Simulizi : Mimi Kabla Yako
Sehemu Ya Tatu (3)
Mtoto huyo alimshtua bwana Abraham kwa vile alikuwa amefanana kwa kiasi kikubwa na Sabinus, mwanaye aliyekuwa ameshafariki. Akiwa bado hajaongea jambo msichana aliyekuwa ameongozana naye alisikika akiongea. “That’s your child Mr. and you don’t have to argue because you two have cloned” (“yule ni mtoto wako na hustahili kubishia kwa vile mmefanana”).
Bwana Abraham alimwangalia msichana huyo kabla ya kumkimbia na kwenda kumnyanyua mtoto huyo na kuanza kumbusu akiwa na furaha. Baada ya sekunde kadhaa Aminata alitokea na kumwona bwana Abraham eneo hilo. Hakuongea jambo zaidi ya kuanza kulia akimlaani mwanaume huyo kwa kumtelekeza mwanaye. Bwana Abraham aliligundua kosa lake hilo huku akiwa na amani baada ya kumpata mtoto ambaye alikuwa tatizo katika maisha yake. Alimsogelea Aminata aliyekuwa akitulizwa na msichana aliyefika naye, hakupoteza muda kwani alipiga magoti na kuanza kuomba msamaha na zaidi aliahidi kumwoa Aminata. Huku akilia bwana Abraham alikuwa na furaha ya kumpata tena mtoto jambo lililokuwa tatizo kwake.
Baada ya wiki mbili Aminata na mwanaye Gray walikuwa katika nyumba ya kifahari ya bwana Abraham huku maisha yakionekana kubadilika ndani ya muda mfupi. Wakati huo bwana Abraham alikuwa na wake wawili huku mkewe wa zamani akiwa hana nafasi tena kwani alilala katika chumba cha peke yake. Mama huyo alikuwa amekonda ndani ya muda mfupi huku akiwa na majereha mwili mzima kutokana na kipigo alichokipokea kutoka kwa mumewe kila siku. Bwana Abraham alikuwa amembadilikia kama siyo mwenyewe ambaye alishirikiana na mwanamke huyo kuupata utajiri huo baada ya kumuua mdogo wake Johnson. Akilini bado alikuwa akipanga mipango ya kumuua kabisa mwanamke huyo kwani Aminata aliyekuwa mrembo na kijana alimtosha kwa wakati huo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Bado alikuwa anampiga mwanamke huyo kila siku ambaye hakujua hatma ya maisha yake. Hatimaye alimuamuru aanze kufanya kazi ya kusambaza bidhaa za kampuni yake ya nguo ya Abraham Textile Industry sehemu tofauti za nchini humo. Alifanya jambo hilo ili kumfanya mkewe asiwepo nyumbani kwake muda wote lakini pia alikuwa akiandaa mikakati ya kumuua kabisa. Agizo hilo la bwana Abraham lilichukua nafasi na mwanamke huyo alianza kuzunguka na magari ya mizigo ya kampuni hiyo sehemu tofauti za nchini humo. Wakati huo bwana Abraham alibakia jijini Entebbe na familia yake mpya akiwa na amani kwa kiasi lakini zaidi akimwazia David, mtoto aliyekuwa bado anamsubua.
Akiwa na huzuni juu ya kila jambo lililokuwa linaemdelea aliutambua unyama wa mambo yote waliyowahi kufanya na mumewe. Mkewe mkubwa bwana Abraham alijikuta akitamani sana kuonana na David ili amwombe msamaha kwa makosa yote aliyohusika katika familia ya marehemu Johnson. Wakati huo aliamini mwisho wa kukaa na mumewe bwana Abraham ulikuwa umefika ikiwa ni baada ya Aminata kubadili nafasi yake. Alikuwa amedhoofu kiafya huku akiwa hajijali kama ilivyokuwa awali. Muda wote alikuwa kwenye gari aina ya Scania ambalo lilikuwa likisambaza bidhaa za kiwanda cha mumewe sehemu tofauti za nchini humo. Kwa muda wa zaidi ya mwezi mmoja hakulala nyumbani kwake huku akiwa hana mawasiliano na mumewe ambaye hakutaka kumsikia kabisa. Wakati huo hata imani ya dini ilimrudia na mara kadhaa alikuwa akimwomba Mungu amwokoe David asinase kwenye mkono wa mumewe bwana Abraham.
Siku moja wakati akiendelea na zoezi hilo la kusambaza bidhaa katika eneo la Kiriri lililokuwa kusini mwa Uganda alifanikiwa kumwona David. Katika harakati za kukutana na mtoto huyo alimkimbia. Hakushangaa sana ingawaje aliuumia juu ya tukio hilo huku akiamini mtoto huyo alidhania kuwa bado alikuwa mtu katili kama mumewe. Aliamua kuacha fedha na namba ya simu yake katika duka moja akiamini kama David angerudi na angechukua fedha hizo na mwishoe angemtafuta. Haikuwa hivyo kwani siku kadhaa zilipita pasipo kupigiwa simu na mtoto huyo. Hakumweleza mumewe juu ya jambo hilo huku akiamini akimwambia angesababisha David atafutwe katika eneo hilo la Kiriri na mwishoe angeuawa.
Wakati akiendelea na zoezi hilo la kuuza bidhaa hizo alishtuka siku moja baada ya kuona mumewe akimpigia simu kwani alishamtoa kabisa akilini. Bwana Abraham alimtaka mwanamke huyo arudi nyumbani ili wakaendelee kuishi kama kawaida na alionekana akikili makosa juu ya kila jambo lililokuwa limetokea. Alifurahi juu ya taarifa hizo huku akiamini kuwa huenda mumewe alikuwa amebadilika kutokana na upole aliouonesha. Wakati huo alikuwa akiwaza kuitumia nafasi hiyo ya kuwa karibu na mumewe tena katika kumbadilisha mtazamo wake wa ukatili aliokuwa nao. Siku ya Jumamosi majira ya saa moja alikuwa akifika nyumbani kwao, moyoni alikuwa na hofu akiamini Aminata aliyekuwa mke mpya wa bwana Abraham huenda alikuwapo pia nyumbani hapo. Haikuwa hivyo kwani nyumba hiyo ilikuwa tulivu huku ikiwa imepambwa kwa mwonekano tofauti.
Mapambo mengi yalikuwa yameandikwa ujumbe wa kumwomba msamaha juu ya mambo yote aliyokuwa amefanyiwa na mumewe huyo. Aliingiwa na faraja juu ya ujumbe huo aliokuwa anaendelea kuusoma. Ghafla bwana Abraham aliingia eneo hilo la sebuleni kabla ya kuanza kuomba msamaha kwa mkewe na mwishoe aliishia kupiga magoti kabisa. Alidai alikuwa amemfukuza Aminata baada ya kuona umuhimu wa kurudiana na kuimarisha ndoa yao. Zaidi alidai aligundua Aminata hakuwa mwaminifu katika mahusiano. Mkewe bwana Abraham hakuwa na makuu zaidi ya kumsamehe mumewe huyo kwa kila jambo alilokuwa amefanya. Wakiwa na furaha walikumbatiana huku wakionekana kuwa na mwanzo mpya wa maisha yao. Majira ya saa tano usiku walikamilisha hafla yao hiyo iliyokuwa ya watu wawili. Ni wakati ambao wote walikuwa wamelewa baada ya kutumia kiasi kikubwa cha pombe. Walielekea kulala wakiwa tayari wamepata hatma mpya ya ndoa yao iliyoanza kuingia dosari baada ya kufariki kwa mwanao pekee Sabinus.
Majira ya saa tisa usiku magari mawili aina ya Land Cruiser yalionekana yakiingia katika nyumba hiyo ya bwana Abraham baada ya geti kufunguliwa na mlinzi wa nyumba hiyo. Magari hayo yaliongozwa mpaka katika eneo la maegesho la nyumba hiyo. Walishuka vijana wanne kutoka katika kila gari huku wakiwa katika mwonekano wa kihalifu. Walikuwa wamevaa miwani iliyopoteza mwonekano wa sura zao. Pia walikuwa wamevaa makoti marefu huku mabuti yao yakiwa kama ya jeshi la polisi. Mwonekano wao wa mavazi hayo yaliyokuwa ya rangi nyeusi haukuwa wa amani hata kidogo kwani wachache wao walikuwa na bunduki mikononi mwao. Wengine walikuwa na zana tofauti yakiwapo mapanga. Katika eneo hilo la maegesho ambalo vijana hao waliokuwa na miili iliyojengeka walionekana wakielekezwa jambo na mtu aliyekuwa kama kiongozi wao. Kiongozi huyo hakuwa mwingine, bali ni Joseph Kanyenzi maarufu kama Killa Jose, kijana aliyehusika na matukio tofauti aliyotumwa na bwana Abraham. Alihusika na matukio yote ya mauaji ambayo yalitokana na amri ya bwana Abraham. Uwezo wake katika kazi hizo haramu ndio uliomfanya apendwe sana na kiongozi wake huyo.
Baada ya mazungumzo ya muda mfupi na vijana wake, Killa Jose akiwa na ufunguo mkononi aliwaonyeshea ishara vijana wenzie ambao walianza kumfuata nyuma. Aliongoza mpaka katika mlango wa kuingilia katika nyumba ya bwana Abraham kabla ya kuonekana akiufungua mlango huo. Baada ya kuufungua mlango huo vijana hao wakiongozwa na Killa Jose wote waliingia katika nyumba hiyo. Walitulia kidogo katika eneo la sebuleni huku wakionekana kuangalia huku na huko. Kisha walionekana wakianza kutembea kuelekea eneo lililokuwa na chumba cha kulala cha bwana Abraham. Mara baada ya kuufikia mlango wa chumba hicho, Killa Jose alijaribu kuufungua kabla ya kugundua ulikuwa umefungwa. Aligeuka na kuomba shoka kutoka kwa kijana wake mmoja, mara baada ya kuchukua shoka hilo alilinyanyua na kulielekeza katika kitasa cha mlango huo huku akiwa na lengo la kuuvunja.
Hakupoteza muda aligonga kitasa cha mlango huo akitumia shoka hilo, alirudia zoezi hilo kwa mara tano hatimaye mlango huo ulifunguka kabla ya kuingia kwao ndani ya chumba hicho. Mara baada ya kuingia walimkuta bwana Abraham na mkewe waliokuwa wamelala wakiwa wameshtuka kutokana na kelele za mlango huo uliovunjwa. Wote walikuwa wamevaa nguo za kulalia huku wakionekana kutoelewa jambo lililotaka kuendelea. Killa Jose aliamuru bwana Abraham na mkewe washuke kitandani haraka iwezekanavyo jambo lililochukua nafasi. Baada ya kushuka kwao huku wakitetemeka zaidi mkewe bwana Abraham. Killa Jose aliwaamuru vijana wake wamfunge kamba bwana Abraham jambo lililochukua nafasi haraka, kwani baada ya dakika kadhaa tajiri huyo alikuwa amefungwa kamba. Aliamuriwa na Killa Jose apige magoti na bila kupoteza muda alitekeleza amri hiyo.
Mkewe alibaki akiwa amesimama huku akitetemeka akihofia jambo ambalo lingetokea usiku huo. Tayari moyoni alikuwa na hisia za kuamini kuwa mwisho wake wa maisha ulikuwa umefika. Akiwa bado anatafakari mambo mengi kwa muda mfupi alishtukizwa na teke la uso alilopigwa na Killa Jose lililopelekea aanguke chini. Alianza kulia kwa uchungu juu ya kipigo hicho huku akiwa anamfahamu Killa Jose kuwa ni miongoini mwa vijana wa mumewe. Wakati akiendelea kulia kwa uchungu bwana Abraham naye alikuwa akilia huku akisisitiza kuwa yuko tayari kutoa kitu chochote lakini mkewe asipigwe. Haikuwa hivyo Killa Jose aliwaamuru vijana wake wampige mkewe bwana Abraham eneo alilokuwapo. Bila huruma vijana hao walijongea sehemu husika na kuanza kumpiga mwanamke huyo kila sehemu ya mwili wake. Alilia kwa uchungu lakini hakusamehewa hata kidogo. Baada ya dakika tano eneo alilokuwapo mwanamke huyo lilikuwa limezungukwa na damu huku akiwa hana fahamu.
Ni wakati ambao ulikuwa wa kushangaza kwani bwana Abraham alikuwa akitabasamu huku akionekana kama alikuwa mmoja wa vijana hao. Kijana mmoja alikuwa akimfungua kamba walizokuwa wamemfunga na baada ya muda mfupi alikuwa huru kabla ya kusimama na kumkumbatia Killa Jose. “ Well done my killer, I appreciate you then make sure you kill this woman in two hours” ( “Vizuri muuaji wangu, nakukubali na uhakikishe unamuua huyu mwanamke ndani ya saa mbili”) Alisikika bwana Abraham baada ya kukumbatiana na Killa Jose, aliongea huku akimgusa mkewe kwa mguu wake. Ni wakati ambao aliamini mipango yake ilikuwa imekamilika kiasi, kwani bwana Abraham alikuwa anahusika na kila jambo la tukio hilo la kutekwa kwao. Aliitumia njia hiyo ili mkewe asigundue kuwa yeye ndiye alipanga kifo dhidi yake.
Abraham aliwahurusu vijana wake wakiongozwa na Killa Jose waondoke nyumbani kwake hapo kwa safari ya kwenda kumuua kabisa mkewe huyo. Mkewe alibebwa na vijana wanne ambao waliongoza mpaka kwenye gari moja kati ya magari mawili waliyokuwa nayo. Walimpakiwa mwanamke huyo kwenye buti ya gari hilo, baada ya zoezi hilo magari hayo yaliwashwa na kuondolewa kwa kasi eneo hilo la nyumbani kwa bwana Abraham huku tajiri huyo akiwa amebaki nyumbani kwake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Walikuwa wakielekea katika msitu mmoja uliokuwapo nje kidogo ya eneo hilo la Entebbe. Magari yao yaliendeshwa kwa kasi nyakati hizo za majira ya saa kumi usiku wakiwa na lengo la kukamilisha kazi hiyo haraka ili kuendelea na shughuli zao nyingine. Wakati safari hiyo fupi ikiendelea Killa Jose alikuwa mtulivu tofauti na awali huku makunyanzi ya sura yake iliyojaa hasira muda wote yakiwa hayapo. Alionekana kama alikuwa akifikiria jambo. Vijana wake walikuwa wakiendelea kutumia dawa za kulevya na pombe huku wakiwa na furaha juu ya kila jambo lililokuwa likiendelea.
Killa Jose alikumbuka mambo mengi yaliyokiumiza kichwa chake wakati huo. Alikuwa akihisi ni vigumu kumuua mkewe bwana Abraham hiyo ilifuata baada ya kukumbuka mambo mengi yaliyomhusu mwanamke huyo aliyeshirikiana kwa kila jambo na mumewe kabla ya kukorofishana kwao. Alikumbuka mambo mbali mbali ya mipango ya mauaji ikiwa ni pamoja na jaribio lililoshindwa la kumuua David ambalo mwanamke huyo alihusika pia. Zaidi alikuwa akimheshimu mwanamke huyo kutokana na fedha nyingi alizokuwa akiwalipa mara baada ya kufanya kazi tofauti. Mambo hayo ndiyo yaliyomfanya Killa Jose abadilishe msimamo mzima wa tukio hilo. Aliwaza kuto muua mwanamke huyo huku akiamini jambo jema lilikuwa ni kumwacha aendelee na maisha yake pasipo bwana Abraham kujua kama alikuwa hai.
Alichukua karatasi na peni kabla ya kuonekana akiandika kitu, aliandika juu ya msimamo wake katika tukio hilo wa kuto muua mkewe bwana Abraham. Katika ujumbe wake aliowaza usomwe na mwanamke huyo alisisitiza kuwa kila jambo lililokuwa limetokea lilikuwa chini ya mpango wa bwana Abraham. Mwishoe alimtaka mwanamke huyo aihame kabisa nchi hiyo ya Uganda ili kuokoa maisha yake kama angeweza. Baada ya kuuandika ujumbe huo kwenye karatasi hiyo aliikunja na kuiweka katika mfuko wake wa shati. Alitulia kidogo kabla ya kuonekana katika mwonekano wa mtu aliyekuwa hana huruma huku akiwa anaiandaa bastola yake. Wakati huo walikuwa katika misitu iliyofungamana kila upande ambayo ililifanya eneo hilo liwe na giza nene kupindukia. Killa Jose aliamuru magari hayo yasimamishwe akidai muda wa mauaji dhidi ya mwanamke huyo ulikuwa umefika.
Magari hayo yalisimamishwa na vijana wote walishuka, Killa Jose aliwaamuru wamshushe mkewe bwana Abraham jambo lililochukua nafasi ndani ya dakika kadhaa. Mara baada ya mwanamke huyo kushushwa kwenye gari Killa Jose alisikika akisisitiza kuwa mauaji dhidi ya mwanamke huyo yangefanywa kwa mkono wake mwenyewe. Hakuna kijana aliyebishia na jambo hilo lilieleweka huku wakiamini angeua kama alivyoahidi kwa vile hakuwa mtu mwenye huruma hata kidogo. Killa Jose akiwa na bastola katika mkono wake wa kushoto alianza kumburuza kwa kumvuta mwanamke huyo, alitumia mkono wa kulia huku akielekea upande wa msituni kulikokuwa na giza nene. Vijana wake walimshuhudia taratibu akizamia msituni humo kabla ya kutomwona tena kutokana na giza hilo lililokuwapo eneo hilo. Kulikuwa na mwanga wa wastani eneo lililokuwa na magari hayo lakini sehemu nyingine zilitisha kutokana na kuwa giza.
Killa Jose huku akimvuta mkewe bwana Abraham alimburuza kwa umbali wa mita hamsini, umbali huo alikuwa amelizika nao. Ni muda alioona ulikuwa muafaka kunusuru maisha ya mwanamke huyo kadri alivyoweza. Aliichukua karatasi aliyokuwa ameandika ujumbe mfupi wakati akiwa kwenye gari na karatasi hiyo aliiweka katika kichwa cha mwanamke huyo. Baada ya zoezi hilo aliichukua bastola yake kisha akaikoki kama vile alihitaji kuua wakati huo, aliielekeza silaha hiyo pembeni kabisa chini na kuifyatua risasi zake nne mfululizo. Baada ya kufanya hivyo alianza kukimbia akirudi eneo alilowaacha vijana wake huku akiamini wangejua amemuua mwanamke huyo kutokana na kelele za risasi zilizosikika kwa kiwango kikubwa katika eneo hilo.
Baada ya sekunde kadhaa alifika eneo alilokuwa amewaacha vijana wake ambao nao bila kuchelewa walikimbilia magari hayo na kupanda. Wote kwa pamoja waliondoka na magari hayo yaliyoondolewa kwa kasi eneo hilo huku safari ikianza wakirudi Entebbe. Vijana walioongozana na Killa Jose walikuwa wakimsifia kiongozi wao kwa ujasiri dhidi ya kila jambo. Killa Jose alizipokea sifa hizo kwa kutikisa kichwa lakini katika mawazo yake aliwaona wajinga kwa vile walikuwa hawajui jambo lolote lililokuwa limetokea. Moyoni alikuwa na hofu ya usalama wa mke wa bwana Abraham kutokana na mazingira ya kutisha yaliyokuwapo msituni lakini alipojifikiria yeye alijiona hana kosa. Aliwaza kuwa hata kama ingetokea mwanamke huyo akadhuriwa na wawanyama wakali mpaka kufa, yeye aliona hana kosa.
Wakati huo walikuwa wakielekea nyumbani kwa bwana Abraham ili kutoa taarifa juu ya kukamilika kwa mauaji hayo aliyoagiza yafanyike. Majira ya saa moja walifika nyumbani kwa tajiri huyo na kutoa taarifa hiyo. Bwana Abraham alifurahia taarifa hizo juu ya kifo cha mkewe huyo wa zamani na wakati huo aliona ulikuwa mwanzo wa maisha ya ndoa na mke wake mpya Aminata wakiwa na mwanao mpedwa Gray. Kutokana na furaha aliyokuwa nayo aliwaeleza vijana wake kuwa jioni ya siku hiyo angeandaa hafla ya kusherekea mauaji hayo huku akiwataka wahudhulie hafla hiyo. Jambo hilo lilitekelezwa na usiku wa siku hiyo kulikuwa na hafla fupi nyumbani kwa bwana Abraham ambayo Aminata akiwa na mwanaye waliitambua kama hafla ya kawaida. Aminata alielezwa na mumewe huyo kuwa hafla hiyo ilikuwa ya kumkaribisha rasmi katika nyumba ya tajiri huyo iliyokuwa ya kifahari. Siri ya hafla hiyo alikuwa nayo bwana Abraham na vijana wake waliosherekea kifo cha mke wa ndoa wa bwana Abraham. Ni wakati ambao pia alimdanganya Aminata kuwa mkewe mkubwa alikuwa haeleweki alikoenda na alikuwa hapatikani kwenye simu. Jambo hilo lilikuwa la faraja kidogo kwa Aminata aliyehitaji uhakika wa nafasi yake katika ndoa hiyo siku zote.
Siku iliyofuata kila jambo lilikuwa sawa huku mwanzo mpya wa familia hiyo ya bwana Abraham ukiwa umepatikana. Jambo ambalo lilikuwa bado likiisumbua akili ya tajiri huyo ambaye alikuwa akiona kwa jicho moja lilihusiana na David. Alikuwa ni mtoto ambaye alimkosesha usingizi mara kadhaa kwa vile aliamini lazima angeufuatilia utajiri huo uliokuwa wa baba yake. Majira ya saa saba mchana wakati akiendelea kufikiria juu ya jambo hilo, simu yake iliita alipoitazama aligundua ilikuwa imepigwa na askari wa jeshi la polisi. Bila kupoteza muda aliamua kuipokea kabla ya kupokea taarifa ambazo hakuzitegemea. Alielezwa kuwa David alikuwa amekamatwa katika eneo la Kiriri lililokuwa Kaskazini-Magharibi mwa Entebbe. Furaha yake iliongezeka baada ya kuelezwa kuwa mtoto huyo alikuwa chini ya ulinzi wa jeshi la polisi huku akiwa safarini kuelekea jijini Entebbe ili hatua za kisheria zichukue nafasi juu yake. Alielezwa kuwa jeshi la polisi lilikuwa na imani mtoto huyo aliyekuwa na kosa la kuharibu jicho la bwana Abraham pia, alikuwa mfuasi wa kundi la Eastern Black Killers, jambo hilo lilipelekea David awe na makosa mawili likiwapo la kuhusika na mauaji ya Sabinus pamoja na Otieno Ndakufurila. Bwana Abraham akiwa na furaha majira ya saa nane mchana alikuwapo katika kituo kikuu cha polisi cha Entebbe huku akiwasubiria askari waliokuwa njiani wakiwa na David, mtoto aliyeamini mwisho wa muda wake wa kuishi ulikuwa umefika kama ilivyokuwa kwa mkewe.
* * * *
Gari la polisi lilikuwa katika kasi likizidi kuliacha eneo la Kiriri likielekea Entebbe. Ndani ya gari hilo walikuwapo askari wanne ambao saikolojia zao hazikuwa sawa kwa kiasi kikubwa kwani walikuwa wakiwaza pesa toka kwa bwana Abraham aliyekuwa akitangaza dau kila siku kwa mtu ambaye angefanikisha kukamatwa kwa David, mtoto aliyeharibu jicho la kushoto la tajiri huyo na kumfanya asione tena katika maisha yake. Furaha ya askari hao walioamini wangepewa fedha nyingi kwa ajili ya kumkamata David ndio iliyopelekea dereva wa gari hilo aliendeshe kwa kasi lengo lao likiwa ni kufika jijini Entebbe haraka. Huko waliamini bwana Abraham angewatunuku fedha nyingi kutokana na kazi yao waliyoifanywa ya kumkamata David kirahisi.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mambo yalikuwa tofauti kwa David aliyekuwa amefungwa pingu akiwa chini ya ulinzi wa askari watatu waliokuwa wameelekeza bunduki zao katika paji lake la uso. Moyoni alikuwa anaumia juu ya kila jambo lililokuwa likiendelea huku akimini mwisho wa maisha yake ulikuwa umefika. Wakati huo alikuwa akiumia kwa kuikosa ahadi ya Natalie Brown, mrembo wa kimarekani aliyeahidi kuwasaidia yeye na rafiki yake James waliyekuwa wakiishi wote kama watoto wa mitaani. Jambo lililomuuma kuliko yote lilihusiana na kufa pasipo kulipa kisasi kwa bwana Abraham aliyeamini alihusika na kifo cha wazazi wake. Alikuwa mtulivu muda wote bila kuleta ubishi, aliwasikia askari hao wakipongezana kwa kumkamata huku wakiamini wangepata fedha za kutosha kutokana na zoezi hilo walilololifanikisha kirahisi.
Gari hilo la polisi lilikuwa katika kasi kubwa huku dereva wake akiwa hana mpango wa kupunguza kasi hiyo. Jambo lililomkaa kichwani lilihusiana na kufika jijini Entebbe na siyo kitu kingine. Alikimbiza gari hilo bila kujali kasi yake kwa vile askari wenzie nao walikuwa wakimsifia kutokana na mwendo huo. Wakiwa umbali wa kilometa arobaini kutoka eneo la Kiriri, wote walishtuka kutokana na mlio mkubwa uliosikika kutoka katika gurudumu la upande wa mbele wa gari hilo. Wakiwa bado wanautafakari mlio huo uliosikika kama vile kuna kitu kilikuwa kimepasuka, ghafla gari lao lilianza kuyumba yumba likiwa limekosa mwelekeo katika kasi hiyo ya mia moja arobiniiliyokuwapo. Dereva wa gari hilo alipiga kelele zisizo eleweka kutokana na hali hiyo jambo lililomfanya auachie hata uskani wa gari hilo kutokana na mtikisiko mkubwa uliokuwapo.
Askari waliokuwa wameelekeza bunduki zao kwa David waliacha zoezi hilo na kujishikilia katika kingo za gari hilo huku wakiwa na hofu kupindukika. Likiwa na kasi hiyo ya ajabu gari hilo liliongoza moja kwa moja na kwenda kugonga mti mkubwa uliokuwa kando kidogo ya barabara. Baada ya sekunde kadhaa eneo hilo lilikuwa na sura tofauti, askari aliyekuwa anaendesha gari hilo alikuwa amebanwa na uskani huku ukiwa umemtoboa tumbo lake. Damu ilikuwa ikimtoka kwa kasi mdomoni na puani, hakuwa hai tena tayari alikuwa amefariki. Askari mwingine alionekana umbali wa mita kadhaa kutoka eneo hilo huku kichwa chake kikiwa kimepasuka lakini pia akiwa na majeraha mengi.
Askari wengine wawili nao wakiwa wameumia vibaya walikuwa karibu na eneo hilo huku wakihangaika kutokana na maumivu waliyoyapata. David akiwa na majeraha mengi alionekana akiwa ametupwa katikati ya barabara hiyo huku akihangaika pia. Kiasi kidogo cha damu ilikuwa imezunguka eneo alilokuwapo. Gari la polisi lililokuwa likitumika lilikuwa limeharibika vibaya na halikuwa na dalili ya kuweza kutengenezwa na mwishoe kurudi tena barabarani. Eneo hilo lilikuwa tulivu huku kukiwa hakuna gari lolote lililokuwa likielekea eneo hilo. Wakati huo askari wawili waliokuwa wakihangaika walikuwa wametulia hali iliyoashiria kuwa walishafariki.
Baada ya dakika kumi lilionekana basi moja kama la abiria lililokuwa na kasi likiwa linatokea jijini Entebbe. Gari hilo lilikuwa likionekana chakavu ambalo askari wa barabarani wangeweza kulikamata sehemu yeyote ambayo lingengekuwa likipita. Likiwa katika kasi hiyo lilizidi kusogea eneo la ajali hiyo, baada ya sekunde kadhaa lilikuwa karibu kabisa na eneo hilo huku kasi yake ikiwa imepungua. Dereva wa gari hilo alikuwa wa kwanza kuishuhudia ajali hiyo lakini hakuwaeleza wenzie waliokuwa wamelala, ghafla alifunga breki kali baada ya kumwona mtoto mmoja akiwa amelala katikati ya barabara. Basi hilo dogo liliburuzika barabarani kabla ya kwenda kusimama kando kidogo na eneo alilikuwapo mtoto huyo.
Dereva wa gari hilo alikuwa wa kwanza kushuka kwenye gari hilo akifuatiwa na wenzie walioshtushwa na breki hiyo kali iliyokuwa imefungwa. Baada ya sekunde kadhaa watu hao waliokuwa saba walikuwa wameshuka katika gari lao huku wakiangalia huku na huku katika eneo hilo la ajali. Gari lao lilikuwa la ajabu huku likiwa halina hata namba za gari zaidi halikuwa na kadi ya bima pamoja na ile ya kodi ya mapato. Ubavuni mwa gari hilo kulikuwa na matundu madogo madogo ambayo kwa haraka yalionekana kama yalikuwa ya risasi. Kwa ujumla gari hilo lilionekana kama la wahalifu ambao hawakuogopa mkono wa sheria. Hilo lilithibitika kwa jinsi watu hao walivyokuwa, walikuwa wakionekana kama wahalifu kwa vile walikuwa na vifua vipana vilivyojengeka kimazoezi huku wakiwa na bunduki zao walizoziweka mabegani. Mavazi yao yalikuwa kama ya waasi wafanyao mapigano kupigania haki ya kitu fulani.
Mmoja wa watu hao aliyeonekana kama alikuwa kiongozi wao aliwaita wenzake na kuonekana kama alikuwa akiwaeleza jambo. Baada ya maelezo hayo vijana wanne kati yao walielekea katika gari lao hilo walilofika nalo na kushusha sanduku moja kubwa lililokuwa limetengenezwa kwa chuma. Vijana wengine wawili walionekana wakichukua bunduki za askari hao waliopata ajali hiyo ambao walikuwa wamefariki. Baada ya zoezi hilo lilitolewa sanduku jingine dogo kwenye gari lao ambalo lilifunguliwa kabla ya kuonekana likiwa na vifaa tofauti ndani yake. Vilikuwapo visu vilivyong’aa sana kutokana na makali yake lakini pia yalikuwapo mapanga na shoka dogo. Vilevile kulikuwapo na mabomba ya sindano pamoja na chupa kadhaa zilizokuwa na dawa. Watu wanne kati yao walichukuwa visu vinne kabla ya kuanza kutembea wakielekea eneo ambalo askari hao walikuwapo. Walikuwa wakifanya mambo hayo haraka huku wakionekana kutazama huku na huko wakihofia usalama wao. Watu hao kila mmoja aliongoza kwa askari mmoja kati ya wale wanne na baada ya sekunde kadhaa walionekana wakivikata vichwa vya askari hao pasipo huruma hata kigodo.
Mmoja wao kati ya watu hao walioonekana kuwa wauaji alikuwa akifanya zoezi hilo kwa askari aliyekuwa amebanwa na uskani wakati wengine waliwafanyia zoezi hilo askari wengine. Hatimaye walikamilisha zoezi hilo kwa muda mfupi na kuongoza na vichwa hivyo mpaka eneo alilokuwapo mkubwa wao. Lilifunguliwa sanduku kubwa na vijana wengine mbali na hao waliokuwa na vichwa na hapo ndipo ukweli juu ya shughuli ya watu hao ulionekana. Kulikuwa na vichwa vingi katika sanduku hilo ambalo wauaji hao walivitupia vichwa vingine vinne vya askari waliokuwa wamewakata. Katika sanduku hilo pia kulikuwa na ngozi ambazo kwa haraka mtu angeweza kugundua kuwa zilikuwa ngozi za binadamu.
Kiongozi wa watu hao alimwamuru mmoja wao amwangalie mtoto aliyekuwapo barabarani. Kijana mmoja limsogelea mtoto huyo na kuonekana akimchunguza mapigo yake ya moyo na hatimaye alinyanyuka na kuonesha ishara ya kidole akiashiria kuwa alikuwa mzima. Kiongozi wa kundi hilo aliwaamuru wampakie mtoto huyo kwenye gari lao. Jambo hilo lilichukuwa nafasi baada ya kuikata pingu aliyofungwa David kwa shoka ikiwa ni pamoja na kupakizwa kwa masanduku mawili yaliyoshushwa awali. Watu hao waliingia kwenye gari lao kabla ya kuwashwa kwa gari hilo na kuondolewa kwa kasi eneo hilo likiwa limeshika barabara iliyokuwa ikielekea Kiriri kwa kasi.
* * *
Bwana Abraham alikuwapo katika kituo kikuu cha polisi cha jijila Entebbe huku akiwasubiria kwa hamu askari ambao walikuwa wamemkamata David, mtoto aliyekuwa akikiumiza kichwa chake siku zote. Wakati huo alikuwa akiwaza mambo mengi tofauti, moja ya mambo aliyokuwa akiwaza alipanga kuhakikisha David anauawa ndani ya usiku wa siku hiyo. Alipanga kufanya mpango na askari wa kituo hicho cha polisi ili David auawe usiku wa siku hiyo kabla ya mwenendo wa kesi yake kuanza kuchukua nafasi. Alimchukia mtoto huyo wa marehemu mdogo wake Johnson na alimwona kikwazo katika kila jambo. Aliamini mara baada ya kuuawa kwa mtoto huyo angekuwa mmiliki halali wa mali za marehemu Johnson na angeanza maisha mapya yenye furaha akiwa na mkewe Aminata.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/--
Furaha ya mipango yake ilianza kuingia dosari baada ya kusubiri kwa muda mrefu askari hao wafike kituoni hapo bila mafanikio. Jambo hilo ndilo lilipelekea awaombe askari wa kituo hicho cha jijini Entebbe wawasiliane na askari alioelezwa walikuwa wakimshikilia David. Askari wa kituo hicho walitumia simu ya upepo kujaribu kuwasiliana na wenzao hao lakini walikuwa hawapokei simu yao. Jambo hilo lilianza kuwapo hofu juu ya imani yao kuwa David bado alikuwa chini ya ulinzi. Walibaki wakitafakari juu ya jambo la kufanya baada ya kukosa mawasiliano na askari wenzao wakati huo ikiwa yapata saa kumi na moja jioni. Ni wakati huo ambao mkuu wa kituo hicho cha polisi alipokea taarifa juu ya ajali mbaya iliyokuwa imewapata askari waliokuwa wakimshikilia David. Alielezwa kuwa ajali hiyo ilikuwa imetokea umbali wa kilometa ishirini kutoka hapo jijini Entebbe. Taarifa zilizowashtua zaidi zilieleza kuwa vichwa vya askari hao waliofariki vilikuwa vimekatwa na haikueleweka vilipelekwa wapi huku bunduki za askari hao zikiwa hazipo pia.
Mtu aliyepiga simu alisisitiza kutomwona mtoto aliyeelezwa kuwa ni mtuhumiwa katika eneo hilo la ajali. Taarifa hizo ziliwashtua askari hao hususani bwana Abraham aliye changanyikiwa kabisa, mkuu wa kituo akiwa na askari kadhaa wa barabarani waliondoka kituoni hapo wakielekea eneo la tukio hilo huku wakiwa wameongozana na bwana Abraham. Tajiri huyo usoni alikuwa amebadilika na kuonyesha hasira dhahiri na zaidi alionekana kuchanganyikiwa. Alikuwa amevaa miwani ambayo haikuhurusu mtu kumwona macho yake. Huo ulikuwa utamaduni wake mpya kwani hakutaka kabisa mtu ajue kama alikuwa mlemavu wa jicho la kushoto baada ya kupigwa na David, mtoto aliyemchukia, miezi kadhaa iliyokuwa imepita.
Alikuwa na hasira kupindukia ambazo hakutaka kuzielezea kwa maafisa hao wa jeshi la polisi ambao walikuwa hawajui jambo lolote juu ya uovu wa tajiri huyo. Moyoni aliumia juu ya taarifa hiyo waliyoipata na wakati safari hiyo ikiendelea kuelekea eneo la ajali alikuwa akishtuka kila mara simu ilipopigwa kwa mkuu wa jeshi la polisi. Alikuwa akihisi labda mkuu huyo angepewa taarifa za kuwa David amefariki pia katika eneo la tukio lakini haikuwa hivyo. Baada ya nusu saa walikuwa wamefika katika eneo la tukio lililokuwa na ajali hiyo, eneo ambalo lilikuwa na watu wachache. Pia kulikuwapo na gari la hospitali kuu ya jiji la Entebbe lililokuwa likisubiri uchunguzi juu ya ajali hiyo ufanyike ili miili ya marehemu hao ipelekwe mochuari.
Askari waliofika eneo hilo la tukio walifanya uchunguzi wao wa awali dhidi ya ajali hiyo kabla ya kuwahurusu wauguzi waliofika eneo hilo kuichukua miili ya marehemu hao, swali kubwa lililokuwa vichwani mwa askari hao pamoja na watu wote waliokuwapo eneo hilo lilihusiana na vichwa vya askari waliopata ajali hiyo ambavyo vilikatwa. Zaidi vichwa hivyo havikupatikana kabisa katika eneo hilo la tukio. Jambo hilo lilianza kuwapa hisia tofauti wakiamini huenda ajali hiyo ilikuwa imepangwa. Kukosekana kwa David eneo hilo la tukio kuliwafanya waamini hisia zao zilikuwa za kweli juu ya suala hilo. Kwa vile bado walikuwa wakiamini mtoto huyo alikuwa mfuasi wa kundi la Eastern Black Killers lililohusika na mauaji ya Sabinus, aliyekuwa mtoto wa bwana Abraham na zaidi mauaji dhidi ya Otieno Ndakufurila.
Jambo lililomaliza ukweli wa hisia zao ni tukio zima alilolifanya David na kusababisha ulemavu wa jicho la kushoto la bwana Abraham. Hata hivyo askari hao walihitaji muda wa kwenda kutafuta mwanzo wa upelelezi juu ya tukio hilo huku wakiamini bwana Abraham angetoa mchango mkubwa. Wakati huo tajiri huyo alikuwa ametulia huku akiwa na hasira zilizomkaba shingoni, alikuwa akielewa wazi David alikuwa hahusiki na jambo lolote kama zilivyokuwa hisia za askari hao. Jambo lililomuuma lilihusiana na uhai wa mtoto huyo, alikuwa haelewi watu hao walimbeba akiwa amefariki au akiwa hai!Mwishoe taratibu nyingine zote zilihurusiwa na askari hao ziendelee wakati upelelezi zaidi juu ya tukio hilo ukitarajiwa kuendelea siku iliyofuata.
* * * *
Gari la wauaji waliomchukuwa David ikiwa ni baada ya kuvikata vichwa vinne vya askari wa jeshi la polisi wa nchini Uganda lilionekana likiwa kwenye kasi katika misitu iliyokuwapo eneo la Bukavu, katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ndani ya gari hilo kulikuwapo na wauaji hao waliokuwa wanakunywa pombe. Mikononi mwao walikuwa wameshika bunduki zao ilhali wakionekana wakiwa hawana hofu ya jambo lolote. Wakati huo David alikuwa amejilaza huku akiwa mtulivu katika siti ya nyuma kabisa ya basi hilo dogo.Alijikaza mbali na majereha kadhaa aliyokuwa nayo mwilini yaliyosababishwa na ajali. Alikuwa kama mtu aliyekata tamaa juu ya kila jambo lililokuwa linaendelea katika maisha yake. Wakati huo hakujua jambo lililokuwa linaendelea kwa vile hakukumbuka kitu chochote tangu mwisho wa hatari ya ajali aliyoipata na askari waliomkamata.
Akiwa na hofu dhidi ya watu hao waliokuwa wamemkamata ambao hakuamini kama walikuwa askari pia hakuielewa lugha waliyokuwa wakiitumia. Jambo hilo ndilo lilimfanya abaki amelala katika siti hiyo ilhali akiwa hana nguvu kabisa. Bado aliendelea kuamini kuwa mwisho wake ulikuwa umefika na suala la kulipa kisasi lilikuwa limeisha. Gari lao bado liliendelea kuendeshwa kwa kasi na watu hao walianza kuimba nyimbo ambazo yeye hakuzifahamu. Jambo pekee aliloligundua katika nyimbo hizo liliuhusiana na furaha waliyokuwa nayo watu hao waliokuwa wamelewa. Alibaki ametulia eneo alilokuwapo huku akiwa na hofu, ghafla alishtushwa gari hilo likifungwa breki kali zilizopelekea aanguke kutoka eneo alilokuwa amelala na hatimaye alisimama na kutulia wakati watu hao alioamini walikuwa majambazi walianza kushuka kwenye gari hilo kwa haraka.David kwa kupitia dirisha la gari hilo alielekeza macho yake nje ya gari hilo kabla ya kuwashuhudia watoto wengine wa rika yake wakiwa wameoneshewa silaha na watu hao.
Watoto hao walikuwa watano, wakiwapo wasichana watatu na wavulana wawili. Alimsikia mmoja wao aliyeonekana kama kiongozi akiwaamuru watoto hao waliokuwa wakilia waingie katika gari hilo. Watoto hao waliokuwa eneo hilo la porini huku walionekana kama walikuwa wakitokea shambani kutokana na majembe waliyokuwa nayo. Walitii amri hiyo na kuanza kuingia katika gari hilo huku wakilia kwa sauti kutokana na hofu juu ya watu hao. Tukio hilo ambalo David alilishuhudia lilimfanya na yeye aanze kulia kwa sauti ya chini huku akielewa wangeuawa ndani ya muda mfupi. Watoto hao waliotekwa waliingia katika gari hilo na kwenda kukaa eneo alilokuwapo huku wakilia jambo lililomwongezea hofu zaidi. Hatimaye watu hao waliowateka waliingia katika gari na safari iliendelea huku wakiimba nyimbo zao pia.
Baada ya saa tatu gari hilo lilikuwa katikati ya misitu ya eneo la Shabunda likiwa katika kasi ileile na mwishoe dereva wa gari hilo aliiacha barabara kuu. Akiwa katika kasi pia aliendelea kuendesha gari hilo akitumia barabara ndogo iliyopita katikati ya misitu hiyo minene ambayo ililifanya eneo hilo kuwa giza majira hayo ya saa kumi na nusu jioni. Jambo hilo lilipekea gari hilo liendeshwe huku likiwa limewashwa taa zake, wakati huo watu hao walikuwa wakiimba kwa bidii tofauti na awali. David alianza kuhisi kuwa tayari walikuwa wamekaribia eneo walilokuwa wanapelekwa. Watoto wenzie ambao walionekana kama walijua jambo juu ya kutekwa kwao walikuwa wamekumbatiana huku wakiwa wamepoteza matumaini baada ya kulia kwa muda mrefu. Mara kadhaa aliwasikika watoto hao wakiongea kwa sauti ya chini lakini hakuifahamu lugha waliyoitumia.
Wakiwa wanaendelea na safari hiyo walishtushwa na mwanga wa gari jingine lililokuwa likitokea eneo walilokuwa wanaelekea. Hatimaye gari hilo lilijongea kabla ya kukutana lile walilokuwa nalo, madereva wa magari hayo walisimamisha magari na kuonekana wakiongea jambo. David alishtushwa na gari hilo kwani lilikuwa la kijeshi huku katika bodi lake kukiwa na vijana wengi ambao wengine walikuwa wadogo waliokuwa wakipiga kelele za kusalimiana na watu waliokuwa nao. Vijana hao waliokuwa katika gari hilo wote walikuwa na bunduki jambo lililomchanganya zaidi. Hatimaye walipishana na gari hilo kabla ya safari yao kuendelea.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Majira ya saa moja walikuwa wakiingia katika kijiji kilichokuwa katikati ya msitu huo katika eneo lililokuwa mlimani. Kijiji hicho ambacho nyumba zake zilijengwa kwa udongo na kuezekwa kwa majani kilikuwa na umeme ulioangaza kila mahali. Ni wakati ambao David alifanikiwa kulisoma bango kubwa lililoandikwa katika geti la kuingilia eneo hilo lililokuwa na walinzi wengi. Bango hilo lilikuwa limeandikwa Revolution Army, akiwa bado anaangalia huku na huko aliwashuhudia askari wengine wakiwa katika kila kona ya eneo hilo wakiwa na bunduki zao. Walikuwa na hofu huku wakiwa tayari wameelewa kuwa eneo hilo lilikuwa la waasi. Gari lao liliendelea kuendeshwa taratibu ndani ya kijiji hicho, ghafla yule kiongozi wa wenzie aliwasha tochi na kwenda eneo la nyuma walilokuwapo.
Alielekeza tochi hiyo kwenye nyuso zao na kuonekana kama alitaka kufanya jambo fulani. Hatimaye walimshuhudia akitikisa kichwa kabla ya kumshika mkono msichana mmoja kati ya wale watatu waliokuwapo, alianza kumvuta msichana huyo ambaye alianza kulia. Aliongoza naye mpaka eneo alilokuwa amekaa awali kabla ya kutulia kidogo huku akiwa amempakata kinguvu. Wenzie ambao aliamini walikuwa waasi pia walitulia huku nao wakigeuka geuka eneo alilokuwapo David na wenzake. Tayari David alielewa mazingira yaliyofuata kwa msichana aliyechukuliwa na kiongozi huyo yangekuwa ya kubakwa. Mwishoe gari lao liliegeshwa mbele ya jengo kubwa lililojengwa kwa tofali na kuezekwa kwa bati ambalo lilionekana kama lilikuwa jengo la utawala. Walishtushwa na kelele za waasi wengine wakiwa na silaha ambao walifika eneo ambalo gari hilo liliegeshwa huku wakipiga kelele za shangwe na risasi hewani.
Kiongozi aliyemshika yule msichana kinguvu ndiye alikuwa wa kwanza kushuka kabla ya kuendelea kumvuta msichana aliyekuwa naye na Mwishowe alizamia katika nyumba ndogo iliyoezekwa kwa majani. Nyumba hiyo ilikuwa umbali wa mita kadhaa kutoka eneo hilo ambalo basi hilo dogo la waasi lilikuwa limeegeshwa. Msichana aliyekuwa akivutwa na kiongozi huyo alikuwa akilia huku akiomba msaada lakini hakusikilizwa. David na wenzake pamoja na wasichana wengine wawili walielezwa watulie ndani ya gari hilo. Wakati huo waasi waliobakia walikuwa wakishusha masanduku mawili waliyokuwa nayo. Wachahe walibeba sanduku moja kubwa ambalo awali waliweka vichwa vinne vya askari. Sanduku hilo pia lilikuwa na vichwa vingine pamoja na ngozi za watu.
Waliwashuhudia waasi waliokuwa wakishangilia kufika kwao wakiwasaidia wenzao kubeba masanduku hayo kabla ya kuongoza nayo mpaka katika jengo la ofisi hiyo ya waasi. Baada ya zoezi hilo walirudi kabla ya kuwaamuru David na wenzie watoke jambo lililochukua nafasi haraka. Wakati bado wanaendelea kushuka waasi hao waliwavamia kabla ya kusabisha waanguke chini. David akiwa na hofu alikanyagwa sehemu tofauti za mwili wake na waasi hao walioanzisha vurugu za ghafla. Baada ya sekunde kadhaa waasi hao walimaliza vurugu hizo kabla ya kuonekana wakiondoka katika makundi mawili huku wakienda sehemu tofauti. David akiwa haelewi vizuri jambo lililoendelea alishtuka kuona kuwa eneo hilo alikuwa amebaki yeye pamoja wavulana wenzie wawili. Tayari alitambua jambo lililoendelea kwani waasi hao walikuwa wamewabeba wasichana wawili ambao alisikia kelele zao wakilia.
Walibaki wametulia eneo hilo kabla ya kuitwa na askari mmoja wa kundi hilo la waasi aliyewamuru wamfuate. Waliongoza naye mpaka katika jengo moja lililojengwa kwa tofali ambalo lilikuwa kubwa huku likiwa limefungwa na kufuli kubwa nje. Wakiwa nje ya jengo hilo walisikia kelele za watu waliokuwapo ndani. Askari huyo aliyewaamuru wamfuate alifungua mlango wa jengo hilo kabla ya kuwasukuma waingie ndani na Mwishowe aliufunga mlango huo. Mara baada ya kuingia waliwashuhudia watoto wengi wa rika ya miaka kama kumi na nne ambao waliwavamia na kuanza kuwapiga huku wakipiga kelele. David alilia kwa uchungu kutokana na maumivu aliyoyapata kutokana na kipigo hicho. Maumivu hayo yalizidi kwa vile watoto hao walioonekana kama wakorofi kupindukia walikuwa wakimpia sehemu ambazo alikuwa na majeraha ya ajali aliyoipata.
Majira ya saa nne usiku David alikuwa amelala sakafuni kama ilivyokuwa kwa watoto waliowakuta ambao wao walilalia maboksi. Wakati huo akiwa karibu na watoto wenzie aliofika nao alikuwa hana nguvu hata kidogo. Usoni alikuwa amevimba kutokana na kipigo alichokipata huku akiwa na maumivu mwili mzima. Hakutambua hatma ya maisha yake mpaka wakati huo zaidi hakuelewa lengo la waasi hao waliokuwa wamewakamata. Bado alikuwa akimfikiria baba yake mkubwa, bwana Abraham ambaye aliamini ilimpasa alipe kisasi. Alijipa matumaini moyoni akiamini kuwa ndoto zake zingeweza kutimia siku moja.
* * *
Revolution Army lilikuwa kundi la waasi waliokuwapo katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kundi lililokuwa likipingana na serikali. Sera yao ilikuwa ni moja, kufanya mapinduzi katika nchi hiyo kwa kuingia kinguvu madarakani. Mpango huo ulikuwa endelevu na walitarajia kufanya mapinduzi hayo baada ya maandalizi ya miaka saba waliyokuwa wamebakiwa nayo. Walipanga kuhakikisha wanamtoa madarakani kiongozi wa wakati huyo bwana Maabutu Lozefu ambaye waliamini hakupaswa kuishikilia nchi hiyo. Kundi hilo la waasi lilikuwa chini ya Zichura Msowoya ambaye alikuwa na mipango thabiti ya kuhakikisha lengo lake la kuingia madarakani linatimia.
Moja ya mpango aliokuwa nao ulikuwa ni wa kuwakamata watoto wadogo wa kiume ambao walipelekwa katika kambi ya jeshi hilo la waasi na kupewa mafunzo. Aliamini watoto hao wangekuwa tegemeo baada ya miaka saba waliyopanga kufanya mapinduzi. Kundi lake halikuwa na haja na wanawake lakini walipofanikiwa kuwapata waliwakamata pia na kuwapeleka katika kambi hiyo. Huko wanawake wachache waliishi kama wake wa viongozi wa jeshi hilo la waasi wakati wengine wengi walikuwa wakiishia kufariki kwa sababu ya kubakwa na kundi kubwa la askari hao. Zichura pia akiwa katika harakati hizo za kupindua nchi alikuwa akifanya kila aina ya biashara haramu ambayo ilikuwa chini ya uwezo wake. Alikuwa akijihusisha na biashara ya dawa za kulevya ambapo katika eneo iliyokuwapo kambi hiyo ya waasi alikuwa na ekari nyingi za zao haramu la bangi. Aliuza zao hilo kwa watu tofauti kutoka nchi mbalilimbali na lengo lake kubwa lilikuwa dogo tu kwani alikuwa akihitaji fedha kwa ajilia ya kununua silaha alizoziagiza kutoka nchi mbalimbali za ulaya.
Alikuwa na kundi la askari ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kuteka na kufanya unyan`ganyi wa silaha za kijeshi za serikali ya nchi hiyo ikiwa ni pamoja na magari. Zichura hakuishia hapo katika mipango yake hiyo endelevu kwani alikuwa na askari wa jeshi lake hilo la Revolution Army ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kufanya ujambazi katika eneo la Afrika Mashariki na kati. Lengo haswa lilikuwa ni kutimiza adhma ya mapinduzi katika nchi hiyo. Ingawaje alikuwa akipata misaada kadhaa kutoka kwa makundi mengine ya waasi wa nchi nyingine ikiwa ni pamoja na nchi za Ulaya lakini hakutaka kuwategemea kwa aslimia zote.
Matendo yake ya uovu yaliyoendeshwa na kundi lake ndiyo yaliyowafanya hata waganga wa jadi wampe kazi tofauti ili kuwatimizia malengo yao. Wapo waganga waliokuwa wakihitaji vichwa vya watu wakati wengine walikuwa wakihitaji ngozi za watu. Zichura alikuwa akiwatimizia mahitaji yao kupitia kwa askari wa jeshi lake hilo la Revolution Army. Askari waliokuwa wamemfikisha David katika ngome hiyo wao pia walikuwa wakihusika na hitaji hilo la vichwa vya watu pamoja na ngozi zao. Yote hayo walikuwa wakiyafanya kwa lengo moja tu la kuweza kuipindua serikali ya bwana Maabutu Lozefu.
* * *
David akiwa amelala sakafuni alishtushwa na kelele za watoto wenzie majira ya saa kumi usiku ambao walikuwa wameamka huku wakiwa wamesimama kama vile walikuwa tayari kwa ajili ya jambo fulani. Mwonekano wa watoto hao ndio uliomfanya ashtuke na kukaa sakafuni akiwa na lengo la kutaka kujua jambo ambalo lingefuata. Hatimaye alisikia mlango wa jengo hilo ukifunguliwa na watoto wenzie walisogea mlangoni kama vile walikuwa tayari kwa kuondoka. David akiwa na watoto wenzie aliofika nao waliamua kusimama pia kabla ya kuwafuata wenzao. Mwishowe mlango wa jengo hilo ulifunguliwa na waliwashuhudia wenzao wakitoka wanakimbia na wao waliwafuata nyuma kwa kujikongoja mbali na maumivu waliyokuwa nayo. Waliongoza mpaka katika uwanja mkubwa uliokuwapo mita kadhaa kutoka katika jengo hilo ambako walienda kuungana na wenzao ambao walikuwa wamesimama katika mistari nane mirefu iliyonyooka. Kulikuwa na idadi kubwa ya watoto katika eneo hilo jambo lililowapa hisia kuwa huenda kulikuwa na jengo jingine walilokaa watoto zaidi ya lile walilolitumia wao.
Walitulia kwa muda mfupi kabla ya kuwa shuhudia askari kama kumi wakitembea kuelekea katika eneo hilo. Askari hao walikuwa wamebeba fimbo nyingi mikononi mwao mbali na bunduki walizokuwa nazo. Hatimaye askari hao waliwafikia kabla ya mmoja wao kuonekana akitoa maelezo kwa lugha ambayo David hakuifahamu. Baada ya sekunde kadhaa watoto hao walianza kurukaruka ilhali wengine wakianza kuondoka kwa kukimbia kwa makundi tofauti. David naye alikuwa akirukaruka huku akiwa ameingiwa na hisia kuwa walikuwa wanaelekea sehemu fulani. Makundi manne tofauti yaliondoka eneo hilo huku nyuma yake wakifuata askari wawili wawili waliokuwa na viboko pamoja na bunduki.
Hatimaye ulifika wakati wa kuondoka kwa kundi la tano alilokuwapo David, waliondoka wakikimbia wakiwa wanatumia barabara ambayo siku moja kabla waliitumia kina David kufika eneo hilo na waasi waliowateka. Baada ya dakika kadhaa walikuwa wametoka katika geti kuu kabla ya kuanza kuzamia katika pori hilo lililokuwa na giza. Kulikuwa na tochi walizokuwa nazo askari hao zilizowaongoza kupita katika barabara hiyo. David alijitahidi kukimbiua huku akiwa haelewi eneo walilokuwa wakielekea. Walikimbia kwa muda wa robo saa pasipo kufika katika eneo walilokuwa wanaelekea jambo lililoanza kumtia shaka kwani tayari alikuwa amechoka.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati huo pia hata wale watoto wenzie aliofika nao walikuwa wamechoka, mmoja wao aliamua kusimama baada ya kuishiwa pumzi na kushindwa kukimbia. Askari waliokuwa nyuma yao walimpiga kwa fimbo walizokuwa nazo jambo lililomfanya mtoto huyo apige kelele kabla ya kuanza kukimbia tena. David aliamua kuendelea kujituma baada ya kutambua kuwa askari waliokuwa nao walikuwa hawana huruma. Walikimbia kwa muda mrefu pasipo kufika eneo walilokuwa wanaelekea, hatimaye David aliona zoezi hilo gumu. Aliamua kusimama kabla ya kulala chini akiwa tayari kwa jambo lolote ambalo lingetokea. Alikuwa amechoka sana huku akipumua kwa taabu, hakuwahi kukimbia umbali kama huo katika maisha yake hata siku moja.
Askari waliokuwa nyuma yao waligundua kuwa David alikuwa amelala chini baada ya wenzake kujikwaa mara kadhaa katika eneo alilolala. Walipolifikia eneo hilo walielekeza tochi zao kabla ya kumshuhudia David akiwa amelala eneo hilo huku akipumua kwa taabu sana. Askari hao hawakuwa na swali juu ya mtoto huyo zaidi ya kuanza kumpiga fimbo kila eneo la mwili wake. Askari mwingine alimpia David kwa mateke pia. Alitulia kwa muda mfupi wakati karaha hiyo ikiendelea kabla ya kusimama na kuamua kuendelea kukimbia. Aliona kipigo alichokipata kilikuwa zaidi ya ugumu wa kukimbia, ni wakati ambao David alikuwa akiwaza mambo mengi pasipo kupata jibu. Alikuwa akihisi kuwa angekufa akiwa katika ngome hiyo ya waasi wa Revolution Army.
Waliendelea kukimbia kwa muda mrefu kabla kufika eneo husika walilokuwa wakielekea. Kulikuwa kuna mlima mmoja mkubwa uliokuwa umezungukwa na miti mingi mikubwa. Katika eneo la juu la mlima huo kulikuwa na uwanja mkubwa huku kukiwa na jengo moja kubwa katika eneo hilo lililokuwa na nafasi. Waliambiwa wapumzike kwa muda wa dakika tano, David hakuyatambua maelezo hayo alilala huku akiamini wangepumzika kwa muda mrefu. Baada ya muda mfupi alishtuka akipigwa kwenye mbavu zake na buti la askari, alipofungua macho yake alimwona askari mmoja akiwa na bunduki aliyemsihi asimame haraka. Aliponyanyuka aliwashuhudia wenzie wakimalizia kupanga mistari katika eneo hilo. Akiwa bado hajapumzika hata kidogo aliongoza na kuwafuata wenzie kabla kupanga mstari pia.
Wakati huo ilikuwa majira ya saa moja asubuhi wakiwa eneo hilo la kusini mwa ngome ya Revolution Army iliyokuwapo umbali wa kilometa ishirini na tano kutoka eneo hilo ambalo lilikuwa likitumika kwa mazoezi ya kijeshi kwa watoto hao waliokuwa wakiandaliwa kwa ajili ya mapinduzi ya nchi hiyo. Hatimaye mafunzo ya kijeshi yalianza kuchuku nafasi, ilikuwa siku ngumu kwa David ambaye kila kitu kilikuwa kigumu kwake. Kulikuwa na mazoezi ya kila aina yakiwapo ya kulenga shabaha pamoja na kupigana wao kwa wao. Ugumu huo kwa David ulimzidia zaidi kwani karibu kila zoezi alilopewa alishindwa ikiwa ni pamoja na kupigwa na kila mtoto aliyepangwa kupigana naye.
Kulikuwa na mahandaki ya kijeshi katika eneo hilo ambayo nayo yalitumika katika mafunzo yao. Majira ya saa nne walisimamisha mazoezi yao kwa dakika saba baada ya gari moja la kijeshi kufika eneo hilo likiwa na uji. Walipewa vikombe kwa ajili ya kuchukua kifungua kinywa hicho. Mara baada ya kupewa uji David alienda kutulia eneo lake huku akiwa amechoka lakini hakuweza kunywa uji huo hata kidogo kwani ulikuwa wa moto kupindukia. Alijaribu kunywa mara moja kabla ya kuutema uji huo baada ya kuungua ulimi. Hali ilikuwa tofauti kwa wenzake ambao walionekana kuzoea kifungua kinywa hicho kwani walikuwa na njia tofauti za kunywa uji huo. Baada ya dakika saba kuisha ambazo walipewa kwa ajili wa kunywa uji huo filimbi ilipigwa wakiamriwa kwenda kupanga mistari kwa ajili ya kuendelea na mazoezi.David aliuacha uji wake eneo alilokuwapo huku akiwamini angeurudia baada ya mazoezi hayo ya mara ya pili lakini jambo lililomtoa machozi ni pale alipomshuhudia askari mmoja akikusanya vikombe vyote kikiwapo kile kilichokuwa cha kwake.
Mazoezi hayo ya kijeshi yaliendelea katika siku ngumu ambayo David hakuwahi kukutana nayo katika maisha yake. Majira ya saa tisa walimaliza mazoezi hayo kabla ya kulishuhudia gari lililowapelekea uji likifika kwa mara ya pili. Chakula kilichopelekwa kilishushwa kabla ya askari hao kuanza kugawa chakula hicho. Walikuwa wamepelekewa ugali na maharage ambavyo pia vilikuwa vya moto lakini wakati huu David alijitahidi kula kwa bidii na kufanikiwa kumaliza chakula hicho. Baada ya dakika tano filimbi ilipigwa na wale wote waliokuwa hawajamaliza chakula hicho walinyan`ganywa sahani zao na Mwishowe walilishuhudia gari hilo likiondoka. Walipewa muda wa nusu saa kwa ajili ya kupumzika na ilipotimia saa kumi kamili safari yao ya kurudi katika ngome ya Revolution Army ilianza.
Wakati huo David aliona amepata unafuu kwani walikuwa wakitembea ingawaje kwa haraka sana na mara kadhaa ilimlazimu kukimbia ili kwenda sambamba na wenzake. Majira ya saa kumi na mbili na nusu walikuwa wakifika katika kambi yao akiwa na wenzie hao walielekea sehemu moja iliokuwa na uwazi na kutulia wakipumzika. David hakuwa ameongea na mtu mpaka wakati huo kila alipozungumza kiingereza wenzie walikuwa hawamuelewi. Majira ya saa moja kasoro usiku aligundua jambo lilolomuuma sana, aliwaona askari wawili wakiwa wamemshika msichana mmoja mguu mmoja mmoja huku wakimburuza ilhali wakipita karibu na eneo hilo. David aliweza kumgundua msichana huyo aliyekuwa amefariki akiwa mmoja kati ya watatu waliotekwa siku iliyopita na kufikishwa pamoja na yeye katika ngome hiyo.
Nguo za msichana huyo zilikuwa na madoa ya damu, David hakujiuliza jambo lolote juu ya sababu ya kifo cha msichana huyo kwani alielewa alikuwa amebakwa mpaka akafariki. Aliumia sana juu ya tukio hilo ila hakuwa na jinsi na aliamua kukubaliana na jambo hilo kutokana na ukatili alioutambua ambao askari wa jeshi hilo walikuwa nao. Majira ya saa moja walipewa chakula na baada ya zoezi la kula walifungiwa kwenye majengo yao husika huku wakiisubiria ratiba ya siku iliyofuata.
* * * *
Baada Ya Miaka Saba.
David akiwa na miaka kumi na tisa alikuwa ni mtu tofauti na vile alivyokuwa miaka kadhaa iliyokuwa imepita. Akiwa mrefu wastani, alikuwa na kifua kipana huku akiwa kiongozi wa kikosi cha Black Army alichojiunga nacho miaka kadhaa iliyokuwa imepita. Kikosi hicho kilikuwa miongoni mwa vikosi kadhaa tofauti lakini vyote vilikuwa vya ngome hiyo ya Revolution Army iliyokuwa chini ya kiongozi mkuu Zichura Msowoya. Mbali na asili yake ya upole alikuwa amefanya mabadiliko kadhaa kwani alisaidia kupunguza uonevu katika ngome hiyo na siku zote alikuwa akiwatetea wanyonge. Zichura Msowoya akiwa anaamini David angetoa mchango mkubwa katika mapinduzi waliyopanga kuyafanya katika serikali ya bwana Maabutu Lozefu, wazo lake hilo lilikuwa potofu. David hakupanga kujihusisha hata kidogo katika mapinduzi hayo na jambo pekee alilokuwa akiwaza lilikuwa ni kuiacha ngome hiyo na kurudi uraiani ili aendelee na mambo yake mwenyewe.
Jambo kubwa lililokuwa kichwani mwake wakati huo alikuwa akiwaza mali za baba yake marehemu Johnson ambazo zilirithiwa kinguvu na bwana Abraham. Alikuwa akiwaza kufanya mauaji dhidi ya baba yake mkubwa huyo aliyeamini siku zote alikuwa akihusika na mauaji dhidi ya familia yake. Akiwa katika ngome hiyo hakuna mtu aliyependa kumfanyia utani kwani alikuwa akiogopa kutokana na misimamo yake na uwezo wake wa kupigana. Tofauti na imani ya Zichura Msowoya, David alikuwa akiwatorosha mara kadhaa watoto waliokamatwa na kufikishwa katika ngome hiyo. Alikuwa akifanya hivyo hata kwa wanawake waliotekwa kwani siku zote aliutambua mwisho wao ulikuwa ni kubakwa mpaka kufa.
Askari wengi walikuwa wakimshangaa kwani alikuwa kiongozi pekee ambaye hakuwa na mke kama ilivyokuwa kwa wenzie. Viongozi wengi walikuwa wakichagua wanawake wazuri waliotekwa na kuwafanya wake zao tofauti na ilivyokuwa kwa David. Wakati huo alikuwa akiweza kuzungumza vizuri lugha ya Tshiluba iliyokuwa ikitumika katika ngome hiyo mbali na lugha ya Lingala na Kifaransa ambazo hazikutumika sana. Ngome yao hiyo ilikuwa ikiwaumiza vichwa viongozi wa serikali hiyo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwani ilikuwa haieleweki ilikuwa eneo lipi katika misitu iliyokuwa eneo Bukavu pamoja na Shabunda. Ngome yao ya Revolution Army wakati huo ilikuwa na silaha za kutosha kwa ajili ya kufanya mapinduzi na walikuwa wamebakiwa na miezi miwili ili zoezi hilo lianze.
Hatimaye mwezi wa nane ulifika ambao ulishapangwa rasmi kwa ajili ya kufanya mapinduzi dhidi ya serikali ya Maabutu Lozefu. Siku ya Jumamosi ya tarehe mosi ndiyo iliyokuwa rasmi kwa ajili ya zoezi la mapinduzi kuanza. Walipanga kwenda kuanza zoezi hilo kwa kuvamia miji ya Kalima, Pangi, Kindu pamoja na Kasonga. David akiwa kiongozi wa kikosi cha Black Army ndiye aliyepaswa kuongoza msafara kwenda kuanzisha uvamizi huo. Majira ya saa tatu asubuhi magari makubwa ishirini ya kiheshi yalikuwa na askari wa kikosi hicho chini ya David. Magari hayo yalitangulia huku mwishoni kabisa akifuata David katika gari dogo lililokuwa likiendeshwa na dereva wake. Ni wakati ambao David alikuwa amepanga kutoroka katika kikosi hicho cha Black Army. Siku zote hakuwa tayari kuua watu wasio na hatia zaidi hakuona sababu za msingi za kuwasaidia waasi hao kumtoa madarakani rais Maabutu Lozefu. Dereva aliyekuwa naye alikuwa ni mmoja kati ya watoto wawili aliofika nao katika ngome ya waasia hao miaka kadhaa iliyokuwa imepita. Tayari alikuwa amemweleza dereva wake huyo juu ya adhma yake ya kutoshiriki katika mapinduzi hayo na alimtaka waelekee nchini Rwanda ili kukwepa kushiriki katika mapinduzi hayo. Dereva huyo alikuwa amekubaliana na David kwani naye pia hakuona umuhimu wa mapigano hayo.
David akiwa na simu yake ya upepo katika gari hilo alilokuwapo alikuwa akiwapigia simu madereva wa magari ya kijeshi yaliyokuwa yametangulia akiwataka waongeze kasi ya magari yao. Lengo lake lilikuwa waachwe nyuma ili wawatoroke waasi hao. Hilo ndilo lililotokea kwani baada ya dakika kadhaa David na dereva wake walikuwa umbali wa kilometa moja nyuma ya waaasi hao. Baada ya masaa matatu walikuwa wakikaribia eneo la barabara kuu ya Shabunda ambayo upande wake wa magharibi ndiko kulikuwa na mji wa Kalima ambako walipaswa kwenda kuanza nao kuuteka. David na dereva wake walipanga kutoelekea upande huo wa magharibi na walipanga kwenda upande wa Mashariki kulikokuwa na mpaka wa nchi hiyo na Rwanda katika eneo la Bukavu.
Katika kuhakikisha zoezi lao hilo linafanikiwa David alimwamuru dereva wake asimamishe gari na walitulia katika eneo la misitu hiyo kwa dakika kadhaa huku lengo lao likiwa ni kuhakikisha hawagunduliki kama walikuwa wamewatoroka wenzao.Baada ya dakika kumi alimhurusu dereva wake huyo waendelee na safari yao, hatimaye baada ya nusu saa waliifikia barabara kuu. Dereva huyo aliliongoza gari hilo wakiifuata barabara iliyokuwa inaelekea Bukavu, aliliendesha gari hilo kwa kasi ya ajabu ili kuhakikisha hawafuatiliwi.
Wakati huo David aliamua kukata waya uliounganisha mawasiliano ya simu ya upepo baina yake pamoja na waasi aliowaongoza lakini pia kiongozi wao mkuu bwana Zichura Msowoya. Dereva aliyekuwa naye alijitahidi kukimbiza gari hilo na majira ya saa tano asubuhi walikuwa eneo la Bukavu lakini gari lao walikuwa wameliacha kilometa kadhaa kutoka katika eneo la mpakani mwa nchi hiyo na Rwanda. David alikuwa akitafuta njia ya kupita katika mpaka huo jambo lililomfanya amtafute askari mmoja wa wa nchi ya Rwanda ili awasaidie kuvuka katika mpaka huo. Haikuchukua muda kumpata askari huyo ambaye walianzisha naye mazungumzo huku askari huyo akiwa anahitaji fedha.
Baada ya kupewa fedha alizoahidiwa na David askari huyo aliwasaidia kuvuka mpaka huo, aliwapatia nguo za kijeshi za nchi hiyo ya Rwanda pamoja na namba ya gari hilo ambalo halikuwa na namba. Aliwaeleza David na dereva wake wavuke mpakani kama vile askari wa Rwanda waliokuwa wakifanya doria eneo la karibu na mpaka wa nchi hiyo. Hilo ndilo lilitokea kwani askari aliyewasaidia pia alikuwa zamu ya kuwapo mpakani majira ya saa kumi jioni, mwishoe David na dereva wake walivuka kirahisi katika mpaka huo. David alimweleza dereva huyo juu ya imani yake ya kufuatiliwa na waasi wa Revolution Army hivyo alimtaka wauze gari hilo pamoja na silaha walizokuwa nazo ili kila mmoja aelekee anakotaka. Baada ya siku nne walifanikiwa kuuza gari hilo pamoja na silaha walizokuwa nazo na mwishoe waligawana fedha walizopata. David alienda kupanga katika nyumba moja ya wageni iliyokuwapo jijini Kigali na muda wote alikuwa akisikiliza kituo kimoja cha redio ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kilichokuwa kikielezea mapinduzi yaliyokuwa yameshaanza kuchukuia nafasi.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tayari miji ya Kalima, Pangi, pamoja na Kindu ilikuwa ikishikiliwa na waasi hao huku mapigano makali yakiwa yanaendelea katika misitu ya nchi hiyo kati ya wanajeshi wa serikali na waasi hao. Muda wote alikuwa katika nyumba hiyo ya wageni huku akitambua kuwa ni lazima bwana Zichura Msowoya angetuma baadhi ya waasi ili wamtafute kwani alikuwa amekiuka sheria za waasi hao ambao hawakuwa na huruma hata kidogo. Siku iliyofuata alisikia kupitia redio mafanikio ambayo waasi hao walikuwa wakiendelea kuyapata kwani walikuwa wameiteka miji ya Kibomba pamoja na Kasonga na wanajeshi wa Serikali walikuwa wamezidiwa kwa kiasi kikubwa kwani walikuwa wakiomba msaada kutoka katika jeshi la Jumuiya ya Umoja wa Mataifa ili liende kusaidia karaha hiyo.
Akiwa bado anatafakari juu ya jambo la kufanya alipigiwa simu na dereva ambaye alitoroka naye ambaye alimweleza kuwa aliwaona baadhi ya waasi nchini hapo Rwanda. Baada ya kupata taarifa hiyo David alitambua kuwa lazima waasi hao walikuwa wakiwatafuta wao baada ya kuidhalilisha ngome ya bwana Zichura. Jambo hilo ndilo lilimfanya David afikirie kuondoka Rwanda ili ikiwezekana akimbilie Tanzania au Uganda. Alikuwa akielewa hofu aliyokuwa nayo kiongozi wa waasi hao, huku akiamini huenda waasi walikuwa wakiamini angetoa siri zao kwa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Majira ya saa tano asubuhi aliondoka katika nyumba ya wageni aliyofikia huku akiwa na lengo la kuikimbia nchi hiyo.
David hakuwa na hofu ya kukamatwa na askari wa waasi kwa vile alikuwa akijiamini kutokana na mafunzo aliyokuwa ameyapata kwa miaka saba huku akiwa anaogopwa kutokana na uwezo wake katika mapigano. Jambo ambalo lilimpa hofu lilikuwa juu ya idadi ya waasi waliokuwapo nchini hapo Rwanda wakimtafuta kwa vile hakujua idadi yao. Mara baada ya kuondoka aliongoza mpaka katika kituo kikuu cha mabasi cha jiji hilo la Kigali. Alikuwa ameva kofia pamoja na miwani ambayo kwa kiasi fulani ilikuwa imepoteza mwonekano wa sura yake. Katika kituo hicho cha basi alienda kuwatafuta vijana wahuni wa eneo hilo na aliwaomba msaada wa kujua jinsi ambavyo angeweza kuondoka katika nchi hiyo. Kijana mmoja alikubali kumsaidia baada ya makubaliano ya malipo. Walichukua teksi katika eneo hilo kabla ya kuondoka kwa kasi wakielekea sehemu ambayo David hakuifahamu. Baada ya nusu saa walikuwa nje kidogo ya jiji hilo la Kigali ambako kijana huyo alimpeleka David kwenye nyumba moja iliyokuwa katika eneo la wazi.
Baada ya kushuka kwenye gari hilo kijana huyo alimwambia amfuate na alitekeleza jambo hilo. Nje ya nyumba hiyo kulikuwa na watu wengi waliokuwa eneo hilo ambao walikuwa katika makundi tofauti huku wakiongea. Wao waliongoza mpaka ndani ya nyumba hiyo ambako walimkuta mzee mmoja ambaye alikuwa katika sebule ya nyumba hiyo. Kijana aliyeongozana naye ndiye aliyeanza kuongea na mzee huyo kwa lugha ya Kinyarwanda ambayo David hakuifahamu. Baada ya muda mfupi kijana huyo alimgeukia David na kumweleza kwa lugha ya kiingereza juu ya makubaliano waliyokuwa wamefikia. Mzee huyo alikuwa akihitaji kiasi cha laki mbili za kitanzania ili amsaidie David kuvuka mpaka wa Rwanda na Tanzania.
Alielezwa kuwa watu wotewaliokuwa nje ya nyumba ya mzee huyo nao walikuwa wakisubiri kusafirishwa kuingia Tanzania pia. David hakukataa maelezo hayo kwani alitoa fedha hizo akiwa na lengo la kumpatia lakini alishangaa kuona mzee huyo akionesha ishara ya kumzuia asimpatie fedha hizo. Alimgeukia kijana aliyefika naye na kumuuliza sababu iliyomfanya mzee huyo akatae fedha hizo. Kijana aliyekuwa na David alianza kuongea tena na mzee huyo na baada ya sekunde kadhaa walimaliza maongezi yao huku kijana huyo akiwa amepewa kikaratasi kidogo kilichokuwa kimeandikwa. Alimweleza David amfuate na alitekeleza jambo hilo, walipofika nje ya nyumba hiyo kijana huyo alimweleza kuwa mzee huyo alikuwa akitaka fedha hizo ziwekwe kwenye akaunti yake ya benki ya National Bank of Rwanda ya nchini humo. Alielezwa pia safari hiyo iliyokuwa kinyume na sheria ingeanza saa moja jioni ya siku hiyo.
Walikaa barabarani kwa dakika kadhaa kabla ya kupata gari na kuanza kurudi eneo la kituo kikuu cha mabasi cha jiji hilo ambako awali ndiko walitokea. Baada ya nusu saa tayari walikuwa mjini na kijana huyo alimwongoza David mpaka katika benki husika na walifanya malipo hayo. Wakati huo kijana huyo waliagana na David kwani tayari alikuwa ameifahamu sehemu ya kuanzia safari na zaidi alikuwa ameshamlipa fedha zake.
David aliichukua karatasi ya malipo ya fedha hizo ya benki na alianza kutembea akiondoka eneo hilo la benki, lengo lake lilikuwa ni kupata chakula ili awe tayari kwa ajili ya safari. Ilikuwa yapata saa nane mchana na alipanga kukodi teksi mara baada ya kupata chakula ili arudi kwa mzee aliyehusika na zoezi la kumsaidia kuingia nchini Tanzania kinyume cha sheria.
Aliongoza mpaka katika mgahawa mmoja uliokuwapo karibu na kituo kikuu cha mabasi cha jiji hilo la Kigali. Mgahawa huo ulikuwa wa kawaida na ulitumiwa zaidi na watu waliokuwa na kipato cha kawaida. Bila kupoteza muda David aliagiza chakula na baada ya kuletewa alianza kula taratibu huku akiwa mtulivu katika kiti alichokaa. Akiwa amevaa kofia pamoja na miwani kama alivyokuwa awali, kichwa chake alikuwa amekielekeza kwenye chakula. Baada ya dakika kadhaa akiwa bado ameinama alisikia vishindo vya watu wakiingia katika mgahawa huo, alikigeuza kichwa chake kidogo kwenye mlango wa mgahawa huo kabla ya kushuhudia mabuti ya kijeshi ya watu walioingia. Taratibu kwa utulivu alinyanyua kichwa chake na mwishoe aligundua jambo. Walikuwa askari watatu wa waasi wa Revolution Army ambao alielewa ujio wao katika mgahawa huyo.
David hakuwa na hofu hata kidogo mbali na bunduki alizozishudia kwa askari hao. Siku zote alikuwa akijiamini juu ya mafunzo aliyoyapata katika ngome ya waasi hao kwa muda wa miaka saba na hakuogopa jambo. Kudhihirisha hilo aligeuza kichwa chake na kukielekeza kwenye chakula alichokuwa akila. Aliendelea na zoezi hilo bila hofu huku akiwasikia askari hao wakiwauliza jambo wateja wenzie waliokuwapo katika mgahawa huo. Wakati wakiendelea na zoezi hilo la kula, wasi hao walimkaribia na aligundua walikuwa wakionesha picha yake pamoja na ya dereva aliyetoroka naye. Baada ya sekunde kadhaa askari mmoja alimfikia na kumshika bega lake, David alinyanyua kichwa chake kidogo pasipo kuonesha sura yake.
“Do you know this guy?” (“unamfahamu mtu huyu?”) Lilikuwa swali la kwanza la askari mmoja wapo wa waasi hao ambaye alikuwa akimkabidhi picha David. Bomba la mbele la bunduki ya askari huyo lilikuwa karibu na uso wa David kwa vile bunduki hiyo aliiweka begani. Mara baada ya kuipokea picha hiyo, David aligundua ilikuwa ya yake “Mmh! Soldier... I know him but what can I help you?” ( “Mmh! Askari…. Namfahamu lakini niwasaidie nini?”) Alijibu huku akivua kofia na miwani yake. Wakati huo askari aliyemwuliza alishtuka na kuonekana akiwageukia wenzake ambao nao walishtuka. David alipotoa kofia na miwani, kwa kasi ya haraka aliikamata bunduki ya askari aliyekuwa akimwonyesha picha kabla ya kuivuta bunduki hiyo kwa nguvu.
Askari wengine walitambua kuwa tayari kulikuwa na shari walielekeza mikono yao wakiwa na lengo la kutoa bunduki zao walizoziweka mabegani mwao. Kabla hawajafanya jambo hilo kwa kasi ya ajabu David alimpiga ngumi tumboni askari mwenzao aliyenyan`ganywa bunduki. Askari huyo alipepesuka na kuwasukuama wenzie hao ambao wote kwa pamoja waliishia kuanguka chini. David aliiweka sawa bunduki aliyoinyan`ganya na kuwaonyeshea askari hao. “Silent is all what I need, leave your guns and walk three step behind” ( “Ukimya ndio kitu pekee ninachokihitaji, acheni bunduki zenu na rudini nyuma hatua tatu”) Alisikika David akiwaambia askari hao ilhali wateja waliokuwapo katika mgahawa huo walionekana wakiwa wameinamisha vichwa vyao kwa hofu.
Askari wa waasi hao walionyesha hofu dhahiri na walitekeleza amri hiyo ya David. Hofu yao ilizidi kwa vile walimtambua kijana huyo kutokana na uwezo wake katika mapigano ya kijeshi. David alisogea eneo waliloacha bunduki hizo kabla ya kuzichukua na kuziweka katika bega lake la kushoto ilhali mkono wa kulia ukiwa na bunduki aliyowaonyeshea. Kwa kasi aliwasogelea na kuwatoa pingu za polisi walizokuwa nazo ikiwa ni pamoja na funguo za pingu hizo. Pingu mbili aliwafunga waasi hao kwa pamoja na pingu ya tatu aliiunganisa katika meza kubwa iliyokuwapo katika mgahawa huo ili wasiweze kuondoka. Baada ya zoezi hilo lililochukua takribani dakika mbili, David alisikika akimwita mhudumu mkuu wa mgahawa huyo.
Mara baada ya mhudumu huyo kutii wito huo, alimwomba kufuli na funguo za mgahawa huo, jambo hilo lilichukua nafasi kwa haraka na baada ya sekunde kadhaa mhudumu huyo alimpa makufuli mawili pamoja na funguo zake. David ambaye bado alikuwa akisisitiza ukimya alichukua pia khanga kwa mteja mmoja aliyekuwa ameinama huku akiwa hajitambui vizuri kutokana na hofu aliyokuwa nayo. Alianza kutembea akielekea nje ya mgahawa huo na hatimaye alitoka kabla ya kuufunga na makufuli mlango wa mgahawa huo. Baada ya zoezi hilo aliziviringisha bunduki zote tatu alizokuwa nazo na khanga kisha aliziweka katika mlango wa mgahawa huo. Hatimaye aliondoka akikimbia eneo hilo akiamini watu hao wangepata msaada baada ya muda mfupi.
Wakati akiendelea kukimbia alikuwa haogopi jambo na ukweli ndani ya moyo wake ulikuwa ukiendelea kujirudia. Alishawahi kujiapiza wakati akiwa katika ngome ya waasi kuwa kamwe asingethubutu kuua mtu asiye na hatia. Jambo hilo ndilo lilikuwa pia sababu kubwa ya kutoshiriki vita iliyokuwa ikiendelea katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kati ya waasi na wanajeshi wa nchi hiyo. Mara baada ya kukimbia katika mgahawa aliokuwapo aliongoza mpaka katika eneo la kukodisha teksi kabla ya kukodi na safari kuanza. Walikuwa wakielekea upande wa mashariki wa jiji hilo la Kigali ambako David alipaswa kwenda kuanza safari yake ya kuelekea Tanzania.
Baada ya kufika katika nyumba ya mzee aliyehusika na safari hiyo, David aliongoza mpaka katika sebule ya nyumba hiyo ambako alimkuta mzee huyo na alimkabidhi karatasi aliyofanyia malipo katika benki ya National Bank of Rwanda. Mzee huyo alimwelewa kabla ya kumwelekeza sehemu ya kukaa ili asubirie safari hiyo. Alienda kukaa na kutulia sehemu aliyoelekezwa, kichwani alikuwa akiwaza mambo mengi, moja wapo likiwa ni kwenda kuanza maisha nchini Tanzania kama angefanikiwa kuvuka mpaka huo salama. Alipanga kwenda kutuliza akili yake kabla ya kufanya maandalizi ya kulipiza kisasi kwa bwana Abraham aliyeamini alikuwa muuaji wa familia yake.
Eneo la nje la nyumba hiyo alikuwa na watu wengi ambao awali aliambiwa kuwa angesafiri nao. Bado alikuwa haelewi usafiri ambao ungetumika ila alihitaji kufika nchini Tanzania kwa vile alikuwa ameshafanya malipo kwa ajili ya safari hiyo. Majira ya saa moja kasoro usiku alilishuhudia gari moja la mizigo aina ya Isuzu likifika nyumbani kwa mzee huyo. Wakati gari hilo likifika aliwasikia wenzie wakipiga kelele za kushangilia kufika kwa gari hilo jambo lililompa wazo kuwa huenda ndilo lingetumika kwa safari hiyo. Walishuka katika gari hilo watu watatu ambapo mmoja wao alionekana akiwa amevaa suti. Watu hao waliongoza mpaka ndani ya nyumba ya mzee huyo waliyefanya naye mazungumzo ya muda mfupi kabla ya kutoka kwao.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Watu hao hawakuwaeleza jambo lolote zaidi ya kuwataka waingie kwenye gari hilo lililofika kwani muda wa safari ulikuwa umefika. David hakuwa nyuma huku akiwashuhudia wenzie wakiingia katika gari hilo naye alifuata mwishoni. Baada ya kuingia kwao, gari hilo lilifungwa na turubai na kuacha eneo la juu mbele ya gari hilo kwa ajili ya hewa. Safari ilianza na tayari David alishaelezwa kuwa suala la kuvuka mpaka halikuwa dogo na endapo wangekamatwa fedha alizotoa hazingerudishwa. Muda wote akiwa katika gari hilo alikuwa mtulivu tofauti na wenzie waliokuwa katika maongezi. Baada ya saa tatu gari lao lilisimamishwa na walielezwa kuwa utulivu ndio ulikuwa ukitakiwa kwani walikuwa wakikaribia katika mpaka wa Tanzania na Rwanda. Kulikuwa na askari ambao siku zote walikuwa wakizitambua safari hizo za watu kutoka Rwanda. Askari hao ndiyo waliopokea rushwa na kufanikisha watu hao kuingia nchini.
Baada ya muda mfupi walikuwa katika eneo la mpakani lililokuwa na askari wengi waliokuwa wakifanya ukaguzi wa magari yaliyokuwa yakipita. Wakati huo ilikuwa yapata saa tano usiku. Kiongozi wa msafara wao ambaye alikaa siti ya mbele ya gari hilo alishuka kabla ya kwenda kuanza kuongea na askari mmoja ambaye alionekana kama walikuwa wakifahamiana. Baada ya kuongea naye kwa muda mfupi askari huyo naye alipanda katika gari hilo kabla ya kurihurusu liondoke. Wakati huo nyuma ya bodi la gari hilo kulikuwa na utulivu wa kutosha huku vijana wengine wakionekana wanasali ili wapite salama. David alikuwa ametulia huku akiwa hajui hatma ya safari yao hiyo. Hatimaye gari hilo lilianza kuondoka taratibu eneo hilo la mpaka huku likiyapita magari mengine ambayo yalikuwa bado yakikaguliwa. Baada ya kutembea umbali wa mita kama ishirini, askari mmoja alilizuia kwa mkono gari hilo na dereva wake alitii kwa kulisimamisha. “Afande vipi? Mbona hili gari sijaona likikaguliwa!” Aliuliza askari mmoja akiwa amemsogelea askari mwenzie aliyekuwa amekaa siti ya mbele ya gari hilo. “Aah! Afande hili gari lina chakula cha wakimbizi wa kituo cha Ngara na nimepewa jukumu niwasindikize” Alijibu askari mwenzie aliyekuwa kwenye gari hilo kabla ya kuhurusiwa kwao tena.
Dereva wa gari hilo aliliondoa taratibu eneo hilo na baada dakika kumi wakiwa umbali mrefu kutoka eneo la mpaka huo aliongeza kasi ya gari hilo ambalo lilikuwa likizidi kuingia Tanzania. Bado wahamiaji hao haramu akiwamo David walikuwa hawaelewi kama wamefanikiwa kupita katika mpaka huo kwani walielezwa wakae kimya muda wote. Gari hilo liliendeshwa kwa umbali wa kilometa tano kabla ya askari waliyekuwa naye kushuka akiwa na lengo la kurudi tena mpakani. Mara baada ya kushuka kiongozi wa wahamiaji hao haramu alionekana akimpatia fedha askari huyo huku wakiwa wanaangalia kila upande wa eneo hilo lilokuwa na giza. Walikuwa wakihofia uwezekano wa kuwapo kwa mtu katika eneo hilo la porini. “Karibuni Tanzania lakini kila mtu amwombe Mungu wake kwani bado hamjafanikiwa lengo lenu sawasawa na jambo lolote linaweza kutokea…. Safari njema” Alisikika askari huyo mara baada ya kuagana na kiongozi huyo aliyempatia fedha hizo.
Maelezo hayo yaliwafanya wahamiaji haramu kadhaa waliojua lugha ya Kiswahili kushangilia kwani waliamini tayari walikuwa wamefanikiwa lengo lao. Gari hilo liliwashwa tena kabla ya kuendelea na safari hiyo wakiwa katika ardhi ya Tanzania. Wakati huo walikuwa wakiendelea kuliacha eneo hilo la Ngara huku wakielekea eneo la Keza lililopo kusini mwa mkoa huo wa Kagera. Wakiwa Keza walipanga kuendelea na safari yao ili kuingia mikoa ya kati ya nchini. Kulikuwa na kelele za kila aina za wahamiaji hao ambao walikuwa wakiamini wamefanikiwa kuingia Tanzania kirahisi. Ndani ya gari hilo la wahamiaji haramu, watu walikuwa na malengo tofauti kwani wengine walikuwa wakielekea nchi za kusini mwa Afrika. Idadi yao kubwa wakiwa na malengo tofauti na David, walikuwa wakielekea nchini Afrika Kusini ambako vijana hao waliamini wangefanikiwa kimaisha.
Wakati vijana hao wakiwa na furaha ya kufanikiwa kufauru mtihani huo wa kwanza wa kupita mpaka huo. Hali ilikuwa tofauti kwa David ambaye hakujumuika nao kufurahia, alikuwa mtulivu kama alivyokuwa awali.
Wakati vijana hao wakiendelea kufurahia huku wakipiga kelele, lilionekana gari moja dogo la kijeshi lililokuwa likitokea upande wa Keza walikokuwa wakielekea. Gari hilo la kutembelea lilizidi kusogea na hatimaye walipishana nalo huku wakiwa bado wanashangilia kwa kuvuka mpaka wa Tanzania na Rwanda. Hofu waliyokuwa nayo ilikuwa imepungua tofauti na awali. Wahamiaji hao haramu walikuwa wakizifahamu sheria za kosa ambalo walikuwa wakilifanya, ikiwa ni kifungo cha miezi sita pamoja na fedha walizopaswa kulipa. Jambo hilo ndilo lililowapa furaha na kuamini kuwa walikuwa wamepona adhabu hizo.
* * *
Kamishina Fabian Mutayoba alikuwa kiongozi wa ngazi ya juu katika usimamizi wa shughuli zote zilizokuwa zikiendelea katika mpaka wa Tanzania na Rwanda. Alikuwa ni kiongozi ambaye siku zote hakukubaliana na rushwa hata kidogo. Siku hii majira ya saa sita usiku alikuwa akitokea eneo la Keza alikokuwa na shughuli za kikazi. Wakati akiendelea na safari yake hiyo ya kurudi mpakani, alishtushwa na kelele alizozisikia kutoka katika gari moja la mizigo aina ya Isuzu. Kelele hizo zilizompa shaka zilitokana na majira ya nyakati hizo za usiku na zaidi namba za usajili za gari hilo zilizokuwa za nchi jirani ya Rwanda. Jambo hilo ndilo lilimfanya achukue jukumu la kuwapigia simu askari wa eneo la mpakani ili walifuatilie gari hilo aliloamini lilikuwa la wahamiaji haramu. Aliamini jambo hilo lingewezekana kwa vile gari hilo la mizigo halikuwa umbali mrefu kutoka eneo la mpaka huo.
Kamishina huyo alikuwa akiwaza uwezekano wa uzembe ambao askari wa mpakani hapo walikuwa wameufanya. Alikimbiza gari lake akiendelea kurudi mpakani huku akiwa anaamini hisia zake juu ya gari hilo lenye usajili wa Rwanda alilokuwa ameliona. Baada ya dakika arobaini na tano alipishana na gari la polisi aina ya Land Rover lililokuwa katika kasi huku likielekea Keza, gari hilo lililokuwa na askari zaidi ya saba lilimfurahisha kwani aliamini amri yake ilikuwa imetekelezwa. Tayari alielewa ukweli juu ya hisia zake lazima ungefahamika baada ya muda wa saa kadhaa.
Gari lililokuwa na wahamiaji haramu bado lilikuwa likizidi kusogea eneo la Keza huku baadhi ya wahamiaji hao haramu wakiendelea kushangilia juu ya kila dakika iliyokuwa ikipita. Baada ya safari ya muda mrefu, tayari ilikuwa yapata saa nane na nusu usiku. Walikuwa wamebakiwa na umbali mfupi ili wafike Keza, ni wakati ambao wahamiaji hao haramu waliomba gari hilo lisimamishwe ili waweze kujisaidia haja zao tofauti katika msitu uliokuwa pembeni mwa barabara hiyo. David naye alihitaji kutimiza haja zake hivyo alishuka na kuingia msituni kwa umbali wa mita kadhaa tofauti na wenzie ambao hawakuingia sana. Waliingia katika upande wa mbele ambao gari hilo walilolitumia lilikuwa limeelekeza taa zake.
Baada ya dakika kadhaa wahamiaji hao haramu walikuwa wametimiza haja zao na walianza kurudi katika gari walilokuwa wakilitumia ili safari iendelee. David naye alikuwa akivaa suruali kwani alikuwa amemaliza haja zake pia. Baada ya zoezi hilo alianza kutembea taratibu akiwafuata wenzie. Ghafla alishtushwa na mwanga mkali wa gari lililokuwa likielekea eneo walilokuwapo, mbali na mwanga huo gari hilo lilionekana kama lilikuwa katika kasi isiyo ya kawaida. Alipata msukumo ndani ya moyo wake uliomtuma asirudi katika gari lao mpaka gari hilo aliloliona lipite. Kutekeleza hilo aliamua kuchuchumaa eneo alilokuwapo lililokuwa na miti mingi na kumfanya asionekane. Wenzie waliuona mwanga huo lakini walikuwa wakiendelea kutembea wakirudi katika gari lao. Baada ya dakika tano hisia zake zilitimia, gari hilo aliloliona lilikuwa la polisi, lilifika eneo hilo kabla ya wenzie wote kuonyeshewa bunduki huku wakipewa onyo la kuto kimbia hata mmoja.
David alitulia eneo alilokuwapo na askari hao walikuwa wakiangalia huku na huko, waliwaamuru wahamiaji haramu wenzie waingie katika gari walilokuwa nalo. Jambo hilo lilichukua nafasi na baada ya dakika kumi wote walikuwa wameingia katika gari hilo ambalo liligeuzwa na safari ilianza wakirudi eneo la mpaka wa Rwanda na Tanzania. Wahamiaji haramu walionekana kupoteza furaha waliokuwa nayo ghafla kutokana na imani yao ya awali ya kufanikiwa kuingia Tanzania salama. Baada ya gari hilo la wahamiaji haramu kuondoka huku likifuatwa nyuma na gari la polisi. David alitulia eneo alilokuwapo kwa dakika kadhaa kabla ya kuanza kutembea akielekea Keza, eneo walikokuwa wakielekea. Alikuwa akitembea katika eneo hilo lililokuwa na giza pasipo hofu huku moyoni akiwa na amani tofauti na ilivyokuwa awali.
Mara kadhaa alipoona mwanga wa gari lililojongea eneo alilokuwapo alikuwa akijificha msituni ili asionekane na watu waliokuwa wakiendesha magari hayo. Majira ya saa mbili asubuhi alifanikiwa kufika katika eneo la Keza ambako aliongoza mpaka katika nyumba moja ya kulala wageni iliyokuwapo eneo hilo. Alikuwa akifanya mambo yake kwa uangalifu huku akihofia kukamatwa kama ilivyokuwa kwa wahamiaji haramu wenzie. Wakati huo alikuwa amesikia pia kuwa waasi waliokuwa wakifanya mapinduzi nchini Kongo walikuwa wamesalimu amri baada ya kushindwa na jeshi la serikali lililosaidiwa na jeshi la umoja wa mataifa. Siku iliyofuata alifanikiwa kupata usafiri wa gari lililokuwa likiingia mikoa ya katikati ya Tanzania. Majira ya saa sita mchana, safari hiyo ilianza na hapo ndipo aliamini mwanzo wa mafanikio yake ulikuwa umefika.
* * * *
Baada Ya Miaka Sita
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
David alikuwapo katika wilaya ya Njombe mkoani Iringa, alikuwa akifanya kazi katika duka la Sabinus store lililokuwa maarufu katika mji huo. Duka hilo lilikuwa likiuza vifaa vya umeme huku likimilikiwa na tajiri mmoja aliyekuwapo wilayani humo. Hakuna mtu aliyehisi kuwa hakuwa Mtanzania kwani alikuwa amepita mikoa kadhaa kabla ya kuingia katika wilaya hiyo. Suala la malipo juu ya mauaji dhidi ya familia yake bado lilikuwa limemkaa kichwani na alikuwa akiwaza kurudi siku moja nchini Uganda. Jina la duka alilokuwa akifanyia kazi, siku zote lilikuwa likimkumbusha binamu yake aliyefariki miaka kadhaa baada ya kuuawa na kundi la wauaji la Eastern Black Killers ambao walimuua kimakosa.
Wakati huo bado alikuwa hajafikiria kuoa mbali na vishawishi kadhaa alivyokuwa akivipata kutoka kwa wanawake waliokuwa wakivutiwa naye. Hiyo yote ilitokana na ukweli wa utanashati na zaidi mwonekano wake wa kuvutia. Alikuwa mrefu wastani huku kifua chake kikiwa kimejengeka kimazoezi mbali na tabia yake ya upole iliyowavutia wengi. Hakuwajali wanawake waliotaka kuwa karibu naye ambao walikuwa tayari kuolewa ingawaje hakuwa na kitu mpaka wakati huo. David siku zote alikuwa akiwaza mambo mengi, jambo lilimfanya asipende kuwafikiria wanawake. Alielewa jambo hilo lingefuata mara baada ya kufanikiwa kwake kimaisha. Zaidi alikuwa akiwaza kuoa baada ya kulipiza kisasi kwa bwana Abraham aliyeamini alihusika na mauaji ya familia yake.
Siku moja majira ya jioni alionekana akitembea kutoka katika duka alilokuwa akifanyia kazi. Wakati huo alikuwa akielekea katika nyumba waliyokuwa wakiishi, alikuwa kando ya usawa wa barabara kuu ielekeayo mkoani Ruvuma. Ghafla David alionekana akiwa ametoka macho kama vile alikuwa amekiona kitu cha ajabu. Aliendelea na hali hiyo kwa sekunde kadhaa ilhali akiwa amepunguza kasi ya mwendo wake wa kutembea. Mapigo yake ya moyo yalikuwa yakienda mbio huku akihisi kuishiwa nguvu kadri alivyotembea.
Alikuwa amemwona msichana mmoja aliyekuwa amesimama umbali wa mita kadhaa toka eneo alilokuwapo. Uzuri wa msichana huyo ndiyo ulioweza kuelezea picha nzima ya kila kitu kilichokuwa kinaendelea. David hakuwahi kumwona msichana mzuri kama huyo katika maisha yake jambo lililopelekea mshtuko alioupata. Huku akiwa mrefu wastani kama yeye alikuwa mweupe kidogo zaidi akiwa na kila kigezo cha kushiriki mashindano ya urembo. Alikuwa akivutia jambo lililopelekea watu waliopita wamwangalie pia tofauti na David aliyechanganyikiwa kabisa. Pembeni yake kulikuwa na begi kubwa huku akionekana kama alikuwa safarini. David aliendelea kujongea eneo alilokuwapo msichana huyo taratibu huku akiwa hajui jambo ambalo angeongea.
Mpaka wakati huo msichana huyo aliyekuwa akiangalia saa yake kama vile alimsubiria mtu alikuwa hajamwona David aliyezidi kujongea. Mara baada ya kuangalia saa yake alionekana kama alikuwa amechanganyikiwa kwani alijishika kichwani na kuanza kuvuruga nywele zake. Baada ya sekunde kadhaa alionekana akipepesuka kabla ya kuonyesha dalili zote za kutaka kuanguka kabisa. David alishtuka pia juu ya jambo hilo lililomfanya asimame akiwa haelewi tatizo lililokuwa limempata msichana huyo. Hatimaye alionekana dhahiri akianza kuanguka na David alimwahi kabla ya kumdaka akiwa umbali wa sentimeta kadhaa ili afike chini kabisa.
Alipomwangalia msichana huyo aligundua alikuwa amepoteza fahamu jambo lililomtisha, alipiga kelele za kuomba msaada. Baada ya dakika kadhaa wapita njia wengine walijongea pia kabla ya kumsaidia. Walikodi teksi iliyomchukua msichana huyo huku wakiwa wamepakia begi lake pia. Gari hilo liligeuzwa kabla ya kuondolewa kwa kasi likielekea katika hospitali kuu ya wilaya ya Njombe iliyopo eneo la Kibena, kilometa tano kutoka Njombe mjini. Ndani ya gari hilo mbali na dereva alikuwapo David pamoja na mpita njia mmoja. Baada ya robo saa walikuwa katika hospitali hiyo wakimshusha msichana huyo katika gari hilo.
Kelele alizokuwa akipiga David akihofia uhai wa msichana huyo ndizo zilizopelekea wauguzi wafike haraka eneo hilo wakiwa na machera wakihofia uhai wa mgonjwa aliyekuwa amewasili. Hatimaye walimchukuwa msichana huyo na waliongoza naye ndani ya hospitali hiyo huku David akiwa anaonekana kama amechanganyikiwa. Akiwa na mpita njia aliyeongozana naye hawakuhurusiwa kuingia katika chumba maalum ambacho uchunguzi dhidi ya msichana huyo ulienda kufanyika. David alimlipa dereva teksi aliyewapeleka hospitali hapo ambaye aliondoka baada ya ujira huo. Walikaa nje ya chumba walichoambiwa wasubiri kwa muda wa nusu saa pasipo kupewa taarifa yeyote. Jambo hilo lilimuumiza sana kichwa David kwani alikuwa amegundua vitu vingi kutoka kwa msichana huyo na jambo kubwa alikuwa amebaini kwamba anampenda.
Alikuwa amekutana na wanawake wengi katika maisha yake lakini huyo alimwona wa tofauti jambo lililopelekea awe tayari kwa jambo lolote. Alikuwa tayari kumwoa msichana huyo kama angemkubalia na zaidi saikolojia yake ilikuwa imevurugika kwani kila mara alikuwa akirudiwa na picha ya msichana huyo kichwani akikumbuka jinsi alivyokutana naye.
Baada ya dakika arobaini na tano, wauguzi walitoka na msichana huyo kutoka katika chumba walichokuwa naye huku akiwa amefungwa pamba kichwani. Kulikuwa na maji ya baridi yaliyokuwa kwenye mfuko ulifanana na rambo yakiwa yamewekwa eneo la kichwani la msichana huyo. Alikuwa kwenye kitanda chenye magurudumu na wakati huo alikuwa akipelekwa katika wodi la wanawake. David alimkimbilia muuguzi mmoja kabla ya kusikika “Atapona?…. Aah! niambie kama atapona, halafu anaumwa nini?” “Usijari kaka mgonjwa wako atapona ila inaonyesha ana maumivu makali ya kichwa jambo lilopelekea apoteze fahamu mpaka muda huu”. Baada ya maelezo hayo, David alielewa na aliongozana na wauguzi hao mpaka katika kitanda ambacho msichana huyo alienda kulazwa.
David alitulia pembeni ya kitanda hicho huku akionesha hofu kubwa juu ya uhai wa msichana huyo. Mpita njia aliyemsaidia kufika hospitalini hapo alikuwa ameondoka hata wauguzi walimwacha na msichana huyo waliyeamini alikuwa ndugu yake. Wakati huo David alikuwa akimchunguza msichana huyo kupindukia, hata angeitwa ingeweza kuwa vigumu kuitika kwani akili yake ilikuwa kwa msichana huyo. Alionekana akiziweka vizuri nywele za msichana huyo zilizokuwa zimevurugika. Baada ya zoezi hilo alitulia kidogo kabla ya kuelekeza macho yake tena usoni kwa msichana huyo ambaye bado hakuwa na fahamu.
Hatimaye ilitimia saa tatu usiku na bado hakufikiria kurudi nyumbani kwao alikuwa akizunguka zunguka katika eneo hilo la kitanda alicholala msichana huyo. Majira ya saa tatu na nusu usiku aligundua kulikuwa na karatasi katika shati alilokuwa amevaa msichana huyo. Aliamua kulichukua karatasi hilo na baada ya sekunde kadhaa za kulisoma aligundua jina la msichana huyo, alitambua kwamba aliitwa Jacqueline John. Karatasi hilo lilikuwa la matibabu ya kichwa pia ambayo alionekana kuyapata siku mbili zilizokuwa zimepita katika wilaya ya Songea mkoani Ruvuma. Jambo hilo ndilo lilimpa hisia na kuamini kuwa msichana huyo alikuwa mpita njia eneo hilo la Njombe.
Majira ya saa tano usiku David alikuwa amechoka sana kutokana na uchovu dhidi ya shughuli alizokuwa akizifanya katika duka la Sabinus Store. Ni wakati aliowaza kuondoka ili arudi nyumbani kupumzika. Hilo lilipaswa kuchukua nafasi kwa vile alikuwa hajatoa taarifa kwa mwajiri wake pia juu ya kuondoka kwake siku hiyo. Aliamua kumpa muuguzi mmoja kiasi cha shilingi elfu kumi ili amfanyie uangalizi wa karibu mgonjwa wake. Pia alimtaka amlindie begi msichana huyo ambalo lilikuwa limefungwa. Aliahidi kuwa angerudi hospitali hapo siku iliyofuata asubuhi. Baada ya makubaliano hayo kuchukua nafasi, akiwa mnyonge David alionekana akiondoka huku akiwa ameelekeza kichwa chake akimtazama Jacqueline katika kitanda alichokuwa amelazwa. Mara baada ya kutoka nje kabisa alifanikiwa kupata teksi iliyompeleka mpaka eneo la Njombe mjini alikokuwa akiishi na mwajiri wake.
Mara baada ya kufika nyumbani kwa mwajiri huyo alimweleza juu ya kila jambo lililokuwa likiendelea na zaidi alihitaji siku iliyofuata aelekee katika hospitali hiyo ya wilaya ili kwenda kumjulia hali Jacqueline. Hakupata pingamizi kwani alipewa ruhusa ya kwenda kumwona msichana huyo. Siku iliyofuata aliamka majira ya saa kumi na mbili na nusu, mara baaada ya kujiandaa alitumia usafiri wa teksi tena kurudi katika hospitali ya wilaya hiyo ya Njombe. Majira ya saa moja alikuwa ameshuka kwenye gari huku akionekana anatembea kuelekea katika wodi la wanawake ambako Jacqueline alikuwa amelazwa. Baada ya dakika moja alikuwa akizidi kutembea akijongea katika kitanda alichokuwa amelazwa msichana huyo. Macho yake yaliposhuhudia alihisi miguu yake ikianza kukosa nguvu kadri alivyozidi kukisogelea kitanda alicholazwa Jacqueline. Hakikuwa katika hali aliyoiacha usiku wa jana yake kwani msichana huyo hakuwapo katika kitanda hicho na kilikuwa hakina mtu. Zaidi hata begi lake halikuwapo jambo lililompa hisia kuwa msichana huyo hakuwa ameenda sehemu. Hisia pekee zilizoanza kumwingia kichwani alianza kuhisi huenda msichana huyo alikuwa amefariki usiku wa kuamkiwa siku hiyo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Huku akitembea kwa taabu alijitahidi kujongea katika kitanda alicholazwa msichana huyo kabla ya kuishia kukaa akiwa ameinamisha kichwa chake. Alikuwa akiwaza mambo mengi ndani ya muda mfupi ambayo majibu yake hakuyapata. Machozi yalikuwa yakimtoka pasipo kujitambua akiwa amekaa katika kitanda hicho. Hata muuguzi aliyepewa jukumu la kumwangalia Jacqueline siku iliyopita alifika na kukaa kado yake kabla ya kumwita lakini akili ya David ilikuwa mbali na alikuwa kama hajasikia. Muuguzi huyo aliamua kumshika bega David ambaye alishtuka kabla ya kusikika “Amekufa!... amekufa…” Alipomwangalia muuguzi na kumgundua alisikika akiongea kwa mara nyingine tena. “Niambie dada yangu kama ameshakufa, niambie, mbona sijamwona?”
***Mtihani!
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment