IMEANDIKWA NA : HUSSEIN ISSA TUWA
*********************************************************************************
Simulizi : Miss Tanzania
Sehemu Ya Kwanza (1)
Kijiji kidogo wilayani Tarime, mkoa wa Mara, miaka 19 iliyopita…
Mwanamama aliyekuwa amebeba mtoto mchanga kifuani alikuwa akikimbia kwa taabu na mashaka makubwa. Alikuwa ametapakaa damu mwili mzima, na alikuwa akipiga kelele za kuomba msaada bila ya kujali au kufahamu kuwa hakukuwa na mtu yeyote wa kumsaidia usiku ule, kwani hakika kila mmoja alikuwa katika mashaka mazito.
Kijiji chote kile cha jamii yake ya wakulima, ambacho kwa kawaida muda kama ule huwa kinakuwa kimya na kilichogubikwa kiza kizito, kilikuwa kikirindima kwa mayowe ya ghadhabu, vilio vya woga na miguno ya uchungu.
Baadhi ya nyumba zilizoezekwa kwa makuti zilizotapakaa pale kijijini zilikuwa zikiwaka…zimechomwa…moto, na mioto ile ilitupa mwanga mkubwa kila upande na kukifuta kabisa kiza ambacho kwa kawaida huwa kimekigubika kijiji kile muda kama ule, na kuzidisha joto la woga lililotanda kijijini pale.
Ni balaa…usiku wa balaa! Balaa kubwa!
Kama kwamba naye alijua kuwa hali haikuwa ya amani hata kidogo pale kijijini, mtoto mchanga aliyekuwa mikononi mwa yule mama naye alikuwa akilia kwa sauti. Mama yake aliyekuwa na wiki zipatazo tatu tu tangu ajifungue,alikuwa taabani sio tu kwa kipigo na majeraha yaliyotokana na mapanga na marungu, bali pia kwa kukimbia umbali mrefu na kuishiwa nguvu kutokana na kutokwa damu nyingi.
Ni vita! Vita kubwa…
Kelele za watu wenye jazba zilikuwa zikirindima masikioni mwake, na kadiri zilivyokuwa zikirindima, ndivyo alivyozidi kujilazimisha na kujisukuma mbele ili azidi kujiweka mbali na watu wale waliopandwa jazba na mori wa kumwaga damu.
“Nyamaza mwanangu…Nyamaza! Mama atakuokoa tu mwanangu…Mungu atatusaidia!” Mwanamama alisema kwa sauti ya chini huku akikimbia kwa kuyumbayumba, akianguka na kujiinua tena, akimkinga mwanae asidhurike na kuanguka kwake.Nyuma yake, mayowe ya jazba na ghadhabu pamoja na vilio vya uchungu na kuomboleza vilisikika kutoka kila kona.
“Eee Mungu wetu wa mbinguni…ni nini tena hiki umetuletea…?” Mama mtoto alibwabwaja huku akizidi kukimbia kujiweka mbali na mapambano yale yaliyomkuta nyumbani kwake bila hadhari yoyote na kumlazimisha kukimbia kuokoa maisha yake na ya mwanae.Watu wenye ghadhabu walivamia nyumba yao na kumshambulia vibaya kwa mapanga na marungu, kabla mumewe hajajiingiza katikati ya kundi la wale wavamizi kumtetea huku akimpigia kelele akimbie na mtoto kutoka eneo lile.
Lakini hakuweza.
Alibaki akipiga kelele kutaka msaada wakati mumewe akiendelea kushambuliwa kwa mapanga, na hakuweza kukimbia hadi alipomshuhudia mumewe akikata roho ndipo alipozinduka na kuanza kukimbia huku akilia ovyo.
Ni machafuko! Machafuko makubwa…
Wanakijiji wa kijiji cha jirani, ambao walikuwa ni kutoka jamii ya wafugaji, walikuwa wamevamia kijiji kile cha jamii yake ya wakulima, wakiwashutumu kwa kusababisha vifo vya ng’ombe zao kwa kuwawekea sumu kwenye bwawa la kunyweshea maji. Sababu kubwa iliyodaiwa na wafugaji wale ni kwamba wanajamii ya wakulima walikuwa wanataka kulipiza kisasi kwa wafugaji baada ya ng’ombe wao kuvamia shamba la mmoja wa wanakijiji wale wa jamii ya wakulima na kusababisha hasara kubwa.
Ujinga ulioje jamani!
Ni kweli ng’ombe wengi wa wafugaji wale walikufa kwa mpigo, wengi wakiharisha vibaya na kutoa malenda-lenda yasiyoeleweka vinywani, lakini ni kweli kuwa wakulima waliwawekea sumu? Nani anajua hilo? Je haiwezi kuwa ni ugonjwa tu wa mlipuko uliowavamia wanyama wale?
Mazungumzo ya kistaarabu hayakupewa fursa hata chembe. Ni jazba ya kisasi tu ndiyo iliyotawala, na ndipo kwa ghadhabu wanakijiji wa jamii ya wafugaji walipovamia kijiji cha wakulima na kuanza kupita nyumba hadi nyumba kutafuta mtu aliyefanya kitendo kile kisichosameheka kabisa kwao, na kila aliyeleta upinzani alikumbana na ghadhabu zilizopindukia uwezo wa fikra.
Wakulima walipoamua kujitetea, ndipo vita na machafuko vilipoibuka na kupamba moto kwa kasi. Ikawa kila mwanakijiji wa jamii ya wakulima anamshambulia mwanakijiji kutoka kwenye ile jamii ya wafugaji wenye jazba, na kila mfugaji anamshambulia mkulima.
“Kamata yule! Shenzi kabisa…ua!” Kundi la wafugaji wenye mapanga lilimuona yule mama asiye na silaha wala hatia aliyekuwa akijaribu kuokoa maisha yake na ya mwanae mchanga.
Mbio!
Mama mtoto alitimua mbio kwa kadiri alivyoweza, wafugaji wakimfuata mbio huku wakimpigia kelele za ghadhabu. Mama alijitosa katikati ya vichaka kando ya njia ya miguu aliyokuwa akikimbilia, vichaka ambavyo viliibukia kwenye msitu mnene. Adui zake walizidi kumfukuza huku wakilia kwa mori. Nguvu zilimuishia mama mtoto, hakuwa na uwezo wa kuendelea kukimbia zaidi. Damu iliyomtapakaa mwilini ilimlevya vibaya sana na alihisi akipoteza fahamu.
Oh, Mungu wangu…hivi ndio unaniacha nauawa hivi hivi kweli?
Alijitupa chini ya mti mkubwa na kujibanza nyuma ya shina la mti ule, akimlaza mwanae kando yake pale chini. Alimtazama kwa kuchanganyikiwa yule mwanae aliyekuwa amefungwa kipande cha khanga tu, na ambaye alikuwa akilia kwa kelele. Kwa namna ile hakuna namna yoyote ya kujificha bila ya wale wafugaji wenye jazba kumkurupusha kutokana na vilio vya yule mtoto.
Alimuacha yule mtoto pale chini ya mti huku akibubujikwa machozi na kukimbia kwenda kujibanza kichakani hatua kadhaa kutoka pale alipokuwapo, mkononi sasa akiwa amekamata jiwe kubwa kwa ajili ya kujitetea pindi ikibidi.Alisikia vishindo vya adui zake vikielekea usawa wa kule vilipokuwa vikitokea vilio vya mwanae.
“Yuko huku mbwa mkubwa huyu!” Mmoja wao alibwata kwa hamaki.
“Ah, limemuacha mtoto lenyewe limekimbia bwana, unaona mijanamke ya kikulima hii?” Mwingine alimaka kwa hasira. Mama alifinya macho na kuuma midomo kwa uchungu, moyo ukimdunda, akisubiri kuona ni nini wataamua wale watu wenye ghadhabu.Alibaki akichungulia kule walipokuwako wale watu wenye jazba, jasho lililochanganyika na damu likimtiririka, moyo ukimdunda kwa nguvu.
“Tukachinje tu haka katoto!”
Moyo ulimlipuka mwanamama, na alianza kujinua kutoka pale alipokuwa amejibanza huku lile jiwe kubwa likiwa mkononi mwake.
“Acha! Huyu mtoto anajua nini wewe…? Tukaache tu katakuja kuliwa na fisi sasa hivi!”
Mama alishusha pumzi za shukrani na kurudi tena kujibanza pale chini.
Ghafla, kutokea kule kwenye ule ujia wa miguu alipokuwa akikimbilia muda mfupi tu uliopita, vilisikika vilio vya mwanamke mwingine aliyekuwa akikimbia huku akilia kuomba msaada. Wale watu wenye silaha walikurupuka kwa pamoja bila hata ya kushauriana, na kukimbilia kule ilipokuwa ikitokea ile sauti, wakiamini kuwa ndiye yule mama wa yule mtoto waliyekuwa wakimkibiza, na kumuacha yule mtoto pale pale chini ya mti.
Mama mtoto aliinua mikono juu kumshukuru Mungu, na kuinuka taratibu, akisikia mayowe ya yule mwanamke mwenzake aliyetiwa mbaroni na wale watu waliokuwa wakimkimbiza yeye muda mfupi tu uliopita.
“Ee Mungu nisamehe kiumbe wako…sina uwezo wa kumsaidia masikini…!” Alisema kwa huzuni huku akimkumbatia mwanaye kwa nguvu, machozi yakimbubujika.
“Twende mwanangu…twende tu…Mungu atatuongoza…” Hatimaye alisema kwa sauti iliyotoka kwa taabu, akihisi maumivu makali tumboni. Alipeleka mkono sehemu ile na kuhisi unyevu wa vuguvugu.
Hakuhitaji taa kujua kuwa ule unyevunyevu ulikuwa ni damu iliyotokana na jeraha baya aliloachiwa na panga la mmoja wa wale watu waliokuja kuwashambulia kule nyumbani kwao kabla hajaanza kukimbia na mwanae.
“Oh, Mungu wangu…tusaidie tafadahali…”
Kwa taabu yule mama alianza kuelekea ndani zaidi ya ule msitu, akijua kuwa kama akifanikiwa kuumaliza msitu ule, angetokea mtoni, na kama angefanikiwa kuuvuka mto ule, angetokea kijiji kingine.
Labda huko angeweza kupata msaada…kama ataendelea kuwa akiwa hai.
***
Mtawa Marietta alishitushwa kutoka usingizini na kishindo kilichosikika kutokea nje ya nyumba yake ndogo. Aliinuka kwa taabu na kuketi kitandani akiwa amelaza kichwa upande mmoja, akijaribu kusikiliza kwa makini iwapo alikuwa amesikia sawa sawa kishindo kile au ni njozi tu za usiku.
Mara alisikia sauti nyingine. Hii haikuwa ya kishindo, bali ni kama ya kitu kigumu kikikwaruza matete ya mlango wa nyumba.
Kwaarrr…..kwaaaarrr…..kwaaarrr!!!
“Mnh! Ni nini tena hicho saa hizi?” Mtawa Marietta alijisemea mwenyewe huku akiinuka kwa taabu kutoka kitandani na kukiendea kibatari kilichokuwa kikitupa mwanga hafifu mle ndani kutokea kwenye kona moja ya chumba kile.
Kwaarrr…ngo, ngo! Kwaarrrr…ngo…ngo…ngo….!
Mtawa Marietta aliguna na kuisukuma miguu yake iliyochoka kwa uzee kuelekea mlangoni, sasa akiwa na hakika kabisa kuwa mikwaruzo na vishindo vile vilikuwa vikitokea nje ya kile kile kibanda chake, na hata pale alipokuwa akizidisha mwendo kuelekea mlangoni, alihisi kusikia na sauti ya mtu..mtoto…ikilia sambamba na vishindo na mikwaruzo ile.
Udadisi mkubwa ulimjaa, na moyoni mwake alishapata hisia kuwa jambo lolote lililosababisha mikwaruzo na vilio vile alivyokuwa akivisikia nje ya nyumba yake usiku mzito kama ule, halikuwa jema.
“Hili ni tatizo tu…! Sasa kwa nini bwana aliye mbinguni ameamua kuniletea mimi, mtawa mzee nisiye na nguvu wala jamaa, tatizo hili ni yeye mwenyewe ndiye ajuaye…” Alizidi kujisemea mwenyewe huku akijaribu kuchungulia nje ya nyumba yake kupitia kwenye mianya ya mlango wake wa matete.
Kiza tu huko nje.
“Ni nani yuko hapo?” Aliita kwa sauti yake iliyochoka, na kubaki akisikiliza kwa muda. Kutokea kule nje hakusikia chochote! Kote kulikuwa kimya kabisa!
“Jamani! Nina hakika kabisa nimesikia…” Mtawa Marietta alianza kujisemea kwa kuchanganyikiwa, lakini kabla hajamaliza alikatishwa na kilio kikali kabisa cha mtoto mchanga kilichomjia wazi wazi kutokea kule nje.
“Ah, Mungu wangu…kuna malaika wako huko nje…!” Mtawa Marietta aliropoka na kuufungua ule mlango kabla ya kutoka nje, kibatari chake kikiwa mkononi. Upepo mkali wa kule nje ulitishia kukizima kabisa kibatari kile, naye akainama kwa taabu na kukiweka ndani ya nyumba yake pembeni ya mlango. Haraka kadiri alivyoweza alijikongoja kuelekea kule kilipokuwa kikitokea kile kilio cha mtoto mchanga, lakini ghafla alijikuta akijikwaa kwenye kitu kama gogo na kuanguka mpaka chini.
“Eh, Mungu wangu uliye mbinguni…ni nii tena hiki kimekaa hapa…??” Mtawa alijisemea peke yake huku akijizoazoa na kupapasa kile kitu kilichomkwaa.
Hakikuwa kitu, bali ni mtu!
Aliachia mguno wa mshangao. “Hah! Ni nani wewe…? Mbona umelala hapa…” Aliuliza huku akimpapasa yule mtu aliyelala pale chini, na ni hapo ndipo alipogundua kuwa yule mtu aliyelala hatua chache kutoka pale mlangoni kwake alikuwa ni mwanamke…na alikuwa amesharudisha roho yake kwa muumba wake. Mtawa Marietta alifanya ishara ya msalaba na kuinuka kwa taabu. Hatua chache kutoka pale ulipolala ule mwili wa yule mwanamke aliyekutwa na umauti wakati akijaribu kumgongea mtawa yule kuomba msaada, alikuwa amelazwamtoto mchanga aliyekuwa akilia kwa sauti.
Mtawa Marietta alimuendea yule mtoto,akamuinua kwa upole na kumtazama kwa makini.
“Eee mungu wangu…kwa nini umeniletea malaika wako huyu wakati ukijua kuwa mimi mwenyewe sijiwezi kwa lolote?”Aliinua uso wake mbinguni na kulalamika kwa sauti ya chini. Hakika bwana aliye mbinguni hakuwa na jibu lolote kwake muda ule. Mtawa Marietta alifumba macho na kusoma sala ya kumuomba msamaha bwana wake aliye mbinguni, kisha taratibu akaingia ndani mwake na yule mtoto. Alimlaza kitandani yule mtoto ambaye sasa alikuwa ameacha kulia na kubaki akimkodolea macho malaika yule huku akili ikimzunguka.
Afanyaje sasa? Nje kuna mwili wa mwanamke asiyemjua, bila shaka ndiye mama wa yule mtoto, na mikononi ameachiwa mtoto mchanga asiyeweza hata kujieleza. Naye hajawahi kulea mtoto hata siku moja maishani mwake!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hakika Mtawa Marietta alikuwa kwenye wakati mgumu sana. Alibaki akimtazama yule kiumbe aliyelala pale kitandani kwake kwa muda mrefu sana, na hatimaye alipitisha uamuzi pekee alioona muafaka katika mazingira yale.
“Ee Mungu baba…sasa itakubidi unisamehe tu mola wangu, kwani itanibidi nitoke nikatafute msaada kwa wanakijiji…na nitawezaje kupata msaada huo nikiwa nimejitawia tu humu ndani? Nisamehe bwana wangu…nisamehe kwa jina la mama yetu Bikira Maria aliyetukuka!” Mtawa Marietta alizoea kuongea na mungu wake kama kwamba anaongea na mtu anayeonana naye uso kwa uso, tena kwa sauti. Akiwa na yule mtoto mikononi, alitoka nje ya nyumba yake iliyojitenga na nyumba za wanakijiji wengine, na kuelekea usawa nyumba ya mwenyekiti wa kijiji kile.
Mtaa wa Aggrey,Kariakoo, Jijini Dar es Salaam – Wakati uliopo:
Binti wa urembo namba tatu Afrika Mashariki wa mwaka 79 aliyependa na aliyezoeleka kutambulika kwa jina moja tu la Bishkuku, alikuwa amefura kwa hasira wakati akitazama pilika pilika za jiji zilizokuwa zikiendelea nje ya nyumba ya msajili iliyokuwa eneo lile lenye harakati lukuki jijini Dar. Akiwa katika ghorofa ya nne ya jengo lile la msajili, aliweza kuona eneo kubwa sana la jiji, lakini yote aliyoyaona kule nje hayakuleta maana yoyote akilini mwake, na hayakuleta maana kutokana na ukweli kwamba akili yake ilikuwa ikichambua jambo moja tu wakati ule.
Lakini kadiri alivyozidi kulichambua ili angalau limuingie akilini, ndivyo jambo lile lilivyozidi kuivuruga akili yake!
Jambo lililokuwa likimvuruga akili asubuhi ile lilikuwa nyuma yake wakati ule, ameligeuzia mgongo, na lilikuwa likijidhihisha katika namna ya binti mmoja mrembo na mwenye uelewa wa hali ya juu, ambaye alikuwa anafanya jambo lisiloendana kabisa na uelewa wake.Na kwa sababu hiyo Bishkuku alikuwa amechukia vibaya sana.
Alitoa sauti ya kukereka na kutupa mikono yake hewani huku akigeuka kutoka pale dirishani na kumtazama yule binti aliyeketi kwa pozi ya kuvutia kwenye moja ya makochi yake pale sebuleni.
“Tunis…! Kwa nini lakini Tunis, eenh?” Alimuuliza kwa hasira iliyofungamana na kushangazwa na hicho ambacho yule kiumbe mwenye urembo wa sura na maumbile aliyekuwa pamoja naye mle ndani alikuwa anataka kukifanya.
“Ah…Si nd’o ka’a hivyo n’livyokwambia Bishkuku…?” Tunisizye Mwakabaga, au “Tunis”, kama jinsi ambavyo warembo wenzake walivyozoea na kupenda kumwita, alimjibu huku akibadili mkao pale kwenye kochi, na akimtazama kwa macho ya pozi.
“Khah! Eti ‘Si nd’o ka’a hivyo n’livyokwambia Bishkuku…’,” Bishkuku alimuigiza yule binti huku akibana pua yake kwa vidole vyake na kuifanya sauti yake itoke kwa wembamba uliozidishwa na kubanwa zile pua huku akimtikisia kichwa yule binti, kisha akaacha kuibana ile pua na kuendelea kwa sauti yake ya kawaida, “…hivi we’ unataka kunifanya mi’ majinuni eenh?”
“Sio hivyo bwana…”
“Nani bwana’ako hapa? Yaani mi’ nikutoe kusikojulikana mpaka nikufikishe hapo ulipo halafu unakuja kuniambia eti …,” akabana tena pua yake na kuigiza sauti nyembamba na ya deko ya yule binti, ‘…nimepata mdhamini mwingine!’” akaacha kuibana ile pua yake na kuendelea kwa sauti yake ya kawaida, “…mdhamini mwingine? (akasonya) Ye’ huyo mdhamini mwingine alikuwa wapi wakati mi’ nakutoa huko machokoani na kukupa mafunzo na kukugharamia mpaka leo unaonekana mrembo miongoni mwa warembo hapa mjini, eenh?”
Tunis alibetua midomo yake kwa kiburi na kugeukia pembeni.“Mi’ hukunitoa machokoani bwana!”
“Mi’ s’o bwana’ako wewe…umesikia hiyo?Alla!”
“Sasa kwani ni nini lakini anti Bishi jamani…!” Tunis alilalama huku akimtazama kwa macho ya huzuni yule mwanamama aliyekuwa mbele yake mle ndani.Bishkuku alimtazama kwa muda yule msichana ambaye sasa alikuwa akimuona kuwa ni mjinga kuliko alivyotarajia na msaliti kuliko Yuda.
“Ina maana huelewi ni nini kinachotokea hapa Tunis?” Alimuuliza kwa sauti iliyojaa utulivu wa kulazimisha, kwani hakika utulivu ulikuwa ni mgumu sana kwake muda ule. Tunis alimtazama, kisha akamjibu huku akiinamisha chini kichwa chake.“Wewe hunimiliki mimi kama paka wako wa ndani bwana…mi’ n’na uhuru wa kufanya maamuzi ninayoona kuwa ni ya msingi kwa maisha yangu, Anti Bishi!”
Na hata wakati akisema maneno yale, paka mnene wa Bishkuku, mwenye mkia wenye manyoya mengi ya kupendeza aliyekuwa amejilaza kivivu kwenye kochi jingine pale sebuleni alipiga mwayo na kuunguruma kidogo, kama kwamba alikuwa akimlaumu yule binti kwa aidha kumtaja kwenye mjadala wao usiomhusu, au kwa kumtolea majibu ya jeuri yule bosi wake.
“Maamuzi unayoona Tunis? Au maamuzi unayoshawishiwa kuyaona na huyo “mdhamini” uliyempata…?” Bishkuku alimuuliza kwa jazba, na hapo hapo, kabla Tunis hajajibu, aliunganisha kwa swali jingine, “Na huyo mdhamini mwenyewe ni nani khaswa, enh?”
“I doesn’t matter Bishi…mi’ nimeshafanya maamuzi na nimeshakubaliana naye. Hapa nimekuja kukupa taarifa tu.”
Bishkuku alitikisa kichwa kwa kuchanganyikiwa.
“Na unadhani kuwa huyo…huyo…mdhamini uliyempata…atakuwezesha kutwaa taji la u-miss hapa nchini!” Halikuwa swali, bali ilikuwa ni kauli iliyodhihirisha wazi kuwa yule binti alikuwa akijidanganya.
“Sio hapa nchini tu Bishi…hata u-miss wa dunia! Huyu mtu ana pesa na uwezo wa kutosha…inatakiwa nawe ufurahie maendeleo yangu anti Bishi, lakini kama hutaki kuniunga mkono sawa tu. Mi’ nimeshakubaliana naye na hapa nimekuja kukuaga rasmi…”
“Lakini sio haki namna hii binti! Sio baada ya muda, nguvu na gharama nilizopoteza kwako Tunis…na definitely sio wakati huu ambapo mashindano ya Miss Tanzania tuliyokuwa tukijandaa nayo siku zote hizo yako miezi mitano tu mbele!” Bishkuku alisema kwa hamasa kubwa, huku akimsogelea yule binti na kumshika mabega na akimtazama usoni kwa macho ya kuomboleza.
“Gharama zako atakurejeshea…” Tunis alisema, na hapo hapo alianza kupekua mkoba wake aliokuwa ameupakata juu ya mapaja yake ya mviringo.
“Khah!” Bishkuku alimaka, “sasa atawezaje kunirejeshea gharama zangu? Vipi na muda niliopoteza? Vipi na ujuzi wangu niliokupatia…mafunzo niliyokupa? Navyo atarejesha? Kivipi khaswa, hebu nijuze tafadhali kisura wangu.”
Tunis alitoa hawala ya fedha kutoka kwenye ulemkoba wake na kumkabidhi. “Ameniagiza nikuletee hii cheki kufidia gharama zako zote…” Alimwambia huku akimtazama. Jicho alilokutana nalo lilimfanya ainamishe macho yake pasina kupenda, huku bado akiwa amemnyooshea ule mkono uliokamata ile hawala ya fedha.
Bishkuku alishusha macho yake na kuitazama ile hawala ya fedha iliyokuwa mkononi kwa yule binti, lakini hakufanya bidii yoyote kuipokea. Alimtazama yule msichana kwa dharau kubwa huku akiwa amebetua midomo.
“Milioni mbili!” Alisema kwa kutoamini, “ yaani nawe unaamini kabisa kuwa thamani yako ni milioni mbili? Unajiuza sasa Tunisizye? Huyo mdhamini wako sijui, mfadhili wako…anakununua kutoka kwangu kwa milioni mbili?” Alimuuliza kwa uchungu na dharau.
“Anti Bishi!” Tunis alimaka kwa uchungu, “yaani unaniambia mi’ najiuza kweli?” Alimuuliza kwa sauti iliyoonesha kuumia.
“Bado nina jingine la kukwambia mrembo…” Bishkuku alimjibu kwa hasira, “…hutafika mbali katika fani hii mwanangu. Sio kwa mfumo huu uliouanzisha…na utakuja kunikumbuka sana baadaye!”
Tunis alimtazama kwa huzuni, alitaka kusema kitu akakosa la kusema. Akabaki akimkodolea macho ya aibu huku machozi yakimlenga, na ile hawala ya fedha bado ikiwa mkononi mwake.
“Sasa toka nyumbani kwangu bi mdogo.” Bishkuku alimwambia huku akimtazama kwa macho makavu, “Toka…! Ondoka na nisikuone tena ndani ya nyumba yangu, mwana mjaa laana usiye na hata chembe ya shukurani we!”
“Anti Bishi…”
“Tena ondoka na hicho kijicheki chako, sina shida na vijisenti vyenu. Kamwambie huyo mrubuni wako kuwa amefanya kosa kubwa sana kuniingilia kwenye anga zangu!”
“Ah, jamani anti Bishi…sasa…”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“TOKAAAA!” Bishkuku alifoka kwa sauti huku akiwa amemtolea macho ya ghadhabu. Tunis na yule paka mnene wa Bishkuku waliruka kwa pamoja kutoka kwenye makochi waliyokuwa wamekalia, paka akitoa mlio wa woga na kukimbilia jikoni, ilhali Tunis akibweka kama mbwa aliyeshtushwa ghafla wakati akijisaidia, na kutoka mbio hadi mlangoni, ambako alisimama kibwege akiwa ameshikilia mkoba wake kwa mkono mmoja, na ile hawala ya fedha kwa mkono mwingine. Alibaki akimtazama yule mkufunzi na mfadhili wake mkubwa kwa macho yaliyojaa woga na kutatizika kukubwa kabisa, midomo ikimcheza.
“Hebu n’tokee mimi hapa wewe!” Bishkuku alimfokea tena huku macho yakiwa yamemuwiva na kupiga hatua kumfuata pale alipokuwa amesimama. Yowe jingine la woga lilimchomoka Tunis huku akigeuka na kutoka mbio nje ya sebule na nyumba ile, akiitupa chini ile hawala ya fedha.
Dakika tano baadaye, Bishkuku alimuona yule binti mrefu akitoka kwa mwendo wa haraka nje ya jengo lile alilokuwa akiishi, na kwenda moja kwa moja hadi kwenye gari moja la kifahari lililokuwa limeegeshwa upande wa pili wa barabara mbele ya jengo lile. Nje ya gari lile alikuwa amesimama mwanadada mmoja mwenye asili ya ushombe-shombe aliyekuwa amevaa mavazi ya kileo.
Kutokea dirishani kwake kule ghorofani, Bishkuku alimuona yule mwanadada akimkumbatia Tunis na kumhoji kitu fulani, kisha akainua uso wake kutazama kule juu ambapo dirisha la Bishkuku lilikuwepo.
Ah,kumbe ni huyu…huyu ndiye mdhamini mpya wa Tunis!
Bishkuku alimfahamu fika yule mwanadada aliyekuwa na Tunis kule chini, na kama yeye ndiye huyo mdhamini wake mpya, basi hakika alikuwa na fedha ya kutosha.
Lakini u-miss haupatikani kwa fedha Tunis!
Kule chini, yule mwanadada shombe-shombe aligeuka na kumfungulia mlango wa gari Tunis ambaye aliingia, kisha naye akazunguka na kuingia upande wa dereva na lile gari likaondoka eneo lile.Bishkuku alibaki akikodoa macho kutazama kule chini, huku akitiririkwa na machozi ya fadhaa…
***
Alibaki akiwa amesimama pale nyuma ya dirisha lake kwa dakika zipatazo kumi zaidi, sasa akili yake haikuwa ikimzunguka tena, bali ilikuwa imeganda…isiwe na muongozo wowote juu ya hatua gani ifuate baada ya usaliti ule wa Tunis. Ni baada ya dakika zile zipatazo kumi alizobaki akiwa amesimama pale nyuma ya dirisha lakendipo hatimaye alipojizindua na kupangusa machozi yaliyokuwa yakimbubujika bila hata ya yeye kujitambua.
“Mtoto mjinga sana yule!” Alijisemea peke yake, kisha akasonya huku akirudi na kuketi kwenye moja ya makochi ya pale sebuleni.
“Yaani baada ya maandalizi yote niliyofanya kwake! Na mafunzo niliyompa…! Anathubutu kweli kunitosa namna hii mimi? Tena katika dakika za mwisho-mwisho kiasi hiki?” Alizidi kujisemea peke yake, safari hii ikiwa ni kwa hasira zaidi kuliko fadhaa.Mara paka wake mnene alirudi pale sebuleni na kumrukia mapajani huku akitoa sauti za deko.
“Haya nini tena na wewe? Unataka kunitosa pia? Eenh?” Alimsemesha yule paka wake huku akimpapasa kichwani. Paka alitoa milio ya kuliwazwa na mipapaso ya mmiliki wake huku akifumba macho. “Yaa, hata mimi najua kuwa huwezi kunitosa rafiki yangu…” Alimjibisha yule paka huku akili yake ikiwa mbali kimawazo, na akiendelea kumpapasa kichwani paka wake mtiifu.
Lazima nitafute ufumbuzi juu ya swala hili…lazima niingize binti kwenye mashindano ya Miss Tanzania mwaka huu…lazima! Hii ni nadhiri yangu…na ni lazima niitimize! Tunis alikuwa tegemeo kubwa sana kwangu lakini sasa…Dah!
Mara alipata wazo. Aliinuka kutoka kwenye lile kochi, akimsahau paka aliyekuwa amejikunyata mapajani mwake, na hivyo kumuangusha huku paka naye akitoa mlio wa kulalamikia kitendo kile.
Alichukua simu yake na kuanza kupiga namba ya mtu ambaye alijua angeweza kumsaidia katika tatizo lile.Simu yake ilikuwa haipatikani!
“Aaaargh…Sheeeeyiiit! Mambo gani tena haya sasa…? Ah!” Alibwata kwa kuchanganyikiwa huku akiruka juu na kutupa mikono yake hewani. Paka aliachia mlio wa woga huku akitimua mbio na kupotelea jikoni.
“Na we’ acha woga wa kijinga bwana, ebbo!” Alimfokea yule paka wake ambaye tayari alikuwa ameshapotelea chini ya uvungu wa moja ya makabati yaliyokuwa kule jikoni. Bishkuku alijibweteka kwenye kochi kwa hasira.
Wakati Bishkuku akibishana na Tunis, Mwalimu Kokos Wandiba, p.a.k.(pia akijulikana kama) “Ticha”, tayari alishakuwa katika ari mbaya sana siku ile. Akiwa ni mwanasheria kijana wa kujitegemea aliyenyang’anywa kibali cha kufanya kazi ile ya uwakili mahala popote nchini na baraza la sheria la taifa, wakili Kokos alijikuta akirejea katika fani ile ya ualimu, ambayo pia aliisomea na kuifanya kabla ya kuingia kwenye fani ya uanasheria, kama njia tu ya kujipatia pesa za kujikimu. Lakini kitendo cha mkuu wa shule ile binafsi alipokuwa akifundisha masomo ya kiingereza na historia kumtaka atoe maelezo ya kina juu ya mambo yaliyo nje ya uwezo wake, kilimkera sana.
Eti ajieleze ni kwa nini wanafunzi wengi wamefeli kwenye masomo yake katika mtihani wa taifa wa majaribio, au mock, kidato cha pili! Tena atoe maelezo yale kwa maandishi na ayawasilishe kwa mkuu yule wa shule kabla ya muda wa kwenda nyumbani siku ile ile!
Ebbo!
“Hivi huyu anadhani mi’ ni mwalimu wa kubabaisha eenh? Mitoto yenyewe mitundu kama nini! Haielewi na wala haitaki kueleweshwa…kazi kutongozana tu darasani bloody fools! Halafu eti mi’ nitoe maelezo kwa nini wamefeli!” Kokos alijisemea huku akiwa amejikunja mezani kwake kwenye ofisi ya waalimu akiandika “maelezo” aliyotakiwa kuyawasilisha kwa yule mkuuwa shule mjinga.
Akilini mwake alikumbuka majibizano yaliyopitikana baina yake na yulemkuu wa shule majinuni.
“Hivi unaelewa lakini kama mimi nimekaa na wanafunzi hawa kwa miezi minne tu kabla hawajafanya mtihani wa taifa?” Alimuuliza yulemkuu wa shule, ambaye alikuwa ni mama mmoja mnene sana na mwenye kuvaa nguo zisizompendeza siku zote. Yule mama alimbetulia midomo, “Kwa hiyo…?”
Kokos alimtazama kwa mshangao, kisha akaamua kumkumbusha zaidi, “Na pia unakumbuka kuwa kabla ya mimi kuanza kuwafundisha hawa watoto, tayari walikuwa wameshakaa bila mwalimu wa historia wala kiingereza kwa miezi mingine mitatu?”
“Hivyo vyote ni visingizio tu vya kuziba utendaji wako mbovu na uwezo wako duni mwalimu!”
“Uwezo duni…? Uwezo wangu duni mimi…?”
“We’ ulijua kabisa kuwa watoto wale hawakuwa na walimu wa masomo hayo kwa muda mrefu, na bado ulikubali kuwafundisha na kutuchaji mshahara mkubwa…”
“Anha! Kwa hiyo tatizo hapa ni mshahara mnaonilipa, sio?”
“…sasa leo umetufelishia watoto! Nataka maelezo ya kina, tena nataka maelezo haraka sana…by close of business today, mwalimu, ama sivyo…” Mkuu wa shule alifoka kwa hasira. Kokos naye akaja juu.
“Ama sivyo nini mama, eenh? Ama sivyo nini?” Alimuuliza huku akimtolea macho.
“Maelezo by close of business today mwalimu! Huu mjadala umekwisha!” Mkuu wa shule alimkatisha kwa ukali, na Kokos alitoka mle ofisini akiwa amefura kwa hasira.
“Mwalimu…”
Kokos alishtushwa kutoka kwenye kumbukumbu ile na kuinua uso wake kumtazama yule mwanafunzi aliyemsimamia mbele yake pale ofisini.
“Nini…?” Alimuuliza, kalamu yake ikielea juu ya ile karatasi aliyokuwa akiiandika hapo awali.
“Mu…muda wa kipindi umefika mwalimu…” Mwanafunzi alimwambia huku akimtazama kwa woga. Kokos alimkodolea macho yule mwanafunzi.
“Kipindi gani?”
“Historia mwalimu…”
“Kwa hiyo…?”
“Ah, nimekuja kukukumbusha tu mwalimu…dakika kumi zimeshapita…”
Kokos alimtazama yule mwanafunzi kama kwamba alikuwa mwehu, kisha akazungusha macho yake na kuona kuwa walimu wengine waliokuwamo mle ofisini nao walikuwa wakifuatilia mjadala ule.
“Sasa wewe ndio umekuja kunikumbusha…ukiwa kama nani?” Alimgeukia yule mwanafunzi na kumuuliza kwa utulivu, akiweka kalamu yake juu ya ile karatasi iliyokuwa mbele yake, huku akijiegemeza vizuri kitinina akifumbata mikono kifuani kwake.
“Amm, mi’ nd’o kaka wa darasa mwalimu…class monitor…”
“Ooow, class monitor…” Kokos alisema huku akitikisa kichwa taratibu kuonesha kuwa alikuwa ameelewa, na kuendelea, “…kwa hiyo, umekuja kunikumbusha kutokana na kuujua sana wajibu wako kama class monitor, au kwa kuwa wenzako wamekutuma…?”
“Ah, wameniagiza nije kukuita mwalimu…” Kaka wa darasa alijibu. Mwalimu Kokos alitikisa tena kichwa taratibu kuashiria kuzidi kuelewa yale maelezo ya yule mwanafunzi, akabaki kimya kwa muda akiwa ameinamisha kichwa chake, kisha akainua uso na kumtazama moja kwa moja usoni yule mwanafunzi na kumueleza kwa ufasaha sana ili kuhakikisha kuwa maneno yake yanaeleweka vizuri sana kwa yule mwanafunzi, na kwa wale walimu wenzake waliokuwa wakifuatilia ule mjadala pale ofisini.
“Sasa nakwambia hivi, wewe mwenyewe kwanza (akamtukania mama yake)…,” Jicho lilimtoka pima yule mwanafunzi, walimu wakiachia miguno ya mshangao na kutoamini mle ofisini.
Kokos akaendelea kwa utulivu na kwa ufasaha ule ule, “…na hao wanafunzi wenzako waliokutuma nao pia (akawatukania mama zao)…,na huyo mkuu wenu wa shule naye pia (akamtukania mama yake)!Sasa TOKA MBELE YA USO WANGU NYAU WEE!!!”
Mwanafunzi alitoka mbio mle ofisini, akiparamia meza mbili mle ofisini, kabla ya kuufikia mlango na kutoweka.
Kokos aliwageukia walimu wenzake mle ofisini waliobaki wakimkodolea macho ya kutoamini, ilhali wengine wakiwa vinywa wazi.
“What?” Aliwauliza huku akiwatazama mmoja baada ya mwingine, “Na nyi’ mnataka niwape zenu?” Aliwauliza.
Walimu wote pale ofisini wakainamia meza zao, kila mmoja akiwa bize kuandika anayoyajua wenyewe.
“Good!” Kokos alisema na kumalizia kusaini ile karatasi aliyokuwa akiiandika kabla ya ujio wa yule mwanafunzi.
Alikusanya vitu vyake vichache na kutoka nje ya ofisi ile, akiiacha ile barua yake ya kuacha kazi ndani ya saa ishirini na nne pale mezani, ikiwa imekandamizwa na mashine nzito ya kutobolea karatasi.
***
Siku ile ile, maeneo ya manzese ndani ya jiji la Dar es Salaam, binti mmoja alikuwa katika wakati mgumu sana maishani mwake. Si kwamba ile ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kujikuta katika wakati mgumu, la hasha. Alishakuwa kwenye nyakati ngumu mara kadhaa kabla ya hapo, ila hili lililokuwa likimkabili safari hii lilikuwa la aina yake. Ugumu wa jambo lililokuwa likimkabili wakati ule, ulimfanya awe amejiinamia akiwa ameketi juu ya kitanda kidogo na kichafu, akili ikimzunguka.
“Sasa ndio itakuwaje…ndio au hapana?” Binti mwingine aliyekuwa pamoja naye mle ndani ya chumba kile kidogo cha kupanga alimuuliza kwa nongwa. Huyu alikuwa amesimama mbele yae huku ameegemea ukuta wa kile chumba, mikono yake akiwa ameifumbata kifuani, na mwilini akiwa hana nguo hata moja.
“Mi’ siwezi bwana!” Binti alimjibu yule mwenzake huku bado akiwa amejiinamia.Kwa jibu lile, yule binti mwingine alipiga makofi mara moja kwa viganja vya mikono yake na kuhamishia uzito wa mwili wake kutoka mguu mmoja kwenda mwingine huku akijishika kiuno.
“Sasa hapo ndipo utakapokuwa kwenye tatizo kubwa sana shoga, kwa sababu itakubidi uweze tu ndugu yangu…vinginevyo utafute uelekeo, upo?”
“Lakini mi’ sijawahi kufanya mambo hayo Jackie…sipendi kwanza!” Binti wa kwanza alizidi kupinga.
Cheko ya bezo ilimtoka yule binti aliyeitwa Jackie, ambaye alikuwa mwembamba na mrefu, na mwenye sura iliyoonesha ukomavu wa kimaisha kuliko umri wake halisi.
“Kwa taarifa yako hakuna anayefanya mambo haya kwa kupenda bibi, upo? Ni ugumu wa maisha tu mdogo wangu. Sasa kama mi’ najiuza na naweza kumudu maisha yangu na kukuhifadhi na wewe kwa siku mbili tatu hizi, kwa nini na wewe usiingie sokoni ukaanza kujikimu mwenyewe? Kwanza we’ una sura nzuri sana, shepu yako bomba kweli kweli, muonekano wako ni baab kubwa! Kwa nini uendelee kuninyonya kama kupe wakati una kila rasilimali ya kukuweka matawi ya juu hapa jijini, eenh?” Yule binti asiye nguo alimwambia mwenzake.
“Najua kuwa maisha ni magumu Jackie, lakini mi’ siwezi…” Binti alizidi kujitetea.
“Candy sikiliza eenh! Tena sikiliza vizuri bibi wewe…mi’ nimeshaweka mambo hadharani upo? Aidha uchukue kilicho chako utafute uelekeo, au leo jioni tutoke sote kuelekea viwanja. Uamuzi ni wako. Sasa hebu nipishe mi’ nilale huko!” Jackie alisema huku akijilaza pale kitandani na kumsukuma yule binti asiyejua mambo kwa mguu wake.
Kwa unyonge yule binti aliyeitwa Candy alijisogeza pembeni kumpa nafasi, kisha akaendelea kukaa kwenye pembe ya kitanda kile ilhali bado amejiinamia.Muda si muda, alimsikia Jackie, ambaye ndiyo alikuwa amerudi asubuhi ile kutoka “viwanja” alipokesha usiku kucha, akikoroma kwa usingizi mzito.
Alimtazama yule mwanadada aliyelala akiwa uchi wa mnyama kwa muda mrefu, na mwili ukamsisimka alipojifikiria na yeye kuwa katika hali kama ile.
Alianza kulia…
***
Kokos Wandiba alikuwa ameshalewa kiasi cha kutosha, na kadiri alivyozidi kumfikiria yule mama mwenye sura iliyokosa mvuto aliyepachikwa cheo cha mkuu wa shule ndivyo alivyozidi kubugia kinywaji. Hali ile haikusaidiwa kabisa na kitendo cha akili yake kuendelea kumrudisha katika wakati alipokuwa akiitumia fani yake ya uanasheria na jinsi ambavyo alivyoweza kuwaweka watu kama lile jimama linene livaalo nguo zisizompendeza, mahala panapowastahili.
Na kadiri alivyoikumbuka enzi hiyo iliyozimika ghafla mwaka mmoja uliopita, ndivyo alivyozidi kujisokomeza kilevi.
Baada ya kutoka pale shuleni mchanaule alielekea moja kwa moja kwenye ile baa aliyoizoea na kuanza kukata ulabu huku akitafakari mporomoko wa mfumo mzima wa maisha yake. Mara simu yake ilianza kuita, na alipobaini kuwa ilikuwa ni namba ya yule mkuu wa ile shule aliyokwisha ifuta kutoka kwenye sehemu ya maisha yake, aliizima ile simu na kurudia kushambulia kilevi kwa ari, kasi na nguvu mpya. Kutokea hapo alipoteza kabisa kumbukumbu ya muda, na pale alipokumbuka kutazama saa yake tayari ilikuwa imetimia saa moja jioni.
“Unajua nini faza…?” Alimwambia kilevi yule muuza vinywaji pale kaunta.
“Sijui nini Ticha…hebu nijulishe nini basi!” Yule muuza vinywaji, ambaye alimfahamu vizuri, alimjibu kwa maskhara huku akimcheka jinsi alivyolewa.
“Wweeery good! Basi subiri nikujulishe…” Kokos alimwambia kilevi huku akicheka kibwege, “…ni kwamba sasa nahitaji kujipatia kimwana kimoja matata sana, unasikia bwana? Na hapo siku yangu itakuwa imekamilika kabbb…bisa!” Kokos alisema kilevi huku akipigapiga uso wa ile kaunta kwa kiganja cha mkono wake.
Yule jamaa wa kaunta alimcheka.
“Haya na ukishampata huyo kimwana mmoja matata sana unamfanya nini, Ticha?”
Sasa ilikuwa zamu ya Kokos kumcheka. “Unauliza majibu eenh…?” Alimwambia huku akiweka pesa juu ya ile kaunta na kuanza kuondoka huku akiyumbayumba kidogo.
“Oyaa, subiri chenji yako basi!” Jamaa wa kaunta alimpigia kelele.
“Keep the change, kimwana!”
Nje ya ile baa aliingia kwenye gari lake aina ya Suzuki Escudo, likiwa ni matunda ya kile kipindi alichokuwa akiitumia ile fani yake ya uanasheria kama wakili wa kujitegemea, na kupiga stati huku mbwewe za kilevi zikimtoka.
Sifa moja ya Kokos Wandiba ni kwamba huwa halewi kiasi cha kushindwa kuendesha gari, au kiasi cha kupotea nyumbani kwake, hivyoaliliingiza barabarani lile gari na kushika uelekeo wa nyumbani kwake Mbezi Beach, akichukua njia ya kinondoni makaburini kutokea pale kwenye ile baa iliyokuwa katikati ya jiji…
***
***
Jackie alimtazama Candy kwa jicho la kuchuja lilichokuwa likikiona, na kutikisa kichwa kuafiki kile alichokiona. “Hapo uko bomba mwanangu…yaani si mchezo!” Alimwambia huku akimpandisha juu kijisketi kifupi cha jeans alichokuwa amemvika, ambacho Candy alikuwa akikivuta chini kila dakika.
Walikuwa “viwanja”, na Candy alikuwa amevaa nywele za bandia kichwani kwake na uso wake ulikuwa umekolea poda na nakshi za kilimbwende, midomo yake ikiwa imekolezwa rangi nyekundu, ilhali machoni alikuwa amepaka wanja kwa mtindo wa ki-misri. Hakika alionekana mrembo maradufu, na moyo wake ulikuwa ukimpiga kuliko ulivyowahi kumpiga maishani mwake.
“Acha kushusha hiyo sketi sasa bwana, we’ vipi? Lazima uoneshe mapaja yakohayo ili uvutie wateja!” Jackie alimkemea.
“Ah, lakini mi’ sitaweza mambo haya Jackie…sijawahi!” Candy alilalama huku akiivuta tena chini ile sketi.
“Tulishamaliza mjadala huo Candy…na kumbuka, ukiwa viwanja wewe sio Candy tena…wewe ni Judy, okay? Na…lazima uhakikishe kuwa kondomu inatumika, si unazo kwenye pochi yako humo?”
“Ndiyo, lakini…”
“Good, hakuna cha lakini tena hapo. Kondomu ni muhimu, bado hujafikia kiwango cha kwenda kavu-kavu wewe! Na kama n’livyokwambia…nitajitahidi twende pamoja kwenye kazi yako ya kwanza, lakini kama mteja akikataa itabidi tuachane, kila mmoja awe kivyake…tutakutana maskani.” Jackie alimwambia kwa msisitizo, na muda huo gari moja lilisimama kando ya barabara na kupiga honi. Haraka Jackie alimshika Candy mkono na kumvuta huku akilikimbilia lile gari, wakiwashinda akina dada poa wengine wawili waliokuwa wakijaribu kuliwahi.Aliinama kishawishi na kuegesha viwiko vya mikono yake kwenye kingo ya dirisha la lile gari na kumchungulia dereva.
“Hello lover boy, unataka raha?” Alimuuliza yule dereva kwa sauti ya kuchombeza huku bado akiwa amemkamata Candy kwa mkono wake mmoja. Candy alikuwa akimtupia jicho la woga yule dereva huku akigeuka huku na huko, moyo ukimwenda mbio. Kokos Wandiba alimtazama Jackie na hakuvutiwa na alichokiona.
“Raha naitaka, tena usiku kucha…lakini sio na wewe. Hebu msogeze huyo mwenzako naye nimuone vizuri!” Kokos alimjibu kilevi, akimtupia Jackieharufu ya pombe kutoka kinywani mwake. Jackie alifinya uso na kupunga kiganja chake mbele ya pua yake.
“Ai! Mtu mwenyewe umelewa hivyo? Basi tutakuja sote wawili…mi’ na mwenzangu na tutakupa raha mpaka uchanganyikiwe…ushawahi kupewa mapigo ya chuma mboga we? Basi twende tukakupe mambolover boy!Elfu thelathini tu mpaka majogoo, unasemaje?”
“Toka ‘uko! Elfu thelathini unaniuzia nini? Mi’ sitaki wawili…hebu msogeze huyo mwenzio kwanza naye nimuone…” Kokos alimwambia.
Jackie alimvuta Candy pale dirishani. “Judy hebu msalimie mteja wetu basi, ana hamu ya kukusalimu huyo…! Na anataraji raha usiku kucha…”
“Shhk…sh’kamoo!” Candy aliamkia kwa woga. Jackie alimfinya kwenye makalio kwa nguvu. “Aaah, sasa shikamoo ndio salamu gani tena maeneo haya na wewe?” Alimnong’oneza kwa hasira. Kokos aliinamia upande wa lile dirisha ili amuone vizuri zaidi yule dada poa wa pili.
“Ewaaa! Wewe ndiye haswa ninayekutaka…ingia twende mtoto…” Alisema huku akimfungulia mlango. Uso ulimsawajika Candy na akamgeukia Jackie kwa woga, akimtazama kwa macho ya kuomboleza.
Haraka Jackie alimvutia pembeni kabla hajasema neno lolote la kuharibu biashara.
“Sikiliza wewe! Huyu jamaa kalewa, kwa hiyo hatokupa tabu…mwepesi sana huyu, na bila shaka hataweza kufanya lolote. We’ mchezee-chezee tu kama nilivyokuonesha kule nyumbani mpaka alale. Cha msingi ukifika tu dai pesa yako kabisa, asubuhi unaondoka tu…nimemwambia elfu thelathini kajitia kugoma, lakini we komaa humo humo…n’tajaribu kuingia nawe kwenye gari, akizidi kugoma basi ujue habari ndiyo hiyo…”
Kokos alipiga honi. “Vipi tena nyie…mnaringa?”
Jackie alimvuta Candy mpaka pale kwenye gari. “Don’t worry honey, tuko tayari…” Alimwambia mteja wao huku akimsukumia Candy ndani ya lile gari naye akianza kufungua mlango wa nyuma.
“We’ unaenda wapi? Nimesema sitaki wawili bwana…huyu mwenzako anatosha sana!” Kokos alimkemea. Jackie aliteremka na kuubamiza mlango kwa hasira. Candy alimgeukia Kokos. “Twe…twende naye tu, kaka…” Alimwambia kwa sauti ya kuomboleza.
Kokos aliliondoa lile gari taratibu kutoka eneo lile. “Hakuna haja ya kuja wawili mrembo wangu…we’ mbona watosha sana my pretty, eenh? Unataka kunichanganyia biriyani na ugali saa hizi?” Alimjibu kilevi huku akitabasamu. Candy alihisi mwili ukimyong’onyea na meno yakigongana kinywani mwake.
“Unaitwa nani wewe…mbona unaonekana muoga-muoga sana, vipi?” Kokos alimuuliza huku akimpapasa paja lake kwa mkono wake wa kushoto.
“Judy…naitwa Judy…” Candy alijibu, machozi yakimlenga-lenga, moyo ukimbamiza vibaya sana ndani ya kifua chake huku akijilazimisha kutokwepesha mapaja yake.
Eeh Mungu wangu, balaa gani hili unaloniletea sasa lakini…? Sifanyi kwa kupenda Mungu wangu, ila sioni namna nyingine kwa sasa…nisamehe mola wangu…nisamehe….
Safari ya kwenda kusikojulikana ilikuwa imeanza, na kadiri walivyodizi kukata mitaa, ndivyo Candy alivyozidi kukaribia kwenye tukio lililokuja kubadili kabisa maisha yake.
***
Vishindo vya mlango wake wa mbele ukigongwa kwa pupa na vurugu vilimshitua Kokos Wandiba kutoka kwenye usingizi mzito uliokolezwa na kilevi. Alijigeuza pale kitandani huku akisonya na kuzamisha kichwa chake chini ya mto aliokuwa amelalia na kuzidi kujikunja pale kitandani huku akifinya macho yake ili ule usingizi wake mzito usikatishwe na vishindo vile, lakini wapi!
Vishindo vilizidi.
“Aaaaah! Nani tena huyu saa hizi jamani!!” Alimaka peke yake na kuinuka kutoka pale kitandani huku akifikicha macho. Aliitupia macho saa ya mezani iliyokuwa juu ya mtoto wa meza aliyekuwa kando ya kitanda, na kuona kuwa muda ulikuwa ni saa kumi na mbili kasoro robo asubuhi.
“Ama! Hii nini sasa! Huu ni muda wa kugongea watu majumbani mwao kweli?” Kokos alilaani huku akitembea kwa kupepesuka kuelekea nje ya chumba chake cha kulala, akipita kwenye sebule yake ghali iliyoenea kila kitakiwacho kwenye sebule, na kuuendea mlango wa mbele wa nyumba yake akiwa na bukta tu, akilini akijiuliza ni vipi mlinzi wake huko nje ameweza kuruhusu hali ile itokee. Nje ya mlango ule, mgongaji alikuwa akizidi kugonga.
“Nani wewe lakini?” Kokos aliuliza kwa ukali.
“Hebu fungua mlango huo wewe!” Sauti ambayo aliitambua mara moja ilimkemea kutokea kule nje, na hapo Kokos alizungusha juu mboni za macho yake na kutupa mikono yake hewani kwa kukata tamaa. Alifungua mlango na kubaki akimkodolea macho yule mgongaji, ambaye bila ya salamu alipita moja kwa moja ndani ya nyumba ile na kwenda kuketi kwenye moja ya makochi mazuri sana yaliyoipamba ile sebule ghali. Kokos alibaki akiwa ameshikilia mlango huku akimtazama yule mgeni aliyeingia mle ndani kwa mshangao.
“Hivi unajua ni saa ngapi saa hizi lakini Bishkuku?” Hatimaye alimuuliza kwa hisia kali huku bado akiwa ameshikilia mlango wake.
“Hebu nijie hapa mimi, sio unasimama tu hapo mlangoni kama askari kea! Hutaki kujua nimepatwa na nini hata nikaja kwenye hili kasri lako la kifakhari lukwili namna hii…we’ unachojua ni kuniuliza saa hizi ni saa ngapi?” Bishkuku alimjibu kwa fedhuli huku akikunja nne pale kwenye kochi. Kokos alimtazama kwa muda, kisha akatikisa kichwa kwa masikitiko na kuufunga ule mlango kabla ya kurudi pale sebuleni na kukalia mkono wa moja ya makochi yaliyotapakaa eneo lile huku akiachia mwayo mrefu na kubaki akimtazama kwa macho ya kuuliza.
Walibaki wakitazamana kwa muda, kisha Bishkuku alipoona haulizwi kilichompeleka pale muda ule akaanza kuongea.
“Haya kisa cha kuzima simu jana kutwa nzima ni nini?” Alimuuliza, na kabla Kokos hajajibu, akaendelea,“…halafu ulikuwa umelewa wewe…mtizame kwanza!”
“Ni nini kilichokuleta kwangu saa hizi Bishi?” Kokos alimuuliza huku akibana mwayo mwingine, akidharau zile shutuma za Bishkuku. Bishkuku alimtazama kwa muda, kisha uso wake ukabadilika na kuwa makini.
“Tunis kanitosa.” Alisema kwa uchungu. Kokos alibaki akimtazama kwa mshangao. “What do you meanTunis kakutosa…?” Alimuuliza kwa mshangao.
“Namaanisha kanitosa Kokos…kachukuliwa na mtu mwingine!” Bishkuku alisema kwa uchungu.
Kokos alimtazama kwa mshangao mkubwa sana kama kwamba wakati ule ndio alikuwa anagundua kitu ambacho siku zote hakuwa amekigundua kwa mwanamama yule aliyekuwa mbele yake, kisha kama kwamba aliyeshukiwa na uelewa wa kile alichokigundua kwa mara ya kwanza, alimwambia huku macho yake yakionesha kuumia sana.
“Ah! Bishi…yaani…ah! Yaani unataka kuniambia kuwa wewe na Tunis…mlikuwa na uhusiano wa ki…mlikuwa mnasagana? Alikuwa mpenzi wako? Na sasa kachukuliwa na mpenzi mwingine, amekutosa? Mungu wangu, nyie wanawake wa siku hizi! Sasa hicho ndicho kilichokuleta huku saa hi…”
“Kokos!” Bishkuku alimaka kwa hasira huku akiinuka kutoka kwenye kochi alilokuwa amekalia. “Sio hivyo unavyofikiria wewe, alla! Sina maana hiyo kabisa. Nina maana kuwa Tunis sasa kaamua kuungana na msimamizi mwingine katika maandalizi yake ya kugombea taji la Miss Tanzania, we vipi? Mi’ msagaji tangu lini, una wazimu nini?” Alimjia juu.
“Khah! Sasa hiyo itawezekana vipi? We’ si nd’o uliyemfikisha hapo, yule?” Kokos sasa alielewa na kuonesha kushangazwa na hali ile.
“Sa’ si nd’o maana nimechanganyikiwa? Yaani Tunis amenisaliti vibaya sana…”
“Pesa, muda na mafunzo yote yale uliyompa?” Kokos naye aliongea kwa mshangao.
“Sasa unaona ni jinsi gani nilivyohamanika?”
“Mambo haya yametokea lini lakini?” Kokos aliuliza.
“Jana. Na nikawa nakupigia simu hupatikani, nikaja kule kazini kwako nikaambiwa kuwa umeondoka katika mazingira yasiyo muafaka kabisa…umetukana kuanzia wanafunzi hadi mkuu wa shule!”
Kokos alitabasamu kidogo alipokumbuka jinsi yule mwanafunzi alivyotoka mbio pale ofisini, na jinsi wale walimu wenzake walivyoangusha midomo kwa mshangao.
“Ah, wale nimeshaachana nao…” Alisema, sasa akiwa makini zaidi ya alivyokuwa hapo awali, na kuunganisha kwa swali. “Sasa…kwa hiyo sasa huyo mrembo wako amekwenda kushirikiana na nani?”
Bishkuku alibetua midomo na kukunja uso kwa hasira kabla ya kumjibu.
“Sanura Kashogi.”
Sasa ilikuwa zamu ya Kokos kuacha kinywa wazi.
“Sanura Kashogi!Huyu mwanamitindo mkubwa jijini?” Alimuuliza.
“Ndiye haswa!” Bishkuku alijibu, na hapo wote wawili walisikia kishindo kizito pale sebuleni, na kwa pamoja wakageuka kule kilipotokea kishindo kile.
Walibaki vinywa wazi…
***
Akiwa ndani ya lile jumba la kifahari aliloingizwa usiku uliopita, Candy naye alishitushwa na vile vishindo vilivyomshitua Kokos kutoka kwenye usingizi mzito. Baada ya kufika ndani ya jumba lile usiku uliopita, alijikuta kwenye wakati mgumu kweli kweli, kwani yule bwana aliyemuopoa hakuwa mchovu kwa ulevi kama jinsi ambavyo Jackie alivyomwambia kuwa angekuwa. Jamaa alikuwa na nia kweli kweli ya kutimiziwa haja zake za kimwili usiku ule, na Candy alishindwa kabisa kumdhibiti. Jamaa alianza kumshika-shika na kumtomasa-tomasa huku akijaribu kumbusu na mara akijaribu kumbeba na kumuingiza chumbani kwake. Candy alijitahidi kumkwepa na kumpumbaza ili angalau achoke kutokana na ulevi ule na hatimaye alale usingizi, lakini wapi! Jamaa alikuwa na nguvu na nia ile ile, pamoja na kulewa kwake. Candy alizidiwa kabisa, na alipoona hali imekuwa ngumu ilibidi aangue kilio huku akimuomba jamaa msamaha, akijieleza kuwa yeye hakuwa amewahi kufanya jambo lile hata siku moja, na kwamba ni dhiki tu ndiyo iliyomfikisha pale, na kwamba hatochukua malipo yoyote kutoka kwake ili yule bwana amsamehe na asimshurutishe kufanya kitendo kile.
La haula!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wacha Jamaa aje mbogo! Alimchachamalia huku akimtukana matusi mazito mazito na kumfukuza kutoka mle ndani. Candy alizidi kulia na kuomboleza. Angeondokaje usiku ule? Alimuomba amsitiri tu mpaka asubuhi naye ataondoka na hatotaka malipo yoyote.
“Hebu niletee kinywaji kule kwenye friji upesi, kabla sijakubaka bure hapa ebbo!” Hatimaye jamaa alimfokea kilevi, na Candy alikimbia hadi kwenye jokofu, ambamo alikuta kumesheheni vinywaji vya kila aina. Alitaka kumuuliza ampelekee kinywaji gani lakini jamaa alimfokea kwa ukali, naye akanyakua chupa moja ya pombe kali na kumpelekea.
Jamaa alimkamata mkono na kumwambia kilevi, “Sasa lazima ufanye kazi hapa sio ukae bure bure tu ndani mwangu, umesikia?”
Candy aliafiki kwa pupa.
“Nenda pale kabatini uchukue gilasi kubwa kuliko zote uje nayo hapa…” Jamaa alimuamuru kilevi, “…halafu utakuwa unanimiminia hii pombe kwenye gilasi nami nakunywa…mpaka nikwambie basi, sawa sawa?”
Doh, maneno yale yalikuwa kama wimbo mzuri sana masikioni mwake. Alikimbia haraka na kuleta gilasi kubwa iliyokuwa katika lile kabati zuri na ghali, na kuanza kum-miminia kinywaji yule bwana. Mara moja jamaa alijimwagia kinywaji kwenye suruali na kumkemea kwa hasira, na Candy akanywea kwa woga.
“Ole wako unimwagie tena…nakubaka hapa hapa…Shwain we!” Alimkemea, na Candy akaendelea kum-miminia kinywaji kwa umakini mpaka alipoelemewa na kilevi na kuchapa usingizi mzito.
Ndipo alipoanza kuivinjari ile nyumba kutoka chumba mpaka chumba, na akajionea jinsi yule mtu aliyokuwa ameenea kiuwezo. Hatimaye alirudi pale kwenye kochi alipokuwa amelala yule “mteja” wake na kuanza kumvua nguo kwa woga. Kisha alimburura kwa taabu hadi kwenye chumba ambacho kufikia muda ule alijua kuwa ndio kilikuwa chumba chake cha kulala na kumlaza kwa taabu kitandani. Akiwa amemlaza chali pale kitandani, Candy alimvua viatu na soksi yule bwana na kumuacha aendelee kulala. Kisha naye akaingia chumba kimojawapo mle ndani na kujifungia, akijaribu kutafuta usingizi, akilini akijifikiria itakuwaje pindi kukicha na atakapokutana tena na yule bwana…
***
***
Baada ya kushtushwa na vile vishindo vya kugongwa mlango wa nyumba ile, Candy alitoka taratibu nje ya kile chumba alichokuwa amejifungia na kunyata kuelekea sebuleni ambako alisikia sauti zikitokea, na aliposikia sauti ya kike mara moja moyo ukampaa.
Mama yangu! Mkewe kafika! Nitasema nini leo mimi masikini ya mungu jamani!
Huku moyo ukimpiga alizidi kusogea kule sebuleni taratibu ili asikie yale yaliyokuwa yakiongelewa na wale watu waliokuwa kule. Lakini alipoufikia mlango wa kuingilia kule sebuleni, hakuziona kandambili zilizokuwa zimevuliwa nje ya mlango ule naye akazivamia kiasi cha kumfanya apepesuke kidogo, akinyoosha mikono yake ili awahi kujishikilia ukutani. Badala yake mikono yake ikauparamia ule mlango, ambao ulifunguka naye akajikuta akipitiliza nao mpaka kule sebulenikwa mweleka mzito.
Ayyaa! Nimegundulika…
Alijiinua haraka na kubaki akiwa ametumbua macho pale akiwatazama wale watu wawili waliokuwa pale sebuleni. Kokos Wandiba alitumbua macho kumtazama yule mrembo aliyeibuka ghafla ndani ya nyumba yake. Alifinya na kufinyua macho mara tatu mfululizo, kabla hajagungua kuwa alikuwa ameacha kinywa wazi.
Mrembo aliyesimama mbele ya macho yake alikuwa hajapata kumuona hata siku moja na akili yake ilikuwa ikijaribu kuvuta matukio ya siku iliyopita kujaribu kujua ilikuwaje hata mrembo yule akawa ndani ya nyumba yake muda ule.
Bishkuku naye alibaki akimkodolea macho ya masataajabu yule binti aliyesimama kibwege hatua chache kutoka pale mlangoni. Alizitazama zile nguo alizovaa yule binti, na kubaki kwenye kile kijisketi kifupi alichokuwa amekivaa, na kumgeukia Kokos kwa macho ya kuuliza.
“Shhk…sh’kamooni….” Candy alijikuta akitupa salamu huku akiviringa-viringa vidole vya mikono yake kwa woga.
“We…wewe nani…?” Kokos alimuuliza kwa mastaajabu makubwa, na Candy akapigwa na butwaa. Bishkuku akazidi kumtazama Kokos kwa mshangao.
“Unajifanya humjui? Hujui kafikaje humu ndani huyu wewe?” Alimuuliza kwa hasira, kisha akamgeukia yule binti aliyesimama mbele yao, na Candy akahisi moyo wake ukipiga tikitaka ndani ya kifua chake.
“Nakuuliza wewe binti…” Kokos alizidi kumuuliza Candy kwa ukali, “…umefikaje humu…na unataka nini?”
Na Bishkuku alimjia juu Kokos. “Toka hapa wewe! Mtu unaona kabisa kuwa huyu ni changudoa uliyemuopoa huko majiani halafu sasa unajitia humjui?”
“Mi’ s’o Changudoa!” Candy alijikuta akimaka kwa ukali.
Bishkuku alimtulizia macho kwa muda, kisha alianza kumsogelea taratibu. Candy alitamani kukimbia, lakini alijikaza na kujipa ujasiri wa kuendelea kusimama pale pale huku akimtazama yule mwanamke aliyekuwa akimjongelea huku akimtazama kwa namna ambayo hakuweza kuielewa mara moja ilikuwa inamaanisha nini. Kokos alibaki akimkodolea macho yule binti huku akili ikimzunguka. Bado hakuwa na kumbukumbu kabisa ya jinsi yule msichana mrembo alivyoweza kufika ndani mwake namna ile.
Bishkuku alimfikia Candy na kumtazama moja kwa moja machoni. Candy naye alijitutumua na kumrejeshea mtazamo huku akiwa ametunisha midomo yake tayari kwa makabiliano.
“Sasa kama we’ si changudoa ni nani basi?” Bishkuku alimuuliza huku bado akimtazama kwa makini, nyuso zao zikiwa zimekaribiana sana.
“Mi’ naitwa Candy, na…”
“Na ulifikaje humu ndani? Maana hata mwenye nyumba anakushangaa!” Bishkuku alimkatisha kwa swali jingine, na hapo Kokos naye akaingilia kati.
“Sio bwana! Jina lake…jina lake ni Judy…au Julia…au Ju-kitu fulani hivi, lakini sio Candy, nimeshakumbuka sasa!” Alibwata, akiilazimisha akili yake kukumbuka zaidi matukio ya usiku uliopita. Sasa Candy alikuwa amechanganyikiwa, hakujua ajibu hoja ya nani kati ya wale watu wawili.
Bishkuku alimgeukia Kokos.“Kwa hiyo kumbe ni wewe mwenyewe ndiye uliyemleta humu ndani huyu binti, sio?”
Kokos alimtazama na kujikuna kichwa kizembe. “Yeah…nadhani ni hivyo. Nilikuwa nimelewa sana hata hivyo, na…”
“Kwa hiyo hata hujui kama ulitumia kondomu au la?” Bishkuku alimuuliza kwa ukali na shutuma.
“Aa-aah, nakuhakikishia anti hakuna chochote kilichofanyika baina yetu!” Candy alidakia kwa kiherehere, na Bishkuku alimtulizia macho ya kuuliza. “Ni kweli huyu kaka…sijui mumeo, au mpenzi wako…alinileta hapa, lakini nilimuomba tusifanye mambo hayo…” Candy aliendelea kujieleza haraka haraka, lakini kufikia hapo Bishkuku alianza kuangua kicheko kikubwa, na Candy akapigwa butwaa.
“Mume wangu…? Mpenzi wangu…? We’ binti usiwe mjinga…” Bishkuku alimwambia huku akicheka na akirudi kuketi kwenye moja ya makochi pale sebuleni.
“Kwa…kwani sio mumeo…?” Candy aliuliza kwa mshangao.
“Huyu ni dada’angu,” Kokos alimwambia, “na hana mamlaka ya kuingilia maisha yangu binafsi!” Akaendelea huku akimtazama dada yake kwa jicho kali. Bishkuku alimrejeshea jicho kali mdogo wake, kisha akamgeukia Candy.
“Kwa hiyo binti sasa unakiri kuwa we’ ni changudoa uliyeopolewa na mdogo wangu jana?”
Candy hakuwa na jibu, akainamisha uso.
“Sawa nilichukua changudoa, na sawa najua kuwa siku zote huwa unanikanya kuhusu swala hilo, lakini hilo ni swala la maisha yangu, si la kwako. Tuongee kilichokuleta halafu uniache na usingizi wangu!” Kokos aliingilia kati.
Candy alitembeza macho kutoka kwa kaka kwenda kwa dada, na kuyarudisha tena kwa kaka.
“Ba…basi mi’ naomba niende tu kakaangu, nashukuru kwa yote…”
“Hapana…”
“Usiondoke…!”
Kokos na Bishkuku walisema kwa pamoja. Candy alizidi kupigwa mshangao.“Ni…nisiondoke? Kwa nini…?”
“Wewe na mimi bado tuna mambo ya kuwekana sawa mrembo...” Kokos alimwambia, “…jana nilikuwa nimelewa sana, na huenda nilikosa adabu kwa kiasi fulani, ila leo niko safi kiasi. Kwa hiyo naomba usubiri kidogo…tupate chai…kisha utaondoka kama utapenda, okay? Kwa sasa nina maongezi kidogo na dada’angu hapa, akiondoka nitaongea na wewe.”
Candy na Bishkuku walimtazama kwa mshangao, kila mmoja kwa sababu yake. Candy alitaka kusema neno lakini akaghairi. Aligeuka na kurudi kule chumbani alikokuwa amejifungia usiku uliopita, akilini akijiuliza ni maongezi gani ambayo yule jamaa alitaka kuongea naye.
Mara baada ya Candy kuondoka eneo lile Bishkuku alimgeukia Kokos kwa wahka.
“Umeona jinsi binti alivyoumbika yule? Umeona?”
Kokos akamshangaa. “Una maana gani, mbona sikuelewi? Umekuja kuongelea juu ya Tunis na jinsi alivyokusaliti…haya ya huyu binti kuumbika yanakujaje tena?”
“Ah, yaani huelewi? Ni kwamba tangu Tunis anisaliti nimekuwa nikijisemesha kuwa ni lazima niingize mrembo kwenye miss Tanzania ya mwaka huu, na nilikuja kwako nikitegemea kupata ushauri juu ya hatua gani za kisheria nimchukulie Tunis na huyo mtu aliyemrubuni …” Bishkuku alimjibu, na hapo hapo Kokos alimkatisha.
“Aa-aa, hapo hapo Bishkuku! Mi’ nilikubali kukuunga mkono kwenye hizo harakati zako tangu ulipoanza na Tunis, na nilikushauri kuwa umsainishe mkataba yule mtoto mbele ya mwanasheria, we’ ukapuuza. Ona alivyokufanya sasa!”
“Ni kweli uliniambia Kokos, na hilo ni moja ya sababu za ujio wangu kwako asubuhi hii…sababu nyingine ikiwa ni kukuomba msaada wa kifedha. Lakini sasa naona kumbe nimeshapata na mrembo wangu mpya hapa hapa. Sina tena haja ya kumshitaki Tunis, kwani nitapoteza muda bure…ila nataka kumuonesha kuwa hawezi kunisaliti halafu akapata taji la urembo nchini, na huyu binti ndiye atakayeniwezesha kutimiza azma hiyo!” Bishkuku alimweleza kwa hamasa kubwa.
Kokos alimshangaa kupita kiasi.
“Khah, Bishi! Hivi we unamjua huyu binti kiundani kweli? Unajua katoka wapi?Unajua historia yake…?Mi’ nimemuopoa kwenye uwanja wa machangudoa jana! Hivi unaelewa maana yake hiyo? Hiyo maana yake ni kwamba huwezi kumuingiza mtu wa aina hiyo kwenye mashindano yenye hadhi na heshima kama hayo…!”
“Ila kuingiliana naye kimwili bila kinga ni sawa, sio?”
“Awww come on Bishi! Hii sio kuhusu mimi na matamanio binafsi ya mwili wangu bwana…!Hii ni kuhusu wewe kujiaibisha kwa kuingiza mtu mwenye historia ya uchangudoa kwenye mashindano makubwa kama hayo Bishi! Wewe unatarajia huyu binti atwae taji, na hivyo awe kioo cha jamii wakati yeye mwenyewe ni mchafu…unaona mkanganyiko huo?”
“Sasa kama mchafu mbona ulitaka kulala naye?” Bishkuku alimjia juu.
“Akh, nimeshakwambia kuwa ni mchafu kumuweka kwenye mambo ya u-miss Bishi…huko alipo ni sawa kumtoa na akaendelea na maisha kwa njia nyingine, lakini sio kwenye u-miss…kule si pa kupeleka watu wenye historia chafu-chafu Bishi, nawe walijua hilo!”
“Mnhu! Laiti ungejua machafu waliyonayo hao waliokuwamo kwenye mashindano hayo wala usingesema hivyo mdogo wangu…hata hivyo, sijui ilikuwaje tu hata huyu binti akaangukia huko ulipomuopoa, ila naamini kuwa anaweza kurekebishwa Kokos!”
“Aaaa come on, Bishi…come on!”
“Nipe huyu binti nimfunde Kokos, na nakuhakikishia Tunis atausikia u-miss Tanzania kwenye bomba tu, na taji la huo u-miss ataishia kuliona kichwani kwa huyu binti aliyemo ndani mwako hivisasa!”
Kokos aliishia kutikisa kichwa tu huku akimtazama dadaye kwa machoya kukata tamaa. Bishkuku aliinuka kwa kwenda kuketi kwenye mkono wa kochi alilokalia mdogo wake na kumzungushia mkono wake mabegani.
“Yule binti ana urembo wa asili Kokos…yaani ile ndio chapa halisi ya mrembo sio tu wa Tanzania, bali hata Afrika na dunia!”
“Una wazimu Bishkuku, tena una wazimu sana! Na kama unadhani nitakuunga mkono juu ya hili utakuwa umekosea sana. We’ hujui huyu mtu ana aibu ngapi huko atokako, halafu unataka umpandishe jukwaani mbele ya kadamnasi…unataka kuwapa chati ya kuuza magazeti waandishi wa udaku bure tu hapa!” Kokos alimjia juu.
“Hayo yote tutayafanyia kazi taratibu Kokos, wacha tuongee naye kwanza…kama kweli alipofika hapa alishindwa kufanya ngono nawe na akakuomba usimfanyishe huo mchezo wako mchafu, huoni kuwa huyu ni mtu mzuri? Kwamba labda ni matatizo tu ndiyo yaliyomfikisha hapo?”
Kokos alibaki kimya kwa muda, akitafakari maelezo yale, kisha akamuuliza dada yake.
“Okay, kwa hiyo unataka nini kwangu…naomba twende hatua kwa hatua tafadhali, usinichanganyie habari”
Bishkuku alishusha pumzi ndefu. “Sawa kabisa. Kwa sasa ninachotaka ni kuongea na huyu binti, na ikiwezekana nimchukue, nimfunde ndani ya huu muda mfupi ili nimuingize kwenye mashindano ya urembo ya mwaka huu…elewa kuna miezi mitano tu mbele, na tayari baadhi ya vitongoji vimeshapata warembo wao kikiwemo cha Temeke ambako yule maluuni Tunis ndio ametoka kinara…kwa mafunzo na jasho langu!”
“Na baadaye akakutosa.”
“Ndiyo, na baadaye akanitosa…! Sasa nataka kuanza upya, unajua mi’ huwa sikati tamaa kirahisi!”
“Na kwa mfano tuseme tunakubaliana kuwa umuingize huyu binti kwenye mashindano haya, unadhani ataingia kwa tiketi ya mkoa gani? Kwani Dar es Salaam si tayari imeshapata warembo wake wa kuiwakilisha katika mpambano wa mwaka huu?”
“Ni kweli, nami nimepata muda wa kulifikira sana swala hilo, lakini, sasa Dar imeongezewa nafasi moja iitwayo Miss Dar City Center! Na hii ndio nataka niishindanie, nikiweza kuingiza mrembo akatwaa taji la miss Dar City Center tu, basi…safari ya kuukwaa u-miss wa taifa itakuwa imeanza!”
“Inaelekea unajiamini sana juu ya hilo.”
“Sana tu. Kama watu wakitaka haki na taaluma vitumike badala ya ubabaishaji na upendeleo,basi jua wazi kuwa hakuna wa kumzuia binti nitakayemfunda mimi kutwaa taji lolote la urembo hapa nchini!”
“Sawa, hilo nimelielewa. Nini kingine unachotaka kutoka kwangu?”
“Unajua kuwa nataka msaada wa fedha kutoka kwako, maandalizi ya swala hili yanahitaji pesa, na we’ unazo nyingi tu hazina kazi!” Bishkuku alimjibu na kuanza kucheka pale aliposema lile neno “hazina kazi.”
Kokos naye alianza kucheka. “Tatizo lako dada unapenda kutia maskhara kwenye mambo ya msingi…haya alokwambia kwamba pesa zangu hazina kazi ni nani?”
“Si naona tu? Mtu una pesa nzuri, lakini huwezi kuitumia kwa nafasi, wala huianzishii miradi yoyote, imekaa tu…unaishia kujitia kufanya kazi za ualimu mara utukane wanafunzi…yote ya nini hiyo?”
Kokos alitikisa kichwa. “Yataisha tu hayo dada…ni swala la muda tu!”
“Kwa hiyo umenikubalia ombi langu?”
“Siwezi kukukatalia kitu Bishkuku, nawe wajua hilo. Ila tu ujue kuwa nitakuunga mkono katika hili lakini mimi binafsi siliafiki kabisa swala la kumtumia huyu binti ambaye humjui vizuri…”
“Madhali utaniunga mkono, na utanipatia fedha nikizihitaji, hayo mengine yote niachie mimi…haya natuongee naye basi.”
***
Candy alirudi pale sebuleni kwa mashaka baada ya kuitwa na Bishkuku. Kokos alimuelekeza aketi kwenye kochi ambalo lilimfanya awe anatazamana uso kwa uso na wale watu wawili. Kufikia hapa alikuwa amepata taulo kubwa mle ndani na akawa amejifunga kiunoni.
“Binti naomba uwe na amani tu, hakuna baya lolote tutakalo kukufanya, ila tungependa kujua zaidi kuhusu wewe…” Bishkuku alimwambia.
“Kujua zaidi kuhusu mimi…? Kivipi…!” Candy aliuliza huku akitembeza macho baina yao.
“Tungeanza na jina lako halisi…kama ni Candy au Julia…halafu baada ya hapo utujulishe zaidi kuhusu wewe, maisha yako, na makazi yako hapa mjini…” Kokos alifafanua. Bado Candy alionekana kuwa na mashaka.
“Sasa…kwa nini niwaeleze mambo yote hayo kuhusu mimi? Mi’ nataka kuondoka zangu tu, sina haja ya jambo jingine zaidi…”
“Kwa sababu tunataka kukujua zaidi…” Bishkuku alimjibu yule binti huku akizidi kumtazama kwa makini. Bado swala lile lilikuwa zito kwa Candy kulielewa.
“Kwa nini mnataka kujua zaidi kuhusu mimi?”
Bishkuku na Kokos walitazamana.
“Labda tuseme kuna kazi tunataka tukupe, lakini kwanza tungependa kukufahamu japo kidogo kabla ya kukupa kazi hiyo…na nakuhakikishia kuwa kama kweli we’ si changu…”
“Mie sio changu jamani!” Candy alidakia kwa hamasa.
“…na kama kweli hutaki kuwa katika maisha hayo uliyotaka kuyaingia, basi hii ni nafasi ambayo hutakiwi kujiuliza mara mbili, kwani itabadilisha kabisa muelekeo wa maisha yako!” Bishkuku alimwambia.
“Jamani kweli mimi sitaki kabisa hayamaisha niliyo nayo, na kama nitapata namna halali ya kuyaepuka nitaifuata namna hiyo kwa moyo wangu wote!”Candy alisema huku akiwatazama watu wale mmoja baada ya mwingine.
“Sasa hii ndio nafasi yako bi mdogo…anza kutoa maelezo tupate kukuelewa!” Kokos alimwambia. Candy alimtazama kwa mashaka, ni wazi kuwa alikuwa na imani zaidi na Bishkuku kuliko Kokos, hasa baada ya yale matukio ya usiku uliopita.
“Ni…ni kazi gani mnayotaka kunipa…?” Aliuliza kwa mashaka.
“Unapoteza muda bure binti!” Kokos alimjia juu. Bishkuku alimtupia jicho la kukanya, na kwenda haraka kuketi kando ya yule binti mwenye mashaka. Alimzungushia mkono wake mabegani. “Usiwe na wasi wasi binti…kazi tunayotaka kukupa si ya ukahaba…na wala si ya kuvunja sheria. Lakini ni muhimu sana tukufahamu zaidi, na kisha nawe utapata nafasi ya kutufahamu sisi vile vile, sawa?”
Bado Candy alionekana kuwa na mashaka na mwenye kusita sana kutoa maelezo ya maisha yake.
Kwa nini? Kokos alijiuliza huku akimtazama kwa makini binti yule mwenye urembo uliotukuka. Muda huo Candy alivuta pumzi ndefu na kuzishusha, akiwa ameshapitisha uamuzi juu ya swala lile ambalo wale watu wawili asiowajua kabisa walitaka alifanye.
“Sawa…nitawaeleza.”
“Safi sana. Tuanze na jina lako halisi!” Kokos alimwambia huku akimkodolea macho kisura yule, na kwa mara nyingine asubuhi ile, aliuhisi moyo wake ukipaparika ndani ya kifua chake.
Hakika huyu mtoto kaumbika jamani, Dah!
“Jina langu halisi ni Candy Gamasala…” Candy alianza kuwaeleza, na ndipo Kokos na Bishkuku waliposikia kisa cha kusikitisha kuhusu maisha ya yule binti…
***
Candy aliwaeleza kuwa alifika jijini Dar miezi miwili iliyopita akitokea Magu ambako alikuwa akiishi tangu utoto wake. Aliwajuza kuwa yeye ni yatima aliyekuwa akilelewa kwenye kituo kimoja cha kulelea watoto yatima kilichokuwa chini ya kanisa huko Magu. Na akiwa kituoni hapo alipata elimu yake ya msingi na ya sekondari hadi kidato cha pili, ambapo kufikia muda huo alilazimika kutoka kwenye kituo kile baada ya kupatiwa walezi wa kuishi nao katika mazingira ya nyumbani. Bahati mbaya walezi wake hao walifariki kwa ajali ya gari muda mfupi baada ya yeye kuanza kuishi nao, naye akabakiwa na njia kuu mbili za kufanya, aidha kurudi kwenye ile nyumba ya watoto yatima, au aendelee kuishi na familia ya wale walezi wake wa kufikia. Kwa kuwa wanandugu walishaanza kugombana wenyewe kwa wenyewe juu ya mali zilizoachwa na marehemu wale, yeye akaonelea ajiondoe mwenyewe kutoka kwenye familia ile. Na kwa kuwa maisha ya kwenye ile nyumba ya watoto yatima yalishamchosha sana, hakutaka tena kurudi huko. Ndipo alipopanda basi na kuja jijini.
“Sasa we’ ulikuwa na ndugu au jamaa yoyote unayemfahamu hapa jijini?” Kokos alimtupia swali.
Alimjibu kwamba hakuwa na ndugu yoyote hapa jijini zaidi ya msichana aliyeitwa Jackie, ambaye walilelewa pamoja kule kwenye kituo cha watoto yatima, na ambaye alitoka kwenye ile nyumba na kuja jijini baada ya kufikia umri mkubwa. Kwa kuwa pale kwenye nyumba ya watoto yatima kulikuwa kuna simu, yule dada alikuwa akipiga simu mara kwa mara kuwasalimu walezi wao na baadhi ya watoto wengine waliokuwa pale kwenye ile nyumba ya watoto yatima. Na ni huyu ndiye aliyemwambia wakati fulani kuwa alikuwa anaishi Dar es Salaam eneo la Manzese, akimpa maelekezo ya kina jinsi ya kufika pale alipokuwa akiishi. Hivyo, baada ya kuona kuwa hakuwa na nafasi tena kwenye ile familia ya walezi wa kufikia, na kwa kuwa hakutaka kurudi tena kwenye ile nyumba ya watoto yatima, Candy aliamua kusafiri mpaka Dar na kwenda Manzese, akifuata maelekezo aliyopewa miezi kadhaa iliyopita na Jackie, na hatimaye alifanikiwa kuonana naye.
“Jambo ambalo sikulijua ni kwamba mwenzangu alikuwa ameingia kwenye maisha ya ukahaba, na akanilazimisha na mimi niingie kwenye shughuli hiyo, ama si hivyo nihame kutoka pale kwenye chumba chake…sikuwa na namna kwa kweli, na ndipo nilipokutana na huyu kaka pale viwanja jana…ile ndio ilikuwa siku yangu ya kwanza!” Candy alitoa maelezo yake.
Hakika ile habari ilimsikitisha sana Bishkuku, ingawa Kokos alionekana bado kuwa na maswali mengi.
“Pole sana mdogo wangu…pole sana…” Alimwambia huku akimpiga-piga mgongoni. Candy alibaki akiwa ameinamisha kichwa.
“Sawa…sasa, hukuwahi kupatikana na kosa lolote la jinai huko nyuma? Kukamatwa na polisi hivi, au kitu kama hicho?” Kokos alimuuliza.
“Hapana! Sijawahi kabisa kukutwa na jambo kama hilo maishani mwangu.”
Bishkuku na Kokos walitazamana. Bado uso wa Kokos ulionekana kutaka kujua zaidi, lakini hata hivyo, alimuashiria Bishkuku kuwa aendelee kuongea yale aliyotaka kuongea na binti yule.Na ndipo Bishkuku alipompasulia Candy azma yake.
Mshituko alioupata Candy baada ya kujua azma ya Bishkuku ulikuwa mkubwa mno.
“Mimi…!” Wazo la yeye kushiriki shindano la kugombea umalkia wa urembo nchini lilikuwa ni zaidi ya ambavyo alitaraji kusikia kutoka kwa Bishkuku. Kuuza duka, sawa. Kufanya kazi za ndani, sawa. Hata kutembeza karanga barabarani pia ingekuwa sawa, lakini kuwa miss!Hapana.
“Ndiyo Candy…wewe.” Bishkuku alimthibitishia. Candy alitikisa kichwa kwa mastaajabu na kutoamini.
“Lakini…mimi yatima jamani…tangu lini yatima naye…”
“Hilo si tatizo hata kidogo. Yatima pia anaweza kushiriki shindano hili, na nadhani wewe utawapa moyo na kuwafanya yatima wengine wote wajivunie sana!”
“Lakini, mi sijawahi hata siku moja jamani…!” Candy alizidi kulalama kwa wasiwasi. Sasa alimfanya Kokos acheke. “We’ kila kitu hujawahi, eenh Candy?” Alimuuliza kwa maskhara, na wote wakaangua kicheko, ingawa Candy alicheka kwa wasiwasi.
“Nitakufundisha kila kitu unachopaswa kujua katika urembo, Candy…na zaidi ya hapo!” Bishkuku alimthibitishia.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Tutakufundisha…” Kokos aliingilia kati, akimrekebisha dada yake, kumaanisha kuwa nayeye pia atashiriki kumfundisha. Candy alimgeukia kwa macho ya kuuliza.
Ah, jamani yale macho!
“Na wewe pia…?” Candy alimuuliza. Kokos alikuwa ameshachanganywa na mvuto wa macho ya yule binti, alibaki ameduwaa kwa muda.
“Ndi…ndiyo! Mi’ mwalimu…n’takufundisha jinsi ya kuongea kimombo...kwa pozi…kwa nidhamu, au…?” Alimjibu huku akimgeukia Bishkuku kwa swali. Ni wazi Kokos alitaka apate nafasi tu ya kuendelea kuwa karibu na yule binti aliyeumbika.
“Wazo zuri sana Kokos!” Bishkuku alidakia kwa hamasa, na kumgeukia Candy, “…Tutakupa azma mpya katika maisha Candy…uachane na hayo maisha uliyotaka kuyaingia, na hatimaye ujipatie heshima katika jamii. Huoni kuwa hilo ni bora zaidi kwako?” Bishkuku alimwambia na kumuuliza. Hakika Bishkuku alikuwa sahihi, na Candy aliliona hilo.
“Sasa…” Bado Candy alikuwa amechanganyikiwa,“… kwa nini mimi? Mnadhani mimi ninafaa kweli kushiriki u-miss?”
Bishkuku aliachia tabasamu la kumhakikishia yule binti kabla ya kumjibu.
“Bila shaka hujitambui Candy, lakini wewe ni mrembo kweli kweli…” Hapo Kokos alitikisa kichwa kwa nguvu kuafikiana na kile kilichosemwa na dada yake, ambaye aliendelea, “…na sisi tunaokuona tunaamini kabisa kuwa wewe ndiye haswa unayetakiwa kuwa mrembo wa taifa hili. Amini hivyo mdogo wangu.”
Candy alikumbuka maneno ya Jackie.
…kwanza we’ una sura nzuri sana, shepu yako bomba kweli kweli, muonekano wako ni baab kubwa! Kwa nini uendelee kuninyonya kama kupe wakati una kila rasilimali ya kukuweka matawi ya juu hapa jijini, eenh?
Labda hii ndio nafasi ya kutumia rasilimali ya urembo anaosemekana kuwa anao kujiweka katika nafasi ya heshima hapa duniani…
Huku akibubujikwa na machozi kwa kutoamini kile kilichokuwa kikimtokea wakati ule, Candy alikubali kujiweka chini ya himaya ya Bishkuku katika kugombea umalkia wa urembo nchini, akitaraji mabadiliko makubwa katika maisha yake.
Laiti angejua ambayo yalikuwa yakimsubiri huko mbele, bila shaka asingekubali hata kidogo…
***
Candy alijaribu kumshawishi Bishkuku amchukue na rafiki yake Jackie ili naye aondokane na maisha yale mabaya aliyomkuta nayo.
“Mnh! Yule hana hadhi ya u-miss kabisa Bishkuku, mi’ si nimemuona bwana!” Kokos alidakia, na kuendelea, “Yaani pamoja na kwamba nilikuwa kwenye kilevi, niliweza kujua kuwa alikuwa amekubuhu katika ukahaba, na ndio maana nilimkataa pale pale…kwanza hana mvuto kabisa! Atatusumbua bure. Tena nashauri Candy akate kabisa mawasiliano na huyo binti…yule ameshabobea katika maisha yale. Sura yake tu inaonesha…!”
Hoja ya Candy ikaishia hapo hapo, naye hakuwa na namna, ilimbidi akubaliane na ukweli ule. Bishkuku alirejea nyumbani kwake mtaa wa Aggrey akiwa na mrembo wake mpya. Na ni wakati akiingia ndani ya nyumba yake ile ndipo alipoiona ile hawala ya fedha iliyotupwa pale sebuleni kwake na Tunis siku iliyopita. Aliiokota na kuitazama kwa muda, kisha uso wake ukafanya tabasamu dogo huku akiiweka ndani ya mkoba wake.
Walishakubaliana na Kokos kuwa Candy atakuwa akiishi naye pale Kariokoo, kwa sababu hiyo ndiyo ingeleta uhalali wa Candy kushiriki kinyang’anyiro kile cha Miss Dar City Centre. Wakiwa pale nyumbani kwake, Bishkuku alichukua kamera yake maalum aina ya Polaroid, ambayo ilitoa picha papo kwa papo na kumpiga Candy picha kadhaa, zikiwemo za ukubwa wa pasipoti. Kisha alitoa fomu za kujiandikisha shindano la urembo alizokuwa nazo ndani mwake na kwa pamoja walizijaza na kubandika picha ya Candy ya ukubwa wa pasipoti mahala palipohitajika. Kisha walitoka pamoja na kwenda kuziwasilisha rasmi fomu zile mahala husika.
Wakiwa njiani, Candy alimwambia Bishkuku kuwa angependa kwenda kuagana na rafiki yake Jackie na achukue baadhi ya vitu vyake vichache kule Manzese alipokuwa akiishi awali.
“Sawa, lakini baada ya hapo ningekushauri uwe mbali sana na huyo rafiki yako…si mtu ambaye unatakiwa kuonekana naye tena sasa.” Bishkuku alimuasa.
Hivyo basi, baada ya kupata usajili katika shindalo la Miss Dar City Centre, walielekea Manzese. Bahati mbaya Jackie hakuwepo nyumbani, ila Candy alichukua ufunguo kwa mama mwenye nyumba, na kuingia chumbani kwao, ambako alichukua mkoba wake mdogo uliokuwa na baadhi ya nguo na vitu vyake muhimu, kisha akamuachia Jackie ujumbe wa maandishi kuwa yeye ameondoka na hatarudi tena pale kwake, akimtakia maisha mema na akimshukuru kwa msaada wake wote kwa siku zile alizokuwa amemsitiri pale chumbani kwake. Ndani ya barua ile aliweka shilingi elfu kumi na tano alizomuomba Bishkuku, na kuacha ujumbe ule juu ya kitanda. Alitoka nje ya nyumba ile chafu akiamini kuwa hatoonana tena na msitiri wake yule mbaya…
Saa nane mchana siku ile, Bishkuku alimuongoza Candy ndani ya ofisi moja kubwa na ghali ya mwanamitindo mkubwa nchini, Sanura Kashogi.
“Nahitaji kuonana na Sanura.” Bishkuku alimwambia binti waliyemkuta pale mapokezi. Binti alimtazama kwa muda, kabla ya kumuuliza, “Una appointment…?”
“Sikiliza binti, yeye ndiye aliyenipigia simu akinibembeleza nije kumuona, sasa kama analeta mbwembwe tena…”Bishkuku alidanganya bila kupepesa macho.
“Basi anti, samahani… nimwambie nani?” Binti aliuliza haraka.
“Mwambie Bishkuku!”
Binti aliinua simu na kuongea na bosi wake, kisha aliiweka chini ile simu na kumuelekeza Bishkuku apite ofisini kwa Sanura Kashogi. “Twende Candy!” Bishkuku alisema huku akielekea ofisini kwa hasimu wake.
Sanura Kashogi alikuwa ameketi nyuma ya meza kubwa na ghali, miguu yake mirefu na mizuri akiwa ameitundika juu ya meza ile, sigara ikiwa imebanwa kwenye vidole vyake virefu vilivyotapakaa pete za vito ghali na adimu, akipuliza moshi wa sigara hewani.
“Hello, Bishkuku…nikusaidie nini mpenzi…” Sanura alianza kuuliza kwa pozi, na akakomea hewani pale alipomuona Candy akiingia nyuma ya Bishkuku mle ndani, na akabaki akimkodolea macho yule mwanadada mwenye kila nukta ya urembo. Bishkuku alibaki akimtazama jinsi alivyopigwa na kutwaa huku uso wake ukiwa umefanya tabasamu jepesi. Kutoka kwenye kochi kubwa lililokuwa kwenye kona moja ya ofisi ile kubwa, Tunis aliinuka na kumtazama Bishkuku kwa woga.
“Sh’kamoo anti Bishi…!” Alimsalimu huku akiviringa-viringa vidole vyake. Bishkuku alimtazama kutokea utosini hadi kwenye vidole vyake vya miguuni, na kumpandisha tena hadi usoni, kisha bila ya kuijibu ile salamu yake alimgeukia Sanura.
“Sanura umefanya kosa kubwa sana kuramba haya matapishi yangu…” Alimwambia huku akimuoneshea Tunis kwa kidole chake cha gumba, na kuendelea, “…ingawa mwenyewe ulikuwa ukiamini kuwa ulikuwa ukininyang’anya tonge kinywani.”
Candy na Tunis walitazamana. Candy alianza kumsalimu yule msichana mwenye urembo wa kuvutia, lakini Tunis aliwahi kugeuzia uso wake kule kwa akina Sanura.
“Ai anti Bishi jamani!” Tunis alilalama.
“Bishkuku n’takuitia polisi sasa hivi hapa!” Sanura alimtolea ukali huku akishusha miguu yake kutoka juu ya meza na kusimama, sasa akiwa amehamishia macho yake kwa Bishkuku. Candy alibaki akishangaa tu. Bishkuku alibetua midomo na kuketi kwenye kiti kilichokuwa mbele ya ile meza.
“Hebu keti kitini mdogo wangu…” Alimwambia Candy, ambaye aliketi, na kisha akamgeukia tena Sanura. “Haya uniitie polisi kwa kosa gani Sanura?” Alimuuliza.
“Huwezi kuja ofisini kwangu na kutoa maneno ya kashfa kwa mrembo wangu namna hiyo!”
“NHhaaaah, Lloooh! Mrembo wako? Huyu ni mrembo wako?” Bishkuku alimuuliza huku akimnyooshea kidole Tunis, na kuendelea, “…ama kwa hakika we’ nd’o hujui urembo pindi uuonapo! Mambo haya tuachie sisi wazoefu bibi eenh, upo?”
Sanura alibaki akiwa amefura. “Ni nini unachotaka kwangu Bishkuku? Usinipotezee muda wangu bure hapa!”
“Sina nitakacho. Nimekuletea huu upuuzi wako…” Bishkuku alisema huku akiitoa ile hawala ya fedha iliyoachwa nyumbani kwake na Tunis. “Nakumbuka ulimtuma huyo kijakazi wako aje kuniletea…eti ni kufidia gharama nilizotumia kumfikisha hapo alipo! Hujui hata thamani ya kitu unachoparamia bi mkubwa weye, halafu wataka kujitia miongoni mwa kundi la wajuaji! Basi jua kuwa safari hii umeula wa chuya bibi eenh…” Bishkuku alimjibu kwa mfumo wa mpasho uliotukuka, kisha huku Sanura akitumbua macho kwa kutoamini, aliichana vipande vipande ile hawala ya fedha, na kusimama kutoka kwenye kiti alichokuwa amekalia.
“Sina haja na vijisenti vyako mimi, na nakuhakikishia kuwa huo u-miss TZ unaotaraji kuupata kupitia kwenye hayo matapishi yangu…” alimuoneshea tena Tunis kwa kidole chake cha gumba, “…utausikia kwenye bomba tu bibi!” Alimalizia na kumgeukia Candy aliyekuwa amepigwa na butwaa, “Twen’zetu mrembo wangu!”
Walitoka nje ya ofisi ile wakiwaacha Sanura na Tunis wakitazamana.
“Heh, Anti…ile yote inahusu nini?” Candy alimuuliza Bishkuku wakiwa ndani ya gari kurejea nyumbani kwao. Bishkuku alitabasamu kidogo, kisha akamjibu. “Ile inaitwa kumjaza hofu adui…” Kisha huku akiendesha gari kuelekea nyumbani kwake, alimuelezea kisa chote baina yake na Tunis.
“Hah, ama kweli kuna watu hawana shukrani…yaani yule dada ndio kakufanyia hivyo?” Candy aliuliza kwa simanzi baada ya kupata kisa kile.
“Naam, na ndio maana nataka kujua iwapo nawe hutonitenda kama alivyonitenda Tunis.”
“Hapana anti, mimi siwezi kufanya hivyo hata kidogo!” Candy alimhakikishia.
“Nakuamini…lakini pia nadhani haitakuwa vibaya kama tukiandikishana mkataba wa makubaliano juu ya hilo, na tukaupitisha kwa mwanasheria ili uwe unatufunga sote kisheria, unaonaje?”
“Niko tayari kabisa Anti…mi’ nataka kubadili maisha yangu anti, na wewe ndiye unayenipa nafasi hiyo. Siwezi kuipoteza kwa kukusaliti!”
“Good!Kokos anashughulikia mkataba huo na leo jioni utakuwa tayari…sasa twende tukaanze mafunzo ya kuwa malkia wa urembo Candy…”
***
Wiki nne baadaye:
Warembo waliokuwa wakigombea taji la urembo wa Miss Dar City Centre walikuwa wamejiandaa kwa mpambano ule ambao ungetoa nafasi kwa mshindi kuingia katika kinyang’anyiro kikubwa zaidi cha kugombea taji la urembo wa taifa, maarufu kama Miss Tanzania. Miongoni mwao alikuwamo Candy Gamasala, msichana ambaye kabla ya mpambano ule hakuwa akijulikana kabisa katika medani za urembo nchini. Yeye alikuwa anaingia kwenye kinyang’anyiro kile baada ya wiki nne za mafunzo mazito na ya hali ya juu. Na ndani ya wiki nne zile alizokuwa akipata mafunzo ndipo picha zake pamoja na zile za wagombea wengine wa taji lile, zilipochapishwa kwenye magazeti na vyombo vya habari mbali nchini ikiwa ni sehemu ya kulinadi shindano lile na pia kuwanadi wagombea wale mbele ya jamii. Kama ilivyokuwa kwa wale wagombea wenzake, sura yake ikawa miongoni mwa sura zilizozoeleka machoni mwa watanzania hasa wafuatiliaji wa maswala ya urembo. Bishkuku alikuwa mwalimu mzuri, na akishirikiana na Kokos Wandiba alihakikisha kuwa Candy anakuwa tayari kwa siku ile. Mafunzo yake yalijumuisha namna ya kutembea kwenye ulingo wa urembo, mavazi, namna ya kujibu maswali ya majaji, na jinsi ya kuweka uso wenye tabasamu muda wote; jambo ambalo kwa Candy lilikuja bila hata ya kujilazimisha, kwani mrembo yule alikuwa na uchangamfu wa asili na mwenye tabasamu la aina fulani usoni mwake muda wote.
Kokos alihakikisha anamnoa ufahamu wake wa mambo ya historia ya tanzania na ulimwengu, ufahamu wa mambo mbali mbali na pia akimnoa uwezo wake wa lugha ya kiingereza.
Kwa upande wake,Candy alikuwa mwanafunzi mwenye ari kubwa, na aliwarahisishia sana kazi wakufunzi wake. Na ile siku ya shindano ilipofika, wakufunzi wake waliamini kuwa alikuwa tayari kukabiliana na mtihani ulio mbele yake. Lakini Candy alikuwa na wasiwasi mkubwa sana, na moyo wake ulikuwa ukimwenda mbio kuliko kawaida.
Shindano lilifanyika usiku wa siku ya Ijumaa na ukumbi ulifurika mashuhuda lukuki, Sanura na Tunis wakiwa miongoni mwao. Bishkuku alikuwa makini kwa kila kitu kilichotakikana kwa yule mrembo wake. Shindano lilianza na warembo kumi na saba waliojitokeza na kupasishwa kushiriki walianza kupita mmoja baada mwingine, na ilipofika wakati wa majaji kupitisha maamuzi, Candy alikuwa miongoni mwa wale warembo kumi waliovuka hatua ya kwanza. Ilikuwa ni furaha isiyo kifani kwa Bishkuku na Kokos Wandiba.
“Safi sana mwanadada! Nilikuwa nakuona ukivuka hatua ya kwanza hivi hivi! Una mvuto wa ajabu uwapo pale juu Candy, na sasa ni nafasi yako ya kujitengenezea njia ya kuuendea urembo wa taifa…hii sehemu ifuatayo ni ngumu zaidi, na inahitaji utulivu wa akili…” Bishkuku alimwambia Candy wakiwa kwenye chumba cha kubadilishia nguo.
Mchujo wa wale warembo kumi waliobakia ulijumuisha mavazi ya jioni, ufukweni na vazi la ubunifu. Bishkuku alikuwa amemtafutia nguo muafaka mrembo wake, na ingawa Candy alikuwa na aibu sana katika kuvaa vazi la ufukweni wakati wa mafunzo, kufikia muda huu alikuwa ameshazoea. Lakini ulipofika muda wa majaji kupitisha majina ya washindani watano kati ya wale kumi watakaovuka kuingia hatua ya fainali, Kokos na Bishkuku walihamanika pale majina ya waliovuka yalipozidi kutajwa pasina Candy kutajwa.
Akiwa nyuma ya jukwaa, Candy alijikunyata huku moyo ukimpiga wakati akisikia majina ya washiriki wenzake yakitajwa. Wa kwanza, wa pili, wa tatu…
Machozi yalianza kumlenganga.
Huku ukumbini Bishkuku na Kokos walitazamana kwa wahka.
Wa nne…
Kokos na Bishkuku walijikuta wakishikana mikono kwa nguvu, macho yao yakiwa yameelekezwa kwa yule mshehereshaji aliyekuwa akitaja majina ya washindani waliovuka hatua ile, mioyo ikiwaenda mbio, wakishindwa kuamini kile kilichokuwa kikitokea…
Nyuma ya jukwaa Candy alijiziba uso kwa viganja vya mikono yake, machozi yakimtiririka.
Si bahati yangu tena hii…na tangu lini yatima naye akapata ushiandi wa u-miss,kama si kujitamanisha visivyotamanika?
Aliinuka na kuelekea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo akiwa amekata tamaa.
“Na…wa tano ingawa si kwamba ndio wa mwisho kwa ubora, ni…Candy Gamasala!”
Bishkuku na Kokos waliruka kwa furaha huku wakipiga kelele za shangwe, muda huo huo wakishangaa kuona kundi kubwa la watazamaji nalo likiibuka kwa vifijo na hoi hoi huku wakisimama…
***
Nyuma ya jukwaa Candy alisimama ghafla na kubaki akiwa amepigwa butwaa, kisha aligeuka taratibu kuwatazama washindani wenzake.
“Candy…! Ni wewe! Jina lako…” Mmoja wa washiriki wenzake alimwambia. Kilichofuata baada ya hapo kilikuwa ni kama njozi tu kwake. Candy alikumbuka kuwa alijitokeza mbele kwenye ukumbi na kusimama pamoja na wale wenzake wanne, ilhali watazamaji waliofurika pale ukumbini wakiwa wamesimama huku wakipiga makofi, mbinja na ala mbali mbali za muziki vikirindima kutoka kila kona ya ukumbi ule.
Nimeingia fainali!
Akiwa amesimama pale jukwaani mbele ya maelfu ya watazamaji waliokuwa wakiwapigia makofi huku wakiwatazama kwa heshima na furaha kubwa, Candy Gamasala alihisi msisimko wa ajabu ukimtambaa mwilini. Alitembeza macho ukumbini huku bado akitabasamu kwa majivuno ya kilimbwende, kama jinsi alivyofundishwa na mkufunzi wake Bishkuku…
Bishkuku!
Alizungusha macho yake pale ukumbini na kumtazama yule mwanadada mtu mzima, na macho yao yaligongana. Bishkuku alikuwa akitabasamu kwa faraja iliyo wazi na katika macho ya mkufunzi wake yule, Candy aliona mng’ao uliotokana na mchanganyiko wa hisia. Walitazamana, wote wakitabasamu, na Bishkuku alibana midomo yake kwa nguvu huku akimtikisia kichwa kumuashiria kuwa alikuwa pamoja naye.
Candy alihamishia macho yake kwa Kokos Wandiba, mwanaume aliyeanza kwa kumuogopa, na ambaye sasa alikuwa akimuona kama rafiki wa karibu, na aliona jinsi mwanaume yule asiyeisha kumshangaza kila siku, alivyokuwa akimtazama kwa upendo na heshima iliyo dhahiri kabisa, huku akipiga makofi na akicheka kwa furaha.
Alirudisha macho yake kwa watazamaji waliofurika pale ukumbini, na alijikuta akistaajabu jinsi wale watu, ambao iwapo angekutana nao katika mazingira tofauti na yale, angewaona kuwa ni bora kuliko yeye kwa zaidi ya mara kumi, walivyokuwa wakimtazama yeye na wale washiriki wenzake wanne kwa heshima kubwa namna ile, na alihisi donge likimkaa kooni ilhali machozi yakianza kujivuta machoni mwake.
Ah, leo hii Candy mie ndio nimekuwa wa kuheshimiwa na kuthaminiwa namna hii…!
Alimeza funda kubwa la mate.
Leo napigiwa makofi nikiwa na wenzangu wanne hapa jukwaani…lakini nitahakikisha kuwa siku moja makofi haya n’takuwa napigiwa mimi tu hapa jukwaani …ipo siku…siku moja…one day!
Kutokea kwenye kiti kilichokuwa mstari wa pili kutoka mbele kabisa ya ukumbi ule, mwanaume mmoja mfupi mwenye mwili ulioshupaa alikuwa akimtazama Candy kwa makini na utulivu wa hali ya juu. Alikuwa amevaa suti ya bei ghali sana na mkononi alikuwa amevaa kijibangiri cha dhahabu. Na hata pale alipokuwa akimtazama namna ile, macho yake yaliyohifadhiwa na miwani ghali ya kusomea yalitoa mng’ao na kujifinya kwa kuongeza umakini.
***
Hatua ya fainali ilihusisha warembo wale watano kujibu swali moja kutoka kwa majaji, na baada ya hapo, majaji wangejumuisha alama walizopata warembo wale huko nyuma na zile watakazopata kwenye kujibu swali, na kuibuka na mshindi. Usahihi wa jibu, utulivu katika kujibu swali, na ufahamu wa mambo kwa ujumla ndivyo vilikuwa vigezo katika hatua hii. Warembo walirudi kwenye vyumba vya kubadili nguo, na mwanamuziki wa hip hop alipanda jukwaani kutumbuiza kwa muda.
“Okay mrembo wetu, hapa ndipo pa kutumia yote uliyojifunza kutoka kwa Kokos…zingatia sana…” Bishkuku alimwambia kwa msisitizo wakiwa kwenye chumba cha kubadilishia nguo, lakini kabla hajamaliza, Candy akamkatisha, “Kuelewa swali, kuwatazama majaji moja kwa moja usoni, na kutoonyesha kubabaika hata kama unajiona hutaweza kujibu swali uliloulizwa…” Alimalizia yale maneno ambayo alijua Bishkuku alitaka kumkumbusha, akimthibitishia kuwa alikuwa anayakumbuka vizuri maelekezo ya Kokos Wandiba.
.
Bishkuku aliachia tabasamu, “Na muda wote uwe na tabasamu usoni!” Alimkumbusha huku akimshika kidevu kwa utani. “Safi sana mrembo wangu…kila la kheri sasa…” Alimwambia huku akimkumbatia kwa muda kabla ya kutoka na kurudi kule kwa watazamaji wengine.
“Inaelekea mrembo wetu yuko tayari kwa hatua ya mwisho ya mpambano huu.” Alimnong’oneza Kokos huku akiketi kwenye kiti kando yake.
“Una hakika…?” Kokos aliuliza kwa mashaka.
“Yep…!”
Na ndivyo ilivyothibitika dakika ishirini baadaye pale ambapo baada ya kila mmoja wa wale warembo watano kuulizwa swali na majaji, na kila mmoja kujibu swali lake kwa namna ambavyo uelewa wake ulivyomtuma, mwenyekiti wa kamati ya shindano lile alipomtangaza Candy Gamasala kuwa mshindi wa taji la Miss Dar City Centre.
Ukumbi ulilipuka kwa hoi hoi kubwa sana, mbinja zikitawala huku na huko, Kokos Wandiba na Bishkuku walijikuta wakirukaruka ukumbini huku wakiwa wamekumbatiana kwa furaha. Hakukuwa na shaka kabisa pale ukumbini kuwa taji lilikuwa limekwenda mahala panapostahili.
Huku machozi yakimbubujika Candy Gamasala alijitokeza mbele huku akiwapungia mkono wananchi waliokuwepo pale ukumbini na kuvikwa taji lake.Kamera za wapiga picha za televisheni na wa magazeti mbali mbali zilikuwa zikifyatua picha mfululizo kwa ajili ya kulihabarisha taifa kesho yake juu ya tukio lile maridhawa.
Akiwa upande wa watazamaji Bishkuku alikuwa akibubujikwa machozi bila kizuizi wakati akimtazama mrembo wake akivikwa taji pale jukwaani. Akiwa amebetua midomo, Sanura Kashogi alimshika mkono Tunis na kuanza kumburura ili waondoke pale ukumbini, lakini naye alijikuta akikamatwa mkono wake wa pili na kuzuiwa.
“Hey kwani vip…”
“Mbona mbio namna hiyo Sanura, imekuwaje kwani?” Bishkuku alimuuliza huku akimtawanyia tabasamu la kimbea. Sanura alimkunjia uso kwa ghadhabu.
“Naomba uachie mkono wangu Bishkuku…”
Kabla hajamaliza kauli ile Bishkuku alikuwa ameshamuachia na alibaki akimtazama moja kwa moja usoni kwa macho ya kubeza. “Nendeni mkajiandae Sanura…tutakutana kwenye mpambano wa Miss Ti-Zedi sasa…” Alimwambia. Sanura alibetua midomo na kuondoka bila kumjibu huku akimvuta Tunis, ambaye alimgeukia Bishkuku kwa macho ya wasiwasi na tahayari. Bishkuku alimtolea tabasamu la upande lililojaa kebehi na dharau ya hali ya juu. Haraka Tunis aligeuka na kufuata kule alipokuwa akielekezwa na bosi wake mpya.
Kule jukwaani Candy Gamasala alikuwa akitoa shukrani zake kwa Mwenyezi Mungu, majaji, waandaaji wa kinyang’anyiro kile pamoja na wananchi wote waliofika kushudia tukio lile.
“…lakini zaidi ya yote napenda kumshukuru sana, sana, tena sana mkufunzi na mlezi wangu Anti Bishi…” Alisema huku akizungusha uso wake kujaribu kutafuta mahala Bishkuku alipo, na alipomuona alimnyooshea mikono yake. Bishkuku alijikuta akipanda pale jukwaani na mara alikuwa akimkumbatia yule binti aliyemnusuru kutoka kwenye janga la uchangudoa na kumfikisha kwenye medani ya umalkia wa urembo. Ukumbi ulilipuka kwa shangwe kubwa zaidi, na Candy aliugeukia ukumbi akiwa ameshikana na mkufunzi na muasisi wake. “…Anti Bishi ndiye aliyenitoa nilikokuwa na kunifikisha hapa leo hii…amenipa mafunzo na maelekezo yanayofaa na leo nimefanikiwa kuwa malkia wa urembo wa Dar City Center…” Akamgeukia Bishkuku, “Ahsante sana anti Bishi…hakika sina cha kukulipa na bado nahitaji sana msaada wako!” Kisha wakakumbatiana tena kwa hisia kali, wote wakitirikwa machozi ya furaha. Kufikia hapo watunza usalama pale ukumbini walikuja na kumchomoa Bishkuku kutoka kwa yule mrembo mpya wa kitongoji cha Dar City Center na Candy akabaki peke yake pale jukwaani.Aligonganisha macho na Kokos.
“Mwisho napenda nimshukuru sana mwalimu na mfadhili wangu mkubwa…bwana Kokos Wandiba…Ahsante sana Kokos…”
Kutokea pale alipokuwaamesimama Kokos alimpa ishara ya dole gumba huku akiwa amejawa na furaha ya hali ya juu.
Nusu saa baadaye, wote watatu walikuwa kwenye gari wakirejea nyumbani kwa Bishkuku wakiwa na zawadi kemkem zilizokuwa zimeahidiwa kwa mshindi wa taji lile, ikiwemo cheki ya shilingi milioni tano.
“Sasa bado taji la Miss Tanzania…” Bishkuku alisema kwa sauti ya chini iliyojaa hamasa. Hakuna aliyemjibu, ingawa wazo hilo ndilo lililokuwa likizunguka vichwani mwa Candy na Kokos wakati ule.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Bila ya wao kujua, gari jeusi aina ya Toyota Caldina, lilikuwa likiwafuatilia kwa nyuma tangu walipoondoka pale ukumbini usiku ule. Walipofika nyumbani kwa Bishkuku, wote waliteremka na huku wakisaidiana kubeba zile zawadi walizorudi nazo, waliingia ndani ya jengo lile bila ya kulitilia maanani lile gari jeusi,ambalo lilikuwa limeegeshwa upande wa pili wa barabara mbele ya lile jengo ambamo Bishkuku na Candy walikuwa wakiishi.
Yule mtu mfupi mwenye suti ghali alibaki akiwa ametulia nyuma ya usukani wa ile Caldina huku akilitazama lile jengo, na alipoona taa za madirisha ya gorofa ya kwanza ya jengo lile zikiwashwa dakika chache baadaye, alitikisa kichwa kwa namna ya kuridhika na kuondosha gari lake eneo lile.
***
John Koccho alifinya uso na kupepesa macho haraka haraka kama yaliyoingiwa na vumbi, kisha akayatumbua macho yake madogo na makali huku akili ikimwenda mbio pale utambulisho wa kile alichokuwa akikiona ulipojidhihirisha akilini mwake.
Haiwezekani…! Lakini…ndiye!
Alizidi kunyoosha shingo yake juu ya vichwa vya wale watu aliokuwa amesimama nao pale mbele ya meza ya muuza magazeti, wakidondoa vichwa vya habari vya magazeti mbalimbali, ili apate kuona vizuri.Lakini kila alivyojitahidi ndivyo jamaa walivyozidi kumziba.
Oh shit…isiwe taabu.
Alijipenyeza kwenye kundi lile hadi mbele kabisa ya ile meza, macho yake yakiwa kwenye ukurasa wa mbele wa gazeti moja la mambo ya udaku. Maandishi makubwa kabisa mbele ya ukurasa ule yalinadi habari ambayo bila shaka mhariri wa gazeti lile aliiona kuwa ni ya uzito wa juu sana kuweza kuuza gazeti lake kwa siku ile.
NI CANDY GAMASALA DAR CITY CENTER!
Kile kichwa cha habari hakikuleta maana yoyote kwake.Macho yake yalikuwa yameganda kwenye picha kubwa iliyochukua nusu nzima ya ukurasa wa mbele wa lile gazeti.Nipicha iliyomuonesha mrembo mpya wa taji la Miss Dar City Center akiwa amevaa taji lake kichwani na utepe uliokuwa ukimnadi kuwa ndiye mshindi wa taji lile ukiwa umepita begani kwake na kukatisha kifuani kwake. Ilikuwa ni picha kubwa iliyoishia chini kidogo ya kifua chake, na kwenye picha ile, yule malkia wa urembo alikuwa ameitazama moja kwa moja kamera ya mpiga picha wa gazeti lile huku akiwa ameachia tabasamu pana, macho yake yakiwa na mng’ao uliotokana na machozi ya furaha yaliyokuwa yakimbubujika ilhali akiwa ameinua kiganja cha mkono wake wa kushoto kuwapungia watu waliokuwa wakimshuhudia wakati akikabidhiwa taji lile.
Akili iliacha kumwenda mbio John Koccho, na sasa moyo wake ukaanza kumwenda mbio huku akili yake ikianza kufanya kazi haraka haraka lakini kwa umakini kama ifanyavyo siku zote anapokuwa amekabiliwa na jambo zito mbele yake.
It’s her gaddemmit…ni yeye!
Hapo hapo alifanya kile ambacho akili yake ilimtuma kwa kulinunua lile gazeti na kuondoka haraka mahala pale.Saa mbili baadaye alikuwa miongoni mwa abiria waliokuwa wakisafiri kwa basi kutokea Sumbawanga kuelekea Dar es Salaam, lile gazeti likiwa mkobani mwake…
***
Wiki zilizofuatia ushindi wake zilikuwa ni za heka heka nyingi sana kwa Candy. Yeye na washindi wa vitongoji na mikoa mingine walitakiwa kushiriki kwenye matukio mbalimbali ya kitaifa kwa namna ya kuwanadi mbele ya jamii. Walitembelea viwanda na makampuni mbalimbali makubwa ambayo kwa namna moja au nyingine yalikuwa yamedhamini mashindano ya kumtafuta mrembo ya taifa, Miss Tanzania, yaliyopangwa kufanyika miezi michache baadaye.
Walitembelea nyumba za watoto yatima, walishiriki kwenye kazi za kujitolea kwenye mashule mbalimbali, walitembelea hospitali kadhaa na kuwafariji wagonjwa ikiwa ni pamoja na kutoa misaada ya vyakula, madawa na vyandarua. Yote haya yalizidi kumpa Candy upeo mkubwa wa ufahamu wa mambo, naye aliyahifadhi akilini kwake kama akiba ya baadaye.
Katika harakati zote hizi, alijikuta akilazimika kushiriki bega kwa bega na Tunis, mrembo wa Temeke aliyemsaliti Bishkuku hapo awali; na tangu siku ya kwanza, Tunis alionesha kumchukia na kumtupia vijembe vya hapa na pale. Kwa upande wake, Candy hakumfuatilia wala kutilia maanani vijembe vyake.
Moja kati ya harakati hizi ilikuwa ni kuhudhuria dhifa maalumu iliyoandaliwa na wadhamini wakuu wa shindano la miss Tanzania wakishirikiana na Kamati ya Miss Tanzania nchini. Mabinti wote waliofuzu kushiriki shindano lile kubwa kabisa la mabinti wa urembo nchini walitakiwa kuhudhuria, na wote walifanya hivyo. Kama kawaida yake, Candy aliambatana na mkufunzi na muasisi wake Bishkuku, pamoja na mdhamini wao Kokos Wandiba.
Dhifa ilifanyika kwenye ukumbi mwanana wa The Slipway ambapo pamoja na waalikwa mbalimbali katika dhifa ile, pia walikuwako watu wengine mbalimbali wasio waalikwa waliofika kwenye hoteli ile maarufu kwa ajili ya kujiburudisha.
Mabinti wa urembo waliohudhuria dhifa ile walikuwa kivutio kikubwa kwa wote walikuwako pale hotelini usiku ule, waalikwa na wasio waalikwa. Kwa kuwa dhifa ile ilikuwa katika mfumo wa mchapalo, au cocktail party, waalikwa walikuwa wakiranda huku na huko mle ukumbini wakiwa na vinywaji vyao mikononi huku wahudumu wakiwa makini kila kona kuhakikisha kuwa hakuna mualikwa anayekaukiwa kinywaji.
“Sasa tena usijibugize mi-laga hapa mpaka tuanze kukukokota hivyo, maana we’ ukishaona pombe unakuwa kama uliyepagawa!” Bishkuku alimuasa Kokos, ambaye alimtupia jicho Candy na kumgeukia dada yake.
“Acha kunisimanga kwa vinywaji vya kualikwa Bishi! N’takunywa kidogo tu kuondoa balaghamu, baada ya hapo itakuwa ni juisi tu.”
Candy aliwacheka mtu na nduguye huku akiwa ameshikilia gilasi ya kinywaji kisicho na kilevi. Muda huo wakaja warembo wenzake wawili na kuungana nao. Aliwatambulisha wale wenzake kwa akina Kokos, kisha akaondoka na wale wenzake kujichanganya na warembo wengine pale ukumbini. Kokos na Bishkuku walimtazama jinsi alivyokuwa akiondoka na wale wenzake.
“Hebu mtazame yule binti Kokos…yaani kama hakuchukua taji la Miss Ti-Zedi mwaka huu basi kweli nitaamini kuwa nchi hii imejaa wachakachuaji!” Bishkuku alisema.
Kokos aliinua juu gilasi ya kinywaji iliyokuwa mkononi mwake.
“Amen to that!” Alisema na kubugia kile kinywaji chote kwa funda moja, na hapohapo akamdaka mhudumu aliyekuwa akipita na sinia lenye bilauri zilizosheheni vinywaji na kujinyakulia bilauri nyinginehuku akiiweka ile bilauri yake tupu kwenye lile sinia. Aliendelea kumtazama binti yule mwenye mvuto huku akiipeleka kinywani ile bilauri yake ya pili.
Ambalo hakulijua ni kwamba si yeye na Bishkuku tu waliokuwa wakimtazama Candy akiondoka na wale warembo wenzake pale ukumbini wakati ule.Watu wengine watatu nao walikuwa wakimfuatilia binti yule kutokea kwenye maeneo tofauti ya ukumbi ule.
Kutokea kwenye kaunta ya wateja iliyokuwa kwenye kona moja ya ukumbi ule, John Koccho alikuwa akimtazama binti yule kutokea chini ya ukingo wa kofia yake ya pama, akiwa anaihudumia bilauri ya bia ya safari aliyoinunua huku moyo ukimuuma kwa ughali wa kinywaji kile kwenye hoteli ile yenye hadhi.
Bila Candy wala John Koccho kujua,mtu mfupi mwenye mwili uliojengeka kikakamavu aliivuta vizuri suti yake ghali yenye rangi ya kahawia na kujigeuza taratibu kwenye kiti alichokuwa amekalia kwenye eneo la maakuli la ukumbi ulena kujiweka katika mkao ambao ulimuwezesha kufuatilia vizuri zaidi nyenendo za Candy mle ndani huku akidokoa-dokoa saladi iliyokuwa mbele yake kwa uma.
Baada ya kurandaranda ukumbini kwa muda, Candy alimkabidhi mmoja wa wale wenzake ile bilauri yake ya kinywaji.
“Hebu nish’kie kinywaji changu…naenda kujisaidia…” Alimwambia.
“Pouwa, ila hakikisha unajisaidia ki-miss huko…” Miss Mtwara, ambaye tayari kinywaji kilishaanza kumuelemea alimwambia, na wote wakaangua kicheko.
Candy aliingia kwenye eneo nadhifu la msalani huku bado akitabasamu kutokana na ule utani wa Miss Mtwara na kujifungia kwenye moja ya vyumba vidogo sita vya kujisaidia.Muda huo alisikia mtu mwingine akiingia mle msalani na kujifungia kwenye choo cha pembeni yake. Alipomaliza haja zake alitoka kule chooni na kwenda kwenye moja ya mabeseni sita ya kunawia mikono yaliyokuwa nje ya vile vyoo ndani ya ule ukumbi mdogo wa pale msalani na kuanza kuosha mikono yake.
Kutokea nyuma yake alisikia mlango wa choo kingine mlendani ukifunguliwa na hatua hafifu zikielekea kwenyemlango wa kutokea nje ya eneo lile la msalani, lakini alishituka aliposikia ule mlango ukikomewa badala ya kufunguliwa. Aligeukakule mlangoni na kupatwa na mshituko mkubwa huku akipeleka mikono yake mdomoni kama namna ya kujizuia asipige ukelele wa woga.
“Hello, helloo mlimbwende wa Dar City Centre…remember me?” Jackie alimuuliza huku akimsogelea taratibu hali akimtazama kwa hasira.
“Ja…Jackie…? Un…afanya nini huku? Yaani umenishtua!” Alimuuliza na kumwambia huku akimtazama kwa mashaka.
“Oh Yeah? Kwa maana kidampa, chokoraa na changudoa kama mimi ninafanya nini huku kwa watu wa matawi ya juu wenye urembo uliotukuka kama wewe na wenzako kule, sio?” Jackie alimuuliza kwa kejeli huku akiashiria kule mlangoni kwa kidole chake cha gumba.
“Mnh, sasa ndio maneno gani hayo Jackie! Mi’ sikutegemea kukuona huku nd’o maana nikakuuliza vile, na …are you alright? Halafu mbona umekomea mlango…?”
Jackie alichia kicheko cha kejeli.
“Mnhu! Eti ‘aa yuu oow rhwaait?’ ” Alimuigiza kwa kubana sauti kidogo, kisha akaendelea huku akitikisa kichwa, “Ama kweli duniani kuna mambo. Yaani leo Candy, Changudoa wangu mwenyewe, ananisemesha kizungu mie?”
Candy alimtazama kwa mshangao, kisha ikamfunukia kuwa uwepo wa Jackie mle msalani wakati ule sio tu haukuwa wa bahati mbaya bali pia haukuwa wa heri hata kidogo. Alijaribu kumpita pembeni ili auendee mlango wa kutokea mle msalani, lakini Jackie alimdaka shingoni kwa nguvu na kumgandamiza ukutani huku akiwa amemuwekea mkono kooni.
“Not so fast wewe! Na mi’ pia najua maneno ya kizungu, upo?”Jackie alimkoromea. Macho yalimtoka Candy na alijitutumua kutoka kwenye himaya ya Jackie pale ukutani.
“Hebu niache bwana, we’ vipi? Unaniumiz…”
“Shut-up, na unisikilize wewe! Sina muda wa kupoteza zaidi,kwani nataka kuwahi viwanja mimi saa hizi…natumai unaikumbuka ofisi yako ya zamani? Viwanja? Kabla hujapanda cheo kutoka changudoa wa walala hoi kule kinondoni makaburini hadi kuwa changudoa wa majaji wa miss Dar City Centre?”Jackie alizidi kumkoromea.
“Sio changudoa mimi Jackie,na nakuomba uniachie mara moja!” Candy alimkemea na kumsukuma kwa nguvu. Jackie aliyumba na kujikuta akitaka kuanguka,kisha kabla Candy hajajiweka sawa, akamrukia na kumbana tena pale ukutani.
“Okay, naondoka sasa hivi bibie usijali…lakini elewa una saa ishirini na nne kunipatia milioni mbili ama si hivyo nchi nzima itajua kuwa miss Dar City Centre wao si lolote zaidi ya changudoa mzoefu!”
Khah!
Macho yalimtoka Candy.
“Jackie una wazimu? Sote twajua kuwa hilo si kweli! Kwa taarifa yako sijawahi kabisa kuufanya huo uchangudoa uliokuwa ukinilazimisha niufanye…mola ameniokoa kwa hilo, ingawa siwezi kusema hivyo kwa upande wako! Let me go now, kabla sijaanza kupiga kelele humu, au kabla watu hawajatukuta hapa!” Alimkemea kwa ukali, sasa naye akiwa ameghadhibika.
Kwa muda walibaki wakitazamana huku wakitweta, kisha bila ya kusema neno Jackie alitoa simu ya kiganjani na kumuonesha picha iliyokuwa kwenye simu ile.
“Okay, fikiria juu ya madhara yatakayotokea kwako na kwa wadhamini wako wakati picha hii itakapoyafikia magazeti ya udaku…au itakapoenea kwenye mitandao ya intaneti na facebook, halafu ndio uniambie kuwa mola amekuokoa na uchangudoa, malaya wa chekechea we!” Alimwambia kwa sauti ya kuogofya, akimrushia harufu ya pombe aliyokunywa huko alikotoka.
Macho yalimtoka pima Candy na kubaki akiikodolea macho ile picha iliyokuwa kwenye uso wa ile simu huku akihisi kichwa kikimuelea. Jackie alimsukumizia ile simu mikononi,naye kama zuzu alijikuta akiipokea huku bado akiwa ameikodolea macho ile picha iliyokuwa kwenye ile simu.
Jackie alimuacha na kwenda kuufungua ule mlango wa kuingilia mle msalani, kisha akamgeukia akiwa pale mlangoni.
“Twenty four hours, changudoa wangu. Muda huo ukipita nami sina Milioni mbili mikononi mwangu…unajua kitakachotokea.”
Candy aliinua uso na kumtazama kwa simanzi isiyo kifani.
“Lakini Jackie…hii si kweli! Ume…umeipata wapi hii picha…I mean how…?”
“Si kazi yangu hiyo. Utakaponikusanyia hiyo pesa, unajua pa kunipata…”
“Kwa nini unanifanyia hivi lakini…nimekukosea nini?”
Jackie alimtazama kwa muda, badala ya kumjibu alimwambia, “Tena wala usijidanganye eti kwa kuwa nimekuachia hiyo simu ukadhani unaweza kuifuta na kupoteza ushahidi…utacheza patapotea mbaya sana mrembo. Nina nakala kibao za hiyo picha, na hicho kimeo nimekuachia kama kumbukumbu, nikishapokea milioni mbili zangu n’tanunua Blackberry…Chaoo!” Alimjibu na kutoka nje, akiufunga mlango taratibu nyuma yake.
Candy akijikuta akichutama pale msalani bila kujitambua huku akiikodolea macho ile picha.
Ilikuwa ni picha iliyomuonesha yeye akiwa katika mavazi ya kichangudoa hali akiwa ameirembulia macho kamera, pembeni yake machangudoa wengine watatu wakiwa wanaichekea kamera.
Alihisi kuta za mle msalani zikimzonga na kumbana kutokea kila upande.
***
Nitapata wapi milioni mbili mimi jamani? Nimwambie Anti Bishi? Sina jinsi…itabidi nimwambie tu…lakini nitaanzia wapi huko kumwambia?
Alikuwa akijiwazia peke yake huku akirejea kule kwenye ukumbi wa tafrija, mawazo yakiwayamemzonga na akijihisi kuchanganyikiwa.
Nuru ya matumaini ilishaangaza maisha yangu…sasa inakuja kuzimwa kirahisi namna hii jamani! Kwa nini?
Akiwa katika mkanganyiko ule wa mawazo huku akipishana na baadhi ya waalikwa waliokuwa wakizagaa na bilauri zao za vinywaji huku na kule pale ukumbini, hakuweza kumuona yule mtu mwenye suti ya kahawia aliyekuwa akimvizia atoke kule msalani. Jamaa alikuwa akimwendea kutokea mbele yake huku akiwa na dhamira thabiti dhidi yake, mkononi akiwa ameshika kwa uficho bomba la sindano lenye kimiminika hatari.
Na hata nikiweza kumpatia hiyo milioni mbili aitakayo, nitakuwa na uhakika gani kuwa hataibuka tena baada ya wiki,mwezi, miezi mitatu au sita na kudai tena hela nyingine?
Sasa kulikuwa kuna hatua tano tu baina yake na yule mtu mwenye suti, ambaye alilikamata vizuri lile bomba la sindano tayari kumdunga.
“There you are!Miss gani unayekaa chooni miaka? Unatuaibisha ma-miss namna hii!” Mawazo yake yalikatishwa na Miss Mtwara aliyemwambia huku akimshika bega na Candy aliruka kwa mshituko. Jamaa mwenye suti alikenua meno kwa hasira na kupitiliza bila kuwatazama, akilitumbukiza kwenye mfuko wa koti lake lile bomba la sindano lenye kimiminika hatari.
Worry not mrembo. Umeponea tundu la sindano this time…tutakutana tena tu kisura!
“Ah, no…na…nahisi sijisikii vizuri…naumwa!” Candy alidanganya.
“Duh, pole sana mrembo! Sasa…?”
“Usijali…n’tamudu tu…” Candy alimjibu huku akiketi kwenye moja ya makochi yaliyokuwa pale ukumbini, kichwa kikimzunguka juu ya ule mtego aliotegwa na Jackie.
“Ngoja nikakutafutie msaada shosti, usije ukatuangukia hapa ikawa stori magazetini…!” Miss Mtwara alimwambia, lakini wala Candy hakumsikia.
Hivi Jackie ananitaka nini mimi lakini? Ina maana nd’o n’taendelea kuwa mnyonge wake siku zote mimi?
Hakumtilia maanani John Koccho aliyefika na kuketi kando yake pale kwenye lile kochi refu huku akimtupia jicho la pembeni.
Ndio maana Bishkuku alikataa kabisa kumchukua pamoja nami…alijua atakuwa habari mbaya kwangu…na kweli!
“Vipi Candy…nasikia hujisikii vizuri?”Bishkuku alimkatisha mawazo yake huku akiketi pale kwenye kochi, baina yake na John Koccho. John Koccho aliendelea kuketi pale pale akiwa ameshusha pama lake na ameinamisha kichwa.
“Ndio…yeah…tumbo linanikata kweli, Anti Bishi…nani kakwambia?” Candy alishtuka na kujibalaguza.
“Mmoja wa hawa warembo wenzako…nadhani ni miss Mtwara yule…”
Muda huo Kokos naye alifika. Alimtazama John Koccho aliyeendelea kujiinamia huku amekunja nne pale kwenye kochi, kisha akawageukia akina Candy.
“Yaani limenianza ghafla tu, hata sijui ni nini…tuondoke Anti Bishi, siwezi kabisa…” Candy alilalama.
“Okay, twendeni moja kwa moja hospitali basi!” Kokos alisema.
“Yeah, lakini ni lazima tuwataarifu waandaji wa shughuli hii ili wajue…hivi vitu huwa vinazingatiwa na majaji bwana. Huwezi kuchoropoka tu kwenye shughuli kama hii kama unaenda ukweni…” Bishkuku alisema, na Candy akamakinika.
“Majaji…? Kuna majaji hapa?”Aliuliza.
“Majaji wa shindano gani sasa, wakati watu taji tumeshatwaa Bishkuku?”Kokos naye alimjia juu. Bishkuku alifunua kinywa kutaka kuwajibu, na hapo ndipo alipogundua kuwa kulikuwa kuna mtu mwingine pale kwenye kochi pamoja nao. Alimtazama John Kochho aliyejikunja pale kwenye kochi, kisha akainuka bila kujibu, akimuinua Candy pamoja naye. Wote wakajitenga pembeni pale ukumbini.
“Naongelea majaji wa shindano kubwa la Miss Tanzania bwana!” Aliwaambia walipokuwa mbali na John Koccho.
“Sasa kwani majaji wameshatangazwa?”Candy aliuliza, macho yakiwa yamemtoka. Bishkuku alitikisa kichwa kwa masikitiko.
“Majaji hawajatangazwa, ila kufikia sasa watakuwa wameshachaguliwa. Na hapa wapo…huenda hata yule jamaa aliyeketi nasi pale kwenye kochi akawa mmoja wao…”
Wote walijikuta wakigeukia pale kwenye kochiwalilokuwa wamekalia muda mfupi uliopita.
Kochi lilikuwa tupu.
Wakatazamana.
“Kwa hiyo kama wapo hapa…?”
“Wanachunguza tabia za kila mmoja wa warembo waliopo.Unafikiri hii shughuli huwa inaandaliwa hivi hivi tu? Upembuzi wa warembo huanzia kwenye sehemu kama hizi. Kule kwenye shindano lenyewe ni kujumuisha tu alama zote alizopata mrembo kuanzia kwenye matukio kama haya…” Bishkuku alizidi kufafanua.
“Sasa mbona hukuniambia mapema Bishkuku jamani?”Candy alilalama.
“Kwa sababu unatakiwa uwe na uhalisia mrembo, sio kuja kuigiza tabia usizonazo hapa. Majaji wamefundishwa jinsi ya kumsoma mtu mwenye kuigiza tabia njema na mwenye tabia njema kiukweli!”
“Lakini ulipaswa utuambie mapema, Bishi!”Kokos alidai.
“Ningekuwa nimechukua binti mapepe ningefanya hivyo…lakini namuamini mrembo wangu. Ila yule mwenzako aliyekuja kunipa habari za kuugua kwako yule…”
“Miss Mtwara?”
“Yule atapoteza pointi hapa, maana tayari yuko bwii!”
“Heh!” Candy aligwaya, akilini akifikiria nivipi ingekuwa iwapo mmoja wa hao majaji waliojichanganya pamoja nao pale ukumbini angekuwa mle msalani wakati akikabiliana na Jackie, na kusikia yale majibizano yao.
Mwili ilimsisimka.
“Okay…kaage basi kwa hao waandaaji wa tukio, tusepe!” Kokos alimwambia Bishkuku, ambaye alienda kutekeleza hilo na kuwaacha wao wakimsubiri.
Dakika tano baadaye, watatu wale waliongozana kuelekea kwenye lango la kutokea nje ya ukumbi ule mwanana.
Kutokea kwenye nguzo aliyokuwa ameigemea mle ukumbini huku akiwa na bilauri ya bia mkononi, John Koccho alikuwa akiwatazama kutokea chini ya ukingo wa pama lake. Kinyume na yule mtu mkakamavu mwenye suti ambaye naye aliyekuwa akiwaangalia watatu wale kutokea upande mwingine wa ukumbi huku akiwa ameuma meno kwa ghadhabu, yeye alikuwa akitabasamu.
***
Ingawa alijisikia vibaya kuwadanganya wafadhili wake namna ile, Candy aliendelea kujitia anaumwa wakati wakionana na tabibu, na kuandikiwa dawa. Muda wote akili ilikuwa ikimzunguka kuhusu kile kitisho alichopewa na Jackie. Kufikia muda ule akili yake ilikuwa ikivutana na maamuzi mawili makubwa.
Niwaambie akina Bishkuku?
Au nisiwaambie?
Nisipowaambia na Jackie akatimiza lile alilokuwa amenitishia…si ndio utakuwa mwisho wangu jamani?
Na Bishkuku atanielewaje?
Si ndio nitakuwa nimemsaliti vibaya kuliko hata alivyosalitiwa na Tunis?
Tunis!
Wazo la Tunis lilimfanya amkumbuke Sanura Kashogi, mpinzani mkubwa wa Bishkuku.
Sasa hapo si ndio nitakuwa nimempa ushindi Sanura dhidi ya Bishkuku?
Lakini Bishkuku amekuwa mtu mzuri sana kwangu, hastahili kusalitiwa kwa namna yoyote ile!
Mawazo haya yalimfanya azidi kunyong’onyea, na muda Bishkuku alipowaacha na Kokos kwenda kumchukulia dawa baada alizoandikiwa na tabibu pale hospitali, alijikuta akimgeukia Kokos.
“Kokos…”
“Yes, Candy, unasemaje…”
“Kuna…jambo linanisumbua, na sijui nilitatue vipi…” Alisema kwa mashaka, na Kokos akawa makini.
“Okay, ni jambo gani hilo Candy…na…unadhani naweza kuwa na msaada kwalo…?”
Lakini Candy alishindwa kuendelea. Aliinamisha kichwa kwa tahayari.
Oh, Mungu wangu…nazidi kulikoroga sasa!
“Okay, twendeni sasa!” Bishkuku alisema akiwa na kifuko cha dawa mkononi.
Afadhali!
Candy aliinuka na kuongoza haraka kuelekea kwenye gari, akiwaacha Kokos na Bishkuku wakimfuata nyuma, Kokos akiwa na uso ulijaa maswali.
Alitaka kuniambia nini?
Hakutaka Bishkuku ajue hilo alilotaka kuniambia? Ni lipi hilo?
Hakuelewa kabisa.
Wakiwa ndani ya gari kuelekea nyumbani kwa Bishkuku, Candy alijiegemeza kwenye kiti cha nyuma alipokuwa amekaa peke yake na kulaza kichwa chake kwenye mgongo wa kiti kile huku akiwa amefumba macho. Kutokea nyuma ya usukani kule mbele, Kokos alikuwa akimtumpia macho mara kwa mara kwa kutumia kioo cha kuonea nyuma kilichukuwa kule mbele.
Jackie amenipa saa ishirini na nne nimpatie milioni mbili…la si hivyo ananiharibia maisha yangu.
Alizidi kujiwazia.
Ni kwamba nina saa ishirini na nne za kupata namna ya kujinasua kutoka kwenye mtego huu alioninasisha kwa lazima, mshenzi yule!
Alijikuta akimchukia sanayule dada ambaye alianza kwa kumpenda na kumuamini, kabla ya kuja kumjua undani wake baada ya kuja hapa jijini.
Walipofika mtaa wa Aggrey, Kokos aliwaacha wateremke naye akabaki ndani ya gari lake. Walipoanza kuelekea ndani ya jengo lao, alimwita Candy.
“Er, Candy…”
Candy aligeuka na kurudi pale kwenye garo, moyo ukimwenda mbio.Bishkuku hakusubiri.
“Ulitaka kuniambia kitu kinachokutatiza…ulitaka kuniambia tukiwa peke yetu?” Alimuuliza huku akimtazama kwa makini, kwa mara nyingine mvuto wa yule binti ukimatahini kupita maelezo.
“Oh, na…nadhani nitakuwa okay tu, Kokos…ipotezee tu.” Candy alimjibu na kugeuka kuelekea ndani ya jengo alilokuwa akiishi na Bishkuku kwa mwendo wa haraka.
Kokos alibaki akimkodolea macho huku akiwa amepigwa na butwaa.
***
***
Usiku ule Candy hakulala. Alijilaza chali kitandani akiwa amefumbata viganja vya mikono yake nyuma ya kichwa chake, akili yake ikimuwaza Jackie na ule usaliti mkubwa aliomfanyia. Mara kwa mara alijikuta akiitazama ile picha iliyokuwa kwenye simu aliyoachiwa na Jackie na alijikuta akishangaa ni jinsi gani Jackie alivyokuwa na nia mbaya naye kiasi cha kumjia na jambo kama lile.
Siwezi kuacha nafasi hii ya kujipa heshima kwenye jamii inipotee kwa jambo la kutengenezewa kama hilli…siwezi!
Alilala chali kitandani kwake namna ile kwa muda mrefu, akisikia harakati mbali mbali za usiku zilizokuwa zikiendelea huko chini nje ya jengo lao . Magari yalikuwa yakipita, honi zikipigwa, muziki kutokea kwenye baa iliyokuwa pale jirani ukisikika..ilikuwa kama vile ni mchana na si usiku.
Kufikia saa tisa usiku, Candy alipitisha uamuzi.
***
Kokos Wandiba naye hakupata usingizi usiku ule.
Ni nini Candy alichokuwa akitaka kumwambia, ambacho kwanza hakutaka Bishkuku akijue, nakisha akaamua kuacha kabisa kumwambia?
Alikumbuka jinsi yule binti mwenye urembo uliotukuka alivyoinamisha kichwa kwa tahayari pale alipotaka kumwambia lililokuwa likimtatiza kabla Bishkuku hajafika pale walipokuwa, hospitali usiku ule.
Dah! Ni nini alitaka kuniambia yule?
Je, itakuwa ni lile lile linalonitatiza mimi? Je na yeye ana hisia za utashi kwangu kama jinsi mimi nilivyokuwa na utashi kwake?
Alijikuta akitabasamu peke yake kitandani.
Usijali Candy, tutapata tu muda wa kuyafanyia kazi mambo yanayotutatiza…
***
Jackie alijitupa huku na huko kitandani, usingizi mzito aliorudi nao kutoka viwanja ukishindana na hali isiyo ya kawaida iliyomvamia pale kitandani. Harufu ya mafuta ya taa ilikuwa ikimzonga kutoka kila upande, na alikuwa akijilazimisha kuamka wakati usingizi nao ukilazimisha kuendelea kuzidhibiti fahamu zake.
Alijigeuza kutoka upande mmoja kwenda mwingine huku uso ameukunja kutokana na ile harufu kali iliyozidi kumzonga, na hapo tena akahisi kitu kingine. Unyevunyevu wenye kukera ulikuwa umetanda kwenye godoro lake.
Amejikojolea?
Alijigeuza na kulala kifudifudi akiwa uchi wa mnyama pale kitandani, na hapo ukali wa ile harufu mbaya ya mafuta ya taa ukazizonga fahamu zake zote, na bila kupenda alijiinua ghafla na kubaki akiwa amepiga magoti pale kitandani huku akikohoa na kutupa pumzi nje kwa nguvu. Aliinua kiganja chake na kukitazama kwa mshangao pale alipoona kimelowa mafuta ya taa.
“Akah!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alilibonyeza lile godoro kwa mkono wake na kushuhudia jinsi lilivyotota kwa mafuta ya taa. Akili ikimzunguka, alijigeuza haraka pale kitandani na kuketi tayari kujiandaa kuteremka kutoka pale kitandani, na hapo aliachia kiyowe chembamba cha mshituko pale alipoona kuwa kulikuwa kuna mtu aliyekuwa amejitanda khanga mwili mzima akiwa ameketi kwenye stuli iliyowekwa mbele ya kitanda chake mle ndani.
E bwaba we!
Na hata pale alipokuwa ameshituka namna ile yule mtu aliwasha kiberiti cha gesi kilichokuwa mkononi mwake, na mwale mkali wa moto ukaangaza kile chumba kwa muda, kisha ukazima.
“Wew!Nan…nani wewe!” Jackie alimaka kwa woga usiomithilika, usingizi na pombe alizorudi nazo kutoka viwanja vikimyeyuka haraka sana, mwili wote ukimlegea.
Yule mtu hakumjibu.
Alibaki akiwa akimtazama tu jinsi alivyokuwa akihamanika bila nguo pale kitandani. Jackie alijitahidi kumchungulia Yule mtu ili amuone lakini kiza cha alfajiri kilichotanda mle ndani hakikumuwezesha kuona vizuri.
“Please…ni nani wewe…!” Alibwabwaja huku akilia kwa woga uliothibiti.
Na hapo yule mtu aliikwapua khanga aliyokuwa amejitanda kichwani na kuitupia pembeni, kisha haraka akainuka na kuwasha taa yamle ndani.
Mshangao, woga na taharuki alivyokuwa navyo Jackie hapo awali viliongezeka maradufu.
“Ww…wewe!”Alimakakwa kihoro, macho yakiwa yamemtumbuka hadikiwango cha mwisho kabisa cha utumbukaji.
“Yes, ni mimi Jackie, remember me?” Candy alimjibu akiwa amesimama kando ya kile kitanda huku ameshika kile kiberiti cha gesi mkononi, machozi yakimbubujika, midomo ikimtetemeka. Chini ya zile khanga alizokuwa amejitanda, alikuwa amevaa suruali na fulana za mazoezi, na miguuni alikuwa amevaa viatu vya raba.
“Un…unafanya nini hapa…?” Jackie alimuuliza kwa kutojiamini huku akianza kuteremka pale kitandani, na akahamanika pale alipogundua kwamba mguu wake mmoja ulikuwa umefungwa kwa mmoja wa mikanda yake ya nguo iliyokuwa mle ndani, na kufungiwa kwenye tendegu la kitanda kile.
Aliinua uso wake na kumtazama Candy kwa taharuki.
“Candy! Ni…ni vipi kwani…?”
“Tulia hapo hapo unisikilize Jackie!” Candy alimkemea huku akilia, naJackie alitumbua macho zaidi kwa mshangao. Hakika Candy aliyesimama mbele yake muda ule hakuwa Candy yule aliyezoea kumtia tashtiti na kumuonea atakavyo. Huyu alikuwa amebadilika kabisa.
Hata hivyo, alijitahidi kujitutumua.
“ Yaani we’ unakuja kunitilia kibesi kwenye anga zangu mimi?”Alimkoromea.
“Nazitaka hizo picha nyingine, Jackie…na nazitaka sasa hivi, la sivyo haki ya Mungu nakuwasha moto!” Candy alimwambia huku akishindana na kilio kilichotokana na mchanganyiko wa hasira na woga wa kile alichokuwa akikifanya wakati ule.
“Sina picha…!” Jackie alijibu huku akikitupia jicho la woga kile kiberiti cha gesi kilichokuwa mkononi mwa yule mrembo mwenye ghadhabu.
Candy alitaka kumjibu, akaghairi.
Alibaki akimtazama kwa hasira, kisha akashusha pumzi ndefu na kujilazimisha kutuliza jazba iliyokuwa ikimuelemea. Alirudi hadi pale kwenye ile stuli na kuketi huku akimtazama moja kwa moja usoni kwa macho yasiyokuwa na shaka hata kidogo.
“Sikiliza Jackie…tena unisikilize vizuri sana!” Alimwambia kwa sauti ya chini iliyojaa ithibati, na Jackie akagwaya alipoona kuwa Candy hakutishika kabisa na ule mkwara wake.
“Umekuja kunitishia amani maishani mwangu, ukijua kabisa kuwa nimepata nafasi moja tu ya kubadili mwelekeo wa maisha yangu…ukataka kunipokonya nafasi hiyo kwa hila zisizo na ukweli wowote…”
Jackie alimeza funda la mate na kubaki akimtazama kwa kutoamini.
“Sasa hilo ni kosa kubwa sana Jackie, kwani limenifanya na mimi niamue kuipigania nafasi yangu hiyo kwa nguvu zote!”
“Candy…”
“Kimya!” Candy alimkemea na Jackie akaguna kwa mshangao.
“Mimi najua ni muda gani huwa unarudi kutoka viwanja, na jinsi gani unavyolala kama gogo ukitoka huko. Leo nimekuja na kuingia humu ndani we’ huna hata habari. Nimekufunga mkanda mguuni nawe bado hukuwa na habari…”
Uso wa Jackie ulikuwa ukisajili woga uliokuwa ukiongezeka kadiri Candy alivyokuwa akizidi kumweleza.
“Nimekimwagia mafuta ya taa hicho kitanda nawe bado hukuwa na habari…nikakaa hapa kwenye stuli na kukutazama ukiwa unakoroma hapo kwa robo saa nzima kabla hujaamka…”
“Candy…”
“Kimya! Mi’ nimekuja nahayo mafuta ya taa na hiki kiberiti…” Candy alisema na hapo akakiwasha tena kile kiberiti, nacho kikatema mwale mkali wa moto, “…ili nikuchome moto ukiwa umelala hapo kitandani kwako nami nipotee…na nilikuwa na muda wa kutosha sana kufanya hivyo na kutoweka, bloody fool wewe!”
Jackie alitoa sauti ya mgwayo mkubwa.
“Lakini sikufanya hivyo leokwa vile tu bado nilikuwa nahitaji kuongea nawe…na ninachotaka kukiongelea ni ile picha uliyoniachia kwenye kile kimeo chako…” “Candy mdogo wangu…”
“Shut-up, Jackie! Najua ile picha itakuwa imepigwa siku ile ile uliyonilazimisha kwenda nawe viwanja, nisichojua ni kwamba ilipigwa na nani na muda gani. Sasa nataka unieleze ni jinsi gani ilikuwa mpaka ile picha ikawa mikononi mwako, na nataka unieleze sasa hivi!”Candy alimjia juu.
Jackie alimtazama kwa hasira, na Candy akawasha kiberiti na kutishia kukirushia pale kwenye godoro lilotota mafuta ya taa. Jackie alishtuka na kukwepesha mguu wake.
“Ongea!”
Jackie alimtazama na kukutana na mtazamo wa ghadhabu kutoka kwa Candy.
“Okay Candy…ni kweli ile picha ilipigwa siku ile nilipokushawishi twende viwanja…”
“Uliponilazimisha!”
“Yes…siku nilipokulazimisha kwenda viwanja. Unakumbuka wale marafiki zangu walikuja hapa ndani, na tukawa tunasaidiana kukuvalisha nguo za kazi?” Jackie alimwambia na kumuuliza. Candy aliafiki kwa kichwa.
“Halafu mi’ nikawa nakuelekeza namna ya kutembea kwa mbwembwe za kichangu?”
“Nakumbuka…so what?”Candy alimjia juu.
“Nilipomaliza nyie mkawa mnaendelea kucheka tu jinsi nilivyokuwa nikionesha zile mbwembwe… wakati mnacheka mi’ nikawapiga pichakwa kutumia simu yangu.”
“Hah! Kwa hiyo ulikuwa na nia mbaya nami tangu wakati huo hadi ukaamua kunipiga hiyo picha? Ni nini nilichokukosea wewe hata ukaamua kunifanyia njama namna hiyo?”
Jackie aliguna na kubetua midomo.
“Wala sikuwa nimeipiga ile picha kwa nia baya…”
“Ila?”
“Niliipiga tu kwa kuwa mlionekana kupendeza…”
“Sasa ikawaje tena?”
“Ah, ilipojitokeza hii nafasi ndipo nilipoona niitumie ile picha kwa maslahi yangu!” Alimjibu bila kujali, sasa akianza kuwa na utulivu.
Candy alimshangaa.
“Maslahi yako? Yaani ulikuwa tayari kuniharibia maisha yangu, kwa ajili ya kujitafutia maslahi ambayo hukuyafanyia kazi hata kidogo?”
Jackie alimtazama kwa muda, na ghadhabu ya wazi ikajionesha usoni kwake.
“Hivi wewe unadhani mi’ nilijisikiaje siku ile nilipokuja nikakuta umeniachia kiji-ujumbe chako hapa kuwa eti hoo nimepata mfadhili na hivyo naondoka, nawe nakutakia maisha mema…halafu ukaniachia kishilingi elfu kumi na tano…khah?” Alimwambia na Candy akapigwa butwaa.
“Khah!Yaani hilo ndilo kosa langu?” Alimuuliza kwa mastaajabu.
“Yaani we’ kukuhifadhi kote hapa kwangu na kukulisha ukaona fedha halali kwa wema wangu ule ni elfu kumi na tano? Nilichukia kwa kweli. Tena hata hukuniambia umepata ufadhili wa kitu gani, mpaka nakuja kukuona kwenye magazeti na televisheni! Nilikumaindi kwa kweli, na ndio maana nikaamua kuitumia ile picha kujilipa kwa wema niliokufanyia!” Jackie alimjibu kwa hasira iliyo wazi.
Candy alichoka. Alitaka amjibu kuwa hakuwa akijua asemacho, na kwamba yeye alitaka amchukue naye aondokane na yale maisha mabaya, lakini wafadhili wake hawakuridhia. Lakini hakufanya hivyo, kwani aliona kuwa angepoteza muda bure.
“Hebu niache nikajisafishe Candy…umenilowesha mafuta ya taa kiasi hiki!” Jackie alimwambia huku akijaribu kujiinua tena pale kitandani, na kwa mara nyingine akakwazwa na ule mguu wake mmoja uliokuwa umefungwa kwamkanda pale kitandani, na kwa mara nyingine ikamdhihirikia kuwa huenda kweli Candy alikuwa amedhamiria kumchoma moto mle ndani.
“Candy…!” Aliita kwa hamaniko.
“Tulia hapo hapo Jackie!Nilivyokwambia nilikuja kukuchoma moto humu ndani unadhani nilikuwa natania? Sasa sikiliza, tena sikiliza vizuri maana sitakuwa na muda wa kurudia maelekezo haya…” Candy alimchachamalia, na Jackie akaona kuwa hakika alikuwa amekabiliana na Candy mwingine.
Alianza kuhangaika kujifungua ule mkanda na hapo Candy akawasha tena kile kiberiti chake na kutishia kukitupia pale kwenye lile godoro lililotota mafuta ya taa, na Jackie aliachia yowe dogo la woga.
“Sikiliza Jackie…Nimekitazama kile kimeo chako. Ile picha umeihifadhi kwenye simu, na sio kwenye memori kadi. Memori kadi haimo mle…”
“Kwa hiyo…?” Jackie aliuliza haraka na kwa mashaka, na hapo Candy akajua kuwa hisia zake zilikuwa sahihi.
“Kwa hiyo nikajua kuwa hizo picha nyingine ulizonazo zitakuwa kwenye memori kadi…naitaka!” Alimwambia huku akimtazama kwa kitisho kilicho wazi.
Jackie alipepesa macho na kumeza funda la mate.
“Mem…memori kadi? Si… sina memori kadi mie…na hizo picha nyingine ziko kwa rafiki yangu…nikipatwa na lolote tu anazieneza…”
Candy alipiga hatua na kumsukuma kwa nguvu, na Jackie akajibwaga chali pale kitandani huku yowe la woga likimtoka.
“Acha ujinga wewe! Lete memori kadi ama sivyo nakuwasha moto nami natoweka…!” Alimtumbilia macho yenye dhamira ya kutimiza alichokuwa akikisema.
Jackie alibaki akimtumbulia macho huku akitweta.
“Na kwa taarifa yako…kama hunipi hiyo memori kadi, nitaendelea kukuibukia kila alfajiri humu ndani, na utakuwa unaamka kwenye dimbwi la mafuta ya taa hapo kitandani kila siku mpaka siku nitakayoamua kukuteketeza Jackie…si mfano umeuona hii leo? Nimeingia, nimekufunga kamba na nimekiloweka mafuta ya taa kitanda nawe huna habari!” Candy alizidi kumtisha, na Jackie aligwaya vibaya, kwani aliyoambiwa na Candy yalikuwa ni kweli tupu.
“Najua uwezo wa kuhama hii nyumba kwa sasa huna mpaka kodi yako iishe, nami sitasubiri kodi iishe kabla sijakukaanga humu ndani…na hata ukijitia kuweka komeo hapa mlangoni, sishindwi kuparamia juu na kukushukia huku ndani maana chumba chenyewe haina dari hiki… na nyumba hii watu hawaamki mpaka saa nne za asubuhi, si unaona kulivyo kimya alfajiri hii?Sasa utatoa memori kadi hutoi?” Candy alimtemea maneno kwa ukali huku akiwa amemuwekea ule mwale wa moto kutoka kwenye kiberiti chake karibu ya uso wake na Jackie akawa anajitahidi kujiweka mbali na moto ule.
“Okay, Okay! N’takupa!”
“Fasta tena!”
“Kwenye mkoba wangu pale juu ya meza!” Jackie alibwabwaja huku akiioneshea meza ndogo iliyokuwa katikati ya chumba kile kwa kidole chenye kutetema.
Kwa muda Candy alibaki akimtazama kwa hasira huku bado akiwa amemuelekezea ule moto.
“Kweli Candy, mdogo wangu! Hebu toa huo moto basi mwenzio nywele zote zimelowa mafuta ya taa hapa…zitawaka!”Jackie alilalama.
Candy aliuchukua ule mkoba na kumtupia pale kitandani.
“Toa hiyo memori kadi…upesi!” Alimuamuru, na huku akitetemeka Jackie alipekua ndani ya mkoba ule na kumnyooshea mkono uliokuwa umeshika memori kadi iliyokuwa imefungashwa kwenye kipande cha karatasi.
Candy aliikwapua nakuitazama, kabla ya kuiweka kwenye mfuko wa suruali yake ya mazoezi na kufunga zipu ya mfuko ule.
“Kwa hiyo picha nyingine ziko kwenye hii memori kadi, sio?”
“Ndiyo…!” Jackie alijibu huku akimtazama kwa woga.
“Leo nakuacha.Nisikusikie tena ukinijia na huu upuuzi wako Jackie, sawa?”Alimwambia.
“Poa tu.”
“Na bado sijamalizana nawe, Jackie.” Candy alimwambia huku akitoa kifuko cha nailoni chenye unga mweupe kutoka kwenye mfuko mwingine wa suruali yake. Jackie alimakinika kutaka kuona ni nini kilichokuwa kinafuata.
“Kwa kuwa wewe umeamua kunichezea mchezo mchafu, nami nimeamua kukujibu kwa mchezo mchafu zaidi…” Candy alimwambia huku akimuoneshea kile kifuko cha nailoni, na Jackie akakitolea macho kwa mshangao.
“Ni…nini hiyo?”
“Huu ni unga wa dawa za kulevya Jackie, nami nimekutegeshea vifuko sita vya unga huu humu ndani kwako….”
“Hah!”
“Ndio!We’ si umetaka kuniharibia maisha yangu? Sasa muda wowote naweza kupiga simu polisi na kuwaelekeza mahala nilipoficha unga huo na utakuja kubebwa mzima mzima hapa…utapotezwa! Wafadhili wangu ni watu wenye kujuana na watu wanaoweza kuhakikisha hilo…”
Jackie aliogopa vibaya.
“Jamani Candy! Hivi ni wewe kweli?”
“Kelele Jackie! Sasa mi’ sitatoa hii taarifa.Ila nikihisi tu kuwa unataka kunifuata-fuata tena, nakupoteza!”Alimtishia.
Jackie aligwaya vibaya.
“Na utatafuta mpaka uchoke, hutaona ni wapi nipoficha hizo kete za unga wa kulevya humu ndani…sasa bado unataka vita na mimi?” Alizidi kumkoromeana kumuuliza.
Jackie alimtazama hakummaliza.Machozi yalianza kumbubujika.
“Basi Candy…yameisha mdogo wangu…”
“Sio mdogo wako mie!”
“Sawa…Sina tena haja na mambo hayo…naomba uniache!” Jackie alijibu kwa fadhaa.
Candy alimtazama kwa muda kisha akaokota khanga zake na kujitanda haraka haraka, kabla ya kuugeukia mlango wa kutokea mle ndani.
“Sa…sasa nirudishie ile simu yangu basi!” Jackie alimwambia kwa mashaka.
“Nimeitumbukiza chooni!” Alimjibu bila ya kugeuka, na kutoka nje ya chumba kile.
Nje ya chumba kile aliegemea ukuta na kushusha pumzi kwa nguvu. Miguu ilikuwa ikimtetema na moyo ukimwenda mbio kwa wasiwasi. Hakuamini kama ameweza kuutimiza mpango wake wa kumpora Jackie zile picha chafu zilizotaka kumharibia ndoto yake ya kuutwa umalkia wa urembo nchini.Hatimaye alijilazimisha kuondoka eneo lile kwa mwendo wa haraka akiwa amejitanda khanga mwili mzima kuelekea barabara kubwa. Huko alisimamisha bajaji na kumwamrisha dereva amrudishe Kariakoo mtaa wa Aggrey huku akikitupa barabarani kile kifuko cha unga wa ndimu ya mchina alichokuwa amemtishia Jackie kuwa ni unga wa dawa za kulevya.
Saa yake ya mkononi ilimwambia kuwa muda ni saa kumi na mbili na dakika tano za asubuhi…
Bila shaka sasa swala la Jackie litakuwa limekwisha…ee Mungu, naomba liwe limeisha! Nilikuwa natetea baraka uliyonitunuku tu Mola wangu…we’ unajua undani wa nafsi yangu kuliko binadamu yeyote hapa duniani!
Alijiwazia peke yake ndani ya Bajaji, huku akijitandua zile khanga alizokuwa amejitanda na kuanza kuzikunja huku bado akili ikiendelea kumzunguka.
“Eh! Samahani kaka…naomba unipitishe hadi Mnazi Mmoja…n’tateremka huko!” Alikurupuka kutoka kwenye mawazo yake na kumwambia dereva wa Bajaji, ambaye hapo hapo alibadili uelekeo na kukamata barabara ambayo ingewafikisha Mnazi Mmoja.
“Ah, sasa anti itabidi uongeze jelo hapo basi, maana…”
“Haina neno…twende!”
***
Kufikia saa kumi za alfajiri siku ile ile, Kokos Wandiba alikubaliana na hali halisi kuwa usingizi ulikuwa umemtupa mkono kabisa usiku ule.
“Na yote hii ni sababu ya mtoto Candy,Gaddemit, whats the matter with me?” Alijisemea peke yake huku akiinuka kutoka kitandani na kwenda kuketi sebuleni.
“Yaani nimekuwa kamabarobaro anayetafuta penzi kwa mara ya kwanza, bwana!” Alizidi kujilaumu huku akiwasha luninga yake kubwa sana ya kioo bapa na kuanza kuperuzi chaneli mbali mbali za DSTV.
Hakuna kilichomvutia luningani, akili yake ilikuwa imeganda kwa Candy tu na urembo wake.
“Tatizo hiki si kipindi kizuri kumchanganya na maswala haya. Mi’ n’litaka amalize harakati zake za u-misskwanza…nd’o niweke wazi hisia zangu kwake…lakini sasa kama yeye naye anatatizwa na jambo hili hili, na anataka kulipatia ufumbuzi sasa hivi mi, nifanyeje…?” Alizidi kujisemesha mwenyewe mle ndani.
Alibaki akiikodolea macho luninga bila ya kuona au kuelewa kile kilichokuwa kikiendelea kwenye luninga ile, kisha akatoa mguno wa kukata tamaa na kuliendea jokofu lake lililosheheni vinywaji kwa kila namna.
Akaanza kupata kinywaji taratibu kupoteza mawazo.
Kinywaji hakikuelekea kumsaidia katika hilo, kwani saa moja baadaye, bado akili yake ilikuwa imezongwa na fikra juu ya yule binti mrembo, ikimrudisha mara kwa mara kwenye tukio la ile siku alipokutana kwa mara ya kwanza na binti yule na kumfikisha pale nyumbani kwake.
Alitupa mikono hewani kwa kuchanganyikiwa huku akitoa sauti mithili ya kokoto zinazomiminwa ndani ya debe na kuinuka kutoka kwenye kochi alilokuwa amekalia.
“Hii hainisaidii lolote bwana…Ah!”Alimaka.
Ile kumbukumbu ya siku alipomfikisha Candy mle ndani akiamini kuwa ni changudoa na kushindwa kutimiza azma yake huwa inamkosesha raha siku zote.
Huko nje alimsikia mnadi swala akianza kuwaamsha waumini kwa adhana ya swala ya alfajiri.
Alikwapua ufunguo wa gari lake na kutoka nje.
“Bora nirande tu mitaani na gari nipigwe upepo, kuliko kukaa nikijinyanyapaa mwenyewe humu ndani, bloody shit!”
Ilikuwa ni saa kumi na moja na dakika kumi za alfajiri.
***
Wakati Candy akikabiliana na Jackie kule Manzese alfajiri ile, na Kokos Wandiba akijaribu kupoteza mawazo juu ya binti yule kwa kujidunga kinywaji kule nyumbani kwake Mbezi beach, huko maeneo ya mikocheni jijini Dar,Gino “GTZ” Tzaspaparos alikuwa amelala chali kitandani kwake huku amefura kwa hasira, chumba chake kikiwa kimegubikwa kiza totoro.
Kama ilivyokuwa kwa Candy na Kokos Wandiba, Gino Tzaspaparos, au “GTZ” kama baadhi ya rafiki zake walivyozoea kumwita, naye alikuwa amepitisha usiku uliopita akiwa macho, usingizi ukigoma kabisa kuziingia fahamu zake.
Akiwa ni chotara aliyetokana na mchanganyiko wa baba wa kigiriki na mama wa kingazija, GTZ alikuwa na kila sababu ya kufura kwa hasira, kwani alishajijengea nidhamu ya kupanga mambo yake kwa uangalifu mkubwa, nidhamuiliyomuwezesha siku zote kutimiza malengo yake bilamatatizo wala vikwazo vyovyote.
Lakini sio kwa Candy!
Safari hii, kwa mara nyingine tena, mkakati wake dhidi ya Candy umevurugika, na hili lilimkera na kumkosesha kabisa usingizi GTZ.
Leo nilikuwa namaliza kabisa biashara ya Candy, baada ya kumpoteza kwa muda, lakini yule malaya mwenzake aliyeibuka ghafla pale The Slipway akaja kutibua kabisa plan zangu, bloody bitch!
Aliinuka kutoka pale kitandani na kuwasha taa.
Na muda unazidi kwenda! Natakiwa nimalize biashara ya Candy kabla wengine hawajamshtukia na kuja kuniharibia kabisa mikakati yangu!
Akachukua simu yake aina ya Samsung GalaxyS3 na kutumia mtandao unaopatikana kwenye simu ile kuingia kwenye wavuti wa Miss Tanzania na kujaribu kuangalia ratiba za matukio yajayo kwa warembo wa shindano lile, ili kujua ni wapi tena Candy ataweza kupatikana.
Tukio la mwisho kunadiwa kwenye wavuti ile lilikuwa ni lile la ile pati ya mchapalo iliyofanyika pale The Slipway usiku uliopita.
GTZ alisonya kwa hasira na kuirushia ile simu kitandani. Aliranda huku na huko mle ndani, akihisi ghadhabu zikimuelemea.
Akiwa na bukta tu alienda chini na kuanza kupiga push-up za haraka haraka kwa mkono mmoja huku mwingine akiwa ameuweka mgongoni kwake. Alipofikisha push-up hamsini, alibadili mkono na kupiga push-up nyingine hamsini.
Alipomaliza alikuwa akivuja jasho, na ghadhabu zilikuwa zimempungua.
Sio ishu…nitaendelea kumfuatilia tu kisonoko yule mpaka nafasi muafaka ijitokeze…
Alitoka mle chumbani na kuelekea bafuni.
Ilikuwa ni saa kumi na moja na nusu alfajiri…
***
Candy aliteremka eneo la Mnazi Mmoja na kumlipa yule dereva wa Bajaji, kisha akaingia ndani ya eneo la ule uwanja wa Mnazi Mmoja na kuanza kukimbia kimazoezi pembezoni mwa uwanja ule.Kwenye kona moja ya uwanja ule kulikuwa kuna pipa kubwa sanala takataka, na alipolifikia pipa lile alizitupia zile khanga alizokuwa amezikunja pamoja ndani yake bila ya kusimama. Aliendelea kukimbia kimazoezi kutoka nje ya uwanja ule na kuchukua uelekeo wa mtaa wa Aggrey…
***
GTZ alikuwa ameegemea pikipiki yake kubwa yenye nguvu na uwezo wa kukimbia kwa kasi, iliyobinuka nyuma kiasi cha kumfanya muendeshaji awe ameinamia mbele. Kutokana na ule usafiri alioamua kuutumia asubuhi ile, hakuwa amevaa suti kama kawaida yake, na badala yake alikuwa amevaa suruali nyeusi ya khaki na fulana nyeupe ambayo juu yake alikuwa amevaa jaketi jeusi la ngozi. Miguuni alikuwa amevaa viatu vikubwa vya ngozi, ambavyo navyo vilikuwa vyeusi, hali kichwani akiwa amevaa kofia nyeusi ya kepu.
Alikuwa akivuta sigara taratibu huku akiwa amelielekea ghorofa la msajili ambalo alijua kuwa Candy alikuwa akiishi ndani yake pamoja na wapangaji wengine. Alikuwa na hakika kabisa kuwa kwa muda ule wa alfajiri, Candy na mfadhili wake watakuwa bado wamelala.
Na ukiamka tumi’na wewe leo mrembo…mpaka ujiingize kwenye kona niitakayo!
Alijiwazia huku kibaridi cha asubuhi kikimpiga kifuani kupitia kwenye ile fulana yake nyepesi, kwani jaketi lake alikuwa ameliacha wazi sehemu ya kifuani.
Hasira zake dhidi ya binti yule ziliongezekamaradufu pale alipokifikiria kitanda chake alichokiacha asubuhi ile na kwenda kusimama pale nje ya jengo lile pale mtaa wa Aggrey akipigwa baridi, na alijikuta akitafuna kishungi cha sigara yake kwa hasira.
Aliitema ile sigara na kuikanyaga kwa hasira, na hapo hapo akatoa sigara nyingine kutoka kwenye paketi iliyokuwa kwenye mfuko wa ndani wa jaketi lake na kuiwasha kwa kiberiti cha gesi
ambacho nacho alikitoa kwenye mfuko ule wa ndani wa jaketi lake.
Alijiinua kutoka kwenye ile pikipiki yake aliyokuwa ameiegemea na kutupa-tupa mbele miguu yake kwa namna ya kuinyoosha kisha akarudia kuiegemea tena pikipiki ile. Alipiga mwayo mrefu huku akigeuka kulia kwake, kisha akauvuta kwa wingi moshi wa sigara iliyokuwa mkononi mwake huku akigeukia kushoto kwake, na hapo akahisi moyo wake ukipiga chogochemba.
Kutokea kule kushoto kwake, alimuona Candy akikimbia kimazoezi kuelekea kule alipokuwa amesimama na akili ikamchecheta.
Ah! Si yeye yule?
Alijiuliza
Ndiye!
Alijithibitishia huku akimtazama yule binti wa urembo akizidi kukimbia kuelekea ule upande aliokuwapo, ila akiwa ng’ambo ya pili ya ule mtaa, upande ambao ndio lile jengo alilokuwa akiishi yule binti lilikuwapo.
Hah! Alikuwa mazoezi…? Lakini…alitoka saa ngapi huyu...?
Aligeuka kulia kwake na kisha akalitazama lile jengo lililokuwa mbele yake, ambalo alijua kuwa ndipo Candy alikuwa akielekea.
GTZ alihamanika kidogo.
Dah, hii ni nafasi…lakini si nzuri sana!
Alikuwa amejiandaa kumfuata Candy pindi atakapotoka ndani ya jengo lile, ndio maana akaenda kumvizia pale nje alfajiri ile.Sasa hili la kumuona Candy akirudi ndani ya jengo, badala ya kutoka, lilikuwa nje kabisa ya matarajio yake.
Nafanyaje sasa?
Alitembeza macho eneo lile, na kwa mara ya kwanza aligundua kuwa mtaa ule ulikuwa umeshaanza kutawaliwa na harakati za wapita njia na wafanya biashara mbali mbali wa sehemu ile ya jiji, nalo lilikuwa ni jambo lililoongezea ugumu katika lile alilotaka kulifanya kwa binti yule.
Sasa…?
Alimgeukia tena yule binti na kuona alikuwa anazidi kulikurubia lile jengo la msajili alilokuwa akiishi ndani yake.
No time to waste!
Alishusha chini kofia yake ya kepu kuificha sura yake kisha akavuka barabara kuhamia ule upande ambao Candy alikuwepo.
***
Kule kukimbia kutoka Mnazi Mmoja hadi pale mtaa wa Aggrey kulimsaidia sana Candy kutuliza akili na wahka aliotoka nao kule kwa Jackie. Sasa alikuwa amekaribia kufika nyumbani na akili yake ikarudi kwa Bishkuku ambaye hakuwa na shaka atamkuta ameshaamka na amejawa wahka.
Alijifuta jasho lililokuwa likimtirirka kwa mkono wa fulana yake ya mazoezi, na kushtuka ghafla pale alipohisi akikaribia kupamiana na mtu. Aliguna kwa mshutuko huku akiinua macho yake, na kujikuta uso kwa uso na mtu mwenye kapelo. Alijaribu kumkwepa kwa kuruka pembeni lakini hapo alihisi maumivu makali mguuni pale mguu wake ulipogongana na ule wa yule mtu, ambaye alipayuka kwa kukereka huku akipepesuka.
Watu wachache waliokuwa eneo lile walipiga kelele za ushabiki, na Candy alikuwa anaanguka bila kizuizi wakati aliposhitukia akidakwa kwa mikono yenye nguvu na kurudishwa wima.
“Oh, samahani…naahsante san…”
“Kimya wewe!Tulia na uongozane nami!” Sauti nzito ilimkoromea sikioni na mwili ukamfa gazi.
“Khah! We’ vip…”
Alihisi kitu chenye ncha kali kikimbonyeza ubavuni.
“Ni kisu aina ya stiletto kilichopiga kambi ubavuni kwako hicho, miss Dar city center! Ukijitia ujanja nakididimiza na kutoboa ini lako mara moja…!”
Heh!
“Oyaa, vipi hapo?”Sauti moja iliuliza.
“No problem…namsogeza tu kwenye gari pale kisha atakuwa poa!” GTZ alimjibu yule jamaa aliyeuliza huku bado akiwa amemkamata Candy kwa nguvu juu ya kiwiko kwa mkono mmoja huku kwa mkono mwingine akiwa amemuwekea ncha ya kile kisu chake kikali kwa uficho.Candy alikuwa ameingiwa ganzi mwili mzima.
Hii sauti! Nimeisikia wapi hii?
Candy alihamanika huku akili ikimzunguka.
“We…kwani ni nani…?” Aliuliza kwa woga mkubwa huku akiongozana na yule mtekaji wake bila kupenda, ncha ya kile kisu akimtomasa ubavuni.
GTZ alikuwa na mashaka yake, hivyo hakumjibu.
Hapa watu wengi! Laiti ningekuja na gari ningeodoka naye, lakini kwa pikipiki itakuwa ngumu sana!
“Please jamani…mi’ sina kitu chochote, unanitakia nini mimilakini wewe?” Candy alizidi kulalama, machozi yakimtiririka.
“Kelele! We’ unajua kabisa kuwa unatafutwa kwa udi na uvumba halafu unaenda kujianika ovyo magazetini na kwenye televisheni, ulitegemea nini?” GTZ alimkoromea, macho yake yakitua kwenye teksi iliyokuwa imeegeshwa hatua chache mbele yao.
Pikipiki itabidi niiache tu kwa kweli…
Candy alichanganyikiwa.
“Natafutwa??”
“Shut-Up! Sasa tutaingia kwenye ile teksi mimi na wewe,na humo utakaa kimya mpaka tutakapoteremka la si’vyo nakuua hapo hapo utakapojaribu kufunua kinywa chako, umenielewa wewe?”
Ah, hii sauti naijua!
“Unanipeleka wapi?Na…natafutwa na nani mimi…?” Alimuuliza kwa kitetemeshi.
“Ulidhani tutasahau, eenh?Basi tulia...n’takukumbusha tukifik…”
“Candy!”
Kokos!
GTZ alisikia sauti ya Kokos ikiita jina la yule mateka wake na hapo akashituka kumuona yule mfadhili mwingine wa yule binti akiwa hatua chache mbele yao, akiwaendea.
“Kokos ananitekaaa!” Candy alipiga kelele huku akimtumbulia macho Kokos, ambaye alipigwa butwaa kwa muda, pombe alizobugia alfajiri ile bado zikiwa zinafanya ziara kwenye mfumo wake wa fahamu.
“Pumbaavu!” GTZ alimsukuma Candy pembeni kisha akaruka kwa hatua moja kubwa na kumtandika Kokos kofi kali la uso.
“Waaahrgh!” Kokos alilia kwa maumivu huku akijishika uso, na hapoGTZ akamchota miguu yake yote miwili kwa ngwara kali ya mtindo wa “pecha”, ambayo hupigwa kutokea mbele badala ya kutokea nyuma, na Kokos akaenda chini kwa kishindo huku akitanguliza uso na mikono.
Sasa Candy alikuwa akipiga kelele za kuombamsaada na baadhi ya wananchi wengine nao wakiungana naye kupiga mayowe, wengi wao hata kabla ya kuelewa kilichokuwa kikiendelea.
Hapa pamenuka!
GTZ aliikimbilia pikipiki yake huku akibonyeza kitufe kutoka kwenye ufunguo wa pikipiki ile, na lile pikipiki kubwa likaamka na kuvuma kutokea kule lilipokuwa, naye aliirukia na kuirusha mbele kwa nguvu, watu wachache waliokuwa pale walipiga kelele huku wengine wakimkimbilia pale alipokuwa.
Aliizungusha kwakasi pikipiki yake, tairi zikipiga kelele nakurusha vumbi jepesi lililokuwa pale barabarani, kisha akaiweka sawa barabarani ile pikipiki na kutokomea kwa kasi kutoka eneo lile, akiacha mayowe ya hamaniko kutoka kwa baadhi ya mashuhuda, hali baadhi ya mashuhuda wakiachia mbija na mayowe ya shangwe kwa namna alivyochomoka na ile pikipiki hukuakiacha kizaazaa pale mtaani.
Candy alimkimbilia Kokos aliyekuwa akianza kujizoazoa kutoka pale alipoangukia huku maluweluwe yakiwa yamemzonga.
“Oh, Kokos! Kokos…pole jamani…!” Candy alibwabwaja huku akijaribu kumuinua, lakini Kokos alimsukuma pembeni.
“Nenda ndani upesi!Kimbia!”Alimkemea.
“Lakini wewe…?” Candy alilalama.
“Achana na mimi Candy! Go inside now! Watu wasikutambue bure hapa. Ala!” Kokos alimkoromoea kwa hasira huku akiinuka. Candy alijifunika kofia iliyoungana na ile fulana yake ya mazoezi kuficha kichwa na uso wake, kisha akakimbilia ndani ya jengo alilokuwa akiishi na Bishkuku huku machozi yakimuanguka.
“Anti Bishi! Anti Bishiii…oh Anti Bbishhh….” Aliingia mbio sebuleni kwao huku akipayuka kwa hamaniko lililokithiri, na akakutana na Bishkuku aliyekuwa amevaa gauni jepesi la kulalia naye akija mbio pale sebuleni kutokea jikoni.
“Nini weye lakini?” Alimuuliza kwa wahka.
“Kokos kapigwa!Alitaka kuniteka…Kokos akatokea, Anti Bishi!”Candy alipayuka huku macho yamemtoka, maneno yakipandana hovyo kinywani. Bishkuku alimshika mkono na kumketisha kwenye kochi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hebu tulia kwanza wewe, mi’ sikuelewi ujue!Kokos alitaka kukuteka kivipi, halafu akapigwa…wapi?” Alimkemea, na Candy akatikisa kichwa na kuvuta pumzi na kuzitoa haraka haraka, akijua kuwa alikuwa hajielezi vizuri.
Alijitahidi kumueleza kilichotokea kule nje kwa utulivu kadiri alivyoweza, na alipomaliza Bishkuku akampiga swali.
“Haya na we’ huko nje ulikuwa ukitafuta nini lukwili yote hii hata kuku hawajanya?”
“Kuku hawajanya…?” Candy alimuuliza kwa mshangao.
“Msemo tu huo na wewe vipi?Unamaanisha ni mapema mno….we’ ulikuwa unatafuta nini huko nje saa hizi?” Bishkuku alimjibu kwa kukereka.
“Ah, nili…nilienda jogging anti…mazoezi!”
Bishkuku alimtazama kwa muda.
“Mada haijaisha hii!Kaa hapo hapo kwanza, mi’ naenda kumcheki huyo Kokos huko nje…usitoke humu ndani!” Alimwambia huku akikwapua upande wa khanga na kutoka nje ya sebule ile.
Candy alifumbata kichwa chake kwenye mikono yake na kujiinamia.
Oh, Mungu wangu ni mambo gani haya yanayoniandama namna hii lakini? Nimemaliza la Jackie, sasa laja la huyu mtu wa ajabu…eti mi’ natafutwa…! Natafutwa…?
Mwanadada aliangua kilio cha masikitiko.
***
Kule nje Kokos aliinuka na kurudi kwenye gari lake kwa mwendo wa kuyumbayumba, akipuuzia maneno ya pole na udadisi kutoka kwa wale mashuhuda wa tukio lile la kushangaza. Huku uso ukimchonyota kwa lile kofi alilozabwa na yule jamaa, aliingia ndani ya gari lake na kuchukua chupa ya pombe kali iliyokuwa mle ndani na kupiga funda kubwa la kinywaji kile, kisha akatikisa kichwa huku akigumia kwa msisimko.
Akairudisha ile chupa pale ilipokuwa mle garini na kuteremka. Alikomea milango ya gari lake na kurudi pale nje ya jengo la akina Bishkuku, ambako bado kulikuwa kuna watu wachache wakiliongela tukio lile.
Alimuuliza mmoja wao iwapo alikuwa anamfahamu yule jamaa aliyetoroka na pikipiki baada ya kumtembezea mkong’oto.
“Hapana bwana yule jamaa ndio leo namuona hapa mtaani…!” Jamaa alimjibu.
“Ina maana ukimwona tena utamkumbuka?”
“Ah, wapi! Sikumpata sura yake vizuri…yule si wa hapa, yule!”Jamaa alimjibu.
“Ila alikuwa amepaki pikipiki yake muda mrefu sana pale…ka’ vile alikuwa akisubiri kitu au mtu f’lani hivi!” Jamaa mwingine aliyekuwa akiuza kahawa alidakia, na Kokos akamakinika na hilo.
“Kwa nini unasema hivyo?” Alimgeukia na kumuuliza.
Muuza kahawa alifinya uso kutafakari namna ya kujieleza.
“Ah, yaani alivyokuwa amesimama akivuta fegi zake pale…iliashiria kitu kama hicho.Mara akitazama kwenye hilo gorofa, mara huku, mara kule…ni kama alikuwa anavizia kitu hivi…sa’ sijui ikawaje tena mara nikaona makofi, mateke…kisha huyooo, na pikipiki lake!” Alijieleza kwa kirefu.
Jamaa wengine wakaanza kutawanyika huku wakicheka kutokana na namna muuza kahawa alivyokielezea kisa kile.Kokos alikunja uso kwa tafakuri, bado uso ukimchonyota kwa lile kofi alilolambwa na yule jamaa.
Akageuka na kuelekea kule nyumbani kwa Bishkuku, akili ikimzunguka.
Yule jamaa ni nani…? Na alikuwa anataka nini kwa Candy?
“Kokos!Ni nini kimetokea?” Bishkuku alimuuliza kwa wahka huku akitoka nje ya jengo lile kwa mwendo wa haraka, akikutana naye mlangoni.
“Twende ndani kwako Bishkuku…yaliyotokea hapa nje ni kitendawili kitupu!”Kokos alimjibu bila ya kusimama wala kumtazama, akiendelea kuingia ndani ya jengo lile.
Bishkuku alimtazama kwa kuchanganyikiwa, kisha akatupa macho huku na huko pale mtaani, kabla ya kugeuza na kumfuata ndani ya jengo lile.
***
Kokos na Bishkuku waliingia pale sebuleni, na Candy alijikuta akiinuka kwa wahka na kumkimbilia Kokos huku akimtazama kwa udadisi mkubwa.
“Vipi Kokos! Um…umeumia sana? Utakuwa umeumia tu, pole sana…” Alimwambia huku akimshika bega na kuanza kumkung’uta vumbi.
“Dah, nimeumia kidogo Candy, sio ishu.Lakini wewe vipi…hukuumia?”Kokos alimjibu huku akimshika mkono kumzuia asiendelee kumkung’uta vumbi.
“Ah, mi sikuumia…ila…nimetishika sana kwa kweli!” Alijibu na mwili ulimsisimka bila kupenda.
“Hebu sasa tueleze vizuri Candy…ilikuwaje?” Bishkuku alimuuliza, na hapo hapo akamgeukia Kokos, “Na we’ pia utueleze ni kipi kilichokuleta mjini mapema yote hii huku mipombe inakunuka kinywa chote…ulilala baa?”
Kokos alimtazama kwa hasira, halafu akamgeukia Candy, kisha akainamisha kichwa.
“Candy hebu tueleze kilichotokea pale…yule jamaa ni nani?” Alimuuliza Candy huku akilipuuzia swali aliloulizwa naBishkuku.
“Ah, mi’ simjui!Kwanza hata sura yake sikuiona vizuri…yaani nilikuwa natoka mazoezi ya kukimbia, mara nikashtukia tumepamiana. Kilichofuata ananikamata na kuniwekea kisu ubavuni…!”
“Hah!”
“Kisu…?”
“Ennh, Kaniwekea kisu kabisa ubavuni.Akaniambia nimfuate na nisilete ubishi ama sivyo ananitoboa maini!”Candy alijieleza, na Kokos akajikuta ameketi kwenye kochi lililokuwa karibu yake bila kupenda.
Akili yake ya ki-uwakili mara moja ilianza kufanya kazi, ikizisukuma pembeni pombe zilizokuwa zikijivinjari kwenye fahamu zake muda ule.
“Huo ni utekaji nyara huo…adhabu yake kifungo cha kuanzia miaka mitano kwenda juu!Kwa nini alitaka kukuteka?” Alisema huku akiwa makini sana.
“Akh!Mi’ sijui!”
“Yaani alikuwa anataka kukuteka nyara?” Bishkuku aliuliza kwa woga mkubwa.
“Sio alikuwa anataka Bishkuku…alishaniteka! Bahati ndio Kokos akatokea…!”
“Heh, haya makubwa!” Bishkuku alisema huku akijishika kichwa, uso wake ukisajili mkanganyiko mkubwa.
“Ni nini kingine alichokwambia wakati ule?”Kokos alimuuliza.
Candy alikumbuka maneno ya yule jamaa.
We’ unajua kabisa kuwa unatafutwa kwa udi na uvumba halafu unaenda kujianika ovyo magazetini na kwenye televisheni, ulitegemea nini?
“Ha…hakuniambia kitu kingine zaidi…nilimuuliza ananitakia nini huku akinikokotea kwenye teksi iliyokuwa imepaki mbele yetu…”
“Na…?”
“Akanijibu kuwa tukifika anapotaka kunipeleka nd’o ataniambia anachokitaka kwangu.Na hapo ndipo we’ ulipotokea!” Candy alimjibu, akificha kueleza ukweli juu ya yale maneno ya kukanganya aliyoambiwa na yule mtu.
Kokos na Bishkuku walitazamana, kisha Kokos akamgeukia Candy na kumtazama kwa macho makali.Akili yake ya ki-anasheria ikamwambia Kokos kuwa kuna kitu Candy alikuwa anaficha, na hili likamkosesha amani kidogo.Candy akagwaya, akihisi yale macho yalikuwa yanamuona mpaka ndani kabisa ya nafsi yake.
“Look Candy…hili swala si dogo. Mtu hawezi kutoka tu huko atokako aje akuvamie na kutaka kukuteka namna ile bila sababu au bila kuwa na uhusiano fulani nawe…” Alimwambia huku akizidi kumtazama moja kwa moja machoni.
“Oi!Wait a minute Kokos…unataka kusemaje sasa?Kwamba Candy anamjua huyo mtu?” Bishkuku alimjia juu, lakini Kokos akamuinulia kiganja chake kumnyamazisha bila kuhamisha macho yake kutoka kwa Candy aliyezidi kugwaya.
“Una hakika ulitueleza ukweli wako wote kuhusu maisha yako ya huko nyuma Candy?Hukutuficha kitu chochote?”Alimuuliza hukuakiwa amemkazia macho yenye kusaili.
Candy alihisi kuumbuka.
“Jamani…mi’ sina lolote baya la kuwaficha ndugu zangu…niliyowaeleza ndiyo niyajuayo!” Alijitetea huku akitembeza macho baina ya Kokos na Bishkuku. Kokos alizidi kumkazia macho yaliyomwambia kuwa bado alikuwa anahitaji kujua zaidi.
“Kama kuna unaloficha bora utwambie sasa Candy, maana matukio kama hili la leo hayaendani kabisa na hiki kinyang’anyiro cha u-miss ulichoingia ujue!”Kokos alimng’ang’ania.
Candy alitikisa kichwa kwa kuchanganyikiwa.
“Kweli Kokos, mi’ sina lolote nilifichalo lenye kuhusiana na tukio lile! Sijui ni kwa nini yule jamaa alitaka kuniteka kwa kweli!” Alijibu huku sauti yake ikivunjika kwa kilio.
“Er, okay Candy, sawa, sio ishu…” Bishkuku aliingilia kati kidiplomasia, kisha akamgeukia Kokos, “Kokos hapa sio mahakamani bwana, na Candy sio mtuhumiwa, upo?Hapa kuna tatizo ambalo inabidi sote tuunganishe vichwa vyetu kulipatia ufumbuzi, sawa?”
“Na ndio maana inabidi tuwe wawazi bwana!Mi nahisi Candy kuna kitu hajatuambia Bishi…sasa hatuwezi kusaidiana kutatua tatizo kwa mtindo huu!”
“Sina nilichowaficha Kokos! Ukweli ndio huo…mi’ yule mtu simjui, na sijui kwa nini alitaka kuniteka!”
“Basi labda ye’ kwa namna fulani anakujua!” Kokos alimjibu.
“Hilo pia silijui!”
Kimya kikatanda mle ndani.
Kokos alijisikia vibaya kujibizana na Candy namna ile na kumbana kwa maswali, lakini hakuona njia nyingine ya kulipatia ufumbuzi swala lile.
“Dah! Hii kali…na wala hakuonesha kuwa anakufahamu? Labda kwa kukuita kwa jina lako hivi?”Bishkuku alimuuliza.
“No. Hakuniita kwajina, ila alinitambua kuwa mimi ni Miss Dar City Center…”
“What?” Kokos aliuliza, umakini ukiongezeka, kisha akaendelea, “alikutambuaje?Yaani, ulijuaje kama amekutambua kuwa we’ ni miss Dar City Center…?”
Candy alivuta kumbukumbu akiwa amefinya sura yake.
“Ah, alisema…alisema kitu kama… ‘kuna kisu ubavuni kwako, miss Dar city center, ukijitia ujanja nakutoboa maini…’ Kitu kama hicho, ila alinitamkia kabisa neno miss Dar City Center…!”
“Ah!” Kokos aliguna huku akiinuka kutoka kwenye kochi alilokuwa amekalia, na Bishkuku akadadisika.
“What? Hilo lina maanisha nini Kokos?”Alimuuliza.
“Motive! Hiyo inatupa angalau motive…yaani sababu…ya yule jamaa kujaribu kumteka Candy…” Kokos alijibu huku akianza kuranda taratibu mle ndani, na wale akina dada wakamtumbulia macho.
“Sababu itakuwa nini sasa?”Hatimaye Bishkuku alimuuliza.
“Nadhani itakuwa inahusiana na Candy kushiriki shindano la u-miss, Bishi! Kwa nini yule jamaa amwite kwa wadhifa wake wa u-miss na si kwa jina lake?”
“Ah, sasa labda jina langu halijui?”Candy alidakia.
“Hapana. Hawezi kujua kuwa weweni miss Dar City Center, halafu asikujue jina lako…we’ umenadiwa magazetini kiasi cha kutosha Candy! Yaani kama angekuwa na kisa binafsi na wewe basi lazima angekuita kwa jina lako na si kwa wadhifa wako!”
“Kokos sikuelewi…” Candy alimwambia kwa mashaka.
“Tuambie lugha ya kawaida Kokos, sio zile lugha zako za ki-mahakamani bwana!”Bishkuku naye alimjia juu.
“Okay, iko hivi…watu wengi wenye visasi na mtu, pindi wakiwapata wabaya wao hupenda zaidi kuwaita kwa majina yao halisi! Lakini yule jamaa pamoja na kuwa jina lako atakuwa analijua, amekuita kwa wadhifa wako. Hii inaniambia kuwa kisa chake na wewe anakihusisha zaidi na mambo ya u-miss!” Kokos alijieleza kwa kirefu na kwa hamasa.
“Eh, basi labda tujitoe…?” Candy alisema kwa mashaka.
“Huenda ndilo haswa analotaka litokee yule mtu…akutishe ili ujitoe!”Kokos alidakia.
“Khah, sa’ kwa nini? Na kwa nini mimi?”Candy alihamanika.
“Basi huyo ni Sanura nakwambia!” Bishkuku alidakia kwa jazba, akimalizia kauli yale kwa kumtukania mama yake yule hasimu wake mkubwa.
“Sanura Kashogi?” Candy aliuliza kwa mshangao.
“Nani mwingine…ni yeye tu!” Bishkuku alisisitiza, safari hii akimalizia na kumtukania bibi yake yule hasimu wake.
Candy alimkodolea macho kwa mshangao.
Kokos naye alisimama kwa muda katika mirando yake mle ndani na kumtazama Bishkuku huku akionekana kuendelea kuwaza juu ya ile hali waliyokuwa wakikabiliana nayo muda ule.
“Hebu fikiria! Ni nani anayemhofia Candy katika kinyang’anyiro hiki kuliko wote…ni yeye!” Bishkuku aliuliza swali na kujijibu, kisha akaendelea.
“Na kwa nini anahofia Candy asishinde? Kwa sababu mrembo wake Tunis hatashinda…na Tunis asiposhinda na Candy akashinda, ina maana mimi nitakuwa nimemshinda. Nakwa Sanura hilo ni chungu sana kulimeza…”
“Sasa nd’o atume mtu kuniteka?”
“Sio kukuteka mrembo…kukutisha ili uogope…ujitoe mwenyewe, akiamini kuwa ukijitoa Tunis wake atashinda!” Bishkuku alisema kwa hasira.
“Ah, sasa kwani nani kamwambia kuwa mi’ nd’o n’tashinda!” Candy alimaka kwa mshangao.
“Atajua mwenyewe mshenzi yule ngoja nimuendee hewani nimpe vipande vyakemimi, mwanakharamu mkubwa!”Bishkuku alifoka huku akiiendea simu yake iliyokuwa juu ya meza.
“Acha hizo Bishkuku, tulia! Huna ushahidi juu ya hilo…!” Kokos alimwambia huku akiiwahi ile simu pale mezani na kuitumbukiza mfukoni mwake.
Bishkuku alitoa sauti ya kukereka na kurudi kuketi kwenye kochi.
“Sasa we’ ulikuwa na rai gani juu ya hili Kokos, twende polisi?” Alimuuliza.
“Tulia!Najaribu kufikiri kwanza!” Kokos alimjibu na kuzidisha kasi ya kuranda kutoka kona moja ya sebule ile kwenda nyingine.
Candy na Bishkuku walitazamana.
***
GTZ aliingia chumbani kwake na kwenda kupiga ngumi ukutani kwa hasira. Alirudi tena hadi mlangoni na kuurudia tena ukuta kwa kasi na kuurukia teke kwa hasira kali zaidi, akibabatiza unyayo wa kiatu chake kikubwa kwenye ukuta ule na kuaachia alama ya soli ya kiatu chake.
Huko nje ya chumba alimsikia msaidizi wake wa kazi za ndani akikimbia mbio kuelekea pale chumbani kwake.
“Kuna nini tena huko baba? Tatizo…?” Msaidizi wake alimuuliza kutokea nje ya chumba kile, na GTZ aliuma meno kwa namna ya kujaribu kupoza ghadhabu zilizokuwa zikimtuma afungue ule mlango na amvutie mle ndani yule mama mtu mzima na amshindilie mangumi ya mfululizo hadi hasira zake ziishe.
“No…no problem Bi.Mwana…endelea tu na kazi zako!”Alimpigia kelele kutokea kule chumbani huku akiketi taratibu kitandani kwake.
Alisikia hatua za yule msaidizi wake wa ndani aliyeitwa Bi. Mwana zikiondoka kutoka pale nje ya mlango wake, na akashusha pumzi za ahueni.
Alikuwa amechukia sana.
Hasira zake hazikuwa tu dhidi ya yule mfadhili wa Candy aliyeibuka bila kutarajiwa namna ile pale mtaani na kumvurugia mkakati wake mwingine dhidi ya Candy, bali pia zilikuwa dhidi yake yeye mwenyewe kwa kujaribu kumnyakua Candy namna ile pale mtaani bila ya mpango wowote wa kueleweka. Hakuwa ameandaa gari la kuondoka naye, na bado akashindwa kujizuia kumwacha tu mpaka itokee nafasi nyingine muafaka zaidi.
“Napoteza utulivu sasa…na hii ni mbaya sana!” Alijikemea na kubaki akiwa amejiinamia pale kitandani.
“Natumai yule mjinga hatakuwa amenikariri sura yangu…bila shaka lile “palanja” la uso nililomchapa litakuwa limehakikisha hilo, bloody fool!”Alizidi kujisemea.
Alibaki kimya mle ndani kwa muda mrefu, kisha akavua viatu na kujilaza kitandani.
Hata hivyo, itabidi nijichimbie kwa muda…wale jamaa watajitia makini sana baada ya tukio la leo. Sasa mi’ n’tawaacha wajisahau kwa muda, na nitakapowaibukia tena namaliza mchezo, shenzz taipp!
***
Kokos Wandiba aliendelea kuranda kutoka upande mmoja wa sebule ya Bishkuku kwenda mwingine, na akishafika huko kwenye huo upande mwingine wa sebule, anarudi tena ule upande aliokuwa hapo mwanzo, mkono wake wa kushoto ukiwa mfukoni mwake, wa kulia ukiwa unachezea-chezea ndevu zake za kidevuni zilizokuwa zimechongwa vizuri kwa muundo wa “O”, uso akiwa ameukunja kwa tafakuri nzito huku akimung’unya midomo yake kama kwamba ilikuwa ikimuwasha na kwa kuimung’unya namna ile ndio alikuwa anaikuna.
Candy na Bishkuku walikuwa wameketi kwenye makochi tofauti pale sebuleni, wakimtazama jinsi alivyokuwa akiranda huku na huko mle ndani. Hali ya hewa pale sebuleni ilikuwa inanuka mashaka matupu, na kwa muda ule si Bishkuku wala Candy aliyetaka kumsemesha yule bwana.
Candy alimtazama Kokos jinsi alivyotapakaa vumbi kwenye nguo zake na jinsi uso ulivyomtutumka kutokana na kofi alilobandikwa kule nje, alama za vidole vya yule jamaa aliyemzaba kofi lile zikiwa wazi pale usoni kwake. Moyo ukamnyongea na huruma kubwa ikamtawala kumuelekea yule jamaa aliyekutana naye katika mazingira mabaya kabisa wiki kadhaa zilizopita.
Alijiuliza iwapo alikuwa amefanya jambo la busara kutokuwa muwazi kuhusu zile kauli tata za yule jamaa aliyejaribu kumteka kule baranarani asubuhi ile.
Eti ninatafutwa! Natafutwa na nani…? Na kwa kisa gani…?
Alijikuta akiachia mguno wa mastaajabu na kutikisa kichwa.
Bishkuku alimtazama,na kwa kuhisi kuwa alikuwa ameguna kutokana na mkasa ule, akampa pole. Aliiafiki kwa kichwa pole ile, huku bado akiwaanamfikiria yule jamaa.
Halafu anasema kuwa eti nilidhani wamesahau…alimaanisha nini? Eeeh, Mungu wangu mbona mitihani hii ni mizito sana kwangu? Sijayasahau ya Jackie, yanatokea haya tena…sasa sijui ninini tena kitafuata Yarabi!
“Halafu yule ms--ge alinizaba kofi la uso kusudi ili nisimuone sura yake, mwanaharamu mkubwa!” Kokos aliropoka ghafla kutoka kwenye mawazo yake, na kuyakatisha yale ya Candy.
“Ennh?” Candyna Bishkuku waliropoka kwa pamoja.
“Ndio! Ndio…mjinga hakutaka nimuone sura…” Kokos alisemana kuendelea, “…hiyo ina maana bado ana nia ya kukurudia tena, Candy!”
“Heh, sasa mi’ nifanyaje jamani?”Candy alipayuka.
“Mi’ nakwambia huyo atakuwa ametumwa na Sanura tu!” Bishkuku alisema na kumtukania tena mama yake yule hasimu wake, kabla ya kuendelea, “…hivi kwa nini na si’ tusimshushie mikwara, au tusiende kushitaki polisi?”
“No, and no, Bishi!” Kokos alimjibu huku akiketi juu ya meza iliyokuwa pale sebuleni.
“No and no kivipi, Kokos? ‘Asa unadhani tutakabiliana vipi na hali hii?” Bishi alimuuliza, na Candy akawa makini kufuatilia majibizano yale.
“Okay, No ya kwanza ni kwamba tusimuulize chochote Sanura kwa sasa, kama ni yeye tunahitaji tumkabili tukiwa na ushahidi wa kutosha…na No ya pili,ni kwamba hatuhitaji kuihusisha polisi juu ya hili swala!” Kokos alijibu na wale akina dada wakapigwa butwaa.
“Tusiende polisi…kwa nini?”Hatimaye Candy aliuliza.
Kokos alimtupia jicho Bishkuku, na uelewa fulani ukapita baina yao. Candy aliwatazama nahakuelewa. Alihamisha macho yenye viulizo kutoka kwa kaka na kuyagandisha kwa dada.
“Ah…Kokos haelewani na ma-polisi…hivyo itabidi tusilifikishe polisi hili swala, Candy.Mi’ nilisahau juu ya hilo.” Bishkuku alimwambia kwanamna ya kulipotezea swala lile, lakini Candy hakumuacha alipotezee kirahisi.
“Kwa nini haelewani na polisi?”Alisaili.
“Ni hadithi ndefu Candy.Inahusisha maisha yangu ya hapo nyuma…kuna matukio fulani ambayo yanawafanya polisi wawe standby muda wote kusubiri nifanye kosa dogo tu wanifanyizie…sasa sitaki kukuburuza na wewe kwenye mashaka hayo…” Kokos alimjibukwa kirefu, na Candy akazidi kudadisika.
“Ah, sasa…ndio hayo mambo yaliyosababisha unyang’anywe leseni yako ya uwakili?”Alimuuliza.
Kokos alizungusha macho yake kuonesha kuwa ule haukuwa mjadala alioupendelea sana.
“Ndio Candy, lakini hapa tunatakiwa tuzungumzie swala lako na sio langu.Naomba turudi kwenye hili lililopo mbele yetu hivi sasa, sawa?” Alimjibu kwa utulivu wa kujilazimisha.
“Sawa…sasa tunafanyaje?” Bishkuku alidakia na kuukata ule mjadala.
“Mi’ naona hapa kwako si salama tena kwa Candy hivi sasa…” Kokos alimwambia.
“Kwa hiyo…?”
“Itabidi nyote mhamie kwangu kwa muda, mpaka hapo tutakapomdhibiti yule fala aliyetaka kumteka Candy leo hii.”
Bishkuku na Candy walitazamana, kisha Bishkuku akamgeukia mdogo wake.
“Na…umepanga kumdhibiti vipi sasa Kokos? Maana polisi ndio kama hivyo…hatuwezi kuwashirikisha!”
“Unadhani hata tungewashirikisha wangetusaidia kitu?” Kokos alimuuliza kwa hasira kiasi, na Candy akapata hisia kuwa lolote ambalo limetokea baina ya Kokos na wanausalama lilikuwa likimghabisha kila anapotajiwa polisi.
“Okay, tuliache hilo…sasa tunamdhibiti vipi yule jamaa? Maana kwa mambo mliyoniambia kuwa ameyafanya huko nje, ni wazi kuwa yule ni mtu hatari sana kimapigano…!” Bishkuku alimwambia.
Kokos alifinya uso kwa tafakuri kidogo.
“Yeah, jamaa liko vizuri lile…” Alisema huku bado akiwa amefinya uso kwa mawazo.
“Sasa itakuwaje…?” Candy aliuliza.
“Hilo niachieni miye.N’tampatia dawa yake tu, pumbavu zake!” Kokos alisema kwa hasira, wazi akiwa amepitisha uamuzi juu ya kumdhibiti yule adui yao.
“Sasa hilo litakuwa vipi Kokos wakati sote hatukumuona sura yake?”Candy aliuliza.
“Ni kweli…lakini atarudi tena tu yule…na atakaporudi atanikuta niko tayari, don’t worry!” Kokos alimjibu na kimya kikachukua nafasi kwa muda mle ndani.
“Sawa Kokos. Kwa hali ilivyo ni kweli itabidi tuhame hapa.”Hatimaye Bishkuku alisema.
“Okay, basi na tuondoke sasa hivi!Maanayule jamaa hawezi kurudi tena hapa muda huu.Bila shaka nyie mtahitaji kufungasha baadhi ya vitu vyenu sio?”Kokos aliwauliza.
“Yeah…itabidi tufungashe haswa tena, sio kidogo…” Bishkuku alimjibu.
“Okay basi. Mi’ nashuka huko chini kidogo,nikirudi… safari!”
“Unaenda wapi sasa?”Candy alimuuliza.
“Kuna ile teksi uliyosema kuwa yule fala alikuwa anataka kuitumia kukutoroshea…”
“Ndio…”
“Nataka kwenda kuuliza iwapo naweza kumpata dereva wake nimsaili kidogo…”
“Unadhani naye alikuwa anashirikiana na yule jamaa?”Candy aliuliza.
“Si mbaya kufuatilia, ingawa sidhani…kama angekuja na teksi kwa ajili hiyo asingekuja na pikipiki pia.”Kokos alijibu.
“Yeah, hata mi’ nilikuwa nahisi hivyo…” Bishkuku alidakia.
“Kwa jinsi ilivyokuwa mi’napata hisia kuwa swala la teksi alilifikiria pale pale…hakuwa ameiandaa awali yule…” Candy naye alichangia.
“Sawa…lakini haitaumiza lolote kwenda kuhakikisha…” Kokos alijibu na kutoka nje.
Nusu saa baadaye walikuwa barabarani kuelekea nyumbani kwa Kokos, Bishkuku na Candy wakiwa kwenye gari la Bishkuku aina ya STI muundo mpya, hali Kokos akiwafuata nyuma kwa Escudo yake, muda wote akiwa makini sana kuangalia iwapo kulikuwa kuna gari lolote lililokuwa likiwafuata.
Wakati akiendesha gari lake Kokos alikuwa akiwaza mengi sana juu ya tukio la asubuhi ile.
Baada ya mwendo wa muda, alichukua simu yake ya kiganjani na kupiga namba aliyokuwa akiifahamu kwa kichwa. Simu iliita kwa muda mrefu, na alikuwa anataka kukata wakati mtu wa upande wa pili alipopokea.
“Ni mimi…nahitaji kuonana nawe haraka sana!” Kokos alimwambia Yule mtu wa upande wa pili bila ya kusalimia.
Alimsikiliza kwa muda mtu aliyepokea ile simu aliyoipiga, kisha akasema, “Okay basi, no problem…nitakutumia meseji ya kukujulisha tukutane wapi na saa ngapi.”
Akakata simu.
Aliendelea kuendesha gari akiwa makini huku uso wake ukiwa umejifinyanga kwa tafakuri iliyokithiri.
***
Kiasi cha kama saa tatu baada ya ile tafrani ya GTZ kule mtaa wa Aggrey, sehemu nyingine ya jiji John Koccho aliangalia kulia na kushoto kabla ya kuvuka barabarana kuingia kwenye jengo lenye ofisi zinazoshughulika na uratibu wa mashindano ya Miss Tanzania nchini, lililokuwa kwenye makutano ya barabara za Jamhuri na Indira Gandhi jijini Dar.
Aliingia eneo la mapokezi la ofisi zile za ulimbwende nchini na kuangaza macho kwenye ubao wa matangazo uliokuwa pale ndani kwa muda huku akimtupia jicho la pembeni mrembo aliyekuwa pale mapokezi, ambaye alikuwa anawahudumia wazungu wawili.
Hakuona kipya cha kumkidhia haja yake pale kwenye ule ubao wa matangazo, na alipoona wale wazungu wakiondoka kuingia kwenye ofisi nyingine mle ndani, aliiweka sawa tai yake na kuisogelea ile kaunta maridhawa ya pale mapokezi.
“Habari yako Miss Tanzania wa mwaka…?” Alimsalimu yule binti wa mapokezi huku akimtandazia tabasamu lake mwanana ambalo siku zote limekuwa likimpatia akitakacho kutoka kwa mabinti, akiliacha lile swali lake likielea kusudi ili yule binti atoe jibu.
Binti alimtazama kama kwamba alikuwa ana kichaa, lakini akakutana na tabasamu maridhawa na macho madogo, makali, yenye tashwiwisi na ahadi ya tashwishi nyingi zaidi, na akajikuta akitabasamu pasina kupenda.
“Hah, miss Tanzania wa mwaka gani huyo awe miye? I wish! Mi’ ni karani tu wa mapokezi hapa. Nikusaidie nini, kaka?” Binti alimjibu huku lile tabasamu lake likipanda cheo na kuwa kicheko laini,na John Koccho akaongezea chachu nyingine kwenye tabasamu lake, nalo likabadilika kutoka lile la tashwishi na kuwa la ushindi.
“Aww! Ndo maana kila siku tunashika mikia tu kwenye miss world…yaani warembo halisi tunawaweka mapokezi, na warembo kidogo nd’o tunawapeleka kugombea urembo wa dunia? Mbaya sana!”Koccho alijitia kusema kwa masikitiko ya yakini huku akiwa amekunja uso, na binti akaachia kicheko cha sauti.
“Hebu acha kunizeveza huko kakaangu, hebusema kilichokuleta!” Binti akamwambia huku akimalizia cheko na John Koccho akajua kuwa alilolifuata pale amelipata. Alimpa mkono na kujitambulisha.
“Ismail Mrisho,production managerwa KIU Investments…nimekuja kuulizia juu ya ratiba za matukio yajayo kuelekea kwenye kinyang’anyiro cha Miss Ti-Zedi mwaka huu, sijui natakiwa nionane na nani?” Alimwambia na kumuuliza huku akimtazama moja kwa moja machoni, akijua fika kuwa ile kauli yake itamchanganya yule binti.
Na kweli.
“Production Manager? Kiu Investment?” Binti aliuliza kwa mashaka huku bado akitabasamu, naye akatanua tabasamu zaidi.
“Ndio, hujawahi kusoma gazeti la KIU we’?”
“Ah, Kiu ya Jibu…?Hilo mbona huwa silikosi?”
“Haswa!Basi mi’ nd’o production managerwa gazeti hilo. Sasa tulikuwa tunataka tufanye matoleo maalum ya Miss Tanzania ya mwaka huu kuanzia huku kwenye maandalizi hadi kule kwenye shindano lenyewe…hiyo ratiba itanisaidia mimi kupanga vijana wangu wa kukusanya habari hizo vizuri..” Alidanganya bila wogana kwa hujiamini, na alipoona yule binti bado hajaelewa analolitaka, akaendelea.
“Yaani itanisaidia kujua bajeti yangu niipangaje.Kwanikama ma-miss wanapelekwa kutembelea mikumi, basi na mi’ napeleka waandishi wangu mikumi…sasa nisipokuwa na taarifa za mapema sitaweza, unanipata?”
“Oh, kumbe na nyi’ mko makini kwenye kazi zenu hivyo? Sikujua bhana…sasa hiyo itabidi uende ofisi ya afisa habari wetu…” Binti alimjibu.
“Ambako ni wapi…?” Koccho aliuliza.Binti alianza kumuelekeza lakini akamkatisha.
“Huko sio kuna wale wazungu niliowaona ukiwaelekeza muda mfupi ulipita?” Alibahatisha kutupa jiwe kizani.
“Oh, yesbhana, Dah! Itabidi usubiri watoke kwanza basi…”
“Ah, natakiwa ofisi kwa kikao fulani…huwezi kunisaidia kunipatia hiyo taarifa fasta na mi’ nikawahi majukumu mengine dadaangu?” Alimuuliza, sasa uso wake akiwa ameuweka kwenye mashaka mazito.
Binti alisita kidogo, na Koccho akammaliza.
“Sio kama ni taarifa ya kuhatarisha usalama wa taifa niitakayo dadaangu. Ni kwakunirahisishia utendaji kazi tu na kulitangaza ipasavyo shindano la Miss Ti-Zedi mwaka huu, eenh…Please!” Aliomboleza, na binti akaingia laini.
“Okay…subiri hapa kidogo!” Akamjibu na kuinua simu. Akaongea na mtu mwingine kwa sauti ya chini kwa muda mfupi, kisha akairejesha mahala pake ile simu na hapo mteja mwingine akafika kuhitaji huduma zake.
“Subiri kidogo basi mista Mrisho, okay?” Alimwambia kwa tabasamu pana. Koccho akamshukuru kwa tabasamu. Alijisogeza pembeni na kubaki akipiga-piga ncha za vidole vyake kwenye uso wa ile kaunta wakati yule binti wa mapokezi akimuhudumia yule mteja mwingine. Muda mfupi baadaye, binti mwingine mwenye hadhi ya urembo wa taifa alikuja pale mapokezi na kumkabidhi yule binti wa mapokezi karatasi iliyotolewa kwenye kompyuta.
Binti aliitazama kwa muda, kisha akamtazama Koccho na kumkabidhi.
“Here you are Mister Mrisho…natumai sasa kazi ya kutupa shavu Miss Ti-Zedi itakuwa nyepesi, ratiba yote iko hapo!”
“Oh, thank you, thank you, thank you so much bibie! Wewe ni zaidi ya malaika wa upendo!” John Koccho alimwambia huku akiipokea ile karatasi na akimruzuku lile tabasamu lake la kunyong’onyeza.
Alimuacha yule binti akiendelea kuyeyushwa na zile tabasamu zake naye akatoka nje ya jengo lile akiwa na ratiba kamili ya matukio yajayo kuelekea kwenye kinyang’anyiro cha Miss Tanzania.
Akiwa na uso uliomakinika kwa kile alichokuwa amekidhamiria, na sio ule uliokuwa ukiruzuku matabasamu dakika kadhaa zilizopita, John Koccho alivuka barabara na kujichanganya katikati ya jiji.
“Okay Miss Dar City center…utakapokuwa na mi’ nitakuwepo, na labda nitapata wasaa wa kuwa nawe chemba japo kwa dakika tano…zitanitosha sana!
***
***
Nyumbani kwa Kokos Wandiba Candy alipitiliza hadi kwenye chumba alichoelekezwa na kujifungia. Aliitoa ile memori kadi ya Jackie na kuiweka kwenye simu yake. Alipogundua kuwa ni kweli ile picha aliyopigwa na Jackie ilikuwamo mle kwenye
na kuitumbukiza chooni.
Aliingia bafuni kuoga huku akili ikimzunguka juu ya matukio ya asubuhi ile, kubwa zaidi likiwa la yule mwendesha pikipiki aliyejaribu kumteka. Alikuwa na hakika kabisa kuwa alishawahi kuisikia sauti ya yule mtu.
Lakini wapi…? Na lini…?
Na hii habari ya kuwa eti mi’ natafutwa…inahusu nini?
Hakukuwa na hata moja lililoleta maana akilini mwake.
Baada ya kuoga alibadili nguo na kwenda sebuleni, ambako alimkuta Kokos akiwa ameshaoga na kubadili nguo, na akisikiliza nyimbo za marehemu 2Pac kwa sauti.
Bishkuku alikuwa akijishughulisha kuandaa staftahi kwenye eneo la maakuli pale ndani.
“Oh, bora umejitokeza mrembo wangu, maana Miss Tanzania wamenipigia simu muda si mrefu uliopita…” Bishkuku alimwambia na Candy akamfuata pale kwenye eneo la maakuli.
“Wanasemaje?” Alimuuliza, na Bishkuku akamjuza kuwa alitakiwa kujumuika na warembo wenzake siku iliyofuata kwa ajili ya safari ya kwenda kutembelea kituo cha watoto yatima kilichokuwa nje kidogo ya mji.
“Ah, angalau huko nitakuwa nimejichanganya na watu! Sitakuwa na mashaka tena na yule mwendesha pikipiki…” Candy alisema huku akiketi mezani kwa ajili ya kupata staftahi.
“Huna haja ya kuwa na wasiwasi wowote Candy…we’ zingatia maandalizi ya mashindano yako tu …yule jamaa hatokusumbua tena…” Kokos alidakia, na Candy na Bishkuku walitazamana.
“Sawa bwana. Siye twakutusikiliza wewe tu.” Bishkuku alimjibu.
Kokos aliendelea kusikiliza miziki yake huku akionekana kuwa na mawazo tele.
“Un…unadhani Kokos ataweza kupambana na yule jamaa Anti Bishi? Yule mtu ni hatari sana yule!” Candy alimuuliza Bishkuku kwa sauti ya chini, mashaka ya wazi yakijidhihirisha usoni kwake.
“Ah, kupambana naye kimapigano hawezi…Kokos ni msomi…na anaweza kuwa na uhuni fulani wa kimjini, lakini sio mtupa makonde…” Bishkuku alimjibu kwa sauti ya chini pia. Candy akahamanika kidogo.
“Ah, sasa anavyosema atamdhibiti yule mtu…atawezaje?”
“Ah, hata sijui…ila namjua Kokos ni mwingi wa mbinu, kwa hiyo kama kasema tusiwe na wasiwasi basi na iwe hivyo…tusiwe na wasiwasi, okay? Mi’ namuamini sana. Kwa hiyo naomba na we’ umuamini katika hili.”
Candy alikaa kimya kwa muda, kisha akakubaliana na ushauri wa Bishkuku.
“Okay, Anti Bishi…”
Muda mfupi baadaye, walitoka walitoka kwenda saluni na kutafuta mahitaji mengine ya kilimbwende mjini, wakimuacha Kokos peke yake mle ndani.
***
Saa kumi na mbili za jioni siku ile, Kokos Wandiba aliegesha gari lake nje ya baa moja tulivu sana iliyokuwa maeneo ya Masaki jijini Dar. Ingawa ile baa ilikuwa na sehemu ya nje iliyokuwa wazi, pia ilikuwa na sehemu ya ndani ambamo watu wapendao faragha huitumia. Aliingia moja kwa moja kwenye ukumbi wa ndani wa ile baa na kuchagua kiti kilichompa nafasi ya kuona kila aliyekuwa akiingia ndani ya ukumbi ule. Akiwa amefika nusu saa kabla ya muda wa miadi, aliagiza juisi ya boksi na kujiweka sawa kwenye kiti chake kuanza kumsubiri mtu aliyekuwa na miadi naye.
Muda huo ujumbe mfupi uliingia kwenye simu yake ya kiganjani na alipousoma alijikuta akiachia mguno wa fadhaa. Aliinuka na kutoka nje ya baa ile, akiiacha ile juisi aliyoilipia pale juu ya meza. Aliingia kwenye gari lake kuelekea kwenye baa nyingine iliyokuwa maeneo ya jirani na ile aliyokuwa amekaa hapo awali. Dakika kumi baadaye aliingia kwenye hiyo baa aliyoelekezwa na ule ujumbe ulioingia kwenye simu yake.
Aliangaza huku na huko mle ndani bila ya kumuona mtu aliyemkusudia. Alichagua kiti kilichomuwezesha kuona waingiao na watokao kwenye ile baa na kuagiza kinywaji kingine kama kile alichokiacha kwenye ile baa ya kwanza. Alijiegemeza kwenye kiti na kusubiri, akili yake ikimrudia yule mtu aliyekuja kumsubiri pale kwenye ile baa…
***
Miaka mitatu iliyopita wakili Kokos Wandiba alifanikiwa kumtetea mfungwa aliyekuwa akikabiliwa na kesi nzito ya mauaji. Pamoja na kuwa ni kweli jamaa aliua, alifanikiwa kutumia vifungu adimu na vigumu vya sheria pamoja na mbinu kali iliyosababisha jamaa aachiwe.
Aliendesha uchunguzi binafsi baada ya kupewa taarifa muhimu na yule mtuhumiwa wa mauaji yale, na utetezi wake ukalazimisha afisa muhimu na wa ngazi ya juu katika jeshi la polisi aitwe mahakamani kutoa ushahidi na kujibu maswali ya upande wa utetezi.
Afisa aligoma kuja mahakamani, wakili Kokos akasisitiza ni muhimu na lazima apande kizimbani kwani naye alihusika na kosa ambalo mteja wake, ambaye pia wakati huo alikuwa ni afisa wa jeshi la polisi alikuwa anashutumiwa kwalo.
Afisa alipozidi kugoma, Kokos akashinikiza mahakama kumuachia huru mteja wake kwa kutumia kipengele cha “mistrial”, yaani kesi ambayo tangu mwanzo haikupaswa kuwa kesi.
Hakimu hakuwa na namna. Akaamuru yule afisa wa jeshi la polisi apande kizimbani achapwe maswali na wakili wa utetezi Kokos, au mteja wa Kokos aachiwe na jamhuri itafute muuaji halisi…
Swala la kumpandisha kizimbani yule afisa wa polisi lilikuwa gumu sana kwa upande wa jamhuri kwani afisa yule alikuwa anajua mengi ambayo jamii haikupaswa kuyajua, na Kokos alikuwa ameshayajua kupitia kwa mteja wake.
Basi jaji akaamuru jamaa akaachiwe huru.
Hilo na mengine aliyoyafanya wakati wa enzi zake za uwakili vilichangia sana kwa maaskari kumuwekea kinyongo kikubwa Kokos. Ni miongoni mwa mambo yaliyochangia hata akanyang’anywa leseni yake ya uwakili hapo baadaye.
Baada ya kuokolewa na kitanzi, yule jamaa alijiweka kwenye deni kubwa kwa Kokos, akimuahidi kujitolea hata nafsi yake ili kumlipa kwa ile nafasi nyingine ya kuendelea kuishi aliyompa. Na ingawa walikuwa wakiwasiliana kwa nadra sana tangu wakati huo, Kokos hakuwahi kumoumba msaada wowote yule jamaa.
“Okay wakili…what is it?” Sauti nzito ilikatisha mawazo yake, na akajikuta akiruka huku akigeukia kulia kwake ambako ile sauti ilitokea, na kumuona mtu mrefu na mweusi akiketi kwenye kiti kilichokuwa kando yake pale mezani.
“Morandi!” Aliita huku uso wake ukiachia tabasamu la mshangao naye akisimama.
“Um..umepitia wapi… sijakuona kabisa!” Alimuuliza yule mtu huku akiketi tena kitini kwake.
Morandi Gwaza alimtazama kwa muda kabla ya kumjibu.
“Mimi sio tena afisa wa usalama bwana wakili, lakini mbinu zote bado ninazo. Unadhani kwa nini nilikwambia uje hapa badala ya pale ulipochagua wewe hapo mwanzo? Hili eneo nalijua nje ndani…” Alimjibu kwa sauti yake nzito na lafudhi yake ya pole pole.
Kokos alitabasamu.
“Na mimi sio wakili tena mtuhumiwa wangu, lakini pia mbinu zote bado ninazo!” Akamjibu na wote wakacheka huku wakigonga na kupeana mikono.
“Hatujaonana kitambo Morandi…” Kokos alimwambia, na Morandi akaafiki kwa kichwa huku akimtazama usoni.
“Unaonekana uko kwenye matatizo, wakili wangu…” Alimwambia.
“Yeah! Yaani hujawahi kusema lililo ndilo kama leo Morandi, niko kwenye tatizo na nahitaji msaada wako.” Kokos alimjibu.
Morandi alikaa kimya kwa muda huku akiendelea kumtazama usoni.
“Na hiyo alama ya kofi hapo usoni…ni sehemu ya matatizo uliyo nayo?” Alimuuliza.
Kokos alibana midomo yake na kuafiki kwa kichwa.
Morandi Gwaza alitikisa kichwa kukubaliana na ukweli kuwa hakika Kokos alikuwa kwenye matatizo, na muda huo muhudumu alifika kumuuliza kinywaji atakacho. Aliagiza Grand Malt na yule mhudumu akaenda kutimiza aliloagizwa. Hakuna aliyeongea kwa muda wote mpaka yule mhudumu alipoleta kile kinywaji na kuondoka.
“Okay…ni msaada gani unaouhitaji kutoka kwangu Kokos? Lolote liwalo, elewa kuwa bado nina deni kwako na siku zote nimekuwa nikisubiri kupata nafasi ya kulilipa deni hilo. Sasa niambie…wito huu ndio nafasi yangu ya kulipa deni hilo?”
“Ndio ndugu yangu. Nimefikwa na jambo zito ambalo kama nisingekuwa na hakika kuwa unaliweza, wala nisingekusumbua…”
“Tatizo ni nini Kokos?” Morandi alimkatisha.
Kokos akamwelezea kila akijuacho kuhusu Candy na ule mkasa wa yule jamaa mwenye pikipiki. Alipomaliza maelezo yake, Morandi alishusha pumzi ndefu na kubaki akiwa amefinyanga midomo yake kwa muda. Kisha akamtazama moja kwa moja usoni.
“Okay…nimesikia kisa cha huyo mrembo wa Dar City center na madhila yake…unataka mimi nifanyaje sasa?”
“Nataka Candy awe salama Morandi. Zaidi ya hapo nataka tumdhibiti yule jamaa, tujue yeye ni nani na anataka nini kwa Candy.”
“Na nikitimiza hilo nitakuwa nimelipa deni langu kwako?”
“Deni pamoja na riba!”
“Okay. Hilo hesabu limetimia. Ila nitalifanya kwa njia nizijuazo mimi…sitaki kuingiliwa!” Morandi alimjibu bila kusita.
“Sawa. Na kama utahitaji msaada wowote…fedha, taarifa…lolote. Nijulishe.”
“Sawa. Ila kuanzia sasa hutawasiliana tena nami kwa hii namba yangu uijuayo…” Morandi Gwaza alimwambia, na hapo akampatia namba nyingine ya simu.
“Nawe nataka utafute namba nyingine kabisa ya simu ndio uitumie hiyo kuwasiliana nami kwenye hii namba mpya niliyokupa. Mara ya kwanza utakaponipigia kwa hiyo namba yako mpya neno lako la kwanza kusema liwe ‘Candy’. Hapo nitajua kuwa ni wewe, sawa?”
“Duh…sawa, bwana.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Na…hakuna kutumiana meseji. Tukihitajiana ni kwenda hewani tu, hivyo hiyo simu mpya utakayotumia uwe nayo muda wote!”
“Nimekusoma kaka.”
Baada ya hapo Morandi alimuuliza maswali kadhaa kuhusu yule jamaa mwenye pikipiki, lakini Kokos hakuwa na majibu yoyote ya msaada kwake.
“Tutawasiliana!” Hatimaye alisema na kuinuka kutoka kwenye kiti alichokuwa amekalia na kutoweka kama upepo kutoka eneo lile.
Kokos Wandiba alibaki akiwa ameketi peke yake pale baa.
***
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment