Simulizi : Miss Tanzania
Sehemu Ya Tatu (3)
” Alisema.
“Okay…ila mi’ nitafikia moja kwa moja chooni nikajiweke sawa kwanza!” Nuru alijibu na wakatoka kuelekea kule ukumbini.
Walihakikisha kuwa wamejifuta vumbi kadiri walivyoweza, lakini Nuru alikuwa amechafuka sana mgongoni pale alipoanguka baada ya kupigwa kumbo na John Koccho, bingwa wa kuingia mitini.
Morandi alimpa koti la suti yake naye akalivaa juu ya lile gauni lake ilikuficha hali ile.
“Yule fala n’na hasira naye kwel’ kweli, Mo…nikimpata atajuta!” Nuru alinong’ona kwa hasira huku wakiingia tena mle ukumbini.
“Yaa…hilo mbona nililijua kitambo? Safari hii katuotea…na hatopata tena nafasi hiyo next time…” Morandi alimjibu.
Kule ukumbini walimuona msema chochote akipanda jukwaani baada ya watumbuizajiwa mwisho kumaliza onesho lao la muziki, naye akanadi kuwa majaji walikuwa wameshafikia maamuzi na kwamba baada ya muda wale warembo watano watatoka tena pale jukwaani kuvuna walichopanda.
Shangwe na hoi hoi zikatawala ukumbini.
“Okay…mchezo ndo’ unaishia hapa sasa…” Morandi alisema, na Nuru akaguna. Morandi akamgeukia na kumuuliza kulikoni.
“Ah, sijui bwana, lakini kuna wazo kimenipitia hapa kidogo linanipa mashaka…” Nuru alimjibu.
“Wazo gani tena hilo, Nuru?”
“Ah, yaani…unadhani itakuwaje kama Candy akichukua ubingwa hii leo?” Nuru alimjibu kwa swali, na Morandi akakunja uso kulitafakari swali lile, wakati kule ukumbini warembo wakiingia tena pale jukwaani kwa mbwembwe zote, muziki maalum ukiwasindikiza, watazamaji wakiwapigia makofi kwa shangwe.
“Mnhu! Sijui bwana…lakini nafikiria iwapo tulizuiwa kumhoji Candy wakati akijiandaa kwa shindano la Miss Tanzania…unadhani tutapewa nafasi hiyo akitoka mshindi hii leo na akijiandaa kwa shindano la Miss World?” Nuru alimuuliza.
Morandi alisonya na kumgeukia kwa jazba.
“Halafu huyu Kokos asijaribu kuniletea ujinga huo nakwambia!” Alikoroma kwa hasira.
“Ni wazo tu lililopita kichwani mwangu hilo!” Nuru alimjibu, na kugeuka kuelekea msalani kujiweka uso wake sawa, akimuacha Morandi akiwa ameuma meno kwa hasira.
***
Wale warembo watano walionesha shoo moja maridhawa pale ukumbini. Wakicheza kufuatisha midundo maalum ya muziki uliondaliwa rasmi kwa ajili ya shoo ile ya kuwaaga watazamaji kabla mmoja wao hajavikwa taji la urembo wa taifa usiku ule. Ilikuwa ni shoo kali sana na wanachi waliohudhurua walijikuta wakisimama na kuwapigia makofi, mbija na hoi hoi zikitawala ukumbi mzima.
Kokos alimgeukia dada yake, na kumuona akiwa ameinama huku amefumbata viganja vyake kifuani, akiomba dua. Alimshika viganja vya mikono yake na kumtoa ile mikono pale kifuani.
“Aamin! Tayari tumeshaitikia dua Bishkuku, mtazame mrembo wetu anavyoshambulia jukwaa kule…dua tushaomba sana tu, sasa ni wakati wa kushuhudia matokeo ya dua zetu bwana!” Alimnong’oneza, na Bishkuku alitabasamu kwa mashaka.
“Okay…this is really it, sasa!” Alisema na kutazama kule jukwaani.
Warembo walimaliza shoo yao, na kuamsha shangwe nyingine kubwa zaidi kutoka kwa wahudhuriaji. Wao walirudi na kusimama kilimbwende kama kawaida yao, nyuso zao zikiwa zimepambwa kwa matabasamu mwanana.
“Yeah…this is really it!” Kokos alikubaliana na dadaye, akimaanisha kuwa sasa mambo ndio yalikuwa yameiva.
Akiwa amesimama pale jukwaani mbele ya maelfu ya watazamaji waliokuwa wakiwapigia makofi huku wakiwatazama kwa heshima na furaha kubwa, Candy Gamasala aliuhisi tena msisimko wa ajabu aliouhusi siku aliyokuwa amesimama namna ile akisubiri kunadiwa mshindi wa taji la Miss Dar City Center.
Lakini hii ni zaidi ya vile…niko mbioni kupata…au kokosa…umalkia wa urembo wa taifa! EeMungu nijaalie mimi!
Alijiwazia huku moyo ukimwenda mbio, na bila kupenda alijikuta akipeleka macho yake kwa kina Bishkuku.
Kutoka pale alipokuwa amesimama, aliweza kuona wahka uliojaa usoni kwa Bishkuku na utulivu ulitanda usoni kwa Kokos. Alijikuta akiombea kulipata lile taji sio kwa ajili yake tena, bali kwa ajili ya Bishkuku. Alijua ni jinsi gani ilivyokuwa muhimu kwa yule mkufunzi wake kuingiza mrembo katika shindano la Miss World, na hakutaka kumuamgusha,
Lakini swala ndio haliko mikononi mwangu tena sasa!
Alihamishia macho yake kwa Kokos Wandiba, ambaye sasa alikuwa ameshamzoea kwa kiasi kikubwa, na alikumbuka jinsi alivyokutana kwa mara ya kwanza na yule jamaa, na akajikuta akitabasamu zaidi na akikaribia kuangua kicheko.
Akawageukia watazamaji waliofurika pale ukumbini, na kwa mara nyingine akajikuta akimshukuru Mungu kwa kumfikisha pale, hakujua iwapo atashinda au atashindwa, lakini kamwe maishani mwake hakutaraji kama watu wale wenye heshima na hadhi zao wangekuwa ni miongoni wa wanaomtazama kwa matumaini huku wakimchekea na kumpigia makofi namna ile.
Aliikumbuka ahadi aliyojiwekea siku alipokuwa amesimama mbele ya hadhira kama ile kule Diamond Jubilee akisubiri kunadiwa mshindi wa Miss Dar City Center.
…nitahakikisha kuwa siku moja makofi haya n’takuwa napigiwa mimi tu hapa jukwaani …ipo siku…siku moja…one day!
Sasa hiyo siku ndio leo… je itakuwa?
Hapo msema chochote aliwajulisha wahudhuriaji kuwa mwenyekiti wa kamati ya Miss Tanzania alikuwa tayari kuja kuwanadi washindi watatu wa shindano lile, na Candy akameza funda kubwa la mate huku akimtazama yule mwenyekiti mwenye asili ya kiasia, Prakshantji Prakteshji akielekea pale jukwaani akiandamana na mratibu wa shindano la Miss Tanzania nchini, Miss Tanzania anayemaliza muda wake usiku ule na baadhi ya watu wengine ambao hakuweza kuwatambua.
Moyo wake ukaongezeka kasi maradufu.
Muda huo luninga zote tatu kubwa sana zilizokuwa zikionesha kila kilichokuwa kikitokea mle ukumbini zilibadilika na kuonesha jumba kubwa la kifahari, na gari ghali sana la kifahari aina ya Vogue likiwa limepaki mbele ya jumba lile, na miguno ya matamio ikawatoka watazamaji wote waliokuwa pale ukumbini, pamoja na wale warembo watano waliokuwa wamejipanga kusubiri hatima yao pale jukwaani.
Prakshantji Prakteshji alitabasamu na kuanza kuongea kwa kiswahili fasaha kilicho chovywa-chovywa na lafudhi ya kihindi.
“Mabibi na mabwana, inanipa furaha na heshima kubwaleo hii kusimama hapa mbele kumnadi mshindi wa shindano hili kubwa kabisa la urembo hapa nchini. Lakini inanipa furaha kubwa zaidi kuweza kuonesha zawadi kubwa kuliko zote zilizowahi kutolewa kwa mshindi wa taji la urembo wa Miss Tanzania…” Alisema huku akioneshea kwa mkono wake kwenye moja ya zile luninga kubwa pale ukumbini na kwa mara nyingine ukumbi ukaachia mguno wa pamoja kustaajabia zawadi zile.
“Na hii inanifanya niwe na fahari kubwa kuweza kumnadi mrembo pekee wa taifa letu aliyeweza kunyakua taji na zawadi kubwa kama hii…na yote haya ni kutoka na ufadhili mkubwa wa wafadhili wetu, hususan benki ya…”
“Hebu acha longolongo kemcho…tutajie huyo mshindi tupate kwenda sawa hapa saa hizi, vipi wewe?” Kokos alisema kwa wahka kutokea pale alipokuwa ameketi, kukereka na kuishiwa subira kukijieleza wazi wazi kwenye sauti yake, lalamiko lake likimezwa na makofi ya wananchi waliokuwepo, bila shaka kuishangiia ile benki iliyotoa zawadi ya lile jumba la kifahari.
“…kwa hiyo kabla sijamtangaza mshindi atakaye ondoka na funguo mbili muhimu leo hii pamoja na zawadi nyingine…ufunguo wa nyumba na ufunguo wa Vogue…” Prakshantji alisema, na ukumbi ukaachia shangwe kutokana na kauli ile, naye alibidi asubiri shangwe ziishe ndipo alipoendelea kuongea.
“…kabla sijafanya hivyo, napenda nianze kwa kumtaja mshindi wa tatu wa shindano hili, naye si mwinginine bali ni…”
Eee Mungu jaalia huyo asiwe mimi!
Candy alifumba macho na kuomba mungu, na hapo alimsikia yule mwenyekiti akimnadi mshindi wa tatu.
“Miss Kigoma, Mboja Kisesa!”
Ukumbi ulishangilia kwa hoi hoi, wakati Candy akishusha pumzi za ahueni na yule mrembo kutoka Kigoma akijitokeza mbele huku akitabasamu na akiwapungia wananchi. Wasichana wawili waliondaliwa maalum kwa zoezi lile walimfuata na kumvika utepe uliopita juu ya bega lake la kulia na kukikata kifua chake, utepe uliomnadi kuwa yeye ndiye mshindi wa tatu, maadishi “2nd Runner-Up” yakiwa yameandikwa kwenye utepe ule. Nderemo hafifu zilizochagizwa na muziki maalum wa kuwapongeza washindi wa shindano lile zilitawala ukumbini.
Mshindi wa tatu alikwenda kusimama kando ya kiti maalum kilichoandaliwa kwa ajili ya mshindi ya mpambano ule. Candy alikitumbulia macho kile kiti na donge likamkaba kooni.
“Na sasa nataka niwatajie mshindi wa pili wa shindano letu la leo mabibi na mabwana…” BwanaPrakshantji alikuwa akiongea kule mbele, na Candy akamakinika, akihisi miguu ikimwisha nguvu.
Eee Mungu nijaalie na huyu atakayetajwa sasa asiwe miye…please!
“The first runner-up, mshindi wa pili wa shindano la miss Tanzania mwaka huu ni kutoka hapa hapa jijini Dar es salaam…”
Oh, My God!
Candy alihisi akiishiwa nguvu za miguu na kichwa kikimuiwa chepesi.
“Naye ni TUNIS MWAKABAGAAA!”
Ukumbi uliruka kwa hoi hoi na nderemo, Candy ajashusha tena pumzi za ahueni, na kule kwa watazamaji Bishkuku alijikuta akiruka juu na kupiga yowe kubwa la shangwe, kisha akaketi na kumgeukia Sanura Kashogi, ambaye alikuwa amepigwa bumbuwazi la kutoamini.
“Hongera sana Sanura! Keep it up!” Bishkuku alishindwa kujizuia na kumpigia kelele hasimu wake kule kule alipokuwa huku akimuoneshea alama ya dole gumba lililoinamia chini, na Sanura akamtumbulia macho kwa hamaniko. Hakuamini kuwa Tunis hakuchukua ubingwa ule aliokuwa ameutarajia kwa kiwango kikubwa.
“Sasa we’ ndo nini tena?” Kokos alimuuliza dada yake.
“Ah potelea mbali bwana! Sijajua kama Candy atatoka mshindi au la, lakini madhali yule nyau naye kaukosa ubingwa poa tu!” Bishkuku alisema.
“Candy anachukua taji hili Bishi…!” Kokos alisema kwa msisitizo, na Bishkuku hakumjibu kwani hoi hoi zilikuwa zikirindima kila kona mle ndani, wakati Tunis akienda kwa mwendo sio wa pozi tena bali wa kukata tamaa na kusimama upande wa pili wa kile kiti cha mrembo wa taifa baada ya kuvikwa ule utepe wenye maadishi yaliyomnadi kuwa ni mshindi wa pili.
Hapo muziki ulikuwa ukitumbuiza kwa mbali wakati mrembo wa Miss Tanzania anayemaliza muda wake alipoenda na kuketi kwenye kile kiti cha enzi, lile taji ghali lenye mng’ao wa vito vya thamani likiwa kichwani kwake.
Huku jukwaani Candy alikuwa amesima pamoja na wale warembo wenzake wawili aliobakia nao. Wote wakijua kuwa yeyote kati yao angeibuka mshindi. Jinsi mioyo ilivyokuwa ikiwadunda ni wao tu na Mungu wao ndio waliojua.
“Na sasa….” Bwana Prakshantji alianza kuongea kwa hamasa kule mbele, na bila ya kujadiliana wale warembo watatu wakakumbatiana kwa hisia kali, wote wakibubujikwa namachozi ya mashaka juu ya kile kilichokuwa kinaelekea kuwatokea.
“Jamani…tutakiane heri ndugu zangu!” Mmoja wa wale mabinti, Miss Kanda ya Ziwa alibwabwaja, na Candy nayule mwenzao mwingine walijikuta wakitikisa vichwa tu kuafikiana na kauli ile. Hakuna aliyekuwa na nguvu ya kujibu lolote.
“…nikwa heshima ya kipekee kabisa napenda kuwatangazia mrembo aliyenyakuwa taji la Miss Tanzania mwaka huu, naye si mwingine bali ni CANDY GAMASALAAA!”
E bwana we!
Mlipuko wa shangwe uliosikika hapo haukuwa na mfano. Ni kama kwamba watazamaji wote walikuwa wakisubiri kusikia jina la Candy likitajwa.
Candy aliachia mgunowa kutoamini huku akiwaachia wale wenzake na kuinua mikono juu, na wale wenzake nao wakamkubatia tena kwa kumpongeza, wote watatu wakibubujikwa na machozi ya furaha.
Shangwe, mbinja, hoi hoi na nderemo za kila fani vilitawala ukumbini. Kule nyuma ya ukumbi ule, Nuru aliishuhudia hali ile na kumgeukia Morandi.
Kule mbele Bishkuku alijikuta anapiga mweleka kutoka kwenye kiti chake na kubaki akilia machozi kama mtoto pale chini. Kokos aliruka hewani na kutupa ngumi hewani, tusi zito la nguoni likimtoka bila ya kujali kuwa alikuwa miongoni mwa watu wenye heshima zao pale ukumbini.
“THAT’S MY CANDY, BLOODY HELL!” Alibwata kwa jazba, kabla ya kuinama na kumuinua dada yake kutoka pale chini.
“Ah! Mtoto kanitoa kimasomaso Kokos! Candy katwaa taji jamani, eeeeh!” Bishkukualikuwa akilia kama aliyefiwa kwa furaha, akiwa amekumbatiana na nduguye.
“Yeah!Nilijua tu kuwa mtoto atafanya kweli, shenzz Taipp!” Kokos alisema kwa hamasa iliyovuka mipaka.
“Nenda kule mbele sasa Candy! Huu ni wasaa wako bwana…make the most of it!” Miss Arusha aliyekuwa pamoja nae pale jukwaani alimwambia, na ndipo Candy alipojitenga na wale wenzake na kuisogelea hadhira.
Alitembea kilimbwende pale jukwaani huku akiwapungia watu mkono. Wale mabinti maalum walimfikia na kumvika utepe uliomnadi kuwa yeye ndiye Miss Tanzania. Kisha wakamkabidhi shada la maua, maalum kwa ajili ya mshindi wa taji lile la ulimbwende. Candy akasimama akiwapungia watu mkono huku akibubujikwa machozi pasi kizuizi. Sasa alisikia sauti ya pamoja kutoka kule kwa watazamaji ikilinadi jina lake naye hakuamini.
“Candy…caandy…caaaandy…!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akiwa amesima pale alimtafuta Bishkuku na kumuona akiwa amesimama na Kokos wakiwa wamejawa na furaha nyusoni mwao, michirizi ya machozi ikimtirika Bishkuku. Aliachia tabasamu la furaha na kumpeperushia busu kutokea pale jukwaani, na Bishkuku aliishiwa nguvu na kujikuta akiketi huku mlipuko mpya wa kicheko na kilio vikimzonga kwa wakati mmoja, na ukumbi ukiachia shangwe mpya kwa kitendo kile.
Miss Tanzania wa mwaka uliopita alimsogelea pale alipokuwa amesimama, na warembo wale wawili wakakumbatiana. Yule mrembo aliyemaliza muda wake alimbusu Candy mashavu yake yote mawili kisha akavua lile taji kutoka kichwani kwake na kuliweka kichwani kwa Candy.
Mlipuko mpya wa hoihoi ulitawala ukumbini pale waliposhuhudia tukio lile la makabidhiano ya madaraka kutoka kwa mtawala wa urembo aliyemaliza muda wake kwenda kwa mtawala mpya wa urembo nchini.
Candy alikuwa akicheka kwa furaha ilhali machozi yakimbubujika wakati akivikwa lile taji, waandishi wa habari wakikanyagana kila mmoja akitaka nafasi ya kuipata ile picha ya makabidhiano ya madaraka ya urembo wa taifa.
Kisha yule Miss Tanzania aliyemaliza muda wake akamuongoza Candy hadi pale kwenye kile kiti cha enzi na kumketisha.
Candy akaketi pale kitini huku Tunis akiwa upande wake mmoja na Miss Kigoma akiwa upande wake mwingine. Vimuli-muli vya kamera za waandishi wa habari viliwashambulia kutoka kila kona, ilhali mianga ya taa za kamera za televisheni na video zikiwamulika kurekodi kumbukumbu ile adhimu.
Kule hospitali ya Aga Khan, GTZ alipasua kioo cha luninga ya mle wodini mwake kwa kuitupia bilauri nzito kwa hasira, muungurumo wa ghadhabu ukimtoka.
***
Huku Mlimani City, ukumbi ulilipuka kwa hoi hoi kubwa sana, mbinja zikitawala huku na huko, Kokos Wandiba na Bishkuku walijikuta wakirukaruka ukumbini huku wakiwa wamekumbatiana kwa furaha. Kama ilivyokuwa kule Diamond Jubilee wakati Candy akikabidhiwa taji la umalkia wa urembo wa Dar City Center, ilikuwa wazi kabisa pale ukumbini kuwa taji la Miss Tanzania lilikuwa limekwenda mahala panapostahili.
Ndani ya shamrashamra zile, Kokos alimuona Sanura Kashogi akisukuma watu ili atoke nje ya ukumbi ule, midomo akiwa ameibetua kama anayehisi kichefuchefu.
“Jamaa yako anaingia mitini kule Bishi!” Alimnong’oneza Bishikuku, ambaye aligeuka na kumwona Sanura akiondoka. Bishkuku alijifuta machozi na kujipenyeza kwa watu kumfuata.
“Vipi tena shostiso…mbona unamuacha mrembo wako kule mbele? Msubiri umrudishe nyumbani bibie,au ndo ameshanuka ghafla?” Alimsemesha kwa kebehi huku akimsimamia mbele yake.
“Ah, Bishkuku sitaki ugomvi!”
“Na aliyekwambia anataka ugomvi nani? Nilikwambia mambo huyawezi haya bibie, oo! Ona sasa, Candy ndo yule pale na taji kichwani, hayo matapishi yangu ulong’ang’ania kuyaramba yanasubiri tu nyuma yake kule…” Bishkuku alimpasha kwa nyodo.
“Bishkuku!” Sanura alimtolea ukali huku akimnyooshea kidole.
“Habari nd’o hiyo bibi! Candy nambari wani, Tunis anasubiri uwani, hallllooo!” Bishkuku alimjibu na kumtolea cheko kali ya kimbea, kisha akageuka kurudi kule alipokuwa amekaa hapo awali.
Sanura alitoka nje ya ukumbi akiwa amefura.
Kule jukwaani Candy Gamasala alikuwa akitoa shukrani zake kwa Mwenyezi Mungu, majaji, waandaaji wa kinyang’anyiro kile pamoja na wananchi wote waliofika kushuhudia tukio lile.
“…lakini zaidi ya hayo napenda kurudia tena kuwashukuru sana, sana, tena sana mkufunzi na mlezi wangu Anti Bishi…na mdhamini wangu bwana Kokos Wandiba…” Alizungusha uso wake na kuwatazama wale watu wawili muhimu sana maishani mwake, kamera za televisheni zikawaelekea Kokos na Bishkuku waliokuwa wameketi kwa majivuno kwenye viti vyao, machozi yakimlengalenga upya Bishkuku.
“Ahsanteni sana walezi wangu…”
Kokos na Bishkuku walitikisa vichwa vyao kuafiki shukrani yake huku madonge yakiwa yamewakwama, na ukumbi uliibuka kwa shangwe mpya. Itifaki ya shindano la Miss Tanzania ilikuwa tofauti na ile ya Miss Dar City Center, hivyo wale walezi wake hawakuruhusiwa kupanda pale jukwaani kukumbatiana naye.
Walipata fusra hiyo baadaye.
Baada ya hapo lilifuata zoezi la warembo kukabidhiwa zawadi zao pale pale ukumbini, na nusu saa baadaye, Candy aliondoka pale ukumbini akiwa na Bishkuku na Kokos Wandiba, kuelekea hoteli kubwa ya kitalii ya The Kilimanjaro Hyatt Regency, ambako wote watatu walipatiwa vyumba vya kulala kwa muda wa siku tatu, vikilipiwa na kamati ya Miss Tanzania. Mkobani mwake kukiwa funguo mbili, moja ya jumba la kifahari ambalo ataandaliwa sherehe maalum ya kulifungua na kuingia, na nyingine ikiwa ya gari la kifahari aina ya Vogue, likiwa na nembo za Miss Tanzania kila upande.
“Sasa bado taji la Miss World…” Bishkuku alisema kwa sauti ya chini wakiwa ndani ya gari, na wote watatu waliangua vicheko vya furaha na ahueni.
Kwa wakati ule, si yeyote kati yao aliyejua ni kipi kilikuwa kikiwasubiri huko kwenye kinyang’anyiro cha Urembo wa Dunia.
Kama kawaida…usilolijua, siku zote huwa ni usiku wa kiza!
***
John Koccho aliingia kwenye chumba cha nyumba ya wagenialiyopaga na kujikomea kwa ndani. Alipiga teke tendegu la kitanda kwa hasira na kuachia msonyo mkali.
Wale askari wamenitambauje kirahisi namna ile?
Ina maana Candy amediriki kuwahusisha askari kwenye swala hili? Haogopi matokeo yake iwapo swala lake litafika mikononi mwa dola? Ni wazi kuwa hajui lolote lakini kitisho nilichompa kilitosha sana kumfanya asitamani hata kidogo polisi wajue juu ya swala nililomfikishia. Sasa tena…!
Aliguna.
Mawazo yalimzonga na hakuelewa afanye nini. Aliketi kitandani na akazidi kukosa amani pale alipoona kuwa mikono yake ilikuwa ikimtetemeka vibaya sana.
Pumbavu! Hii sasa ni mbaya. Mbaya sana!
Alikaa kwa muda mle chumbani akijiwazia.
Wale jamaa wangenitia mbaroni leo pumbavu zao…sasa hapa sina namna John Koccho miye. Nimejaribu karata yangu ya mwisho kwenye kujipatia mfereji wa pesa na nimeramba garasa…
Alikaa kimya kwa muda mrefu akitafuta wazo jipya, na hakuna lililomjia. Hatimaye alisonya na kuinuka. Alienda nyuma ya ule mlango wa chumba kile na kuchomoa nguo zake mbili zilizokuwa zikining’inia nyuma yake, kasha akazishindilia kwenye begi lake dogo.
Hapa ni kutoweka tu, biashara hii imeshakuwa siyo! Nimepoteza tu vijihela vyangu vichache stupid me!
Aliamua, na kutoka nje ya chumba kile.
***
Asubuhi ya siku ya pili Miss Tanzania mpya alipata mwaliko wa kiamsha kinywa pale hotelini alipolala usiku uliopita kutoka kwa mratibu wa shindano la miss Tanzania nchini, mualiko ambao uliwahusu Kokos na Bishkuku pia, kama walezi wa mrembo yule wa taifa.
Katika kiamsha kinywa kile cha bei ghali ndani ya moja ya hoteli ghali sana nchini, pia alikuweko miss Tanzania aliyemaliza muda wake.
Ilikuwa ni fursa adhimu sana kwa Candy na Bishkuku ambao siku zote wamekuwa wakiiombea nafasi ya kuliwakilisha taifa katika shindano la urembo la dunia. Kwa Candy, binti aliyetokea kwenye mazingira magumu na aliyenusurika kuingizwa kwenye biashara ya kuuza mwili wake ili apate riziki, hii ilikuwa ni pepo asiyoitarajia asilani.
Baada ya kiamsha kinywa kile maridhawa, mratibu wa Miss Tanznaia nchini alikohoa na kuaza kuwaeleza.
“Eh, jamani sina haja ya kuelezea ni furaha kiasi gani tuliyo nayo sote kwa kumpata mrembo mpya wa taifa letu. Ila kama mjuavyo, haliya rais wa Venezuela kule sio nzuri na hivyo ratiba yetu imebidi isogezwe mbele…hivyo kuanzia sasa tuna muda mfupi sana wa kumuandaa Candy kwa mpambano wa miss world, na lazima niwaambie kuwa kule ni mchezo tofauti kabisa. Hakuna lele mama kule!”
“Ah hilo liko wazi, na sisi pia tuko imara. Tutajipanga kwa kadiri ya uwezo ili kuhakikisha kuwa tunafanya maajabu huko Venezuela!” Bishkuku alidakia.
“Na hilo ndilo nililotaka kuliweka wazi kwenu, Bishkuku. Najua kuwa we’ ni mzoefu sana katika mambo haya,ila kamati imeamua kuwa kuanzia sasa Candy atakuwa chini yetu sisi na si vinginevyo!”
“What? Yaani mi nawekwa pembeni tena?” Bishkuku alikuja juu.
“Sio hivyo. Wewe utaendelea kuwa na Candy pale tu itakapobidi. Sisi ndio tutasimamia maandalizi yake yote. Na atapata twisheni kutoka kwa mrembo mwenzake aliyemaliza muda wake. Msaada wako utakapohitajika tutakutaarifu tu.” Jamaa alimjibu, na Bishkuku na Candy wakatazamana.
“Hiyo inamaanisha nini?” Candy aliuliza.
“Hiyo inamaanisha kuwa kuanzia leo hutaishi tena nyumbani kwenu. Utaishi hapa hotelini, na utakuwa chini ya usimamizi wa watendaji wa kamati ya Miss Ti-Zedi mwanzo mwisho!” Mratibu alimjibu, na wote pale walitazamana.
“Ah sasa vipi aendelee kuishi hotelini wakati keshakabidhiwa jumba la thamani kule?” Bishkuku aliuliza, na mratibu na Miss Tanzania aliyemaliza muda wake wakacheka.
“Usiwe na shaka Bishkuku…jumba ni lake lile, ila hatahamia humo sasa hivi mpaka afanyiwe sherehe maalum ya kuingia kwenye jumba…hilo zoezi linasimamiwa kwa pamoja kati yetu na benki iliyofadhili jumba lile…wenyewe tumekubaliana kuliita “The Beauty Palace One…!” Mratibu alifafanua.
“Heh, Beauty Palace One…?” Bishkuku aliuliza huku akimtupia Candy jicho la pembeni.
“Yeah…ni kwa kuwa ile benki imekubali kutoa majumba kwa kila mrembo atakayetwaa taji hili kila mwaka baada ya hapa, na hivyo jumba litakalofuata litakuwa beauty palace two, beauty palace three…na kuendelea…yaani haijawahi kutokea!” Miss TZ aliyemaliza muda wake alifafanua, kisha akaendelea, “…laiti wangeanzisha mpango huu mwaka jana!”
Vicheko vilitawala mezani.
“Ah, malikia wa jumba la urembo namba wani huyo! Chezea Candy weye?” Bishkuku alimwambia Candy kwa sifa huku akimpigapiga mgongoni, na wote walicheka zaidi.
Candy alitabasamu huku akisikiliza mambo yale bila kuamini. Alijiona kama yuko ndotoni.
Yaani kutoka uyatima usio na mbele wala nyuma, kunusurika kuwa changudoa, hadi kuwa malkia mwenye kumiliki beauty palace one! Ama hakika Mungu mkubwa!
“Aha…okay….sasa tukimhitaji Candy tunafanyaje?” Kokos aliuliza, akilini akiifikiria ahadi aliyompa Morandi ya kumfikisha Candy mbele yake kwa mahojiano juu ya kadhia ya wale watu wanaomuwinda.
“Ah, hilo litawezekana iwapo kuna dharura ya msingi…kifo katika familia,kwa mfano. Otherwise, tunaomba Candy asibughudhiwe na jambo lolote zaidi ya maandalizi yake ya safari ya Venezuela…kuna mengi hayajafanyika kabla ya safari hiyo na muda umeshakuwa hautoshi. Nataraji mtanielewa.” Mratibu alimjibu.
Ilibidi wamuelewe.
Mchana ule Candy aliongozana na watendaji wa Miss Tanzania kwenda kuonana na waandishi wa habari ambapo alithibitisha lengo lake la kuchagiza kampeni za kukomesha mapigano baina ya wafugaji na wakulima.
***
Jioni ile ghadhabu za Morandi Gwaza zilimshukia Kokos Wandiba.
“Sasa haya ndiyo mambo nisiyoyapenda wakili wangu! Unadhani mi’ n’tafanyaje kazi yangu ikiwa sipewi ushirikiano namna hii? Kwanza ilikuwa Bishkuku kazuia mrembo asihojiwe eti anajiandaa na shindano la Miss Ti-Zedi…”
“Ni kweli Morandi, lakini safari hii…” Kokos alianza kumuelewesha, lakini Morandi hakuwa na muda wa kumsikiliza.
“…na sasa imekuwa mrembo haguswi wala haulizwi kitu kwa kuwa mratibu wa miss Ti-Zedi hataki abughudhiwe kwa kuwa anajiandaa na shindano la miss world! Acheni mizengwe bwana! Kama vipi tukubaliane hapa hapa kuwa deni langu kwako liwe limeisha, mi’ nirudi kwenye hamsini zangu!”
Kokos alimtazama na kutaka kumjibu, lakini bado Morandi alikuwa hajamaliza kumkoromea.
“Na ndilo Nuru alilolisema hili…ikiwa Miss Ti-Zedi tu tumenyimwa nafasi ya kuonana naye, hiyo Miss World itakuwaje? Haya nd’o ishakuwa hivi sasa! Kokos tumalizane tu kaka…siwezi kuendelea na hili zoezi kwa mtindo huu. Nahisi nimeshalipa deni langu kwako, kwa hiyo naomba tukubaliane kuwa niko huru sasa na hatudaiani!”
Kokos alitazama na kumgeukia Nuru aliyekuwa kimya pamoja nao pale sebuleni kwa Bishkuku, ambaye muda ule alikuwa kule nyumbani kwa Kokos Mbezi Beach ambako Kokos alisisitiza aendelee kuwa huko mpaka baada ya shindano la miss world.
Kisha akamgeukia tena Morandi aliyefura kwa hasira. Alishusha pumzi ndefu na kujiegemeza vizuri kwenye kochi na kukunja nne.
“Ni sawa Morandi.” Hatimaye alimjibu, na Nuru akaguna.
“Ni sawa? Yaani tuondoke zetu na tumuache Candy akiendelea kusakwa na wale watu…are you guys crazy?” Aliwawakia huku akiwatazama kwa zamu wale wanaume wawili.
Morandi alifinya macho na kumtazama Kokos kwa hasira.
Alishamsimulia kila kilichotokea kule Mlimani City ule usiku wa shindano la Miss Tanzania, na aliona jinsi Kokos alivyohamanishwa na taarifa ile. Sasa tena anakubali kirahisi tu kuwa tayari Morandi ameshalipa deni lake na aondoke?
“Ndio Nuru. Nashukuru sana kwa msaada wako kwa Morandi katika hili, ila Morandi alikuwa anafanya haya kwa makubaliano maalum, ambayo nawe najua uniayafahamu. Nami nimekubaliana naye kuwa kufikia hapa tayari ameshalipa deni lake kwangu…” Kokos alisema, na kwa mara nyingine Nuru akaachia mguno wa mshangao huku akihamishia macho yake kwa Morandi aliyevimba kwa hasira.
“…ila bado hajalipa riba ya deni lile!” Kokos alimalizia kauli yake huku akimgeukia Morandi na kumtazama moja kwa moja usoni.
“Whaat?” Morandi alimaka.
“Ndiyo, mtuhumiwa wangu…tulikubaliana kuwa ukinisaidia kumuweka Candy salama kwa kuwasambaratisha hawa wanaomfuatilia utakuwa umenilipa deni langu pamoja na riba yake…sasa bado riba kaka, na kwa hiyo bado unahitajika kulifanyia kazi hili swala mpaka mbivu na mbichi zijulikane!” Kokos alimjibu.
Uso uliofura wa Morandi ulibakia katika hali ile ile kwa muda huku akimtazama kwa hasira, kisha ukabadilika na kufanya tabasamu pana.
“Halafu usin’letee utundu wako wa mahakamani hapa wewe, umes’kia hiyo? Natakupa mashuti hapa hapa, fala we! Yaani mi’ niko serious we’ unaleta michezo? Hili sio swala la masikhara wewe, ala!” Alimwambia kwa jazba ya kicheshi huku akimnyooshea kidole.
Kokos akamcheka.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Haya, sasa kwa kuwa tumeshapoza lile fukuto la jazba lililopanda, nadhani tunaweza kuongea vizuri ni jinsi gani tunalifanikisha zoezi letu katika mazingira tuliyonayo, ambayo kwa kweli hayaepukiki!’ Kokos alisema huku akitabasamu, na Nuru akashusha pumzi za ahueni.
“Dah! Halafu we’ una masihara mabaya ujue! Yaani nilitaka kushangaa. Candy yuko kwenye matatizo mazito hivi halafu tumuache hivi hivi tu?” Alisema, na Kokos alimtazama na kucheka.
“Jamaa yako huwa ana jazba sana sometimes…na ashukuru kuwa mimi nilikuwa wakili wake wakati ule, vinginevyo jazba zake zingemharakishia hukumu ya kifo mapema sana huyu!” Alimjibu huku akimtupia Morandi jicho la pembeni.
“Basi yameisha hayo…turudi kwenye mada!” Morandi alikatisha.
“Okay tunafanyaje sasa katika mazingira haya Morandi? Candy ndio hayuko tena kwenye himaya yetu kwa sasa. Nimesikia atakuwa na safari kadhaa za muhimu nje ya jiji akiwa na hao watendaji wa Miss Ti-Zedi…” Kokos alimgeukia na kumuuliza.
“Hiyo ni mbaya…hao jamaa wanaweza kumuibukia huko huko na kufanya wafanyalo!” Nuru alidakia.
“Hapana. Huko hawataweza…Candy atakuwa amezongwa na watu muda wote. Cha msingi afikishiwe ujumbe kuwa asikubali kubaki popote peke yake…” Morandi aliyerudisha umakini wake wa kikazi alisema.
“Ujumbe atafikishiwa.” Kokos alisema.
“Haya, na vipi kuhusu kumuonesha ile picha ya GTZ ili tujue iwapo anamfahamu au la?” Nuru alisaili.
“Mh! Sasa hilo sijui itakuwaje…si ndio itakuwa inambughudhi katika maandalizi yake kwa miss world jamani, kama alivyoonya Mratibu?” Kokos aliingilia kati.
“Kwa hiyo tusilifuatilie hilo kabisa? Mpaka amalize shindano la Miss world?” Morandi alimuuliza huku macho yake yakionesha kuwa hakupenda iwe hivyo.
Kokos aliguna na kutikisa kichwa.
“Jamani hebu tufikirieni…hili ni shindano la urembo wa dunia. Binti anaenda kuliwakilisha taifa. So far mamiss wetu wote waliofanikiwa kufikia hatua hiyo wameshia kwenda kutalii tu huko…”
“Na huyu unadhani atakuwa tofauti na hao waliopita?” Morandi alimuuliza, macho na sauti yake vikiashiria kuwa alikuwa haamini hilo asilani.
“Candy yuko tofauti mjue! Huyu mtoto anaweza kwenda kufanya maajabu kule watanzania tukapigwa butwaa…! Nadhani tumpe hii nafasi. Tufanye kila linalowezekana kuendelea kuwadhibiti hawa jamaa wawili wanaomfuatilia mpaka atakapopanda ndege kwenda Venezuela. Baada ya hapo hatutakuwa na sababu yoyote tena ya kushindwa kumkabili na maswali yetu…au huenda tukawa tumeshapata baadhi ya majibu kutoka kwa hawa hawa jamaa wanaomuwinda!” Kokos alijieleza kwa kirefu, na Morandi akamshangaza.
“The guy is in love!” Alisema huku akimgeukia Nuru na akimuoneshea Kokos kwa kidole chake cha gumba.
“KHAAAH!” Kokos alimaka huku akimtumbulia macho.
“Tumbua macho utakavyo Kokos, lakini ukweli uko hivyo! We’ umemzimikia yule mtoto na unamtaka kama nini! Mi’ nimeshaliona hilo kitambo…ndio maana inabidi umjue huyu binti nje ndani kabla hujamuingiza kimwili na kiroho maishani mwako!” Morandi alimwambia.
“Ama?” Kokos aliishia kuguna huku akimgeukia Nuru kwa macho ya kuuliza.
“Hilo linaoekana wazi kaka Kokos…hata mi’ nimeliona hilo. Jinsi unavyobadilika wakati ukimuongelea Candy, ajuaye atajua tu kuwa umemzimikia yule anti!”
Heh!
“Ambalo ni jambo baya kwetu. Sisi tunafanya kazi bila kuhusisha hisia zetu za mioyo…wewe unahusisha hisia hizo na unatupa taabu!” Morandi alimpasha zaidi.
“Jamani…sio hivyo…sina hisia…”
“Wee!” Morandi alimkanya huku akimnyoshea kidole.
“Okay…hisia zangu haziwezi kuingilia lolote…”
“Wacha hizo wakili wangu! Kubali tu kuwa huo ndio ukweli na acha sisi tukusaidie katika hili. Ila nilishakwambia…jiandae kusikia lolote kutoka kwa huyu mrembo wa moyo wako kaka…huenda akawa hana makosa, lakini pia huenda pia akawa ana makosa…ukijiingiza kwake, na akawa ana makosa, jua utaangamia pamoja naye. Si unajua kuwa mimi na wewe sote tumewekewa vinyongo na vyombo vya dola hususan jeshi letu adhimu la polisi? Sasa we’ endekeza tu mapenzi hapa halafu uone. Mi’ nakupa ukweli huo! Utakavyoupokea ni juu yako!” Morandi alimtolea uvivu.
Kokos Wandiba alikosa la kusema, na kimya kilitanda mle ndani.
“Okay…sasa nini kinafuata?” Hatimaye aliuliza baada ya kujikohoza kusafisha koo. Hata hivyo, sauti yake bado ilikwaruza.
“Sisi tutaendelea na kazi yetu kwa namna tujuavyo…tukihitaji lolote kutoka kwako tutakwambia.” Morandi alimjibu bila kumuangalia, uso akiwa ameukunja.
Nuru alimtupia jicho la pembeni mpenziwe, na kutazama chini.
Kokos alijikohoza tena kusafisha koo kabla ya kuongea.
“Okay…kwa hiyo mtaendelea kuwafuatilia wale jamaa?” Aliuliza, bado sauti ilimtoka kwa kukwaruza.
“Kama kawa!” Morandi alijibu tena kimkato bila kumtazama.
Kimya kilitanda tena, kisha Kokos akaingiza mkono kwenye mfuko wa koti alilokuwa amevaa na kutoa kitita cha pesa na kukiweka mezani.
“Najua mtahitaji pesa katika kufanya kazi yenu. Milioni moja hii itasaidia kupunguza makali ya gharama za kiutendaji…ikihitajika zaidi mtaniambia…” Alisema.
“Shukrani za dhati kwako!” Morandi alimjibu kwa mkato bila kumtazama.
Kokos alimtazama kwa muda, kisha akamgeukia Nuru, ambaye alimtolea tabasamu la pole.
Aligeuka na kutoka nje ya chumba kile bila kuongea neno zaidi.
“Umekuwa mkatili sana kwake, Mo!” Nuru alimwambia mpenziwe kwa kushutumu baada ya Kokos kuondoka.Morandi Gwaza alibaki kimya akiwa amekunja uso.
Asubuhi ya siku iliyofuata vyombo vya habari vilitangaza na kumuonesha mrembo mpya wa taifa Candy Gamasala akipanda ndege kuelekea Tarime kuzitembelea jamii za wafugaji na wakulima kama sehemu ya kampeni yake aliyoinadi kwa waandishi wa habari na watanzania wote. Safari yake ilikuwa imedhaminiwa na kampuni kubwa ya utalii nchini.
Pamoja naye safarini, lilikuwepo kundi la waandishi wa habari na watendaji wengine wa kamati ya Miss Tanzania.
Kokos na Bishkuku walibaki Dar.
***
Wakati asubuhi ya siku ile ile inaishia-ishia, Ngamao Kijambia aliingia jijini. Alipitiliza moja kwa moja hadi Aga Khan hospital na kwenda mapokezi kumuuliza mhudumu wa pale mahala ilipo wodi ya VIP alimolazwa GTZ. Alielekezwa naye akaenda na kujitoma ndani ya wodi ile akiwa mwingi wa wahka.
Alimtazama GTZ akiwa amelala pale kitandani huku mguu wake ukiwa umefungwa mabandeji maalum sehemu ya goti na uso wake ukiwa una michubuko iliyoashiria kuwa alipokea kipigo cha haja kabla ya kufikishwa pale hospitali, na uso wake ukaingia ugumu, akimakinika na hali aliyomkuta nayo yule jamaa ambaye alimjua kuwa alikuwa mahiri sana katika makabiliano ya kimapigano.
Sasa ni nani huyu aliyemfanya hivi?
GTZ alimtazama yule Inspekta mzoefu akiwa amesimama kando ya kitanda chake, na kubana midomo kwa uchungu. Hakupenda kabisa mtu yeyote amuone akiwa katika hali ile.Lakini alijua kuwa hakuwa na namna…ilibidi tu amwite pale hospitali.
“Niambie kilichojiri GTZ, na niambie yote bila kunificha…nini kimekukuta?” Ngamao alimuuliza huku akivuta kiti kilichokuwamle wodini na kukisogeza pale kando ya kitanda na kuketi.
GTZ alimtazama kwa muda.
“Ndio umeingia mida hii?” Alimuuliza.
“Nimekuja moja kwa moja mpaka hapa, hata sijatafuta hoteli ya kufikia…niambie kilichokukuta wewe…nani kakufanya hivi?”
GTZ alishusha pumzi ndefu na kuguna.
“Nilimuona Candy hapa jijini Ngamao…na nikaanza kumfuatilia…”
“Ndio akakufanya hivi?” Ngamao alihoji kwa kutoamini, akimtumbulia macho.
“Tuheshimiane Ngamao…yule kisonoko ataweza kunifanya hivi mimi yule?” GTZ alimjia juu.
“Niambie basi kila kilichojiri GTZ! Tunapoteza muda!” Ngamao naye alimjia juu.
Kwa taabu GTZ alimueleza kila kitu. Alipata taabu kumueleza kwa kuwa kila alilokuwa akilifanya wakati akimfuatilia Candy lilikuwa ni kinyume kabisa na jinsi ambavyo Inspekta Kijambiaalitaka iwe. Alipomaliza Ngamao alibaki akimtazama kwa macho makali yaliyojaa ghadhabu.
“Ni bora ambavyo hukufanikiwa mshenzi wewe!” Alimwambia kwa hasira, na GTZ alivimbisha midomo kwa hasira, macho yakimchonyota kwa machozi machanga.
“Ulitaka kumuua yule mtoto wewe! Naunajua kama ungefanikiwa nini kingetokea? Ningekutia pingu mimi mwenyewe na kukusweka ndani mpuuzi wewe! Na baada ya hapo ungepigwa kifungo cha maisha au hata kulambwa hukumu ya kifo bwege wewe!” Alimfokea zaidi.
“Mi nikimuua yule malaya yote hayo ni burudani tosha tu kwangu!” GTZ alimkoromea, na Ngamao alimtazama kwa hasira.
“U-mgonjwa wewe! Uko mgonjwa kichwani GTZ…nilikuasa sana dhidi ya hilo…na nilikwambia na tulikubaliana kuwa iwapo ukimtia machoni tu, unifahamishe…lakini wapi! Umemuona muda mrefu na badala ya kunifahamisha mapema, ukaamua kujitia Vin Diesel…ona sasa!” Ngamao alimtemea cheche kali.
“Anachostahili ni kifo tu na si kingine yule!”
“Ndio…na atakipata kwa taratibu za kisheria fala wewe, sio kwa kupitia mikono yako!” Ngamao alimfokea kwa sauti ya kunong’ona. Muda huo nesi mmoja aliingia mle wodini nao wakapiga kimya kwa muda.
“Okay sasa…huyu jamaa aliyekufanya hivi…ulipata kujua ni nani?” Hatimaye Ngamao alimuuliza baada ya yule nesi kuondoka.
“Hapana! Ila jamaa alikuwa ananuka uaskari mwanzo mwisho! Atakuwa ni askari tu yule, maana hata aliweza kushirikiana na askari wa usalama barabarani kunidhibiti!”
Ngamao alikunja uso.
“Sasa najiuliza, ni askari gani atakayeshirikiana na yule kisonoko kunidhibiti?” GTZ alisema.
Ngamao hakumjiu, bali alizidi kuonekana mwenye kulifakari lile jambo.
“Okay…hilo tutalipatia jibu mara tukimtia Candy mikononi…sasa unaweza kuniambia ni wapi naweza kumpata?” Hatimaye Ngamao alisaili, na GTZ akamtolea macho.
“Ina maana hujui?”
“Sasa ningejua unadhani ningeanza kuja kupoteza muda wangu hapa kwako? Si ningeazia huko aliko? Na kwa nini unasema hivyo…natakiwa nijue? Na nijue kivipi?” Ngamao alimvurumishia maswali.
“We bwana uko ulimwengu gani? Hata magazeti husomi? Redio husikilizi? TV hutazami?” GTZ alimhoji huku akimtupia gazeti lililokuwa ubavuni kwake pale kitandani.
Ndipo Ngamao alipojikuta akiitazama sura ya mtu aliyekuwa akimsaka kwa muda mrefu ikiwa imejaa tabasamu pana hali ikibubujikwa machozi…ikiwa na taji la urembo wa taifa kichwani.
“HOLY SHIIT!” Aliropoka huku akilisogeza karibu zaidi ya uso wake lile gazeti, na wakati huo huo naye akiusogeza uso wake kuliendea lile gazeti lililokuwa mikononi mwake.
Aliinua uso wake na kumtazama GTZ kwa mshangao mkubwa.
“Yaani huyu laana ndio kawa miss Tanzania?”
“Ndio hivyo bwana…ina maana we ulikuwa husomi magazeti?” GTZ alimuuliza.
Ngamao alimtazama.
“Mama yangu alikuwa anaumwa GTZ…ilinibidi niende kijiini kumuuguza, na kule hakuna mawasiliano kabisa. Nilikuja naye Mwanza mjini kwa matibabu, na kwa hakika wakati namuuguza mama nilikuwa mbali sana na habari za kilichokuwa kikiendelea duniani…”
“Ah, pole sana…”
“Yah, na alipofariki ilinibidi nikamzikie kijijini kama mwenyewe alivyotaka…”
“Mamaako amefariki?”
“Yah…ametangulia mbele ya haki bwana…niliporudi ndio nikapata ujumbe wako, na ndio unaniona hapa!”
“Ah, sasa…mbona hukuniambia wakati wote huo tangu anaumwa mpaka anafariki?”
“Ili isaidie nini? Achana na hilo…turudi kwa huyu Candy…yaani baada ya yote yaliyotokea bado amediriki kujiinguza kwenye mashidano kama haya ambayo ni wazi yangemuweka wazi mbele ya jamii yote?”
“Hana akili yule…” GTZ alisema kwa hasira.
Kimya kilitanda, kisha Ngamao akataka kujua Candy alipo muda ule.
“Nimesikia redio ikitangaza kuwa leo hii ameelekea Tarime huko, tena kwa ndege maalum pumbavu zake! Eti ameenda kutembelea jamii za wakulima na wafugaji zinazouana huko!” GTZ alisema kwa hasira.
Ngamao alikunja uso kwa muda. Kisha aliinuka.
“Okay, wapigie simu watu wako wanitafutie ndege ya haraka…naenda huko!” Alisema.
GTZ alimkodolea macho.
“Unaenda Tarime?”
“Sasa wapi kwingine? Lazima nimtie mbaroni huko huko nyang’au wa kike yule!”
GTZ alibabaika kidogo.
“Sasa…kwa nini usiwapigie simu tu wenzio kule ili wamkamate? Unajua mi niko mwenyewe hapa na sina namna ya kujitetea yule jamaa akiniibukia hapa? Si nimekwambia kuhusu ule ujumbe alionitumia?”
“So unataka niwe yaya wako hapa? Mi nimekuja kwa ajili ya Candy…na kwa kuwa kaenda kule basi nami natangulila kule ambako najua hataacha kwenda, baada ya kuwa sasa amekuwa miss Ti-Zedi…”
“Tarime?”
“Kule kwenye nyumba ya watoto yatima alipolelewa…si ni huko huko? Lazima atataka kwenda tu huko ili akawaoneshe yatima wenzake kuwa sasa amekuwa mrembo wa taifa, na ajitie kuwaachia misaada pale na apigwe picha na waandishi wa habari…na katikati ya furaha yake hiyo, mi’ namuibukia na namuweka chini ya ulinzi…mbele ya waandishi wa habari (akamtukania mama yake)!” Ngamao alisema kwa hasira.
GTZ aliachia tabasamu pana.
“I like that!”
“Basi piga simu hiyo nipate ndege haraka!”
“Hilo limepita.”
“Okay, kwa sasa nahitaji kuoga na kubadili nguo…”
“Nenda nyumbani kwangu kule masaki Ngamao…nitampigia simu mfanyakazi wangu Bi. Mwana akuandalie kila kitu kule…” GTZ alisema.
Bila ya kuongea neno zaidi, Ngamao alitoka nje ya ile wodi kuelekea Masaki.
Nje ya wodi kulikuwakuna watu kadhaa waliokuwakuwa wamekwenda pale hospitalikutembelea wagonjwa wao, ambao walikuwa wameketi kwenye viti maalum vya kusubiria.
Hakuwatilia maanani.
Hivyo hakuweza kumtilia maananni Nuru aliyekuwa ameketi miongoni kwa wale watu walioonekana kusubiri muda wa kuingia kuwaona wagonjwa wao pale hospitali, na hakuweza kabisa kujua kuwa wakati akionekana akiandika ujumbe kwa kutumia simu yake miongoni mwa wale watu pale nje ya wodi ile, kamera ya simu ile ilimfyatua picha tatu za haraka haraka wakati akitona nje ya wodi ya GTZ, ambayo kwa hadhi yake ya VIP, watu waliweza kuingia na kumtembelea wakati wowote, madhali afya yake iliruhusu kuonana na wageni.
Nuru alimtazama yule jamaa akitoka nje ya hospitali ile, kisha akamfuata kwa mwendo wa haraka huku akijitia hana haraka. Aliwahi kumuona akiingia kwenye ile Land Cruiser yake iliyojaa mavumbi na tope, jambo lililomjulisha kuwa lile gari lilikuwa limesafiri umbali mrefu kutokea nje ya jiji. Aliikariri namba ya lile gari na kugeuka, akichukua uelekeo tofauti kwenda mahala ambako alikuwa ameegesha pikipiki yake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akiwa anaelekea kwenye pikipiki yake alitoa simu na kumpigia Morandi.
“Mo! Narudia tena we kichwa, wa ubani!” Alisema kwa wahka simuni, na kule kwake Morandi akamakinika.
“Huwa unaniambia hivyo kila mara kisura…nini kimetokea safari hii?” Alimuuliza huku tabasamu laini likijijenga usoni kwake.
“Kama ulivyotabiri…hatimaye leo jamaa yetu amepata mgeni pale hospitali bwana!”
“Ala! Kwa hiyo sikuwa nikikupotezea muda wako nilipokuwa nakulazimisha kwenda kupiga kambi pale hospitali mara moja moja eenh? Vipi, umeweza kumtambua huyo aliyemtembelea?”
“Yah, leo hilo limezaa matunda! Jamaa sijamtambua, ila ni wazi kuwa yule ni njagu Mo! Ni askari yule…” Nuru alimjibu na kule kwake Morandi akafinya macho kwa umakini, na Nuru akaendelea haraka, “…ila nimepata picha zake kama tatu hivi…nakutumia sasa hivi kwa whatsapp…pia nimepata namba za za gari lake!” Alimwambia, akimaanisha kuwa atamtumia zile picha kwa kutumia mfumo wa kutuma ujumbe wa simu uitwao whatsapp unaotumika sana kwenye simu za mfumo wa Android.
“Okay, nitumie, lakini usimfuate…madhali umepata namba za gari lake yatosha kwa sasa…hatujui huyo mtu atakuwa makini kiasi gani.Pia nahisi atarudi tena kumtembelea hapo hospitali…na muda huo bila shaka tutakuwa pamoja. Tuma hizo picha bibie…kazi nzuri sana!”
Nuru alimtajia zile namba za gari la Ngamao, na dakika tatu baadaye akamtumia zile picha za Ngamao Kijambia kwa simu.
Kule kwake, Morandi ulifungua ujumbe wenye picha za Ngamao, na alipoziona tu aliachia mguno mkubwa.
“Ngamao????” Alijibwatia mwenyewe baada ya kumaliza mguno wake.
***
Jambo la kwanza alilofanya Candy baada ya kufika tarime ni kwenda kuzuru kaburi la mtu ambaye amekuwa akimuona ni muhimu sana maishani mwake. Msafara wake kuelekea kwenye kijiji cha jamii ya wakulima wa eneo lile ulimpitisha makaburini naye bila ya kusita wala kubabaika alienda moja kwa moja hadi kwenye kaburi alilolikusudia.
Alisimama mbele ya lile kaburi kwa muda mrefu akilitazama jina lililoandikwa kwenye msalaba uliosimikwa upande wa pili wa lile kaburi kutokea pale aliposimama.
Marietta Nicodemus.
Mtawa
Chini ya jina lile kulikuwa kuna tarehe za siku aliyozaliwa na siku aliyoaga dunia,jumla ya miaka sabini na miwili ya uhai wa hapa duniani.
Chozi lilimtoka Candy alipomkumbuka yule mtawa ambaye kwake alikuwa ni kama mama ambaye hakuwahi kumtambua.Alikumbuka jinsi yule mtawa ambaye pamoja na mwenyekiti wa kijiji, walimfikisha kwenye kituo cha kulelea watoto yatima ambako ndiko pamekuwa nyumbani kwake tangu siku hiyo, miaka kumi na tisa iliyopita.
Alikumbuka jinsi mtawa yule mwenye upendo uliotukuka alivyokuwa akienda kumtembelea kule kwenye nyumba ya watoto yatima kila Jumapili…na jinsi yeye alivyokuwa akipewa ruhusa kwenda kumtembelea mtawa Marietta nyumbani kwake kila jumapili wakati mtawa yule aliyelala ndani ya kaburi lile muda ule,alipoelemewa na uzee na hivyo kumfanya ashindwe kuendelea kwenda kumtembelea kule kwenye nyumba ya watoto yatima.
Ni katika nyakati zile alizokuwa akitembeleana na yule mtawa ndipo alipokuja kujua historia iliyomfikisha pale kwenye ile nyumba ya watoto yatima. Na kwa hakika alimshukuru sana mwenyezi Mungu kwa kumpa ujasiri na upeo wa kuongelea swala la kupigania kukomeshwa kwa mapigano kati ya jamii za wakulima na wafugaji nchini wakati wa shindano la Miss Tanzania, kwani ndani kabisa ya moyo wake, hilo ni jambo lililokuwa likimkereketa sana.Kwa mujibu wa maelezo aliyopewa na mtawa Marietta, mapigani yale ndiyo yaliyochangia kumharibia maisha yake kwa kumpotezea wazazi wake.
Roho ilimuuma.
Alipiga magoti na kumuombea malazi memamtawa Marietta huko alipotangulia.
Baada ya muda aliinuka na kwenda kwenye kaburi jingine lililokuwa kwenye kona kabisa ya eneo lile la makaburi. Alisimama mbele ya kaburi lile na kulitazama kwa mchanganyiko wa hisia, maneno yaliyoandikwa kwenye msalaba uliosimikwa kwenye kaburi lile yakimsisimua mwili kama yalivyokuwa yakimsisimua kila mara alipokuwa akilizuru kaburi lile kabla na hata baada ya kifo cha mtawa Marietta.
Mama kutoka kijiji cha Gamasala
Mzazi wa yatima wa kike aliyeachwa mlangoni kwa Mtawa Marietta
Chini ya maneno yale kulikuwa kuna tarehe ambayo yule mama alifariki.
Mama yake mzazi…
Ambaye hakuwahi kumtambua…na ambaye hakuwa na kumbukumbu yoyote juu yake…
Mtawa Marietta alimwambia kuwa ni kutokana na kutambua kuwa yule mama alitokea kijiji cha Gamasala ambako ndiko mauaji yalitokea usiku wa tukio miaka kumi na tisa iliyopita, ndipo yeye na mwenyekiti wa kijiji walipoamua kumpa Candy ubinti ule wa “Gamasala”, kwani hawakufanikiwa kabisa kulijua jina la baba yake.
Na Mtawa Marietta ndiye aliyempa jina la Candinista…ambalo baadaye likaja kuzoeleka kama Candy.
Alipiga magoti na kulia kwa huzuni, akimlilia mama ambaye hakuwahi kumuona wala hakuwa na kumbukumbu yoyote naye.
“Pumzika kwa amani mzazi wangu….huenda leo mwanao nikafanikiwa kuweka msingi wa kumaliza chuki na dhambi iliyotutenganisha!” Alisema kwa uchungu na kuinuka.
Alirudi kwenye gari na safari kuelekea kwenye kijiji cha jamii ya wakulima, ambako ndiko uzawa wake ulipotokea, ikaendelea.
***
Nuru alimtumbulia macho Morandi.
“Yaani huyo jamaa unamtambua?”
“Yap! Anaitwa Ngamao Kijambia…ni mpelelezi wa muda mrefu. Nilitaraji awe amestaafu, kumbe bado! Jamaa mbaya sana huyu kwenye fani!” Morandi alisema.
“Mbaya?”
“Namaanisha ni mpelelezi makini! Ila…alihamishwa jijini na kupelekwa mikoani huko…sijui ni mkoa gani.” Morandi alimwambia huku uso wake ukionesha mashaka makubwa.
“Sasa…mbona unaonekana una mashaka. Unamwogopa?” Nuru alihoji, na Morandi akamkata jicho.
“Nimwogopee kitu gani? Mimi najiuliza ni kipi kinachomuunganisha Ngamao na yule jamaa…GTZ. Kuna nini kati yao?”
“Mnh…haiwezekani jamaa akawa ametoa ripoti polisi juu ya kifinyo ulichompa, na Ngamao ndo amekwenda kumhoji?”
“No! Ngamao si askari wa hapa Dar tena…kwa nini apewe yeye kesi hii? Hapa kuna kitu hakipo sawa. Ila kitajiweka wazi tu.Sisi tuzingatie kuwatenganisha wote hawa na Candy…wasipate nafasi ya kuonana naye mpaka atakapopanda ndege, kwa mujibu wa maelekezo ya bosi wetu aliyetopea kwenye penzi!” Morandi alisema, huku bado akiwa na mawazo.
Kimya kilitanda kwa muda, kisha Nuru akahoji.
“Haya…umegundua nini kwenye zile alama za vidole vya yule fala aliyenizaba kofi kule mlimani city siku ile?”
Morandi alibofya kwenye kompyuta mpakato yake iliyokuwa pale mezani, sebuleni kwa Bishkuku.Baada ya muda alama za vidole alivyovitoa kwenye ile karatasi laini aliyotumia kukopi alama zile kutoka shavuni kwa Nuru na kuziigiza kwenye kompyuta yake baada ya kui-scan ile karatasi laini ikatokea pale kwenye uso wa ile kompyuta.
“Bila-bila!” Alisema huku akizitazama tena zile alama za vidole zilizoganda pale kwenye uso wa kompyuta yake maalum.
“Dah, kwa hiyo ina maana hakuna rekodi yoyote ya jinai kuhusiana na mwenye hizo alama za vidole?” Nuru alisaili kwa fadhaa.
“Hivyo ndivyo kompyuta yetu inavyotuambia…lakini sio kwamba huo ndio ukweli!” Morandi alimjibu kwa upole, bado akiwa na tafakuri. Nuru akamkodolea macho ya kuuliza.
“Sikuelewi!”
Morandi alimzungushia jicho na kumtazama kwa muda, kisha akaigeukia tena ile kompyuta yake. Halafu akamgeukia.
“Unajua nilipoondoka kwenye jeshi la polisi niliiba hii programu ya kompyuta yenye alama za vidole za wahalifu wote waliokamatwa na wanaotafutwa…”
“Hilo nalijua Mo…nd’o maana nashangaa kwa nini huyu mtu ambaye anaonekana kabisa kuwa ni mhalifu, alama zake zisiwemo humo? Sitaki kuamini kuwa hili ni kosa lake la mwanzo bwana!”
“Ni kweli. Lakini pia ni kweli kuwa hii programu ina kumbukumbu ya alama zote za vidolehadi pale mi’ nilipoacha jeshi. Kwa hiyo alama mpya za vidole zilizoingizwa kwenye programu hii huko kwenye jeshi la polisi baada ya mimi kuondoka sitakuwa nazo humu!”
“Duh, kweli…”
“Yeah…hii inamaanisha kuwa kama kuna rekodi ya alama za vidole vya huyu jamaa, basi zitakuwa zimeingizwa katika database ya manjagu ndani ya miaka mitatu tu iliyopita!” Morandi alihitimisha.
***
Ngamao Kijambia alijiweka sawa ndani ya gari la polisi alilopewa na mkuu wa polisi wa kituo kidogo cha Tarime na kutazama saa yake. Muda ulikuwa ni saa nne za asubuhi, na kwa mujibu wa matangazo aliyokuwa akiyasikia redioni, ni kwamba mrembo wa taifa Candy Gamasala alikuwa anatarajiwa kukitembelea kituo cha watoto yatima ambacho yeye alilelewa, muda wowote kuanzia saa nne ile.
Kwa namna fulani hili lilionekana kuwa ni tukio muhimu sana, na vyombo vingi vya habari vilikuwa vikilinadi tukio lile kwa ushabiki uliopitiliza.
Yatima wa kwanza kunyakua taji la urembo wa taifa anaenda kukitembelea kituo cha kulelea watoto yatima ambacho yeye mwenyewe ndipo alipolelewa kabla ya kutwaa taji hilo. Lilionekana kama ni tukio la aina yake, naye akazidi kujawa kiherehere, akisubiria wakati ambapo ataingia kwenye nyumba ile na kuzipasua na kuzichanachana furaha za hao waandishi na huyo mrembo wao wa taifa kwa kumuweka chini ya ulinzi huyo mrembo wao.
Alitupa macho mbele na kuona kundi la waandishi wa habari wa pale wilayani tayari wakiwa wamejirundika nje ya ile nyumba ya watoto yatima, ambayo nayo ilikuwa imepambwa ilhali watoto waliokuwa wakilelewa mle ndani wakionekana wakipita huku na huko ndani ya uzio wa senyenge wa nyumba ile wakiwa na bashasha ya kumpokea Miss Tanzania aliyetoa miongoni mwao.
Nyie chekeleeni tu…mudo si muda mtakuwa mkimsaidia huyo Miss Tanzania wenu kulia na kusaga meno hapa!
Alijiwazia huku akitazama zile harakati zilizokuwa zikiendelea kule kwenye ile nyumba ya watoto yatima kutokea nyuma ya miwani yake ya jua.
“Muda wowote sasa mtuhumiwa wetu atawasili eneo hili…nasi tutamuweka chini ya ulizi!” Alisema kuwaambia askari wawili wa kike aliokuwa nao mle garini, wakiwa wameketi kwenye kiti cha nyuma ilhali yeye akiwa kwenye kiti cha mbele na dereva wa gari lile.
Miguno ya kuafiki taarifa ile ilisikika kutokea kule nyuma.
Ingawa alifanikiwa kumshawishi mkuu wa kile kituo kidogo cha polisi pale Tarime ampatie askari wa kike pamoja na usafiri, hakuwa amemtajia mtuhumiwa huyo aliyekuwa amemkusudia kummuweka chini ya ulinzi ni nani. Alichomwambia ni kwamba amepewa taarifa kuwa mtuhumiwa aliyekuwa akitafutwa kwa muda mrefu atakuwa katika msafara wa miss Tanzania utakaotembela kituo cha watoto yatima kilichopo pale wilayani, na hivyo kwa kuwa yeye alikuwa amekwenda Tarime kwa mambo yake binafsi, ofisi yake ilimuomba awasaidie kumuweka chini ya ulinzi mtuhumiwa huyo.
Mkuu wa kituo akampatia askari na usafiri, na sasa ndio alikuwa akisubiri ujio wa miss Tanzania atimize azma yake.
Mwili ulimsisimka kwa hamasa ya lile alilokuwa ameazimia kulifanya kwa muda mrefu. Msako wa miaka miwili sasa ulikuwa umefikia hatima, naye alizidi kujawa hamasa pale alipoona waandishi wa habari wakizidi kumiminika pale nje ya ile nyumba ya watoto yatima.
Ama zako, ama zangu leo. Kisonoko mkubwa we!
Kilomita chache tu kutoka pale kwenye ile nyumba ya watoto yatima, Candy Gamasala alikuwa akiendelea na kampeni yake iliyoanzia kule kwenye kijiji cha jamii ya wakulima. Tukio lake pale kwa wanakijiji wa jamii ile lilikuwa la mafanikio makubwa. Aliongea na wakuu wa jamii ile na kuwathibitishia juu ya nia yake na kwamba naye ni mtoto wa jamii yao. Aliwaambia kuwa hakwenda pale kuwahamasisha kuandaa vikundi vya ulipizaji visasi, bali kuandaa jamii itakayowapokea wenzao wa jamii ya kifugaji kama ndugu waliopotezana, na ambao sasa wanakutana tena.
Hili lilipokelewa kwa shangwe na wanajamii wale.
Picha nyingi zilipigwa akiwa na wazee wa jamii ile, pia akiwa na akina mama wa jamii ile mashambani, pamoja na watoto wengi wa jamii ile. Pia alipiga picha akicheza ngoma na akina mama na watoto wa jamii ile.
Picha hizo zilitumwa mara moja kwenye mitandao mbali mbali ya kijamii pamoja na kwenye tovuti ya Miss Tanzaniana kwenye vituo vya habari ilihali wale waandishi wa habari wa vituo vya redio wakitangaza moja kwa moja kila kilichokuwa kikitokea pale na wale wa televisheni wakirekodi kwa ajili ya kurusha matangazo yale baadaye.
Ujumbe ule ukatoka pale kuelekea kwenye kituo cha watoto yatima ambapo Candy alilelewa, na baada ya hapo uelekee kwenye jamii ya wafugaji kumalizia ziara ile muhimu kwa propaganda za u-miss. Kila kitu kilikuwa kinaelekea kwenda kama kilivyopangwa, wakati mratibu wa kamati ya miss Tanzania nchini alipopokea simu iliyoleta mtafaruku kwenye ule msafara…
***
Ngamao Kijambia alilitazama gari kubwa aina ya Toyota Prado lenye nembo za miss Tanzania likiingia ndani ya uzio wa ile nyumba ya watoto yatima huku waandishi wa habari wakilikimbilia na kulizonga kwa kamera zao, ilhali wale watoto yatima nao wakijipanga kwa bashasha huku wakiimba nyimbo za shangwe.
“Okay askari! Nadhani mtuhumiwa wetu ameingia mtegoni sasa…lets go!” Alisema huku akiteremka kutoka kwenye lile gari, wale askari wawili wa kike wakimfuata nyuma yake.
“Er, afande…si tungeenda na gari mpaka pale tu?” Dereva wao alimuuliza, na Ngamao akamgeukia, akimtazama huku akiichomekea vizuri suruali yake ya polisi aliyoivaa maalum kwa ajili ya tukio lile.
“Hapana koplo…wewe subiri hapa hapa. Tukishamkamata mtuhumiwa wetu, tutatembea naye kwa miguu kutoka pale kwenye geti…” Alimjibu huku akilioneshea lile geti la ile nyumba ya watoto yatima kwakidole chake, kisha akaendelea, “..hadi hapa kwenye hili gari. Akiwa na pingu mikononi!”
Kisha akageukia kule kwenye ile nyumba ya watoto yatima.
“Na wakati akitembea na pingu mikononi kuja hapa kwenye gari, waadishi wa habari watapata muda wa kutosha sana kumpiga picha za kwenda kupamba magazeti yao!” Alisema huku akiweka vizuri kofia yake ya polisi kichwani, na akiongoza njia kuelekea kule kwenye ile nyumba ya watoto yatima.
Kule ndani ya nyumba ya watoto yatima mkuu wa kile kituo, wale watoto yatima wenye bashasha, na waandishi wa habari walipigwa butwaa pale walipomshushudia msaidizi wa mratibu wa kamati ya Miss Tanzania na mmoja wa watendaji wa kamati ile, mwanadada mrembo aliyekuwa sehemu nya msafara wa Candy, wakitelemka kutoka kwenye lile gari.
“Vipi…yu wapi miss Tanzania…yu wapi Candy jamani?” Mkuu wa kituo kile aliuliza kwa mshangao, waandishi wa habari wakiwazingira, wazi nao wakitaka kujua kilichotokea mpaka mrembo wa taifa akakosekana kwenye ugeni ule. Msaidizi wa mratibu alimuomba yule mkuu wa kituo waingie ofisini na kuongea kwa kituo juu ya kilichojiri.
Waliingia ofisini, na dakika tano baadaye walitoka nje ya jengo lile kwa lengo la kutoa taarifa kwa waandishi wa habari, ndipo walipokutana na Inspekta wa polisi akiingia ndani ya lile eneo akifuatiwa na askari wawili wa kike.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mkuu wa kituo hakushangaa sana alipowaona wale askari wakiingia ndani ya eneo lake.
“Oh, jamani poleni sana wana usalama…naona mkuu wetu wa polisi hapa kijijini aliwatuma kuja kutuwekea usalama kutokana na ugeni wetu uliotukuka…” Alisema huku akimtazama Ngamao na wale askari wenzake, na Ngamao akawa anatembeza macho kumtafuta Candy bila mafanikio. Alishangaa kumuona mrembo mmoja ambaye hakuwa Candy,akiwa na afisa mmoja tu wa ile taasisi ya Miss Tanzania. Alianza kuwasogelea wale maafisa kutoka kwenye ile kamati ya uratibu wa shindano la miss Tanzania wakati yule mkuu wa kile kituo cha kulelea watoto yatima aliposema maneno yaliyomchoma moyo wake kama msumari wa moto.
“Bahati mbaya Miss Tanzania amelazimika kukatisha ziara yake ghafla kutokana na muingilianao wa majukumu ya kitaifa na kimataifa, na hivyo ametuma hawa wawakilishi wake hapa kuja kututaka radhi na kutuwasilishia misaada aliyokuwa ameiandaa kwa ajili yetu…”
Ngamao alihisi mwili ukimwingia baridi na akili ikimvurugika.
Hah!Hakuja?
Kwa nini?
Kuna nini kimetokea…unataka kuniambia kuwa alishtukia picha?But how? Mi’ sikuweka wazi ni nani niliyekusudia kumkamata hapa!
Alijwazia kwa wahka mkubwa huku akisimama palepale alipokuwa, akitazama jinsi waandishi wa habari wakiwazingira wale wawakilishi wa Miss Tanzania huku wakiwatupia maswali. Wala hakuweza kufuatilia majibu yaliyokuwa yakitolewa na yule msaidizi wa mratibu wa Miss Tanzania. Wazo pekee lililokuwa kichwani mwake ni kwamba Candy hakuwepo pale, naye alikuwa anataka kujua afanye nini muda ule kuhakikisha kuwa hapotezi nafasi ile aliyokuwa ameisubiri kwa muda mrefu.
“…kwa hiyo imelazimu mrembo wetu wa taifa arejee Dar es Salaam haraka sana ili afanye maandalizi ya muhimu kuelekea kwenye shindano la urembo wa dunia. Na ndio maana ametutuma kuja kuwataka radhi, na pia kuahidi kuwa pindi atakaporudi tu nchini kutoka Venezuela, safari yake ya kwanza itakuwa ni kuja hapa na kutimiza ahadi yake hii!” Mratibu msaidizi alimalizia maelezo yake.
Watoto yatima waliangua vilio vya uchungu kwakukosa kuonana na mrembo wa taifa aliyeokea kwenye ile nyumba yao, akiwa ni miongoni mwao, na baadhi ya wafanyakazi wa ile nyumba ya watoto yatima nao wakajikuta wakilia pamoja naowakati waandishi wa habari wakichukua picha za tukio lile, wakiliona kuwa nalo pia ni habari.
Ngamao alilisogelea lile gari la Miss Tanzania na kulichuguza kwa makini.Zaidi ya baadhi ya zawadi ambazo zililetwa kwa wale watoto yatima pale kituoni, kulikuwa kuna dereva tu ndani yake.
Hakukuwa na mtu mwingine mle garini.
Dah! Malaya kanipiga chenga ya mwili (akamtukania mama yake).
Akasonya.
“Lets go!” Aliwakoromea wale askari wa kike aliokwenda nao pale kwa lengo la kumuweka chini ya ulinzi Miss Tanzania, ambao walimshangaa na kumfuata nje ya nyumba ile.
“Hah, vipi afande…? Mbona…?” Mmoja wa wale askari alimuuliza kwa mshangao.
“Ah, taarifa nilizopewa hazikuwa sahihi…mtuhumiwa wetu hakuwepo kwenye msafara huu…” Alijibu kwa hasira, akili ikimzunguka.
Miss Tanzania anarudi Dar es Salaam kujiandaa na safari ya kwenda kwenye shindano la urembo wa dunia!
Aliingia kwenye gari na kubamiza mlango kwa hasira.
“Nipeleke moja kwa moja uwanja wa ndege! Kisha nyie mtarudi kituoni kwenu baada ya hapo!” Aliunguruma, uso ukiwa umekoza weusi kwa hasira.
Huyu mshenzi hanitoroki kirahisi safari hii…hiyo ndege hapandi pumbavu zake!
Alikuwa na saa nzima ya kusafiri kwa gari kutokea pale Tarime hadi Musoma mjini ambako ndiko angepanda ndege ya kumrudisha Dar.
Na n’tamuweka chini ya ulinzi huko huko Dar (akamtukania mama yake)! Hapandi ndege kwenda popote, pumbavu zake!
***
Nusu saa kabla ya kuwasili kwa wale wawakilishi waliotumwa kwenda kumtolea udhuru Miss Tanzania pale kwenye ile nyumba ya watoto yatima, Prakshantji Prakteshji, mwenyekiti wa taasisi inayosimamia mashindano ya Miss Tanzania nchini alikuwa akiongea kwa wahka mkubwa simuni.
“Hali si nzuri nakwambia mratibu wangu…si nzuri kabisa! Hata sijui tunafanyaje sasa! Mwaka huu umekuwa hovyo kabisa!” Alimaka kwa kiswahili chake kilichochovywa-chovywa lahaja za kihindi, na mratibu akamtupia Candyjicho la pembeni, aliyekuwa kando yake kwenye kiti cha nyuma ndani ya moja ya magari mawili yaliyokuwa kwenye ule msafara wa kuelekeakule kwenye kile kituo cha kulelea watoto yatima, kabla ya kwenda kwenye kile kijiji cha jamii ya wafugaji.
“Hali gani hiyo unayoiongelea Prakshantji? Kumetokea nini tena huko? Sisi huku kila kitu kiko kwenye mstari…”
“Hali ya rais wa Venezuela imezidi kuwa mbaya bhabha! Nimepokea email na simu pia kutoka kamati ya Miss World na kutoka kamati ya Miss Venezuela pia! Yule rais anaweza kufa muda wowote sasa, kwa hali ilivyo!”
“HAH! Sasa…? Duh!” Mratibu alimaka kwa mshangao mkubwa, na Candy akamakinika naye.
“Kuna nini tena…tatizo?” Aliuliza, lakini mratibu bado alikuwa anaongea na Prakshantji.
“Nhaa, nhaa, nhaaa mere bhai…tena bonge la Duh, hilo!” Prakshantji alipayuka,akichanganya na kihindi bila kujitambua, kisha akaendelea, “…hivi niongeavyo Miss Kenya na Miss Rwanda wanaondoka usiku wa leo kwenda Venezuela!”
“What?”
“Sasa kumbe we’ unadhani mein paagal ho gaya kyaa, bhabha? Hii imeshakuwa bal…” Mhindi alizidi kupagawa, na mratibu akamkatisha.
“Prakshantji!Unajua kuwa mi’ kihindi sikijui! Hebu ongea Kiswahili tupate kwenda sawa bwana…hii paagal-hoga-vitu gani tu sijui huko ndo nini tena?” Mratibu alimjia juu mwenyekiti wake, na upande wa pili Prakshanji akaachia mguno wa kuchanganyikiwa.
“Ah, sorry bhana...nilikuwa namaanisha we unadhani mi’ napandwa na wazimu kwa nini hapa? Kule Venezuela shindano linaanza ndani ya siku nne zijazo bhabha! Washiriki wote wanatakiwa waanze safari immediately, yaar!” Prakshatji alibwata simuni, na bila kufikiri zaidi mratibu akamwambia dereva ageuze gari.
“Tunarudi Dar sasa hivi, Prakshant…sasa hivi!” Mratibu alimwambia mwenyekiti wake na kukata simu. Candy akamtolea macho, ilhali mwenzao aliyekuwa na dereva kule kwenye kiti cha mbele akiwageukia akiwa ametumbua macho pima wakati dereva akiliegesha gari kando ya barabara kabla ya kugeuza.
Mratibu hakutoa maelezo haraka.
Gari jingine lililokuwa nyuma yao kwenye msafara ule nalo likasimama baada ya kuona wenzao wanaegesha gari pembeni.Mratibu aliteremka na kwenda kuwapa maelekezo wale wenzao waliokuwa kwenye lile gari jingine, akiwataka kwenda kutoa udhuru kule kwenye nyumba ya watoto yatima na kwa waandishi wa habari; na baada ya hapo aliwaagiza waendelee na safari hadi kule kwenye kijiji cha jamii ya wafugaji na kutoa udhuru kama ule aliowataka wakautoe kule kwenye nyumba ya watoto yatima.
Kwisha kufanya hilo ndipo aliporudi kwenye lile gari alilokuwamo na kuwapa akina Candy maelezo juu ya kilichojiriwakiwa njianikurudi uwanja wa ndege wa kampuni ya kuchimba madini ya Barrick Gold uliokuwa pale pale Tarime, ambako ndege yao ilikuwa ikiwasubiri. Barrick Gold walikuwa ni moja wa wadhamini wa shindano lile, hivyo hawakusita kuwapatia ile ndege yao na kuwaruhusu watumie uwanja wao binafsi wa ndege, badala ya kulazimika kurudi mpaka Musoma mjini kutumia uwanja wa ndege wa serikali.
Njia nzima Candy alikuwa akilia kwa uchungu, kwani hakika alikuwa ameiwekea hamu sana safari ile ya kwenda kuitembelea tena ile nyumba ya watoto yatima aliyolelewa kwa sehemu kubwa ya maisha yake.
Lakini wote mle garini walikubaliana kuwa kwa hali ilivyokuwa, hawakuwa na namna zaidi ya kurudi Dar na kuanza maandalizi ya safari ile muhimu kwao na taifa kwaujumla.
Bila ya Candy kujua, ni taarifa ile kutoka kwa mwenyekiti Prakshantji, na uamuzi wa haraka wa mratibu wakati ule ndivyo vilivyomnusuru kutokana na aibu na idhilali kubwa iliyokuwa ikimsubiri kiasi cha kilometa moja na nusu tu kutokea pale gari lao lilipokuwa wakati mratibu akitoa amri ya kubadili uelekeo.
Candy na baadhi ya watendaji wa kamati ya Miss Tanzania pamoja na mratibu walirudi Dar kwa ndege asubuhi ile ile, wakati wale wawakilishi waliobaki kwenda kutoa udhuru kwenye kijiji cha wafugaji, wangeondoka siku iliyofuata.
Na Ngamao Kijambia akaambulia patupu.
***
Mchana ule ule Candy aliingia jijini na kukuta taratibu za kumuandalia safari zikiwa zimeshaanza. Alitakiwa apande ndege usiku wa manane siku ile ile kuelekea Venezuela. Kokos Wandiba na Bishkuku nao walishajiandaa kuandamana naye pamoja na msafara wa watendaji muhimu kutoka kwenye ile kamati ya Miss Tanzania, akiwemo mratibu na mwenyekiti wake Prakshantji.
Saa tisa mchana alikutana na waandishi wa habari ambako mwenyekiti aliwafahamisha watanzania kupitia kwa waandishi wa habari kuwa hali ya rais wa Venezuela imesababisha shindano kiharakishwe ili kuepusha kuahirishwa, na hivyo Candy angeondoka usiku ule ule kwenda Venezuela kuwahi sherehe za ufunguzi wa shindano lile kubwa kabisa la urembo duniani.
Moja kwa moja baada ya hapo Candy na ujumbe wote wa kamati ya Miss Tanzania pamoja na akina Bishkuku walielekea kwenye ukumbi wa hoteli ya kitalii ya The Kilimanjaro Hyatt Regency kwa ajili ya tafrija maalum ya kumuaga kwenda kuliwakilisha taifa huko ughaibuni. Waziri wa utamaduni, maendeleo ya vijana na michezo alikuwa ndiye mgeni rasmi kwenye tafrija ile na ndiye aliyemkabidhi bendera ya taifa.
Baada ya hapo alirudi chumbani kwake pale hotelini kujipumzisha kusubiri muda wa safari usiku ule. Bishkuku alikuwa naye muda wote mle chumbani, wakati Kokos alirudi nyumbani kwake kuchukua baadhi ya mavazi ya mrembo yule ambayo Bishkuku alikuwa amemuandalia kabla, kwa ajili ya shindano lile.
Katika harakati zote zile zilizokuwa zikiendelea Morandi Gwaza na Nuru walikuwa wakifuatilia kwa makini, hususan kumtafuta Ngamao Kijambia katika mikusanyiko ile.
Ngamao hakuonekana kabisa kwenye mikusanyiko ile iliyomhusisha Candy. Hili lilimpa taabu sana Morandi. Lakini hata Nuru pia lilimpa wakati mgumu.
“Sina amani Morandi…” Nuru alimwambia wakati wakimtazama Candy akirudi chumbani kwake baada ya kumalizika kwa ile tafrija fupi ya kumuaga, na Morandi akamgeukia.
“Kuhusu nini, Nuru?”
“Sijui kwa kweli…moyo wangu hauna amani tu juu ya hili. Kwa nini Ngamao aende kuongea nini na GTZ halafu apotee kabisa jijini?” Nuru alisema.
“Na hilo kwako ndio linakukosesha amani?”
“Of Course, Mo! Hawezi kwenda kwa GTZ burebure tu! Mi nadhani kama kuna kitu GTZ amekiandaa dhidi ya Candy atakifanya kabla hajaondoka kwenda Venezuela…”
“Ina maana atalifanya leo?”
“Kwani si leo nd’o Candy anaondoka kwenda Venezuela na wewe? Mi sina amani nakwambia!”
“GTZ atafanya nini wakati yuko hoi bin taabani huko hospitali wewe…pongezi za dhati zinijie mimi kwa hilo?” Morandi alimsaili.
“Sa’ si nd’o nikawa na imani kabisa kuwa yule Ngamao atakuwa somehow anahusiana na hii kadhia…lakini sasa mbona kapotea hivi hivi tu?” Nuru alizidi kuchangia hoja.
“Okay, okay…hata mimi sielewi kwa nini Ngamao asionekane kabisa hapa…labda kama alienda kwa GTZ kuhusiana na mambo mengine tu. Ila na we’ ukishaanza kuwa na hali za wasiwasi kama hizo lazima kutakuwa kuna kitu tu…”
“Umeona eeenh? Sa’ tufanyaje?” Nuru aliuliza.
Morandi alifinya uso kwa mawazo.
“Najua la kufanya kisura…niache nipige simu kadhaa kwanza!” Morandi alimwambia, na kidogo Nuru akatulia.
Kama Nuru alikosa amani kwa sababu zake binafsi, GTZ naye alikosa utulivu kabisa akiwa kitandani kwake pale Aga Khan hospital, wakati akisikiliza matangazo ya luningani kuwa Candy alikuwa amerudi jijini kwa ajili ya safari yake ya Venezuela usiku ule.
Na alikosa utulivu maradufu pale kila alipokuwa akijaribu kumpigia simu Ngamao, simu yake ikawa haipatikani. Alibaki akiikodolea macho luninga nyingine iliyoletwa mle chumbani kwake baada ya kuwa ile ya kwanza ameivunja, na kulazimika kuilipa ile hospitali kwa hasara ile.
***
Ngamao aliingia jijini saa kumi na robo mchana ule akiwa amenuna na amejawa wahka mkubwa. Safari yake kutoka Tarime kwenda Musoma mjini ilimpotezea saa nzima, kinyume na Candy ambaye alipandia ndege yake maalum pale pale Tarime kwa kutumia uwanja wa ndege wa binafsi. Kibaya zaidi, yeye alishafanya utaratibu wa tiketi mbili za ndege kutokea pale Musoma kwenda Mwanza, tiketi ya pili ikiwa ni kwa ajili ya mtuhumiwa wake Candy. Alipanga kurudi naye kule kule ambako makosa yake yalitokea. Sasa kufika musoma alikuta tatizo la usafiri wa kurudi Dar na kubadilisha tiketi badala ya kwenda Mwanza arudi Dar. Ndege ya karibu kabisa kuondoka pale ilikuwa ni saa nane mchana, ambayo haikupaa angani mpaka saa tisa na nusu mchana ule.
Alimpigia simu GTZ kumpa hali halisi, na alipoona GTZ amechaga kufoka tu na kutukana hovyo akamkatia simu na kuizima kabisa.
Jambo la kwanza alilofanya baada ya kutua Dar ni kufungua simu yake na kumpigia GZT.
“Malaya anaondoka kwa ndege usiku huu Ngamao! We’ umezima simu masaa yote hayo! Sasa sijui…”
“Basi haondoki huyo. Nimeshaingia mjini na nitamuweka chini ya ulinzi kabla hajafika hata huko uwanja wa ndege (akamtukania mama yake)” Ngamao alimkatisha, uso wake ukionesha kuwa alikuwa amedhamiria alilokuwa akilifanya.
Muda huo huo, sehemu nyingine ya jiji simu ya Morandi ikaita.
Alitazama jina la mtu aliyempigia simu ile kwenye kioo cha simu yake na akaachia tabasamu la upande mmoja wakati akiipokea ile simu na kuipeleka sikioni.
“Niambie, jembe langu!” Aliongea kwenye simu.
“Taarifa za kuaminika kutoka kwa jamaa zangu zinasema kuwa kifurushi kimeonekana jijini mchana huu!” Jamaa aliyempigia ile simu alimwambia, na Morandi akamtupia Nuru jicho la pembeni.
Walikuwa wamekaa kwenye kona mbili tofauti eneo la mapokezi la pale hotelini kwa Candy. Nuru alikuwa akimtupia jicho la kuuliza.
“Okay…good. Kimeonekana wapi?” Aliuliza huku bado akimtazama Nuru.
“Ndio kwanza kimeshuka kutoka kwenye ndege ya kutokea Musoma, huko uwanja wa ndege!” Yule askari wa usalama wa barabarani aliyemtumia kumdhibiti GTZ wakati anataka kwenda kumfuata Candy Mikumi alimjibu, na Morandi akamakinika maradufu.
“Umesema Musoma?” Macho yalimtoka, na akili ikamzunguka.
“Yah! Ameshuka kwenye ndege…na ndege pekee iliyoingia mida hii ni kutokea Musoma…so ukiweka mbili na mbili hapo lazima jibu liwe nne tu. Au we unapata tisa?” Jamaa alimuuliza halafu akaishia kucheka kwa ule utani aliomfanyia Morandi.
Morandi hakuwa katika ari ya kucheka. Uso ulimbadilika na akajua kuwa Ngamao alikuwa ameenda Musoma kumfuata Candy. Nuru aliona badiliko usoni kwake, na akabaki akimtupia macho yenye viulizo.
“Okay…kwa hiyo utaratibu tuliokubaliana unaendelea?” Aliuliza tena.
“Of course…askari mwingine wa barabarani analifuatilia gari lake kila liendapo hivi tuongeavyo!”
“Safi sana. Basi nataka kila baada ya dakika tano unitumie meseji kuniambia mahala alipo…sawa?” Morandi alitoa maelekezo
“Yes Sir! Na vipi kuhusu mpunga wetu sasa?”
“Hilo si tatizo…utapokea MPesa ndani ya dakika kumi kutoka sasa. Kazi nzuri!”
“No sweat! Lakini si unajua kuwa safari hii siko peke yangu kamarade?” Jamaa aliongezea kwa msisitizo.
“Yap! Na ndo maana nikakwambia ukinifanyia hii kazi kwa kiwango nikitakacho, laki mbili zitakuhusu…sasa hizo hazitoshi kukutoa wewe na hao wenzako?” Morandi alisaili, na akasikia jamaa akicheka upande wa pili.
“Hicho tu ndicho ninachopendea kufanya madili na wewe Mo…huna longolongo kwenye mshiko. Subiri meseji zangu kamanda!” Jamaa alimjibu, na Morandi akakata simu.
Bila kumtazama Nuru aliinuka na kuelekea eneo la la vyumba vya kulala vya hoteli ile kubwa.
Alienda moja kwa moja na kuingia kwenye chumba kilichokuwa kinatazamana na kile cha Candy na kuketi kitandani akiwa amekunja uso kwa tafakuri nzito. Dakika tano baadaye, Nuru alifungua mlango wa chumba kile na kuingia ndani huku akimtazama kwa macho ya kuuliza.
“Jamaa alikuwa Musoma pumbavu zake!”Morandi alimwambia bila utangulizi mara baada ya Nuru kuingia mle ndani.
“Ina maana alimfuata Candy huko?”
“Ndivyo ninavyoamini, bloody shit! Ina maana kama si kuharakishwa haya mashindano kulikomfanya Candy akatishe ziara yake kule, bila shaka saa hizi Ngamao angekuwa ameshamfanyia lolote lile ambalo alilokuwa anataka kumfanyia…”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Duh!”
“Ndiyo! Na siye tugekuwa tumekaa tu huku ka’ mabwege! Hii ni mbaya sana!” Morandi alizidi kulaani na hapo meseji ya tatu ikangia kwenye simu yake. Aliisoma ile meseji na kumtazama Nuru.
“Na sasa inaelekea Ngamao anakuja katikati ya jiji…sijui anaelekea wapi, lakini naweza kukupa asilimia mia kwa mia kwa anakuja hapa hotelini!” Alisema, na Nuru akasaili ni vpi anajua habari zote hizo.
Ndipo alipomwambia juu ya mazungumzo yake na yule askari wa usalama barabarani aliyempa kibarua cha kumfuatilia Ngamao.
Nuru akahamanika.
“Sasa…unadhani Ngamao naye anashirikiana na GTZ katika kumdhuru Candy? Kwa nini aje moja kwa moja mpaka hapa bila ya woga wowote?”
Morandi alipiga kimyakwa muda.
“Jamaa ni mzoefu kwenye kazi Nuru, na ndio maana nikashtuka sana nilipoona anajihusisha na hili sakata…Hii itamaanisha kuwa kiukweli Candy atakuwa anahusika na jinai fulani huko nyuma. Ngamao atakuwa amekuja katika hadhi ya kiserikali zaidi kuliko ilivyokuwa kwa GTZ.” Hatimaye alimjibu na Nuru akaguna kwa kukata tamaa.
“Haya majanga sasa…”
“Yap!Sijui alifanya nini tu huyu binti! Asije akamtumbukiza na Kokos tu kwenye hayo majanga!”
“Duh, sa’ tunafanyaje?”
“Tunaendelea na kazi yetu kama kawaida Nuru! Si unajua mi bado n’na deni la kulipa?Kama si Kokos bila shaka ungekuwa umeshajipangia ratiba ya kwenda kupeleka mashada ya maua kwenye kaburi langu kila mwaka saa hizi, sio?” Morandi alimjibu, na Nuru alimpiga ngumi ya kimaskhara kwa utani ule.
***
Njia nzima kutoka uwanja wa ndege Ngamao alikuwa amefura kwa hasira. Moyo ulikuwaukimwenda mbio kwa kiherehere cha kumtia Candy mbaroni kabla hajaondoka nchini. Hata hivyo alifarijika kidogo kusikia kupitia redio ya gari lake kwamba mrembo yule angeondoka usiku wa manane siku ile kuelekea Venezuela, na hivyo alijua kuwa angepata muda mzuri wa kupanga shambulizi lake. Pia kupitia redio ile alipata kusikia kuwa mrembo yule alikuwa anapatikana kwenye ile hoteli kubwa ya kitalii ya Kilimanjaro Grand Hyatt, naye hakutaka kupoteza muda.
Akiwa amepata utulivu juu yahili baada ya kupata habari hizi kupitia redio iliyokuwa mle garini, umakini wake wa kipelelezi ukamrudia.Na ndipo alipogundua kuwa kulikuwa kuna askari wa usalama barabarani mwenye pikipiki ambaye amekuwa nyuma yake kwa muda mrefu.
Katika mazingira ya kawaida asingemtilia mashaka yule askari, lakini alipokumbuka maelezo ya GTZ, kuwa jamaa aliyemlaza pale hospitali kwa kummong’onyoa goti aliwahi kutumia askari wa usalama barabarani kumdhibiti ili asimfuate Candy Mikumi alimakinika mara dufu.
Ah! Ina maana hawa jamaa wameshajua kuwa niko hapa mjini na kwamba ninamfuatilia Candy?
Au ndio sababu wakamrudisha Candy jijini haraka, wakijitia kuwa ameitwa Venezuela?
Lakini mbona haingii akilini? Kwani kwa hakika nimesikia kwenye vyombo vingi vya habari kuwa hali ya raisi wa Venezuela ni mbaya!
Alizidi kujiuliza huku akimtupia jicho yule mwendesha pikipiki aliyekuwa kwenye sare za askari wa barabarani kupitia kwenye vioo vyake vya kuonea nyuma.
Akawa makini zaidi na yule askari wa usalama barabarani mwendesha pikipiki.
Kadiri alivyokuw aakiendelea kumtupia jicho kwa kupitia vioo vyake vya kuonea nyuma, ndivyo alivyopata msisimko zaidi, kwani alipobaini kuwa jamaa alikuwa akitumia mbinu za kipolisi katika kumfuatilia, mara akiacha magari mawili baina yao, mara akiacha moja, namara akiwa moja kwa moja nyuma yake.
Alijaribu kumuona sura lakini hilo lilikuwa gumu kutokana na kofia ngumu ya kuendeshea pikipiki aliyokuwa ameivaa ambayo ilimziba kabisa uso wake.
Msisimko wa kipelelezi ukamtambaa mwilini.
Aliongeza kasi ya gari na kuzipita gari mbili zilizokuwa mbele yake, na hivyo kusababisha kuwe na magari matano baina yake na yule jamaa ambaye sasa alikuwa na hakika kuwa alikukwa akimfuatilia.
Mwendesha pikipiki naye akaongeza kasi na kupunguza lile pengo baina yao na kubakisha magari matatu kati yao.
“Ah, mshenzi anaifuatlia huyu!Kwa nini?”Ngamao alijisemea peke yake garini.Muda ule alikuwa ameshaanza kuingia katikati ya jiji. Alitupa macho huku na huko mjini na kuona mgahawa mmoja maridhawa. Aliegesha gari nje ya mgahawa ule, kisha akateremka na kuingia ndani yake huku akijaribu kuzungusha macho kuitazama ile pikipiki iliyokuwa ikimfuatilia.
Hakuiona, lakinialijua kuwa yule mwendesha pikipiki alikuwa anamuona kutokea sehemu ambayo yeye hakuweza kumuona.
Kweli.
Kutokea kwenye kona iliyokuwa mwanzo kabisa wa ule mtaa ambao ule mgahawa ulikuwepo, yule askari wa usalama barabarani mwendesha pikipiki aliongea kwenye simu yake kupitia visikilizio alivyochomeka masikioni mwake na kisemeo kilichokuwa kikining’inia karibu na kinywa chake.
“Kaka kifurushi chetu kimeingia mgahawani hapa katikati ya jiji!”
“Oh, mgahawa gani huo?” Mshirika wa Morandi alimuuliza kutokea upande wa pili wa simu ile.
Mwendesha pikipiki akamtajia.
“Hmmm…okay. Kaa naye hapo mpaka ujue atatoka baada ya muda gani, na akitoka, endelea kuwa naye mpaka tujue mwisho wake! Bila shaka anapata msosi huyo!” Mshirika wa Morandi alitoa melekezo.
“Poa!”
Dakika mbili baadaye Morandi alipokea ujumbe kwenye simu yake ukimfahamisha mahala ambako Ngamao alikuwa muda ule.
Morandi alikunja uso kwa tafakuri.
“Haileti maana, mrembo wangu!” Hatimaye alisema, na Nuru akamtumbulia jicho la mshangao.
“Ni nini hiyo isiyoleta maana tena, Mo?” Alimuuliza, na Morandi akamueleza juu ya ule ujumbe wa mwisho kuingia kwenye simu yake.
Nuru aliishia kuguna tu.
***
Kule mgahawani katikati ya jiji, Inspekta Ngamao Kijambia alipitiliza moja kwa moja hadi msalani huku akitembeza macho yake eneo lote mle ndani. Alikaa humo kwa dakika kadhaa kisha akatoka na moja kwa moja akachukua uelekeo wa jikoni, ambao aliuona wakati akielekea kule msalani. Huko alipitiliza hadi kwenye mlango wa kutokea nyuma ya mgahawa ule ambako magari yaliyokuwa yakipeleka bidhaa za kupikwa pale mgahawani ndipo yalipokuwa yakiingilia. Alifuata njia hiyo na kutokea mtaa wa nyuma ya mgahawa ule, ambako aliita teksi na kujitosa kwenye kiti cha nyuma.
“Wapi bosi?”Dereva aliuliza.
“Kilimanjaro Grand Hyatt hotel, kaka…fasta!” Ngamao alimuangiza dereva na kujiegemeza kwenye kochi kule nyuma.
Gari lilichukua uelekeo alioelekeza kwakuzungukia kule kule mbele ya ile hoteli, na kutokea kwenye dirisha la kiti cha nyuma ndani ya ile teksi, Ngamao alimuona yule trafiki mwendesha pikipiki akiwa ameegesha pikipiki yake kwenye kona iliyokuwa mwisho wa mtaa ule, akitazama kule kwenye ule mgahawa.
Tabasamu baya likaipamba sura yake…
Akiwa mle garini Ngamao Kijambia alimpigia simu GTZ.
“Yule jamaa yako alikuwa ameniwekea watu wa kufuatilia nyendo zangu…” Alimwambia, na GTZ akapayuka kwa kiherehere.
“Hah! Sasa amejuaje kuwa uko hapa? Au ndio aliyesababaisha Candy akatishe ziara kule Tarime?”
“Sijui kwa kweli, ila nimeshawapiga chenga ya mwili…hawawezi kunichezea mchezo ule ule ambao mimi ndio huwa nawachezea mabwege kila siku…” Ngamao alijigamba.
“Ala? Kwa hiyo uko poa? Hakuna kitakachobadilika?” GTZ alisema kwa matumaini.
“Of course niko poa kwa sasa. Lakini naona kwa kasi yao hawa watu wanaoshirikiana na na huyu binti inabidi tuchukue hatua mara moja…bila kuchelewa!”
“Nakubali…na nadhani pia sasa ungewahusisha askari wa hapa jijini Ngamao…ili swala liwe jepesi?”
“No. Kiofisi mimi niko kwenye likizo ya uraufu GTZ. Si unajua nimetoka kufiwa na mama? Sasa nikiwahusisha ni kwamba mimi nikae pembeni, niwaachie wao walishughulikie hili swala. Wanaweza kuleta lelemama hapa muda ukaenda, na binti akapaa. Hii ngoma nataka niicheze mwenyewe mpaka namtia mkononi…”
“Ah, sasa hilo la kuwa uko likizoni halitakuletea matatizo?”
“Halitaweza kwa kuwa tayari mtuhumiwa atakuwa mikononi mwa sheria. Kutokea hapo wakiendelea naye wao ni sawa tu...mimi faraja yangu ni kumtia mbaroni mimi mwenyewe!”
Kimya kilitanda kidogo.
“Okay…so nini kinaendelea sasa?” Hatimaye GTZ aliuliza.
“Hivi tuongeavyo mi ndo naenda kumaliza mchezo sasa…” Ngamao alimjibu huku ile teksi ikimuingiza kwenye wigo wa ile hoteli kubwa ya kitalii ambamo Candy Gamasala alikuwa ndani yake muda ule.
Ilikuwa ni saa kumi na moja na robo za jioni…
***
Inspekta Ngamao Kijambia aliingia kwenye ukumbi wa mapokezi wa hoteli ile .ghali na kupita moja kwa moja hadi kwenye dawati la mapokezi na kumkabili mmoja kati ya mabinti watatu waliokuwa wakifanya kazi ya kupokea wageni wapya na kuwatoa wageni waondokao pale hotelini.
Aliweka kitambulisho chake juu ya ile kaunta mbele ya yule msichana na kujinadi huku akimtazama moja kwa moja machoni yule binti.
“Inspekta Ngamao Kijambia wa kitengo cha makosa ya jinai, jeshi la polisi la Tanzania!”
Binti alishtuka kidogo, kama jinsi ambavyo Ngamao alitaka iwe.
Alikitazama kile kitambulisho kwa muda kikiwa pale pale juu ya kaunta na kuinua macho yake kumtazama Ngamao.
“Ah, okay…ni…nikusaidie nini Inspekta?”
Ngamao akamchanulia tabasamu la kumtoa mashaka, baada ya kuwa tayari ameshamtisha.
“Usiwe na wasi wasi binti…nimekuja hapa kuhusiana na mrembo wetu wa taifa…bi. Candy Gamasala?” Alimwambia huku akikirudisha kwenye mfuko wa ndani wa koti lake kile kitambulisho.
“Ooh! Yaaa…yupo hapa, sasa umekuja hapa kuhusuana naye kivipi?”
“Ah mimi ni afisa niliyepangiwa jukumu la usalama wake kuanzIa hapa mpaka huko Venezuela aendako…nahitaji kuona chumba chake na niongee naye maswala muhimu ya kiusalama, maana anaenda kuliwakilisha taifa huko…yuko chumba namba ngapi?”
Binti akashangaa kidogo.
“Hah!Kwa hiyo kumbe kwenye mambo haya hata mapolisi huwa mnahusuka, eenh?”
“Of course…ni kulinda usalama tu. Si unasikia kwenye vyombo vya habari siku hizi jinsi watu wanavyowatumia ma-miss kupitisha vitu mbali mbali vya haramu kama madawa ya kulevya na kama hivyo?”
“Aaa…ndiyo…”
“Sasa nataka nihakikshe mizigo yake inafungwa kwa usalama na hafanyiwi mchezo wowote mchafu kama huo…ni hilo tu” Ngamao aliongopa bila aibu. Binti akamtajia namba ya chumba cha Candy, kisha akainua simu kutaka kumpigia Candy kule juu ili kumfahamisha kuwa kuna mgeni alikuwa anaelekea kule chumbani kwake.
Ngamao akamshika mkono na kuirudisha ile simu mahala pake.
“Haina haja ya kumpigia…nitaenda tu moja kwa moja…” Alimwambia, na alipona binti anasita, akaendelea, “…ni taratibu za kikazi tu, bibie.” Kisha akamchanulia tabasamu. Binti akatabasamu kwa mashaka na kuiacha ile simu mahala pake.
Ngamao aligeuza na kuiendea lifti iliyokuwa pale kwenye ile sebule kubwa sana ya hoteli ile na kubonyeza kitufe kuiita. Bila ajizi milango ya lifti ikafunguka naye akaijitoma ndani, msisimko wa kumtia Candy mbaroni ukimrudia tena kwa nguvu, kasi na ari mpya.
Lifti ilimshusha ghorofa ya tatu na akaenda moja kwa moja hadi mbele ya mlango wa chumba cha Candy, kwa mujibu alivyoelekezwa na yule binti wa mapokezi. Kishikio cha kufungulia mlango ule kilikuwa kimebadikwa kikadi kilichosomeka “Do Not Disturb.”, ujumbe ule ukimaanisha kuwa aliyemo kwenye chumba kile alikuwa hahitaji kusumbuliwa, bila shaka amelala. Ngamao akaachia tabasamu baya. Aligeuka kulia na kushoto na kuona ile korido ya pale ghorofa ya tatu ikiwa pweke. Alibisha hodu pale mlangoni kwa nguvu, na akashangaa kuona ule mlango ukifunguka taratibu, kwa maana haukuwa umefungwa sawasawa.
Aliguna huku akikunja uso.
“Hodi…! Hodi humu…Candy Gamasala?” Aliita huku akichungulia mle chumbani. Sauti ya luninga ikiongea kwa sauti ya chini ikamfikia, lakini hakuna aliyemuitikia.
Aligeuka tena nyuma na kuona bado korido ilikuwa pweke. Aliusukuma ule mlango na kuingia ndani haraka, na hapo hapo akaushindilia ili ujifunge na kutembeza macho mle ndani.
Chumba kilikuwa kitupu!
Akiwa amehamanika alienda hadi sehemu ya bafu ya chumba kile na kuona kuwa hakukuwa na mtu. Alichanganyikiwa.
Ni kwamba yule dada wa pale mapokezi amenidanganya, hiki si chumba cha Candy?
Aliliendea kabati la nguo lililojengewa kwenye moja ya kuta za chumba kile kwa lengo la kutazama kama kulikuwa kuna mabegi au nguo zozote vitakavyomjuza kuwa kile chumba kilikuwa kimekaliwa na mtu.
Sitaki kuamini kuwa huyu mtoto amenipiga chenga nyingine ya mwili…
Aliwaza kwa wahka huku akilifungua lile kabati.
La haula!
Mlango wa lile kabati ulisukumwa kwa nguvu kutokea ndani na kumbabatiza usoni vibaya. Ukelele wa mshituko ukamtoka wakati akipepesuka nyuma na huku akijaribu kupeleka mkono wake kiunoni kuchomoa bastola yake.
Mtu mrefu alitoka mle kabatini akiwa amemnyooshea bastola na usoni akiwa amevaa kofia maalum ya soksi, iliyofunika kichwa chake chote hadi uso, na kuacha matundu ya sehemu za macho tu.
E bwana we!
Ngamao hakuuweka.
Aliiona ile hali huku akipepesuka kimgongo-mgongo na yule jamaa mwenye bastola akimfuata kwa kasi. Haraka sana akaacha kujaribu kutoa bastola yake iliyokuwa kiunoni na akaweka mikono yake yote miwili sakafuni na kujitupa wima. Wakati huo huo mvamizi wake alikuwa akimwendea kwa kasi, na hivyo wakapamiana vifuani, mkono wa Ngamao ukienda moja kwa moja na kumdaka adui yake ule mkono wake ulioshika bastola.
Jamaa akamtosa bichwa la uso, lakini Ngamao naye akashtukia mapema kitendo kile na hivyo akawahi kuinamisha kichwa chake na wakaishia kugongana vichwa vyao utosini kama makondoo yapambanavyo.
Ngamao akaibuka na sumbwi zito la kutokea chini lililotua sawia chini ya kidevu cha adui yake, ambaye aligumia kwa uchungu na kidogo akalegeza mkono ulioshika ile bastola. Akiwa amepata imani kuwa atampora ile bastola,Ngamao akajigeuza haraka huku akipeleka mkono wake wa pili kuishika ile bastola.
Kosa.
Jamaa akajivuta nyuma kwa nguvu na kumchota ngwara kali sana na Ngamao akaenda chini mzima mzima, ilhali bado akiwa ameung’ang’ania ule mkono wa adui yake wenye bastola. Jamaa aliachia ukelele wa maumivu pale mkono wake ulipopindwa vibaya wakati Ngamao akianguka huku ameung’ang’ania.
Akaachia bastola bila kupenda.
Na wakati huo huo Ngamao naye akawa amepoteza mshiko wake kwenye ule mkono hivyo akajibwaga chini ilhali ile bastola ikianguka kwenye zulia zito la mle ndani.
Bila ya kusema neno jamaa alimfuata pale chini na kumshindilia teke zito la mbavu, na Ngamao akaguna kwa maumivu huku akibiringika pale chini.
Jamaa akamfuata tena na kumtupia teke la pili, lakini Ngamao akamuinulia mguu wake na kuzuia pigo lile kwa soli ya kiatu chake, soli ile ikikutana na ugoko wa yule mvamizi, ambaye aliyumba na kupoteza uelekeo.
Ngamao akajizungusha haraka sana pale chini na kujitupa wima huku akipeleka mkono wake kiunoni kutaka kuchomoa bastola yake, lakini jamaa akaenda hewani mzima mzima na kumshindilia soli ya kiatu kifuani.
Upepo ulimtoka Ngamao na kubabatizwa ukutani, naye hapo hapo akajisukuma mbele akitumia ule ukuta kujipiga jeki, akienda hewani mzima mzima na kumbebesha jamaa bichwa la uso. Jamaa akalia kama nguruwe, huku akitupwa nyuma na kujipamia kwenye kochi lililokuwa pale chumbani kabla ya kusambaratika nalo mzima mzima mpaka chini.
Ngamao akachomoa bastola yake kutoka kiunoni kwake na kumfuata kwa kasi huku akiwa amechukia vibaya sana.
“Simama na mikono yako niione ikiwa juu sana, nyau wewe!” Alifoka huku mishipa ya kichwa ikiwa imemtutumka na pua zikimtanuka.
Jamaa alimsukumia lile kochi na kumkumba nalo, wote wawili wakasambaratika zuliani shaghala baghala, Ngamao akiwa amebanwa na lile kochi kifuani ilhali yule mvamizi akiwa juu ya lile kochi na akipeleka mkono wake kuukamata ule wa Ngamao wenye bastola, na akiukosa.
Ngamao alimsukumia pigo la nguvu kwa mtutu wa ile bastola, lakini hesabu zake hizikuwa sahihi kwani lile pigo halikumfikia adui kutokana na lile kochi lilokuwa baina yao.
Jamaa alijurusha kutoka kwenye lile kochi na kuangukia nyuma ya Ngamao aliyebanwa pale chini na lile kochi. Na hata pale jamaa aliporuka namna ile, Ngamao naye akajikurupusha pale chini akilisukuma pembeni lile kochi na kuanza kumgeukia yule adui yake kutoka kabatini, lakini jamaa alimuwahi na kuukanyaga ule mkono wake uliokuwa umeshika bastola.
“Tulia babu para!” Jamaa alimkoromea huku akiwa amemkanyaga ule mkono wake wenye bastola, na Ngamao akainua macho kumtazama kutokea pale sakafuni alipolala chali na kujikuta akikodolewa na mtutu mwingine wa bastola.
Macho yakamtumbuka zaidi alipouona ule mtutu wa bastola.
“Nini? Ulidhani nilikuwa na ile bastola moja tu?” Jamaa alimkoromoea.
“Ni nani wewe?” Ngamao aliuliza kwa hasira.
“Nilipokwambia tulia nilimaanisha utulize kila kitu chako wewe…hadi hilo domo lako!” Jamaa alimkemea huku akitweta. Akadidimiza zaidi mguu wake pale kwenye mkono wa Ngamao aliokuwa ameukanyaga, na Ngamao akauma meno kwa maumivu na akaiachia ile bastola. Haraka jamaa aliipiga teke ile bastola kutoka pale karibu na mkono wa Ngamao naye akaruka nyuma huku bado akiwa amemuelekezea ile bastola yake iliyofungwa kiwambo cha kuzuia sauti.
“Inuka babu para…tena taratibu mno! Nataka nione kila hatua yako katika hilo…” Alimkemea huku akiwa amemuelekezea ile bastola, akizidi kuisukuma mbali na Ngamao ile bastola aliyompora.
Ngamao aliinuka na kumtazama kwa hasira huku akijichua nyuma ya shingo yake.
“Kaa chini hapo!” Jamaa alimuashiria kwa bastola kuwa akae chini ya kitanda kilichokuwa mle ndani. Ngamao alimtazama kwa hasira.
“Mimi ni afisa wa polisi ujue!” Alimwambia huku akimkata jicho.
“Na mimi ni mtu mwenye bastola mkononi, fala wewe…kaa chini hapo!” Jamaa alimkoromea huku akizidi kumlengeshea ile bastola.
Ngamao akatii.
“Toa pingu hiyo ujifunge mkono wako mmoja hapo kitandani!” Jamaa aliamrisha, na Ngamao akajua kuwa alikuwa amebanwa pabaya. Alimfikiria Candy na moyo ukazidi kumuuma.
“Pingu gani wewe…?”
Jamaa akaikoki ile bastola yake na kumsonya.
“Wacha kucheza na mimi wewe! Najua una pingu hapo. Fanya nikwambiavyo au nitakupa shaba ya mguu sasa hivi hapa!”
Kwa hasira Ngamao akatoa pingu yake aliyokuwa amemuandalia Candy kutoka nyuma ya kiuno chake alipokuwa ameipachika, na kujifunga kwenye mkono wake mmoja.
“Nitakufanya kitu kibaya sana wewe nitakapokutia mikononi nakwambia!” Alimtemea maneno ya hasira yule jamaa.
“Sasa unasubiri lini kunitia mikononi fala wewe? Si mimi hapa nipo hapa? Njoo unitie mikononi basi!” Jamaa alimkoromea.
“Mnhu! Kwa kuwa una bastola, sio?” Ngamao alimwambia kwa uchungu.
“Ndio! Kwa kuwa nina bastola…sasa we’ una tatizo na hilo?”
Ngamao alifunua kinywa lakini hasira zilimzonga akakosa la kusema.
“Jifunge pingu kitandani hapo wewe!” Jamaa alimfokea.
Kwa hasira Ngamao alianza kuufunga ule upande wa pili wa ile pingu kwenye tendegu la kitanda, lakini jamaa akamjia juu.
“Sio hapo wewe fala nini? Jifunge kwa juu huko! Sasa hapo si ukiinua mguu wa kitanda tu unaitoa hiyo pingu?”
Ngamao hakuwa na namna.
Akaibana ile sehemu ya pili ya ile pingu kwenye chuma cha ile sehemu ya kuegemeza kichwa pale kitandani.
“Haya, nini kinafuata sasa?” Alimuuliza kwa hasira yule mvamizi wake.
“Sasa tunasubiri tu mzee…” Jamaa alimjibu huku akiliinua lile kochi na kuliweka sawa.
Ngamao akabaki mdomo wazi.
“Tunasubiri?”
Jamaa akavuta kijimeza kidogo na kukiweka mbele ya lile kochi. Kisha akaenda kuukomea ule mlango wa kile chumba kwa ndani. Akaziokota zile bastola nyingine mbili zilizokuwa mle ndani na kuzishindilia moja kwenye kila mfuko wa suruali yake. Akarudi na kuketi pale kochini huku akipandisha miguu yake juu ya ile stuli.
“Yap, njagu wangu…tunasubiri tu!” Alimjibu huku akijinyoosha pale alipoketi, ile bastola yake akiiweka juu ya mapaja yake.
“Tunasubiri nini wewe? Unajua unamzuia afisa wa jeshi la polisi kufanya kazi yake hapa?” Ngamao alimkemea.
“Yeah…nalijua hilo. Tunasubiri Candy aondoke nchini…hilo ndilo tulisubirialo!”
“Hah! Ina maana yote hii ni kwa ajili ya Candy?”
“Sasa we’ ulidhani ni kwa ajili ya nini? Niambie, ni kwa nini wewe na GTZ mnanfuatilia Candy namna hii eenh? Amekosa nini huyu binti?” Jamaa alimuuliza, na Ngamao hakuamini masikio yake.
Yaani kumbe Candy amekuwa na mtandao mkali namna hii! Hapana shaka huyu ndiye yule jamaa aliyemvunja goti GTZ…sasa na wale askari wa usalama barabarani nao…?
“Sijibu maswali yoyote kutoka kwako mimi!” Ngamao alimjibu kwa kiburi. Jamaa akajitia anapiga mwayo.
“Okay, sio ishu, Barker Haines…wacha nijilaze kidogo hapa…bado tuna masaa mengi tu ya kusibiri kabla Miss Tanzania hajapaa usiku huu…” Alisema kivivu, akimtania kwa jina la muigizaji maarufu wa tamthilia ya huko Afrika Kusini mwenye upara kama yeye..
“Unafanya kosa kubwa sana wewe!” Ngamao alimkoromea.
“Yeah, Barker Haines…mama yangu alikuwa akiniambia hivyo tangu niko shule ya msingi bwana…lakini naona mi’ bado nadunda tu mpaka sasa!”
Ngamao akasonya kwa hasira.
***
Dakika ishirini baadaye simu ya Ngamao ikaita. Jamaa aliruka haraka na kumuwahi pale alipokuwa ameketi na kumnyooshea ile bastola na hapo hapo akimunyooshea mkono wake mwingine kwa ishara ya kumuomba ile simu.
“Toa simu na unipe…kwa upole zaidi!”
Ngamao akatii bila kipingamizi. Jamaa akaipokea na kurudi nayo kwenye kochi, ile simu iliendelea kuita. Akatazama mpigaji na akaona “GTZ” ikionekana kuwa nditye mpigaji wa simu ile.
Jamaa aliipokea na kuiweka sikioni.
“Dah, vipi Ngamao..umekuwa kimya sana…umeshamdhibiti Candy? Maana huku kwenye TV habari zinaoonesha ni kuhusu maandaliza yake tu kwenda huko Venezuela usiku huu…nilitaraji labda saa hizi habari zingekuwa nyingine kuhusu kukamatwa kwake! Niambie kinachoendelea basi mzee, eenh?” GTZ aliongea kwa wahka wa mfululizo simuni.
Jamaa akamcheka, na GTZ akaguna.
“Ngamao?” Aliuliza kwa mashaka.
“Ngamao yuko taabani hapa jamaa yangu…nimempa kifinyo cha haja, hajijui hajitambui!” Alimjiu na kule upande wa pili GTZ akaja juu.
“Hah! WEWE! Haiwezekani…hebu nipe Ngamao niongee naye sasa hivi, alla!” Alifoka na jamaa akakata simu, na kuizima kabisa.
Ngamao alibaki akimtazama kwa ghadhabu kubwa sana.
Lakini hakuwa na la kufanya.
***
Kule Hospitali ya Aga Khan, GTZ alipiga ukelele wa ghadhabu, na moyo ukaanza kumwenda mbio.
Hah! Ngamao kadhibitiwa kweli?
Ina maana yeye na mimi sote tumemshindwa Candy?
Aaaa, hii haiwezekan aisee…haiwezekai kab-saaa!
Alijiwazia kwa ghadhabu.
Alijaribu kujiteremsha kutoka pale kitandani bila ya hata kujua alitaka aende wapi, lakini mguu ukamgomea kabisa.
Akabaki akibubujikwa na machozi ya kukata tamaa.
***
Huku hotelini mlango wa chumba ambamo Ngamao alikuwa amedhibitiwa na jamaa aliyejiziba sura ulibishwa hodi kutokea nje, na wote wawili mle ndani wakamakinika.
Ngamao alimtazama yule jamaa kisha akageukia kule mlangoni, na kumtazama tena yule jamaa.Aliona jamaa alikuwa ameketi tu kitini akitazama kule mlangoni bila ya kufanya bidii ya kwenda kuufungua ule mlango.
“INGIAA...NIKO NDANI HUMU NIMEVAMIWAA!” Ngamao alipiga kelele kuelekea kule mlangoni. Jamaa mwenye bastola alimuashiria kwa mtutu wa bastola yake akae kimya.
Mlango ukabishwa tena.
Mara moja.Kimya.Halafu mara mbili.Kimya.Halafu mara tatu.
“KAITE POLISIII!” Ngamao alibwata kumwambi huyo aliyekuwa akibisha hodi kule nje, wakati yule jamaa akiuendea ule mlango na kuufungua.
Ngamao akawa makini kuona nini kitatokea.
Hakuna aliyeingia.
Jamaa ilikuwakama amechukua kitu fulani kutokakwa yule aliyekuwaakigonga ule mlango, kisha akaufunga tena ule mlango naye akirudi mle ndani.
Ngamao akashangaa.
“Huna adabu wewe…nimekwambia utulize hilo domo lako hukutaka kusikia. Huyo alikuwa mshirika wangu, KTY… na nilikuwa namsubiri aniletee hii!” Jamaa lilimwambia huku likimuoneshea bomba la sindano likiwa na kimiminika ndani yake.
“KTY…?”
“Inamaanisha “Kwa Taarifa Yako”, bwege wewe!”
Macho yakamtoka Ngamao.
“Ni…nini hiyo wewe?” Ngamao alihoji kwa wahka hukuakijaribu kujiinua kutoka pale chini, macho yake yakiwa kwenye lile bomba la sindano lililokuwa mkononi kwa yule jamaa.
“Tulia wewe!” Jamaa alimnyooshea ile bastola huku akimfuata pale alipokuwa.
Macho yalizidi kumtumbuka Ngamao.
“Unataka kunifanya nini wewe, eeenh?” Aliuliza, na bila ya kumjibu, jamaa akamdunga ile sindano kwenye upande wa shingo yake na kushindilia kile kimiminika kilichokuwa ndani ya bomba la ile sindano.
“Aaaarrghhh!” Ngamao alilia kwa taharuki wakati akishindiliwa mwilini kile kimiminika asichokijua.
Alipomaliza jamaa alisimama na kurudi nuyma huku akimtazama, na kwenda kuketi kwenye lile kochi.
“Um…umenitia vitu gani mimi wewe, eeenh?” Ngamao alimuuliza kwa wahka huku akijikukurusha pale alipofungwa, akikisukasuka kile kitanda ghali.
“Usiwe na shaka babu para…nimekuchoma sindano yenye kimiminika cha Rohypnol…unaijua hiyo?” Jamaa alimuuliza na Ngamao akatumbua macho kwa hasira.
“Rohypnol…?” Alimaka kwa woga, macho yake yakimjulisha yule adui yake kuwa alikuwa anafahamu ni kimiminika cha aina gani alichodungwa.
“Yap! Rohypnol kaka…hiyo ni kali kuliko Valium kwa zaidi ya mara kumi, si unajua hiyo?” Jamaa alimjibu na kumuuliza.
Ngamao aliunguruma kwa hasira na kumtukana tusi zito la nguoni, akijikukurusha kwa nguvu kutoka pale alipokuwa amefungwa. Alifanikiwa kusimama na kuishia kubaki akiwa amejipinda mgongo, kwani ile pingu ilimzuia kusimama wima.
Akarudi chini kwa kukata tamaa.
“Unaifahamu Rohypnol, eenh? Good. Kwa hiyo utakuwa unajua kuwa hiyo itakulaza kwa zaidi ya saa kumi, ikiwa inaongezeka uwezo wake wa kukulevya kadiri saa zinavyosogea…ndani ya dakika kumi tu…no…” Aliangalia saa yake, “…dakika nane tu kutoka sasa utaanza kulala hapo upara wangu…na utazidi kutopea kwenye usingizi mzito kadiri saa zinavyozidi kusonga, muda utakapoamka tayari Candy atakuwa ameshapasua anga mzee…hapo vipi?”
“Ah, we’ hujui umm…mefanya nin..nini!” Ngamao alimwambia, akianza kuuhisi mdomo ukimuwia mzito.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Oh, nimesahau…hutamaliza dakika kumi wewe, maana kiwango nilichokuwekea kimezidi kidoogo kile cha kawaida...nadhani utazimika ndani ya dakika tano tu wewe!” Jamaa alimwambia.
“Candy! Ni mttt…toto mbbbb…bhhayyya!” Ngamao alimwambia kwa taabu.
Jamaa akamakinika.
“Candy mtoto mbaya? Kivipi…niambie fasta basi!”
“Ni mto ttt...mu…mu…muuuuuu……rrrghhhkhkkkkhhhhhhhhh!” Jamaa akaangusha kichwa chake upande na kutekwa ka usingizi mzito wa madawa.
“Shit, Ngamao! Sasa mbona hukusema yote hayo kabla wewe?” Morandi Gwaza alimuuliza yule bwana aliyetopewa usingizi mzito huku akiitoa ile kofia aliyokuwa ameivaa kichwani kwake muda wote alipokuwa mle ndani.
Haraka alimuinua na kumlaza pale kitandani, kisha akatumia muda wa kutosha kufuta sehemu zote alizohisi kuwa alizishika kwa mikono yake, halafu akaiweka mfukoni ile kofia yake ya soksi nakutoka je ya chumba kile.
Kibao cha “Do Not Disturb” bado kilikuwakikining’inia nje ya mlango ule...
***
Kiasi cha kama dakika ishirini na tano kabla Ngamao hajaingia kwenye lile eneo la mapokezi la ile hoteli kwa lengo la kwenda kumuweka Candy chini ya ulinzi, Kokos Wandiba aliingia chumbani kwa Candy na Bishkuku na kuwaambia kuwa walihitajikakuhama kile chumba haraka sana.
“Kwa nini Kokos, na sie tunapumzika saa hizi?” Candy alihoji.
“Nimepata habari kuwa kuna kamera za paparazzi zimetegeshwa humu…wakichukua picha mbali mbali za Candy kwa ajili ya kuuza magazetini na mitandaoni…bila ya ridhaa yake…” Kokos alitekeleza uongo aliotumwa na Morandi.
“Haaah!Ni nani huyo mwana izaya naye?” Bishkuku alimaka huku akiangaza macho huku na huko mle ndani, na Candy akajikuta akifumbata mikono yake kifuani kama kwamba ndio anajiziba hizo kamera za paparazzi zisimuone.
“Sio la msingi kwa sasa…hebu tutokeni humu jamani. Nitaleta watu wa kukichunguza chumba kwa makini, kisha mkipenda mtarudi tena kujipimzisha humu…” Kokos aliwaambia.
“Nani? Miye tena? Hata harudi mtu humu…!” Candy alisema kwa hasira.
Hivyo wakahamia kwenye chumba cha Kokos pale pale hotelini, kilichokuwa ubavuni tu mwa kile cha Candy na Bishkuku.
Huku nyuma, Morandi akaingia mle ndani kwa Candy na kuuacha mlango ukiwa wazi kidogo, kisha akaingia kabatini kumsubiri Ngamao.
Wakati Ngamao anaingia kwenye lifti kuelekea kule ghorofani, Nuru aliyekuwa ameketi kwenye moja ya masofa maridhawa pale mapokezi, alimpigia simu Morandi aliyekuwa tayari ameshajichimbia kabatini.
“Jamaa ndio ameingia kwenye lifti kuja huko juu!” Alimwambia baada ya Morandi kupokea simu yake.
“Roger that, Kisura!” Morandi alimjibu na hapo hapo akaizima ile simu.
Huku chini, Nuru alitoka nje ya hoteli ile na kwenda kuparamia pikipiki ya Morandi kuelekea mahala ambako Morandi alimuelekeza kwenda kuchukua kile kimiminika cha usingizi, na amletee pale chumbani kwa Candy pindi atakaporejea.
Kule juu, Morandi alijiweka sawa ndani ya lile kabati, tayari kukabiliana na Ngamao pindi atakapofika mle ndani…
***
Usiku wa manane siku ile, Candy Gamasala, Bishkuku, na Kokos, waliungana na watendaji muhimu wa kamati ya Miss Tanzania na kupanda ndege kuelekea Venezuela, ambako mrembo yule wa taifa alikwenda kuanza kutupa karata zake za mwanzo katika harakati za kuleta taji la urembo wa dunia nchini.
Kinyume na matarajio ya wengi, Candy Gamasala alifanya maajabu makubwa sana kule Venezuela, kwani wiki moja tu baada ya Candy kuondoka nchini kwenda Venezuela, dunia ilihabarishwa kuwa katika warembo ishirini na tano waliopita robo fainali ya kinyang’anyiro cha taji la mrembo wa dunia, alikuwemo mrembo kutoka Tanzania, Candy Gamasala.
Lakini kabla ya taarifa hizi kutoka Venezuela kulifikia taifa na ulimwengu, mengi yalikuwa yameshatokea huku nyumbani…
***
Nusu saa baada ya ndege ya Candy kupasua anga kuelekea Venezuela usiku ule wa manane, bibi wa kisomali aliyejitanda mabaibui aliingia kwenye eneo la mapokezi la ile hoteli ghali ya Kilimanjaro Grand Hyatt na kujisali kwa ajili ya malazi ya siku moja, yeye na mumewe mlemavu wa miguu.
Binti wa mapokezi alimtazama yule mama wa kisomali aliyejioleza wanja na poda za usiku, kisha akamtazama huyo mumewe aliyekuwa amejibweteka kwenye kiti maalum cha matairi kilichokuwa hatua chache nyuma ya yule mama, kikiwa kimeelekea kule kwenye lifti ya pale hotelini.
“Er, sasa kwa hali hiyo itabidi tuwapatie vyumba vya ghorofa ya chini bibie…” Mwanadada wa mapokezi alimwambia kwa kimombo.
“Oh, Hapana. Mume wangu ye’ hupenda kukaa juu kwenye veranda atazame nje, so tungefurahi kupata chumba japo ghorofa ya kwanza tu na kiwe na dirisha linaloekekea upande wa bahari tafadhali!” Msomali alimjibu kwa kimombo kilichonyooka, na mwanadada wa mapokezi akatekeleza.
Alipewa kadi yake ya kufungulia chumba chake kwenye hiyo ghorofa ya kwanza, naye akamsukuma mumewe aliyekuwa amejiegemeza kwenye kile kiti maalum cha matairi akiwa amejifunika mablanketi na kichwani akiwa amejifunga kilemba kama jinsi wanaume wa kisomali wapendavyo kujifunga, kuelekea kwenye lifti.
Mhudumu wa pale hotelini alimshikia mlango wa lifti wakati yule mama wa kisomali akikisukuma kile kiti ndani ya lifti na kujifungia.
Alipitiliza na ile lifti hadi ghorofa ya tatu, ambako alikisukuma kile kiti hadi kwenye mlango wa chumba kimoja pale ghorofa ya tatu, kikiwa na kibango kilichozuia watu kumsumbua mkaazi wa chumba kile.
Bila ya wasi wasi aliufungua ule mlango kwa kutumia kadi maalum ya kufungulia mlango ule aliyokuwa nayo tangu awali, na kukisukuma ndani ya kile chumba kile kiti kikiwa na mumewe juu yake.
Ndani ya chumba aliubana mlango, na hapo yule mumewe alitupa pembeni yale mablanketi aliyokuwa amejifunika na kusimama wima mbele ya kile kiti, akijitandua kile kilemba alichokuwa amejifunga kchwani.
“Okay, tufanye haraka tumalize huu mchezo hapa, kisha tutawanyike kisura, sawa?” Morandi alisema huku akikiendea kitanda kilichokuwa mle ndani, Ngamao Kijambia akiwa amelala fofofo juu yake.
“Okay, Mo…” Nuru aliyekuwa katika mavazi ya kisomali, wigi lake la nywele za kisomali zikichungulia ukingoni mwa mtandio aliojitanda, alisema.
Haraka Morandi alimfungua ile pingu Ngamao na kuiweka mfukoni mwake, kisha akamuinua kutoka pale kitandani na Nuru akasukuma kile kiti hadi pale kitandani.
Wakasaidiana kumketisha pale kitini ihali mwenyewe akiendelea kukoroma na kupangilia njozi tu usingizini. Walimfunika yale mablanketi na Morandi akamfunga kile kilemba kama jinsi yeye alivyokuwa amejifunga wakati akiletwa pale hotelini na Nuru.
“Okay, sasa kama tulivyopanga kisura. Mi’ n’tatangulia kule mapokezi, na wewe utashuka naye na kutoka nje. Wakikuuliza utawaambia mnapunga hewa ya usiku…ni jambo la kwaida sana kwa mahoteli makubwa kama hii okay?”
“Poa.”
“Good. Hatutaki kukipambazuka wafagiaji wakute jitu limelala likiwa limefungwa pingu kwenye chumba ambacho awali kilisajiliwa kwa Miss Tanzania…italeta mashaka makubwa sana kwa mrembo wa Kokos!” Morandi alisema na Nuru akaguna.
“Ni mrembi wa taifa yule Mo, sio wa Kokos, vipi wewe?”
Morandi akaguna.
“Tayari?” Aliuliza, na Nuru aliyejifanya bibi wa kisomali akamtikisia kichwa kukiri kuwa alikuwa tayari.
Morandi akajitahidi kufuta kwa kitambaa chake sehemu ambazo alihisi kuwa walikuwa wamezishika wakiwa mle ndani, kisha akatoka nje ya chumba kile.
Kule mapokezi aliangaza huku na huko eneo lile. Kulikuwa kuna watu wachache sana usiku ule, na pale mapokezi alibaki binti mmoja tu. Alitoka nje na kubaki akiwa amesimama akitupatupa miguu kama mtu anayejaribu kupitisha usiku baada ya kukosa usingizi usiku ule.
Dakika chache baadaye Nuru akiwa kama mwanamama wa kisomali alitoka akikisukuma kile kiti, Ngamao aliyefanywa aonekane kama mume mlemavu aliyejifunika mablanketi akiwa amejibweteka kwenye kiti kile.
Mara moja mhudumu wa pale hotelini alifika na kutaka kumsaidia, lakini haraka Morandi akawahi huku akimuashiria yule mhudumu atulie tu, naye akamnyanyua Ngamao kwa taabu kidogo na kumketisha kwenye kiti cha abiria kwenye gari la kukodi aina ya Noah, ambalo walilikodi kule kule uwanja wa ndege baada ya kuhakikisha kuwa Candy na akina Kokos wamepaa bila kituko chochote kuwatokea.
Nuru alizunguka ubavuni kwa lile gari na kukiweka kile kiti cha matairi ndani ya gari, na akajitia kutaka kumpa hela Morandi kwa kumsaidia kumbeba “mumewe”.
Morandi akamtikisia kichwa huku akiashiria kwa mkono wake kuwa hakuwa akihitaji ile hela. Nuru msomali alizidi kumpa huku akimsemesha kwa kizungu, na Moradi akamuoneshea yule mhudumu wa hoteli ambaye alibaki akiwa ameduwaa, kisha Morandi akapokea ile elfu tano aliyokuwa amepewa na yule “bibi wa kisomali” na kumpa yule mhudumu.
“Ah, hii ilikuwa halali yako kamanda kama nisingekuzuia kwenda kumsaidia yule horiya…” Alimwambia.
“Dah! Kweli wangu…ahsante sana mzee!” Mhudumu alimshukuru huku akiipokea ile hela wakati lile gari la kukodi likiondoka eneo lile, Nuru akiwa nyuma ya usukani, Ngamao akiwa amejibweteka kizembe ndani ya usingizi wa madawa.
“Usijali mzee…” Morandi alimjibu yule mhudumu huku akilitazama lile gari likitokomea nje ya wigo wa hoteli ile.
Aliendelea kuzubaa pale nje kwa muda, na yule mhudumu akarudi ndani ya ile hoteli. Morandi aliiendea haraka pikipiki yake na kuiondoa taratibu nje ya wigo wa hoteli ile, na alipofika barabarani, akaongeza kasi kuwahi eneo ambalo alijua kuwa Nuru alikuwa anampeleka Ngamao…
***
Asubuhi ya siku ya pili manesi wa pale Aga Khan hospital walishangaa kuona mgonjwa akiwa ameachwa pale hospitali akiwa kwenye usingizi mzito, bila ya uangalizi wowote, kiti cha matairi alichokuwa amekalia kikiwakimebanishwa kwenye kona pweke kabisa katika moja ya korido za hospitali ile.
Haikuwa mpaka saa sitamchana ndipo Ngamao Kijambia alipofumbua macho na kubaki akiwa amebutwaika alipojikuta akiwa amelazwa pale hospitali ya Aga Khan, na mwanadada mmoja akiwa ameketi kando ya kitanda chake ndani ya moja ya wodi za ile hospitali.
“Uunnhhh! Aam…nik…niko wapi hapa?” Aliuliza kwa taabu huku akifinya macho kumtazama vizuri yule dada.
“Uko hospitali ya Aga Khan, Inspekta!” Dada alimjibu.
Kichwa kilimuwanga Ngamao.
“Inspekta? Unajua kuwa mimi ni afisa wa polisi?” Aliuliza.
“Yah, najua hilo…”
“Na unalijuaje hilo…wewe ni nani?”
“Mimi ni Konstebo Happiness Daniel wa polisi kituo cha kati jijini. Tulipigiwa simu na uongozi wa hii hospitali kuwa kuna askari wa jeshi la polisi amekutwa tu hapa hospitali akiwa ameleweshwa kwa madawa…er, walikuta kitambulisho chako kwenye nguo zako!” Konstebo Happiness alimwambia, na Ngamao akauma meno kwa hasira.
Ah, hii picha imeshaungua sasa!
Alijkuta akimchukia vibaya sana yule mtu aliyemtia aibu ile.
“Sasa nilikuwa nimepewa jukumu la kukaa nawe mpaka upate fahamu, kisha wakubwa wenzio ndio watakuja kuongea nawe!” Yule konstebo alimwambia
“Shit!” Ngamao alilaani, kisha akahoji uhalali wa yule mwanadada kuwa pale kwa kuwa hakuwa kwenye mavazi ya kiaskari, na yule konstebo akamuonesha kitambulisho chake. Hakuwa na la kusema zaidi, akabaki akiwa amelala tu kitandani akiumia moyo kwa yale aliyotendewa na yule jamaa aliyejiziba sura.
Nusu saa baadaye uvumilivu ukamshinda na alijiinua kutoka pale kitandani huku akijinyofoa ile mirija ya dripu aliyokuwa amewekewa.
“Oi! Vipi pale Inspekta, nhe! Unafanya nini sasa…?” Konstebo Happy alimuuliza huku akiwa ametumbua macho.
“Naondoka! Unafikiri nafanyaje…siwezi kulala tu hapa!” Ngamao aliunguruma, na hapo akajiona kuwa alikuwa amevikwa mapajama maalum ya hospitali.
“Nguo zangu wapi? Na kitambulisho changu…? Silaha yang…?” Alizidi kumvurumishia maswali yule konstebo, lakini hapo akaganda, akikumbuka kuwa lile jamaa lilimpokonya bastola yake. Akakunja uso.
“Silaha afande? Ulikuwa na silaha…? Hukukutwa na silaha yoyote hapa! Umeipoteza?” Konstebo alimtolea macho kwa mshangao na kushutumu.
“Nguo zangu na kitambulisho wapi konstebo? Una mamlaka ya kunihoji mimi wewe?” Ngamao alimkoromea.
“Kitambulisho kiko ofisini…mkuu wa kituo anacho. Si nimekwambia kuwa wakubwa wanataka kuongea nawe pindi uamkapo?” Konstebo alimjibu.
Ngamao alitembeza macho mle ndani akili ikimzunguka.
Moyoni akamtukania mama yake yule jamaa aliyempiga pingu kule hotelini usiku uliopita na kumdunga sindano yenye madawa ya kulevya.
Kaniharibia pozi vibaya sana kenge yule…na nikimjua!!
Kwenye ukuta mmoja wa wodi ile waliyokuwamo kulikuwa kuna kabati la nguo. Aliinuka na kuliendea huku akihisi kama kwamba miguu na maungo yake vyote vilikuwa vimeingia kutu.
“Hey, afande! Hutakiwi kutoka humu wewe, vipi?” Konstebo Happy alimkemea.
“Jaribu kunizuia basi uone!” Ngamao alimkoromea huku akilifungua lile kabati na kutoa nguo zake kutoka ndani yake.Akaanza kubadili nguo pale pale na yule afande mwanadada akimkodolea macho.
“Khah! Inspekta hivi uko sawasawa lakini wewe?” Konstebo Happy alimhoji.
“Unataka tupande hapo kitandani tuhakikishe?” Ngamao alimkoromea kwa kisirani huku akivaa suruali, na yule askari wa kike akatumbua macho na kutikisa kichwa kwa kutoamini.
Alitoa simu yake na kumpigia mkuu wake wa kazi.
“Jamani huyu baba huku kaamka na sasa anataka kuondoka kinguvu!” Alimaka simuni, kisha akasikiliza majibu ua mswali ya upande wa pili,
“Si huyu inspekta Kijambo sijui huyu?” Aliendelea kupayuka simuni, na Ngamao akarudi pale kitandani na kuvuta viatu vyake kutoka chini ya uvungu wa kile kitanda.
“Kijambia wewe! Kijambo ndio kitu gani? Waambie n’takwenda mwenyewe kituoni kufuata kitambulisho changu!” Ngamao alimkoromea kwa nongwa.
“Akh, ‘asa mi’ n’tamzuiaje afande? Halafu kumbe alikuwa na silaha… kaipoteza!” Happiness alizidi kumchongea kwa wakuu wake.
Ngamao alimaliza kuvaa viatu vyake na kuuendea mlango.
“Sasa nd’o nakwambia afande! Silaha kapoteza na ndio anatoka hivyo huyu…s’jui anaenda wapi!” Konstebo Happiness alizidi kuchonga simuni, na Ngamao akatoka nje ya wodi ile. Yule konstebo akamkimbilia.
“Unapoenda na mi’ nipo afande! Siwezi kupewa onyo kwa kutorokwa na mtuhumiwa mimi!” Alimwambia wa kiburi huku akitembea ubavuni mwake, na Ngamao akasimama,akamgeukia kwa hasira.
“Mi mtuhumiwa?”
Happy akagwaya.
“Ulikuwa chini ya uangalizi wangu afande…kwa hiyo nina wajibu wa kuhakikisha kuwa hupotei machoni mwangu mpaka nikukabidhi kwa wakubwa wenzako….samahani sana afande!” Konstebo Happy alimwambia kwa msisitizo.
Ngamao akazungusha macho kwa kukereka, kisha akatupa mikono hewani kwa kuchanganyikiwa.
Akageuka na kuelekea kwenye sehemu ya maegesho, na hapo akavutwa mkono. Aligeuka kwa hasira akiwa ameinua mkono kwa namna ya kumzaba kofi yule konstebo.
Na akashangaa kuona kuwa ni nesi ndiye aliyemshika mkono na si yule askari wa kike.
“Heh, mbona unaondoka kienyeji tu bila ruhusa ya daktari, babu?” Nesi alimuuliza, na Ngamao akashusha pumzi za hamaki.
“Hivi nyie akina mama hamna mabwana huko mtokako? Mbona mnanipapatikia hivi lakini? Mi’ naondoka, sihitaji ruhusa ya mtu yeyote!” Alifoka na yule nesi akashangaa pasina kiwango. Akamgeukia Happy kwa mshangao.
“Nampapatikia mimi huyu?” Aliuliza kwa hamaniko na kutoelewa.
Happy akambetulia mabega tu.
Nesi akageuka na kuondoka kwa hasira.
“One down, one to go, pumbavu zenu!” Ngamao alisema kwa hasira.
“Afande mi’ huniondoi kirahisi…kazi yangu iko mashakani. Kwa nini tusiende kituoni tu kwanza basi?” Konstebo Happy alimwambia.
Ngamao alimtazama kwa hasira.
“Okay…twende!” Alimwambia kwa kisirani.
Pale alipokuwa akimtazama yule konstebo kwa hasira kabla ya kumkubalia kwenda naye kituo cha polisi, mawazo mengi yalimpitia kichwani haraka haraka Ngamao. Na walipokuwa njiani kuelekea huko kituoni alipata muda wa kuutafakari vizuri zaidi mustakbali wake.
Yule jamaa aliyejiziba sura alikuwa ameshamharibia mpango wake wote. Candy bila shaka atakuwa ameshapaa kwenda huko Venezuela muda ule, na yeye mpango wake wa awali ulikuwa ni kumdhibiti Candy kabla hajaenda huko ughaibuni. Na kwa kuwa sasa ameondoka ilikuwa wazi kabisa kuwa alihitaji kubadili mkakati.
Lakini achukue mkakati gani?
Wazo la kwanza lililomjia kichwani ni kwamba kwa kuwa Candy ameshaenda, hakuwa na namna zaidi ya kumsubiri arudi tu, kwani alikuwa na hakika kwamba atakuwa ameenda kusindikiza tu huko mashindanoni, hivyo angeaga mashindano mapema tu.
Sasa swala la wale wakuu wa yule konstebo kuchukua kitambulisho chake lilimfanya akose namna zaidi ya kwenda kuonana nao tu.
Iwe wakati ule au baadaye haikujalisha…ilibidi akaonane nao tu.
Alikuwa amenuna njia nzima wakiwa kwenye teksi kuelekea kituo cha polisi makao makuu jijini.
Hasira zake dhidi ya yule jamaa aliyemtaiti kule hotelini zilizidi kumkaba.
Walifika makao makuu ya polisi na Ngamao akakutana na mkuu wa utawala katika jeshi lile.
“Vipi Inspekta…ni nini kilichokutokea? Dar ni mbali sana na Mwanza. Inakuwaje uko huku na inakuwaje umekutwa katika mazingira kama hayo uliyokutwa nayo?” Aliulizwa, na Ngamao alikuwa ameshajiandaa.
“Afande, kuna mtuhumiwa nilikuwa nikimfuatilia kwa muda mrefu sana kule Mwanza na ambaye nilipata taarifa za ki-intelijensia kuwa yuko hapa Dar…nikaja kujaribu kuhakikisha hilo…” Alijibu.
“Mkuu wako huko Mwanza hana taarifa hizo, tumeongea naye mara tulipopata habari zako!” Mkuu wa utawala mwenye cheo cha mrakibu mwandamizi alimwambia.
“Na bila shaka atakuwa amekwambia kuwa niko kwenye likizo ya uraufu afande?” Ngamao alimuuliza, na mkuu wake akaafiki.
“Ndio maana sikutaka kuja hapa kuliwasilisha hili swala kwa kuwa niko likizo, lakini kama ningejihakikishia kuwa mtu nimtakaye haswa ndiye huyu niliyemkuta hapa, basi ningekuja tu hapa makao makuu kutoa taarifa ili sheria ichukue mkondo wake afande!” Ngamao alijitetea.
“Hilo ni kinyume cha taratibu Inspekta! Ulitakiwa uanzie hapa na kueleza hali halisi kabla ya kwenda huko peke yako!” Mrakibu Mwandamizi alimfokea, na Ngamao akapiga kimya.
“Halafu nasikia umepoteza silaha…unajua huo ni uzembe wa hali ya juu Inspekta?”
Ngamao alighadhibika.
Akainua uso na kumtazama yule mtawala, kisha akapitisha uamuzi.
Akamueleza kila kitu tangu alipoingia kwenye ile hoteli ya kitalii ya Kilimanjaro Grand Hyatt, hadi pale alipojikuta kule hospitali ya Aga Khan. Kitu pekee alichoficha ni uhusika wa GTZ katika kadhia ile.
“Sasa utaona afande, kuwa kupoteza kwangu silaha kulikuwa nje ya uwezo wangu kwa wakati ule…nilichomwa sindano ya usingizi…” Alisema baada ya kumaliza kutoa maelezo yake, na yule mkuu wa utawala katika jeshi la polisi akachoka.
“Okay…sasa umeeleza yote haya, ukisema kuwa mtuhumiwa uliyekuwa ukimfuatilia…mtuhumiwa uliyekuwa ukimfuatilia…lakini hujamtaja mtuhumiwa mwenyewe…ni nani yeye?” Mkuu wake alimuuliza, na hapa ndipo Ngamao alipokuwa anapataka ili kutekeleza mkakati wake mpya dhidi ya Candy…
***
Asubuhi ile ile, kabla Ngamao hajaamka kule Aga Khan, Morandi Gwaza alifumbua macho kutoka kwenye usingizi mzito na kupiga mwayo. Aliinamisha kichwa na kumtazama Nuru aliyekuwa anatoa mikoromo hafifu huku akiwa amemlalia kifuani.
Alitabasamu, kisha akamsogeza pembeni taratibu na kumlaza pembeni, naye akainuka kutoka pale kitandani.
“Awww come on, Mo…! Leta chesti hilo nililalie bhana, aanh!” Nuru alinung’unika kwa deko na Morandi akamcheka.
“Kumekucha tena kisura…muda wa kazi huu!” Mo alimwambia huku akiketi kwenye kochi lililokuwa mle chumbani, nyumbani kwa Bishkuku.
Nuru akainuka na kuketi kitandani kivivu.
“Ah, kazi gani tena wakati Candy keshaondoka bhana? Mi’ n’lijua hapa sasa ni kula bata tu mpaka atakaporudi?” Nuru alinung’unika tena huku akijiziba mwayo.
“No way bi mdogo…sasa ndio wakati wa kumfuatilia yule fala mwingine yule…” Morandi alimrekebisha.
“Yupi tena? Yaani Mo kwa kupenda kujipa mashughuli weye!” Nuru alimjibu huku akiinuka kutoka pale kitandani na kwenda kumkalia mapajani pale kwenye kochi.
Morandi akamcheka.
“Usiniambie kuwa umemsahau yule jamaa aliyekuzaba makofi kule mlimani city…!” Alimwambia, na Nuru akaganda, uso wake ukiingia ubaridi.
Akasonya na kuinuka kutoka pale mapajani kwake.
“Sio makofi…kofi! Moja tu! Na pia kumbuka kuwa na mi’ nilimpa madochi mpaka akatoka mbio kule Mikumi yule…!” Alimjibu kwa kisirani.
“Good!”
“Good? Good kivipi sasa, Mo?”
“Good kwamba umemkumbuka…sasa tunaanza kumfuatilia yeye mrembo. Nataka Kokos na mrembo wake wakirudi bongo tuwe tumeshampata yule fala…!” Morandialisema, na Nuru akaachiatabasamu.
“Okay…twende kazi!”
Dakika ishirini baadaye, wakiwa wameshaoga, walitoka na kwenda kupata kiamsha kinywa kwenye mgahawa wa jirani na pale walipokuwa wakiendelea kupafanya kuwa ni makazi yao ya muda. Wakiwa mgahawani walipata fursa ya kujadili lile swala lililokuwa mbele yao.
“Sasa yule jamaa atakuwa wapi unadhani Mo…maana tangu zile songombingo za kule Mlimani City siku ile ametoweka kabisa!” Nuru alisema, na Morandi akaguna.
“Yule alikimbia kwa sababu alitaka atoweke Nuru, angetaka tuendelee kumuona asingekimbia…” Morandi alimjibu huku akimcheka.
“Ah, sawa bwana. Ila mi’ sifanyi masihara ujue…”
“Najua, ila uliuliza swali linaloshawishi jibu kama nililokupa…anyway, mi’ nilishaanza kulifanyia kazi swala lake, na nikaamua kuliacha kwa muda wakati tunafuatilia uondokaji salama wa mrembo wa Kokos hapa nchini. Madhali sasa ameshaondoka, tunaweza kurudi kumshughulikia yule jamaa mchapa makofi watoto wa kike!” Morandi alisema, na Nuru akaguna.
“Umelifanyia kazi kivipi? Na lini?”
“Ah, we’ elewa tu kuwa nimelifanyia kazi. Kuna askari mmoja mwenye akili ambaye nilimpa hiyo kazi…nadhani sasa tunaweza kulifuatilia kutoka kwake…” Morandi alimwambia.
“Ni nani huyo, Mo…na unamuamini?” Nuru alimuuliza kwa mashaka.
“Ah! Unadhani nitamhusisha mtu mjinga-mjinga tu kwenye hili? Of course namuamini!”Alimjibu.
Waliporudi nyumbani kwa Bishkuku baada ya kupata kiamsha kinywa, Morandi alimpigia simu huyo jamaa yake, miongoni mwa askari wenzake ambao bado alikuwa na mahusiano mazuri nao.
“Hey Eddy…mambo vipi? Ulifanikiwa kupata taarifa zozote kuhusu zile alama za vidole nilizokutumia kaka? Nilikwambia zifanyie kazi halafu utulie nazo tu mpaka nitakapo kupigia mwenyewe…” Aliongea simuni huku Nuru akifuatilia kwa makini mazumgumzo yake.
Morandi alimsikiliza kwa muda yule mtu aliyempigia ile simu, kisha akauliza, “Una hakika?” Uso wake ulionekana kushangazwa na alichokuwa akielezwa.
Akasikiliza tena kwenye ile simu.
“Okay…sasa ina maana ndio basi tena, au?” Aliuliza na Nuru akafa moyo. Morandi alisikiliza tena kwa muda, kisha akaagana na jamaa yake, akakata simu.
“Imekuwaje? Nahisi ni ziro tu!” Nuru alimwambia.
“Yes…and no!” Morandi alimjibu huku akiwa amekunja uso kwa tafakuri.
“Una maanisha nini, yes and no?”
“Hakuna kitu kwa sasa. Jamaa hajaweza kumtambua mtu mwenye zile alama za vidole…”
“Kwa hiyo ndio “yes” hiyo…kwamba hamna kitu. Haya hiyo “no” nayo inaingilia wapi?” Nuru alizidi kuhoji.
Morandi alikuwa amekunja uso kwa mawazo, kisha akaguna.
“Yaani jamaa amefanikiwa kuona kuwa kuna rekodi ya zile alama za vidole nilizomtumia kwenye mfumo wa kumbukumbu za kompyuta za jeshi la polisi, na akaona kuwa ni kweli rekodi ya alama zile imeingia kwenye kumbukumbu za jeshi la polisi baada ya mimi kuwa nimeshatoka jeshini…”
“Sasa kilichomshida kukutajia muhusika wa alama hizo ni kipi?” Nuru alisaili.
Morandi akaguna tena.
“Utambulisho wa muhusika wa zile alama za vidole umefichwa, na hautatolewa mpaka aingize neno maalum la siri, yaani “password”, ndio taarifa zaidi juu ya jinai inayohusika na mmiliki wa zile alama za vidole zipatikane. Akakwama!”
“Duh! Hiyo mbona mpya? Huwa inakuwa hivyo kweli?” Nuru alizidi kushangaa.
“Yap, lakini kwa kesi chache sana…hususan za kiusalama wa hali ya juu kitaifa. Hii inazidi kuniumiza kichwa…Candy alifanya nini huko nyuma? Kwa nini mtu kama huyo awe anamfuatilia yeye? Na kwa nini Ngamao pia awe anamfuatilia… na wakati huohuo, bwege GTZ nalo liwe linamfuatilia?” Morandi alisema kwa hisia kali.
Nuru alipiga kimya, hakika naye aliuona ugumu wa hali ile kwa Candy.
“Dah! Sasa hiyo password ya kuzifungua taarifa za hiyo kesi inayohusiana na yule jamaa mwenye zile alama za vidole inapatikana wapi?”
“Kwa afisa aliyekabidhiwa kesi inayomhusu huyo jamaa sasa!”
“Ambaye ni nani?”
“Jamaa hamjui! Ndio anajaribu kulifanyia kazi…akimjua atanijuza!”
Walitazamana.
“Bila shaka huyo atakuwa Ngamao sasa, Mo!” Nuru alisema.
“Ambaye anashirikiana na GTZ katika kumsaka Candy? Hainiingii akilini kisura!” Morandi alitia shaka.
Kimya kingine kikatanda mle ndani.
“Hii ni mbaya sana Mo…mbaya sana!” HatimayeNuru alisema.
“Umeona eenh?” Morandi alishadidia.
“Yap! Nimeona Mo… Candy yuko kwenye kona mbaya sana kwa kweli…!” Nuru alikubali.
Lakini kwa wakati ule, Candy Gamasala alikuwa kwenye wakati bora kabisa maishani mwake, kule Caracas, Venezuela…
***
Kwa namna fulani Morandi Gwaza na Nuru walijikuta wakikosa namna ya kuendelea na upelelezi wao dhidi ya John Koccho, kwani taarifa walizopewa na yule jamaa wa Morandi hazikubadilika. Bado sura na jina la yule mtu mwenye zile alama za vidole haikuweza kuonekana kwenye mtandao wa polisi. Ingawa walikuwa wamemuona sura yule mtu, hawakuwa na picha zake ambazo wangeweza angalau kutembea nazo mitaani kuuliza iwapo kuna mtu aliyemuona yule jamaa.
“Kwa hiyo ndo kusema kwamba tunakaa tu tukimsuburi Candy arudi?” Nuru aliuliza kwa kukosa raha.
“Ah, ikibidi itakuwa hivyo…nijuavyo Candy akirudi hapa wote hao watajitokeza tu…na mchakamchaka utaanza upya. Hapa tutaraji kuwa yule jamaa yangu atatuletea jina la huyo mpelelezi aliyepewa kesi ya huyu mtu mwenye hizi alama za vidole…yeye atakuwa ndio njia pekee ya kuanza kumfuatilia huyu jamaa.” Morandi alimwambia.
Kutokana na kukosa pa kuanzia, waliamua kujiliwaza tu mjini.Mara wakienda sinema, mara wakienda kwenye kumbi za starehe ili mradi walipata muda wa kujisahaulisha yale matafrani ya Candy na wafuatiliaji wake.
Pamoja na hayo, Nuru hakuacha kwenda kupiga kambi pale Aga Khan akiwa amejibadilisha badilisha kujaribu kuona iwapo Ngamao ataenda tena kuonana na swahiba wake, na katika moja ya siku hizo alifanikiwa.
Pamoja na hayo, Nuru hakuacha kwenda kupiga kambi pale Aga Khan akiwa amejibadilisha badilisha kujaribu kuona iwapo Ngamao ataenda tena kuonana na swahiba wake, na moja ya siku hizo alikafanikiwa.
Ngamao alifika pale hospitali na kukaa nje ya wodi ile kwa muda mrefu, wazi kuwa alikuwa akijaribu kuangalia iwapo kuna yeyote anayefuatilia nyendo zake, na alipojihakikishia kuwa hakuwepo aliingia wodini kwa GTZ.
“Ah! Ngamao! Vipi bwana wee? Umepotea kabisa? Yule jamaa aliniambia kuwa amekudhibiti! Imetokeaje?” GTZ alimaka, na Ngamao akaketi kando ya kile kitanda taratibu.
“Picha limebadilika GTZ…inabidi tuihusishe polisi ya hapa Dar sasa katika hili!” Alimwambia, na GTZ akamtolea macho.
“Si nilikwambia ufanye hivyo kitambo tu lakini, Ngamao? Haya ilikuwaje sasa mpaka jamaa akakutaiti na wewe?” GTZ alimuuliza.
Ngamao alipiga kimya kwa muda.
“Ukweli jamaa aliniotea…hivyo akawahi kunifunga pingu…ilikuwa mbaya sana. Lakini sasa hataweza kuniotea tena nakwambia…tukikutana ni mimi ndiye nitakayetoka kidedea!” Ngamao alisema, na GTZ akaonekana kutoliamini hilo.
“Okay, ina maana umeweza kumtambua? Si nilikwambia yule alikuwa anaonekana kama ni polisi hivi? Hukuweza kumtambua?”
“Alijiziba sura kwa soksi maalum…sikumuona sura!”
“Basi ye’ atakuwa anakutambua Ngamao…huyo ni polisi mwenzenu tu! Kwa nini anashirikiana na Candy katika hili sasa?” GTZ alimaka.
Ngamao alikunja uso kwa tafakari.
“Inawezekana kweli akawa amejiziba sura kwa kuwa anahofia ningemtambua aiseee!” Alisema, na GTZ akasisitiza kuwa hilo ndilo haswa lilivyo.
“Kwa hiyo sasa wewe utakuwa nje ya kesi hii?” GTZ alimuuliza.
“Nitakuwamo lakini sio kwa undani kama ilivyokuwa hapo mwanzo…nitakuwa kama askari mwenye kesi ila askari wa hapa mjini ndio wakatakaofuatilia kukamatwa kwa Candy. Kwa hiyo na wewe nakutaka ukae pembeni kabisa katika hili…”
“Nitaenda wapi mimi unadhani?” GTZ alisema kwa uchungu huku akiuoneshea ule mguu wake.
Dakika chache baadae Ngamao aliondoka, na huku nyuma GTZ alichukua simu yake na kumpigia mtu ambaye siku zote alijizuia kumpigia juu ya hili. Lakini sasa hakuwa na namna, Ngamao ameshapoteza umiliki wa kesi ya Candy, na kibaya zaidi ameshaonesha kuwa na yeye hamuwezi yule jamaa aliyemvunja yeye goti, kwa hiyo GTZ hakuwa na uhakika kama azma yake dhidi ya mwanadada yule ingetimia.
Simu iliita kwa muda kisha mtu aliyekuwa amempigia akapokea.
“Haya leo imekuwaje mtoto wa halali ananipigia simu?” Mtu wa upande wa pili aliongea simuni, na GTZ akauma meno kwa kauli ile.
“Sisi bado ni ndugu tu Kaka…haijalishi kama ulizaliwa na baba mwingine au vipi…” GTZ alimjibu yule mtu.
“Sema utakalo GTZ…nina mambo mengi mimi!” Jamaa wa upande wa pili alimjibu.
“Niko Aga Khan hospitali kaka…nimelazwa…nimepigwa!” GTZ alisema, na mtu wa upande wa pili akapiga kimya kwa muda.
“Uko wodi gani?” Jamaa aliuliza, na GTZ akamtajia.
“Nakuja huko sasa hivi!” Jamaa alisema na kukata simu.
Inabidi na mimi nibadili mkakati sasa…siwezi kukubali kushindwa!
GTZ alijiwazia.
***
Nuru na Morandi walikutana mchana ule kwenye mgahawa mwingine kwa ajili ya chakula cha mchana. Huko Nuru akamwambia kuwa Ngamao alienda kumtembelea GTZ pale Aga Khan.
“Lakini jamaa alionekana akiwa makini sana, kama kwamba alikuwa hataki mtu yeyote ajue kuwa alienda kumtembelea GTZ pale, kinyume na ilivyokuwa mara ya kwanza…” Nuru alisema, na Morandi akabetua mabega.
“Huenda anaogopa nitamuibukia tena…” Morandi alisema, na hapo wakaona watu wengine wawili wakiwavamia na kuketi pamoja nao pale kwenye meza yao.
“Hello lovebirds…mnanikumbuka mimi?” Moja wa wale watu wawili alisema huku akimtazama Morandi kwa tabasamu baya.
Morandi alimtazama yule mtu na uso wake ukaingia ugumu.
“Unataka nini wewe?” Alimuuliza kwa hasira, akipeleka jicho kwa yule mwenzake aliyefika naye pale mezani, na kuyarudisha tena macho yake kwa yule msemaji wa mwanzo.
“Ni Kamishna wa polisi wewe! Sema unataka nini kamishna, sio “wewe” mimi!” Jamaa lilimkoromea na Morandi akaachia cheko ya kebehi na kujiegemeza vizuri kitini.
“Chakula changu kinapoa wewe…sema ulilo nalo uende!” Morandi alimkoromea yule kamishna wa polisi aliyekuwa kwenye magwanda rasmi ya kiaskari.
“Tumeona mpenzi wako Kokos Wandiba amejiingiza kwenye udhamini wa warembo siku hizi…kisha tukasikia askari wetu mmoja kutoka Mwanza amevamiwa hotelini na kutembezewa kisago kikali na jitu refu lililojiziba sura…sasa tukajiuliza…kwa nini mambo haya yanatokea katika kipindi hiki ambacho na wewe ndio umeanza kuonekana tena mjini baada ya kupotea kwenye sura ya nchi kwa muda mrefu?” Jamaa alimuuliza, na moyo wa Morandi ukapiga chogo chemba kifuani kwake.
Aliinuka.
“Twenzetu Nuru!” Alisema na Nuru akaanza kuinuka.
“No, no noo…kaeni tu wapendanao, kuleni. Sisi tulikuja kuwasalimu tu!” Jamaa lilisema huku likiinuka.
Likageuka na kuanza kuondoka, kisha likasimama na kuwageukia akina Morandi waliorudi kuketi mezani kwao na kuwafanyi ishara ya “I am watching you”, kwa kuweka vidole vyake viwili mbele ya macho yake, na kuvigeuzia kwao, ikiwa ni ishara ya kuwaambia kuwa alikuwa anawafuatilia sana.
Morandi naye akamrejeshea ishara ile ile huku akiwa amenuna vibaya sana.
Nuru alimgeukia kwa wahka baada ya wale askari kuondoka.
“Ni nini hii Mo?”
“Ngamao kaenda kushitaki rasmi jeshini…keshaona hii ngoma peke yake haiwezi pumbavu zake!” Morandi alimjibu.
“Hah, sasa itakuwaje?”
“Haiwi lolote…tutakabiliana na kila hali itakayokuja…!” Morandi alimjibu, na kuendelea kula chakula chake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Yaani yule mjinga ndio kawa kamishna siku hizi?” Nuru aliuliza kwa kutoamini. Wote yeye na Morandi walikuwa wanamfahamu yule jamaa kutokea wakati wa enzi zao katika jeshi la polisi, na wakati Morandi alipokuwa anakabiliwa na kesi ya mauaji, yeye ndiye alikuwa ni miongoni mwa mashahidi muhimu wa upande wa mashtaka, na hakupendezewa kabisa, kama jinsi sehemu kubwa ya jeshi la polisi ilivyokuwa haikupendezewa, pale Kokos Wandiba aliposhinda ile kesi na Morandi akawa huru.
“Sasa ndio uone aina ya askari wanaopendwa na kupewa vyeo kwenye jeshi letu adhimu la polisi kisura… mtu timamu huwezi kumpa u-kamishna mjinga kama yule pumbavu zake! Hebu tupige msosi tutambae zetu hapa!” Morandi alimjibu na Nuru akaguna.
Hakuna kilichoibuka tena mpaka siku ilipotangazwa kuwa Candy amepita katika ishirini bora kule Venezuela, na nchi ikaanza kuwa makini na shindano la miss world kwa mwaka ule.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment