lilikuwa ni mtoto, Mungu tayari ametujaalia mtoto huyu hapa, sasa bado nini? Labda ni Ukimwi tu ndio unapatikana kwa Ondiek, siku akinipigia tena simu.., atajuta kunifahamu.” Hayo ndio aliyokuwa akiyawaza Eve.

Akanyanyuka na kutoka akiwaacha Lidya na Bill waliwa chumbani yeye akaelekea nje kunyoosha miguu kidogo huku akizidi kutafakari maneno ya Ondiek juu ya ahadi ambazo anamuahidi.

*******



Victor aliwasili Jijini Nairobi kama alivyoahidi na kupokelewa na familia ya Mr. Ommy Bazo. Wote walitawaliwa na furaha kwa kukutana tena wote ugenini katika nchi ambayo hakuna mtu mmoja ambae ambae amezaliwa kule, hiyo ilisababisha kabisa wawe na furaha tupu.

Nyumbani kwa Ommy kuliandaliwa sherehe fupi kwa ajili ya kufurahia kukutana kwao tena wakiwa nje ya kwao. Tangu kuingia ndani hakutoa hata dakika moja kwa mtu mwingine yeyote kumshika mtoto.

Muda wote Bill alikuwa mikononi mwake na kama inavyojulikana, pale anapokuwepo yeye, basi ni lazima ataongea, akawatazama zamu kwa zamu na kisha

“Pamoja nanyi kusema kuwa mna furaha, lakini mie na familia yangu tuna furaha zaidi kwa sababu tumepata nafasi ya kuwatembelea nyinyi, hiyo imetupa furaha zaidi yenu kwani tumewaona hadi mnapoishi na kizuri zaidi kilichoongeza furaha ni hali ya kuzaliwa Bill kwenye mikono yenu, nashukuru sana kwa msaada wenu wa hali na mali, ahsante sana ndugu zangu.”

Shukrani zilimtoka Victor kwa niaba ya Eve, kisha akanyanyua glasi na kugonga na wenzie pale ndani. Lidya ambae muda wote alikuwa busy, akaelekea nje, Ommy akasema

“Victor sasa hivi sisi ni ndugu, haya tunayofanya sasa ni haki yetu kjabisa, huna haja ya kutushukuru kwani ni sawa na haki ya mtoto kusomeshwa na mzazi wake, hivyo nasi tuna haki yakumhudumia Eve kama shemeji yetu.” Victor alikuwa akimuangalia Ommy huku akitikisa kichwa chake ishara ya kukubaliana nae.

Lidya ambae hakuwepo muda huu wa mwishoni mwishoni, akaingia akiwa amebeba sahani kubwa iliyokuwa na nyama tupu ndani yake, Eve akamtania huku akitabasamu

“Dada Lee, huogopi RVF?”

“Ah! Wapi… hiyo Rift Valley humu ndani haitogusa, halafu na daktari tunae hapahapa, eti Dr. Victor, hiyo homa ya bonde la ufa ina nafasi humu ndani?” wote wakacheka kisha Victor akamwambia Lidya aacha utani wale kwanza, wakaanza kupata mlo taratibu.

Baada ya kimya kifupi, Victor akatoa wazo binafsi, akawaambia kuwa kwa sasa anaona kama wana uwezo wa kujiendesha kikampuni iwapo tu watajipanga vizuri, wakawa hawajamuelewa kutokana na swali la Lidya alietaka kujua kujua Victor anamaanisha nini.

Victor akasema anawashauri waanzishe kampuni yao ambayo itakuwa inajiendesha yenyewe kupitia wao watu wane waliopo pale mezani

“Kifupi tuanzishe kampuni yetu ambayo itakuwa ambayo itakuwa inahusisha mambo yote yanayohusu burudani, labda matibabu, ushauri, ajira kutafuta na mambo mengine mengi mengi, nafikiri tunaweza kabisa kujinyanyua zaidi kimaisha, au mnaonaje ndugu zangu?” Hivyo ndivyo alivyomaliza Victor na kuwaangalia kwa zamu mmoja mmoja.

Alivyofikisha jicho kwa Eve akamkonyeza, Eve akashindwa kujizuia, akacheka na kusema

“Victor mi sitaki utani, we haya tu!” Victor nae akamjibu

“Ah basi nisamehe mama Bill” kauli iliyofanya Lidya na Eve kucheka na Lidya kutikisa kichwa huku akisema kwamba Victor hawezekani.





Wote wakarejesha macho yao kwa Ommy aliekuwa akionekana kama yupo mbali sana kimawazo, Victor akamsemesha kwa kumuuliza vipi mbona yupo kimya?

“Ujue Victor mdogo wangu, ni kama mtu uliekuwa ndani ya mawazo yangu, wazo kama hilo hata name nilikuwa nalo siku nyingi, ila akili yangu ikashindwa kuishawishi nafsi yangu ikubaliane na wazo lile, hatimae nikaachana nalo. Leo wewe umelirudisha upya, sasa nambie, unafikiri tufanyeje?”

Walijadiliana kwa muda mrefu sana hadi usiku wa manane. Lidya alitoa wazo la kuinunua RM Classic na idara zake zote zilizo ndani yake, kwani ile tayari ina jina kubwa mjini, hawatopata tabu kuiweka sokoni kwenye mapambano.

“Tena itakuwa ni rahisi tu kuiboresha, maana kila mtu mjini anaijua, wazo zuri sana dada Lidya!” alichangia Eve. Ommy akatikisa kichwa kukataa huku akimuangalia Eve na kumwambia yeye anapinga wazo hilo, aliwaeleza kwamba wazo lile ni zuri lakini halina msaada kwao.

“Watatusumbua sana hasa baada ya kujua kuwa ni sisi ndio tunao itaka, wataipandisha sana thamani yake na hatimae itauzwa kwa bei kubwa, kwa sababu wao hawajatangaza kuiuza” walimuelewa ni nini alichokuwa akikimaanisha Ommy na kuanza upya mjadala.

Baada ya mjadala mrefu wakafikia muafaka kuwa, waanzishe kampuni yao wao wenyewe, na ile RM Classic ndio iwe ni kipimo chao. Yaani ifikie hatua waizidi kwa kila kitu, japo kampuni ile ni kubwa na kongwe kwenye burudani, ndani na nje ya mipaka ya nchi.

Yakabaki maswali matatu; Swali la kwanza likawa ni je kampuni iitweje? Swali la pili ni hili; makao makuu ya kampuni yawe wapi? Nairobi ama Dar? Kwa kuwa ulikuwa tayari ni usiku mnene na walikuwa wamechoka, wakaamua suala lile waliache kwa muda hadi ciku ya pili patakapokucha. Wakaagana na wakaelekea vyumbani kwao.

Siku ya Jumamosi asubuhi jijini Nairobi hali ilikuwa ni baridi kiasi, familia mbili za Kitanzania zikiwa ugenini zimeketi chumba cha chakula zikifungua kinywa. siku ya leo haikuwa sawa na siku mbili zilizopita ambazo zilikuwa ni siku za furaha, leo ilikuwa ni siku ya huzuni, kwani moja ya familia hizo ilikuwa ikiondoka kurejea nyumbani Tanzania.

Bill alikuwa mikononi mwa baba yake na Jamillah akiwa amesimama pembeni akimtazama Bill kwa jicho la tamaa ya kumbeba. Lidya akavunja ukimya kwa kusema;

"Mchana wa leo wapendwa mnaturudisha kwenye hali ya upweke. Pamoja na kukaa nanyi kwa muda mchache, lakini tumewazoea sana hadi kuhisi kama vile tupo Bongo"

"Dada Lidya usiseme, mie ninafikiri nitawakumbuka sana, na kabla sijaondoka ninaomba nitoe shukrani zangu za dhati kwenu na hasa Shem Ommy.. Nina washukuru sana ndugu zangu..." Ommy akamkatisha

"Aah Shem, hakuna shaka, nasi tunaweza kusema kwamba tunapaswa kuwashukuru zaidi nyie kwa kukubali kuitikia wito wetu wa wewe kuja kujifungulia huku, ni heshima kubwa sana mmetupa ya kujifungulia mtoto wenu wa kwanza mikononi mwetu..." Lidya akadakia

"..ni kweli Ommy, na hali wazazi wenu wote wapo, lakini mkakubali kuja huku, sasa ni nani anaepaswa kumshukuru zaidi mwenzie? Eve sisi ndio tunapaswa kusema Ahsanteni sana kwa kutuonesha kujali na kututhamini."

victor yeye alikuwa muda wote akiwa kimya anachezea vidole vya mtotowake, akasema

"Pamoja na yote hayo suala la kampuni hatujali kamilisha, ama mnataka tuliache kama lilivyo?" Lidya akasema kwa ushautri wake, Makao makuu yawe ni hukohuko Dar Es Salaam na pale Nairobi liwe ni tawi tu. Wazo lake likapita bila kupingwa.

Suala likabaki kuwa ni moja, je kampuni iitwaje? Eve akishauri kampuni iitwe majina ya watoto wao, yaani JB Entertainment, lakini hawakuafikiana juu ya hilo. maana wote walijua kuwa walikuwa bado wana nafasi ya kuongeza watoto wengine, sasa kwa nini yawe majina ya watoto wawili tu, wakaamua kutafuta jina lingine lisilo egamia upande wowote.

Wakiwa wameketi pamoja na kutafakari juu ya jina zuri, walianza kukata tamaa, Victor akapata mwanga, akasema ok. ok huku akiwatazama wenzake na kuwaambia

"Jamani sikilizeni, kuna jina moja linatufaa sana, mmelijua ni jina gani?" wote huku wakimtazama wakatikisa kichwa kukataa kuwa hawalijui jina hilo na kuonesha shauku ya kutaka kulijua. Victor akatoa kaamu mfukoni na Notebook kisha akaandika neno moja tu 'LOVE' na kuweka note book ikiwa wazi na kalamu pale mezani.

Wote kwa pamoja wakaliangalia neno lile na kulisoma kwa pamoja kama wameambiana vile, lakini hakuna alieweza kutegua kitendawili kile, Eve ndio akawa wa kwanza kuhoji

"Sasa mume wangu umemaanisha nini? mbona kama sielewi elewi hivi, hebu fafanua vizuri" Ommy alitikisa kichwa kumuunga mkono Eve, Victor akatabasamu na kusema huku akishika kalamu

"Unajua kuwa sisi hapa tunaongozwa na penzi? Na ndio maana tupo hapa, ni kwa sababu tu ya mapenzi baina yetu. Sasa kwa kuwa penzi ndio njia yetu, kampuni yetu pia tuipe jina hilo pia, ama kuna ushauri mwingine?" Akiongea Victor huku akimpa Eve mtoto, Ommy akajibu huku akiwatazama Eve na Lidya kwa zamu;

"Naweza kusema mie sijakubaliana na jina hilo pamoja na sababu ulizozitoa Victor. Suala hili si suala la kukurupuka, ninafikiri bado tuna muda mzuri tu wa kufikiria , leo ni Jumamosi nyie mnaondoka, hadi Jumatatu ndio tutaanza masuala ya usajili, hivyo tulivundike hili ili tukija kupata jina linakuwa ni jina muafaka" Kauli hii ya Ommy ilionekana kuungwa mkono na Eve na Lidya.

Upande wa Victor bado alikuwa hakuabaliani nao, alipinga vibaya na kusema

"Kaka Ommy nina sababu kuu 3 na hiyo mlio ikataa ni moja tu kati ya sababu nilizokuwa nazo, mbona hamjanipa nafasi ya kusikiliza hizo zingine?" Akacheka mwenyewe kuona kama vile wanambania, Eve aliekuwa akimnyonyesha mtoto wake, akamwambia mumewe





"Victor nae kwa ubishi tu, hajambo." Lidya akaingilia kati na kumtaka Victor aendelee

"Sasa nisikilizeni, sababu ya pili ni hii..." Victor hakuongea, bali alichuka kalamu na karatasi toka kwenye note book yake na kumwambia Lidya aandike herufi ya kwanza ya jina lake, kisha ampe Ommy ambae akiisha andika amrudishie yeye, nae atampa mkewe amalizie.

Ommy alifanya alivyotaka Victor kwa shingo upande ilimradi tu amridhishe. Kwa mshangao wa wote, jina lilelile la 'love' likarudi tena. Kwa pamoja wakapiga makofi tena bila kuambiwa na mtu. Nao wakaungana nae kukubali kuwa jina lile linafaa na linajitosheleza hata kabla hawajajua maana ya 3 ambayo ni ya mwisho.

"Naona sasa jina limepita bila kokoro, si ndio?" Aliuliza huku akiwa na tabasamu usoni, akiwatazama wote kwa zamu, Ommy akatikisa kichwa na kusema

"Bwana mdogo unatisha sana wewe, hebu fanya kumalizia tu hiyo maana ya mwisho"

"Ok! hii ya mwisho inataka umakini mkubwa sana ili mnielewe, twendeni pamoja sawa?" alisema huku akijiweka vizuri mezani na kufunua kurasa nyingine mpya na kuanza kuifafanua maana yake ya mwisho kwa kuwakumbusha wamepanga kuwa na kitengo cha maabara ya uchunguzi wa afya za binadamu, neno 'Labalatory' itasimama kama 'L'

"Kikazi itakuwa imemuwakilisha Lidya ambae alikuwa na fani ya unesi, pia kwa jina itakuwa inamuwakilisha Shemeji yangu Lidya, sijui tunaenda pamoja hapo?" Waliitika haraka haraka ili aendelee wote walikuwa na hamu sana ya kujua kila herufi ilikuwa na maana gani, aliwaona wakiwa makini sana kama vile wanamsikiliza mwalimu anae anza kufundisha topic mpya inayotoka kwenye mtihani.

Akaendelea kusema kuwa herufi 'O' inayochukua nafasi ya Ommy, itasimama kama 'Oppoturnity' kwani kutakuwa na kitengo kitakachohusika na kutafutia watu nafasi za masomo na kazi, akahoji kama anaeleweka?

Hakuna aliemjibu bali ile ishara ya kukuta watu wote wakimtazama, ilikuwa ni dalili tosha kuwa wanamsikiliza. kila mmoja alikuwa akimuangalia kijana yule ambae akili yake ilikuwa ikifanya kazi kwa kutumia mlango wa 6 wa fahamu, ambao anao yeye peke yake pale kundini.

"Najua wote mnatambua, Victor ni daktari bingwa aliesomea masomo ya 'Veterinary' anaumia sana kuona wanyama wakifa kwa magonjwa ambayo yanatibika, ndoto yake ni kuona hakuna mnyama hata mmoja ambae atakufa kwa ugonjwa mahala popote duniani yeye alipo," wakacheka kwa kauli yake na kumwambia aache kujifagilia.

"Nadhani imeeleweka kazi ya 'V' kwenye jina letu na hapa ndipo nilipopatikana mie." alikuwa akitabasamu huku bado akiwaangalia wote kwa zamu, lakini aliwakuta wao wakimuangalia kwa umakini kuliko yeye alivyokuwa akiwatazama.

Akajinyoosha na kuendelea huku akimtazama Eve

"Na herufi 'E' ambayo ni herufi ya kwanza ya jina la mpenzi wangu Evelyn, hii itawakilisha 'Entertainment' hapo siweki maneno mengi, kwani sote tunajua burudani kwetu ni nini, je kuna swali la ziada?" Kama walio ambiwa wakateremsha pumzi kwa pamoja, kukubali kuwa hawana swali

Ommy akamtazama Eve na kusema akiwa na tabasamu

"Shem kazi unayo, natamani Bill aje kukaa nami ili baadae nione, maana mama kichwa kinafanya kazi haraka sana wakati huohuo baba nae anafikiri mbali zaidi ya ilipo Mbingu, hongereni sana... Nami natamka rasmi, sina pingamizi, nanyoosha mikono kuonyesha amani" Kweli Ommy akanyoosha mikono.

Lidya akaondoka kuelelea jikoni kurekebisha chakula cha mchana, kwani siku ile ndege ilikuwa ikiondoka jioni. walikula na ilipotimu saa nane mchana wakatoka kuelekea Kenyatta International Airport. walipita madukani kununua vitu vidogo vya zawadi ndio wakaingia Airport ikiwa ni saa 9 mchana.

Saa 11 jioni waliondoka kurudi Bongo na kuiacha familia ya Ommy Bazzo ikiwa na majonzi kwa kubaki wapweke na kuzikumbuka siku 3 za furaha. Wakati wao wakiwaza hivyo, wenzao walikuwa wakiitafuta ilipo lami ya uwanja wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere.

*******

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Mwezi mmoja sasa umekatika tangu Victor aachane na ajira pale TMK Veterinary, japo wafanyakazi wenzie walisikitika sana kwa yeye kuacha kazi, lakini aliwaambia kwamba amezidiwa na majukumu, hivyo maombi yao hayakusababisha Victor abadili uamuzi wake.

Kile alichokisema Victor kilikuwa ni ukweli mtupu, alitakiwa afuatilie suala la usajili wa kampuni yao ya LOVE na wakati huohuo afuatilie bendi yao ya Classic kwa ukaribu, kwani walikuwa na mpango wa kuihamisha kutoka Classic group kuja katika kampuni yao ya LOVE

Hayo yote yalihitaji muda, muda huohuo pia alihitajika kazini kwake TMK Veterinary, akawa anashindwa kujigawa, hivyo ikamlazimu kuachia ngazi serikalini ili aweze kuiendesha kampuni yao ya LOVE kiufanisi na ubora alioutaka ili aweze kuendesha biashara zao.

Siku moja iliyopita, ndio ilikuwa siku ya mwisho ya likizo ya uzazi ya Evelyn, lakini kwa kuwa siku yenyewe ilikuwa ni siku ya Jumamosi, hakwenda kazini akapanga atakwenda siku ya Jumatatu kwenye kipindi chao na Victor cha Romantic. Usiku wa siku hiyo iliyokuwa ni jumapili, Victor aliendesha kipindi chao kama kawaida.

Mada ya siku hiyo ilikuwa ni ‘Love @ 1st sight’ yaani

‘Je unaweza kumpenda mtu kwa dhati ulipomuona kwa mara ya kwanza?’ hilo ndio swali ambalo lilikuwa la siku hiyo ya Jumapili. Wakati Victor akiwajibika huko Studio, huku nyumbani Eve alikuwa akimlaza mtoto wao.

Muziki laini ulikuwa ukiendelea taratibu huku Victor akipokea simu na ujumbe mfupi wa maneno toka kwa wasikilizaji, pia kwenye mitandao ya kijamii, wachangiaji walikuwa wanachangia kwa wingi. Ghafla akaingia Ondiek hadi Studio alipokuwa Victor. Alimsalimia na kuvuta kiti cha pili kisha akakaa.

Haikuwa kawaida kwa mtu kuingia studio bila ridhaa ya mwenye kipindi, Victor alimshangaa, Ondiek akatambua hilo, akamwambia Victor ameingia ili kuomba msaada wake

“Unajua Victor mara tu utokapo hapa, ninapaswa niingie mimi, sasa ninaomba unisaidie kitu kimoja…” Victor alimtazama Ondiek aliekuwa akiongea huku akimtazama yeye kwa jicho la kuomba msaada

“Nikusaidie nini Ondiek?”

“Victor, mke wangu ni mgonjwa, ningependa kuwa nae karibu, kwa sababu sina mtu mwingine nyumbani zaidi ya mama yake ambae alikuwa aingie leo jioni kutoka kwao huko Tabora na basi la HBS, lakini hadi sasa hajafika” Aliongea kwa msisitizo na kuendelea

“Nasikia wanaweza kuingia kati ya saa 6 na 7 usiku huu.” Alimaliza na kusubiri kudra za Victor





“Lakini Ondiek kujasema unataka msaada gani kwangu, ama nikuazime gari au labda pesa imekuishia kwa sasa? Hebu fanya kufunguka.” Alimuuliza huku akicheze vyombo vya muziki.

“Hapana wala si hivyo, Ninachoomba ni wewe kuendelea kuwepo hapa Studio ili kuendesha kipindi changu hadi saa nane nitakaporudi, ili niweze kumpokea mkwe wangu na kumpeleka nyumbani, kisha ndi nije hapa, nafikiri utakuwa umenielewa?”

“Kha! Hilo mbona ni suala dogo sana mtu wangu? Yaani kujipanga kote kule kumbe unaniomba kuwa una udhuru? Basi wala usikonde, nenda kampokee mzaa chema na pole sana kwa kuuguza.” Wakagonga 5 kama wafanyavyo marasta kisha Ondiek akatoka.

Victor akachukua simu na kumpigia mkewe Mama Bill ili kumtaarifu juu ya mabadiliko ya muda way eye kurejea nyumbani kutokana na dharula iliyojitokeza. Eve hakuipokea kwa furaha taarifa ile hadi pale Victor alipomueleza sababu ambazo ni za msingi ndio akaridhika na kumwambia kwamba yeye hatolala hadi muda ambao Victor atafika nyumbani.

Jibu likawa ni sawa, akamuulizia Bill, mkewe akamwambia mtoto tayari kalala, akambusu mkewe na kumwambia anampenda kisha akakata simu.

Baada ya hapo akachukua jagi la umeme na kuchemsha maji ili kutengeneza kahawa kwa ajili ya kiburudisho na kukata usingizi.

Dalili alizokuwa ameziona hazikuwa mzuri, aliamini kuwa iwapo ataendelea kuwa peke yake kama vile alivyo, basi usingizi utampitia. Wakati huohuo sms na ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, ilikuwa ni mingi sana, akaanza kuzisoma.

Zipo zilizosema kuwa hakuna mapenzi hapo bali kuna tamaa tu, wengine walisema hapo ndio kwenye penzi la kweli na baadhi walidiriki kusema kadri mlivyopendana kwa urahisi hivyo, basi na hata kuachana ni hivyo hivyo. Hayo ndio yalikuwa maoni ya wachangiaji na wasikilizaji wa kipindi kile.

Yasmin ambae ndio mke wa Ondiek hakuwa mgonjwa kama ambavyo Ondiek alimwambia Victor, bali alikuwa akitafuta nafasi ya kumuacha Victor pale studio kisha yeye aende nyumbani kwa Victor akiwa na uhakika kuwa Victor hawezi kutoka kazini, hivyo aliamini ataongea na Eve kwa uhakika wa kutokutokea mtu yeyote wa kumghasi.

Naam punde tu akawasili nyumbani kwa Victor. Akiwa nje ya nyumba akampigia simu Eve na kumuomba amfungulie mlango aingie ndani. Eve aligoma kabisa, lakini kwa kuwa Ondiek alibembeleza sana na kuahidi kuto kumsumbua, kwani hakuja kwa nia mbaya, Eve akamfungulia mlango na Ondiek akaelekea moja kwa moja Sitting room.

Ondiek alipoketi tu, Eve akaja na kumuuliza shida yake nini iliyomleta pale kwake usiku ule. Nae alimwambia kuwa sababu iliompeleka pale si nyingine bali ni kumuomba msamaha Eve kwa yote yale yaliyotokea siku za nyuma.

Eve akamwambia mbona tayari ameisha msamehe kitambo sana? Tena hata kabla hajamuomba msamaha, maana alijua kabisa kwamba huko alipo hata nae anajuta, hivyo alishamsamehe. Akamkosha zaidi pale alipomwambia kuwa tayari amemsamehe hadi kosa la leo la kumdanganya mumewe kipenzi.

Mshangao ulimpata Ondiek ambae alikuwa akidhani Eve hajui kuwa amemuaga Victor anakwenda kumpokea mkwewe Ubungo, akamwambia kuwa hata hilo kosa la uongo, yeye Eve ameisha msamehe kwa niaba ya mumewe.

Japo lile suala lilimshitua Ondiek, lakini hakutaka kuuonyesha mshituko wake dhahiri, lakini akasema tu kwamba sababu ya hayo yote ni yeye Eve. Eve alikuwa kimya akimtazama kama mdoli vile, hadi Ondiek akajishtukia mwenyewe, ndio akakumbuka kumshukuru kwa kumsamehe.

Lakini hata kabla jibu halijatoka, Ondiek papo hapo akamuomba warudiane tena na kuwa wapenzi kama awali. Eve akageuka mbogo, akakataa katakata na kutishia kumfukuza Ondiek, akamuuliza kwamba kwani hajui baada ya yeye kumtupa, alidakwa na mtu mwingine anaejua kutunza? Ondiek alikiri ni kweli, kisha akaongeza

“Natambua hilo Evelyn, lakini mapenzi yangu kwako yananisababisha nisahau kila kitu na nipo tayari kuwa hata mwizi juu ya penzi lako Eve” baada ya kauli ile, Eve alisonya na kunyanyuka kuelekea mlangoni, akasimama pale kwenye mlango wa sitting room na kumtaka Ondiek atoke nje haraka.

Huku akimuonesha ishara ya mlango mkubwa wa mbele kwa kidole cha shahada, Ondiek alimfuata Eve na kutaka kumkumbatia, Eve akamkwepa na kutazama kwa hasira. Ondiek alitabasamu na kumwambia Eve akiwa karibu yake kabisa, macho yakitazamana, akasema akumbuke waliyoyafanya wakiwa pamoja ndani ya penzi

“Hebu tafakari kipindi kile ulivyotoka wazazi wako na kukbali kwenda name hadi nyumbani kwetu Kenya kwa wazazi wangu, eti leo hii Eva umekuwa wa kunifukuza mie? Kwa kweli leo mimi sitoki humu ndani hadi kieleweke.” Alisema huku akirejea kuketi kwenye sofa.

Sio siri, Eve alitingwa na mawazo ya ghafla sana na kuanza kuvuta taswira tangu kipindi kile akiwa na Ondiek, ambae ndio alikuwa mpenzi wake wa kwanza. Akakumbuka jinsi ambavyo Ondiek alimuhadaa na kumtorosha kwao na kwenda hadi Jijini Nairobi. Huko walitembelea sehemu mbalimbali.

Kifupi walifurahi sana japo Eve alikuwa na hofu na wazazi wake pindi atakaporejea nyumbani. Kumbukumbu ile ikamfanya ashushe pumzi kwa nguvu, mwili ukamlegea na kujiegemeza ukutani, kichwa akkilaza katika bega lake la kulia ambalo ndio lililo egamia ukutani. Ondiek nae akasimama na kumfuata Eve pale aliposimama.

Alisogelea na kupiga magoti na kusema anaomba msamaha wa dhati na anajua kuwa ni yeye ndie aliekosea, akamshika magoti na huku akimtazama usoni

“Naomba urudishe moyo wako nyuma, nipe nafasi nyingine, naahidi sitakuumiza tena, niamini nisemayo…” huku Eve machozi yakimtoka, hata hayakueleweka yalikuwa ni ya furaha ma ni ya huzuni, akamnyanyua Ondiek na kumwambia amekubali lakini atoke nje.

Ondiek akapigwa na butwaa, alisimama huku akitazama chini na akiwa haamini kile alichokisikia, alikuwa akiwaza, huu ni msamaha ama ni maelewano ya aina gani? Alikuwa akitegemea msamaha kwa tabasamu, sasa alichokiona ni tofauti, akawa anajiuliza.. Nimesamehewa kwa chozi, hivi ni kweli nimesamehewa?





“Eve mimi nakwenda, lakini amini nitarudi siku nyingine, muda na wakati kama huu, tena kwa ajili hiihii, kwa heri mpenzi wangu.” Akamsogelea zaidi nae akarudi nyuma kidogo, lakini akajikuta kabanwa na ukuta na mlango, Ondiek akaweza kumbananisha vizuri na kumuweka mtu kati, akawa anajipindua pindua tu akiwa hana jinsi ya kujichomoa.

Alichokifanya Ondiek ni kumbusu kwenye paji la uso, akafungua mlango na kuondoka akimuacha Eve akifunga mlango kwa ghadhabu na kubaki akiwa amesimama pale pale kwa muda mrefu kidogo akivuta taswira ya mambo yale yanayo jitokeza katika maisha yake.

Tayari aliingiwa na kitu Fulani ambacho hata nae hakukijua ni kipi, yaani tu kifupi hakujielewa elewa, akajivuta na kuangalia saa ya ukutani, akaona imetimia saa nane kasoro robo, akajua muda si mrefu ujao, mumewe atawasili, akaenda kuoga na kukaa kumsubiri. Hakuchukua muda mrefu sana akawa amewasili.

Walikula chakula mezani bila Eve kuonyesha tofauti yoyote, alionekana yupo kawaida kabisa kumbe moyoni alikuwa na kitu ambacho kilikuwa kikimuumiza sana. Ilibaki kuwa ni siri yake moyoni, alitamani Lidya angekuwepo Bongo, huenda angemsaidia, sasa hakuwa na jinsi ila tu kupambana peke yake. Walimaliza kula wakaingia kulala, siku ikawa imeisha.

Siku zilikwenda mbio kweli, miezi nayo ilikatika, nusu mwaka baada ya kuzaliwa Bill, Eve na Victor walifunga ndoa ya hadhi ya kawaida kabisa, wakapanga kufanya sherehe kubwa sana wakati ambao Bill atakapokuwa akitimiza miaka miwili. Lakini walifanya sherehe ndogo tu iliyo hudhuriwa na watu wengi maarufu ambao walikuwa ni marafiki zao, walitoka hapa nchini na wengine walitoka nje ya nchi.

Kipindi hicho LOVE.Com ilikuwa ikizidi kujipatia umaarufu mkubwa na hivyo kupelekea Victor akiwa kama ndie mtendaji mkuu wa Kampuni akawa hatulii. Ikawa kila siku safari, leo hapa kesho kule, akitoka Dodoma, anaelekea Zanzibar, akirudi Kigoma anaenda Tanga mara yupo Mtwara wakati mwingine Ruvuma, hiyo ndio ikawa ni hali halisi.

Classic Band nayo ilizidi kufanya vizuri, sasa hii nayo ilisimamiwa na Victor kwa asilimia 100, hivyo karibu muda wote akawa yupo busy na kazi tu. Shughuli zile nyingi zikawa zinawapa nafasi Eve na Ondiek kukutana mara kwa mara na kujadiliana juu ya amapenzi yao pasina Victor kujua lolote.

Waliutumia muda ule vizuri sana, maana walifurahi na kulirudisha upya penzi lao la zamani. Walirejea kwenye penzi lao kwa kasi ya ajabu na kufikia hatua ya kujisahau kuwa Ondiek ni mume wa mtu na Evelyn ni mke wa mtu. Walianza kuwa wanajiachia popote wanapotaka, bila kujali muonekano kwa watu pindi Victor anapokuwa safarini.

Kwa mara ya kwanza, Eve aliekuwa hataki kabisa pombe, akaonja pombe kwa ushawishi wa Ondiek, taratibu akaanza funda moja hatimae chupa. Jambo la msingi tu ni kuwa hakuweza kabisa kumtelekeza mtoto wake, alimjali kupita kiasi.

Safari za Victor ziliendelea kama kawaida na sasa alikuwa akitoka hadi nje ya nchi. Tayari alikwenda Zambia, Malawi na Msumbiji, huko kote ilikuwa ni kuitangaza kampuni yao juu ya mambo inayodili nayo. Aliweza kutangaza vema, kwani kwa muda mchache wakawa wanapokea oda nyingi za madawa ya mifugo na pia bendi yao kutumbuiza kila sehemu.

Siku moja mwisho wa wiki, Ondiek na Eve wakiwa kwenye ukumbi wa Mango Garden, wakati Victor akiwa nje ya nchi kwa faida ya kampuni yao, mwandishi mmoja wa habari wa gazeti la uchunguzi liitwalo ‘HABARI ndio hiyo’ alikuwa akiwafuatilia kwa muda mrefu wapenzi wale wawili, alipata picha za matukio ambayo aliamini kama yatakaa ukurasa wa mbele wagazeti lao, basi siku hiyo gazeti lao litauza sana.

Akawafuata pale walipokaa ili kupata undani zaidi wa suala lile, walimfukuza na kumtukana matusi ya nguoni hasa ukizingatia walikuwa wamelewa chakari. Aliwabembeleza wamueleze kama habari ile ni uzushi ama ni kweli, hawakuwa tayari kuongea nae.

Asubuhi ya siku iliyofuata, gazeti la ‘HABARI ndio hiyo’ lilitoa habari ile ikiwa na kichwa cha habari ‘Kibopa wa Radio amtafuna mke wa Kibosile wa kampuni kubwa nchini’ Habari ndogondogo chini zikaendelea kusema ‘Inasadikiwa ni wapenzi tangu zamani’ kisha ikaandikwa ‘Kibosile yupo nje ya nchi’ mwisho kichwa kidogo cha habari kikaandikwa ‘Wahusika wagoma kuongea na mwandishi wetu.’ Hivyo ndivyo lilivyosomeka gzeti lile la ‘HABARI ndio hiyo’ la siku hiyo.

Picha ziliwekwa lakini sehemu kadhaa zikawekewa kivuli kwani hazikuwa na maadili ya Kitanzania. Kila alieliona gazeti lile alitamani sana kulisoma na kuwatambua wale watu ni kina nani. Mwandishi akaipanga habari ile kuwa ipo ukurasa wa pili.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Uzito wa habari ukafanya gazeti liuzike sana siku ile na ndio sababu hata Victor aliweza kulipata siku ileile japo alikuwa safarini nchini Kenya akitokea Uganda alipokuwa amekwenda kuweka mambo sawa ya kuhusu kampuni yao.

Alipokelewa uwanja wa ndege wa Kenya na familia ya Ommy, wakati akiwa anatoka, ndio akaliona gazeti la nyumbani tena la siku hiyohiyo, akavutika kulinunua bila kujua kilichomo ndani yake, kifupi alitamani tu kununua gazeti lile. Kwa kuwa alikuwa ana hamu sana ya kuongea na Jamillah, akachukua gazeti na kumpa Lidya.

Lidya ndio akawa ni mtu wa kwanza kuanza kulisoma gaeti lile. Tatizo kama ujuavyo, wanawake wanaposoma habari za udaku, wao huwa makini zaidi kuliko wanaume, hivyo Lidya alipoanza tu kulisoma, akapatwa na mshituko Fulani ambao Victor aliuona na kumuomba Lidya gazeti lile ili nae aone ni kipi kilicho mshitua.

Habari ile ilimvutia Victor, hadi wanafika nyumbani na kupaki gari, yeye alikuwa bado ameketi garini akisoma ile habari. Ajabu hakushughulishwa na picha hata kidogo. Ommy aliekuwa akifungua mlango ili ateremke, akamsemesha Victor

“Mzee shituka, tayari tumefika nyumban, naona gazeti limekuvutia hasa.” Victor nae sasa akanyanyua shingo huku akilikunja gazeti na kusema

“Unajua mambo haya ya nyumbani bhana, unaweza kukuta suala hili linakugusa, ngoja nipige simu niulize ni nani ntu huyu,” akawa anatoa simu mfukoni mwake. Lidya aliekuwa amehisi kitu Fulani pale kati, si kwamba alishtuka tu, bali pia alijibana tu, maana mkojo ulitaka kumpita mara baada ya kusikia Victor akiongea na simu na hasa mtu aliekuwa akiongea nae



 presha tupu

“Hellow Ondiek, mambo vipi?” ndugu yangu msomaji, sipendi kukupa jibu, ila hebu jiulize swali wewe mwenyewe, ni kiasi gani Ondiek alitapatapa mara tu baada ya kusikia sauti ya Victor? Sio siri aliogopa sana ila tu akajipa ujasiri wa kupokea na kujibu simu ile

“Poa tu Victor, habari za huko?” kwa woga ulioshindikana kujificha, Ondiek alijitahidi sana vile kuuliza, lakin nafsi haikumpa kabisa amani wala uwezo wa kuongea zaidi. Victor alihisi kama Ondiek ana wasiwasi Fulani hivi, akamuuliza

“Vipi Boss, mbona unaonekana kama vile una wasiwasi, ama ndio tayari umeisha haribu? Maana wewe unajulikana hahahaaaa!” alimalizia Victor kwa cheko, cheko ambayo kama Ondiek angekuwa hana shaka angeipokea kwa vurugu kwelikweli.

Lakini hebu tafakari hata wewe, japo Victor alikuwa akimtania Ondiek, lakini swali hilo lilimchanganya hata Lidya pia, ambae uzalendo ulimshinda na kumshika mkono mumewe na kumwambia waende ndani mara moja wakaongee, Ommy hakubisha, akamfuata mkewe.

“Ah! Kaka mie ndio nishaharibu home” hapo alijitutumua kweli Ondiek na kujibu lakini akiwa hajiamini hata kidogo, aliona kama anategwa vile. Victor akamwambia wala asijali, ni sehemu ya maisha yetu. Baada ya hapo ndio akamuuliza swali ambalo mimi ninaliona gumu sana iwapo tu ningeulizwa mie

“Ehe! Hivi ni nani alietoka leo kwenye gazeti la ‘HABARI ndio hiyo’ la leo?” mapigo ya moyo ya Ondiek yalitaka kuchana shati lile alilolivaa kwa woga, lakini kwa haraka akajiongeza na kujibu kuwa yeye bado hajaliona

“Umesema la leo si ndio? Ngoja nikalitafute, nipe muda, nitakujibu baadae, kwaheri!” alijibu haraka haraka na kukata simu.

Kitendo kile cha Ondiek kukata simu aliyopigiwa, kilimchanganya Victor, lakini akakumbuka kuwa awali aliisha mwambia kuwa kuna sehemu kaharibu, akajipa moyo kuwa huenda huko ndio kumesababisha Ondiek achanganyikiwe. Akaachana na habari ile, kisha nae akaelekea ndani walipo kina Ommy na Mkewe pamoja na mtoto wao.

Kule ndani Lidya alimuambia mumewe kuwa wale watu yeye anahisi ni Ondiek na Eve, Ommy alibisha na hatimae wakaamua kukata mzizi wafitina kwa kumpigia Eve

“Simu yangu hii hapa ina salio la kutosha, mpigie ili kuondoa utata.” Aliongea Ommy huku akimpa simu mkewe. Lidya alipiga na Eve aliiona, alishtuka sana kuona namba ya Ommy, alijiambia kama ingekuwa ni ya Lidya wala asinge jaribu kuipokea, lakini kwa sababu ilikuwa ni namba ya simu ya Ommy…

Akaipokea lakini pia alikua na shaka tele.

“Hellow Shem…”

“Umekariri namba eeh?” aliuliza Lidya na kumfanya Eve ashtuke, asiemtaka ndio aliepokea

“Ooh, kumbe ni wewe dada Lee, mambo?” alijitoa kimasomaso kwa kumsalimia

“Mmambo sio…” hapo ndio Lidya akamuulia kuhusu hisia walizo nazo juu yake na Ondiek. Eve alitaka kudanganya kwa kusema ile ni project wana andaa kwa ajili ya filamu ya Bongo movie ambayo itatoka siku za karibuni. Lidya akamuuliza kama Victor anajua.

Eve akapata kigugumizi, akathibitisha kabisa kuwa kile akisemacho ni uongo, Lidya akamwambia aache uongo anapaswa kuwa mkweli na asijaribu kuweka uongo wowote ule, kwani kama ni gazeti analo mkononi pale.

Alijuta kuwafahamu, akaamua kusema ukweli, akaona kabisa kusema uongo hakutasaidia, maana wale tu wa mbali kiasi kile wamesikia, itakuwaje? Akasema ‘Nimekwisha’ kwa sauti ambayo aliamini haisikiki, kumbe Lidya na hata Ommy waliisikia. Akaamua kuwa mkweli akiamini hamna njia yoyote ya mkato inayoweza kumsaidia zaidi ya kuwa mkweli, akahisi huenda ukweli ukamuokoa na kusababisha asamehewe.

Ukweli alio ueleza ulimkasirisha Lidya vibaya na akaanza kumshambulia kwa matusi makali mno na maneno mengi ya kejeli. Ajabu Eve akawa kimya mno. Kutokana na ukali wa maneno ya Lidya na sauti ya juu aliyotumia, ikamlazimu Ommy aingilie kati na kumzuia Lidya asiendelee kumshambulia Eve.

Lidya akaamua kumalizia hasira zake kwa kwa kumwambia

“Unasikia Eve, Victor ndio kaisha jua na unakumbuka maneno yangu niliyo kwambia wakati ulipokuwepo huku? Nilikueleza nini? Sasa sitaki unisumbue mimi wala mume wangu Ommy, unalo hilo. Kesho mumeo Victor anatua huko Bongo, nafikiri unatambua fika, mwenye kiranga haliliwi wala hawekewi matanga, kwaheri.”

Hata kabla Eve hajadumkiza neon lolote, Lidya akawa tayari kakata simu na kumgeukia mumewe na kumueleza jambo…

“Unajua Ommy, mimi ndio ninae mjua Eve vizuri kuliko yeyote, mara ya kwanza wakati alipokuwa na Ondiek mimi ndio nilikuwa ni mtu wake wa karibu sana na ndio mshauri wake…” Lidya akamueleza kila kitu hadi kufikia siku ile pale ndani walipokuwa wakiongea Eve na Ondiek kwa simu.

Yeye aliyasikia yote yaliyosemwa na kumwambia Eve kuwa iwapo itatokea siku ambayo yeye Eve atarudiasha mahusiano na Ondiek, basi asimsemeshe tena, Ommy akaingilia kati

“We vipi? Sasa ndio hautasema nae kwa ajili ya penzi lake yeye mwenyewe?” alimuuliza kwa mshangao kutokana na kauli ile aliyoitoa Lidya, kwa msisitizo, Lidya akaongeza

“Hayo ndio makubaliano yetu na hakuna wa kuyabadilisha, maana tulikuwa sisi wawili tu.” Alijibu Lidya akionekana dhahiri hajafurahishwa kabisa na kitendo kile cha Eve alicho kifanya.

Mazungumzo yao wakayakatisha ghafla mara tu Victor alipoingia ndani. Wakamuuliza Ondiek amesemaje? Nae akawajibu kama alivyo ambiwa na Ondiek, kisha wakajitayarisha na kuelekea katikati ya Jiji (City Center).

Baada ya maongezi kati ya Victor na Ondiek, Ondiek alijipa moyo kwamba Victor hajajua lolote, akajipa moyo kuwa huenda habari ile inaweza kusomwa bila mtu kuielewa, akalishika gazeti na kuanza kulisoma upya, hasa habari ile.

Alipomaliza kuisoma habari ile kwa mara nyingine, kuna wazo likamjia kichwani mwake, akawaza kwamba ‘Sio huyu jamaa kaisha jua kuwa ni mimi lakini sasa ameamua kunitega? Na kama mejua sijui itakuwaje upande wangu! Je Eve atalichukuliaje?’ kwa mara nyingine tena Ondiek akajipa moyo kuwa liwalo na liwe.







Nafsi yake iliongea peke yake, ilimuamisha kuwa Victor ni mwanaume kama yeye, kama vipi watapambana. Akaamua kumpigia simu Eve kumuuliza juu ya Victor kama kaisha jua na pia alitaka kumueleza kile alichoongea nae. Hapo ndio zahma ilipozuka, Eve alimlaumu sana Ondiek kwa kudai ndie aliemponza. Akakata simu na kuanza kulia.

Kilikuwa ni kilio cha majuto, hasa akikumbuka maneno ya Lidya ndio alijikuta akipoteza kaabisa kujiamini na kilio kikaongezeka. Ondiek nae akalilkuswanya lile gazeti kwa hasira, kisha akaingia ndani kwa ajili ya kujitayarisha ili akasome taarifa ya habari ya mchana wa siku ile ambayo alipanga kuisoma yeye mwenyewe.

Siku ile alijikuta akikosea sana japo inatambulika kuwa yeye ndio bingwa wa kusoma Taarifa ya Habari, lakini siku ile alikuwa akiomba radhi kila mara kutokana na kukosea kosea kwake mara kwa mara, akili yake haikuwa sawa kabisa.

Usiku uliwadia, muda ambao Eve alitakiwa awepo Studio, lakini ikashindikana ikamlazimu aombe ruhusa. Mtu mwenyewe wa kumuomnba ruhusa ndio huyo huyo Ondiek. Alipompigia simu tu na kumueleza hivyo, Ondiek alimgomea na kumwambia anatakiwa aende ili wakae na kuongea, Eve akagoma na kuzima simu.

Wafanyakazi wengi wa Classic FM tayari walikuwa wameisha jua kilichokuwa kikiendelea. Hali hiyo ambayo Ondiek aliekuwepo kazini aliweza kuiona mapema, ilichangia sana kuwapa hali ngumu kutokana na kuvuja kwa habari ile.

Watu wote walikuwa wakitambua tangu awali kuwa Eve na Ondiek walikuwa ni wapenzi, lakini walikuja kutengana kwa matusi na kashfa kibao, sasa kilichowashangaza ni hali ya kurudiana Eve na Ondiek mara tu baada ya Eve kuolewa.

Usiku ule baada ya kugoma kwenda kazini alikuwa akilia peke yake nyumbani huku akimtazama mwanae Bill, usingizi ulipotea kabisa siku ile, alishindwa kabisa kulala. Akawasha simu baada ya kugundua kuwa Studio tayari kipindi kinaendeshwa na mtu mwingine. Ilipowaka tu, mtu wa kwanza kupiga akawa ni mumewe.

Simu ile kwa siku ile haikumfurahisha, kila siku alipokuwa akiiona simu ya Victor, alikuwa na furaha na alitamani kuongea nae hadi asubuhi, lakini siku ile simu ile ilimchanganya sana, laiti ingekuwa ni ya mtu mwingine wala asingepokea, lakini ya Victor ilikuwa ni lazima apokee.

“Hellow! Mume wangu…” Walisalimiana, lakini Eve alikuwa hayupo katika hali ya kawaida na hata alipoulizwa na Victor alikuwa akijibu kimkato, maana alikuwa akilia na pia hakuonesha kabisa kujiamini, wasiwasi ulimtawala, tayari kichwani mwake aliisha athirika kisaikolojia, alitambua kuwa Victor ameisha jua kila kitu.

Sasa nae akapata ujasiri na kuamua liwalo na liwe, akapanga kama ataulizwa jambo lolote na Victor kuhusu suala lile, atadanganya vyovyote vile ilimradi aweke mambo sawa. Lakini Victor aliweza kuona tofauti hizo na ikamlazimu kuhoji

“Mpenzi leo haupo sawa, kwanini? Una tatizo gani? Ama unaumwa?” maswali yalikuwa ni mengi tena yaliulizwa kwa mfululizo, na sababu kubwa ni mapenzi makubwa ya Victor kwa mkewe Mama Bill, hata hivyo alikana kuwa haumwi ila tu anasumbuliwa na upweke.

“Baby wala usijali, mimi kesho ninafika hapo, tutakuwa pamoja, hivyo huo ugonjwa utapona tu, sawa mama Bill?”

Japo alikuwa na taarifa juu ya kurejea kwa Victor siku ile ifuatayo, lakini moyo wake ulishituka sana kwa kusikia toka kinywani mwake mwenyewe kwamba anafika kesho, akaitikia akiwa kapoteza kabisa ujasiri.

“Sawa Mpen… Sawa Victor,” Hali ile ikazidi kumchanganya Victor na kumuuliza tena;

"Eve una nini leo? Mbona sio kawaida yako? Niambie mke wangu, ni nini tatizo lako. Hivi usiponiambia mimi utamwambia nani? Please mama Bill..." Pamoja na Victor kubembeleza kote kule, lakini bado Eve alishikilia msimamo wake uleule kwamba hana tataizo lolote linalo msumbua zaidi ya mafua.

kisha sasa ndio akaaamua kumpoteza kwa kumuuliza kwa sauti ya upole

"Ninaona tutaongea zaidi ukisha fika nyumbani, kwani unatarajia kuondoka saa ngapi huko?"

"Nafikiri itakuwa ni mchana maana ntaraji kutua hapo Dar muda wa alasiri na hata chakula cha nyumbani natarajia kuja kula hapohapo nyumbani mke wangu, si unajua nime kimiss sana chakula unacho pika wewe?" Alijua atamfurahisha mkewe, kumbe angejua hata asingesema

"Sawa..." aliitika kifupi huku akimuomba Victor akate simu ili alale, maana amechoka sana. Lakini Victor ndio akazidisha maswali

"Subiri kwanza mke wangu, sijakuuliza kuhusu mwanangu, vipi hajambo?" Kwa swali hilo, Eve akamuangalia mwanae Bill aliekuwa amelala na kutamani kulia kwa sauti, ila akajizuia na kujibu

"Hajambo na tayari amelala kitambo!"

"Ok! Usisahau kuja nae Airport kesho, sawa mpenzi wangu wa ukweli?" nafsi ilikuwa ikimsuta, lakini hakuwa na jinsi zaidi ya kuitika

"Poa Victor, bye!" Akalazimisha kuaga

"Miss U Eve..." Victor alijilazimisha tu kukubali, lakini wala hakuwa na nia ya kuaga muda ule

"Me too!" Majibu ya Eve siku ile yalikuwa ni mafupi yakiwa ni yale ya kupoteza matumaini.

Mwisho wa maongezi yale, ukawa ndio mwanzo wa usiku mrefu wa machungu sana kwa Eve. Giza lote la usiku ule lilimshuhudia Eve akilia kwa majonzi na majuto hadi kufikia muda wa alfajiri, ndio usingizi ukampitia. Hakushtuka hadi aliposikia sauti ya Bill akilia wakati akioshwa na msaidizi wao, ikiwa ni karibu saa 3 asubuhi.

Eve alipofungua mlango kwa nia ya kutoka nje kuangalia mazingira, msichana wake wa kazi aitwae Sarah nae akaingia ndani ili kuchukua nguo za Bill kwa ajili ya kumvalisha mara tu baada ya kumaliza kumuogesha. Alimsalimia bosi wake na kuendelea na kazi zake kama kawaida, Eve nae baada ya kuelekea kule uwani, akarejea chumbani kwake.

Chumbani kitu cha kwanza kukifanya ni kufungua kabati ya nguo na kuziangalia kwa majonzi nguo zake. Majonzi yalimtawala mno kwani tayari kichwani alikuwa na maamuzi magumu, naam ni lazima niyaite ni maamuzi magumu, aliamua kujikata mwenyewe kabla ya kukatwa, hivyo akawa ameamua kuondoka nyumbani kwake.

Mwenyewe aliisha ona hawezi tena kuishi na Victor kwa kuzingatia kuwa ni yeye Victor ndio alie sababisha hayo yote kutokana na usaliti wake, roho ilimsuta. Kachukua begi kubwa la kutosha nguo zake na za Bill kwa kiasi kiasi, akaongeza na vitu vyake ambavyo aliona ni muhimu hawezi kuwa mbali navyo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Huku akilia moyoni na machozi yakimtoka kimya kimya bila kelele, alitoka na kwenda kule uwani alipo msaidizi wake na kumkuta bado akimvalisha Bill huku wakicheza. Aliweza kabisa kuiona furaha waliokuwa nayo Sarah na Bill walivyokuwa wakicheza, walionekana kabisa kuwa wameelewana sana japo Sarah hakuwa na muda mrefu tangu wamuajiri.

Akawasogelea na kumwambia Sarah kuwa anampa siku 3 za mapumziko ya kazi, aende nyumbani kwao muda ule ule na arudi baada ya siku 3 kwani mumewe hayupo na hizi siku 3 zote yeye atakuwa yupo busy sana na mambo ya kazi, hivyo yeye pale hatokuwa na kazi za kufanya na hata leo anatoka mapema sana mle ndani.

Sarah akamchukua Bill na kumpeleka ndani huku akiwa na furaha tele kwa kupata nafasi ya kwenda nyumbani kwao kuwaona watu wa kwao na pia kutaka kuwaonyesha vitu vingi ambavyo alikuwa amepewa na Eve, zikiwemo nguo. Baada ya muda aliaga na kuondoka.









ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog