Simulizi : Suprise
Sehemu Ya Nne (4)
“Lakini mi najua tu ipo siku, nitakutana nao nikiwa mie na wao peke yetu, hapo ndio watajua kwanini kuku haangalii juu kwa macho mawili japo anayo."
"Kwani wewe una mpango gani juu ya watu wale?" Aliuliza Ommy akimshangaa Victor
"We utaona tu, haraka ya nini? Wao si ndio wamenikosea, lakini wao ndio watakao kimbilia kama sio kwa wazazi basi wataenda Polisi, tena wala si siku nyingi zijazo." Alijibu Victor huku akiwa na tabasamu, hawakujua tu kuwa lile halikuwa tabasamu la furaha, bali lilikuwa ni la uchungu.
Tabasamu hilo lilimshangaza hata Ommy na mkewe Lidya. Wakatazamana na kuanza kumtuliza tuliza Victor na kumwambia aachane nao wao sasa ni kazi tu, wafanye mabadiliko ya Kampuni yao kwa kufanya kazi na katu wasianze kujipoteza kwa kujiingiza kwenye magomvi na kesi zisizo na kichwa wala miguu. Victor akacheka na kumuuliza Ommy
“Unajisikiaje pale mtu anapokupiga kofi na kukwambia Relax?” lilikuwa swali dogo lakini maana yake ilikuwa ni kubwa sana, Ommy akashindwa kujibu lolote na kushusha pumzi, Lidya akaingilia kati baada ya kuona mumewe amekosa jibu.
“Shem kwa kweli inauma sana, lakini kiukweli nasikitika kuwa ni mimi ndio napaswa kubeba lawama zote shem wangu, na natumia nafasi hii kukuomba msamaha kwa hili,” Ommy akamuangalia mkewe kwa mshangao na kujiuliza moyoni, sasa kosa lake lipi hapo?
Kama mtu aliekuwa akiyasoma mawazo ya Ommy, Victor nae akahoji kwanini Lidya anamuomba msamaha.
“Sababu kuu ni kushindwa kujua mapema kama hawa watu wamerejea kwenye uhusiano wao ambao ulikuwepo awali, ndio maana naomba msamaha kwako,” victor akamtoa wasiwasi na kumwambia yeye wala hahusiki lakini ole wake Eve…
“Lidya shemeji yangu, huchukua dakika moja 0 kumuona umpendae, na huchukua siku 1 kumpenda kwa dhati, lakini inaweza kugharimu maisha yako yote ili kuweza kumsahau, ndio nahisi hawa watu…” Ommy akamkatisha kauli na kusema
“Victor mdogo wangu, kukutana na Eve ilitokea tu kama bahati, kuwa karibu nae ulikuwa ni uamuzi wako binafsi, lakini kumpenda ilikuwa nje ya matakwa yako, ama nakosea?” Victor akatikisa kichwa kuashiria anakubaliana nae, Ommy akaendelea
“Najua nafsi yako inalia, natambua fika moyo wako waumia, hakuna asieijua sababu, sote tunaijua, ila unapaswa kuendelea kuwa na roho ya kuvumilia kama mwanzo, hakuna mvua inayonyesha milele, itakatika na movement zitaendelea tu mdogo wangu,”
Alimaliza ommy na sasa Victor alionekana kuwaelewa washirika wake, akaonesha kidole gumba kuwa powa na palepale akawauliza mchakato ufuatao ni upi?
Lidya akatoa wazo ambalo lilipita bila kupingwa na yeyote kati ya wale wanaume wawili ambao sasa walimuita First lady wa Kampuni.
Wakati akijipanga kutoa wazo lile alikuwa akihofu sana wazo lake kupingwa na Ommy mumewe ambae siku zote alikuwa hamuamini kabisa linapofika suala la kuchangia mada za kampuni.
Alishauri waandae tamasha moja la nguvu sana kwenye hizo nchi mbili walizotoka kwa kuanzia na Burundi kisha wakamalizie Rwanda
"Tuchukue wasanii wengi maarufu na ma DJ kibao pia wasanii kutoka Kenya." Lidya aliongea kwa kujiamini, lakini Victor akahoji kwanini waingie gharama kubwa vile?
"Shem, hii itatupa nafasi ya sisi kumuonesha Eve kuwa hatujatetereka kama Kampuni kwa kuondoka kwake, ama wewe unasemaje?" Victor alionekana kama vile hajaridhika lakini kutokana na ushawishi wa Ommy, akakubali na kuahidi hata nae siku hiyo atasimama kwenye mashine, wakacheka na kunyanyuka kwenda matembezi.
Walipoteza siku 3 ndani ya Jiji la Dar kisha wakaondoka kurejea Nairobi kundelea na majukumu yao wakimuacha Victor akiwa ni majonzi tele na upweke wa kutosha. Lakini upweke ule haukumvunja moyo wa kazi bali ndio ulimpa mori zaidi, hasa wa yale matamasha mawili matamu sana yafuatayo.
Maandalizi yakapamba moto barabara, ndani ya wiki moja walikuwa wamefanikiwa kuwasainisha mikataba wasanii wengi. Kwa upande wake Victor alifanikiwa kufikia malengo yake kwa kuwapata ma DJ wa3 ambao alichukua jukumu la kuwatafuta.
Ma DJ hao walitoka kwenye vikundi vi3 tofauti lakini vyote vikiwa ni vikundi vikubwa na maarufu nchi nzima. Alimpata DJ kutoka Nyuki DJ's na mwingine kutoka Kwa Fujo DJ's na wa mwisho alimtoa Classic DJ's, hawa ndio aliingia nao mkataba wa kufanya maonesho kwa nch zote mbili, yaani Buurndi na Rwanda.
Kulikuwa na Fire DJ's na Funika DJ's makundi yenye upinzani wa jadi nchini Uganda haya yalikula dili la kupiga Burundi tu na kugeuza kurudi nyumbani wakati wenzao wakielekea Rwanda, kwani walikuwa na ratiba nyingine ambayo iliwabana kufanya Tour ya Rwanda.
Ila pia kulikuwa na Kamua DJ's na Aminia DJ's kutoka Kenya ambao Ommy aliweza kuwapata kutoka huko kama walivyokuwa wameelewana kabla ya kuondoka hapa nchini, makundi hayo maarufu nchini Kenya, yalikubali kufanya onesho moja tu la nchini Rwanda.
Upande wa manamuziki napo mambo hayakuwa mabaya, kwani waliweza kuwapata wasanii wakubwa zaidi ya 13, ambapo wasanii maarufu wa4 walitoka Tanzania huku Ommy akileta Wakenya wa3 na Sabrina kutoka Uganda nae alidondosha wasanii wawili sawa na Rwanda na Burundi ambao kila nchi ilileta wasanii wawili.
Hivyo maandalizi yote yakawa tayari yamekamilika, kilichokuwa kimesalia ni muda tu, ndio ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu kubwa mno. Walikuwa wameamua kujipanga kwa miezi mitatu, lakini ndani ya mwezi mmoja kila kitu kikawa kimeenda vizuri.
Wakurugenzi na mameneja wa matawi, walikuwa busy kweli kweli na simu kwa ajili ya maandalizi ya shughuli ile kubwa ambayo kwa wao ilikuwa inatarajiwa kufanyika kwa mara ya kwanza. Victor alipokea mzigo mkubwa wa Madawa ya mifugo na vifaa kadhaa kwa ajili ya maabara na kuituma Rwanda pamoja na CD za matangazo ya tamasha.
Mwezi mmoja kabla ya tukio lenyewe, matangazo yakabandikwa kwenye miji mbali mbali ya nchi husika za Rwanda na Burundi. Kila alie yaona alitamani shughuli iwe iwe siku ifuatayo, lakini kumbe waliwapa muda wa kujipanga na kujikusanya ili wasilalamike kuwa imekuwa ni mapema sana.
Matangazo yalisomeka
'LOVE com (EA. Ltd) inawaletea bonge la show kali toka kwa wasanii wa nchi zote za Afrika Mashariki. Kutakuwa na wasanii zaidi ya 10 kutoka nje ya nchi na wengine kibao wa hapa nchini. pia kutakuwa na bonge la muziki litakalo dondoshwa na ma DJ maarufu zaidi kwenye ukanda wetu huu wa Afrika Mashariki.
Show hii si ya kukosa, na ukiikosa, nenda kapande ndege, ukifika mita 1500 usawa wa bahari, jiachie, ni heri utoweke kabisa duniani kuliko kuikosa hii funga mwaka... Never Miss!' hivyo ndivyo lilivyo maliza tangazo ambalo lilipambwa kwa picha za wasanii na ma DJ.
Pamoja na kuwa Victor na Ommy walikuwa busy, lakini Wakurugenzi na mameneja wao kule kwenye matamasha walikuwa busy zaidi. Hakuna aliekubali kulala, walikesha wakitafuta kila aina ya mbinu kufanya tamasha liweze kufana.
Kila mmoja alitaka amfunike mwenzie ili kampuni isijute kuandaa tamasha sehemu alipo. Hamasa hiyo haikuishia kwa viongozi tu wa kampuni pekee, bali pia ilikuwepo kwa Ma DJ. Kila mmoja alikuwa akijifua kivyake akijitahidi kukusanya aina za muziki alizojipanga kuzitumia.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wasanii nao ndio haikusemeka, hasa walipojua kuwa watakuwa ni zaidi ya nchi 5 za Jumuia ya Afrika Mashariki, kila mmoja alikamia kumfunika mwenzie na kutengeneza jina ughaibuni.
Victor ndio alikuwa mratibu wa Onesho la Burundi, pembeni yake akiwepo Harbush aliekuwa ndio mwenyeji wao, akitoa kampani ya nguvu kwa kipindi kile, wakati huo Sabrina sasa alikuwa ameisha weza kuongoza tamasha hata peke yake, alikuwa ndio Mratibu wa tamasha hilo huko nchini Rwanda.
Ommy ndie alisimama kama Mkurugenzi Mkuu, alihakikisha wasanii wote kutoka nchi tajwa na pia Ma DJ wanasafirishwa kama inavyo takiwa na kufika sehemu husika kwa wakati, kwakutumia usafiri wa ndege, alihakikisha kila mtu anawajibika kama alivyo pangiwa.
Tamasha la kwanza la nchini Burundi hatimae siku ikawadia, ilifanyika kwenye ukumbi wa Saga Plasher. Show ilifanyika kama ilivyopangwa na kifupi walifunika vibaya sana. Wasanii walikonga nyoyo za mashabiki wao waliokuwa na hamu kubwa ya kuwaona moja kwa moja kwani walizowea kuwasikia tu kwenye maredio ama kuwaona kwenye TV.
Ma DJ nao walifanya kile walicho paswa kufanya, waliwaridhisha mashabiki walio hudhuria tamasha lile, hakuna alie simama na kupinga kwamba hakutendewa haki.
Kila aliehojiwa alikubali muziki wa LOVE com na wote walikiri kwamba wameelewa kwamba ile kampuni inaposema burudani, basi inamaanisha nini.
"Tunakiri tumejua ni kwanini imekuja huku na kitu gani imekuja kufanya," aliongea mpenda burudani mmoja alipokuwa akihojiwa na Radio moja ya nje ya Afrika. Mwisho wa onyesho, wananchi wapenda burudani wakaomba onesho lingine mwanzoni mwa mwaka ujao.
Victor ambae alikuwa ni mratibu wa Onesho lile, hakutaka kuwakatisha tamaa, bali aliwaahidi kuwa ikitokea nafasi, basi watatoa upendeleo kwa Burundi, kwani hata nao wamefurahi kwa mapokezi walio yapata ambayo wala hawakutegemea.
Wakationesho la Burundi likiendelea, Ommy na familia yake pamoja na baadhi ya wasanii na maDJ waliopangwa kufanya onesho la Rwanda walikuwa tayari wamewasili wakizunguka mjini kutazama mandhari ya Jiji la Kigali.
Tayari alikuta Sabrina kwa kushirikiana na Kihuna na uongozi wa pale Rwanda, walikuwa wamebandika matangazo na vipeperushi kila sehemu za jiji lile safi, pakiwa na mabango kwenye kona za mitaa, kwenye mabaa pia kwenye vyombo vya habari, huku maandalizi yote yakiwa yamekamilika.
Tangazo lile lilipofikishwa kwenye Radio Kigezi FM, hapo ndio ikawa kazi. Siku hiyo Eve hakuwa Studio, alikuwepo Ondiek peke yake. Baada ya kuliona jina tu la LOVE com na Mkurugenzi kuja kutaka kuongea nae kuhusu suala lile, Ondiek alichanganyikiwa.
Jinamizi la jina lile likampa kimuhe muhe Ondiek na kutaka kuchanganyikiwa hasa mara alipo itikia wito wa Mkurugenzi wake na kumweleza kuwa ana nia ya kuwaalika siku ya tamasha mchana wafike pale Studio kwenye kipindi chao wawahoji.
Ondiek hakutoa jibu lolote bali alijifuta jasho japo AC ilikuwepo na ilikuwa ikifanya kazi, lakini kwake alihisi joto kali. Bila hata ya kujifikiria, Ondiek akaomba likizo fupi, akidai mkewe ni mgonjwa nyumbani kwao Tanzania ndio sababu kachanganyikiwa.
Alifanya hivyo kutokana na swali alilo ulizwa na Mkurugenzi wake inakuwaje anakuwa kama ni mtu aliechanganyikiwa ghafla tatizo ni nini? ndio akajitetea hivyo na Mkurugenzi kwa kujua uzito wa mke, akamruhusu kwa kuamini kipindi kitaendeshwa na Eve pekee na hakito haribika kitu.
Aliwashukuru tena Victor na kuwaaga rasmi wapenzi wa burudani waliojitokeza kwa wingi ukumbini, akisema siku yoyote ile wakipata muda, watarudi tena nchini Burundi.
Jioni Ondiek aliporejea nyumbani ndio akamueleza Eve juu ya yale yaliyojiri ofisini na kumuweka wazi nia yake ya kurudi nyumbani Tanzania ili kwenda kumuona mkewe ambae ni mgonjwa. Eve akamjia juu vibaya sana na kumwambia kama ni kuondoka, wanaondoka wote.
Ondiek alimtazama na kumuuliza kuhusu kazi? Eve akamwambia yeye hakuzaliwa na ile kazi, tayari ameisha acha kazi nzuri zaidi ya ile, itakuwa hii? ataacha ilimradi kama anaondoka, basi ajue wanaondoka wote kurejea nyumbani.
Wala hakuonekana kujali ondiek, Eve akasimama mbele yake akiwa kashika kiuno na kumwambia
"Mimi kwa kweli siwezi kukuelewa kwa suala la wewe kuondoka peke yako na kuniacha mimi huku peke yangu, wakati unatambua fika kuwa wewe ndio chanzo cha yote haya." Walibishana sana hadi kufikia hatua sasa ikaamuliwa kila mtu afe kivyake. Eve alilia sana kwa kauli ile ya Ondiek.
Kilio alichokuwa akilia kilikuwa ni kilio cha majuto, alikuwa akijuta ni kwanini alikubali kudanganywa tena na Ondiek kwa mara ya pili! Pia alijuta ni kwa sababu gani alimsaliti mumewe kipenzi Victor. Alikumbuka mengi sana waliyo yafanya akiwa na kundi la watu wa LOVE com wakati huo akiwa mwanachama.
Zaidi alimkumbuka mno mwanae na alitamani sana kumuona Bill, ambae kwa wakati huo allikwisha jua kuwa anasoma Kenya kwa sababu anaishi na Lidya ambae hapo awali aliwahi kumpa onyo kuwa hatomsemesha tena kama tarudiana na Ondiek.
Masikini Eve, maisha yake yamekuwa machungu, kila mtu afe kivyake, je wataondoka pamoja? Victor tayari kamaliza kazi Burundi, pamnafuata…. Hebu nicheki tena wakati mwingine.
Alipofikiria hapo, kilio kikawa hadharani. hadi Ondiek anaondoka kwenda nyumbani kwake, Eve wala hakuwa hata na habari. Alipokuja kushtuka ndio anagundua kuwa kabaki peke yake, alinyanyuka na kufunga milango ya nyumba yake na kupanda kitandani kulala.
LOVE com hiyo ilikuwa ndio siku ambayo walikuwa wakikamilisha kila pungufu walioliona waliopo kule Rwanda, na pia ni siku ambayo walikuwa wakiwategemea wasanii, ma DJ na baadhi ya viongozi wa LOVE com waliokuwa Burundi walitarajiwa kuwasili Rwanda. Siku hiyo ilifanyika Promo kubwa sana.
Na usiku wa siku hiyo ndio walipokea simu kutoka kwa Mkurugenzi wa Radio Kigezi FM akiwaalika katika mahojiano siku ifuatayo muda wa saa 6 mchana, akiwataka kwenda na DJ mmoja na Msanii mmoja pia.
Ommy hakujiuliza mara mbili wala hakupinga, kwani hicho ni kitu ambacho walikuwa wakikihitaji kuliko hata hiyo show yenyewe ya ukumbini, akawajulisha pia Victor aliekuwa na Sabrina kisha akamwambia na Lidya akaonyesha dole gumba. Walifurahi sana.
Bill na Jam walikuwa wakicheza ndani ya gari na mama yao, akawateremsha na kuwapitiawengine kisha wakaenda kuungana na baaadhi ya wasanii wao waliokuwa wakipata chakula cha usiku hotelini. Walipata faraja sana kuona mabosi wao hawa wabagui.
Baada ya kula chakula kile cha usiku, wakasambaana kila mmoja kishika njia yake, Ommy na mkewe Lidya aliembeba Bill aliekuwa amelala, wakaelekea chumbani kwao, Sabrina akiwa na Jam, nao wakaelekea chumba kingine na kuimaliza siku kwa aina hiyo.
* * * * *
Siku ya Jumapili, ndio ilikuwa siku ya tamasha la nchini Burundi, saa 5 na nusu, Eve alikuwa amefungulia radio yake akisubiri kusikia ni nini kitasemwa na waalikwa pale Studio. Alikuwa amejilaza kwenye kitanda chake akisikiliza matangazo ya biashara yakiendelea.
Kichwa chake kilitawaliwa sana na mawazo ya siku zilizopita, alimkumbuka sana mumewe na ndoto za kuwa nae hadi kifo kuwatenganisha. Akawaza;
“Ndoto huwa ni fikra, matamanio huwa hayatuishi wanadamu, mitazamo na mipango huwa mingi sana moyoni, je kila ndoto ingetimia, maisha haya tunayoishi yangekuwaje? Nafikiri kila kitu kibaki tu kuwa ni mtazamo.”
Mawazo yake yakakatizwa na sauti kwenye radio, kwani ilikuwa kuna muziki lakini ghafla ukakatishwa na akasikia tangazo la show ile ya siku ileile usiku wa leo, muda sio mrefu baadae, akasikia sauti ya mtangazaji ikiwakaribisha waalikwa studio.
Haikuwa sauti nyingine, bali ilikuwa ni sauti ya Mkurugenzi mwenyewe Bwana Kulwa Danga. Japo alikuwa amekaa Tanzania kipindi fulani alipokuwa akisoma lakini Kiswahili chake hakikuwa nyoofu, mara kwa mara alichanganya na Kifaransa na wakati mwingine Kiingereza.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Haikuwa tabu kwa waalikwa, kwani walitambua nchi ile waliopo si nchi yao halisi.
Mtangazaji akawataka radhi wageni wake waalikwa kwa kutokuwepo watangazaji halisi wa kipindi kile, kwani walikuwana dharula. Mmoja wa kiume alikuwa na matatizo ya kuuguliwa na mkewe huko kwao Tanzania, na mwingine ambae ni wa kike, dakika chache zilizopita waliwasiliana nae akiwa nyumbani kwake, lakini ameshindwa kuja kwa sababu ni mgonjwa.
Wakatazamana waalikwa waliopo Studio ambao wanao wajua watangazaji wale waliosemwa kuwa wamepata dharula, wakatabasamu na kujiona kama wao ndio washindi vile kwa sababu wamekimbiwa.
Ilikuwa ni ajabu sana, mgeni unakaribishwa kasha mwenyeji anakimbia, Lidya akamtazama Ommy na kumgeukia Victor kasha akamwambia
“Shem, uchungu na utamu zote ni ladha, vipi utaijua ladha ya kitu? Si hadi uonje kitu chenyewe?”
“Ndio Lee,” alimjibu huku akimtazama aendelee kumwambia ni kipi amemaanisha.
“Binadamu tumekuwa tukifurahia tu utamu huku uchungu tukiuchukia bila kujali kuwa zote ni ladha… leo ofisi imekuwa ni chungu kwa Eve na Ondiek, wakati jana tu ilikuwa ni tamu na walikuwepo ofisini,” alimaliza Lidya na kumfanya Victor atabasamu.
Mahojiano yakafanyika vizuri kama yalivyo pangwa, maswali mengi yaliulizwa na yote yalijibiwa kwa ufasaha, moja ya swali waliloulizwa ni nini maana ya neno LOVE com, akajibu Victor kuwa kile ni kifupi cha majina ya wamiliki wa Kampuni ile ambao mwanzo walikuwa wanne, lakini sasa wamebaki watatu mara baada ya mmoja wao kujitoa.
Alipoulizwa majina yao, yaani majina ya wamiliki wa LOVE com, Victor alikataa kuyataja kwa sababu ambazo alisema si salama kwa LOVE com, hivyo aliwataka radhi tu walio uliza swali lile.
Kauli ile ya Victor ilimchoma sana Eve na kujikuta akilia kimya kimya, na lengo hasa la Victor ilikuwa ni kumchoma hivyohivyo, maana alijua kabisa ni lazima watakuwa wapo pamoja sehemu wakisikiliza mahojiano. Mwisho wakaambiwa watoe neno la kuaga.
"Ninawakaribisha sana Wanyarwanda kwenye ukumbi wao maalum wa Hotel Rwanda pale," Alisema DJ Xtra brain kabla ya msanii J Ram kutoka Burundi nae kuwakaribisha kwa kusema;
"Watu wakuje kwa wingi, wakuje kufurahi," mwanamke pekee aliekwenda Studio alikuwa ni Lidya, kwani Sabrina alibaki na watoto hukohuko hotelini. Akapewa nafasi ya kuongea kwa niaba ya wengine ambao hawakusikika pale.
Lidya aliitumia nafasi ile kuwashukuru wakazi wa Kigali kwa kuchukua tiketi kwa wingi hadi muda ule wameambiwa kuwa idadi ile inayopaswa kuingia ukumbini, tayari imefikiwa hivyo tiketi haziuzwi tena, hivyo akawaomba wale walionunua tiketi wasiache kufika ukumbini huku wakichunga muda.
Wakamaliza mahojiano ambayo yalidumu kwa saa moja na kuelekea sehemu maalum iliyo andaliwa kwa ajili yao ili kupata chakula cha mchana. Mkurugenzi aliwaambia kuwa chakula kile walipaswa kula wakiwa pamoja na watangazaji wa kipindi kile ambacho walialikwa lakini kama wajuavyo, imepatikana dharula.
Walimsihi tu kuwa asijali, madhali yeye amesimama kidete, wameona hakuna chochote kilicho haribika zaidi wamefurahi mno kufanya Interview na mkuu wa Radio mwenyewe.
Baada ya kula na kumaliza, wakaondoka kurejea hotelini ili kufanya mandalizi ya mwisho mwisho ya tamasha lao ambalo walikuwa wamelikamia kwelikweli.
Njiani walipokuwa wakirudi, Ommy aliwaambia Ommy na Victor
"Ujue adhabu wanayo ipata watu hawa ni kubwa mno? Adhabu hii si ya kawaida..." Victor akadakia kwa sauti ya kawaida kabisa
"Kwa hiyo hata kuonana nasi hawataki?" Sauti ilikuwa ni ya taratibu mno, ikajibiwa na Lidya aliekuwa amekaa siti moja na Victor
"Sio kama hawataki, bali wanaona aibu, ila leo usiku nina hakika tutawaona ukumbini." wakacheka na kushuka garini, kwani walikuwa tayari wamefika hotelini. Pamoja na kuambiwa kuwa Ondiek karejea Bongo kwenda kumuona mkewe, lakini wote walikuwa wakiamini Ondiek alikuwa yupo pale pale mjini na hajaondoka kwenda popote.
Ratiba ilifuatwa, kila kitu kilienda kama kilivyo pangwa, shughuli ikaanza kwa wakati uliotakiwa, wapenzi wa burudani waliwasili mapema zaidi na kujaza ukumbi, wanamuziki waliingia ukumbini kwa muda uleule waliopangiwa.
Kila msanii alihakikishwa kuwepo eneo la ukumbini saa moja kabla ya muda wake halisi wa kuwepo, hiyo yote ni kujenga heshima kwa wadau waliokuja ukumbini na kulipia pesa zao ili kupata burudani.
Muda ulizidi kwenda, burudani ilishika kasi vibaya mno, kila mtu ukumbini alichangamka, wasanii walishindana, anaeshuka watu wanalalamika wakitaka aendelee, lakini anaeingia anakuja kumfunika alietoka, hali ikawa ni hiyo.
Wote wakiwa wamekata tamaa kwamba hakuna yeyote katiya Eve wala Ondiek atakae tokea, Lidya alikuwa nje kabisa ya ukumbi akiwa amembeba Bill wakati Ommy alikuwa akitembea tembea ndani ya ukumbi akiwa amemshika Jam mkono, wakati huo Sabrina na Victor walikuwa kwenye dirisha la Ticket kwa ndani wakikagua kupitia tochi maalum walizokuwa nazo mikononi.
Mlangoni kwa nje walikuwepo mtu na ndugu yake, yaani Harbush na Kihuna wakiwa na mabaunsa kwa ajili ya kutunza usalama wa wapenzi wa burudani waliopo ukumbini. Eve akajitokeza akiwa na tiketi yake ya tamasha lile aliyoletewa kutoka ofisini ili akahudhurie onesho.
Alipotazama dirishani, akaweza kumuona Victor kwa mbali akiwa anaongea na msichana ambae alishindwa kumtambua kutokana na yeye kurudi nyuma haraka ili akajipange upya. Alifikiria mbinu mbadala ya kumfanya aingie pale akakosa kabisa.
Mwisho akaamua kuahirisha tu kuingia ukumbini, lakini akawa anajiuliza kesho kazini atasemaje na ikiwa tiketi kaletewa hadi nyumbani? Pia alipokuwa akikumbuka kuhusu mtoto wake kwamba anapaswa kumuona kwa gharama yoyote, akapata ujasiri.
Aliongoza moja kwa moja hadi mlangoni walipo walinzi, hakutaka kupita dirishani ili kukaguliwa tiketi, hivyo kwa kutumia umaarufu wake na kitambulisho chake cha uandishi wa habari, tena kwa radio kubwa pale Rwanda, hakupanga hata msitari.
Alionesha kitambulisho na kuruhusiwa kuingia ndani kwa kupitia upande ambao alikuwepo Sabrina mabae alikuwa hamfahamu vema, hivyo hakuhangaika nae sana kumchunguza.
Baada ya Evelyne kuingia ndani ya ukumbi, akaanza kuwatafuta watu ambao aliamini akiwaona hao, anaweza kumuona mtoto wake.
Mtu wa kwanza kumuona alikuwa ni Ommy aliekuwa amemshika mkono Jam wakiwa wanazunguka huku na kule, kwa vyovyote vile akajua fika kwamba Bill kama wamekuja nae, basi atakuwa na Lidya, lah sivyo watakuwa wamemuacha.
Usijiulize amejuaje, alijiongeza kitu kimoja, alianza kumuona Victor akiwa peke yake pale dirishani, kisha akamuona Ommy akiwa na Jam, sasa piga ua, ni lazima Lidya ndio atakuwa na Bill, hapo sasa ndio akahisi kizungu zungu.
Aliamini kama mtoto angekuwa nae Ommy, angeweza kumuona hata kwa kilio, lakini Lidya, alijiuliza kwanza ataanzaje kumsemesha? Lakini akaamua liwalo na liwe. Akaanza kazi ya kumtafuta Lidya, alizunguka ukumbi mzima bila ya kumuona, akaenda kukaa pembeni.
Kumbe wakati muda ule yeye akizunguka kumtafuta Lidya aliedhani yupo na mwanae, Lidya kwa kusaidiana na Sabrina, walikuwa wamewapeleka watoto kwenda kulala. Dakika kadhaa baadae, walirejea Eve na Sabrina na kuanza kuzunguka zunguka mle ukumbini. Sasa ndio Eve aliweza kumuona Lidya nae akiwa peke yake.
Rasmi sasa akajua kwamba, yawezekana ikawa Bill hawajaja nae, akanyong'onyea na kujihisi kulia. Akawa ni mpole zaidi ya hata ya alivyo ingia mle ndani. Hakuna burudani yoyote aliyoiona yeye zaidi ya machungu tu yaliyompata tangu alipo ingia mle ndani ya ukumbi.
"Na sasa ni zamu ya Msanii Mr. Smile toka Kenya na atafuatiwa na Ramson wa Tanzania kabla ya show kufungwa kwa bonge la muziki toka kwa maDJ wetu machachari, haya sasa, kazi ni kwako Mr... Smileeeeee." Wadau wakapiga kelele baada ya MC kupayuka vile.
Kwa kweli tamasha lile lilipendeza zaidi ya lile la awali lililo fanyika Burundi. Ikawadia muda ambao ma DJ walikuwa wakiusubiri kwa hamu ili nao waoneshe ufundi wao. Wakakandamiza sawasawa hadi mashabiki wakapagawa na burudani.
Ilipofika zamu ya DVJ Victor, alianza kwa kupiga wimbo wa Congo uitwao Evelyn ambao alikuwa na hakika kabisa utamgusa mama motto wake kwani huo wimbo Eve ameusikia mara kwa mara hadi ameupenda japo mwanzo alikuwa haupendi.
Kisha akafuatanisha na wimbo wa Kizungu wa Jay Zee uitwao 'I just be dead in your arms tonight' huu ni wimbo ambao Eve alikuwa ameukarili Chorus yote na akimwambia Victor kuwa anahisi kama Jay Zee aliutunga kwa ajili yake, kwani hiyo ni ahadi yake kwake.
Kadri alivyokuwa akipiga nyimbo hizo, ndivyo alivyokuwa akizidi kumuweka Eve kwenye wakati mgumu zaidi, Eve alikuwa akilia kama kifaranga cha kuku kilichopo hewani kwenye midomo mikali ya Kunguru.
Alifanya vile maksudi, kwani hadi muda ule Victor hakujua kama Eve yupo na alitambua kwamba kama Eve atakuwepo, kwa zile nyimbo ni lazima atajitokeza kwa waliopo ukumbini watamuona tu na watamjulisha, na hicho ndio kilicho tokea.
Katikati ya furaha, Ommy akamuona Eve kwenye pembe moja akilia, hakutaka kumsemesha japo alimuonea huruma, akamtumia ujumbe mfupi Victor aliekuwa mbele kwenye stage na kumwambia
"Kaka, Eve yupo humu ndani, ni mnyonge na amekonda vibaya, hali yake si shwari, yupo peke yake analia lakini sijamsemesha, anatia huruma sana." Ajabu Victor ndio akaona raha na kuanza kupiga nyimbo zenye mafumbo kwa Eve.
Wimbo alioanza nao ulikuwa wa Mwana FA, Unanitega? kisha akafuatia nyimbo nyingi tu zenye ujumbe mbalimbali na kumalizia wimbo wa Msanii aitwae Buibui wimbo uitwao 'Nimekusamehe mpenzi' ambao alisema anau dedicate kwa kinadada wote walio olewa na hadi sasa bado wapo kwenye ndoa zao.
Upande wake Victor akafunga ukurasa wa burudani na kuachia wengine waendelee hadi alfajiri, kwani kile alichokuwa amekitaka yeye, ndio ambacho alikifanya tena kwa kiwango kizuri tu ambacho kilimfanya Ommy na kundi zima la LOVE com limpongeze.
“Nawe jamaa ni mtundu sana, unakuwa kama Google, kila kitu unajua wewe, dah! Heshima mkuu…” alipongezwa na Sabrina na wakacheka kasha Victor akamuuliza kwanini amesema vile?
“We ni daktari, wewe ni mtangazaji, lakini pia hata Udj pia upo vizuri?”
“Yah! Ni kweli, ujue fani yangu wakati nikiwa mdogo ilikuwa ni hii ya Udj lakini huko kwenye udaktari nilipelkwa tu kwa nguvu ya wazazi, hawakuipenda kabisa kazi hii ya muziki,” walimuelewa na kuendelea kugawa majukumu kwa watu waliokuwepo pale kama wasimamizi.
Walipomaliza show na kufunga ukumbi, walimtafuta Eve kimya kimya lakini walishindwa kabisa kujua aliondoka saa ngapi mle ukumbini. wao wakaelekea kulala.
**********
Siku iliyofuata mara tu baada ya kunywa chai, Victor akiwa chumbani mwake pamoja na Bill na Jam, simu ya mezani ikaita. Muda huo Lidya na Ommy walikuwa nje wakirekebisha mambo mengine kwa ajili ya kujiandaa na safari kurejea makwao.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Hellow..." Alipokea Victor.
"Yes Sir, think Im talking with Mr. Victor." Ilikuwa ni sauti ya muhudumu
"(Ndio bwana mkubwa, nafikiri ninaongea na Bwana Victor?)”
"Yes I am"
"(Ndio mimi)"
"Alright, U have a visitor here."
"(Sawa, kuna mgeni wako hapa)" Victor alishangaa kusikia vile ukizingatia hana ahadi na mtu
"Who?"
"(Nani huyo?)"
"She said..."
"(Amesema...)" Victor akawa tayari amemjua mtu huyo ni nani, akamkatiza mhudumu
"Tell her, I dont like to hear her voice even to see her face, Bulldog!"
"(Mwambie hivi, sitaki kusikia sauti yake, na wala sipendi kuuuona uso wake hapa, pumbavu kabisa)" Victor akakata na simubila kutoa nafasi nyingine yoyote ya dada wa mapokezi kuongea.
Bill alivyoona baba yake akiongea na simu, akamsogelea na kumuuliza naongea na nani? Victor akamdanganya kuwa anaongea na dada wa kazi, kisha akawashika mikono na kutika nao kwenda sehemu nyingine kubadili mazingira.
Waliteremka ghorofani na kwenda bustanini, huko walicheza mno na kukaa huko hadi Ommy alipowafuata na kuwataka waende wakale na kujitayarisha kwa ajili ya kuondoka kurejea makwao kupitia Ngara, Kahama, Nzega, Singida, Dom hadi Moro na hatimae Dar.
Wakiwa wanakula, Victor akawaambia juu ya Eve kutaka kuongea nae, walicheka na Sabrina akauliza kajuaje kama wapo pale? Ommy akajibu kuwa itakuwa amesikiliza redioni wakati wa mahojiano walipo wakaribisha watu waje kwa ajili ya kubadilishana mawazo.
Safari ikaanza mara tu baada ya kumaliza kula. walikuwa wamepanga kwenda kulala Burundi na ikiwezekana usiku wa siku ya pili wawe Kahama ili kufidia muda wao. Kweli walipita Burundi kwenye mpaka na Rwanda ukiwa ni usiku wa manane.
kwa kuwa sheria za nchi zile mbili inaruhusu kutembea wakati wowote, wakaendelea na safari hadi asubuhi ya siku ya pili wakawa tayari wapo Manyovu wakisubiri kuingia ndani ya ardhi ya nchi yao waliyo zaliwa. Walikunywa chai pale wote kwa pamoja na kurejea magarini.
Safari ikaendelea kama vile ndio inaanza sasa, mwendo kwa kweli ulikuwa ni mkali sana, hadi kufikia saa 8 mchana walikuwa wakiivuka Udshirombo na sasa walikuwa wakiitafuta Kahama, hapo ndio kwa bahati mbaya wakapata ajali mbaya.
Gari lao moja ambalo lilkuwa limebeba vyombo vya muziki lilipasuka tairi na kuacha njia, likapoteza muelekeo na kuingia porini, huko likapinduka. Hakuna kifo kilichotokea wala majeruhi makubwa, bali watu wa3 waliokuwepo mle ndani ya gari lile walijeruhiwa kidogo sana.
Habari haikuchelewa kusambaa, jioni ya siku ileile, muda ambao ndio muda ambao ajali imetokea, karibu kila sehemu ya Afrika Mashariki zilipztz hzbari ile. Watu wengi walishtuka, hasa wapenda burudani wa nchi za Burundi na Rwanda, ambao wao walifanikiwa kuona burudani siku iliyopita.
Kama inavyo tambulika hapa Duniani, karibu kila sehemu watu wanao toa taarifa huongeza na chumvi kidogo, ndio ilivyo tokea hata kwenye habari ile, ilisemwa kuwa watu wameumia vibaya japo hakuna aliefariki kwenye ajali hiyo.
Watu wengi sana walishtuka, lakini Eve alishtuka zaidi, kwani vyombo vya habari vilivyo tangaza habari ya ajali ile, havikusema wala kutaja majina ya watu walio jeruhiwa, hivyo yeye akapata wakati mgumu mno.
Kwa kuwa LOVE com ilikuwa imeenea karibu sehemu kubwa ya nchi ya Tanzania, wala Victor na watu wake hawakuchelewa kupata huduma stahili, majeruhi walipata tiba ya dharula na kuruhusiwa kuondoka, Victor akamtaka Meneja wa kampuni pale Kahama asimamie mambo mengine na siku ifuatayo atume taarifa makao makuu, wao wakaondoka hadi Kahama mjini.
Wale waliokuwa wakielekea Uganda wakiongozwa na Sabrina, waliishia Biharamulo na kupitia njia ile ya Bukoba, na pale Kahama wakaishia wale waliokuwa wakielekea Nairobi. waliokuwa wakiendelea hadi Dar wakaanza kuitafuta Nzega na hatimae Singida ambapo walipanga kulala pale.
Eve alikaa na kufikiri sana, akajiona yeye ni kama mkosaji mno, inawezekana ndani ya gari lililopata ajali, alikuwepo Victor ambae yeye Eve hadi leo hii hajamuomba msamaha kwa kosa kubwa sana alilomtendea, je ikitokea siku moja Victor akafariki kabla hajamsamehe na hali ni mume wake wa ndoa kabisa, itakuwaje?
Ama yeye mwenyewe Eve akafariki bila ya kumuomba msamaha Victor ambae ni mume wake kabisa, atajibu nini kwa muumba wake? Akapata ujasiri na kuamua ni heri aende, kwani hakuna ajuae kesho, kama kuna lingine basi atalijua hukohuko, kwa leo liwalo na liwe.
Wakati Evelyn amejipanga kuondoka, wadau wa LOVE com walikuwa njiani wakiitafuta mikoa michache iliyo bakia kabla ya kuwasili Jijini Dar Es Salaam na wengine wakiwa wanazitafuta nchi zao wakiwa ni wenye furaha kwa kumaliza tamasha lao kwa amani na mafanikio.
Toyota Hilux Double Cabin, mali ya Radio ya Kigezi FM ya Nchini Rwanda, ndio gari ambayo Ever alipewa kwa ajili ya safari ya kuelekea Kahama, ndani ya gari wakiwa watu watatu, Eve, Dereva na mpiga picha wa kituo chao ambacho pia kinamiliki Televisheni.
Gari ilikuwa mwendo kasi sana, walipowasili Kahama na kuulizia, walijibiwa kwamba watu wale wanao waulizia, huenda muda huu watakuwa Jijini Dar. Eve akashanga na kuuliza kama hawajaumia sana. Jibu likawa wale watu hawajaumia kabisa ila wachache ndio walichubuka chubuka kidogo.
Ikamlazimu kukaa chini na dereva wake na kujadiliana, na mwishoni wakaamua wapige simu kwa Mkurugenzi ili kupata ridhaa ya kuendelea na safari hadi jijini Dar, maana waliambiwa waishie Kahama ambapo ndipo ilipokuwa imetokea ajali.
Mvutano ulikuwa ni mmoja, dereva akisema waendelee na safari hadi Dar, wakati Eve akisema warudi Kigali kwani walikuja kwa nia ya kuwahoji majeruhi ambao sasa hawapo na ajali si mbaya sana kama awali walivyojulishwa.
Hapo ndio uamuzi wa kumpigia simu mkuu ukahusika, na kwa kuwa alieongea nae kwanza alikuwa ni dereva, hii ilitokana na simu ya Eve kuita wakati tayari wamempigi Mkuu, hivyo Eve akampa dereva aongee na bosi wao kwa simu.
Jamaa akatumia fursa hiyo kwa kumshawishi mkuu ambae alionekana kupinga suala la kuendelea na safari, kwa kuepuka gharama.
“Gharama ya mafuta ipo juu sana, si unajua Tanzania mafuta ni bei kubwa kuliko kwetu japo mafuta yetu yanapita kwao?”
Kwanini Eve anakataa kufika Dar? Ataendelea kuikwepa Dar hadi lini? Yu wapi Ondiek? Je mkuu atashikilia msimamo wake ama atalegeza? Tuwemo tena…
Dereva aliekuwa akiongea nae akamshawishi sana mkuu wake wa kazi, akiegemea kuwa lengo la safari ni moja tu, na sasa halijatimia. Akamueleza kwa takriban dakika tano nzima huku akitoa sababu lukuki.
Hivyo hakukuwa na kipingamizi kutokana na sababu waliyoitoa, kwani dereva alisema wanataka kupata undani wa habari ile na kujua na chanzo cha ajali pia na kuwaeleza ukweli wote wananchi wa Rwanda waliokuwa na hamu ya kutaka kujua ukweli halisi.
Hivyo dereva akafanikiwa yeye kushinda, mkuu aliwaruhusu kuendelea kutokana na uzito wa suala lenyewe.
Kwa kuwachanganya zaidi waliopo Rwanda akatuma picha kwa kupitia WhatsApp za eneo la ajali na picha za gari likiwa limeharibika vibaya na Spika zikiwa zimepondeka pondeka, hali iliyo sababisha Mkuu awaruhusu kuendelea na safari hadi Dar ili awapate viongozi ambao watamueleza ukweli.
Dereva alifurahi sana kupata nafasi ile ya kwenda hadi Jijini Dar maana alikuwa na muda mrefu sana hajakanyaga kwenye lile Jiji maarufu zaidi Afrika Mashariki. Alijua akikutana na Ondiek wakiwa huko, basi watafurahi sana, maana wote walikuwa ni walevi kupindukia.
Kwa ukweli ni kuwa Ondiek aliendelea kula raha za Jiji la Dar pasina hofu yoyote, alijiachia kweli, kwani alitambua fika kuwa Victor hayupo nchini. Muda ule simu yake ikaita, alipotazama namba ile akaitambua kuwa ni ya Mkurugenzi wake wa Radio Kigezi.
Alihisi anatakiwa kurejea haraka Jijini Kigali, akapokea na kuongea na bosi wake. Maelezo aliyompa ni kwamba, Eve yupo njiani na msafara unaelekea huko Jijini Dar, hivyo anaaswa kuwapa ushirikiano kwa kipindi cha siku mbili watakazo kuwa huko na arejee nao.
Jioni ya siku hiyo waliwasili Jijini Dar Eve akiwa na watu wake wawili. walikuta tayari Ondiek ameisha watayarishia sehemu za kufikia, hivyo aliwapokea na kuanza kuwapeleka guest.
Baada tu ya kuwaonyesha vyumba vyao wale wawili, akampeleka Eve chumba anacholala yeye.
Evelyn akagoma, akamwambia yeye ana kwao, leo anakwenda kwao, litakalo tokea na litokee tu, wala hana hofu. Ondiek alijaribu sana kumzuia asiende, lakini ilishindikana, moyo wa Eve ulikuwa umeamua hivyo leo, kulala nyumbani katika hali yoyote.
Akatoka nje na kuita Taxi iliompeleka hadi nyumbani kwao ambapo wala hakupokelewa kwa bashasha. Hiyo wala haikumshitua, kwani kitu ambacho alikitegemea, alipoingia tu akapiga magoti na kuanza kulia akiomboleza.
"Umefuata nini Kenge wewe?" Mzee Dotto aliuliza kwa hasira.
"Mmh nawe muache kwanza apumzike..." Mama akamtetea mtoto wake
"Wewe ndio ulie mtuma anidhalilishe mie si ndio?" Akasema Mzee Dotto huku akisimama kumsogelea Eve ambae alijificha nyuma ya mgongo wa mama yake huku akilia.
Wazazi walibishana sana huku wakishindana, baba akitaka kumuadhibu mwana na mama akizuia binti yake kuadhibiwa. Kwa hasira ambazo tayari Mzee alikuwa nazo, akamsukuma mkewe na kuanguka, bahati mbaya aliangukia kwenye ncha ya bobo la plastiki lililokuwa na maua akapoteza fahamu.
Hapo sasa ikawalazimu wote kusahau kile walichokuwa wakishindania, wakaunganisha nguvu na kumbeba ili kumuwahisha hospitali. Walimuingiza ndani ya gari ileile ya Eve ambayo aliiacha pale kwao kabla hajaondoka, leo ameipanda tena akiwa amemshika mama yake wakati baba yake akiwa ndio dereva.
walipata huduma nzuri tu pale hospitali na bada ya nuda alizinduka na hali yake ikarejea katika hali yake ya kawaida. Waliruhusiwa kutoka na kurejea nyumbani. Hadi wanafika nyumbani, hakuna alie lizungumzia suala lolote lile hadi wanaingia vyumbani kulala, walikuwa kimya kabisa.
Kwa mara ya kwanza baada ya takriban miaka miwili ama zaidi, Eve aliingia ndani ya chumba chake kwa nia ya kulala. Hiki ndio chumba ambacho alikuwa akikitumia kabla ya kuolewa na Victor. Aliwasha taa na kusimama akikiangalia chumba chake kama ni kipya vile.
Akiwa bado kasimama, akasikia mlango wake wa chumbani ukigongwa, akasogea pembeni kidogo na kuufungua, akiwa na huzuni usoni mwake imemtawala, ikionekana dhahiri. Mama yake akaingia ndani na kumuuliza mbona hajalala, Eve alikosa jibu.
Mama akamwambia amekuja kumuangalia tu kama kalala. Eve akamtazama mama yake kwa huzuni na machozi yakaanza kumtoka, akamkumbatia mama yake na kuanza kulia huku akimuomba msamaha. Mama akamwambia
Mwanangu dunia hii ya Mungu imejaa vinywaji vingi mno na vya kila aina, kuna baridi na vikali, vipo vitamu na vichungu, lakini pia kuna vya baridi na vya moto, ila hakuna kinywaji mujarrab na kilicho bora kama maji, sawa mwanangu?” Eve akaitika tu bila kuelewa ni nini anamaanisha mama yake.
Muda huo alikuwa bado amemkumbatia, mama akaendelea
“Maji ukiyakana kwenye kuyaoga, utakutana nayo kwenye kuyanywa, sisi ni wazazi wako, ni kama maji kwako, utaweza kwenda popote lakini huwezi kuacha kurudi kwetu, hivyo sisi kama wazazi wako tumekusamehe kwa sababu ndio mtoto wao, watafanyeje sasa?” alimaliza huku akimfuta machozi.
Alichomwambia ni kuhakikisha anamtafuta Victor ambae ni mumewe na kumuomba msamaha, kwani wao pamoja na msamaha wao, hauwezi kumsaidia lolote iwapo hatopata msamaha kwa mumewe ambae ndio hasa alie mkosea. Hapo sasa ndio palikuwa hapatoshi.
Waliachiana na kisha mama akatoka kurejea chumbani kwake akimuacha Eve akibadili mavazi kuvaa ya kulalia. Sasa rasmi mawazo yake yakaelekea kwa mumewe, akajilaza na kuanza kuvuta kumbukumbu muhimu zilizowahi kupitiwa akiwa na mumewe kwenye maisha yao ya ndoa ilipokuwa na furaha.
Kumbukumbu zilimrejesha mbali sana toka alipokutana na Victor hadi sasa hapo alipo kitandani. Alihisi kupoteza kabisa mwelekeo, akaanza kuutafuta usingizi kwa lazima mana kwa hiari tayari ulisha shindikana, kila akifanyacho, usingizi uliparama.
Kuna wakati ulimpitia usingizi wa Mang'amu ng'amu na kuota ndoto ya ajabu, aliota Victor na Bill nao wakipanda ndege kuhamia ughaibuni, sasa kwa kuwa hakuwa tayari kuwapoteza ama hata kuwakosa tena watu wale wawili kwa kipindi hiki, akaamua kupiga simu kwa Victor.
"Ah! Bwana wee, liwalo na liwe, kwani mie ndio wa kwanza kukutana na majanga, hata akinitukana ni sawa tu, ni haki yake," aliwaza Eve huku akinyanyua simu na kuingiza namba ya simu ya Victor ambayo daima huwa haimtoki kichwani.
"Je kama kaibadili itakuwaje?" Akajipa moyo tu ajaribu, iwapo itakuwa inamilikiwa na mtu mwingine atamuomba msamaha na kukata simu kisha kesho ataitafuta namba kwa njia yoyote, njia ya awali aliyo ifikiria ni kumuomba mama yake kwani alijua kwamba ni lazima atakuwa nayo, kwani anawasiliana nae sana kujua hali ya mjukuu wake.
Sekunde chache mbele simu ile ikaanza kuita, ajabu alitegemea simu kuita na ilipoita akapata mshituko na kuikata kama vile hakutegemea kitu hicho. Upande wa pili Victor aliekuwa amelala akashtuliwa na muito ule wa simu ambayo hata kabla hajaipokea, ikawa imekata.
Aliinyanyua simu yake na kuiangalia tu na kuirudisha kitandani akaendelea kuchapa usingizi. Mapigo ya moyo ya Eve yalikuwa juu sana baada ya simu ile kuita na kuikata.
Akafikiri kwa muda na kuamua ni heri tu ampigie na kuongea nae maana yawezekana ikawa alimuamsha kutokana na ile 'Missed call' aliomfanyia.
Sasa akainyanyua tena simu ile na kupiga tena, safari hii iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa na Eve nae sasa hakuwa na nia ya kuikata, alidhamiria kuongea na mwenye simu ile akitarajia kuwa ni Victor.
Baada ya muda mchache, ikapokelewa na Victor mwenyewe ndie alie ipokea.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Hellow..." Kimya
"Hellow..." Kimya, alirudia zaidi ya mara 3, Victor akaitazama kama bado ipo hewani, akaiona bado ipo hewani, akairudisha sikioni na kusema Hellow tena, alipoona haipokelewi, akaikata kwa kuhisi huenda imejipiga yenyewe na mwenye simu nae hajui kama imejipiga.
Akaitazama vizuri namba ile na kukuta ni mpya kwake, akaamua kuipiga yeye sasa, ikaita kwa muda mrefu iliita na hatimae ikakata bila kupokelewa, Victor sasa akaona huu ni utoto, akazima simu na kuchapa usingizi.
Eve alishindwa kuongea kwenye simu aliyopiga mwenyewe kwa sababu sauti ya Victor ilimkumbusha mbali sana, alikumbuka vitu vingi mno, hivyo wakati Victor anaongea, yeye akili yake kitambo ikawa imehama.
“Mpenzi wangu, ukiwa name, utakuwa sehemu salama na kwa wakati sahihi, hivyo utakuwa bora wakati wote, kitu pekee ambacho naweza kukuhakikishia ni amani, furaha ni kitu ambacho una uhakika wa kuwa nacho wakati wote, sitachoka kukujali,” ni sauti ya Victor iliyojirudia masikioni mwa Eve kama mwangwi ambao ulielekezwa kwake, hakusema lolote Victor, bali ni mawazo tu ya Eve.
Nae hapo alikumbuka kauli aliyompa siku wanavishana Pete, alimwambia kuwa jinsi alivyo na thamani maishani mwake kila siku, hawezi kumfananisha na madini ghali, kwani madini yanapochimbwa huisha.
Lakini pia hawezi kumfananisha na Tunda kwa sababu matunda ni ya msimu, bali yeye anamfananisha na damu mwilini mwake, ambayo bila yeye maisha yake si chochote. Alivyokumbuka kauli yake, mwenyewe akajiona msaliti, maana sasa ni miezi kadhaa yupo mbali nae na maisha yanaenda.
Hivyo hata ile simu aliyopigiwa na Victor aliona si vema kupokea kwani alihisi kama hakuwa na cha kuongea kwa sasa, acha ajipange upya kwanza. Akajiamua mwenyewe kuwa atamtafuta kwenye mtandao pindi itakapofika asubuhi.
Kwa wakati huu ambao tayari ilikuwa imefika saa 9 usiku alipojaribu kuutafuta usingizi,hakuweza kuupata bali ni taswira za maisha yao ya nyuma tu ndio zilimtawala.
Kila alipojaribu kujitoa kimawazo ili angalau aweze kuuvuta usingizi, lilikuja wazo jipyaa. Akawaza kuwa ukweli hukupa kujiamini na kukufanya uwe huru kifikra na kimwili pia.
“Bora kujua ukweli kuliko kuka ukihadaika, unaweza ukajua Napata kitu Fulani kumbe unajidanganya, lakini ukifunguka utaujua ukweli na kama ulikuw ukijihadaa italazimu kuukubali ukweli,” baada ya wazo hilo sasa, aliweza kuhisi usingizi ukimnyemelea.
Ilikuwa ni karibia kabisa ya alfajiri, hapo sasa ndio usingizi ulikuja na kujikuta amelala vizuri bila njozi wala maroroso yoyote hadi asubuhi ya siku iliofuata.
Aliamka saa 12 asubuhi kitu cha kwanza kukifanya mara tu alipoamka, ilikuwa ni kumtafuta hewani Victor sasa akiamini yupo tayari kuongea nae. Bahati mbaya simu ya Victor muda ule ikawa imezimwa, akanyanyuka kwenda kufanya mambo mengine kwanza.
Moja ya kumbukumbu kubwa sana aliyoamka nayo asubuhi ile ni motto wake Bill, alitamani mno kumuona, hasa baada ya kukuta picha kubwa pale kwenye ukuta wa sebuleni ambayo jana wakati akiingia wala hakuweza kuiona, lakini leo wakati akifanya usafi ndio aliiona.
Aliishika na kuiangalia kwa huzuni, alihisi kabisa chozi la upweke likitoka ndani ya jicho na kuelekea kubusu mashavu yake ambayo yalionesha kukonda ghafla kutokana na kitendo cha Ondiek.
Kilichofuata pale ni kukumbatia picha ile na sasa dhahiri machozi yakatengeneza njia hadi nje ya macho na akayawahi yasidondoke kwa kujifuta kwa sehemu ya nguo aliyovaa.
Palikuwa na mtu akimtazama, yeye Eve hakumuona, maana akili yake haikuwa pale sebuleni, ilikuwa ipo umbali mrefu toka kilipo kiwiliwili chake, roho ya uzazi sasa ilimrudia na kumkumbuka zaidi mwanae ambae alikuwa na muda mrefu hakaweza kuiona hata picha yake seuze yeye mwenyewe.
Mtu aliekuwa akimtazama alikuwa ni baba yake Eve, muda huu alikuwa akitoka kwenye uwa wa nyumba yake alipokuwa akipalia palia majani madogo madogo ambayo yalikuwa yameota na akiwa anarudi ndani ili kwenda chumbani mwake, ndio akamuona mwanae akilia kimya kimya.
Akamsogelea na kumshika bega moja, Eve akageuka huku akifuta machozi kwa mkono mmoja huku mkono mwingine ukiwa bado umeikumbatia picha ya mwanae kifuani.
Icho lake jekundu, likakutana na sura ya majonzi ya mzazi, ilionesha kabisa kuwa na huruma kwa mwanae, mzazi alihisi kabisa ni kiasi gani motto wake anaumia kwa sababu ya kutokuonana na mwanae.
Eve alipokutanisha macho na baba yake akaanza kulia kwa sauti na kupiga magoti akiomba msamaha, baba yake akamnyanyua na kumketisha kwenye sofa huku akimtaka anyamaze kulia na kuanza kumpa maneno ya busara
“Mwanangu hakika ulitukosea sana sisi wazazi wako, lakini kwa kuwa umejua kosa lako, basi acha tu tuyamalize kwa upande wetu lakini tambua kuwa wakati unaondoka huku wewe ulikua ni mke wa mtu, hivyo jambo la kwanza ni mumeo.”
Tayari Eve alikuwa amenyamaza na sasa alikuwa kimya akisikiliza tu asemacho mzazi wake.
“Eveline, maisha hayabahatishwi, yanapangwa! Ulikosea awali, lakini sasa panga maisha yako upya kwa kusisistiza kazi na si mapenzi, kwani kazi inapanga mapenzi na maisha, lakini mapenzi hayapangi kazi wala maisha..,” Eve akanyanyua sura kumtazama baba yake kwa mara ya kwanza.
“Mapenzi yako mwenyewe kwa Yule Ondiek yalisababisha uharibu maisha yako na kupoteza kazi yako, kwangu mimi Victor alikuwa ni maisha yako, yaani ni zaidi ya mapenzi, lakini kazi yako nayo ukaikosa, wakati huwa haurudi nyuma, umri wako nao unakwenda, kuna mengi unatakiwa uyafanye kwa sasa Evelyne..,”
Eve akazidisha umakini, mzee nae alipotambua hilo, akamwambia
“Unapaswa kumtafuta Victor haraka iwezekanavyo na uongee nae, najua ni vigumu sana kumshawishi, ila huna budi kuonana nae tu kwa sababu ni lazima na hakuna namna,” alimaliza baba yake na kumtaka akaendelee na kazi zake zingine
Basi akamshukuru mzazi wake, nae akanyanyuka na kwenda kumsalimia mama yake na kisha kafanya yote anayopaswa kuyafanya asubuhi ile, ikiwepo suala la kifungua kinywa. Alipoiandaa mezani wakati akiwasubiri wazazi wake, akachukua simu yake na kumpigia tena Victor.
Jibu likawa ni lilelile tu, kuwa namba ile ya simu haipatikani.
Akadhoofu ghafla na kuhisi kama kuna jinamizi pale kati. Lakini akapata wazo mbadala. Wazo lilikuwa ni kumtumia ujumbe mfupi wa maneno ambao pindi atakapo upokea, ndio nae hapo hapo ampigie na kuongea nae.
"Huyu mwanaume hulala hadi saa 3 pindi anapokuwa hana jambo la muhimu, sasa ni heri nifanye hivyo ili kumuomba kuongea nae, sijui atakubali niongee nae faragha ili nimuombe msamaha?" Aliwaza Eve huku wazazi wake wakimsemesha kutokana na kuwepo pale kimwili tu.
Sarah, msaidizi wa Victor alikuwa bado akiishi pale pale kwa Victor pamoja na kuwa Eve ndie alie muajiri, aliona muda umepitiliza sana ikamlazimu sasa amuamshe bosi wake, maana haikuwa kawaida kulala vile. Aliamka na kumshukuru Sarah na kumwambia alichoka sana siku iliyopita ndio maana amelala sana.
Victor aliwasha simu na kuelekea maliwatoni kwenda kujiswafi, akiwa huko alisikia simu yake ikiingia ujumbe mfupi. Hakujali alijua hiyo msg ataikuta tu, akaendelea kuoga huku akiimba wimbo wa Barua toka kwa Kundi la Daz Nundaz.
Akatoka bafuni na kubadili mavazi na kuelekea Mess ili kufungua kinywa alicho andaliwa na Sarah. Alipoanza kunywa chai ndio akakumbuka kuwa kuna ujumbe ulikuwa umeingia kwenye simu yake, akanyanyuka mwenyewe na kufuata simu yake japo alikuwa amemuita Sarah.
Kipande cha yai kikiwa mkononi akamwambia Sarah basi akaendelee na kazi zake, akaifuata simu chumbani na kurejea huku akiwa na simu mkono wa kushoto akisoma ujumbe ule mfupi wa maneno aliotumiwa.
Ujumbe ulisomeka hivi; 'Samahani Victor ninajua kuwa mie ndio sababu ya wewe kufunga simu yako usiku uliopita, nina shida nawe, je ninaweza kukuona wapi? na saa ngapi? Ni suala muhimu. Ni mimi MB' Victor alijitahidi sana kulitafuta jina lile la MB kichwani mwake.
Hakufanikiwa kuijua na hata namba alipoitazama nayo wala hakuitambua, akaamua nae apige namba ile aili amjue mtu yule ni nani, bahati mbaya na namba ile nayo sasa ikawa haipatikani, hivyo nae akadharau na kuendelea kunywa chai.
Baada tu ya Eve kutuma ujumbe kwa Victor, Ondiek alimpigia simu na kumuuliza ni wapi alipo, kwani wao wanataka kumfuata ili kutekeleza kile ambacho kimefanya wawepo pale Dar. Eve akamwambia kuwa yeye hayupo tayari kwa hilo na kumtaka Ondiek atekeleze na hao wengine alionao na watakapo maliza majukumu hayo watamjulisha.
Ondiek nae hakuwa tayari kulifuatilia swala lile kwani bado aliuwa akimuogopa mno Victor na sasa alisha jua kwamba amerudi, yupo Jijini, sasa atakwendaje kumuhoji? Hivyo alitaka kumtumia Eve ili kupata habari zote bila ya yeye kushiriki kwa aina yoyote.
Hicho ndio kitu kikamlazimu amsumbue sana Eve kwenye simu akimtaka wamfuate kwao ili waendekuwatafuta na kuwahoji. Na kwa kuwa Eve hakuwa tayari, akaamua kuchukua hatua hiyo ya kuzima simu kwa muda ili kuzikwepa kero za Ondiek.
Ommy Bazo na familia yake waliwasili Kenya wakiwa salama kabisa pamoja na wasanii waliokuwa nao. Leo ndio Ommy akashika simu na kumpigia Victor na kumueleza kufika kwao salama. Alimshukuru Mungu kwa kufanikisha lile kisha akaongea na Bill kidogo na kuagana nao
Victor alipomaliza kunywa chai na kuongea na Ommy, hapo ikwa tayari ni saa nne na nusu, akajaribu kupiga tena namba ile ambayo tayari aliihifadhi kwenye simu yake kwa jina la MB, bado akaambiwa haipatikani, hivyo nae akaamua kuijibu sms kifupi tu.
'Njoo ofisini, ndio naenda huko, fika kati ya saa 6 na saa 7 ama jioni saa 10 na nusu.' Hakutaka kufafanua vizuri, maana aliamini kwamba mtu huyo anamfahamu vema, ndio sababu alimtaja hadi jina lake. Akamuaga Sarah na kutoka kuelekea kazini.
Akiwa njiani alimpigia simu Sabrina na kumuuliza kuhusu safari yake na kundi lake la wasanii kama walifika salama, alishukuru Mungu kuwa walifika salama wote na hata siku ile amekutana nao baadhi asubuhi ili kujipanga kwa tamasha la pale Kampala ambalo analiandaa yeye.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Waliongea hadi Victor anaingia ndani ya ofisi yake. Hata Katibu Muhtasi wake alimsalimia kwa ishara tu, maana mazungumzo yalikuwa yametawala tena yakiwa ni matamu mno. mwanzo yalianza kwa kuzungumzia biashara, lakini yalipokwenda sasa...
Sauti za kimahaba zilitawala mno maongezi yao, hadi ikamfanya Victor sasa apange safari ya ghafla tena siku ileile kuelekea Uganda kushiriki kwenye maandalizi ya tamasha, lakini lengo likuwa ni kwenda kwa Sabrina. Akamuahidi kuondoka Bongo siku ileile kumfuata.
Victor alipoingia ndani alikuwa ameketi kwenye kiti chake akiwa miguu ameiweka juu ya meza akiongea na mpenzi wake ambae alifurahi kwa ahadi ile ya kwenda kule. lakini kabla hawajaendelea zaidi, simu ya mezani ya pale ofisini kwake ikaita.
Wakaagana kwa ahadi ya kuonana jioni, kisha Victor akapokea ile simu nyingine
"Hellow!"
"Ndio Boss, kuna mgeni wako hapa nje, sijui nimruhusu?" Ilikuwa ni sauti ya Secretary wake.
"Ni nani?" Aliuliza Victor huku akishusha miguu chini na kujiweka vizuri kwenye kiti
"Anasema anaitwa ni MB."
"Sawa, mruhusu aingie, kisha nenda kwa wakala wetu kanichukulie tiketi ya ndege ya kuelekea Uganda ya kwenda na kurudi, sawa eenh?" Aliagiza Victor
"Sawa Boss, lakini umeisha wapigia?"
"Ndio Martha, nimewaambia, nichukulie tu tiketi, kisha utanikuta hapa hapa mi ninakusubiri, sitatoka kwenda popote, ila mwambie Mlinzi asiruhusu mtu yeyote kuingia humu ndani ya ofisi hadi wewe utakaporudi."
"Sawa Boss." Alijibu Martha kwa heshima zote.
“Iwe ya kuondoka leo na kurejea kesho kutwa,”Alisisitiza boss Victor.
“Haina tatizo mkuu,” Alijibu Martha huku akimruhusu MB aelekee zilipo ofisi za Victor.
Mlango ulipoguswa, ulimpa shauku kubwa Victor ya kumjua huyo MB ni nani, sasa mlango ulipofunguliwa alieingia hakuwa mtu mwingine bali ni Eve. Eve alijiita vile akiwa amefupisha majina ya Mama na lile la Bill, Mama Bill akapata MB.
"Umefuata nini hapa? Sema haraka nikusaidie nini?" Maswali yalimtoka Victor kwa hasira na kumfanya anyanyuke kwa ghafla, kwani alipandwa na jazba mno, hata kabla Eve hajajibu kile kilichompeleka pale, Victor akaendelea
"Ulinitenda vile sikukufanya chochote, sasa leo umeamua kuja ofisini kwangu, toka nje, nasema toka." Alimwambia atoke baada ya kumuona akiketi kwenye kiti.
"Samahani mume wangu, nipo hapa kwa ajili ya kukuomba msamaha mume wangu." Alisema huku akinyanyuka kwenye kiti alichokuwa ameketi na kumsogelea Eve aliekuwa amesimama bado, alipoona Victor anakuja, akapiga magoti huku akilia kwa uchungu kwa sauti ndogo tu.
Pale alipokuwa amepiga magoti ilikuwa ni usawa wa mlango, sasa Victor alitaka kutoka kwa nia njema tu, lakini Eve alikuwa njiani akiwa amepiga magoti, Victor akamwambia asogee, Eve nae hakuwa tayari Victor atoke na kumuacha peke yake mle ndani na hali yeye Eve ikiwa amemfuata yeye.
Kutokana na hasira alizokuwa nazo Victor kutoka pale ilikuwa ni kama njia yake pekee ya kujiepusha na shari ambayo alihisi inaweza kutokea, akamtaka ampishe njiani, bado Eve hakukubali, Victor akamsukuma kule na kuangukia kwenye sofa la pale ofisini kwa ajili ya wageni, ambalo alikuwa amelikalia hapo awali.
Eve alitoa kelele kali iliotokana na maumivu ya kujigonga, kelele ambayo ilimshitua hata Secretary wa Victor aliekuwa akikusanya vitu vyake kabla hajatoka.
Akasogea karibu na mlango wa ofisi ya bosi wake na kuugonga.
Victor ndio aliekuwa karibu na mlango, hivyo akaufungua. Aliegonga alikuwa ni Katibu wake, hata kabla hajasema chochote Victor akaanza kumkaripia
"We Martha, we ni mwendawazimu? Kwa nini hukuniambia kama huyo MB ni huyu Mbwa?" Masikini Victor amesahau kuwa huyu Secretary ameajiriwa miezi kadhaa iliopita, kipindi ambacho Eve alikuwa hayupo kwenye mikono ya Victor wala hakujua hata ni wapi alipo, hivyo asingeweza kumjua, kwani hakumuona wakati wakiwa pamoja pale kazini.
"Samahani Boss, mie simfahamu huyu." Alijitetea Martha, Victor akamuelewa na kumwambia
"Haya, mtoe nje sasa hivi..." kisha kamgeukia Eve na kumwambia
"We bundi toka nje, unanisikia?" Eve aliendelea kulia kwa kwikwi na kusema
"Sawa Victor, basi mie ninaomba nimuone hata mwanangu," Aliomba Eve huku akimtazama Victor, nae akamjibu kwa kejeli, huku akiokota kalamu yake iliyokuwa imeanguka chini
"We una mtoto hapa? Kama unae yupo wapi? Hebu toka nje kabla sijakubutua." Victor akasema huku akifungua mlango kumruhusu Eve atoke nje, Eve hakuwa tayari, akajibu
"Mimi sitoki hadi uniletee mwanangu nimuone." Leo Eve alikuwa amedhamiria liwalo na liwe.
"Ahaa! Unajidai kiburi si ndio?" Akasema huku akiuacha mlango unajifunga, akamuelekea Eve kule aliposimama na secretary wa Victor.
Kwa mara ya kwanza sio Secretary tu alie muona Victor amebadilika na kuwa kama chui aliejeruhiwa, bali hata Eve mwenyewe alishangaa kutokana na mabadiliko aliyo yaona ghafla kutoka kwa Victor.
Muonekano wa Victor ulionesha kabisa hakuna tena salama, maana Martha na hata Eve walisikia kauli aliyokuwa akiisema huku akisogea
“Mwenyewe uliamua kuwa njiwa ili usinyonyeshe, iweje leo uone wivu kwa Ng’ombe anaekamuliwa? Sasa ngoja nikuoneshe ni kwa nini kuku hatoroki nyumbani,”
Victor alimfuata Eve na kumnyanyua akampa kofi moja zito sana la shavu, wakati akianguka chini, akamshindikiza na teke moja kali sana la mbavuni, Secretary, akasogea zaidi kwa nia ya kuamua, nae akasukumwa kule na kujigonga kwenye meza ya bosi wake.
Pale mezani ndio akapata akili ya haraka, akanyanyua simu na kumpigia mlinzi kumuita ndani haraka aje kutoa msaada. Wakati huo Victor aliendelea kutoa kipigo kikali sana kwa Eve ambae sasa alikuwa hoi kutokana na kichapo cha maana alicho kipokea kwa muda mchache tu.
Damu ilikuwa ikimtoka puani na mdomoni huku sehemu za kichwani pakiwa pamepasuka. Askari wawili waliingia wakiwa wameongozana na wafanyakazi wengine wawili ambao walikuwa wamesikia kelele zile za kipigo na kumzuia Victor asiendelee kutoa adhabu.
Mlinzi mmoja wa kiume na wafanyakazi wale wawili wakamzuia Victor kisha Martha na mlinzi mwingine wa kike wakamtoa nje Eve hadi garini kwa nia ya kumuwahisha hospitali, ambayo haikuwa mbali sana kutoka pale ofisini kwao.
Akiwa bado na jazba tele, akajitoa kwenye mikono ya wafanyakazi wake na kulegeza tai, kisha akakaa kwenye kiti chake na kuagiza yule mfanyakazi wake mmoja amfungulie friji pale pale ofisini na kumpa maji ya kunywa, akatekeleza na kumpatia.
Walitaka kuhoji ni kipi kilichoendelea lakini wote waliogopa, baada tu ya kumpa maji wakatoka nje wote.
Hakukaa sana ofisini akaamua ni bora atoke mwenyewe ofisini kuelekea kwa wakala wa usafiri wa ndege kuendea tiketi yake ambayo tayari alikwisha ona Martha hawezi tena kuifuata kutokana na kile kilicho tokea pale.
Eve hakukaa sana pale Zahanati, hata Secretery nae akashangaa, akahisi huenda Eve anaogopa gharama, akaongea nae
"Anti vipi? Mbona tiba bado haija kamilika? Wewe wala usiwe na shaka, pesa italipwa na kampuni..." Hata hivyo kauli hiyo haikumfanya Eve kubadili maamuzi yake, akashika msimamo wake wa kuondoka, akawashukuru na kutoka nje ambapo aliita Taxi na kutokomea mbele anapojua mwenyewe, akiwaacha Martha na wengine wakiwa na mshangao.
* * * * *
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment