Simulizi : Anti Ezekiel
Sehemu Ya Nne (4)
“Ufe wewe ili mama ateseke huko bila kuwa na msaada wowote, kufa kwako ni kumkimbia Eva mtoto wako, aibu ilioje Sam. Unawaza kufa, basi sikuwa na haja mimi ya kumuua yule askari kule porini, sikuwa na haja yoyote ya kujiingiza katika utata huu, ni heri ungeniacha nikiwa nauza bajia na sambusa zangu kuliko huku uliponileta. Ungeniacha sasa. Haya si unataka kufa!!!
Naomba unirudishe uliponitoa, nirejeshe stendi na kapu langu la bajia na sambusa lakini usisahau kitu kikubwa kabisa. Naitaka amanmi yangu ambayo umeipoteza!!!” Mama lao Jojina alikuwa amekasirika haswa. Lakini sio hasira zilizozungumza, aliyoyasema yote yalikuwa kweli tena kweli tupu. Nikakumbwa na aibu nikatamani kuomba msamaha lakini Jojina hakuwa tena pembeni yangu!!! Alikuwa ameelekea chumbani.
Nililazimika kumfuata, ikawa zamu yangu kumbembeleza kutoka katika kilio chake.
Nilimsihi sana, hatimaye akanikumbatia miili yetu ikagusana na kila mmoja kujikuta akivuta pumzi ya mwenzake. Baridi kali la Iringa likatusababisha tutamani kuendelea kukumbatiana.
Kilichotokea baada ya hapo hakuna aliyekitazamia kuwa kitatokea.
Tulikurupuka asubuhi kila mmoja akiwa utupu!!!
Hakuna aliyeanzisha mazungumzo juu ya ajali iliyotokea usiku.
****
SIKU yetu ilianzia nyumbani kwa mzee Madati, tulikuwa tunajaribu bahati yetu kama akili zake zitakuwa zimekaa mkao aweze kutueleza ni kitu gani anafahamu kumuhusu huyo Ezekiel.
Utulivu pale nyumbani uliniweka katika wasiwasi, kitu cha kwanza kuhisi ni kwamba mzee Madati anauwezekano mkubwa wa kuwa marehemu ama mahututi zaidi ya awali.
Majirani wakatueleza kuwa familia nzima imealikwa katika kituo kimoja cha redio pale Iringa mjini kwa ajili ya mahojiano juu ya utata wa afya ya mzee wao. Wakatutajia na jina la kituo hicho cha redio. Jojina alikuwa anakifahamu, tukataka kwenda huko lakini wazo la kujiingiza matatani likatuingia.
Tukafikia maamuzi ya kurejea kule Gangilonga mafichoni, kama kawaida tukiwa na tahadhari kubwa kabisa. Tukanunua magazeti mbalimbali kwa ajili ya kujipatia taarifa zozote kuhusiana na mkasa wetu ili tujue adui amejipanga vipi kutuangamiza ili tuzidi kujihadhari.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Majira ya saa moja usiku, tukiwa na amani kabisa tukarejea tena nyumbani kwa mzee Madati ili tuweze kujua ni kitu gani wamehojiwa redioni, na pia kama hali ya mzee ni njema tuweze kuzungumza naye.
Umati wa watu ukatuvutia na kutuweka katika umakini mwingine.
Askari!! Ndo kitu cha kwanza nilichowaza na kumshirikisha Jojina, tukaishi kimashaka eneo lile. Taratibu kwa kupitia upande usiokuwa na watu wengi tukafanikiwa kufika jirani na umati.
Kweli tulikuwa sahihi, walikuwa ni maaskari lukuki wameizunguka ile nyumba. Umati wa watu ukifanya minong’ono mingi kila mmoja na lake.
Mnong’onaji mmoja akanivutia zaidi kumsikiliza.
Akawa anamtuhumu mama Sadiki, mama nisiyemfahamu kuwa ni yeye ameyafanya haya. Lakini mwenzake akampinga na kusema kuwa mama Sadiki amesafiri kwenda Mbeya hiyo ikiwa siku ya nne.
“Kwani kila sumu lazima ikuue hapohapo wewe jamaa yangu vipi wewe.” Alizidi kusimamia msimamo wake.
Akili ikafyatuka kusikia kauli ya huyo bwana ambayo ilionekana kuwa tatanishi lakini yenye kuaminika katika kichwa chake.
“Sikieni jamani, kama kuna anayemjua muuaji askari wale pale akawaeleze sio kutusumbua huku sisi tusiokuwa na msaada wowote.” Mzee mmoja wa makamo akatoa karipio, yule mnong’onaji akatulia kimya asiseme kitu lakini akirusha mikono huku na kule kama anayenyimwa haki zake za msingi.
Jojina alikuwa kama hasikilizi lolote lakini ghafla akamvuta yule bwana aliyekuwa akirusha mikono huku na kule.
Kisha akanivuta na mimi. Tukawa tumejitenga!!
Jojina akajifanya na yeye anaamini kuwa mama Sadiki anaweza kuwa nyuma ya haya, yule bwana akafurahi kupata wanaomuunga mkono.
“Yaani mimi nimewasikiliza redioni wote wakiwa na afya tele hata huyu mzee Madati aliweza kuongea, sawa alikuwa haeleweki na maneno yake hayo ya Ezekiel sijui kitu gani lakini alikuwa mzima wa afya, sasa wanafika nyumbani mzee anafia kitandani, mke wa kwanza anafia bafuni, mwingine akaanguka ghafla tu uani. Mama Sadiki hayupo!! Na hao wanaodai amesafiri, safari gani ya ghafla hivyo kama sio kujitafutia sababu za kuonekana hausiki?
Tangu mwanzo mimi nilisema kuwa huyu mama kisa ana mtoto wa kiume anataka arithi mali za mzee Madati kinguvu. Mtoto mwenyewe sio wa Madati wala nini!!! Ameiteketeza familia ya watu jamani!!!” alilalama bwana yule kwa uchungu. Hakujua kama anatupa faida kubwa sana kujua ni kitu gani kinaendelea.
Kulisikia jina Ezekiel hapohapo nikaikumbuka kauli ya siku ya kwanza kabisa aliponiambia.
UKIMJUA EZEKIEL NA WEWE UNAPOTEA.
Mzee Madati na familia yake ikawa imepotea kwa kumtaja Ezekiel.
Huyu mtu ni nani hadi awe amesambaa kila mahali, na kwani yeye ni nani hadi asitajwe?
Sura yake ipoje kama si yule aliyejifia kitandani Dar es salaam.
Swali gumu kupita yote kati ya yale tuliyowahi kujiuliza.
Miili mitatu ikaondolewa usiku ule na kupelekwa katika hospitali ya wilaya.
Tukajiondokea mapema sana ili kukwepa kuanza kuhojiwa iwapo kuna lolote tunalojua, maana kuna baadhi ya watu walianza kututambua kama ndugu wa karibu wa familia ile.
Ndani ya chumba chetu cha kule mafichoni kila kitu kilionekana kuwa shaghalabaghala. Jojina alikuwa amechoka na mimi nikiwa hoi vilevile. Adui yetu alikuwa ametupiga mapigo makali mfululizo bila sisi kujibu lolote.
Mbaya zaidi ni kwamba hata sisi tuliojua kiasi juu ya Ezekiel tulitakiwa kuuwawa kama ni kweli kila anayetaka kumjua lazima apotee.
Jojina alijaribu kuweka mezani mikakati kadhaa ya kujaribu kukabiliana na huyo bwana wa kujiita Ezekiel ma lolote lile kuhusu Michigani. Tukaamua kujisahaulisha juu ya Anti Ezekiel ambaye niliamini kuwa alikuwa mtu mwenye utata zaidi kupata kuonekana machoni pangu na kisha kutoweka ghafla.
Akiwa mzima, akiwa kitandani maiti na kisha akiwa muuaji Iringa!!
Muuaji asiyeonekana.
SALAMU KUTOKA DAR ES SALAAM
MAAMUZI aliyoyapitisha Jojina ni kugawana majukumu, kujificha Iringa tu haina maana yoyote ile. Kwa sababu mimi nilikuwa nasakwa sana jijini Dar es salaam na yeye akiwa anajulikana Iringa, akaamua kuniacha mimi Iringa na yeye akimbilie Dar es salaam kuangalia iwapo mpango aliokuwa ameupanga utaweza kuleta mafanikio yoyote.
Niliibariki safari yake, kama kawaida akajiweka katika mavazi ambayo yataubadilisha muonekano wake.
Akajihifadhi katika baibui jeusi!!
“Sam, ishi kwa tahadhari, usikae hapa kila siku, watakusoma na mwisho watakudaka kama kuku. Nadhani sina haja ya kukukumbusha juu ya hatari inayotukabili mbele yetu, usilemae. Pesa unayo lala hotelini, ikibidi wakati mwingine nenda Mbeya huko, kimbia Morogoro kidogo.
Wewe na mimi ni wakimbizi. Tusikae kama watu huru kiasi hicho!!” alinisihi mama lao, Jojina alfajiri wakati akiondoka kuelekea Dar es saalam kujaribu kutimiza mipango aliyoiita mipango makini.
Jojina akaniacha mpweke katika ardhi ya Iringa, ardhi inayosadikika kuwa ina mahali panaitwa Michigani ambapo nd’o kuna utata unaotakiwa kutatuliwa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
****
MAJIRA ya saa nne usiku nikapokea simu ya kwanza kutoka kwa Jojina, akanielezea kuwa amefika salama na muda ule naongea naye tayari alikuwa hotelini.
Wakati nataka kumpa pole juu ya safari yake, akanicheka kidogo kisha akaniambia nimpe pole ya mizunguko maana tangu saa kumi na moja jioni alikuwa jijini Dar.
Mizunguko ipi tena huyu mwanamke ama kwa mahawara zake tena.
“Sam, nilikuja Dar es salaam kufanya kazi na sio kulala. Niliposhuka Ubungo kitu cha kwanza kama ulivyonielekeza kuwa mzee Matata anaishi Shekilango, niliamua kuitafuta nyumba yake muda uleule. Bahati nzuri kama ulivyonielekeza kuwa huyo mzee ni maarufu sikuhangaika sana kuipata nyumba anayoishi. Nadhani umaarufu wake umekuwa maradufu!! Kisa kilichokuza jina lake zaidi ni kuchanganyikiwa na kuwa anaongea peke yake barabarani baada ya mtoto wake wa kike anayempenda kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Wamemtafuta kwa kila namna lakini hawajampata!! Kesho nitaenda kuitembelea familia hiyo ili niweze kuanza ule mkakati ambao nilikwambia…..” Anitha alimaliza kuongea, nilishangazwa sana na uchapaji kazi wake mkubwa kiasi kile. Wakati mtu mwingine angefika na kupumzika yeye alikuwa ameingia moja kwa moja katika jambo lililompeleka huko.
“Jojina, naogopa kukupoteza tena naogopa sanma. Ujue ni wewe uliyebaki katika maisha yangu ambaye naweza kukuamini. Niite muoga niite mdhaifu lakini nasema ukweli kuwa naogopa sana kusikia jina Matata. Asije kukuingiza matatani Jojina, yaani usiporudi huku nikwambie kitu kimoja tu. Sitajali kama umekufa ama nini. Mimi ni heri nijiue Jojina. Sitakuwa na nguvu tena za kupambana….” Kabla sijamaliza akanikatisha, “Sam, ukinitia uoga basi yatakuwa kama usemavyo, acha niende na ule mkakati. Kumbuka ni mkakati ambao nimetumia masaa manne kukuelezea na ukakiri kuwa umenielewa Sam. Kama hukunielewa ulimaanisha nini kunibariki nikaondoka huko.
Sasa Sam ni hivi kitu kimoja naomba nikwambie, mkakati huu sitaachana nao, na kama nikishindwa na kuingia matatani, tambua kuwa ni wewe upo nyuma ya haya yote. Wakiniua jua kuwa na wewe kwa maneno ya mdomo wako umechangia, wakinitesa na kuninyima uhuru basi upo pia katika shutuma hizi.
Na pia kama simulizi hiyo ya mwanangu Justin kuwa yu hai mafichoni pia ni kweli basi baya lolote watakalomtenda ni juu yako wewe na si mimi Sam….
Kitu unachotakiwa kufanya kwa sasa ni kuniombea tu yasitokee hayo yote…..nadhani umenielewa vyema kabisa Sam… na usinipigie simu tena kuniambia mambo yako ya kipuuzi puuzi….hujui thamani ya mama yako, mkeo na mtoto wako wa kumzaa Sam… hivi umerukwa akili Sam eeeh!!” Jojina alizungumza haya kwa hisia kali na baada ya hapo akakata simu.
Nilibaki katika zizimo nisijielewe ni mkasa gani huu unaoendelea kunikabili katika maisha yangu. Nikabaki kuumia nisitambue kama siku moja maumivu haya yataisha ama la!! Maana sikuwa naupata unafuu badala yake nilikuwa mtu wa janga hili likiondoka linaibuka jingine!!
Sasa nikaziona dalili zote za kumpoteza Jojina.
Jojina alikuwa katika mlango wa kutokea na kisha kukaribisha maumivu makali katika moyo wangu!!
Jojina alikaribia kabisa kuufunga ukurasa wa mwisho wa maumivu yangu huku nikiamini kuwa bila yeye basi tena sitakuwa na thamani zaidi.
Wakati huu ni moyo tu ulibaki kuuma, machozi yalikuwa mbali nami.
Nikasimama imara tena na kuilazimisha akili yangu kuwa machozi si tiba ya mkasa huu ninaopitia, ni lazima nichakarike ili niweze kuupata mwanga. Kumtegemea Jojina kwa asilimia mia ni kujitafutia msongo wa mawazo pale mambo yatakaposhindikana.
Nikazikumbuka harakati za Anitha punde tu baada ya kuwasili Iringa kisha nikayakumbuka na maneno yake. Na mwisho nikajionya kuwa nikilemaa nitapoteza kila kitu.
Nikalala nikiwa na wazo moja tu!! Jojina anapiga hatua Dar es salaam nami napiga hatua Iringa!!
Haba na haba hujaza kibaba!!
****
**JIFUNZE… Kutojiwekea matumaini ya asilimia mia moja katika jambo, naam! Ni vyema sana kuamini lakini si kuamini kupita kiasi maana jambo ulilolitarajia kwa asilimia mia moja likishindikana waweza kujihisi wewe ni mtu mwenye mikosi kupita wote duniani.
Matumaini ya asilimia hamsini kwa hamsini ni bora zaidi kuliko asilimia mia isiyo na uhakika…..
George Iron, 2012
MSAKO
Niliamini nikimshirikisha Jojina juu ya harakati zangu za kwenda kwenye kile kibanda atazidi kuniona wa ajabu na nisiyejua kitu gani ambacho ninafanya.
Kibanda hicho hakuwa akikipa nafasi hata kidogo kuwa kinaweza kuwa na mwqanzo wowote wa kutufumbua macho juu ya siri hii. Hata mimi binafsi sikuwa na imani tele juu ya kibanda kile lakini ningeendelea kulala ndani kila siku? Ningeendelea kumtegemea Jojina kwa kila jambo!
La!! Ni heri mtembea bure kuliko mkaa bure, wengi wamewahi kutembea bure na mwisho wakaokota pesa.
Nikajionya pia kuwa wapo wanaotembea bure na mwisho kujikwaa barabarani huko na kupoteza kucha za vidole vyao!!!
Nikaamua kuwa mtembea bure!!
Saa tatu asubuhi ilinikuta nikiwa natazamana ana kwa ana na kile kibanda kilichoandikwa Michigan, sikujua ni kipi kitafuata baada ya mimi kuwasili pale lakini nilienda nikiamini yawezekana ni harakati za kuusogelea ukweli.
Ukweli ambao utaniweka huru mimi na watu kadhaa wanaonizunguka!!
Hapakuwa na mabadiliko kama tulivyokiona siku ya awali, kwa mbali nilimuona bwana Massawe ambaye ndiye tulimwona siku ya kwanza akiwa amejikita katika kufagia eneo lililopo mbele ya kibanda chake, nikapiga hatua moja baada ya nyingine hadi nikakifikia kibanda kile, nikalitazama vyema lile neno Michigan. Hakika mwandishi alikuwa anatania ama la! Hakulipwa pesa ya kutosha aweze kulisanifu jina lile.
Halikupendeza kulitazama!! Ni kama liliandikwa ilimradi tu limeandikwa
“Karibu aiseee!!” alinikaribisha huku akiutupa fagio kando na kujongea katika kibanda nikiwa nimeduwaa bado. Akafungua mlango wa mbao na kuingia dukani, akatega sikio kunisikiliza.
“Za asubuhi shehe wangu!!” alinisabahi kwa lafudhi yake ya kichaga, nami nikamjibu kwa utulivu!!
“Kuna maziwa fresh!!” nilijikuta nikimuuliza ilihali macho yangu yaliyofanikiwa kupepesa pale ndani hayakuona hata mfano wa maziwa.
“Hamna maziwa bosi wangu, hapa hata friji sina. Unavyoviona n’do vitu pekee humu dukani.” Alinijibu huku akiufungua mlango tena na kutoka nje. Hitaji langu lilikuwa limemkera kiasi fulani.
“Masawe! Njoo unipatie sigara, samahani kwa usumbufu!!”
Hakujibu kitu akajongea kibandani na kunipatia sigara niliyokuwa nimeagizia. Akataka kunipatia kiberiti, nikamweleza kuwa hicho nilikuwanacho!!
“Yaani tumbo limenisumbua jana Masawe. Hapa sijui hata maziwa nt’ayapatia wapi? Lakini licha ya hayo Masawe wewe hunikumbuki nd’o maana hata hujanichangamkia… hata hivyo siku ile giza lilishaanza kutawala…” nikaingiza maongezi ya kulifikia lengo. Akanitazama akijaribu kuitafuta sura yangu bila mafanikio.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nilikuja hapa na mke wangu usiku mmoja hivi, tukanunua pipi na vocha…. Ni siku kadhaa nyuma, halafu kigiza kilishaanza kuingia usingeweza kunitambua, halafu siku ile sikiwa na miwani hii….” Nilizidi kumuundia mazingira huku nikiupuliza moshi wa sigara juu.
Kumbe Masawe naye alikuwa mvutaji, akachomoa sigara na kuanza kuivuta.
“Hivi Masawe una uzoefu sana na biashara ya duka kwa huku Iringa hasahasa hapa mjini?” nikamuuliza swali lile huku nikijifanya sitilii maanani sana chochote atakachonijibu.
“Nina miaka minane nauza duka, Moshi huko na hapa pia japo si muda mrefu lakini ninaifahamu vyema Iringa” alinijibu huku tukiendelea kushindana kuvuta sigara.
“Masawe na ujanja wako huo hadi leo unavuta SM shehe wangu…” nilihama nikarejea katika utaniii.
“Hapana hataaa ‘sports huwa navuta sema leo nabadilisha ladha” jibu lake likaleta matabasamu na vicheko hatimaye!!!
Urafiki ulianza kujengeka!!
“Masawe mimi ni mgeni huku Iringa, na kitu kikubwa kilichonileta huku ni kufanya biashara ya duka katika mtaa fulani huko karibu na chuo sijui wanakiitaje. Mwanzoni nilitarajia kumweka mke wangu asimamie lakini bahati mbaya ameugua na hali ya huku imemkataa kabisa, sasa natafuta mtu mwingine wa kumweka pale. Wewe nakuona ni mzoefu sana, waweza kunisaidia mawazo kidogo.” Nikatupa karata yangu kubwa zaidi niliyokuwa nimeiandaa.
Masawe akatabasamu kidogo kisha akaingiza utani.
“Mbona mimi nipo waweza kuniajiri tu shehe wangu!! Ilimradi masilahi tu” tukacheka pamoja lakini nikausimamia ule utani wake ili uniongoze zaidi.
“Aaah Masawe mtu mzito kama wewe nitakulipa bei gani, maana utalazimika kuiacha ofisi yako. Sasa ndugu si utanifilisi wewe….. yaani mtaji ukiongezea na mshahara wako n’do nafilisika kabisa.” Nilifanya utani kimalalmiko. Masawe akacheka kabla ya kuleta jibu langu la kwanza kabisa.
“Bora hata kingekuwa kibanda changu asee. Cha wenyewe hiki bwana, kila nikilalamika bidhaa ziongezwe bosi anadai ningoje kidogo, hiyo kidogo huu mwezi wa sita tangu nianze malalamiko!!. Tazama sasa mfano tangu umefika wewe hapa bado hajafika mteja mwingine tena. Eneo lenyewe hili halijakaa kibiashara kabisa na bosi hashauriki hata kidogo!”
“Aah Masawe yaani unataka kuniambia wewe umetoka Arusha na kuja kuajiriwa huku kwenye hiki kibanda kikiwa hivi hivi ama amehamishia bidhaa nyingine mahali. Mbona unanitisha bwana ama huku Iringa maduka hayalipi, niweke wazi bwana Masawe.” Nilifanya udadisi, wakati huu sigara ilikuwa imemalizika.
“Ni stori ndefu shehe wangu, ila bosi wangu aliponitoa Moshi kunileta huku yalikuwa makubaliano mengine kabisa. Alinileta kufanya kazi mahali lakini mwisho wa siku nikaishia hapa dukani. Sema ninachoshukuru nikiwa na shida ananisaidia..” alijibu kwa ufupi lakini nikatambua kuwa kuna mengi sana anayo na si wa kumwendea kwa pupa.
“Aisee Masawe pole ndugu yangu, basi ngoja niingie hapo stendi Masawe nikitoka nitakuja tubadilishane mawazo bwana Masawe. Maana mimi shemeji yako bwana, nimeoa hukohuko kwenu!!” nilijenga undugu wa kilazima huku nikiamua kuonyesha kuwa sihitaji sana kujua kuhusu hicho kibanda.
Laiti kama Masawe angejua kila neno lake lilivyo la muhimu kwangu asingethubutu kuzungumza nami!!
Niliondoka pale na kujizungusha mjini, nikanunua nguo nyingine mpya, kisha nikatafuta nyumba ya kulala wageni nikalipia, nikaoga na kubadili nguo.
Nikatoka na kurejea kwa Masawe tena, kama kawaida kofia kichwani na miwani usoni. Sikutaka Masawe anitambue maana angejua tu kuwa ni mimi yule ninayetafutwa basi mambo yangeharibika. Na nilichoshukuru zaidi magazeti hayakuwa na habari na mimi tena baada ya kuthibitishiwa kuwa nimekufa.
Masawe alinichangamkia baada ya kuniona tena kwa mara nyingine, sasa nilikuwa nadhifu kabisa tofauti na awali. Shida yangu kucheza na akili ya Masawe, nilitambua ni kiasi gani watu kutoka Moshi na Arusha walivyo makini linapokuja suala la kutumia nafasi.
“Haya sasa tazama tangu wewe uondoke wamekuja wateja wawili tu mmoja kununua kibiriti na mwingine mtoto amekuja kununua pipi kifua. Unaweza kuiita hii biashara shehe wangu!! Mimi nataka kuchakarika yaani.” Alianza kujivutia upande wake. Nikaipenda hali hii.
“Kwa makadirio mfano, samahani lakini. Wanakulipa milioni ngapi hapa ili nijipange na mimi nikitaka kukunyofoa.”
Akacheka sana kabla ya kunijibu, “Yaani uuze pipi na sigara ulipwe milioni!! Hata laki mbili haifiki sema nina sehemu ya kulala ya bure.”
Nikatikisa kichwa kisha nikawalaumu mabosi wake ambao sijawahi kuwaona, kuwa ni wanyonyaji sana. Nikalaani na mwisho nikajisemea.
“Mimi siwezi kumlipa mfanyakazi wangu chini ya laki tatu na nusu. Nimesota katika maisha na ninaujua ugumu wa hizi kazi na maisha yako juu pia Masawe.”
Masawe akafanya tabasamu kisha akacheka kibwege huku akiona aibu. Bila shaka lile dau langu lilimkamata akili. Nikaamua kuendelea kumkamata.
“Ujue wakati mwingine unapompa mfanyakazi mshahara kidogo ndo mwanzo wa kuanza kukuibia, mara leo hiki kesho kile. Anakuwa hawezi kujikimu, lakini ukimlipa mtu vizuri akikuibia huyu ni mwizi wa tabia tu!!”
Masawe akatikisa kichwa kuunga mkono hoja!!
“Sasa kwa hii biashara bosi wako anaweza vipi kukulipa mshahara kama leo umeuza pipi na sigara na kibiriti?”
“Inashangaza sana, ananilipa hivyo hivyo, tena anaendesha magari yule ya kifahari. Kuna kipindi zinapita hata wiki mbili sifungui duka, yaani ana maamuzi ya ajabu sana anaamka tu Masawe leo hakuna kwenda dukani mpaka nitakapokwambia. Zinapita hata siku kumi nd’o nafungua tena…. Sijui ana wazimu?” alijiuliza Masawe, mimi nikapata faida nyingine.
Kumbe Masawe hata yeye hajui kwanini bosi wake analing’ang’ania hilo duka. Nikayakumbuka maneno ya Anitha aliponisisitiza kuwa huyu aliyepo dukani si lolote si chochote yupo mwingine mdosi zaidi.
“Looh!! Kwa hiyo ukifunga nd’o hakuna kinachoendelea tena dukani, kumbe nd’o maana mnafukuza wateja.”
“Aaah!! Bosi wangu wa ajabu mno, kuna kipindi alikuja ghafla mimi nikaambiwa kutoka nje, walikuwa wawili. Nilipokuja kuchungulia ndani sikuwaona hata. Baadaye kabisa wakatoka, hata sikuuliza lakini nilipowashirikisha watu kadhaa wakaniambia kuwa hayo ni mambo ya ushirikina tu hakuna la ziada.. nikapuuzia na kusahau.”
“Dah!! Inasikitisha sana!!” nilimaliza maongezi hayo, lakini moyo ukinienda mbio, ni kama kulikuwa kuna kitu cha ziada nilitakiwa kukitambua kutoka katika himaya ile. Kitu cha msingi zaidi!!
Siku hiyo maongezi yakaishia pale nikaaga!! Kwa makubaliano ya kufika tena siku nyingine.
“Bosi wangu wewe ukiwa tayari niambie tu mimi nafanya kazi kama kawaida.” Alinisihi, nikaondoka!!
****
USIKU huo nikiwa nyumba ya kulala wageni nilikuwa nikiunganisha mambo kadha wa kadha, kubwa zaidi kuhusiana na utata wa kile kibanda kilichoitwa Michigani. Nilitaka kujua kiundani zaidi kuhusu mmiliki na mengine ya ziada. Nikajipanga kikamilifu kwa ajili ya kumkabili tena Masawe kwa lugha nyingine ili niambulie mengi zaidi.
Nikaamua kujipa siku tatu mbele zaidi ili niweze kumtembelea tena yule bwana muuza duka.
Wakati huo niliendelea kupokea jumbe kadha wa kadha kutoka kwa Jojina akinijulia hali huku akidai kuwa anaendelea na harakati kwa kasi kabisa. Jambo ambalo lilinitia nguvu na mimi kuendelea
CHEUPE DAWA.
BAADA ya siku tatu kama nilivyojipangia majira ya saa nne asubuhi nilifunga safari kwenda kuonana tena na bwana Masawe. Siku hii nilijipanga kumchukua tukae mahali tuzungumze kwa kina, maswali niliyoyaandaa kutokana na taaluma yangu ya uandishi wa habari niliamini kuwa hata awe mjanja vipi bwana Masawe hawezi kuchomoka!!
Maswali yale nilikuwa nikiyatumia katika matukio magumumagumu hasa hasa kujua ukweli juu ya jambo fulani kutoka kwa mtu mbishi na mjanja mjanja!!
Niliamua kutumia usafiri wa taksi ili niweze kuidhihirisha hadhi ambayo tayari nilianza kuijenga kwa Masawe, tena safari hii nilitaka niendeshe mwenyewe hadi mahali ambapo Masawe ataniona vizuri kabisa.
Nikajivuta hadi katika kijiwe cha taksi nikazungumza na ‘shanta’ juu ya shida yangu!! Yeye hakuwa na kikwazo baadaye akamuita mmiliki halali.
Wakadai nilipe zaidi ya kawaida nikakubaliana nao.
Nikaingia katika usukani, shanta (deiwaka) akawa ameketi kiti cha nyuma!! Nikaanza kunyonga kuelekea kwa Masawe huku Shanta akiniongoza kila nilipotaka kupotea njia.
Ni wakati nataka kukata kona ili gari iweze kutazamana moja kwa moja na duka la Masawe ndipo nikaona gari nyingine ya kifahari ikiwa katika harakati aidha za kuegesha ama kuondoka kutoka eneo lile. Akili ya haraka ikajirusha katika kichwa changu!!CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Sikukata kona badala yake nikanyoosha moja kwa moja!
Shanta akadhani nimekosea njia, nikamsisitiza kuwa nilikuwa sahihi kabisa. Nikaegesha gari kwa mbele kabisa, tukakubaliana na Shanta kuwa ataningojea palepale. Akatoa pakiti ya sigara na kuchomoa moja!!
Nikaondoka na funguo za gari huku nikitembea kimadaha, katika namna ya kuridhika sana kana kwamba ni mdosi kutoka nje ya nchi!! Kwa nje ningeweza kuonekana nimeridhika sana lakini macho yangu yalijikita katika kuitazama Nissan Patrol ilivyokuwa inajaribu aidha kuondoka ama kuendelea kuwa eneo lile. Na hapo nikagundua kuwa ile gari haikuwa ikiondoka bali ilikuwa imewasili.
Akili ikanicheza upesi!! Kwa mbali kabisa nikaangaza sikufanikiwa kuiona sura ya Masawe wala dalili yoyote ya uwepo wake!! Upesi nikatoa simu yangu mfukoni, nikaitazama kana kwamba ilikuwa inaita nikapokea wakati si kweli kuwa ilikuwa inaita.
Nikajizungusha huku na kule kama ninayetafuta mtandao.
Nia yangu ikiwa kutazama kama naweza kuona chochote kitu kinachoendelea!!
Mlango wa duka ukafungwa!! Upesi nikaikumbuka kauli ya Masawe kuwa aliwahi kuchungulia ndani baada ya kutolewa nje! Nami nikajitia jeuri tena nisiyekuwa na hatia nikajisogeza mbele kwa kujiamini funguo zangu zikiruka hewani huku na kule.
Nikakifikia kile kibanda.
“Masaweee!!” nikaita kwa sauti ya chini!!
Kimya! Nikaita tena kwa sauti ya chini bado hapakuwa na jibu. Nikalisogelea lile gari niweze kuangaza kulikoni, nikajifanya natazama kama kuna mtu ndani yake niweze kumuulizia kulikoni mbona Masawe hajafungua duka.
Nilipolikaribia gari nikakutana na vioo vilivyovikwa utando mweusi ‘Tinted’ nikatamani kujua ni nini kinaendelea ndani!!
Nikachungulia!!
Nikaona kitu mfanowe bahasha, bahasha kama ile yangu iliyokuwa na nyaraka zangu kutoka kwa yule bwana wa kuitwa Ezekiel. Nikazidi kukisogelea kioo ili nijihakikishie zaidi juu ya ile bahasha katika kile kiti.
Lahaula!! Pua yangu ikagusana na kile kioo. Ving’ora vya dharula vikaanza kulia, ile gari ikawa inapiga makelele kwa fujo, hofu ikanitanda. Nikapagawa na kuamini kuwa wakati wa kuumbuka na kukamatwa ulikuwa umewadia, nikataka kukimbia lakini nikagundua kuwa ni upuuzi uliopitiliza. Sijaiba cha mtu, nimevaa kofia na miwani machoni, nikimbie nini. Lakini nafsi nyingine ilikuwa inanisihi nikimbie, maana kama ni kweli hiyo bahasha ni ile nilikuwa naisaka basi hao watu lazima watakuwa watu wabaya.
Na hivyo watakuwa wananifahamu fika!!!
Maswali mawilimawili, nikimbie ama nisikimbie!!
Nikakosa maamuzi na kubaki kama zezeta nikingoja kuumbuliwa!!
Akili ikanicheza upesi!! Kwa mbali kabisa nikaangaza sikufanikiwa kuiona sura ya Masawe wala dalili yoyote ya uwepo wake!! Upesi nikatoa simu yangu mfukoni, nikaitazama kana kwamba ilikuwa inaita nikapokea wakati si kweli kuwa ilikuwa inaita.
Nikajizungusha huku na kule kama ninayetafuta mtandao.
Nia yangu ikiwa kutazama kama naweza kuona chochote kitu kinachoendelea!!
Mlango wa duka ukafungwa!! Upesi nikaikumbuka kauli ya Masawe kuwa aliwahi kuchungulia ndani baada ya kutolewa nje! Nami nikajitia jeuri tena nisiyekuwa na hatia nikajisogeza mbele kwa kujiamini funguo zangu zikiruka hewani huku na kule.
Nikakifikia kile kibanda.
“Masaweee!!” nikaita kwa sauti ya chini!!
Kimya! Nikaita tena kwa sauti ya chini bado hapakuwa na jibu. Nikalisogelea lile gari niweze kuangaza kulikoni, nikajifanya natazama kama kuna mtu ndani yake niweze kumuulizia kulikoni mbona Masawe hajafungua duka.
Nilipolikaribia gari nikakutana na vioo vilivyovikwa utando mweusi ‘Tinted’ nikatamani kujua ni nini kinaendelea ndani!!
Nikachungulia!!
Lahaula!! Pua yangu ikagusa na kioo. Ving’ora vya dharula vikaanza kulia, hofu ikanitanda. Nikapagawa na kuamini kuwa wakati wa kuumbuka na kukamatwa ulikuwa umewadia, nikataka kukimbia lakini nikagundua kuwa ni upuuzi uliopitiliza. Sijaiba cha mtu, nimevaa kofia na miwani machoni, nikimbie nini.
Nikaamua kungoja atakayetoka niweze kumuuliza kulikoni!!!
Maajabu!!
Hakutoka mtu hadi king’ora cha dharula cha kwenye hiyo gari kilipokoma kulia.
Ina maana wapo mbali sana hao watu!! Ama ndo mambo ya ushirikina? Nilijiuliza mwenyewe huku nikisogea ule upande ambao Masawe aliutumia kuchungulia ndani siku ile aliyonisimulia!! Nilikuwa natetemeka sana lakini kitu ambacho sikutaka kufanya ni kupiga hatua nyuma!!
Kupiga hatua walau moja tu nyuma ningejidhihirishia ni kwa namna gani mimi ni muoga tena nisiyekuwa na uchungu na nafsi zilizopotea kimasihara!!!
Pia ningekuwa si mzalendo hata kidogo!! Kama Anitha alipotea akinipigania, mimi nikipotea kuna tatizo??
Nikajipa moyo na kupata nguvu mpya!!
Hakika! Hapakuwa na mtu ndani ya chumba kile, nikasogea karibu zaidi nikachungulia kwa ukaribu. Nikaangaza huku na kule bila mafanikio. Hapakuwa na mtu, wala dalili ya kitu chochote chenye uhai.
Wachawi hawa! Nikafikiria, kisha nikaanza kuondoka, nikajiweka mbali kabisa na eneo lile. Nilimwona Shanta kwa mbali alikuwa analalamika akitupa mikono huku na kule ma ajishike tumbo ma ra kichwa. Nikajua ni njaa zinamsumbua, nikachomoa pesa mfukoni na kumwonyeshea kuwa nitamwongezea nyingine akaendelea kulalamika huku akiniita kwa kutumia viganja vyote viwili vya mikono yake!! Kuna jambo alikuwa anamaanisha natakiwa kulifanya labda hasahasa nikiwa karibu yake lakini sikujali sana sikudhani kama lingeweza kuwa na umuhimu wowote ule kwangu kwa wakati ule ambao kila dakika ilikuwa na umuhimu wake.
Nikaenda upande mwingine ili nipate eneo zuri la kuweza kuona kila kona.
Nikalipata jumba bovu lisilotumika tena, baada ya aidha kubomoka ama ujenzi wake kuishia njiani.
Au ndo magofu ya Michigani haya!!! Nikajiuliza.
Nikajiweka pale na kuchungulia nini kinatokea kwa hao watu waliopotea kimaajabu ndani ya duka lile dogo kabisa la Masawe! Nilivuta subira bila kupepesa macho kona nyingine. Nilitaka kukata tamaa baada ya kungoja sana lakini nikakumbuka kitu!!
Subira yavuta heri!
Naam ile heri ikawadia hatimaye!! mlango wa kibanda cha Michigani ukafunguliwa!!
Wakatoka wanaume wawili, mmoja akiwa amevaa suti nyeusi, huyu alikuwa mweusi, na mwingine alikuwa……. Hakika alikuwa ni yeye, haikuwa mara ya kwanza kuonana naye.nisha kichwa chaka kama niliwahi kukiona mahali.
Hatimaye akageuka na hisia zangu hazikuwa potofu hata kidogo!!
Alikuwa yule mzungu, cheupe aliyehusika katika kumkamata mke wangu!!
Alikuwa ni cheupe dawa! Mtu ambaye niliamini kabisa kuwa anahusika katika kuniachia ujumbe wa ‘UTAMFUATA MWENYEWE’.. hakika alikuwa anajua, maana siku aliyomteka mke wangu ndo siku hiyo hiyo yule mtoto mtukutu Selemani alinambia kuna ujumbe upo ndani ya nyumba yangu. Na nilipomwagiza na yeye akakamatwa!!
Sijui walimpeleka wapi watu hawa wabaya!!!
Nilijihakikishia kuwa sijakosea, wakati nikiamini kuwa eneo lile wapo watu wawili, mara nikawaona wawili wale wakigeuka ghafla, na mimi nikageuka nao. Ana kwa ana na shanta wa ile gari. Alikuwa anaangaza huku na kule, bila shaka alikuwa katika harakati za kunifuata nilipokuwa!!
Cheupe dawa akamuita!! Shanta akababaika, lakini alivyoitwa na yule mwafrika akaenda huku dalili za uoga zikiwa bayana. Alifika nan kuzungumza nao kuna jambo walimuuliza lakini sikuweza kulisikia. Shanta akawa anaangaza huku na kule, bila shaka akinitafuta mimi. Sijui walimuuliza mimi nipo wapi ama?
Wakaongozana naye hadi jirani kabisa na gari yao.
Ghafla yule mzungu akamkwida, huku akitazama huku na kule, dereva akawa anarusha miguu huku na kule. Nilijisikia kutetemeka miguu, shanta aliyekuwa mkarimu kwangu alikuwa matatani sasa.
Nikataka kupiga mayowe lakini nikatambua kuwa nitakuza tatizo badala ya kulipunguza. Na ugumu zaidi ungekuja upande wangu!!!
Punde akamrusha ndani ya gari. Milango ikafungwa wote wakiwa ndani kisha ikatimua vumbi, kutoweka eneo lile ikiipita taksi yetu.
Nilibaki nimebung’aa nisijue nini cha kufanya.
Funguo mkononi!! Shanta katoweka, maskini labda walidhani kuwa alikuwa anawafuatilia!!
Kumbe na mimi wangenikuta ningeambulia kipigo na kukamatwa!!.....
Nusu saa baadaye nikiwa katika kuhakikisha kuwa wale watu wametoweka kabisa, na Masawe naye aliwasili, niliusikia mluzi wake kwa mbali kisha akatokea akiwa katika mwendo wake wa kusuasusa na hapo nikatambua kuwa alikuwa ana ulemavu mguu mmoja ulikuwa mfupi.
Kabla ya kufungua duka, alichukua kipande cha fagio na kuanza kusafisha eneo linalozunguka duka, huku akiendelea kupiga mluzi. Baada ya kuhakikisha kuwa Masawe hana walau muonekano wa kujua ama kutaka kujua kilichotokea humo ndani nikatokea mafichoni na kumkabili na asijue ni wapi nimetokea.
“Aisee nimekuja asubuhi sijakupata shehe wangu!!” nilimsemesha kwa lafudhi ya kichaga, akacheka kabla ya kunieleza kama nilivyoona. Kuwa bosi alikuwa na mambo yake!!
“Kwa sasa yupo wapi?” niliuliza ili nipate kujitoa mashaka na usalama wangu!!
“”Wameenda Mbeya huko, hapo safari maana huwa wanaondoka na ndege!!” alinijibu. Amani ikarejea kiasi lakini kuna mambo mawili yalikuwa ya msingi zaidi.
Kujali muda nilimalize hili tukio upesi na pili nitambue juu ya siri iliyopo katika kibanda kile.
“Kwa hiyo akiwa hayupo nani sasa anakusimamia hapa!!”
“Hata akiwepo hakuna wa kunisimamia” alinijibu bila wasiwasi.
“Maana mguu wangu hapa kwako nia yangu unisaidie kuingia mjini kunilangulia vifaa kadha wa kadha vya kazi. Si unajua mimi mgeni wasije kunipiga bei kali…” nilidanganya. Masawe akafurahi kuona kuwa ninamthamini, akazungumza mawili matatu kisha akaniuliza tunaongozana ama aondoke peke yake!!
Nikamwomba aondoke peke yake na mimi kama kuna uwezekano nijilaze kidogo, Masawe akaniruhusu kuingia katika kile kiduka ambacho thamani yake haikuwa ya kumwogopa mwizi.
Masawe akatoweka baada ya kumpa mahesabu ya uongo!
Aliponipa mgongo, nami nikaanza kufanya kilichonipeleka, nikatazama huku na kule bila mafanikio. Nikaituliza akili yangu na hatimaye nikaona kitu.
Tundu la funguo katikati ya makablasha ya kuwekea bidhaa, nikajaribu kuvuta pakawa pagumu kufunguka, nilijaribu tena na tena lakini bado hali ilikuwa ileile.
Nikachukua funguo zilizokuwa pale ndani lakini hazikufanania na tundu lile!!
Nguvu zikaniishia tena, nilitamani dakika za mwisho za uhai wangu ziishie ndani ya huo mlango ilimradi nijue tu ni kitu gani huwa kinaendelea katika maficho yale. Nilitaka kujua kitu kimoja tu, hiyo Michigani ni Michigani kweli? Na je inahusiana vipi na Anti Ezekiel??
Wakati nawaza juu ya ufunguo.. nikakumbuka kuwa kuna funguo nilipewa na Ezekiel Ubungo na kunisihi mambo kadha wa kadha. Nilipotazama kile kitasa hakika kiliendana na ule ufunguo!! Walau matumaini yakajengeka upya huku nikimshukuru Ezekiel kimoyomoyo!!
Lakini mara nikafadhaika!! Na ilikuwa lazima nifadhaike kutokana na kilichopita kwa kasi kichwani mwangu!!!
Nikakumbuka kuwa ufunguo ulipotea ukiwa ndani ya bahasha nyumbani kwa mama lao!!
Kazi ikawa ngumu zaidi!! Tena mpya!!
****CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Aliponipa mgongo, nami nikaanza kufanya kilichonipeleka, nikatazama huku na kule bila mafanikio. Nikaituliza akili yangu na hatimaye nikaona kitu.
Tundu la funguo katikati ya makablasha ya kuwekea bidhaa, nikajaribu kuvuta pakawa pagumu kufunguka, nilijaribu tena na tena lakini bado hali ilikuwa ileile.
Nikachukua funguo zilizokuwa pale ndani lakini hazikufanania na tundu lile!!
Nguvu zikaniishia tena, nilitamani dakika za mwisho za uhai wangu ziishie ndani ya huo mlango ilimradi nijue tu ni kitu gani huwa kinaendelea katika maficho yale.
Wakati nawaza juu ya ufunguo.. nikakumbuka kuwa kuna funguo nilipewa na Ezekiel Ubungo na kunisihi mambo kadha wa kadha. Nilipotazama kile kitasa hakika kiliendana na ule ufunguo!!
Nikakumbuka kuwa ufunguo ulipotea ukiwa ndani ya bahasha!!
Kazi ikawa ngumu zaidi!!
****
Nilirejea kimaficho katika nyumba ya kulala wageni niliyokuwa nimefikia, lakini9 nikakumbuka kununua magazeti kadha wa kadha, nikatilia maanani gazeti la yule mzee Matata, mzee ambaye kwangu mimi alikuwa kama adui tayari.
“MZIMU WA SAM WAONEKANA DAR UKIZURURA”
Nilishikwa na hasira kuiona picha yangu tena katika kurasa za mbele za magazeti. Nikajikuta nakabiliana na donge la hasira kooni, nikakumbuka kuwa funguo nimepoteza tayariu ambazo zingenisogeza karibu na ukweli na sasa gazeti la kipuuzi la mzee Matata linaandika ujinga tena kuwa nimeonekana Dar.
Huyu mzee na shahada zake za kutosha bado anashikiliwa akili na wajinga wajinga hawa. Haoni uchungu mwanaye amepotea? Ama nd’o upendo uliopoa?
Ghafla nikavamiwa na wazo kuwa huenda Anitha alirejeshwa nyumbani kwao, na huu msala umebaki kuwa mzigo wangu mwenyewe!!
Wazo hili halikutaka kutoka kichwani mwangu hata kidogo!! Nikajiaminisha kuwa namuwaza mtu ambaye yu huru!!
Nd’o maana baba yake anaendelea kufanya upumbavu huu!!
Nilijihisi kutetemeka mwili mzima, huku lile gazeti mkononi mwangu nikiliona kuwa mzigo mzito sana tena mzigo wa miiba unaochoma kwa hasira.
Mwendo mfupi wa kuifikia ile nyumba ya kulala wageni niliona ni sawa na kilometa kumi. Nilitamani kukifikia chumba nikivamie kitanda na kujilaza. Sikuwa na la ziada.
Hatimaye nikafika chumbani, nikalifunua lile gazeti. Kama ilivyo kawaida ya wasiojiamini, akaandika kuwa habari ile imeandikwa na ‘MWANDISHI WETU’
Nikasonya kwa ghadhabu na kulichana vipande vipande gazeti lile, kisha nikalala! Bila hata kuvua viatu vyangu!!
HARAKATI ZA JOJINA DAR
Nilikuja kushtuka masaa kadhaa mbele, usiku ulikuwa umeingia tayari na sikuwa nimepata walau hamu ya kula, niliumiza sana kichwa nisijue ni wapi pa kuweza kuanzia tena ili niufungue mlango ule, nikajiuliza mara mbili zaidi na kukosa majibu. Nikaingia bafuni na kujimwagia maji huenda kuna jambo jipya limezibwa na uchovu wa mwili litajitokeza.
Hakuna kilichojitokeza. Nilishika hiki na kuacha kile labda nitapata ufumbuzi lakini sikuwa na ujanja wowote, nikafikiria juu ya kuchongesha funguo za bandia lakini ajabu hata ramani ya tundu lile sikuwanayo na haikuonekana kuwa kazi nyepesi kuchonga funguo zahali pale. Funguo za maajabu.
Simu yangu ya mkononi ambayo namba yake alikuwanayo Jojina pekee ilipatwa na uhai na kuanza kuimba! Nikaisogelea kwa hofu maana sikutarajia simu kutoka Dar es salaam niliamini Jojina alikuwa mwenye ghadhabu na labda hakutaka kusema nami lolote.
Naam hakuwa mwingine aliyepiga simu ile.
Alikuwa Jojina!
“Nambie Mama lao…” nilimuanza kiutani ili kama ana jazba azitulize kidogo
“Safi tu Sam vipi ulikuwa umelala tayari.” Alinijibu kwa uchangamfu, ile saauti yake ya kimahaba ikanituliza woga wangu.
“Hapana nilikuwa bafuni ….”
Nikajirusha kitandani na kujilaza simu sikioni niweze kusikia Jojina ana lipi jipya!!
Alinieleza mambo kadha wa kadha kuhusu uwepo wake jijini Dar na mimi nikamweleza juu ya hali ya hewa ya Iringa, kisha akachukua nafasi kuel;ezea nia ya kunipigia simu usiku ule pasi na matarajio.
JOJINA.
SAM, kwanza sahau kuhusu yaliyopita, nadhani tulipishana lugha tu, nilipokukosea nisamehe nami nishasamehe uliponikwaza. Sam ni siku kadhaa hatujazungumza na ni kama siku yangu ya nne ama ya tano huku Dar es salaam. Kubwa zaidi la kukupigia hii simu ni kwamba hatimaye nikafanikiwa kuonana na mzee Matata. Sam yaleyale ya mzee Madati kurukwa akili ndo huku pia lakini afadhali huyu hajawekewa madawa lakini kupotea kwa mtoto wake kumemchanganya sana. Nilipofika kule mara ya kwanza nilizuiliwa kuingia eti kwamba mzee hatakiwi kuonana na watu madaktari wamekataza.
Nikaondoka kapa siku hiyo! Lakini sikufa moyo.
Sikukata tamaa Sam. Mara ya pili nikajieleza kuwa shida yangu kuonana na mzee ni kuhusu mwanaye. Wacha wee! Hapo sasa nikaonekana lulu mchangani, kila mtu ananiuliza kulikoni. Nikagoma kusema lolote hadi niongee na mzee. Kama yeye atawaeleza ni juu yake! Lakini mimi simwelezi mtu tofauti na yeye, na kama sitaruhusiwa siku hiyo basi tena hawataniona mimi kukanyaga pale nyumbani kwao.
Sam niliyasema haya huku natetemeka, maana najua kuwa maaskari watakuwa wameshirikishwa juu ya jambo hili, hivyo wakisikia kuna mtu anajua wanaweza kumweka kizuizini ili asaidie upelelezi. Nikaamua kujitoa muhanga huku nikiamini kuwa Mungu anamshika mkono mwenye haki.
Ama kweli damu nzito kuliko maji!!
Mzee akaelezwa nikakubaliwa kuingia japo walinionya kuwa ana tatizo la kubadilika badilika yule. Sikujali kuhusu hilo nilichotaka kuonana naye kwanza.
Sam, yule mzee amekwisha na hapa sasa naamini alikuwa akimpenda sana mtoto wake, yaani amekuwa dhaifu sana. Akanikodolea macho nami nikajiweka sawa, tulikuwa wawili tu, nikaanza kumweleza kilichonileta hadi pale, nikamsimulia baadhi ya matukio hadi ujio wa Anitha Iringa, sikukutaja wewe hata kidogo kwanza, nikadanganya kuwa alikuwa amekuja kufanya biashara huko.
Nikamwelezea juu ya mikasa ya ajabu ya Anti Ezekiel mjini Iringa. Mikasa ambayo inasemekana kuwa ni ya kishirikina ama mauzauza mengine!
Hapo akakodoa macho yule mzee, na kwa mara ya kwanza akasema na mimi. Kumbe na yeye ni mtu wa Iringa ni Mbena yule mzee. Hapa tukabadili lugha tukahamia katika kabila, nikasema naye kibena. Ushirikiano ukawa mkubwa sana tukawa marafiki.
Nikamweleza kuwa nauhitaji sana msaada wake maana hata mimi nimepoteza mtoto na kuna mwenzangu familia yake yote inateketea. Kufikia hapa nikaona hakuna haja yoyote ya kuendelea kuficha siri hii ilhali mzee ameonyesha ushirikiano na nilichokisema hakikuwa katika maandishi ningeweza kukibadili muda wowote ule!!!
Nikamtajia jina lako, sikumpa nafasi ya kusema lolote bali nikamlaumu kwa kutotaka kukusikiliza nikamweleza juu ya tuhuma unazozushiwa na watu wabaya na nd’o haohao wamemchukua mtoto wake. Kufikia hapo nikamweleza kuwa Anitha alikuwa katika harakati za kukusaidia wewe na wao wakagundua nd’o wamemshikilia.
Macho yakamtoka mzee na akatoa ushirikiano!!
Akakiri kuwa kuna watu walikuwa wakileta taarifa zile ofisini, na hakujua kama ni watu wabaya. Nikamuonya asithubutu kumweleza mtu yeyote juu ya hili maana hao watu ni hatari, wakigundua umewajua tu wanaanza kukuonya kimatendo, mzee akakiri kuitambua skendo hiyo ya UKIMJUA UNAPOTEA. Akajionya!!! Aliwahi kuisikia Iringa miaka hiyo!!
Kumbe ni mchezo wa miaka mingi tu huu Sam!! Na bado umefumbiwa macho. Anti Ezekiel ni nani hadi alibabaishe taifa letu!! Yeye ni nani katika ardhi hii huru??
Baada ya mazungumzo marefu tukapanga mikakati kabambe! Mkakati wa kumvumbua huyo Anti Ezekiel.
Mzee alichangamka na hakuna hata ndugu mmoja aliyeweza kuamini kuwa yule alikuwa mzee wao.
Leo asubuhi mikakati hiyo imeanza kufanya kazi!
Gazeti la mzee Matata limeandika taarifa zako kuwa umeonekana maeneo ya Dar es salaam mjini ukizurura.
Nia yetu kubwa ni kuwavuta hawa watu waje huku ili tuweze kushughulika nao vyema. Baada ya taarifa hiyo ofisi ya mzee Matata ikapokea simu kutoka kwa watu wanaojiita wapelelezi kutoka Iringa, mmoja akazungumza Kiswahili na mwingine akasema kiingereza. Wakadai wanahitaji kuonana na huyo mtu aliyekuona wewe waweze kujua wapi pa kuanzia ili kuujua ukweli, walilalamika kuwa wao wanaamini umekufa hivyo uzushi kama huo unashusha thamani ya utendaji kazi wao.
Kufikia hapo mzee Matata ameniamini sana na kujua ni kweli kuna jambo linafichwa nyuma ya pazia..
Hao mabwana wakawasili kutoka Iringa na kukutana na watu wa mzee Matata, ni mzungu mmoja na muafrika na wamekuja na gari binafsi aina ya Nissan patrol! Kwa leo wametoa tu salamu, kesho watakuwa ofisini kwa mzee Matata, japo mzee hatakwenda amewaambia wakitoka huko wamtembelee nyumbani kwake.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa hiyo Sam hapo nd’o tumefikia!!
JOJINA AKAMALIZA.,
Nilikuwa natetemeka sana, ilikuwa ni sababu ya baridi pamoja na uoga tele huku kihoro cha matumaini kikinipagawisha. Mwanzoni nilikuwa na hasira wakati namsikiliza mama lao kwa sababu nilihisi mzee Matata ni mnafiki na anamhadaa lakini kumbe ile habari gazetini imepikwa maksudi ili kuwaweka karibu maadui kuwa marafiki ili shambulizi likifanyika wawe katika taharuki bila matarajio wala maandalizi ya kujikinga!!
Watu waliotajwa nilikuwa nimewaona asubuhi hiyohiyo katika kijumba cha Michigan!!
Cheupe dawa na yule mwenzake wapo Dar tayari.
Nikamweleza Jojina juu ya mkasa wangu kwa ufupi sana, nikamwelezea juu ya watu hao na jinsi wanavyoishi kimaajabu katika kibanda cha Michigan. Nikamwelezea kila nilichofanya hadi kufikia hatua ya kukuta tundu la kufunguliwa na funguo. Sikusita kumhakikishia kuwa cheupe dawa huyo ndiye aliyemkamata mke wangu jijini Dar…
“Jojina, tumekaribia kulipata jibu lakini kuna kitu kimoja ambacho kinanipa utata na kuniumiza kichwa, sehemu ya kufungulia geti la kuingia katika maficho yao imeonekana tayari na ninaweza kujua namna ya kupaingia tena. Lakini Jojina funguo hakuna Jojina, ile bahasha tuliyopoteza katika chumba chako kwenye operesheni mbwa okoa, ndani yake kulikuwa na funguo!!
Ni hizo na ninao uhakika kuwa Ezekiel alimaanisha kitu aliponipatia zile funguo!!
Nilimaliza kuongea nikamsikia Jojina akishusha pumzi zake kwa nguvu sana. Ni kama alikuwa ameungana nami katika kukata tamaa.
“Kweli huo ni mtihani mgumu, lakini Sam unakumbuka kuwa kila jaribu linalokuja kwa mwanadamu huwa linayo njia yake ya kutokea? Basi amini kuwa hata kikwazo hiki tukakiruka. Kama unaweza kwenda tena kwa huyo Masawe basi hakikisha kuwa unachukua alama ya hilo tundu ili tuweze kuchonga ufunguo wa bandia…….” Alianza kushauri Mama lao. Nikaingilia kati na kumweleza kuwa kile kitasa ni cha aina yake na hata ule funguo ulikuwa wa aina yake. Mama lao akasihi kuwa ni heri kujaribu kuliko kupuuzia.
Nikakubaliana naye, lakini kila nilivyoujengea picha ule ufunguo chakavu alionipatia Ezekiel na umbo lake la kustaajabisha niliamini kabisa kuwa zile zilikuwa mbio za sakafuni tulizokuwa tunajaribu kukimbia.
Lazima ziishie ukingoni tu!!
Tukaagana na mama lao, na kuahidia kupeana matokeo kwa siku inayofuata.
Huo ukawa usiku wenye matumaini kiasi fulani, lakini sikujua kama asubuhi ya siku inayofuata ingekuwa asubuhi ya kustaajabisha ndani ya jiji la Dar es salaam na wakati huo mjini Iringa!!!
Ni heri tusingefikia maamuzi yale!!
Lakini hatukujua!!!
***
ASUBUHI baada ya stafutahi ya wastani nilijongea katikati ya mji huku na kule nikitazama hiki na kile na hatimaye nikapata mahali ambapo wanachonga funguo. Nikawaeleza shida yangu, wakanielewa na kunitaka nilete alama ya tundu la kitasa ambacho nahitaji kuchonga funguo zake.
Wakanieleza kuwa alama sahihi nitaichukua kwa kutumia kipande cha sabuni.
Nilipotoka pale moja kwa moja nikaenda dukani kwa Masawe.
Alinipokea kwa furaha zote, alikuwa anatabasamu pana ambalo bila shaka lilionyesha dalili ya tumaini jipya!!
Akanisabahi kisha akanihoji kuhusu kutoweka kwangu siku iliyopita bila taarifa.
“Kwanza nilivyokuagiza ulivipata?” nilipoteza uelekeo wa swali lake.
“Sijakosa hata kitu kimoja ati! Vyote nimepata tena kwa bei poa tu!” alinijibu huku akisahau kuwa sijamjibu swali lake la awali!!
Nikataka kutia neno, Masawe akaendelea kuzungumza.
“Nikaona nom asana kuviweka humu ndani maana bosi angevikuta ingekuwa kesi, hachelewi kusema kuwa namwibia. Vipo hapo kwa jirani yangu mmoja…..”
Neno la mwisho la Masawe likanipa mwanga na akili ikafunguka!! Huo ulikuwa mwanya mwingine wa kuweza kufanya jambo.
Nikamsihi aende kuleta vitu baadhi alivyonunua niweze kuvitazama.
Masawe akatoweka akiliacha duka lake wazi. Mguu wake ukitokomea mimi nikaingia ndani ya kile kibanda, moja kwa moja katika lile tundu la funguo. Nikailowanisha sabuni kidogo kutoka katika duka la Masawe kisha nikagandamiza na kuipata alama kama walivyonielekeza mafundi.
Nikaifunika ile sabuni na kuitia mfukoni.
Masawe aliporejea mimi sikuwa na habari, nilichokitaka nilikuwa nimekitimiza tayari.
Mazungumzo kati yetu niliyaona kama kelele tu zinazonisumbua masikio, nikamzuga Masawe kuwa nimepigiwa simu fulani. Nikampa pesa kidogo na kumshukuru kwa wema wake wote. Nikatoweka nikiwa katika haraka, nikapita huku na kule nikachukua taksi.
Nikamwelekeza dereva wapi pa kunipeleka.
Akatia gari moto na kuanza kuitafuta sehemu.
Dereva huyu alikuwa muongeaji sana, akanieleza juu ya jaribio la wizi wa taksi lililofanywa na shanta mmoja akishirikiana na mteja wake. Akanielezea gari ilipokutwa!!
Nikatambua anaizungumzia gari ambayo niliitumia siku iliyopita nikiwa na shanta aliyeingia matatani na kisha kutoweka. Nikajifanya kushiriki katika maongezi yale lakini nilikuwa katika kumchimba tu nipate mawili matatu kuhusiana na na usalama wangu!!
Hali ilikuwa shwari hakuna hata mmoja aliyebahatika kukumbuka walau nguo nilizokuwa nimevaa!!!
Alinifikisha nilipohitaji nikamlipa chake na kuingia katika harakati za kuusaka ufunguo.
Nikawaonyesha wale mafundi alama ya tundu lile, wakalitazama kwa makini na kukiri kuwa hawawezi kutengeneza huo funguo na badala yake wakanielekeza kwa mzee Sendeu. Mkongwe katika kuchonga funguo za kila aina. Hata hao mafundi walikiri kuwa alikuwa kiboko yao na walimkuta katika ufundi huo.
Nikaongozwa hadi katika kibanda chake kidogo!! Akanipokea vyema na kisha tulipobaki wawili akabaki kunisikiliza. Wakati nazungumza niligundua kitu, kuwa mzee yule hakuwa na amani sana na ile miwani yake usoni haikuwa ya heri sana. Nikajipa jibu kuwa huenda huwa anawachongea majambazi funguo bandia maalum kwa shughuli zao, ama la yeye mwenyewe si mtu mwema.
Lakini hayo yote hayakuwa yakinihusu hata kwa mbali, kilichonihusu ni kuupata funguo wangu kwa ajili ya manufaa yangu!!
Nikamweleza shida ileile na kisha kumpa ile sabuni yenye alama.
Ama! Akaiachia ghafla ile sabuni!! Ikaanguka chini, akataka kutoa miwani yake usoni akasita. Akapigwa na bumbuwazi la waziwazi usoni!!
Nikaduwaa zaidi yake!! Na wala hakujishughulisha katika kuiokota ile sabuni!!
“Wewe ni nani? Aliniuliza… nikakosa cha kumjibu na nisijue nini maana ya swali lake. Nikiwa bado naduwaa niliona akibonyeza namba za simu lakini hakuzungumza chochote kile, uso wake ulitawaliwa na ghadhabu!! Nilitaka kuondoka lakini nikajiuliza ni kwanini niondoke. Yawezekana kukutana na mzee yule ni njia mojawapo ya kuifikia siri kuu!! Na mbaya zaidi kuondoka kwangu kusingesaidia chochote kile.
Lakini kubaki na mtu nisiyemjua hili lilikuwa tatizo zaidi.
Nikaamua kusimama niweze kuondoka!! Akabonyeza tena simu yake.
Milango ikajifunga tena!!
“Wewe ni nani nakuuliza??” sasa alikuwa ametoa miwani yake usoni na alikuwa anakanisogelea!!! Nikajaribu kurudiu nyuma.
Mzee alikuwa na miguu ya bandia na hata jicho lake moja!!
Hakuwa na jicho moja!!!
Alitisha kumtazama.
“Naitwa Dickson naitwa Dickson mzee wangu….” Nilijikuta nalainika na kujibu alichouliza japokuwa nilikuwa nadanganya.
Nilidhani jibu lake litamfanya aweze kutulia, lakini mara akaurusha mkono wake. Nilikuwa sijajiandaa kwa tukio hilo, kiganja chake kizito kikatua katika shavu langu.
Naam!! Maumivu makali haswa yakasambaa katika uso wote na kichwa kikakumbwa na maumivu!!
Hakuishia pale yule mzee wa kutisha.
Mara akarusha gongo alilokuwa anatumia, hata hili pia sikulitarajia lakini sijui ilikuwaje nikawahi kujikinga uso wangu. Likanikung’uta mikononi. Maumivu mapya kabisa.
“Kwa hiyo nd’o mnataka kuniua eeh!!” akatokwa na kauli hiyo. Sasa alikuwa ameikamata shingo yangu.
Uso wenye jicho moja ukawa unatisha zaidi ulipokuwa karibu nami!!
“Nilitamani kusema neno lakini alikuwa amenikaba haswa! Macho yakamsihi lakini ni kama hakutambua hilo.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kindo na mwenzake wapo wapi?” aliniuliza swali lile huku akiamini kuwa jibu ninalo basi tu ni kiburi.
Akaniachia ghafla nikawa nakohoa kwa fujo!!
Na hapo akatoa kisu kikali sana.
“Usipojibu maswali yangu nakufanya kama nilivyofanywa, nang’oa jicho, nakata miguu na masikio, nakung’oa na hiyo pua yako mwanaharamu wewe…” Akazungumza haya huku akitetemeka.
“Naitwa Sam mzee wangu, hakuna nijualo kuhusu hayo unayoniuliza niamini mzee wangu sijui lolote na mimi ni mtafutaji tub ado sijapata chochote.” Nilizungumza huku nikitokwa machozi.
Akanisogelea kwa kuchechemea, akanifikia.
“Unataka kufa eeeh!!” akasema kwa sauti ya chini inayosihi.
“Bonge waitio amekutuma kitu gani kwangu? Na nd’o nani huyo bonge waiti…..” akaniuliza tena, ni kweli niliwahi kuyasikia hayo majina mahali lakini sikuwa na maelezo yoyote ya kuweza kujibu.
“Mzee wangu, nipe dakika tano tu za kujieleza kinaga ubaga na baada ya hapo nitakuruhusu unifanye utakavyo iwapo tu itakuwa ni haki yangu kuuwawa kinyama namna hiyo. Na kama ikithibitika mimi ni mtu mbaya mzee wangu, usisite kunisulubu. Lakini amini kuwa ukifanya suluba hiyo bila kunisikiliza basin a kilio changu kiwe juu yako milele.” Nikajitutumua na kutokwa na kauli ile ya mwisho ambayo sikutarajia inaweza kuwa chachu ya kutuliza munkari ya yule mzee mwenye jicho moja!!
Kwa ishara ya kichwa akanipa nafasi ya kuzungumza!! Kisu kikiwa mikononi mwake imara.
Huo haukuwa wakati wa kuficha siri tena, nilikuwa katika dakika za mwisho za uhai wangu.
Nikamweleza mzee juu ya uhalisia wa jina langu, wapi natoka na kisha nikamweleza juu ya kukutana na kijana shoga aitwaye Ezekiel jijini Dar es salaam, nikakumbuka kumwelezea mwonekano wa Ezekiel na sikusahau tarehe za kukutana kwetu.
Nikagusia juu ya utata wa Ezekiel wa Ubungo na yule maiti wa Temeke Dar es salaam.
Sikuuyumbisha ukweli nikamweleza juu ya mke wangu kupotea na kisha mimi kuanza kuzushiwa juu ya mambo kadha wa kadha ikiwemo kifo.
“Wewe kumbe nd’o Samson….. Sam….” Alitokwa na maneno yale mzee huku kisu kikiwa kimemtoka tayari. Alikuwa ameduwaa haswa.
Mara akafungua makablasha kadhaa akatoka na magazeti kadha wa kadha, akachomoa mojawapo. Akakutana nna habari yangu, akaitazama ile sura na kujihakikishia kuwa sikuwa nimemdanganya hata kidogo.
“Sam… umewakwepa vipi hadi sasa hawa watu wasijulikana sura zao” aliniuliza huku akinisaili kwa chati.
Sikuamini kama uso wa yule mzee unaweza kulainika na kuwa katika masikitiko kiasi kile.
Sikuwa na uwezo wa kujibu chochote kile. Ni kama nilikuwa ndotoni tu!!
Mzee akajishughulisha zaidi akachukua pamba na kunifuta damu mdomoni, kisha akaniomba niketi tuzungumze.
Mzee Sendeu!! Akanielezea juu ya mkasa wake. Mkasa uliowahusisha Kindo na mwenzake ambaye hakuwa akimtambua jina lakini alikiri kuwa sura yake na ya huyo Ezekiel niliyemtaja ni kitu kimoja!!
“Wale vijana waliniletea tenda ya kutengeneza funguo, hakuna funguo iliyonitia wazimu kama ile pale. Kila nikijaribu kutengeneza wanaenda na kurejea wakidai haifungui ule mlango. Natengeneza tena na wao wanalipa pesa nzuri tu… nikakataa tenda zote nikabaki na tenda moja tu ya kutengeneza ule funguo wa ajabu. Kila nilipowasihi waende kunionyesha kitasa wakadai kuwa ni mbali sana. Kwa sababu ni wao walikuwa wanasema basi mimi nikaendelea kukuruka huku na kule nifanikishe kuwafurahisha wateja wangu.
Mara ya mwisho kuonana nao wote kwa pamoja ilikuwa ni siku ambayo walidai kuwa walau ule funguo unazo dalili za kufungua japo kwa kulazimisha.
Baada ya hapo wakatoweka moja kwa moja!! Na hapo nikaanza kuandamwa na watu nisiowajua wakinihoji juu ya mambo nisiyoyajua vilevile.
Siku moja nikakamatwa na polisi, lakini sikupelekwa rumande nikafungwa kitambaa usoni na kwenda kukutana na mtu aliyeitwa bonge waiti. Alikuwa anazungumza kiingereza na walitafsiri nami nikawa najibu.
Yule mtu akaniomba funguo! Nikasema sijui lolote juu ya funguo. Ebwana walinishushia kipigo cha hali ya juu sana ndugu yangu!!
Nakuja kupata fahamu nikiwa porini huko, mguu mmoja haufanyi kazi, na jicho moja likiwa halioni, meno yote haya ya mbele unayoyaona ni ya bandia sina meno Sam. Wale watu ni zaidi ya majasusi na sijui niliweza vipi kupona kutoka katika kifo kile.
Niliokotwa na mmoja kati ya majangili ambayo huwa nayatengenezea funguo kwa ajili ya kwenda kuvamia wanapojua wao. Tena waliniokota wakiwa katika shughuli zao za kijangili.
Wakanichukua hadi katika machimbo yao.
Amakweli tenda wema uende zako bila kuangalia ni nani ulimtendea wema. Wale watu walimtafuta daktari na kunipatia tiba, mguu ulikuwa si mguu tena ukakatwa, jicho haliukuwa jicho tena likang’olewa na kubaki na jicho moja.
Nilikuwa naitwa Masta key kabla sijatekwa na kupotezwa, basi nikalazimika kufuga ndevu tele na kisha wale majangili wakanitengenezea maficho haya niendelee na shughuli zangu nikiwa katika usalama wa hali ya juu. Na hapo wakaniita mzee Sendeu. Na hilo nd’o jina langu maarufu kwa sasa.
Watu wanaamini kuwa mimi ni mrithi wa Masta Key ambaye wanadai alitoweka kishirikina.
Hawajui kuwa nd’o mimi hapa.
Sasa leo ulipouleta ufunguo ulionisababishia majanga haya nikakuona kuwa wewe naye ni mmoja wa watu wabaya wanaofahamu siri yangu!! Sam kiuhakika nisingekutambua basi ungekufa kifo kibaya sana leo.” Alimaliza mzee yule kunieleza juu ya simulizi ile ya kutisha na kusisimua.
Mwili ulisisimka haswa nikijaribu kujenga picha juu ya mwanadamu kung’olewa jicho na kukatwa mguu.
Watu ninaokabiliana nao walikuwa wanyama haswa!!!
Wakati nikiendelea kufikiria juu ya tukio hilo la maajabu. Mara katika simu yangu ukaingia ujumbe!!
Hakuwa mwingine alikuwa ni Mama lao..
“SAM HALI SI SHWARI MZEE MATATA MATATANI”
Nilichoka!!!
Mzee akaishtukia hali ile ya hofu niliyokabiliana nayo, nami sikuona hiyana kumshirikisha. Nikamweleza juu ya Jojina na mkakati wetu. Na sasa amenasa huko jijini Dar.
“Mpigie simu tujue!! Kama ni hawa vijana niwaamnbie wakusaidie.” Alinishauri, nami nikapiga namba za Jojina.
Simu ikapokelewa!!
“Sam, huu mtandao ni hatari. Nasi tupo katika hatari kubwa sana. Mzee Matata amesimamishwa kazi, nyumba yake inauzwa juma lijalo.” Jojina alinieleza hayo kwa sauti ya chini tulivu!!
“Sikuelewi Jojina unamaanisha nini hata!!”
“Bosi wake mzee Matata ndo katoa tamko hilo la kumsimamisha kazi eti anaandika habari za kichochezi!!...” alijibu kinyonge.
Nikastaajabu, tangu zamani nilijua kuwa mzee Matata nd’o mmiliki wa ile kampuni, kumbe na yeye ana bosi wake. Nilistaajabu mno, kisha nikajenga picha ya huyo bosi wake na kujiuliza iwapo namfahamu ama nimewahi kuona Matata akiongozwa na mtu yeyote.
Hapakuwa na jibu la uhakika, na kama ningeamua kuwa na jibu basi ni kwamba ofisi kuu ya gazeti lile ilikuwa ile ya mzee Matata.
“Kwa hiyo sasa…” nilijikuta nikiuliza tu bila kuelewa kwa nini nauliza.
“Hatuna hata senti tano, akaunti zake zote zimefungwa. Mkewe tangu atoweke kwenda katika mambo ya vikao vya wanawake hajarudi na simu haipatikani.” Alizidi kunyong’onyea.
“Na mzee mwenyewe yupo wapi?”
“Nimemficha mahali Sam, hali si shwari na nimempa onyo asitoke hata kidogo. Hilo si jambo la kawaida. Amenielewa na ametii. Sam kiuhakika tunahitaji pesa kwa namna yoyote ile huku si kwema tena. Hawa watu wapo Tanzania nzima. Hakika ukiwajua ama ukitaka kuwajua tu unapotezwa!!” mama lao alisihi.
Sikuona haja ya kumweleza lolote ambalo mimi binafsi nilikuwa nimepitia, badala yake nilimuahidi pesa hiyo aliyoihitaji kuwa nitamtumia. Mzee Sendeu alitikisa kichwa kuunga mkono namna nilivyokuwa namjibu mama lao.
Jambo hilo likazidisha imani yangu kwake na mwisho akatokwa na machozi na kuniambia neno lililonifanya niingiwe uoga lakini na huruma vilevile.
“Natamani ningekuwa na miguu yangu yote miwili, natamani wasingeharibu jicho langu hili. Leo hii ningeongozana na wewe katika harakati hizi za kujua kuna nini kinafichwa hapa. Lakini wameniwahi na kunitia ulemavu wa maisha na bila shaka nikithubutu kutoka humu ndani wataniua kwanza mimi kabla ya kuwatesa sana ninyi!! Hawa si wanadamu wa kawaida Sam. Nakushauri kama ipo nafasi wewe jiweke mbali nao. Kaa mbali tu haidhuru kitu.
Sikukatishi tamaa lakini elewa kuwa namna yangu ya kupona na kuendelea kuwa hai si kila mmoja awezaye kupona hivi.” Alimaliza huku akinikazia jicho lake moja.
Chumba kilikuwa kimya kwa sekunde kadhaa kabla simu yangu haijaita tena!!
“Jojina..”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sam…. Nilisahau kukwambia kitu kimoja, katika purukushani hizi za hapa na pale nimegundua kitu, sijui kama ni chenyewe ama la!! Lakini hata kama ni chenyewe Sam, sikushauri uende mbele zaidi. “
“nini tena jojina…”
“Ni ule ufunguo chakavu, sina uhakika sana lakini nimekuta kitu kama hicho katika pochi langu!! Sijui kama ni wenyewe na hata kama ni wenyewe Sam nakusihi, tusitishe kwa muda kidogo harakati hizi hata pale tutakapoonana sote kwa pamoja…” kauli ya funguo ilituliza jazba zangu maana nilipanga kumkaripia mama lao kwa kuwa kigeugeu, mara juzi aniite mimi muoga leo hii tena anasema tuahirishe.
Na hapo likanijia wazo la kucheza na akili ya Jojina.
“Jojina ni kama ulikuwa katika mawazo yangu!! Umoja ni nguvu hakika, nitawangoja. Lakini nakusihi jambo moja ulifanye. Uagizie huo funguo kwa njia nyepesi uweze kunifikia huku. Nihakikishe kama ni wenyewe ili niachane na haya mambo ya kuchonga kisha nawasubiri…..fanya hima Jojina wakati hao wajinga wapo huko huko Dar.” Nikarusha maneno, yakamwingia Jojina…
Akakubaliana nami.
Hakujua kichwani mwangu nawaza nini. Nilikuwa na hasira na sikuwa na hofu tena.
Liwalo na liwe!!!!
Nikaagana na mzee Sendeu nikatoweka na kumwahidi kurejea tena kwake kwa ushauri zaidi.
BAADA ya siku mbili nikapokea funguo zile zikiwa zimetumwa kwa njia ya basi, ziliambatanishwa katika kitabu kikubwa katika bahasha, jina lililoandikwa ni Jonhson Fortunatus. Nami nikajitambulisha kwa jina lile nikapokea bahasha.
Swadakta!! Ulikuwa wenyewe, ufunguo alionipa Ezekiel maeneo ya Ubungo. Kitu ambacho sikujua matumizi yake lakini sasa natambua kuwa ni kitu muhimu sana ninachokihitaji.
Nikiwa na munkari ya hali ya juu sana, nikaondoka muda huohuo na kurejea nyumba ya kulala wageni. Huku nikaweka mikakati sawa. Mikakati ya kumhadaa Masawe tena ili nifanikiwe kutimiza jambo nililowaza!!
Kuingia katika hifadhi ile ya siri!!
Pombe!!
Ni hiki kitamfanya ahadaike na mimi niingie ndani!!
Nikasinzia na wazo hilo!!
*****
KINDO CHIZI
MASAWE alikuwa ameikubali ofa yangu, akaanza chupa ya kwanza, mara ya pili hadi ya sita akili yake ikawa imevurugika na akawa mcheshi sana. Mimi nilikuwa makini sikunywa kwa pupa. Nilitaka yeye alewe mimi nifaidike, wasiwasi ulikuwa kidogo maana nilishahakikishiwa kuwa watu wabaya walikuwa Dar es salaam wakinitafuta.
Nilibeba bia za kutosha na kuzileta katika banda la Masawe!!
Wachaga kwa pombe!! Mbona nilimuweza.
Masawe alipopendeza kichwani nami nikajifanya nimelewa nikaanza kumuuliza maswali hapa na pale.
Hatimaye akaanza kuropoka hapa na pale juu ya bosi wake.
“Bosi wangu mimi mpole sana lakini hataki tu kuchokozwa yule, yaani kingine hataki kabisa ujue mambo yake hovyohovyo, mimi sitaki kujua mambo yake kwa sababu ananilipa lakini mbili yangu, nakula na kulala bure. Bosi wangu mtu safi sana lakini watu wanamchokoza..” akasita kidogo kisha akabeua, akapiga funda jingine kisha akaendelea, “Mambo ya bosi ni ya bosi mimi hayanihusu, hata Kindo nilimwambia aache kuwa na kiherehere akaniona mimi bwege wa mwisho, eti kisa tu aliwahi kufanya kazi sijui wapi huko panaitwa eheee Michigani, nd’o huko na mimi niliambiwa nakuja kufanya kazi lakini nikaishia hapa, hata picha za hiyo hoteli sijawahi kuziona mimi. Kindo alikuwa ananihadithia, mara Michigani sijui inafanya nini mara huko Michigani nd’o kuna raha za dunia. Hebu tazama shehe wangu mfano mimi umeniajiri wewe halafu tena naleta mtu mwingine ndani ya duka lako, we utanielewa kweli. Sio mara moja au mbili, Kindo anamleta ndugu yake humu ndani, anaitwa nani vile sijui Alvin kitu kama hicho. Huyo Alvin akifika mara wananiambia nitoke nje, mara wananiambia mimi sijui mshamba.
Maneno yale yakanikera kweli ndugu yangu nikashindwa kuvumilia nikamweleza bosi.
Siku hiyo Kindo akaitwa na bosi, sijui waliongea nini hata lakini baada ya siku mbili akawa haji tena kazini, nikamkuta akiwa chizi huko anaokota makopo mtaani. Mimi siwezi kumchokoza mtu wa namna hii hata kidogo.”
“Na huyo Alvin wakasaidia kuokota makopo ama?” nikamuuliza Masawe mlevi.
“Alvin hakuonekana tena, bosi alikuwa haijui hata sura yake kwa jinsi alivyoniambia lakini alikuwa akimsaka sana. Nikamuuliza kama kuna tatizo. Akasema kuna vitu fulani havionekani mle ndani, huenda wameviiba…. Kuna kauli moja aliisema nd’o nikaamini kuwa si mtu mzuri huyu bwana. Akasema Kindo mwenyewe nshamtia uchizi hata hawezi kunisaidia kitu!!. Kwa maana hiyo ni yeye aliyemtia uhayawani yule jamaa. Wanadamu we acha tu…” alisikitika kisha akafakamia tena pombe!!
Akaniachia nafasi ya kufanya tafakuri, juu ya Kindo na jina hili la Alvini.
Sasa inamaana Alvin ndo Ezekiel kweli na hili ndo chimbuko lake, na je yawezekana baadhi ya vitu alivyochukua na ufunguo ulikuwa mmoja wa hivyo vitu? Pamoja na makaratasi yale labda!!
“Masawe!! Kwa hiyo Kindo yupo bado hapa Iringa na je akikuona hakukumbuki ama…”
“Hayupo yule, nilimsikia….. ujue bosi wangu ni rafiki yangu sana na ananiamini, nilimsikia akijisemesha ili nimsikie alisema kuwa hatimaye amemkamata huyo wa kuitwa Alvin, kisha akajisifu kuwa ameua ndege wawili wa jiwe moja jijini Dar yaani kindo na Alvin. Mimi kama unionavyo huwa simuulizi maswali na nadhani nd’o kitu anapenda yaani niwe bwegebwege hivi hivi.”
Majibu ya Masawe yakanitoa ukungu machoni!
Huyu bosi wake anajua kila kitu juu ya mkakati unaoisumbua akili yangu na anajua pia juu ya sakata zito la anti Ezekiel.
Nikataka kumhoji zaidi lakini alikuwa anakoroma tayari kwa usingizi.
“We Masawe wewe!! Masawe!!” nikajaribu kumtikisa lakini hakujibu kitu zaidi ya kuendelea kukoroma, hakika alikuwa amelewa!!
Ni hiki nilikuwa nahitaji, alewe sana ili aropoke mengi na kisha asinzie kabisa niweze kufanya yangu!!
Yote yalikuwa yametimia.
Ni mimi tu niliyesalia kuchukua maamuzi!!!!
Nikasimama kwa tahadhari, nikajipekua na kukutana na ule funguo kutoka jijini Dar es salaam.
Nikaingia hadi nikaufikia ule mlango wa siri, nikachomeka funguo ule. Mlango ukafunguka ulikuwa na kuselelesha kushoto na kulia. Nikauselelesha hivyohivyo. Nikapata upenyo nikachungulia ndani, palikuwa na mwanga hafifu sana, nikatega sikio nisikie kama kuna watu ndani yake lakini hapakuwa .
Nikajipenyeza vyema na kuingia ndani nikapokelewa na hewa murua si baridi sana lakini inayoburudisha. Nikashuka ngazi moja baada ya nyingine huku macho yangu yakitazama huku na kule, nilipoikanyaga ngazi ya tatu mara taa kali zikawaka, na mlango huku nyuma ukajifunga.
Hofu ikatanda!!!
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
**SAM amejitoa muhanga na kuingia katika mlango huo wa siri!!!
**NINI KITAJIRI HUMO!!! MILANGO IMEJIFUNGA!!!
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment